Wanaochelewesha posho za wanafunzi wawajibishwe

SIKU hizi wananchi wengi wanapenda sana kusoma na pia kuwasomesha watoto wao katika shule mbalimbali. Licha ya kupenda elimu, wananchi wengi hupenda pia ubora wa elimu. Huo ubora wa elimu hutegemea mambo mengi kama vile mazingira ya kufaa . Kadiri tunavyofahamu mwanafunzi hana budi kuwa katika hali ya utulivu akizungukwa na walimu wazuri na wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo ya kufundisha ipasavyo.

Kwa sababu hiyo tunashuhudia jinsi watu na hasa wazazi wanavyohangaika kupata shule zilizo nzuri na za kufaa. Pengine wako tayari kutoa gharama hata za ziada ili mradi tu elimu bora iweze kupatikana. Moja kati ya mambo yanayosaidia sana kwa kila mwanafunzi kujipatia elimu ni katika shule zile za bweni. Watu wengi wanaamini kuwa mwanafunzi na hasa mtoto akiwa katika shule ya bweni atapata muda mwingi zaidi wa kuzama katika masomo yake na hivyo kuweza kujipatia elimu sawa sawa.

Katika miaka ya zamani kulikuwa na shule nyingi za msingi za bweni. Shule hizo zilijulikana hasa kama Shule za Kati au ‘Middle School’. Shule hizo zilikuwa chini ya Halmashauri za Wilaya na nyingine zilikuwa chini ya Mashirika ya Kanisa. Hapo wanafunzi walilelewa vizuri siyo tu kielimu bali pia kimaadili na kinidhamu . Karibu kila shirika la kidini lilikuwa linajitahidi kuwa na shule hizo za bweni ili kuweza kuwafunza vijana elimu na pia malezi ya kidini. Shule hizo hazikuwa na ubaguzi wo wote ule. Na ndiyo maana tunashuhudia jinsi viongozi wetu mbalimbali walivyofaidika na shule hizo za mashirika ya kanisa na hasa zile za bweni.Kwa hiyo hakuna mtu anayekataa umuhimu na ubora wa hizo shule za bweni, na ndiyo maana wazazi wengi siku hizi wanahangaika katika kutafuta hizo shule za bweni kwa ajili ya watoto wao kuanzia madarasa ya chini kabisa.

Hayo yote yanaonyesha umuhimu au nafasi nzuri ambayo shule za bweni zinayo kwa ajili ya maendeleo ya kimasomo ya mwanafunzi. Lakini ikumbukwe pia kwamba endapo shule hizi zitakosa malezi bora ya kiadilifu, zinaweza kuwa mtambo wa kuzalisha vijana wengi ambao wamechanganyikiwa na hivyo kupelekea taifa la baadaye kuwa la wendawazimu.

Shuleni humo, wanafunzi kutoka katika familia mbali mbali, wakiwa wamepata malezi tofauti na katika mila na destrui tofauti huweza kuambukizana tabia mbaya kama vile uasherati, uvutaji bangi, ukatili na maovu mengine kwa urahisi zaidi kuliko kwa wale wa shule za kutwa.

Siku hizi ni jambo la kawaida kusikia wanafunzi hasa wa masule ya bweni wamegoma, lakini unapochunguza kwa kina utabaini kuwa tatizo kubwa ni udhaifu wa mawasiliano au kutojali kwa uongozi wa shule.

Inakuwaje wanafunzi hawapewi posho yao wakati unaotakiwa? Hakuna kitu kinachoumiza kwa mwanafunzi ambaye siku nzima ameketi darasani kukosa chakula wakati wake. Zamani wanafunzi wale ambao walikuwa wanakaa bweni walionekana kuwa na afya njema zaidi kuliko wale ambao walitoka majumbani na kufika kusoma. Uongozi wa shule ulikuwa ukihakikisha kwamba hao wanafunzi wanapata chakula chao cha kutosha na kwa wakati wake maalum kila siku. Lakini mambo ambayo hufanyika siku hizi katika shule mbalimbali ni mabaya sana na hata pengine ni ya aibu sana katika taifa letu.

Wanafunzi wanapoamua kufanya mgomo eti kwa sababu ya kukosa chakula au kupata chakula kisichofaa, hilo ni jambo la kusikitisha sana na tena ni la aibu mno. Wale viongozi wa mashule hapo awali waliweza kushughulikia maslahi ya wanafunzi bila kuwa na manung’uniko kama yalivyo sasa hivi licha ya mazingira kuwa magumu. Siku ya leo kuna hali ya kutokuwajibika sana kwa wale wahusika katika maofisi. Ni kawaida kusikia kuwa watumishi katika idara fulani hawajalipwa mishahara yao ya miezi kadhaa iliyopita, ingawaje fungu lao lipo. Tunawashangaa sana hao wahusika wanawezaje kuwa mioyo myeusi na hivyo kuwafanyia ukatili wenzao kwa kuwanyima haki zao.

Tunasema tena kuwa ni jambo la aibu kwa Wizara na pia kwa taifa kuona wanafunzi au wanavyuo wanafanya mgomo kwa sababu ya kudai posho zao. Kwa nini mtu akalie posho za watu wengine, na hivyo yeye apate raha na wengine wateseke kwa sababu yake? Kwa nini watu wachelewe kuzipata hizo posho zao na papo hapo kila kitu kimeshakuwa katika mipango ya mwaka mzima? Tunafikiri kuwa kuna hali ya ubinafsi katika watendaji wengi hapa nchini.Pia tungeweza kusema kuwa kuna ukosefu wa uzalendo kwa watumishi wengi.

