Tushiriki katika Uchaguzi Mkuu

HIVI sasa nchini Tanzania kuna lile vuguvugu la Uchaguzi Mkuu wa Wabunge na Rais. Kwa muda huu kunafanyika zile kura za maoni ili kuweza kuwapata wagombea wenye sifa zifaazo ili kuweza kuchaguliwa hapo baadaye na wananchi wote. Tunafahamu kupita katika kura za maoni bado siyo uhakika kwamba mgombea ameshapita, lakini husaidia katika kujua nani anakubalika na wananchi na hivyo kuweza kupita kwa asilimia kubwa katika uchaguzi ujao.

Maaskofu Wakatoliki hapa nchini wanafundisha kwamba ni wajibu wa kila raia na hasa kila mwumini kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.Wanasema kuwa wale ambao wanajiona kuwa ni wenye uwezo basi wanawajibika kugombea sehemu mbalimbali za uongozi. Kwa hiyo inawapasa kutumia karama zao za uongozi walizojaliwa na Mwenyezi Mungu. Kwa kawaida siyo wengi wenye karama hizo za uongozi na hivyo kuweza kuwa Wabunge au madiwani. Kuna sifa maalum zinazotakiwa kwa kila mtu anayetaka kugombea nafasi ya uongozi. Lakini sifa kubwa kwa wale wanaotaka kugombea uongozi ni kuwa na moyo wa kuwapenda raia wenzao na hivyo kuwa tayari kuwahudumia. Ikiwa kiongozi hana upendo, basi hataweza kuwafaa raia au wale wanaomchagua. Ikiwa kiongozi atakuwa na sifa hiyo ya upendo, basi atakuwa mwaminifu, mwadilifu, asiye na ubinafsi na mwenye kujitoa kabisa kwa ajili ya wale waliomchagua, yaani wananchi.

Wakati tunapongojea ile siku ya siku ni wajibu wetu sisi raia kuwachunguza hao wagombea wetu ikiwa kweli wanazo sifa zitakiwazo kama viongozi na hasa kama wabunge wetu. Kwa kura za maoni siyo maana yake mambo yamekwisha, basi hapo kazi inaanza. Tunapaswa kujiuliza kweli hayo maoni tunakubaliana nayo ama sivyo? Sisi wapiga kura bado tuna muda na uhuru wa kukubali au kukataa hayo maoni, kwa vile ni maoni.

Hivi karibuni kiongozi mmoja wa Kanisa Katoliki amesema kuwa kutokwenda kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaofaa ni kosa na tena ni dhambi kubwa. Hiyo ni dhambi ya kutokutimiza wajibu wetu kwa umma kwani inatupasa kufanya hivyo kutokana na maagizo ya mafundisho ya Kanisa kwamba inatupasa tuheshimu uongozi na utawala wa kidunia. Popote siku hizi kanisa linafanya juu chini ili kuwaelimisha wananchi kuhusu wajibu wao katika suala zima la upigaji kura.

Maendeleo ya binadamu licha ya jitihada zake binafsi hutegemea sana viongozi alio nao. Kazi ya viongozi kama tunavyofahamu ni kuongoza, ni kuelekeza na pia kudumisha haki na amani katika taifa. Kwa hiyo tunawajibika kuwachagua viongozi wenye sifa zitakiwazo ili waweze kutuongoza. Kazi hiyo itafanikiwa vizuri sana ikiwa kila mwananchi atatimiza wajibu wake ipasavyo. Kwa hiyo tuna imani kwamba wananchi wengi na hasa waumini watajitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa ajili ya upigaji kura. Tunarudia tena kusema kuwa ni kosa kubwa kwa raia na ni dhambi kwa mumini kutokwenda kujiandikisha na kutokwenda kupiga kura siku ya upigaji kura. Si vema kupuuzia wajibu huo wa kupiga kura kwa kufanya hivyo ni kuliletea taifa hasara. Yawezekana kuwa ni kura yako wewe au yangu mimi ndiyo itakayosababisha tupate kiongozi wa kufaa. Ikiwa hutashiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao, na hivyo kupatikana viongozi wasiofaa hapo ujue kuwa nawe umesaidia kwa namna moja au nyingine katika kuwa na viongozi wabovu.

