Makanisani Wiki hii

ASKOFU AWAAMBIA VIJANA:

Epukeni utamaduni wa kifo

Na Leocardia Moswery, Mbulu

VIJANA wameshauriwa kujenga utamaduni imara wa uhai na kuachana kabisa na masuala yote yenye mwelekeo wa kujenga utamaduni wa kifo.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu,Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi, wakati akiongoza ibada ya shukurani kwa waamini waliohudhuria sherehe za kubariki Kanisa Kuu la Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni hivi karibuni mjini hapa.

Alisema vijana hawana budi kujitambua dhahiri kuwa wao ndio hazina ya Kanisa na hivyo ni jukumu lao kujenga na kuimarisha maneno, matendo na imani ya Kanisa kwa nguvu zote.

Alisema kanisa halikubaliani na aina yoyote ya utamaduni wa kifo na hivyo ni wajibu wa kila mwanakanisa wakiwamo vijana kuwa mstari wa mbele kuziunga mkono juhudi hizo.

Askofu aliliombea kanisa hilo na waamini wote wakiwamo wageni kutoka Ujerumani pamoja na mkandarasi wa jengo hilo Dk. Franzi Wesinger, kutoka Ujerumani na Dk. Janus Parditka, kutoka Hingary

Waonywa kutofuata nguvu za giza

Na Christopher Gamaina, Tarime

ILI waweze kumtumikia Mungu kikamilifu, waamini wa madhehebu mbalimbali nchini wametakiwa kuacha kufuata nguvu za giza na badala yake, wafuate na kuzipokea nuru ambazo ni za Yesu Kristo.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mchungaji Raulent Magike wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship(FGBF), wakati akiwalisha Neno la Mungu kwa waamini walioshiriki ibada ndani ya kanisa hilo, kando mwa barabara ya Cogefer iliyopo Ronsoti mjini Tarime.

Mchungaji huyo aliwataka wote wenye kufuata nguvu za giza, kukubali kuja kanisani ambapo watasafishwa na kutakata na hapo hapo kusahau yote mabaya na kuanza kufuata yenye nuru.

"Nguvu za giza ni zile za kufanya uasherati, ulevi, uvutaji sigara bangi. Mnahitaji kuyapokea vema na kuyashika mafundisho ya Yesu ili kuzishinda nguvu hizo," alisema.

Aliwataka watu kuelewa kuwa Mungu hupenda kuwaona watu wakiwa wasafi ndani na nje ya miili yao na hivyo, tabia ya baadhi ya watu kujidai wameokoka huku wamejaa mzaha na kuvaa nguo zenye mipasuo ya ajabu ni kumkufuru Mwenyezi Mungu.

Alisema kuwa kitendo cha kuoa mwanamke zaidi ya mmoja ni njia mojawapo ya kuitii sauti ya shetani ambayo inaweza ikawazuia wanadamu kuingia katika Ufalme wa Mungu endapo hawatailaani na kuikataa kabisa.

Alisema njia pekee ni kumwomba Mungu awasamehe makosa yao na awajalie kuipokea nuru halisi ili iweze kuangaza ndani mioyo yao.

Aliongeza kuwa nuru halisi huyafuta mambo yote yaliyo machafu na kuyaumba yaliyo mazuri na mapya ndani ya miili ya watu.

Vijana wahimizwa kuboresha mahusiano ya makanisa

Na Getrude Madembwe

IDARA ya Vijana Jimbo Katoliki la Geita imewataka vijana Wakatoliki kuwa kichocheo cha mahusiano mema baina ya Kanisa katoliki na madhehebu mengine ya Kikristo.

Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo Padre Mathew Bulala, alipozungumza na KIONGOZI hivi karibuni

Alisema vijana hawana budi kuwa na uhusiano mzuri na madhehebu mengine ili washirikiane katika maendeleo ya nchi kiuchumi, kiteknolojia na hata kijamii.

"Unajua kuwa na ushirikiano na baadhi ya madhehebu mengine kama ya Kilutheri, Kianglikana na madhehebu mengine ya Kiprotestanti, ni vizuri kwani vijana wakikutana huweza kubadilishana mawazo na vile vile watashirikiana katika maendeleo ya nchi kiuchumi, kiteknolojia na mambo mengine mazuri," alisema Padre Bulala.

Alisema Jimbo lake la Geita lina ushirikiano mzuri na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lililopo Moshi na tayari wameshaenda kushirikiana katika mambo mengi.

Alisema baadhi ya vitu ambavyo wameshafanya ni kuwa na uhusiano na jimbo la DRESDEN MEISEN lililopo Ujerumani ambapo hutembeleana na mwaka huu Jimbo Katoliki la Geita na KKKT Moshi, walipeleka vijana 6 na viongozi 2 katika jimbo hilo.

