Make your own free website on Tripod.com

Makanisani Wiki hii

Hatubatizi kwa siri wala kiholela - Kanisa Katoliki

Na Elizabeth Steven

KANISA Katoliki limesema halina Ubatizo wa siri wala wa kiholela kama baadhi ya madhehebu wanavyofikiria bali hubatiza kwa matakwa na makusudio maalumu ya mhusika.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyasema hayo wakati anabariki kigango cha Kibangu Jumapili iliyopita ambapo Kigango kilibarikiwa na kutangazwa rasmi kuwa parokia.

Alisema baadhi ya watu hushangaza wanapoona na kuogopa kitendo cha kuguswa na maji ya baraka wakati wa kubariki vitu muhimu kama majengo kwa imani kuwa maji hayo yanapowaangukia wakati wa kunyunyizia kubariki, huwa wanabatizwa kwa siri.

"Nilishafanya hivi sehemu nyingi kisha nikaletewa malalmiko kuwa kufanya hivyo ni kuwabatiza kwa siri. Ukweli ni kwamba si hivyo kama wanavyofikiria. Kama watu wa namna hiyo wapo, basi nawasihi msiogope kwa kudhani kuwa mtakuwa mmebatizwa kwa siri," alisema.

Kardinali Pengo aliwataka waamini wa Parokia hiyo mpya kulitumia vema jengo lao la kanisa kwa sala na maombi na si vinginevyo kwani kinyume na hapo, ni kuenenda kinyume na makusudio ya kuwepo kwa jengo hilo na hivyo kumkufuru Mungu.

"Jengo hili linaweza kugeuzwa wakati wowote kuwa nyumba ya dansi hata kuwa godauni. Wanaoweza kufanya nyumba hii kwa matofali ni wanadamu walioamini na kubatizwa na wanaokusanyika kusali pamoja," alihimiza.

Alisema kuwa kanisa kuwa zuri si kitu cha maana au heshima la hasha bali ingekuwa ni balaa kwa jengo la mwenyezi mungu kulitolea kanisa hilo kuja kusali kwa nia tofauti.

Aliwaambia waamini wa parokia hiyo pindi wanapokusanyika kusali kanisani hapo wawe wachache au wengi wajue wanawakilisha waumini wote na si jimbo la Dar es Salam tu bali wanawakilisa ulimwengu mzima.

"Uzuri wa jengo hili, uwe ishara ya nyoyo nzuri ndiyo maana ya kujenga kanisa hili. Mnatuwakilisha kwa sala na maombi yanayotoka moyoni mwenu na kuanzia sasa, Kibangu si kigango bali ni parokia ya Kibangu."

Mwadhama aliendelea kusema kuwa, Kanisa hata liwe kubwa kiasi gani kama halina paroko haliwezi kuwa kanisa na alimtangaza Padre Brian Mkude kuwa paroko wa parokia ya Kibangu akisaidiwa na Padre Steven Kaombe.

Katika sherehe hizo zilizowashirikisha waamini wa parokia ya Kibangu na makuburi, michezo mbalimbali ilioneshwa.

Umoja wa wanawake Katoliki (WAWATA) parokia ya Kibangu na Makuburi walimkabidhi Paroko mpya wa parokia ya Kibangu zawadi siku hiyo pia Kardinali Pengo alitoa Sakramenti ya Kipaimara siku hiyo.

Askofu Sambano ateuwa Mapadre washauri

Na Leocardia Moswery

ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Daiyosisi ya Dar-Es-Salaam,Mhashamu Basil M. Sambano amewateua mapadre watatu kuwa washauri wake.

Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa Msaidizi wa Askofu huyo,Padre Frank Kajembe, amesema kuwa mapadre hao mbali na kumshauri Askofu huyo lakini vile vile watakuwa wanamsaidia kwa baadhi ya kazi.

Alisema kuwa uteuzi huo ulifanyika hivi karibuni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Nikolaus na Mashahidi wa Afrika lililopo Ilala jijini wakati wa Mkutano Mku wa Ukuaji wa Kanisa (SINODI).

Padre Kajembe ambaye pia ni Kasisi Kiongozi wa Daiyosisi hiyo aliwataja mapadre walioteuliwa pamoja na Idara zao kuwa ni Padre Samwel Sepeku ambaye ni mkurugenzi wa Uinjilisti katika Dayosisi ya Dar es Salaam.

