Makanisani Wiki hii

Chagua Kanisa sahihi kati ya haya....

Na Elizabeth Steven

JAMII imetahadharishwa kutambua na kuchagua kanisa sahihi miongoni mwa makanisa mawili yaliyoelezwa kuwapo duniani ili wapate kushinda na kufikishwa katika uzima wa milele.

Padre Aloyce Ntandu, wa Jimbo katoliki la Singida, aliyasema hayo wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya Jumapili iliyopita katika Kanisa katoliki la Makuburi Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam.

Alitaja kanisa mojawapo hayo kuwa ni lile lenye mambo maovu ya kilimwengu ambayo ni pamoja na tamaa, chuki, fitina na mambo mengine yasiyompendeza Mungu ambalo kwa hadhi yake ni "kijikanisa"

Alilitaja kanisa lingine kuwa ni kanisa takatifu katoliki la Mitume ambalo limegawanywa katika makundi matatu.

Alisema kundi la kwanza katika kanisa hilo, ni kanisa la duniani la mahujaji ambalo ni la mpito.

Lingine ni la toharani ambalo kabla watu hawajaingia mbinguni wanamalizia adhabu yao ingawa ipo siku nao watakwenda mbinguni adhabu yao itakopoisha.

La Tatu lililo Kuu, ni takatifu na la Mbinguni la washindi yaani watakatifu.

Padre Ntandu ambaye kwa sasa yuko masomoni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisisitiza kuwa kila mwanajamii hana budi kujijua kuwa anazungukwa na mazingira hayo ya "vijikanisa" hivyo vinavyolisonga Kanisa hilo takatifu na hivyo, kuvikataa.

Alisema ili kuvikataa vijikanisa hivyo, mwanadamu hana budi kuyakana kwa nguvu zake zote, maovu na mambo yote ya kidunia yakiwamo ulevi, ubinafsi, chuki, masengenyo, wizi, mauaji, uzinzi na mambo mengine yasiyompendeza Mungu .

Alionya dhidi ya mambo ya kidunia yanayoonekana mazuri machoni na hivyo kuvutia na hata kutia tamaa lakini, akasema mambo hayo mara nyingi huhitimishwa na matokeo mabaya kimwili na kiroho tofauti na matarajio.

Alisema njia muafaka ya kuepukana na madhara ya hali hiyo, ni kutumia vipaji mbalimbali walivyo navyo.

"Sisi binadamu tumeumbwa na vipaji tofauti na viumbe wengine. Katika vipaji hivyo, kila mtu anakuwa na malengo yake katika maisha. Binadamu wa leo anatawaliwa na malimwengu ambayo ni ushetani," alisema na kuongeza, " Njia ya kushinda, ni kusali kwa pamoja na kufanya ibada kila siku pamoja na kupokea sakramenti."

Linganisheni sadaka, gharama za saluni - ushauri

Na Getrude Madembwe

MCHUNGAJI Edmund Kyando wa Kanisa la Yesu, amewahimiza wanawake kufanya ulinganifu baina ya gharama wanazotumia saluni kujiremba na kutengenezea nywele zao, na kile wanachomtolea Mungu.

Alitoa rai hiyo alipokuwa akihubiri katika Kanisa la African Inland Church Tanzania(AICT), Dayosisi ya Mashariki Pastoreiti ya Magomeni, Jumapili iliyopita.

Alisema inasikitisha kuona akina mama wamependeza baada ya kutumia pesa nyingi hata kwa kutengeneza nywele zao lakini, hao hao wanashindwa kabisa kumtolea Bwana au pengine, kumtolea kiasi kidogo cha sadaka kinachotia hata aibu.

"Sasa, utamkuta mama ameenda kutengeneza nywele saluni lakini akija hapa, hicho kiasi cha fedha alichokuwa nacho, anachukuamo shilingi 200 na kuichenji, yaani anatoa shilingi 50/=, hivi hapo jamani utabarikiwa nini?" Alihoji Mchungaji Kyando na kuongeza kuwa,

"Hata katika Kitabu cha Malaki, Mungu mwenyewe amemuagiza kuwa ni jaribuni muone kama sijawafungulia madirisha ya mbinguni na nikawajazia baraka. Sasa wewe pesa hiyo unaipeleka saluni na wala haifanyi kazi ya Bwana, haujisikii kumkosea Mungu!"

