Makanisani Wiki hii

Balozi wa nyumba kumi ana haki sawa na Rais-Mchungaji

Na Mwandishi Wetu

MCHUNGAJI wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG),John Mmasy amesema kuwa ukimtukana balozi wa nyumba kumi ni sawa na kumtukana Rais wa nchi.

Mchungaji Mmasy alitoa kauli hiyo Jumapili iliyopita wakati alipokuwa akitoa mahubiri katika misa iliyofanyika katika kanisa la TAG, Ilala Jijini Dar-Es-Salaam.

Mchungaji huyo ambaye anatokea katika kanisa la TAG Kibosho mkoani Kilimanjaro, alisema mtu yoyote hana mamlaka ya kumtukana balozi wa nyumba kumi ama kiongozi yeyote wa serikali.

"Wewe kama Mkristo uliyeokolewa, ni marufuku kumtukana balozi wa nyumba kumi. Pia, yeyote anayejihusisha na masuala ya serikali," alisema Mchungaji Mmasy na kuongeza, "Utakapofanya hivyo tayari kabisa umemtukana Rais wa nchi na hapo utakuwa umeenda kinyume na matakwa ya Mungu".

Alisema kuwa kitendo hicho ni sawa na kumtukana mhubiri wa Mungu ama kiongozi yeyote aliye na mamlaka ya kuongoza kondoo wa Mungu badala ya Mungu mwenyewe.

Mchungaji Mmasy alisisitiza kuwa hakuna serikali iliyo macho kama serikali ya mbinguni kwa hiyo waliokolewa ni lazima wamtetee Bwana hata kama wafilisi wanawakata vichwa.

Aliwataka watumishi wa Mungu kujiona kama mawakala wa Mungu na siyo mawakala wa Ulimwengu.

Kauli hiyo ya Mchungaji Mmasy imekuja wakati ambao baada ya mfumo wa siasa wa vyama vingi nchini, baadhi ya wananchi wamekuwa wakiwapuuza na kuwakejele watendaji wa ngazi mbalimbali hasa mabalozi wa nyumba kumikumi na wenyeviti wa serikali za mitaa kwa madai kuwa hawawezi kuwatii kwa kuwa ni viongozi wa vyama tofauti na vyao hali ambayo ni ukosefu wa fikira sahihi.

Msiwe mabubu, viwete, tumieni karama kukomesha maovu- Wito

lTEC wafyatua kibao kipya, kinasema, Wapendeni Adui Zenu

Na Leocardia Moswery

MKURUGENZI wa Chama cha Kitume cha Wanafunzi Wakatoliki, Vyuo na Sekondari Tanzania(TYCS),Padre Lucas Mzuanda ametaka jamii kutokuwa viwete wala mabubu katika kukemea maovu bali watumie karama kuondoa machafuko.

Padre Mzuanda alitoa kauli hiyo Jumapili iliyopita wakati wa ibada ya Misa Takatifu iliyfanyika katika Kanisa la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Jumapili hiyo iliyokuwa kwa ajili ya kusherehekea Jubilei ya Walimu Ulimwenguni ambapo kwa upande wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam ilifanyika kituo cha hiaja Pugu,Padre Mzuanda alisema imekuwa ni kawaida kwa watu kubweteka na kuwa bubu badala ya kutumia karama zao kusaidia makundi ya masikini na kuleta amani amani.

"Watu kwa kushindwa kutumia karama zetu,pia tunashindwa kuishi maisha mema, tumekuwa viwete wa dhambi na kuuana ovyo bila sababu" alisema Padre Mzuanda.

Alisema watu wanachinjana bila kujali huyo ni mwanadamu damu inamwagika bila huruma na huko ni kuwa bubu na kuwa kiwete kwa Taifa la Mungu linaposema.

Alidai wakati Kanisa linasherehekea Jubilei Kuu na Mwaka wa Neema, Wakristo hawana budi kumgeukia Kristo Msalabani bila kujali tofauti zilizopo katika jamii zikiwamo za kidini, rangi, na ukabila.

Alisema mwaka huu mtakatifu hauna budi kutumika kukomesha mateso kwa wote wakiwamo wasiojiweza na kukomesha mauji yanayozidi kutokea ovyo.

Wakati huo huo: Kikundi cha Kwaya ya Watakatifu Wote cha TEC, kimerekodi nyimbo za dini ukiwemo ule usemao "Wapendeni adui zenu" inayotarajiwa kuuzwa hivi karibuni.

Mwenyekiti wa Kwaya hiyo Bw.Dismas Sambala, aliliambia KIONGOZI mwishoni mwa wiki alisema kuwa "WIMBO WAPENDENI ADUI ZENU una ujumbe uilobeba kanda nzima kutokana binadamu walivyo na kwamba wanatakiwa kuwapenda adui zao bila kuonesha chuki dhidi yao. Tunawachukia," alisema Sambala.

Alisema kikundi hicho chenye wanakwaya wasiozidi 30 kilirekodi wiki kanda hiyo iliyopita katika studio za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambapo ndiyo mara ya kwanza kurekodi nyimbo hizo.

