Makanisani Wiki hii

Mchungaji awakoromea viongozi, wasomi juu ya UKIMWI

Na Elizabeth Steven, Kibaha

MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Tumbi katika dayosisi ya Mashariki na Pwani, Issa Mtele, amewalaumu wasomi na viongozi mbalimbali kwa madai kuwa wanachochea maambukizo ya UKIMWI kwa kuwa wanahimiza matumizi ya kondomu kama njia ya kukukwepa ugonjwa huo.

Akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake mjini hapa hivi karibuni, Mchungaji Mtele alisema sio rahisi ugonjwa wa ukimwi kupunguza maambukizi kwa kuwa hata baadhi ya viongozi na wasomi wanachochea vitendo vya uzinzi na usherati kwa kuhimiza matumizi ya kondomu hali ikijulikana bayana kuwa nyingi si salama.

Alisema licha ya kutokuwa salama, matumizi ya kondomu yanapingana na mafundisho ya dini zote kwani yanaruhusu mapenzi kabla na nje ya ndoa na kwamba hali hiyo, ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

"UKIMWI hautakoma kwa kuwa hata viongozi wenye elimu wameshindwa kuyatumia madaraka yao vizuri. Wamekuwa wa kwanza kugawa kondomu. Hawajui huko ni kuruhusu uzinzi sawa na kumpa mkulima jembe. Unapompa hawezi kuliweka uvunguni, ni lazima atalitumia."

Alisema iwapo jamii itaamini kuwa kondomu ni kinga dhidi ya ukimwi, basi itakuwa inajidanganya na itazidi kupukutika kama majani ya miti na kwamba njia iliyobaki ni kupiga marufuku utumiaji wa kondomu

"Hivi kwa mfano, watoto wa shule za msingi wanapewa kondomu, ili wazifanyie nini?" alihoji kwa mshangao.

Akizungumzia ajira kwa vijana, Mchungaji Ntele alisema Serikali haina budi kuwakusanya vijana wasioajiriwa na kuwapatia maeneo ya kulima ili pindi wanapopata mazao, wayauze na kuweza kujikimu kimaisha.

Alisema ukosefu wa ajira kwa vijana unachangia katika uenezaji wa ugonjwa wa ukimwi kwani walio wengi ni vijana ndio wanaoonekana kuathirika zaidi.

Alisema hii inatokana na ukosefu wa kazi na badala yake wengine wnaaamua kutumia biashara haramu ya ukahaba kama njia ya kujiajiri na wengine kujitumbukiza kwenye vitendo vya uhalifu vikiwemo vitendo vya uvutaji bangi, madawa ya kulevya, wizi na unyang’anyi.

Alitoa wito kwa vijana kuwa waaminifu ingawa hawana cha kufanya na akawashauri kuwa kwao, Neno la Mungu liwe taa na muongozo wa maisha yao.

Maisha ya ndoa ni Paradiso na jehanamu - Mchungaji

Na Leocardia Moswery

MAISHA ya ndoa yameelezwa kuwa mazuri lakini magumu na mchungaji mmoja wa kanisa la Moraviani Tanzania. ameyafananisha na Paradiso na Jehanamu na akasema, wengine wamediriki hata kuyajutia wakisema ni heri wasingeoa.

Akihubiri katika ibada ya ndoa baina ya waamini wa kanisa hilo usharika wa Keko jijini, Bw. Bariki Mbembela na Bi. Syoni, Mchungaji huyo wa usharika wa Kigamboni, Jimbo la Kusini katika Wilaya ya Mashariki, Lawi A. Mwankuga, alisema katika maisha hayo, wanandoa hawana budi kuwa waaminifu na na wanyenyekevu baina yao.

Alisema katika ndoa kukiwa na uvumilivu, kuheshimiana, kushauriana, kushirikiana na kusameheana, maisha hayo hata kama ni ya kipato kidogo, hupendeza na kuonekana kama Paradiso lakini kinyume na hapo, huwa machukizo na mateso sawa na jehanamu.

Katika ibada hiyo iliyofanyika Jumamosi iliyopita, na kuhudhuriwa pia na mchungaji wa usharika wa Temeke, Tuntufye A. Mkumbwa na Mchungaji wa usharika wa Keko, salatiel Mwakamyanda, Mchungaji Mwankunga alisema,

"Mtu mwaminifu ni lazima aongozwe na Mungu na Roho Mtakatifu kwa kuwa uaminifu ni miongoni mwa matunda ya Roho Mtakatifu."