Hapo tunapenda kuwahimizi wananchi wote walihangaikie suala hilo la uchaguzi kama ni zoezi la kufa na kupona. Hao viongozi tunaokwenda kuwachagua wawe kweli ni kutokana na kuwafahamu kwa undani kabisa. Tunataka uchaguzi wa mwaka huu utuletee viongozi wanaofaa kweli kutuingiza katika karne hii ya 21 ya sayansi na tekinolojia. Hapo hatuna budi kuona kwamba kamwe hatutawachagua viongozi wetu kufuatana na kila wanachotupatia kama zawadi, bali hasa ule moyo wao wa kujitoa mhanga kwa ajili ya ujenzi wa taifa letu.

Wahenga wanatuambia kwamba chema cha jiuza chenyewe, lakini kibaya chajitembeza. Hivi karibuni tutaanza kushuhudia wale wagombea wanaojitembeaza na wale wanaojiuza.Tunaamini kwamba wale ambao wanazo sifa kweli za uongozi watokeapo tu mbele ya watu watakuwa tayari wamejiuza. Lakini wale ambao hawanazo sifa hizo itatakiwa wafanye kazi marudufu katika kujiuza na kutumia hata pengine rushwa na vitendo mbalimbali vya udanganyifu na ulaghai. Watanzania kwa ujumla tunayo mang’amuzi makubwa sana kuhusu suala hilo la uchaguzi na hivyo tunaamini kwamba kwa mwaka huu mambo hayatakuwa kama siku za nyuma yaani kulizembea jambo la uchaguzi.

Kwa hiyo tunapaswa kuzingatia mambo hayo mawili kuhusu uchaguzi. Kwanza ni lazima kabisa twende huko vituoni tukajiandikishe. Baada ya kujiandikisha ni lazima tuishi tukiwa na kumbukumbu ya hiyo siku ya siku ya kwenda kupiga kura yetu kule kituoni. Ni jambo la aibu na tena la fedheha kubwa sana kuona kuwa baadhi ya wananchi walizembea jambo hilo. Kwa wale waumini wakristo tunawashauri waige mfano wa kiongozi wao, Bwana wetu Yesu na wazazi wake,Maria na Yosefu ambao walikuwa tayari kutimiza wajibu wa kiserikali bila manung’uniko. Walikwenda kujiandikisha kule Betlehemu licha ya mazingira magumu waliyokuwa nayo. Hivyo nasi tunapaswa kufanya hivyo kwa sababu ni wajibu wetu.

Kwa upande mwingine hao wenye kutoa rushwa na zawadi wanatambua kabisa kasoro zao na hivyo hutumia njia hizo ili kuziba hizo kasoro. Ikiwa kweli mgombea anazo sifa za kufaa siyo lazima afanye mambo ya rushwa au kutoa zawadi. Lakini kwa kila mpiga kura ikumbukwe kwamba, licha ya hizo zawadi anapasika kubakia mwenye msimamo wa kumchagua yule anayefaa na siyo yule ambaye amempa zawadi.

Tunaamini kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa ni kweliwa kihistoria kwa vile ni wa kwanza katika milenia mpya, katika karne mpya ya sayansi na tekinolojia. Kwa hiyo ni jambo zuri kama sote ambao tuna haki ya kufanya uchaguzi huo tufanye kwa kutumia maarifa na juhudi zetu za kisayansi na kitekinolojia. Sote tunapaswa kujivunia fursa hii tuliyoipata ya kufanya uchaguzi wakati tuanzapo milenia mpya. Basi tuitumie vema kwani tunaingia katika historia ya karne hii.Vizazi vijavyo vitatukumbuka kama tulikuwa wa kwanza kufanya uchaguzi mkuu mwanzoni mwa karne hii.

