Make your own free website on Tripod.com

Wagombea semeni rushwa mapema msisubiri kushindwa

MARA baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita uliokuwa wa kwanza nchini kidemokrasia uliovishirikisha vyama vingi vya siasa, kesi mbalimbali zilifunguliwa kupinga matokeo yaliyowaweka madarakani baadhi ya waliokuwa wagombea wa ubunge.

Idadi ya kesi za namna hiyo ilikuwa na kasi ya kutisha kutokana na zilivyoongezeka kadri kulivyokucha.

Ni kweli kabisa baadhi ya kesi zilizofunguliwa zilifanikiwa kuthibitisha tuhuma mbalimbali zilizohalalisha kufutwa kwa matokeo na kufanya ulazima wa kuwepo kwa chaguzi ndondogo ukiachia mbali zilizotokana na kifo.

Tunatoa pongezi kwa wagombea wote walioamua kupinga matokeo hayo kutokana na waliokuwa wapinzani wao kukiuka kanuni na taratibu za uchaguzi ikiwa ni pamoja na wengine kutumia lugha za vitisho na matusi, kuanza kampeni kabla ya muda muafaka na kibaya zaidi, wengine kutumia mdudu huyu mbaya anayevuruga haki yaani, RUSHWA..

Kimsingi, tunahimiza Watanzania wote kuiga mfano na ujasiri wa kukemea rushwa kwa kipindi kama hiki ambacho endapo Watanzania hawataichukia na kuikemea, rushwa itazidi kushamiri na kutusababisha kupata viongozi walafi, waongo, wabinafsi, wapenda makuu, wenye tamaa ya kujinufaisha kibinafsi kwa mali na sifa na wauaji na kibaya zaidi, kuchagua viongozi watakaokuwa na mchango mkubwa katika kubomoa na kurudisha nyuma maendeleo ya jamii ya Watanzania.

Hata hivyo, licha ya kuwapongeza kwa kufanya hivyo, bado tunawalaumu na kuwaita wanafiki kwa kuwa kama waliokuwa wagombea walikuwa wanaona madhambi yote hayo yakifanyika hususani suala la mgombea kutoa rushwa kwa wapiga kura,

kama waliyashuhudia hadi kutoa vithibitisho mbele ya vyombo husika hata kuvishawishi vyombo hivyo kukubaliana na pingamizi na hivyo kuamua kutengua matokeo ya majimbo kadhaa ya uchaguzi, kwanini wagombea hao hawakuyasema na kuyathibitisha madai hayo kabla ya matokeo na badala yake wakasubiri matokeo yatangazwe na kuona kwamba wameshindwa, ndipo wafungue madai ya pingamizi?

Tunadhani, pingamizi za namna hiyo ni za kinafiki zinazomfanya yeyote aamini kwamba hata hao waliofungua pingamizi hizo walikuwa kushiriki tuhuma hizo na ndio maana hawakusema kwa wakati huo wakiwa na lengo la kusubiri kwanza waone kama mtaji wao utakuwa "umelipa" au la!

Tunasema ni wanafiki kwa taifa na hata kwa wapiga kura kwa sababu kwanza waliachia na kusababisha taifa kutumia mamilioni ya pesa ambazo zingetumika kutolea baadhi ya huduma za jamii walau kwa kiasi kidogo, lakini zikaenda kwenye chaguzi ndogondogo za marudio.

Pia, walikaa kimya ili baadaye wawatese wananchi wa majimbo husika kwa kuwapa utupu wa kukaa bila wawakilishi huku wakisubiri uchaguzi mdogo. Kadhalika walikuwa na mchango mkubwa katika kutoa adha kwa wapiga kura kutumia muda mwingine kujiandikisha na kupiga kura kuwachagua wawakilishi wao bungeni.

Hali kama hiyo ni dhahiri ilikuwa na mchango mkubwa katika kudumaza maendeleo ya sehemu zilizoguswa na wimbi la namna hiyo.Kimsingi sisi hatukatai mtu kupinga matokeo ya uchaguzi hasa anapobaini kuwa mgombea ameubatilisha.

Tunachokisema ni kwamba, wafichue tuhuma hizo mapema ili kuliepusha taifa kutumia mamilioni ya pesa kwa kurudia uchaguzi na kuwaondolea wananchi kero ya kuwa na vipindi vya kukaa bila wawakilishi pamoja na pia kuondoa kero ya kurudiarudia uchaguzi

Sisi tunaamini kuwa mgombea anayesubiri matokeo yatangazwe na baada ya kuona ameshindwa ndipo aanze kufungua kesi na kutoa mlolongo wa madai yakiwamo ya rushwa, ni dhahiri kabisa alikuwa anayaona tangia mwanzo lakini hakuweza kusema kwa kuwa naye alikuwa anafanya hivyo

Tunaamini kuwa sasa ameona mwenzie ametoa dau kubwa lililomzidi "kete", ndiyo maana sasa anakumbuka na kushituka "kuvuta shuka huku kumekucha". Huyo, sisi tunamwita mnafiki kwa kuwa anasubiri uumie ndipo aseme tatizo alilolijua tangu awali.

