Serikali kukatiwa Umeme ni aibu

KATIKA siku za hivi karibuni tumekuwa tukisikia juu ya watu wanaowaua na kuwachuna ngozi binadamu wenzao kwa tamaa ya kuuza ngozi hizo zikafanyiwe matambiko yanayoaminika kuwa huwaletea wahusika utajiri mkubwa.

Zipo pia simulizi nyingi mitaani kwamba baadhi ya watu wanaoaminika kuwa wachawi huwatoa watoto wao kafara, ili kujipatia utajiri ingawa inaelezwa pia kuwa utajiri huo huwa wa mateso na usiowaletea furaha katika maisha yao yote.

Hayo ni simulizi za wale wanaoamini juu ya nguvu za ushirikina.

Kwamba sisi tunaamini au hatuamini hiyo haitasaidia katika lengo la safu hii, bali kuzitumia simulizi hizo kama mfano wa kukihuisha kile tunachotaka kuiasa Serikali yetu tukufu kuhusiana na kuwa mdeni sugu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kiasi cha kufikia kukatiwa nishati hiyo muhimu.

Mapema juma lililopita TANESCO ililazimika kuzikatia umeme wizara na idara kadhaa za serikali kutokana na usugu wao wa kutumia umeme bila kuulipia.

Kwa mujibu wa TANESCO deni la umeme la serikali linafikia bilioni 15 hadi kufikia Desemba mwaka jana na ndilo lililopelekea serikali kukatiwa umeme.

Jambo la kuhuzunisha ni kwamba serikali, ambayo bila shaka inajua umuhimu wa kuimarisha huduma ya umeme ambao ni nyenzo moja kuu katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi, imekuwa kwa muda mrefu mfano mbaya kwa taasisi nyingine na watumiaji binafsi kwa kutoweka kipaumbele katika kuiboresha nyenzo hiyo.

Kama ilivyo katika mfano wa wale wanaotoa watoto wao kafara ili kujipatia wanachodhani ni utajiri lakini wakaishia katika masikitiko ya kudumu, ndivyo ilivyo kwa jambo hili.

Ikiwa serikali inaweza kutoa zaidi ya shilingi milioni 400 kila mwezi kama ruzuku ya vyama vya siasa ambavyo kimsingi vilistahili kuendeshwa na wanachama wake, lakini ikashindwa kulipa bili zake za umeme, je, busara ya kuchagua kipaumbele cha mambo iko wapi?

Je, huku si sawa na kumtoa mwanawe TANESCO kafara kwa faida ya mashaka?

Serikali ndiyo inayoongoza nchi, na daima kiongozi anapaswa kuwa kitu chema cha kuigwa, sasa je, katika hili la ulipaji madeni ya umeme wengine waige nini kwa serikali yetu tukufu?

Tunatoa wito kwa serikali kuweka kipaumbele kikubwa zaidi katika maendeleo ya nishati ya umeme nchini kwa kuzingatia umuhimu wa nishati hiyo ambayo hata kiwango cha matumizi yake huweza kutumika kupima maendeleo ya nchi. Ni aibu kubwa serikali kukatiwa umeme.

Lipeni madeni hayo haraka.

Nchi yetu iongozwe na dhamira njema, sio mashinikizo

Ndugu Mhaiiri,

Mara nyingi hususan katika mataifa ya Afrika na yale ya kiimla katika maeneo mengine duniani tumekuwa tukisikia vikwazo vya kiuchumi vikitumiwa kama njia ya kuzifanya serikali ziwatendee watu yale ambayo haki inadai watendewe.

Katika matukio mengi karibu yote, serikali zinazohusika hutumia silaha ya maneno matamu na ahadi za kuvutia kujihami na shutuma za jumuiya ya kimataifa, lakini inapofikia katika utekelezaji mambo huwa kinyume.

Kimsingi mataifa mengi ya Kiafrika kutokana na utamaduni huo ambao kiini chake huwa ni ubinafsi umeziingiza nchi hizo katika maafa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe au kuchochea hujuma mbali mbali.

Viongozi wengi wa nchi hizo huwa wagumu wa kushauriwa kwa vile ubinafsi huwa umekwishawapofusha wasiweze kuona kingine chochote na hata hatari zinazowakabili zaidi ya kiburi chao. Viongozi wa namna hii huwa hawawezekani hadi wakabiliwe na mashinikizo makali kama vile kuwekewa vikwazo vya kiuchumi, kukatiwa misaada au kung’olewa madarakani kwa nguvu za mtutu wa bunduki.

Lakini kiongozi mzuri ni yule ambaye haongozi nchi yake kwa kuhofia mashinikizo ya aina hiyo bali dhamira njema kwa wale anaowaongoza.

Matukio yanayojitokeza hivi sasa nchini hususan katika masuala ya mgogoro wa Zanzibar ni dalili kwamba tunakaribia au tayari tumeingiliwa na ugonjwa wa kutofanya tunayostahili kufanya hadi kwa mashinikizo. Kitendo cha Jumuiya ya Ulaya kulazimika kumtaka Rais Benjamin Mkapa aingilie kati mgogoro wa Zanizbar kwangu mimi na bila shaka kwa wengi nakiona kuwa ni cha aibu kwa vile huo haukuwa wajibu uliohitaji kukumbushiwa na watoka mbali hawa. Ni jambo ambalo liko wazi kwamba Serikali ya Muungano ina wajibu wa kusimamia amani ya nchi hii kwa makini na kwa haki bila kusukumwa na wafadhili. Nawashauri viongozi wetu waongozwe na dhamira njema badala ya mashinikizo.

Majeghoanguto Nimakai,

S.L.P 2714

Dar es Salaam.