Mahubiri ya Wakatoliki Jangwani; ni kielelezo tosha cha kutimiza habari ya Yesu kwa wanadamu

Ndugu Mhariri,

KIONGOZI liko mbele yangu Toleo la Julai 8-14- 2000.

Kwa furaha kubwa na ya pekee nilisoma WAKATOLIKI WAAMBIWA AMKENI KUMEKUCHA.

Ahsante sana kwa taarifa hiyo katika Gazeti tukufu la KIONGOZI Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa neema hiyo ya kukutanisha waumini wa madhehebu mbalimbali kwa jina la Yesu na kusahau walau kwa muda mfupi tofauti zote kati ya madhehebu na kuelekeza moyo na masikio ya roho kwa habari Njema Yesu aliyokuja kututangazia sisi wanadamu.

Hakika, kama niko Dar es Salaam, ningalikuwa mstari wa mbele kati ya wasikilizaji na siyo kama msikilizaji tu bali kama mwamini wa moyo wangu wote. Tena ningejiona siyo hasa kama Mkatoliki ama Mroma ama Mluther ama wa Kanisa gani, bali kama ndugu katika Kristu kati ya wote.

Sasa hivi nakumbuka usemi mmoja niliofundishwa nikiwa bado kijana mdogo:

UIHESHIMU IMANI YA KILA BINADAMU, YA KWAKO LAKINI UIPENDE.

Mungu awajalie Waumini wa Yesu Kristu Mwanga na Nguvu ya Roho Mtakatifu kuzidisha utangazaji wa Habari Njema kwa njia ya Ushuhuda wa maisha.

Ahsante Mungu

Nakushuruku tena nikikusalimu katika Kristu,

Wako

Amandus Brigger, OFMCap

Postfach 1269

CH- 9500 WIL 2

Switzerland

Wanakibakwe-Achana na "aguzile egumbi ni nyama kanyi kuna maulaga ndugu"

Ndugu Mhariri,

Tafadhali niweke japo pembeni mwa Gazeti lako tukufu ili nitoe yangu machache kwa wenzangu wa Kata ya Kibakwe na Jimbo la Uchaguzi la Kibakwe wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma.

Wana - Kibakwe wenzangu, ninyi wenyewe mmekuwa mashahidi kwa macho yenu mkishuhudia jinsi rushwa zilivyokuwa zikitendeka wakati wa msafara wa Kura za Maoni kwa ndugu zetu madiwani.

Wamekuwa wakitoa fedha hadharani, wakinunua mapombe, manyama ili wapite katika kura za maoni kuwania nafasi za udiwani.

Kwa nini hawajiamini?Kama ulifanya vizuri huko nyuma wasiwasi wako nini kwa wakati ujao? Au kama unajiamini yanini kutoa mapombe, manyama na mahela kuwavuta watu (wasio na msimamo) kukupigia kura? Je utafanya miaka mitano yote kila siku?.

Wananchi wamekuwa wakigawiwa kadi na kuandikiwa risiti zenye tarehe za nyuma kuonyesha kuwa ni mwanachama wa zamani ili wapiga kura. Na baya zaidi mambo haya yalitendeka na wakapiga kura. Je huo ndio utu, na uaminifu kwa taifa?.

Wenzetu hawa wana usemi usemao, NITASEMA KWELI DAIMA, UONGO, FITINA KWANGU NI MWIKO, RUSHWA NI ADUI WA HAKI". Je ni yapi waliyoyatenda kwa sasa ndio wanaoongoza kwa rushwa , uongo na mengine mabaya kama haya.