Tunalazimika kukumbukia uchaguzi uliopita kwa kuhofia taifa lisipoteze tena mamilioni hayo ya pesa na maelfu mengi ya dakika ambazo zingetumika kuleta maendeleo, sasa zitumike tena kurudia chaguzi.

Tunasema hivyo kwa kuwa ingawa siku rasmi ya kuanza kampeni haijafika, tayari kila kona ya nchi imeenea mazungumzo juu ya tuhuma za rushwa hasa kipindi hiki ambacho chama tawala kimekuwa katika zoezi la kura za maoni.

Hata hivyo tunaupongeza uongozi wa juu wa CCM kwa kujaribu kukemea kwa baadhi ya sehemu ingawa sehemu nyingine hazitajwi. Ni dhahiri hali hiyo inauonesha umma wa Watanzania kuwa bado taarifa hazifiki sawa sawa zinakohitajika kufika kwa usahihi.

Hali hii inatokana na viongozi wengi wa ngazi za wilaya na mikoa kugubikwa na magonjwa ya rushwa na ukabila kiasi kwamba hawatoi ushirikiano kwa Mkapa na Watanzania wengine wapenda haki.Swali tunalojiuliza kwa uchungu ni kwamba, kama kura za maoni tu, hali ya rushwa imegubika anga zima, hivi itakuwaje pale ambapo kinyang’anyiro hicho sasa kitakuwa cha kitaifa ambapo vyama vyote vya siasa vitashiriki uchaguzi ambao ndio wenye maamuzi ya mwisho?

Ni wakati muafaka sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB), Polisi, wananchi wote na hata wagombea kutokufumba macho wala kuoneana aibu bali sasa kuwasema wazi wazi wanaotumia rushwa ili wachaguliwe.

Tunasema kusubiri kwanza matokeo yatangazwe ndipo ufungue madai ya kupinga matokeo kwa sababu kama hizo ni unafiki unaowataka Watanzania wawaone wagombea walioshindwa na kufungua pingamizi kama waungwana kumbe ni "nyoka katika majani".

Mnaotumia mkorogo mnawinda nini?

Ndugu Mhariri,

Nitashukuru sana kupata nafasi kidogo katika gazeti lako la KIONGOZI ili niweze kutoa masikitiko niliyonayo.

Kwa muda mrefu tumekuwa tukisikia madhara ya kutumia haya madawa ya kutafutia weupe na urembo wa "kukopa Dukani" maarufu kwa jina la mkorogo kwa kuwa wengi wa wanaoyatumia, wameathirika vibaya ikiwa ni pamoja na kupata kansa ya ngozi au kutoshoneka kabisa pindi wapatwapo na "dhoruba" hata katika ajali.

Hii inadhihirisha wazi kuwa sisi wanawake hatuiheshimu ngozi yetu na pia tunafanya vitendo hivyo vya kujaribu kumkosoa na hivyo kumchukiza Mungu ndio maana karibia asilimia 99 ya watu wanaotumia mkorogo, ngozi zao huwa kama kenge, hata kenge ana unafuu kutokana na ngozi zao kubabuka.

Kwa kweli kama mtu una akili zako na unajua madhara utakayoyapata hapo baadaye, huwezi ukatumia mkorogo kabisa huku kila siku unasikia na kushuhudia matokeo kwa wengine.

Cha kushangaza, utakuta mtu mzima kabisa, ana familia yake lakini badala ya kuwa mfano bora wa kuigwa na watoto au wadogo zake, ndiye kwanza anatumia maelfu ya pesa ambazo zingesaidia kufanya kazi nyingine za maendeleo katika familia.

Hivi mnafikiri nyie mnapotumia mkorogo, mnategemea watoto watafanyaje? Nao si wataiga tu kile mnachowafundisha kwa matendo yenu wenyewe?.

Jamii inasisitizwa kutumia bidhaa zilithibitishwa viwango vya ubora wake. Je, akinadada na akina mama wenzangu washabiki wa mkorogo, hivi huo mchanganyiko maalumu umethibitishwa viwango vya ubora wake na TBS?

Hicho ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa kwani mchanganyiko ambao unatumika katika kutengenezea huo mkorogo ni hatari kabisa, huchanganywa vitu vingi kama vile Colgate, dawa ya madoa, sabuni ya Omo na nyingine zenye Cream, Dawa ya nywele "Relaxer"na Cream nyingine.

Sasa hamuoni kuwa huu mchanganyiko ni hatari kwa ngozi? Hebu fikiria mwenyewe dawa ya madoa inavyochubua mikono wakati wa kufulia sembuse ngozi ambayo ni laini na itaacha kuathirika au hiyo dawa ya nywele nayo mtu unathubutu kupaka halafu ndio unasema mwanamke deki?

