Makanisani Wiki hii

Shirikianeni, Msihofu kupinduana- Askofu awaambia wachungaji

Na Neema Dawson

ASKOFU wa Kanisa la Kianglikana Dayosisi ya Dar-Es-Salaam, Basil Sambano, amewataka viongozi wa vituo vya dini kushirikian na viongozi wageni wanaokuja makanisani kwao badala ya kuhofu kupinduliwa kwani Injili haina mapinduzi kama ilivyo siasa.

Askofu Sambano, aliyasema hayo wakati akitoa Sakramenti ya Kipaimara kwa watoto 20 waamini wa kanisa hilo usharika wa Kawe jijini Jumapili iliyopita.

Alisema viongozi kadhaa wa dini wamejenga tabia mbaya ya chuki za kimya kimya na wasiwasi dhidi ya wageni wanaotumwa kutembelea na kutoa huduma za kiroho katika makanisa na vituo kadhaa vya kutolea huduma za kiroho katika maeneo kadhaa ya makanisa katika Dayosisi ya Dar-Es-Salaam, wakidhani Mtumishi wa Mungu mgeni wanaweza kumpindua na kuchukua madaraka yao.

"Mbona sisi Maaskofu tunatoka hapa, tunakwenda nchi nyingine; tunatoa huduma katika makanisa ya nchi za nje. Mbona lakini tunapofika tunapokelewa vizuri na kushirikiana na wahudumu wa kule kueneza Injili; mbona hatujawahi kupinduana ? Katika Injili hakuna kupinduana; hayo mambo ya kupinduana yako kwenye siasa sio kwenye Injili",alisema.

Alisema kinachotakiwa kwa watumishi wa Mungu ni mahusiano mema baina yao wenyewe na wafuasi wao katika shughuli za Uinjilisti na utoaji wa huduma muhimu za kijamii kwa kuwa Neno la Mungu haliwezi kutangazwa na kupokelewa ipasavyo iwapo watumishi wa Mungu na wanafanya kazi kwa kunung’unika na kununiana kimyakimya huku wakioneshana ukarimu feki.

Alitahadharisha kuwa endapo hali hiyo itaachwa ieendelee, ipo hatari ikachocheana utoaji duni wa huduma za kijamii kama elimu, afya pamoja na huduma nyingine muhimu.

Akizungumzia suala la umuhimu wa Skramenti, Askofu Sambano alisema, inashangaza kuona kuwa wengi wa watu waliobatizwa na wanaotamba kuwa wameokoka na kuifahamu dini, matendo wanayoyafanya katu hayaendani na ulokole wao na badala yake wanatumia jina la Wokovu na kujitangaza ili kujipatia umaarufu.

Aliwaasa watoto waliopata sakramenti hiyo kuwa kutokuitumia sakramenti hiyo kujivunia na kujitangaza kuwa ni Wakristo wakati matendo yao ni kinyume na hali halisi ya Ukristo kwa kuwa imani bila matendo ni bure.

Askofu Kilaini ataka waliopata kipaimara wasiyumbeyumbe

Na Gertuder Madembwe

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhasham Method Kilaini amesema vijana waliokwishapata Sakramenti Takatifu zikiwamo ya Kipaimara na ubatizo, wameshakomaa kiimani na kamwe wasikubali kuyumbishwayumbishwa na watu wa imani nyingine

Mhasham Kilaini aliyasema hayo wakati akitoa Sakramenti ya Kipaimara katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Katoliki la Parokia ya Maximillian Kolbe lililopo Mwenge Jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita.

Alisema vijana hao wakiwa na Sakramenti hiyo ya kipaimara wanaweza kukataa jambo lolote baya kwa sababu wao tayari wameshafahamu lipi baya linaloweza kubomoa imani yao hasa baada ya kugiribiwa mawazo na watu waimnai tofauti sambamba na matendo yasiyoendana na Mungu.

"Nyinyi vijana mnaopata Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kamwe msikubali kuyumbishwa na imani nyingine sababu nyinyi tayari mmeshakomaa kiimani na tayari mmeshapata sakramenti hizo takatifu za msingi,"alisema na kuongeza kuwa, "Mkiwa na sakramenti hizo takatifu mnaweza kukataa jambo lolote lile baya kwani tayari mmeshajua zuri na baya"

Alisema jamii inapaswa kuwasaidia vijana hao katika kuwaongoza na kutenda yale ambayo ni mema kuwa na maadili yale yanayoenenda na Ukristo wao kwa kuwaelekeza kimaadili na wala sio kwa kuwatishia kuwawachapa.

"Mnapaswa kuwa wachungaji wema maana hata neno linasema kuwa mimi ni mchungaji mwema na mchungaji mwema huwachunga kondoo zake vizuri ili wasipotee, je! Unamjenga mwanao vizuri kwa wema yaani asikuogope?" alihoji.