Aidha, Mchungaji Kyando amewataka waamini hao kujenga moyo wa kupenda kutoa zaidi, kuliko kupokea na akasisitiza kuwa, hilo ndilo jema kwani utakuwa ni mtu kutofikiria kupokea tu.

Pia, aliwahimiza wazazi wa kanisa hilo kuwalea watoto wao vema ili wawe katika misingi mizuri ya kumpendeza Mungu na jamii nyingine inayomzunguka mtoto.

"Kila mzazi ajiulize kuwa, watoto wake ni wa namna gani; ni wale ambao wana matendo mazuri au ni wale wanaoleta karaha katika jamii? Hivyo basi nawaombeni sana muwalee watoto katika njia ya kumpendeza Bwana," Alisisitiza Mchungaji Kyando

Wakristo Afrika, kazaneni mkainjilishe Ulaya

Na Josephs Sabinus

MUUMINI mmoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT) Bw. Amosi Ngemela, ametoa changamoto kwa Wakristo barani Afrika, kuondokana na dhana ya kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili wa mataifa ya Ulaya na badala yake, wajitahidi ili wao wakasaidie mataifa hayo katika uenezaji wa Injili.

Bw. Ngemela, aliyasema hayo wakati akizungumza na kazeti la wandishi wa habari katika kanisa lake la KKKT usharika wa Temeke uliopo katika dayosisi ya Mashariki na Pwani, katikati ya juma lilolopita.

Walikuwa wakizungumza juu ya hali halisi ya uinjilishaji katika mabara ya Afrika na Ulaya.

Alisema kutokana na mataifa hayo ya Ulaya kuwa nyuma katika juhudi za uinjilishaji kadri siku zinavyokwenda, tayari wamekwisha anza kusitisha misaada ya kimisionari katika bara hili na badala yake sasa, wanaielekeza katika mabara mengine ambayo yako nyuma kiuinjilishaji.

Bw. Ngemela alisema hii inatokana na mataifa ya Afrika kuonekana kukomaa na kuiva zaidi katika uinjilishaji na akaongeza kuwa, hali inayoyafanya mataifa hayo ya Ulaya, kuona kuwa Waafrika sasa wamekomaa na hivyo kudhania kuwa hawahitaji tena misaada ya kimisionari na badala yake, kuamua kuelekeza misaada ya namna hiyo katika mataifa mengine.

Alisema ni jukumu la Wakristo wa barani Afrika kuona kuwa, wanatumia uwezo walio nao kumtangaza Kristo mahali pote duniani kwa kuwa sasa, ndio wanaoonekana kukomaa kiimani.

Alidokeza kuwa, tatizo kubwa kiimani linalowakabili watu wa mataifa ya Ulaya, ni pamoja na kwenda kanisani kwa ajili ya ibada na matukio maalumu pekee.

"Unajua wenzetu wa Ulaya kibaya wanachokifanya, ni kwenda kanisani kwa kufuata matukio mapya tu. Tena ni mara chache kwenda kanisani kwa kuwa wanasema wanayokwenda kuona au kusikia, eti ni yale yale. Wanapenda ili wajae kanisani, labda wasikie kuna kwaya kutoka huku kwetu, au kuna tukio au sherehe maalumu. Hiyo ndiyo pia inachangia kuzorota kwa uinjilishaji katika mataifa ya huko." alisema Bw, Ngemela.

Wakati huo huo: Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Jimbo la Temeke, Jumapili hii linaadhimisha Siku ya Mavuno na kwamba waamini wote wameshauriwa kumtolea Mungu shukrani zao kwa kadri ya fadhila walizotendewa na Mungu.

Siku hiyo ilikuwa iadhimishwe Jumapili iliyopita lakini, iliahirishwa kutokana na nchi nzima kuwa katika zoezi zima la kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Pili katika mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi ya siasa.

Mfumo huu nchini ulianza mwaka 1992 na Uchaguzi Mkuu wa kwanza katika mfumo huu, ulifanyika mwaka 1995.

ILI KUKAMILISHA UJENZI WA KANISA

Jumuiya zahimizwa kuwasilisha michango

Na Dalphina Rubyema

JUMUIYA ndogondogo zilizopo chini ya Kanisa Katoliki la Kristo Mfalme, katika Parokia ya Tabata Jimbo Kuu la Dar es Salaam, zimeombwa kuwasilisha mchango wao wa 20,000 kwa kila jumuiya kwa Kamati ya Ujenzi wa Kanisa ili kuiwezesha kuendelea na taratibu zake za ujenzi.