Kwa nini mtu kabla hujaamua kufanya kitu usifikirie hapo baadaye itakuaje? na unavyopaka unapaka kwa malengo gani? na faida yake ni nini? pia madhara yake yatakuaje? Mpaka mtu unafikia hatua ya kumeza vidonge eti ili uwe mweupe? Halafu iweje? ukipata kansa ya utumbo utamwomba nani msaada wa matibabu? wakati yote hayo umejitakia mwenyewe?

Kwa nini mtu usibaki na ngozi yako halisi ambayo Mungu amekupa ambayo hata Wazungu wenyewe wanatafuta namna wanavyoweza kuwa na rangi hii tuliyopewa na Mungu lakini wanashindwa?

Siku hizi kumetokea na kasumba kwa akina dada kuwa mtu ukiwa mweupe ndio unapendwa. Nani amekudanganya? Kwanza hata hao wanaume nawashangaa sana wanaopenda wanawake wa namna hiyo, cha kusikitisha zaidi wewe mwanamke umeolewa, bado unajichubua, ili iweje?

Au unataka nani akupende zaidi ya huyo mumeo?, kwanza mumeo alivyokuoa aliipenda rangi yako ya asili iweje sasa unaamua "kujichuna" ngozi!

Wanawake wenzangu, tusidhani kuwa Mkorogo ndio fasheni hiyo ni kansa tupu ambayo tunaitafuta wenyewe ambapo baadaye tutakuja kupata tabu kupata dawa ya kutibu hiyo kansa tunayohangaika wenyewe kuitafuta kwa makusudi.

Kama umezaliwa mweusi, baki na weusi wako sio wote wanaopenda watu weupe au wanaotumia mkorogo. Kwanini usijivunie rangi uliyopewa na Muumba wako?

Ushauri wangu ninaowapa wakina dada na akinamama kwanini hizo fedha za Mkorogo usiende ukatoa sadaka kanisani, msikitini au ukawapa maskini kuliko kuchezea kwa kununulia kansa?

Kuna wengine wanashinda na njaa siku nzima kwanini hizo hela za kununulia huo mkorogo utakaokusumbua na kukuliza baadaye, usingempatia yeye akala?.

Msimsahihishe Mungu yeye alivyokupa rangi ya ngozi yako ana maana yake wacheni kumjaribu.

Silyvia Nauli,

Amana- Ilala

DAR-ES-SALAAM

PCB hamuoni rushwa katika kura za Maoni?

Ndugu Mhariri,

Nitafurahi sana endapo nitapewa nafasi kidogo katika gazeti lako nieleze niliyo nayo moyoni,

Mimi nashindwa kuwaelewa hawa wanaojiita kuwa ni Taasisi ya Kuzuia Rushwa nchini (PCB), hivi kweli hawayaoni matendo ya wagombea wa ubunge na udiwani namna wanavyojihusisha na vitendo vya rushwa katika nchi nzima?

Hivi mnataka kuieleza jamii kuwa hamuyaoni hayo yanayotendwa hasa katika kipindi kizima cha kura za maoni ndani ya chama tawala cha CCM?

Jinsi mlivyokuwa na kasi ya kuwakamata mahakimu wa makahama za mwanzo kwa rushwa za shilingi 3000/= au 5000/=, jamii ilitegemea kuwa katika hekaheka za uchaguzi mtafanyakazi kubwa kuliko hiyo lakini, mbona hatuoni makali hayo au rushwa kwa wagombea ni ruksa?

Au PCB nikidhani kwamba hamna mbinu za kuchunguza na kubaini namna rushwa za wagombea zinavyotolewa na badala yake mnasubiri tu ofisini, sijui kama nitakuwa katika usahihi.

Naomba mjue kuwa huu ni wakati muafaka kwenu kuwaelimisha wananchi zaidi na kukaza uzi mkitumia mbinu zote ili kuliepusha taifa katika balaa la kupata viongozi wabovu waliopatikana kwa rushwa wanaweza kuliyumbisha taifa kimaendeleo kwa siku za usoni.

Mjue kuwa kosa la sasa linaweza kulipatia taifa kilio cha maisha na kuligharimu taifa mamilioni ya pesa baada ya wagombea watakaoshindwa kufungua mashitaka dhidi ya rushwa.

Ninadhani ni mahala pa kukataa kesi za madai ya rushwa baada ya uchaguzi kwa kuwa kama yanafanyika sasa hivi wagombea wote wanaona, kwanini hawasemi mpaka wanasubiri baada ya matokeo.

Hii inaonesha kuwa nao wanashiriki moja kwa moja

Ninahofu hivyo kwa kuwa kama kwa kura za maoni tu hali imekuwa kama tunavyoona na kusikia kwenye vyombo vya habari, mambo yatakuwaje kampeni zikianza rasmi?

Mnasubiri uchaguzi upite halafu mtoe ripoti ya rushwa mtatoa kitu gani endapo wagawaji rushwa wapo na hamuwachukulii hatua?

Jamii itawaelewaje?

Amon Shayo

(Mkereketwa wa Tanzania)

SLP 10

MOSHI