Aliwasisitiza vijana wa Kikatoliki waliopata Sakramenti hizo za Msingi, kushiriki katika jumuiya ndogo ndogo kwani jumuiya hizo hazina mambo ya ugomvi bali hupatanisha na kuwataka wapeleke majumbani mwao sala yaani wasali kabla ya kula na wakati wa kwenda kulala.

Aliwataka wazazi na wasimamizi wao kutowawekea vipingamizi vyovyote pindi wanapotaka kusali bali wawahimize katika jambo hilo na wao vijana wakifanya hivyo watakuwa wamekomaa kikristo.

Askofu Muanglikana ashauri kuchagua viongozi bila Unafiki

Na Leocardia Moswery

Askofu Msaidizi na Mshauri Mkuu wa Kanisa la Angalikana Dayosisi ya Dar es Salaam, mchungaji Frank Kajembe ametoa wito kwa Watanzania kuwachagua viongozi bila unafiki wala madhumuni ya kujinufaisha kibinafsi katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Alitoa wito huo wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Mchungaji Kajembe alisema, "Wananchi wawachague viongozzi bora na bila unafiki wowote ili waweze kuleta maendaleo na kuiweka nchi iwe katika amani zaidi".

Alisema kuwa uwezo wa kutangaza siasa na dini ni kazi yao na pia kazi kubwa ni waliyonayo viongozi wa dini na waumini wao, ni kuwaombea wanasiasa ili waweze kutenda kazi yao kwa ufasaha.

Mchungaji Kajembe alisema kuwa Wakristo wanapaswa kupiga magoti ili kuiombea nchi iwe na amani na upendo ili kufanikisha Uchaguzi Mkuu ujao ufanyike bila vurungu.

Alisema kuwa viongozi wa upinzani wanapaswa kuomba kwa imani kubwa bila kuwa na vurungu yoyote ili kuiweka nchi ya Tanzania iwe salama pamoja na kumpata kiongozi bora atakayeweza kuwaongoza vema wananchi kulekea maendeleo.

Amewataka wapinzani kuwa watulivu na w kuridhika na matokeo ya uchaguzi bila malalamiko endapo chama chochote kitashinda.

Wasabato waambiwa,tangazeni wenye ukimwi, kunusuru wengine - Ushauri

Na Masha Otieno

IMESHAURIWA kuwa wagonjwa na wanaokufa kwa ugonjwa wa Ukimwi hawana budi kutangazwa wazi ili kuepusha hatari ya kasi ya maambukizo kwa watu wengine wasio wafahamu waathirika.

Ushauri huo umetolewa na Dk. Gilbert John wa hospitali ya Misheni ya SDA Kanisa la Wasabato nchini wakati alipokuwa akizungumza na waamini wa Kanisa hilo juu ya janga la Ukimwi kwenye mkutano wa wiki 3 mfululizo unaofanyika Kurasini jijini Dar es Salaam.

Dk. John amesema ipo kasumba mbovu inayoendelezwa na baadhi ya wanajamii mpaka sasa ambapo mtu akiugua ama kufa kwa Ukimwi, ndugu zake huficha ukweli wa ugonjwa uliopelekea mauti yake na badala yake kusingizia ugonjwa mwingine hali aliyosema inachangia mtu mwenye virusi kujipa moyo kuwa yuko salama hivyo kuambukiza wengine ambao hawajaathirika.

Alifafanua kuwa, kuwatangaza wazi kuwa fulani ana Ukimwi ama amefariki kwa Ukimwi siyo kumdhalilisha bali ni kueleza jamii ukweli wa mambo ili ichukuliwe tahadhari.

Amesema ukweli na uwazi unahitajika katika kutoa taarifa za Ukimwi hususani katika kipindi hiki ambacho ugonjwa huu umekuwa tishio kupita kitu kingine chochote duniani.

Dk. John pia amezidi kufafanua kuwa tabia ya ndugu na jamaa kuficha wenzao wanaougua ugonjwa wa Ukimwi pia imekuwa ikichangia kukwamisha upatikananji wa takwimu kuwa ni watu wangapi hasa wanaogua ugonjwa huo hapa nchini.

Kwa mujibu wa mpango wa Taifa wa kudhibiti Ukimwi NACP mpaka sasa idadi ya Watanzania wapatao milioni 2.4 wanasadikiwa kuwa na virusi vya ugonjwa hatari wa Ukimwi. Tanzania pia imo kwenye ukanda wa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ‘Sub Saharan Afrika’ ambazo ndizo zinaripotiwa kuathirika zaidi na Ukimwi duniani.

Amewatahadharisha Watanzania kokote walipo kujipa matumaini na kutoupuza na badala yake wakuchukue tahadhari dhidi ya ugonjwa huo usio na kinga ambao njia yake kuu ya kuenea ni vitendo vya uasherati

Amewashauri waliokwisha ambukizwa ugonwjwa kuishi kwa matumaini pasipo hofu na kusafisha njia ya matendo yao kwa Mungu wangali hai ili wajitayarishe kwa maisha mapya ya milele na yenye furaha huko mbinguni ikiwa ukimwi utakatiza maisha yao hapa duniani

Fanyeni kazi kwa mikono sio kwa midomo

Na Aghata Rupepo, DSJ

Wito umetolewa kwa wanawake wazee kote nchini kutumia muda wao mwingi kufanya kazi za vidole kuliko kukalia kupiga zogo.

