Make your own free website on Tripod.com

Hivi moto unatibu tabia za watoto?

KUNA usemi usemao uchungu wa mwana, aujuae ni mzazi. Lakini, kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita hatujui ni kwanini hali imegeuka kabisa na kuwa kinyume katika wilaya ya Musoma mkoani Mara juu ya usemi huu.

Wakati jamii ya Watanzania wote, jamii yenye sifa ya upendo na amani ulioidumishia sifa nchi yetu miongoni mwa nchi nyingi duniani, inaelekezwa na kutilia mkazo kuwalinda watoto kwa kuwapa haki zao za msingi kwa upendo na kuwapa mahitaji muhimu ya chakula, elimu pamoja na makazi, baadhi ya ndugu zetu wa mkoa huu, wamegeuka na kuzikana juhudi hizo.

Tunasema tunashangaa kwa kuwa katika mkoa huu wa Mara, umeibuka mtindo wa wakazi kutumia moto kuwachoma watoto wao kama njia ya kuwaadhibu watoto wao kwa makosa mbalimbali hususani kwa madai ya watoto hao kudokoa mboga.

Hivi mbona wakazi wa mkoa huu tunazidi kuharibu jina la mkoa na kupoteza kabisa hadhi yake?

Ikumbukwe kuwa hadi hivi sasa mkoa wa Mara ni mkoa ambao jina lake limeharibika katika vinywa na masikio ya wengi kutokana na vitendo vya ukatili na ugomvi vilivyoshamiri kwa kutumia mapanga maarufu kama KUGECHANA bila huruma.

Wakati juhudi za kulisafisha jina hilo hazijakamilika, inashangaza tena wenyeji wanaanza kuibuka na staili mpya ya ukatili ambayo kweli kama haitadhibitiwa na kukemewa na kila mwana jamii, hatujui tanzania tutakuwa tunakwenda wapi.

Ni staili ambayo ukiilinganisha na hii ya kugechana, kila moja ni mbaya kuliko nyingine.

Mwezi Juni mwaka huu, mkazi mmoja wa mtaa wa Mtakuja alimuunguza miguu kwa moto, mwanae mmoja baada ya kumtuhumu kuwa ni kibaka. Wenye kushangaa walishangaa na hata wenye kusikitika walisikitika lakini mradi tu, alimchoma bila huruma kwa moto wa makusudi.

Katika tukio lingine, katika wilaya hiyo ya Musoma mkoani Mara, mtoto wa kike wa mtaa wa Shabani katika Halmashauri ya mji huo, aliunguzwa mkono wa kulia baada ya mlezi wake kumtuhumu kuwa alidokoa chunguni kinofu cha samaki aina ya sangara.

Inashangza kuwa mtoto huyo aliunguzwa pia mdomo na mlezi wake eti kwa kuwa mlezi huyo, anathamini zaidi kinofu cha sangara na hivyo ni vema eti amtie mtoto kilema kwa sababu hiyo.

Ajabu, ukatili huo unafanywa na watu wenye akili timamu wakiamini kuwa hiyo, ni njia ya kumuadhibu mtoto eti kwa kuwa wananchi hao wanayalinda madhambi yao na kukiita kitendo hicho cha mtoto kuchukua kinofu cha sangara kuwa ni wizi.

Sisi tunasema, ingawa ni jukumu la kila mzazi, mlezi na mwanajamii kumuadabisha na kumlea mtoto katika misingi ya maadili mema ili kuliepushia taifa kuwa na wananchi waliopotoka kimaadili, jamii haina budi kujua kuwa uchungu wa mwana aujua mzazi ambaye ni kila mwanajamii wa Kitanzania.

Ni kwa mantiki na ukweli huo tunasema, hivi sasa jamii inaelekea pabaya kwa kuwa watoto ambao ni taifa la kesho, ndio hao wanaonekana kutokuthaminiwa kwa kuwa wanaadhibiwa kwa adhabu za kikatili na kinyama namna hiyo.

Ni adhabu zinazoonesha kuwa wazazi wa namna hiyo hawana hata chembe kidogo za utu, wala uchungu kwa watoto wao.

Tunasema hivyo kwa uchungu kwa kuwa licha ya mifano tuliyotangulia kuitoa, Juni 21, mwaka huu katika kijiji cha Kizaru katika Wilaya ya Musoma-Vijijini, mwanamke mwingine Nyamboba Nyamurangi, alimchoma kwa moto, mtoto wake wa kuzaa na kumtia kilema cha maisha kwa madai hayo hayo eti kadokoa dagaa wa kukaanga.

Baada ya kumtuhumu kudokoa chunguni dagaa hao wa kukaanga kwa chumvi wenye thamani ya shilingi 100/=, mwanamke huyo bila kujali utu na thamani ya mtu ukilinganisha na dagaa wa shilingi mia moja, alimfunga kwa kamba mwanae huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza, John Nyamurange (8).

Inasikitisha kuwa baada ya kumfunga mikono yake yote miwili, Nyamboba alimwagia mafuta ya taa kwenye mikono na kisha kumbabua na kumuunguza kwa moto mtoto huyo.