Kadhalika ni jambo la fedheha sana kuwafukuza wanafunzi kwa sababu wamegoma kutokana na kutopewa posho zao. Kwa nini hao wenye kusababisha hiyo migomo nao wasiwajibishwe?

Kuna uzembe katika kuendeleza kilimo nchini

Ndugu Mhariri,

INATIA uchungu kuambiwa kuwa Tanzania ni nchi maskini sana duniai na kwamba kama sio ya mwisho ni ya pili katika orodha ya nchi maskini. Hivi kauli hii inaudhi kiasi gani? Je Watanzania wanaichukulia vipi kauli hii? Kwa raia wa kawaida ambaye hajapata bahati ya kutembelea nchi tajiri duniani, hataelewa maana ya kauli kama hiyo.

Kwake kigezo cha umaskini ni kukosa chakula, nguo, madawa hospitalini, vitabu na daftari za watoto wake shuleni na vitu vingine kama hivyo. Ukitupa macho nyuma enzi zile za zamani wanazoita za arobaini na saba utakumbuka kulikuwa na kitu kama Overseas Food Coorparation, Tanganyika Agricultural Coorparation.

Baadaye vikaja vitu kama Masai Land Development Scheme, Ngoni Matengo Development Scheme, Uluguru Land Development Scheme na kadhalika. Miaka ya karibuni kukatokea vitu vingine kama Igembe Nsabho Coperative Union,Nguvu Mali Cooperative Union, Buha Coorperative Union na kadhalika. Vyombo vyote hivyo na vingine vingi ambavyo sikuvitaja hapa vinatimiza historia ambayo sote tunaijua ya kuwepo kwao, lakini havikufanikiwa kwa kiasi kikubwa kukuza kilimo chetu na ndio maana vikafa na vingine vikafungwa na Serikali. Si nia yangu kueleza kwa nini vilishindwa ila nakusudia kutoa maoni kwamba pamoja na kusema kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa taifa bado kilimo chetu kiko nyuma sana.

Tunazo mamlaka za korosho, mamlaka za kahawa, tumbaku, pamba, mkonge, lakini mamlaka hizo hazionekani zikishughulika kwa dhati na matatizo ya wakulima.

Mkulima wa Tanzania hadi hii leo bado analima kwa jembe la mkono. Mkulima anaambiwa kuwa kuna mbolea na madawa ya kuulia wadudu lakini hakuna utaratibu wa kuaminika wa kupata hizo pembejeo. Kwa kweli tukitaka kufuta umaskini lazima tuanze na shibe. Taifa la watu wanaoshinda na njaa haitazamiwi kuwa watafanya kazi kwa bidii na wakazalisha mali kwa wingi. Wakati umefika sasa twende kwenye mzunguko wa chakula kuleta shibe na shibe kuleta chakula na hivyo hatimaye tutashiba na kuuza ziada.

Kwa kuwa muundo wa siasa umebadilika na vyombo nilivyovitaja hapo juu havipo tena bali kuna ubinafsishaji na soko huria, ni vema sasa wawekezaji washawishiwe kuwekeza katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili mbali ya kuwa watafanya biashara kutokana na mazao ya chakula na biashara, ili mbali ya kuwa watafanya biashara kutokana na mazao watayovuna lakini pia watakuonyesha namna ya kulima vizuri na vijana wetu wengi wasio na kazi watapata ajira katika mashamba yao. Hatimaye tutaingia kwenye mtiririko wa mazao yetu kuingia katika viwanda vyetu na kutoa bidhaa bora tunazohitaji kutumia na kuziuza kwa kufanya hivyo tutajenga taifa lenye afya na linalojitegemea kwa maendeleo yetu.

E.G Msuguru

SHUKRANI WATUMISHI WA TUICO TANZANIA

1 Gazeti wachapakazi, Langoni twapiga hodi,

Tuico na uzinduzi, Kamati mumeinadi,

Tawi yawashukuru, Watumishi wa TUICO.

2. Uongozi mumetupa, Tawi la TUICO Nchini,

TUICO dira metupa, Katiba yetu Chamani

TUICO siyo lipapa, Kumeza wake wandani

Kamati yawashukuru, Watumishi wa TUICO.

3 Msaada wenu muhimu, Kuongoza Tawi lenu,

Kamati sasa timamu, Uchunguzi ndiyo wenu

Mawazo yenu hatamu, Kufikiwa nia yenu

Kamati yawashukuru, Watumishi wa TUICO

4. Watumishi wa TUICO, Tanzania twashukuru,

Jira ndani ya TUICO, yanalindwa bila kukuru

Watendakazi TUICO, Chapa kazi kwa Uhuru

Kamati yawashukuru, Watumishi wa TUICO

5. Mumetupa yetu, Kazi lengo letu tufikie,

Kamati tulize zizi, Adui asiingie,

TUICO iwe azizi, Wapambe nuksi walie,

Kamati yawashukuru, Watumishi wa TUICO.

6 Chaguzi za Matawini, sasa zafikia tamati,

Chaguzi za Mikoani, Zitachagua Kamati,

Chagueni wathamani, Wacheni wala chapati,

Kamati yawashukuru, Watumishi wa TUICO.

Ignas. A. Charaji (Kufa si Mwiko)

Mwenyekiti wa Tawi

TUICO Makao Makuu