Mwingine ni Paroko wa Kanisa la Upanga la Mtakatifu Albano ,Padre William Kambaga ambaye sasa hivi ni Kasisi Mkuu wa Mitaa ukiwemo mtaa wa Upanga, Kigamboni, Mafia na Muhimbili.

Msaidizi huyo wa Askofu alimtaja Padre wa tatu kuwa ni Padre Zacharia Scania kutoka Uswisi ambaye yeye atakuwa anashughulikia miradi ya Dayosisi eneo la Mtoni Buza pamoja na ibada za kiingereza kwa wakristo wa Kihindi na ibada ya Kiingereza za kawaida.

Padre Kajembe alisema kikubwa kilichozungumziwa katika Sinodi hiyo ni suala la ujenzi wa makanisa 12 ambapo alisema ujenzi huo utaanza wakati wowote kwani viwanja tayari vimekwisha patikana.

Alisema kuwa makanisa hayo yatajengwa kwa nguvu za waamini badala ya kuwategemea wafadhili kutoka nchi nyingine kitendo ambacho kina warudisha nyuma na kushindwa kuwapata waamini.

"Kanisa lifuate watu na siyo watu wafuate kanisa’ basi nasi ndivyo tutakavyofanya kwa kuwapatia waumini wetu sehemu ya huduma.

Tumieni mali mlizonazo kuendeleza kazi ya Mungu

Na Christopher Gamaina, Tarime

WAAMINI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Tarime Dayosisi ya Mara na jamii nzima kwa jumla,wametakiwa kutumia mali walizonazo kwa kuliendeleza neno la Mungu.

Kauli hiyo ilitolewa Jumapili iliyopita na Mhubiri wa kanisa hilo, Charles G.M Mwarabu katika ibada iliyofanyika katika kanisa la Usharika huo ambayo iliambatana maadhimisho ya sikuu ya mavuno.

Mhubiri huyo alisema ni wajibu wa kila mmoja kufahamu kuwa vyote alivyonavyo vimepatikana kwa majaliwa ya Mwenyezi Mungu na hivyo avitumie katika kuiendeleza injili kama sio kuwasaidia maskini.

Alisema watu hawapaswi kugang’ania kwa kudai utajiri walionao umetokana na juhudi zao pekee bali wafahamu kuwa wamepata hayo yote kwa kuongozwa na Mungu.

Alitoa mfano kwa ardhi ambayo ni mali ya Mungu na kazi ya wanadamu ni kulima na kupanda mazao.

"Ukishampata mazao yako,unayauza na ikumbukwe kuwa kustawisha ni kazi ya Mungu hivyo mali tunayoipata kutokana na mazao hayo hatuna budi kuitumia kwa kuendeleza kazi ya Mungu’ alisema muhubiri huyo.

Aliwataka wakristo kuwa na moyo wa kutoa chochote wakati wote kwa hiari kwa kadri walivyojaliwa na Mungu.

‘Toa shukrani zako kwa Mungu kwa ajili ya mume au mke uliyempata na kwa ajili ya ndoa yako inayoendelea kudumu kwa upendo bila mfarakano’ alisema.

Bw. Mwarabu aliwataka wakristo wasiwe mawakili wasaliti na badala yake wawe mawakili waaminifu ili kuidumisha imani hai.

Alisema Mungu hupenda kutupatia utajiri hivyo tunapaswa kutumia utajiri huo kwa kumtumikia yeye na sio kwa anasa za dunia.

Wazazi: Msilewe mkawaaibisha watoto - Wito

Na Mwandishi Wetu

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini, amewataka Wakristo kote nchini kuwapa malezi bora vijana ili kuwaepusha na vishawishi vinavyowakumba ukiwamo ulevi aliosema ni kitendo kibaya katika maisha ndani ya jamii.

Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa juma lililopita katika parokia ya Makuburi iliyopo katika Jimbo Katoliki la Dar-Es-Salam, alipokuwa akitoa Sakramenti ya Kipaimara kanisani hapo.

Alisema, "Watoto tuwape upendo katika familia. Na tunapaswa kuwafundisha kwa mifano yetu waone kuwa, hata watakapokuwa wakubwa, wawe ni watu wenye kupenda sala na kufanya mambo yanayompendeza Mungu."