Hivi ni unyama ulioje kiasi kwamba hata baada ya kumfanyia mwanae wa kuzaa unyama huo, bado mwanamke huyo ambaye naye alilelewa kwa mapenzi tofauti na hayo anayoyatoa kwa mwanae, alimficha ndani na kujidai kumtibu kwa miti shamba badala ya kumpeleka hospitali?

Hivi kama wasingekuwa watoto wa jirani kutoboa siri kwa mwalimu wake mkuu kwamba mikono ya mtoto huyo ambaye sasa anapata kilema cha maisha hasa baada ya vidole vitano vya mkono kuungua kabisa ilikuwa ikitoa usaha, nini ingekuwa hatima ya mtoto huyo licha ya hali aliyo nayo sasa?

Ni wakati muafaka jamii kutoka usingizini na kuachana na unyama dhidi ya watoto wa taifa hili kwa kuwa Watanzania ndio wazazi wa watoto wa Kitanzania.

Sasa kama sisi ndio hatujui wala kujali uchungu wa wana wetu, nani ataujua na kuwajali?

Hatukatai kuwaadabisha au kuwaadhibu watoto wanapokiuka maadili na malezi. Lakini, tunachokisema, ni kwamba, adhabu ziendani na busara na utu kwa sababu kumchoma moto mtoto, sio matibabu ya tabia yake bali ni kumkomoa na zaidi, kuyaita matatizo yasiyo ya lazima.

Tuna imani vyombo husika vitazidi kuwa mstari wa mbele kuwaadabisha wanaowaadabisha watoto kwa njia za kinyama namna hii.

Sala kwa msalaba mtakatifu

MT. ANSELMO(1033-1109)

Msalaba Mtakatifu

Unaotukumbusha msalaba ambao Bwana Wetu Yesu Kristo alikufa,

Kuturudisha toka kifo cha milele,

Ambako unyonge wetu ulikuwa unatupeleka,

Kuelekea uzima wa milele ambao tuliupoteza kwa kutenda dhambi.

Nakuabudu, nakuheshimu na nakutukuza katika msalaba uliotukabidhi,

Na kwa msalaba namwabudu bwana wetu mwenyehuruma

Na aliyotutenda kwa huruma yake kwetu sisi.

Msalaba unaostahili kupendwa,

Ndani yake kuna wokovu wetu, uhai wetu, na ufufuko.

Mti azizi sana, kwao tunaokolewa na kuwekwa huru,

Ishara ya kuheshimiwa, kwayo tunatiwa muhuri kuwa wa mungu,

Msalaba mtukufu, twapaswa kuona fahari kwako tu.

Hatukukiri kwa sababu ya uovu

Ambao watu wasiomjuamungu na wajinga walikuandaa

Ili kumtendea Bwana aliyemnyenyekevu kabisa,

Lakini kwa sababu ya hekima na wema wa yeye

Ambaye kwa hiyari yake mwenyewe alikubeba.

Kwani wasingeweza kumfanya chochote

Kama si kwa hekima yake kuruhusu,

Na hasingeweza kuteseka kama katika huruma yake hasingeridhia,

Walikuchagua wewe

Ili waweze kutekelezea matendo yao maovu;

Yeye alikuchagua wewe

Ili aweze kutimiliza kazi ya wema wake.

Wao kwa njia yako

Waweze kumtoa mwenyehaki katika kifo;

Yeye kwa njia yako aweze kuwaokoa wadhambi na kifo.

Wao ambao wanaweza kuufisha uhai

Yeye ambaye anaweza kuharibu kifo;

Wao ambao waweza kumhukumu mkombozi

Yeye ambaye anaweza kumkomboa aliyehukumiwa.

Wao ambao waweza kusababisha kifo kwa aliyehai;

Yeye alete uzima kwa aliyekufa.

Walitenda kipumbavu na kikatili;

Yeye kihekima na kihuruma.

Hivyo, ewe msalaba tunakuonea shani,

Hatukuthamini kwa sababu lengo la uovu wao wa kijinga,

Lakini kulingana na utendaji wa huruma na hekima.

Kwa jinsi ngani, hivyo nikusifu,

Kwa namna gani nikutukuze

Kwa upendo gani nisali kwako,

Na kwa furaha gani nione fahari ndani yako?

Kwa njia yako jehanamu inaporwa,

Kwa njia yako mdomo wale unafungwa kwa wate waliokombolewa.

Kwa njia yako mashetani wanaogofywa na kuzuiwa,

Wanashindwa na kukanyagwa.

Kwa njia yako ulimwengu unafanywa upya

Na unafanywa mzuri kwa ukweli

Unaongozwa na mwanga wa uadilifu.

Kwa njia yako ubinadamu wenye dhambi unahesabiwa haki

Waliohukumiwa wanaokolewa,

Watumwa wa dhambi na jehanamu wanawekwa huru,

Wafu wanafufuliwa.

Kwa njia yako jiji tukufu la mbinguni

Linatengenezwa na kufanywa kamili.