"Siri ya amani, ni lazima kila mmoja amuamini na kumuona mwenzie kuwa ni bora zaidi kuliko yeye mwenyewe."

Akihimiza uaminifu katika maisha hayo matakatifu ya ndoa, Mchungaji Mwankunga alisema kuwa inashangaza kuona mtu asiye mwaminifu katika maisha hasa ya ndoa, ndiye huwa wa kwanza kuhofu na kumdhania mwenzake kuwa sio mwaminifu.

"Mtu malaya anafikiri na mwenzie ni malaya. Sio vizuri. Mtu na akili zako unaona mwenzio anatembea usawa na mtu mwingine barabarani au amechelewa na wewe haujui amekuwa nini huko, anafika anakuta umenuna; na hii ni kwa wote. Haijalishi ni kwa mwanamke au kwa mwanaume."

Alisema wanandoa hawana budi kupendana na kuvumiliana bila kujali watu wanawatazama vipi.

"hata akiwa dhaifu, hata kama wenzio watakusema kuwa hukutazama vizuri. Wengine watasema ona, kwanza yuko hivi. Hata kama anajikojolea kitandani, huyo ndiye wako uliyepewa na Mungu. Mwamshe, mvumilie na umpende. Mbona watoto tunawaamsha?" alihoji kwa msisistizo.

Aliongeza kusema, "Ukimpenda na kumuamini kuwa huyu ndiye wangu niliyepewa na Mungu, wengine wote utawaona kama wana ukimwi."

Wachumba msizuzuane kwa mobitel, mali - Ushauri

Na Mwandishi Wetu

VIJANA waliofikisha makamo ya kuoa au kuolewa, wametakiwa kutozuzuka na mavazi au mali walizonazo wachumba wao na badala yake, wazingatie tabia.

Ushauri huo ulitolewa jijini Dar-Es-Salaam hivi karibuni na Padre Ireneus Mbahulila wa Parokia ya Makuburi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

"Mara nyingi vijana wamekuwa wakidanganyika kutokana na vitu wanavyoviona kwa wenzao. Siku hizi kuna simu za mkononi watu wanaziita mtandao. Wengine zinawazuzua mno. Wanaziona kama kipimo cha maendeleo ya mtu.

Au utakuta kijana au baba anataka kumridhisha mkewe au mchumba wake kwa kumuambia kuwa atamnunulia kitu fulani. Labda mtandao au kitu kingine cha ajabu tu ambacho hata yeye mwenyewe hawezi kukipata na wala hanacho.

Sasa anapoacha kazi au pesa zinapomuisha mke au mchumba wake hawezi kumuelewa kwa sababu ndivyo alivyozoea na hii inaonesha kuwa hakumpenda kwa tabia bali mali".

Alisema baba au mama wana wajibu wa pamoja katika shughuli zote za nyumbani. "Baba hatakiwi kumdekeza sana mke," alisema Padre Mbahulila na kuongeza kuwalaumu wanaume wasiopenda wanawake wafanye kazi hata kama ni za nyumbani.

Alisema hali hiyo ni hatari katika ndoa kwani pindi pesa au mali alizonazo mwanaume zinapokwisha, hushindwa kueleweka kwa wake zao kwa kuwa wanawake huwa tayari wamezoea kufanyiwa kazi na wasichana wa kazi (House girls)

Wakati huo huo: Wanandoa wametakiwa kuziheshimu ndoa wakiishi kwa upendo, amani na kuzishika Amri za Mungu.

Kauli hiyo ilitolewa na Paroko Msaidizi Padre Stefano Kaombe wa Parokia ya Kibangu katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam alipokuwa akizungumza katika ibada ya Jumapili parokiani kwake.

Alisema siri ya mafanikio katika maisha ya ndoa na familia, ni upendo, amani na kuheshimiana na kwamba mambo hayo ni wajibu wa kila mmoja kwa mwenzie.

' Tutaua uchumi tukifanya fujo'

Na Getruder Madembwe

UCHUMI wa nchi umehofiwa kuangakuka na pengine kufa kabisa endapo wananchi watauchanganya na fujo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu kwa kuwa hadi sasa bado duni.

