Umuhimu wa upashanaji habari katika Kanisa

BINADAMU anayo mahitaji mengi sana, yale ya muhimu na yale ambayo siyo ya muhimu.Mahitaji ya muhimu ni kama vile chakula, maji, hewa, mavazi, mahali pa kulala nk. Na mahitaji ambayo siyo ya lazima ni kama vile mambo ya burudani, michezo, vinywaji na vileo nk. Lakini licha ya hayo mahitaji ya lazima kuna hitaji moja kubwa ambalo pengine husahauliwa na kumbe ni la lazima kabisa kwa maisha na usalama wa binadamu anapoishi katika jamii. Hitaji hilo ni lile la Mawasiliano au Upashanaji Habari.

Ili binadamu aweze kuishi maisha ya usalama na pia aweze kuwa na mendeleo yo yote yale hana budi kuwa katika mawasiliano na ulimwengu unaomzunguka, yaani na binadamu mwenzake pamoja na mazingira anamoishi. Binadamu inampasa apate habari kutoka kwa binaadamu mwenzake naye pia inampasa atoe habari kwa yule aliye kando yake. Upashanaji huo wa habari huanza mara tu binadamu anapozaliwa mtoto mchanga atatoa habari kama ni mzima kwa kulia licha ya vitendo vingine.

Kuna aina mbalimbali za kupashana habari ya kwanza kabisa ni ile ya ana kwa ana, yaani kwa njia ya kuzungumza mtu na mwenzake wakitumia lugha ya maneno au hata wakitumia lugha ya vitendo vya viungo vya mwili. Binadamu katika utamaduni wake amekuwa pia akitumia vitu mbalimbali kama ishara ya kupashana habari kama vile moshi, ngoma, baragumu nk. Katika kujiendeleza kielimu, binadamu ameweza pia kugundua namna ya kuwasiliana na mwezake kwa njia ya maandishi, yaani vitabu, magazeti, uchoraji wa pia nk. Uandishi wa vitabu ulianza zamani sana, na hivyo tumekuwa na vitabu vyenye elimu kubwa sana katika ulimwengu huu, na kitabu kikubwa sana ni kile tunachokiita ‘BIBLIA’.

Licha ya Upashanaji Habari kwa njia ya maandishi, maendeleo ya sayansi na tekinolojia yametuletea radio na televisheni katika ulimwengu wetu huu. Kwa hiyo siku ya leo kuna mawasiliano kwa njia ya radio na televisheni, fax, internet, simu za mkononi nk. Tunaweza kusema kuna maendeleo makubwa sana katika uwanja huu wa mawasiliano na upashanaji habari kwa ujumla.

Katika Hati ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano kuhusu Vyombo vya Habari tunaambiwa kwamba kati ya maajabu makubwa ambayo binadamu amefanikiwa kuyagundua moja wapo ni hilo la Vyombo vya Upashanaji Habari. Hivyo Mtaguso unahimiza kabisa Kanisa, yaani Wahubiri wanapaswa kutumia Vyombo hivyo vya Upashanaji Habari katika kutangaza Habari Njema. Kwa hiyo Kanisa linashauriwa kutumia siku hizi radio, televisheni,simu na vyombo vingine vya kisasa katika kuhubiri Habari Njema kwa ulimwengu wa kileo. Ili kulitilia maanani jambo hilo Kanisa licha ya kutumia Vyombo hivyo, limeweka Siku moja katika mwaka iwe ni hasa siku ya kuwakumbusha waumini kuhusu Vyombo hivyo vya Habari, na pia kuhimiza utumiaji wa vyombo hivyo, pamoja na kuwaombea wale wote wanaotumia vyombo hivyo vya Upashanaji Habari katika kueneza Neno la Mungu.

Katika siku hiyo ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, Baba Mtakatifu, kama kiongozi wa Kanisa na Mchungaji Mkuu hutoa Hati maalum yenye Ujumbe mahsusi. Dhamira ya Ujumbe wa siku ya Habari ulimwenguni mwaka huu inasema: ‘Kutumia vyombo vya Habari katika Kumtangaza Kristo mwanzoni mwa milenia mpya’. Baba Mtakatifu anawaalika waumini wakatoliki na wale wote wenye mapenzi mema kutumia vyombo vya habari vya kisasa katika kutangaza na kueneza Neno la Mungu. Kwa hiyo waumini wanahimizwa kusoma vitabu vya kidini, kusikiliza vipindi vya dini kutoka radioni, kuangalia na kusikiliza vipindi vya dini katika televisheni. Na kwa upande mwingine wale wenye utaalamu wawaandalie waumini vipindi vizuri vya dini.