Kwa njia yako Mungu, Mwana wa Mungu alinuia kwa ajili yetu,

‘kuwa mtiifu kwa baba, hadi katika kifo’,

Kwa ya hilo ametukuzwa na amepokea

‘jina lililo juu ya kila jina’.

Kwa njia yako ‘kiti chake cha enzi kimeandaliwa’

Na ufalme wake umedhibitika.

Ewe Msalaba,

Uliochaguliwa na kuandaliwa kwa wema usioelezeka,

Kazi iliyokamilishwa juu yako imekukweza zaidi

Kuliko sifa zote za mawazo na ulimi wa wanadamu na malaika.

Ndani yako na kwa njia yako ni wema wangu wote na ulio kamili;

‘mwiko kwangu kuona fahari isipokuwa katika wewe’

Kwani kwa nini nilitungwa mimba na kuzaliwa, na kupewa uhai,

Kama mwishowe nitupwe motoni?

Kama huo ndio hatima yangu ingekuwa vyema kwangu

Kama nisingezaliwa.

Na ni hakika ingekuwa hivyo

Kama nisingekombolewa nawe.

Kwa upendo gani nione fahari ndani yako, Ewe Msalaba,

Kwani bila wewe hakutakuwa na chochote cha kuonea fahari,

Na kwa milele nitakuwa na huzuni na taabu ya motoni.

Kwa furaha gani nishangilie ndani yako,

Ambapo kwa njia yako utumwa wa motoni ambao nimeurithi

Unabadilishwa kwa ufalme wa mbinguni.

Kwa shangwe gani nikusifu wewe

Ambapo bila wewe nautazama wakati ujao unaoniogopesha,

Hata japo ungedumu kwa kitambo kidogo tu,

Kwa njia yako sasa natazamia kufurahi milele.

Japo sasa namtumikia mungu kati ya matumaini na woga,

Ninauhakika kama nitamshukuru, kumpenda na kuishi utukufu wako,

Kwa njia yako mwishowe nitaufikia wema huo.

Basi fahari yangu iwe kwa njia yako na ndani yako;

Tumaini langu liwe kwa njia yako na ndani yako.

Kwa njia yako dhambi zangu zinafutwa kabisa,

Kwa njia yako roho yangu inakufa kwa maisha yake ya zamani

Na inaishi kwa maisha mapya ya uadilifu.

Ninakusihi wewe, nioshe kwa ubatizo kuto katika dhambi

Ambazo nimelitungiwa mimba na kuzaliwa,

Na nioshe mimi tena kutoka katika dhambi nilizozitenda baada ya kuzaliwa upya

Hivyo kwamba kwa njia yako nifikie mambo mema

Ambayo mwanadamu ameumbiwa kwayo,

Kwa nguvu za yeye Yesu Kristo Bwana Wetu

Ambaye amebalikiwa milele na milele. Amina.

(Tafsiri toka The Prayers and Meditations of Saint Anselm : Pd. Stefano Kaombe)

 

 

Demokrasia ya Pilato

Ndugu Mhariri,

Kwa ufupi neno "Demokrasia", maana yake ni utawala wa watu. Watu au raia wanavyoshiriki katika mamlaka ya juu na masuala yanayohusu jamii yao.

Katika mzingira tepetepe ya uchaguzi kama tunayokaribia kufikia kwa siku chache za usoni, mmoja anapoenda kwa watu hasa kikundi fulani na kuuliza, Hivi mwataka niwatendee nini?", anakuwa na maana gani?

Ponsio Pilato(Mrumi) aliyekuwa kiranja(prefect) wa Yuda(Kusini mwa Uyahudi), alipata nafasi nzuri ya kupendwa na watu(Mayahudi) na pia, kujipatanisha na maadui zake(Herode Lk. 23:12) kwa kumtoa Yesu.

Hapo mbeleni, Pilato alishatoa hukumu ya haki juu ya Yesu kwa kusema, "... Sikuona kwake kosa lolote katika mambo hayo mliomshitaki" (Lk. 23:14b).

Tujiulize swali, ni mambo yapi ambayo tunaweza kuyaweka katika hadhi ya kupigiwa kura na kutafakari hatua ya kusema wengi wape?

Kura zinapigwa, majadiliano nahata matakwa ya watu kufuatiwa na maslahi msingi ya jamii husika. Siyo yote tunayapigia kura.

Moja ya kazi kubwa za viongozi ni kulinda, kutetea na kutekeleza ustawi wa maadili ya jamii kwa haki.

Katika enzi za Yesu na hata sasa, kuna hatari ya viongozi wetu kupitia milango ya nyuma kuangamiza nguzo na maadili mbalimbali ya jamii katika azma yao ya kupata vyeo na sifa.

Mathalani mmoja atakwenda katika makundi fulani yenye muelekeo wa udini, ukabila, rangi utoaji mimba, madawa ya kulevya nakadhalika. Huyo naye, akajinadi "Mwataka niwatendee nini?" hapo, tutapotoka.

Jamani tusitoe sadaka maadili na tunu zetu mbalimbali mithili ya Pilato kwa kiu ya kupendwa au kujipatanisha na watu.

KIKOTI

TANGA