Makanisani Wiki hii

Mwinjilisti awachambua wachumba 'galasha'

Na Joseph Sabinus

"Bw. Usinibabaishe, ulinichukua kwetu nikiwa ninakula na kulala bila shida. Usinitishe na viugali vyako vya kila siku. Itafikia anakwambia bwana, ulinikuta kwetu kuna wafanyakazi watatu; ulikuta wananipikia, leo kila mara unataka nikupikie kwani wewe hujui kupika; huna mikono?

Umenioa nije nikikusaidie na wewe unisaidie; na wewe kapike mbona mimi nilipika jana?"

Hayo yalisemwa na Mwinjilisti Anatoli Antoni Shio, wa Kanisa la International Evangelism Church, Mivinjeni jijini Dar-Es-Salaam, wakati akinukuu baadhi ya maneno ya wanawake wasio waadilifu wanavyosaliti na kuvuruga ndoa zao.

Alikuwa anazungumza na waandishi wa habari kanisani kwake eneo la Mivinjeni katika Manispaa ya Temeke mwishoni mwa juma lililopita.

Akitahadharisha wanaotaka kuoa kufanya sala maalumu ili kuepuka kukurupukia ndoa zinazoleta majuto, Mwinjilisti Shio alisema ni muhimu wanaotaka kuoana kuchunguzana kwa kuwa wengi wao hujifanya kuwa watii na wema kabla ya ndoa lakini baada tu ya kufunga ndoa, hubadilika tabia zao na kuwa "mbogo."

Aliwashauri vijana kumuomba Mungu awasaidie kupata wachumba ambao wasiokuja kutafuta maisha ya kifahari, bali walioomba Mungu na akawakubalia kuja kuishi maisha matakatifu ya ndoa kama mke na mume.

Alisema hao ni wale walio tayari kushirikiana na waume zao katika kuhangaika, kuanza kutafuta, na kufurahia maisha yao yote kwa pamoja kwa kuwa, mke mwema hutoka kwa Mungu.

Aliwashauri wanawake kuzingatia ukweli kuwa wao ndio walezi wakuu wa familia na kama hawatakuwa na mifano bora kwa kuwa watii wa waume zao, watakuwa wanakaribisha dosari katika maisha ya familia zao.

Alitwatahadharisha wanaotaka kuoa kutofuata urembo na utajiri wa familia ya binti ili anufaike na misaada toka kwao.

"Lazima ujue yule mtoto unayemfuata kwa urembo au utajiri wa kwao, labda amelelewa katika familia ya kitajiri. Ukimwambia umuoe anataka ajue unafanya kazi gani, una mobitel, ajue kwako palivyo, aone kama una kabati au friji.

Akiona vipo, anajua mambo sawa, nitatanua kama kule nyumbani.

Anakuja kuendeleza maisha yake, na wala si kukaa chini ya mume. Sanasana atakuja pale ili tu, nae asikike kwamba ameolewa. Mke wa jinsi hii utakapokuja kuleta desturi zako ili akae kama mke, hamtawezana kwa kuwa hataafikiana na wewe kabisa.

Alisema wanawake wa namna hiyo, hata mwanaume atakapotaka kuleta taratbu na heshima kama mke anavyopaswa kumfanyia haiwezekani kwa kuwa alizoea kufanyiwa na sio kufanya wala kufanyiwa.

Vaeni rozari mkijua maana, umuhimu wake

Na Leocardia Moswery

WAKRISTO wamehimizwa kuvaa Rozari huku wakijua maana na umuhimu wake kwa kuwa haina maana kuitwa Mkristo kwa kuvaa rozari zaidi ya moja bila kujua maana na umuhimu wake.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mstaafu wa Utume wa Walei Jimbo Katoliki la Kigoma, Padre Cleophes Nyaruchali, wakati wa ibada iliyofanyika katika Kanisa la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Alisema ni aibu na hainisaidii kujionesha tu, na kuitwa Mkristo wakati hata umuhimu wa rozari na hauujui. "Sioni maana ya kuitwa Mkristo, huku ukijua kuwa haujui maana yake," alisema na kuongeza kuwa, wengine wanavaa rozari zaidi ya moja, lakini hawajui na hawataki kufanya juhudi ili kujua umuhimu wake. Alisema hali hiyo si njema kwa kuwa uvaaji wa rozari hauna budi kutotumika kama moja ya mtindo wa mavazi.

Padre Nyaruchali alisema kuwa, inashangaza na kusikitisha kuona kuwa, ulimwengu wa sasa umejaa chuki, vita na fujo na kwamba hata watu hawana haki ingawa wapo watumishi wengi wa Mungu.

Alisema pengine upo uwezekano kuwa hata wanaoishi katika nyumba za kitawa na maparokiani, wakaishi maisha ya chuki baina yao huku wananyimana haki na misaada baina yao. Alisema hali hiyo ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

Padre Nyaruchali alisema, "Pengine hata Wakristo wanawanyima haki zao bila kujua wanafanya nini katika utumishi wa Mungu."

Aliongeza kuwa, ili kuweza kufaulu na kuuona ufalme wa mbinguni hasa katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Mwaka 2000, ni lazima kutenda mambo mema na kuishi katika upendo kwa kuondoa maisha ya ubinafsi na chuki kwa wengine.