Alisema kuwa wakiwa katika jimbo hilo walilokutana na vijana huku na walijifunza mila na desturi za mahali, kujifunza kwa matendo, mambo ya kuendeleza uchumi.

Vitu vingine walivyojifunza ni hali ya siasa, muundo wa siasa viongozi wa sheria za nchi vitu ambavyo ni muhimu kuvizingatia hasa kwa kuwa wao ni vijana.

Alisema pia walijifunza jinsi ya kutatua matatizo ya ajira yaliyokuwa vijana na namna ya kuyakabili kuliko kufanya vitu ambavyo jamii haipendezewi navyo.

Pia alisema kuwa ili kuendelea kupanua nguvu ya mahusiano yao ya watafanya kuimarisha uhusiano wao hasa katika ngazi za maparokia, Usharika, Jimbo na Dayosisi nyingine.

Kutamani dhambi ni kumsulubisha Kristo mara ya pili-Mchungaji

Na Jenifer Aloyce, DSJ

KITENDO cha mtu kufikia hatua ya kuitamani dhambi, kimeelezwa kuwa kinatokana na muhusika kutokumuelewa Mungu aliye naye katika maisha yake na ni sawa na kumsulubisha Kristo kwa mara ya pili.

Hayo yalisemwa na Mzee wa Kanisa la Evanjelist Assemblies of God (EAGT), Usharika wa Mbagala Rangi Tatu jijini Dar-Es-Salaam, Bw. Nchimbi, Jumapili iliyopita wakati wa ibada iliyofanyika kanisani hapo.

"Kuitafuta dhambi hilo siyo suluhisho la matatizo yetu, kama utasimama kwa ukamilifu mbele za Mungu atakuwa ndiyo tegemeo lako, unapotamani kutenda dhambi ni sawa na kumsulubisha Yesu Kristu kwa mara ya pili" alisema.

Bw.Nchimbi alitoa msisitizo wa kauli yake kwa kunukuu maneno ya Biblia Takatifu kutoka katika kitabu cha Mwanzo 39:6-12 isemayo, "Akiyaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu wala hakujua habari za kitu chochote chake, ila hicho chakula alichokula tu, naye Yusufu alikuwa mtu mzuri na mwenye uso mzuri.

Bwana Nchimbi alisema watu wa Mungu wanatakiwa kuikimbia kwa kuiga mfano wa Yusufu alivyokimbia dhambi naye akashinda majaribu kuliko angekaa pale na kuendelea kukemea bila kukimbia angeliingia dhambini alisema.

Aliongeza kuwa watu wa Mungu wanatakiwa kutoangammia kwa kukosa maarifa na mara nyingi unapojichanganya na watu wasiomjua Mungu hapo ndipo ujasiri wa kiroho hupungua kama Samson alipokuwa na Wafilisti, watu wasiomjua Mungu wakambembeleza mkewe aliyeitwa Delila ili wapate kujua asili ya nguvu yake.

Samson alitoa siri na kwa mkewe huyo kuwa tangu azaliwe, wembe haukumpita kichwani mwake na huyo mkewe akatoa siri kwa Wafilisti.

Hiyo ndiyo dhambi iliyomfanya nguvu za Roho Mtakatifu kumwishia Samson na kuachana na Mungu, Wafilisti wakamnyoa nywele kumtoboa macho na Kumpeleka utumwani.

"Mungu anasikitishwa sana na kitendo hicho huruma yake sio sababu ya kukufanya uendelee kutenda dhambi kama ni mtoto wa Mungu unatakiwa kuiga mfano wa Yusufu" alisema.

Padre ashauri mabadiliko yasichochee kumsahau Mungu

Na Elizabeth Steven

"MABADILIKO yanayotokea nchini, yawe ya kiuchumi ,kisiasa ama kiutamaduni, yasiwe kigezo cha kumweka kando Mungu na badala yake, muungane kwa kumwamini kuwa yeye ni mamlaka ya mwisho na si vingine".

Kauli hiyo ilitolewa na Padre Paulo Prosper wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, alipokuwa akiendesha ibada kanisani hapo Jumapili iliyopita.

Alisema mabadiliko katika jamii ya nchi hii hayana budi kutokuchukuliwa kama kigezo cha kukiuka maadili ya Kimungu na kijamii bali ni vema jamii ikatumia mabadiliko hayo kama kipimo cha imani na uwezo katika kuifanya kazi ya Mungu kwa uaminifu.