Kwa kawaida siku ya upashanaji habari katika Kanisa Katoliki la Tanzania huadhimishwa Jumapili ya Kwanza ya Mwezi Agosti, na mwaka huu ilikuwa ni tarehe 6.8.2000. Lakini pia kuna mazoea ya kuiadhimisha siku ya Upashanaji Habari kitaifa kwa kuzunguka katika Majimbo mbalimbali. Mwaka huu ilipendekezwa iadhimishwe Jimboni Tanga. Kwa kuwa kulikuwa na matatizo, basi siku hiyo haikuadhimishwa hapo tarehe 6 Agosti, na badala yake inaadhimishwa tarehe 13.8.2000. Adhimisho hilo la siku ya Habari linatanguliwa na Warsha kwa ajili ya Wakurugenzi wa Upashanaji Habari katika Majimbo ya Kanda ya Mashariki.

Jambo la mafunzo katika kutumia vyombo vya habari hutiliwa mkazo mkubwa sana. Wakurugenzi wa Habari Mjimbo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuvitumia vyombo hivyo vya habari. Wanapaswa kujua namna ya kuandika habari na makala na pia kutayarisha mazungumzo ambayo hutolewa katika radio mbalimbali. Kwa siku hizi vile vile wanapaswa kujua namna ya kuandaa vipindi kwa ajili ya Televisheni. Kwa mneno mengine ni sharti waandaaji wa vipingi na program mbalimbali wawe na ujuzi utakaowafanya wasikilizaji na watazamaji wapende kusikiliza na kuangalia kwa makini na hivyo kufaidika vilivyo.

Kwa hiyo basi tunapenda kutoa rai yetu kwa waumini wote watumie vyombo vya habari katika kujinufaisha vilivyo. Inasikitisha kuona kuwa waumini wengi hawasikilizi vipindi vya dini redioni na wala hawaangalii vipindi vya dini katika televisheni. Pia ni waumini wachache wanaosoma vitabu na magazeti ya kidini kama vile Gazeti letu tukufu la KIONGOZI. Basi, yafaa kabisa wazazi, walezi wawahimize watoto wao kusoma magazeti na vitabu vya kidini, kusikiliza vipindi vya dini kutoka redioni, na kuangalia katika televisheni vipindi vya kidini.

Wanawake Tanzania ondoeni unyonge wenu

Ndugu Mhariri,

WANAWAKE kote Duniani kwa maumbile yao wamekamilika. Wanaume kadhalika. Tangu Adamu na Hawa binadamu wako vile vile hadi leo hii kwa maumbile yao kama Mwenyezi Mungu alivyowakusudia na hii ni kwa utukufu wake.

Kama hivyo ndivyo na wanawake wa Tanzania wanakubali hivyo, nashangaa kuona wanakaidi ukweli huo kwa matendo yao. Tazama wanavyochuna ngozi yao ya asili wanasema ‘Mkorogo’ ili kuibadilisha ngozi yao iwe kama ya Mzungu au ya Mhindi. Tena wengine wasomi na Digrii zao kichwani. Tazama wanavyoangaika kubadilisha nywele zao na kujiremba ili wawe kama maua au mapambo ya maonyesho.

Ni dhahiri tabia kama hizi zinatokana na kutojiamini. Tunasikia viongozi wao wakisema kila mara wakidai haki zao.

Vema, bahati njema katiba ya nchi hii imetoa nafasi wazi sawa kwa akina mama na akina baba na serikali tayari imekwisha panga utaratibu wa kupokea malalamiko au kudai haki katika vyombo vya siasa au vikao vya Kisheria kwa hilo hakuna tatizo.

Tatizo ni kwamba akina mama wa Tanzania hawajiamini. Mimi nashindwa kuelewa ni lini Tanzania tutaweza kupata Rais Mwanamke ikiwa bado Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania kwa unyonge wao bado wanakubali kuwa jumuiya ya Chama cha Mapinduzi au Chama chochote cha siasa.

Sekta hii ya wanawake inapaswa iwe huru inayojiamini na inayojitegemea. Ikibidi wadai sekta yao itoe Mgombea wa nafasi ya Urais Mwanamke ashindane na wagombea wengine.

Wasingoje kila mara kupewa nafasi za upendeleo, watapendelewa hadi lini? Tunataka washike nafasi wanazostahili sio kwa kupendelewa.

Kwa dokezo mimi naamini Adam na Hawa walikuwa Waafrika.

Kamwe sitamani kuwa walikuwa wazungu, sitamani rangi ya ngozi ya Mhindi au Mchina.

Sikubali usemi kuwa majina ya kiarabu ndiyo yenye baraka mbele ya Mungu na kwamba majina yetu ya Kibantu ni ya kishenzi, kwani huko ni kuikana nafsi yangu. Unyonge kama huu kwangu ni dhambi kuwa nao.

Wakina mama Hoyee

E.G Msuguru

S.L.P 45471,

Dar Es Salaam