Hofu hiyo ilielezwa na Mwinjilisti Nicodemus Ubwe, wa Usharika wa Mbezi Beach, wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, wakati akizungumza na gazeti hili jijini wiki iliyopita.

Alisema njia muafaka ya Watanzania kuepuka vita na machafuko ndani ya nchi yao, ni kukubali matokeo ya Uchaguzi bila kulazimisha kushika hatamu za uongozi endapo matokeo hayakumpa ushindi mgombea au chama wanachoshabikia kwa kuwa hiyo ndiyo maana halisi ya ushindani safi wa kidemokrasia.

Alisema katika Awamu hii ya Pili ya uchaguzi wa vyama vingi, Watanzania wanapaswa kuepuka chuki na kuwekeana vinyongo eti kutokana na tofauti za kisiasa.

"Hakuna haja ya kuwekeana vinyongo eti huyu ni wa CUF au huyu ni CCM. Hata chama kingine cha siasa. Wote ni Watanzania, lazima tupendane," alisema.

Aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutenda haki katika kusimamia zoezi la uchaguzi na kutoa matokeo sahihi na kwamba, kiongozi atakayepatikana, hana budi kuilinda amani iliyopo kwani haki na amani ndiyo nguzo ya Taifa.

Mchungaji Ubwe alimuelezea kiongozi safi katika jamii kuwa ni yule anayetekeleza wajibu wake kwa kufuata misingi ya katiba na wala siyo kufuata matakwa yake mwenyewe.

Aliongeza kufafanua kuwa, kiongozi kama huyo daima yuko tayari kulalamikiwa na baadhi ya watu ilimradi tu, havunji sheria na anafuata taratibu zinazotakiwa katika utendaji kazi wake.

"Kiongozi safi mara nyingi hulalamikiwa na huyo ndiye anayetakiwa kuiongoza nchi maana hutenda kila kitu kwa haki," alisema na kuongeza, "Kiongozi anayeongoza kwa kutumia Katiba ya nchi, ni mzuri kwani hata Wakristo wanapaswa kuishi kama katiba ya Kikristo(Biblia) inavyotaka yaani, kuishi kwa kumtegemea Mungu."

Walutheri wahimizwa kutoa sadaka inayotosha

Na Getrude Madembwe

WAAMINI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kawe katika dayosisi ya Mashariki na Pwani, wamehimizwa kumtolea Mungu Sadaka iliyo safi bila kujali vipato vyao.

Wito huo ulitolewa na Bi. Ninaeli Munuo, wakati akihubiri katika ibada ya Jumapili iliyopita iliyofanyika katika usharika huo wa Kawe uliopo jijini Dar-Es-salaam.

Alisema waamini hawana budi kutoa sadaka kwa nia njema toka katika mapato yanayotokana na kazi zao halali zinazotambulika ndani ya jamiii na kukubaliana na maadili ya ki-Mungu.

Bi. Munuo alisisitiza kuwa, kupitia kazi hizo halali, jamii inapopata riziki yake, haina budi kujijengea utamaduni bora wa kumshukuru Mungu kwa njia ya sala na matoleo ya sadaka.

Baadhi ya kazi ambazo si halali ndani ya jamii ni pamoja na biashara ya ukahaba, unyang’anyi, wizi, ulanguzi, ubadhilifu, biashara haramu ya bangi, gongo na madawa ya kulevya, pamoja na mauaji.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wagumu kumtolea Mungu sadaka kwa kisingizio cha kuwa hawana kipato cha kutosha kukidhi mahitaji ya familia zao.

"Utamkuta mtu anaangalia kwanza mshahara wake au kitu chochote alichokipata na akiona hakimtoshelezi huanza kulalamika kuwa kipato chake hakimtoshelezi," alisema Bi. Munuo na kuongeza,

"Hata kama kipato chetu ni kidogo tumtolee Mungu tuone jinsi atakavyofungua milango ya baraka; hebu tujaribu tuone."

Bi. Munuo ambaye ni Katibu wa Fellowship(Uamsho) katika usharika huo, aliwahimiza waamini hao kumtanguliza Mungu mbele katika maisha yao kwani kwa kufanya hivyo, watafanikiwa katika kazi zao.

"Katika mapito tunayopita, tumtangulize Mungu mbele sababu mambo yote tunafanya kwa uwezo wake mwenyewe na ukimtegemea hakika utafanikiwa," alisisitiza.