Mchungaji James Machage, wa Kanisa la Waadiventista Wasabato (SDA), Jimbo la Mara, aliyasema hayo Jumamosi iliyopita wakati wa ibada ya siku ya Dorcas iliyofanyika katika kanisa la (SDA) Ukonga, jijini.

Akitoa mfano, alisema Dorcas alikuwa ni mwanamke pekee aliyependa kufanya kazi za vidole kuliko kushindia maneno mengi yasiyo na matendo, tofauti na ilivyo sasa kwa watu wengi kupenda kufanya kazi za midomo kuliko mikono, (Mdo. 9:34-43).

"Wanawake wazee wa sasa wamechangia kwa kiasi kikubwa kuwapotosha wanawake vijana kwa kushindwa kuwapa mafundisho yanayostahili watakapokuwa katika nyumba zao kitu kinachochangia ndoa nyingi kuyumba".

Aliongeza kusema kuwa wanawake wazee wamesahau wajibu wao kama wazee wa kutoa mafundisho kwa wanawake vijana, kitu kinachosababisha wanawake vijana kutoyaelewa vema majukumu yao ndani ya nyumba zao.

"Sasa inapotokea mitafaruku ndani ya ndoa za hawa vijana ni nani wa kulaumiwa kama si ninyi wazee?" alihoji.

Mchungaji Machage, alisema ni wajibu kama wazee kuwapa mafundisho yanayostahili kwa vijana ili waweze kutoa mafundisho yanayostahili kwa kizazi kijacho.

Akizungumzia suala la imani kwa mashirika, Mchungaji Machage, alisema, kwa sasa imani kwa mashirika imekuwa ikipungua siku hadi siku badala ya kukua kila siku kwa kuwa kiasi ndani ya maisha ya watu kimepungua mno na kwamba hii ndiyo sababu sasa wazee wakubwa wanawabaka watoto wadogo.

Alisema ili mtu aweze kuyaona mafanikio ya Ukristo, ni lazima awe na roho ya imani katika maisha yake, (Mt.17:20).

Mnaookoka msiwanunie wengine, KKKT lashauri

Na Elizabeth Steven

WAKRISTO waliookoka wametakiwa kutowanunua na kuwapuuza ambao hawajajitangaza au kuingia katika madhehebu ya kilokole kwa kuwa huo sio upendo wa ki-Mungu na badala yake ni unafiki.

Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na Mwinjilisti Msafiri Gwasa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, katika usharika wa Mabibo jijini Dar-Es-Salaam, alipokuwa akihubiri katika ibada kanisani hapo.

Alisema ‘wewe ukimwekea mwenzio X kwa vile yeye ni mlevi, au eti kwa kuwa hajaokoka, basi wewe ujue hujaokoka. Ukimwona mwenzio amekunja uso mwambie pole tena mwambie ipo kazi usione uchungu kuwa karibu na mwenzio eti kwa kuwa hajaokoka bali, mpokee na mpende. Hivi unadhani utampendaje Mungu hali ndugu yako humpendi?".

Alisema upendo ndio unaomfanya mtu kuishi hata katika mazingira yenye maudhi uwe umeokoka, au hujaokoka; ni vizuri ukawa na kwa wenzio bila kujali tofauti za kimadhehebu na kudumisha upendo baina yao kwani ndio utaokufanya uishi vizuri na wenzio.

"Haipendezi hata kwa baba na mama kuwa na ugomvi mara kwa wa mara kwa mara katika familia, unadhani katika katika hali kama hiyo, watakuwa na raha? Sana sana baba au mama wa namna hiyo akitoka nyumbani, watoto watabaki wanafurahi, akirudi inakuwa huzuni. Ulokole na upendo wa namna hiyo ni unafiki; haufai." Alisema.

Mwinjilisti Gwasa ameitaka jamii kuwaepuka watu wanaotumia Neno la Mungu kwa kama mwavuli wa kuwakinga maovu yao yasionekane kwa jamii.

"Waepukeni wanaotumia neno la Mungu kumbe ndani ya roho zao sio kama walivyo; waepukeni watu hao maana ni hatari mno." Alisema

Alisema kuwa ili nyumba ziwe na upendo basi hazina budi kumpenda Mungu na wao wenyewe kupendana ili kuepusha matatizo yanayoweza kutokea katika familia kutokana na kukosa upendo.

"Baraka ni wewe mwenyewe ndiye unaweza kuwa unaiondoa katika nyumba yako. Kwanini haujiulizi hayo matatizo yametoka wapi, mbona watoto wangu wamekuwa hivi (machangudoa), au mbona wanakuwa hivi na hivi. Ili nyumba zetu zipendeze, lazima tupendane na kumpenda Mungu" alisema.