Akitoa matangazo katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika Jumapili iliyopita parokiani hapo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi Bw. Gratian Nshekanabo, alisema kuwa makabidhiano ya kanisa yatakayofanyika Novemba 26, mwaka huu hayawezi kufana endapo baadhi ya mambo yatakuwa hayajakamilika.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na uwekaji wa madirisha ambayo kwa sasa yamebaki matatu, ujenzi wa Sakristia ikiwa ni pamoja na kuiwekea sakafu na milango ya kudumu, pamoja na ujenzi wa vyoo na viti vitavyokaliwa na waamini.

"Naomba jumuiya ambazo bado hajizawasilisha michango yake zifanye hivyo mara moja kwani kukamilika kwa mambo haya, kunategemea sana michango yenu," alisema Bw. Nshekanabo.

Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ujenzi alisema kuwa, sherehe za Kristo Mfalme, somo wa kanisa hilo ambazo zitafanyika sambamba na uzinduzi wa kanisa hilo, zitasherehekewa kwa siku mbili mfululizo kuanzia Novemba 25 hadi 26, mwaka huu.

Alifafanua kuwa sherehe za Novemba 25, zitajumuisha hija ya parokia huko Pugu na tafakari ya maendeleo ya ujenzi wa kanisa ambapo sherehe za Novemba 26, zitakuwa za makabidhiano ya kanisa(uzinduzi).

Akiongeza kufafanua juu ya tafakari, Bw. Nshekanabo alisema kuwa, tafakari hiyo itakuwa na namna ya mdahalo ambao utampa kila mtu nafasi ya kutoa maoni yake juu ya maendeleo tangu kuanza kwa ujenzi wa kanisa hilo, hadi hatua iliyofikia kwa hivi sasa.

Alisema vitu ambavyo vitapewa nafasi ya kutolewa maoni ni pamoja na mchoro wa kanisa hilo kama kweli unafaa, hatua za ujenzi kama zinaenda haraka ama zinazorota, fedha iliyochangwa na waamini kama imetumika ipasavyo kwenye ujenzi huo.

Alibainisha pia kuwa, kila mshiriki atapewa nafasi ya kutoa mapendekezo ya kitu gani kifanyike ili kumalizia ujenzi uliobakia.

Bw. Nshekanabo alisema kuwa, ili kumpa nafasi kila mmoja kuwa na uhuru wa kutoa maoni yake, Kamati ya Ujenzi itaweka sanduku ambalo litambukizwa karatasi za maoni kutoka kwa watu ambao hawajisikii kuongea hadharani.

"Kuna watu wengine ambao hawajisiki vizuri kuongea hadharani hivyo ili nao wasinyimwe haki yao ya kutoka maoni, kutakuwepo na sanduku la maoni", alisema.

Ujenzi wa kanisa hilo ambalo kwa hivi sasa umefikia katika hatua za mwisho ulianza miaka 2 iliyopita na kanisa hilo litakuwa na uwezo wa kuchukua waamini 1600 kwa wakati mmoja.

Watoto waomba wazazi wapande mbegu za Umisionari

Na Elizabeth Steven

SHIRIKA la Kipapa la Utoto Mtakatifu katika parokia Katoliki ya Tabata Jimbo Kuu katoliki la Dar-Es-Salaam, limewaomba wazazi na walezi wa watoto kushirikiana ili kupanda mbegu za umisionari kwa watoto wengine.

Katika risala ya watoto hao wa parokia ya Tabata kwa mgeni rasmi Jumamosi iliyopita katika maadhimisho ya Siku ya Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu parokiani hapo, watoto hao walisema wazazi na walezi wao hawana budi kuunganisha pamoja juhudi zao ili kueneza umisionari ndani na nje ya parokia ya Tabata.

Hata hivyo walisema wanawashukuru wazazi, walezi na uongozi mzima wa parokia hiyo kwa kuanzisha shirika hilo parokiani.

"Sisi watoto tumefurahi kwamba tumepata nafasi ya kufahamiana sisi kwa sisi na pia, kuwa karibu na viongozi wetu wa kanisa. Aidha, tunapenda kuwashukuru sana wazazi wetu ambao wametuwezesha kufikia hapa tulipo kimwili na kiroho na kwa nafasi ya pili, tunawashukuru walezi wetu kwa kutufundisha Neno la Mungu," walisema katika risala yao.