Aliendelea kusema kuwa, ni jambo la kusikitisha na la aibu kuona baba au mama anakuwa mlevi katika familia na kwamba sasa umefika wakati wa kutowafanya watoto waone aibu kuwatambulisha wazazi wao mbele za wenzao kutokana na hali wanazokuwa nazo za ulevi

"Tusiwafanye watoto hawa wakaona aibu kusema yule ni baba yangu au ni mama yangu mbele ya wenzake," alisema Mhashamu Kilaini.

Mhashamu Kilaini aliwafananisha watoto na ardhi. Alisema mbegu ikitupwa pasipostahili, haiwezi kuota na kuchanua ili baadaye itoe matunda bora.

Mhashamu Kilaini alihimiza kuwa mwenye wajibu wa kuwalea watoto katika jamii ni wanajamii wote hususani wazazi.

Amewataka vijana wa parokia hiyo kuepukana na magenge na vitendo vya kihuni na kuwa waangalifu wakati wa kuchagua marafiki kwa kuwa wanaoshirikiana na wahuni, na wenyewe hujiunga na vitendo vya kihuni.

Wakati huo huo: Amewahimiza waamini hao kuzidumisha jumuiya ndogondogo za kikikristo kwani kufanya hivyo wanaweza kutatua matatizo yao madogomadogo pindi wanapokutana pamoja kusali.

Alisema kuwa jumuiya ndogondogo si kusali tu, bali pia kupanga kwa pamoja masuala mbalimbali yanayoihusu jamiii ikiwa ni pamoja na yale ya kiuchumi pamoja na kuelewa namna na umuhimu wa kuishi pamoja Kikristo.

Siku hiyo Askofu Msaidizi Kilaini alitoa Sakramenti ya Kipaimara kwa watoto wapatao 300 wa parokiani hapo na kuwataka wadumu katika sala na maombi na wala wasikubali kupokea vishawishi kutoka kwa watu wasiokuwa na mwelekeo mzuri wa kitabia kama ulevi, uvutaji bangi na madawa ya kulevya.

Mchungaji awataka watoa ushuhuda kutopayuka hovyo

Na Getrude Madembwe

‘MTU unapoponywa si vizuri kupayuka payuka bali unachotakiwa kufanya ni kukaa kimya kwani unaweza kusema na ikakuletea tabu tupu’.

Hiyo ilikuwa ni sehemu ya mahubiri ya Mchungaji Moses Maarifa wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Kawe alipokuwa akihubiri katika usharika huo jumapili iliyopita.

"Wewe ukiponywa kaa kimya kabisa usiseme; ukiwa na matatizo ukimwomba Mungu na akikutendea miujiza tulia na sio uende kwa watu ukaanze kusema Bwana asifiwe sana......mimi nilikuwa na kimada nimemuomba Mungu amenisamehe na kimada huyo nimemwacha...... nakuambia hapo unaweza hata ukakorofishana na mke wako au na ndugu wengine’ alisema mchungaji Maarifa.

Alisema kuna baadhi ya watu wengine wakiponywa huongeza chumvi katika shuhuda zao na hiyo ilimletea shida hata Yesu Kristo pale alipoenda kuponya wagonjwa na alipomponya mgonjwa wa ukoma na huyo alipoenda kutoa ushuhuda wake aliongeza chumvi hali iliyosababisha Yesu kuzuiwa kuingia katika eneo hilo.

"Unaona hata huyu mgonjwa wa ukoma alipoponywa akaambiwa kaa kimya usimwambie mtu, lakini yeye alikiuka,akaenda kuongea kwa watu hadi Yesu akazuiwa asiingie maeneo hayo"alisema Mchungaji Maarifa na kuongeza kuwa "miujiza mingine muwe mnakaa kimya".

Mbali na hayo, Mchungaji Maarifa pia ameitaka jamii nzima kuwa watu wa shukrani wanapotendewa mambo mazuri na Mungu.

Wahati huo huo: Ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mabibo unatajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 380.

Akiongea na kiongozi Kanisani hapo hivi karibuni Mwinjilisti wa Kanisa hilo Mwaipile Ismail alisema kuwa ujenzi huo ulianza tangu Julai 1997 na mwanzoni walikadiria kiasi cha shilingi milioni 250 lakini kwa sasa makadirio ya waatalam ni sh milioni 380.

"Tulitegemea ujenzi huu kugharimu kiasi cha shilingi milioni 250 lakini kadri muda unavyozidi kwenda kwa mujibu wa makadirio ya wataalamu ujenzi huo utagharimu kiasi cha shilingi milioni 380' alisema Mwinjilisti Ismail.