Padre Nyaruchali amewataka Wakristo wote kujitokeza kwa wingi kupiga kura huku wakiliombea taifa na kumwomba Mungu awapatie kiongozi bora atakayeweza kuongoza taifa.

Siku ya mavuno KKKT yaupisha Uchaguzi

Elizabethe Steven na Josephs Sabinus

KWA kuzingatia umuhimu wa uchaguzi, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Keko katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani, limeahirisha Maadhimisho ya Siku ya Mavuno toka Oktaba 29 hadi Novemba 5, mwaka huu ili kulipisha zoezi la Uchaguzi Mkuu.

Mkuu wa Jimbo la Temeke la Kanisa hilo, Mchungaji Astorn Kibona, ameliambia KIONGOZI ofisini kwake katika kanisa la KKKT Temeke kuwa, kanisa lake limeamua kuahirisha maadhimisho hayo kwa kuwa linazingatia umuhimu wa zoezi zima la uchaguzi nchini.

"Tumeonelea tubadili siku ya mavuno hadi tarehe 5 mwezi ujao ili watu wapate nafasi ya kushiriki uchaguzi. Hata hivyo, ninazidi kuwasisitizia waamini wangu wamtolee Mungu mavuno yao halali," alisema Mchungaji Kibona.

Awali katika mahubiri yake Jumapili iliyopita, Mchungaji Kibona ambaye pia ni mchungaji wa usharika huo wa Keko, aliwahimiza waamini kila mtu kwa nafasi yake kutoa shukrani kwa kadri Mungu alivyomjalia kwa kipindi cha mwaka mzima.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili, Mchungaji Kibona, alisisitiza utoaji wa mavuno hayo akisema, "Kila mtu aone wema aliojaliwa na Mungu na amshukuru. Kama utaona kwa mwaka mzima eti umshukuru kwa shilingi 500/ au 5000/= au ngapi, sawa.

Lakini, ulinganishe na fadhila. Wengine amewajalia kupata kazi, kufaulu masomo kupata watoto na wengine mambo yamewaendea vizuri wamepata vyeo, ni muhimu kushukuru."

Hata hivyo Mchungaji alisema mavuno au shukrani zinazotolewa kwa Mungu, ni zile zinazotokana na kazi halali machoni pa watu na Mungu.

"Sio eti uibe usishikwe, uje kushukuru na mali ya wizi au ujanjaujanja. Hiyo ujue itakwenda hivi hivi tu, lazima utoe kwa moyo ulichopata kwa jasho lako halali," alisema.

Wakati huo huo: Kwa niaba ya jimbo lake, Mchungaji Kibona ameuombea Uchaguzi Mkuu wa Jumapili hii uwe huru na amani. "Sisi tunaombea uchaguzi ufanyike na watu wapige kura kwa amani," alisema.

Kwa mara ya pili, Jumapili hii(Oktoba 29), Watanzania wanapiga kura kuwachagua Rais, wabunge na madiwani katika mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi vya siasa.

Uchaguzi wa kwanza wa namna hiyo ulifanyika mwaka 1995

Ishini maisha ya uhakika kiimani

Na Getrude Madembwe

PADRE Endrew Mwachibindu wa Parokia ya Magomeni katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, ameitaka jamii kuishi maisha yenye uhakika yasiyo ya kuhama hama.

Padre Mwachibindu alitoa wito huo alipokuwa akihubiri katika ibada iliyofanyika katika Jumuiya ya Mtakatifu Anyesi iliyopo Magomeni Makuti, jijini Dar Es Salaam, hivi karibuni.

Alisema Mkristo anatakiwa kuwa na imani thabiti badala ya kuwa mtu wa kuhangaishwa hangaishwa na kuhamahama kiimani.

"Tunatakiwa tuishi maisha yenye kueleweka mbele za Mungu na kamwe tusiwe watu wa kuhangaishwa na watu wengine," alisema Padre Mwachibindu.

Alimfananisha mtu anayehamahama katika imani yake, na anayeishi katika mabonde ambapo wakati wa mvua humlazimu mtu huyo kuhamia sehemu nyingine.

"Mtu ambaye anaishi maisha ya woga bila ya kuwa na Yesu huwa kama mtu anayeishi katika mabonde kwani mtu huyo wakati wa mvua huhama na kuangaika," alisema Padre Mwachibindu na kuongeza, "Hivyo basi ninyi msiwe kama watu wa namna hiyo. Mnatakiwa muwe na maisha ya kumpendeza Bwana na badala ya kuhangaika."

Wakati huo huo: Wananachi wametakiwa kuwachagua viongozi ambao wataleta matumaini katika nchi badala ya kuangamiza.

Hayo yalisemwa na Mchungaji Profesa Lutahoe, wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Huibert Kaiyiruki, kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, alipokuwa akihubiri katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani usharika wa Kipawa.

Alisema wananchi kwa ujumla hawana budi kumchagua kiongozi ambaye ana uchungu na nchi hii na wake siyo kuwachagua wale ambao wana uchu wa madaraka.

"Uhuru wa mwanadamu ni kuombeana mema na kutenda yaliyo mema na siyo kukandamizana wenyewe kwa wenyewe," alisema Mchungaji Lutahoe.