Wana- Kibakwe, kama hatutakuwa makini tutaongozwa na viongozi wabovu wapenda madaraka, sifa na vyeo wasizostahili na kuturudisha nyuma katika maendeleo yetu tukilinganisha na majimbo mengine. KWA NINI TUNAMZIKA MTU MZIMA NA KUMUACHA ALIYE KUFA? Mmesahau mnanunua madawa,mnachangia madawati, kodi mnalipa, mabarabara mabaya, matumizi ya shule hamsomewi, ya kijiji hamsomewi. Malalamiko kibao, Je huyo anayegombea tena amesahau kuwa huyo huyo amelalamikiwa lakini kayapa kisogo?? Leo nataka kumdanganya nani? Anajijua kuwa hafai hatakiwi ndiyo maana ananunua pombe, nyama, mapilao na kugawa fedha kwa wapambe wake wampigie debe apite tena kuna historia gani itakumbukwa kwa jina lake.. tuache kile cha "Aguzile ugumbi ni nyama kanyi kuna maulaga ndugu (Pilao,Wali) mtubite tukang’we, Tukadye".

Tuchague mtu mwenye sifa za Uwakilishi siyo ujumbe wa posho.

Wasalaam

Damascus A. M Gollan

Kijiji cha Kibakwe,

S.L. P. 114

Mpwapwa - Dodoma.

Serikali ichunguze kwa makini tofauti ya mapato

Ndugu Mhariri,

HAKUNA Mwanadamu aliyekamilika na akaonekana bora kwa kila jambo (wasemavyo wanadamu wengi) atendalo au kwa kila hali alivyo kamwe hatakosa dosari.Ubaya au wema ulio wazi ndio unakuwa nuru iliyotambuliwa na kupewa sifa hiyo kwa mhusika. Mpera hujaa mapera na mpapai kamwe haujai fenesi.

Vuguvugu za uchaguzi zilipoanza tu ilani za aina aina zilitolewa hata hivyo ni vigumu kuchambua yote yanayohitajika kwa ukamilifu wake.

Kukubali kupokea madaraka ni kujiamini kuwa na uwezo wa kuongoza au kutawala kulingana na katiba katika kuyapokea madaraka si rahisi kukataa mambo yote yapo sawa. Inabidi naye achambue lipi la kuendeleza lipi la kuacha na lipi la kuongeza na kadhalika wanaongozwa au kutawaliwa wana mtazamo tofauti kulingana na maongezi yaliyopo.

Watu au nchi hudai kujitawala ni kwa sababu ya kutaka kupata unafuu wa maisha na heshima kwa wote, lakini hayo ni kinyume hapa petu Tanzania. Awamu ya kwanza mambo shwari au nafuu. Elimu, matibabu na mengine mengi ilikuwa nafuu na heshima pia ilikuwepo.

Awamu ya pili ya ruksa ikawa ndio njia panda kutokana na kuvunjwa ujamaa na kujitegemea mambo yote yakafuata mkondo wa ubepari ambao mpaka sasa kufikia tabaka la mabwana (viongozi na matajiri) na watwana ndio akina sisi.

Awamu ya tatu imerithi yote ya awamu ya pili kero kwa wananchi zimebaki zilivyo na kuongezeka . kutokana na kukidhiri rushwa hivyo upatikanaji wa huduma zote muhimu ni kwa rushwa; hospitali, polisi, mahakama na penginepo pote hata kuosha au kutunza maiti, uonevu umezidi sana na hakuna huruma kabisa. Viongozi hawaonekani kirahisi kama zamani ila siku za kampeni sababu ya kuonekana wakati wa kampeni inajulikana.

Ili madhara na kero zisizidi inabidi serikali kwanza ichunguze kwa makini tofauti ya mapato. Kuwepo na mikutano ya mara kwa mara ili kupata malalamiko (kama si maoni) ya wanyonge. Kila Kiongozi awe macho kwa wale wa chini yake na kuwadhibiti bila upendeleo au kulindana. Laiti mtindo uliopo sasa bila kuwa na mabadiliko tutajikuta kuwa lila na fila.

Wenu,

Mzee S. Ngunga

Merry Water Ltd.

S.L.P 7472

Dar es Salaam.