Watoto hao waliongeza kuwa kuanzishwa kwa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu, kumewawezesha kuunganika na watoto wenzao na hata kuwasaidia wasiojiweza kwa mahitaji yao muhimu.

Wakiwashukuru wazazi na walezi hao, watoto walisema, "wametuunganisha na watoto wenzetu wasiojiweza ili tuwaombee wapate faraja na nguvu ya kustahimili matatizo yanayowakumba. Sisi tunajitahidi kujinyima kwa hali a mali ili tuweze kuwasaidia mahitaji yao muhimu."

Katika sherehe hizo ambazo mgeni rasmi alikuwa Padre Steven Kaombe, na kuhudhuriwa pia na Paroko wa parokia hiyo ya Tabata, Padre Albinius Tesha, masista na viongozi kadhaa wa halmashauri walei na wale wa vyama vya kitume, watoto waliahidi kusali kwa dhati na kuomba Mungu awabariki wazazi, viongozi na wazazi walemavu pamoja na watoto wenzao wasiojiweza ili kwa pamoja waishi kwa kuchukuliana kwa kadri ya mpango wa Mungu.

watoto kadhaa wasiojiweza pia walihudhuria na wote kwa pamoja, wakaahidi upendo na maombi yasiyo na ukomo.

Akizungumza katika sherehe hizo kwa niaba ya Padre Kaombe ambaye hakuweza kufika, Padre Tesha aliwaeleza watoto kuwa wao ni mitume wadogo na wamisionari ambao wanaweza kupeleka ujumbe na hata kutenda kazi kidogo inayoweza kuleta mabadiliko makubwa katika familia na ulimwengu mzima.

Alisema, "Sisi ni mitume wadogo. Tukitenda kazi kidogo, tunafanya mabadiliko makubwa katika familia zetu na hata katika ulimwengu mzima maana sisi pia ni wamisionari wadogo ambao tunapeleka ujumbe kwa kuwa tulikwishabatizwa na kwa sababu hiyo, tunapaswa kumtangaza Kristo."

Aliwataka watoto hao kujenga utamaduni wa ukweli na hata kukubali mateso kwa ajili ya kuwasaidia watu wasiojiweza kama njia ya kuyafuata aliyofanya Yesu Kristo.

"Yesu alikuja duniani kufundisha ukweli na wala hakuwa na michezo michezo hii; hakuangalia ‘tausi’, alishinda njaa na hiyo ilikuwa kama kichocheo ili watu wamjue Mungu," aliongeza.

Aliwataka wenye tabia ya udokozi kuacha mara moja na wale wasiozijua Amri za Mungu, wajifunze na kuacha kutenda mambo mabaya na kisha wawafundishe wengine.

Wajane wa Chang’ombe kuadhimisha Jubilei

Na Dalphina Rubyema

PAROKIA Katoliki ya Chang,ombe katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam,imeandaa Jubilei ya wajane itakayofanyika Novemba 11 mwaka huu parokiani hapo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi katika ya juma, Mwenyekiti wa Chama cha Wajane Parokiani hapo, Bibi Stella Kaparata, alisema kuwa, Jubilei hiyo itatanguliwa na hija itakayofanyika Jumamosi hii huko Mbagala Msalabani.

Bibi Kaparata, alisema lengo la kufanya hivyo pamoja na mambo mengine, ni kuwapa nafasi wajane hao kukutana pamoja na kufarijiana na kuwaombea waume zao ambao ni marehemu.

Alizishauri Parokia nyingine kuunda chama cha namna hiyo.

Wakati huo huo: Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini, amemteuwa Padre Andrew Mwachibindu kuwa Paroko wa Parokia Katoliki ya Mburahati ya jimboni humo.

Taarifa kutoka kwa Katibu wa Askofu, Padre Andrew Luanda, zinasema kuwa hadi anateuliwa kushika nafasi ya uparoko, Padre Mwachibindu alikuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Magomeni.

Taarifa zinasema aliyekuwa akisimamia Parokia hiyo ya Mburahati, Padre Sayi amehamishiwa Parokia ya Magomeni ambapo atashika nafasi ya Paroko Msaidizi.