"Mabadiliko haya yasiwafanye mkazihasi imani zetu bali tuzijenge na kuzidumisha," alisema Padre Prosper.

Akizungumzia ajira kwa vijana, Padre Prosper aliwasisitiza vijana waliohitimu masomo yao na hawajapata kazi, wasitumie hali hiyo kujihusisha na vitendo haramu kama wizi, biashara ya madawa ya kulevya na uvutaji bangi kama njia ya kutatua tatizo la ajira na badala yake, wasimame imara katika mafunzo kwa kadri ya imani zao za kidini.

"vijana wengi utakuta wamesoma na wanavyeti vizuri sana lakini hawana kazi. Sasa, hawa wasipokuwa na imani thabiti, ipo hatari ya kuacha imani zao ili mradi tu, wapate kazi. Simameni imara," alisisitiza

Aidha, aliwataka waamini kuepukana na mambo ambayo machoni mwa wananadamu yana sura ya uzuri ingawa undani wake sio sahihi kama yanavyoonekana na akasema matendo kama hayo ya kujifanya mwema kinyume na hali yako halisi, ni unafiki ambao ni machukizo kwa Mungu.

Akitoa mfano alisema, "Wengi tunapenda kuazimisha birthday lakini sikukuu nyingine kama Ubatizo, hamfanyi sherehe. Inafaa kuabudu zaidi, kushangilia kwa vigelegele kisha bado tuendelee kujiuliza je, tunamwamini Mungu wetu na tunabaki katika imani zetu tunayakataa yote ya shetani".

Amewaasa wale wanapinga neno la Mungu ni wakati wao sasa kujimudu na kama wamekorofishana na wenzao ni vizuri wakaombana misamaha.

Ametoa wito kwa wanandoa kupendana na kuheshimiana baina yao kwani kwa kufanya hivyo, watajenga familia bora zisizokuwa na mifarakano na kuhakikisha wanashiriki meza ya Bwana bila kukosa.

"Matatizo tunayoyapata katika familia ni kwa sababu hatupo tayari, wanawake muwe tayari kuwatii waume zenu na kuwatumikia wote mkionesha upendo huo basi familia zenu zitadumu na mtatizo yatapungua," alisema.

Wasiojiandikisha kura waambiwa, akipatikana kiongozi kapi, wakae kimya

Na Getrude Madembwe

"NA kama akipatikana kiongozi mbaya wala usilalamike eeh! Kwa nini ulalamike wakati wewe hukuenda kujiandikisha ili upige kura?".

Changamoto hiyo ilitolewa mwanzoni mwa juma na Mchungaji Mwanafunzi Hery Nyanza, wa chuo cha Uchungaji cha Tumaini kilichopo Iringa anayechukua masomo ya Teolojia katika chuo hicho.

Aliyasema hayo mwanzoni mwa juma katika ibada ya Sakramenti Takatifu iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), usharika wa Kawe jijini Dar-es-salaam.

Hery Nyanza, anayechukua masomo ya Teolojia katika chuo hicho, alisema kila Mtanzania hana budi kwenda kupiga kura kwani kwa kufanya hivyo, atakuwa ametekeleza wajibu wake na kuchukua sehemu ambayo Mungu amemchagulia.

"Kila mtu amepewa nafasi ya kuchagua kiongozi anayemtaka. Hivyo, hatuna budi kutumia nafasi ambayo tumepewa kikamilifu na kama hatutaitumia nafasi hiyo vizuri, tukipata kiongozi mbaya tusilalamike, tukae kimya alisisitiza Mchungaji huyo na kuongeza, "Na iwapo kutakuwa na mtu yeyote atakayelalamika basi na hukumu ya Mungu imshukie; ndio ikushikie au wewe uliejiandikisha kupiga kura halafu ukakataa".

Mchungaji Nyanza alisema hivi sasa Tanzania kuna wakati mgumu wa Uchaguzi Mkuu na hivyo, kila muamini hana budi kuliombea jambo hilo ili lifanyike kwa upendo na amani.

Awali akimkaribisha katika usharika huo, Mchungaji wa usharika huo Moses Maarifa, aliwataka waamini hao kufanya yale ambayo Bwana amewaagiza.

"Jamani jambo hili la uchaguzi si mchezo kwani tukilifanyia mzaha tutajikuta tunatenda dhambi au yakatokea yale ya Nigeria hivyo basi tumejiandikisha, hatuna budi kwenda kupiga kura," alisema na kuongeza kuwa jamii yote ishirikiane kuomba Mungu ili siku hiyo iwe ya furaha na amani tupu.

Mchungaji Maarifa na kuongeza kuwa "tumwombe Mungu ili siku hiyo iwe ya amani na furaha"