Hata hivyo alisema kuwa kanda hiyo itaanza kuuzwa hivi karibuni baada ya kuzalisha nyimbo ambapo wanategemea kutoa kanda ya Televisheni ya Taifa(TVT) ya jijini Dar-Es-Salaam.

Msalaba wakusanya shilingi milioni 2.7 parokiani

Na Getrude Madembwe

ZAIDI ya shilingi 2.755, 266 zimekusanywa katika mzunguko wa Msalaba wa Jubilei katika Parokia ya Mtongani iliyopo Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, katika vigango vya Mtakatifu Dominico, Maria De Mathias na Yohane Merlini.

Pamoja na ukusanyaji wa fedha hizo pia watoto 114, walibatizwa na watu 4 walibadili dhehebu kuwa Wakatoliki kati ya hao walibadilisha madhehebu ambapo wawili kati yao ni Waislamu na mmoja ni Muanglikana, wakati mwingine ni Mlutheri.

Pia, siku hiyo ndoa mbili zilifungwa.

Wakielezea maajabu ya msalaba huo katika kigango cha Yohane Merlin kilichopo Mbezi Beach eneo la Tangibovu jijini Dar-Es-salaam, Sisata Juliana Joseph na Sista Scholastica Nyongo, walisema kuwa msalaba huo wa Jubilei ni wa Parokia,na lengo ni kuinjilisha Ukristo katika jumuiya na kuamisha upya jumuiya ndogo ndogo.

"Tumeamua kuwa na msalaba huu wa Jubilei ili kuinjilisha Ukristo katika jumuiya zetu na kuziamsha upya zile jumuiya nyingine ndogondogo," alisema Sista Scholastica.

Katika Parokia hiyo kuna jumla ya jumuiya ndogondogo 28 ambapo kigango cha Mtakatifu Dominico kuna jumuiya kumi, Maria de Mathias jumaiya 8 na Yohane Marlini kuna jumuiya 10.

Naye Sista Juliana alisema kuwa, msalaba hukaa katika familia kwa siku moja na kesho yake hukabidhi kwa familia nyingine na akaongeza kuwa msalaba huo kwa sasa upo katika kigango cha Yohane Merlini na ulianzia katika kigango cha Mt. Dominico, na kila kigango hukaa kwa muda wa wiki moja.

Wakatoliki waambiwa tena watue viroba saba

Na Mwandishi Wetu

KWA mara nyingine, Wakristo wametakiwa kuvitua viroba saba vya dhambi walivyojitwisha kumpa nafasi Kristo atawale ndani ya maisha yao.

Kauli hiyo ya viroba saba ikiwa na tafsiri ya Mkristo kuacha uvivu, uzinzi, uchoyo, kiburi, ulafi na wivu wa asili imetolewa na padre John Rupia, alipopokea maandamano ya Hija ya Parokia ya Mtakatifu Maurus- Kurasini katika Jimbo Kuu katoliki la Dar-Es-Saalam, Jumamosi iliyopita.

Akizungumza siku hiyo katika kituo cha Hija cha Pugu Padre Rupia aliwataka waandamaji hao kujitua mzigo wa viroba saba ili kumkiri Kristo na kumkaribisha ndani ya mioyo yao.

Aliwaonya kamwe wasivirejee viroba hivyo vya dhambi wala kumpa nafasi shetani.

Kabla ya kupokea maandamano hayo yaliyoongozwa na Paroko wa Parokia ya Kurasini na kutumbizwa na vikundi vya kwaya ya Drums of Heaven Steel Band.

na kwaya ya St. Maurus vilishiriki kutumbuiza katika jubilei hiyo ambayo iliazimishwa jumamosi siku moja kabla ya jubilei mwanzoni mwa juma

Katibu wa parokia hiyo Bw. Cleatus Majani, ameitaja hija hiyo na Msalaba wa jubilei kuwakichocheo kikubwa cha mafanikio ya kiroho kwa waamini wa parokia yake hasa baada ya wengi kujitokeza kushiriki kwa wingi kuliko ilivyotarajiwa.

"Kweli waamini wamepata mwamko mkubwa Mwaka huu Mtakatifu. Walijitahidi kutoa michango na magari mengi yalikuwepo kwa ajili ya kuwachukua, wamekubali maana hija ni tendo muhimu. Hakuna aliyetegemea kuwa hali itakuwa hivi," alisema majni na kuongeza,

"Ujumbe uliotolewa katika Jubilei uwe bendera ya wokovu. Hija kama safari ya kiroho, tuitumie kama nafasi sahihi ya kumuongokea Mungu."

Majani aliwasisitiza waamini kuzingatia mahubiri yaliyotolewa na padre Rupia kwa kutovirejea viroba saba na kuitumia hija hiyo kama uongofu kamili na mabidiliko ya kiroho.

Hivi karibuni akipokea maandamano ya Jubilei ya wanaume wapatao 200 Padre Rupia aliwataka wanaume kujitua mzigo wa viroba saba ambavyo ni dhambi inayomfanya Mkristo ashindwe kuishi ndani ya Yesu.

Katika jubilei hiyo, wanaume walilishwa chumvi ili iwe kichocheo katika kuanzisha na kuendeleza jumuiya ndogo ndogo za Kikatoliki katika maeneo yao.