Makanisani Wiki hii

Kanisa la Assemblies of God lavunjwa, lachomwa moto Dar

Na Leocardia Moswery

Kanisa la Evangelistic Assemblies of God (Sayuni),la Yombo Dovya Wilayani Temeke, limebomolewa ikiwa ni mfululizo wa matukio ya kadhaa yaliyokwishatokea ikiwa ni pamoja na kuchomwa moto.

Kwa mujibu wa Mchungaji wa Kanisa hilo Amani Zeno, kanisa hilo limekuwa likihujumiwa na majirani ambao hakuweza kuwataja.

Alisema kabla ya kuchomwa moto, kanisa hilo lilivunjwa na kwamba hata baada ya kulijenga tena, hivi karibuni limevunjwa tena mara mbili mfululizo na kuwafanya waumini wasalie nje.

"Kwa mara ya kwanza, kanisa lilivunjwa, tukajenga upya, likachomwa moto tukalijenga, wakavunja. Halafu tukajenga tena, wamevunja. Hivi sasa tunasalia nje," alisema na kuongeza,

"Wakazi wa hapa wanatupiga vita mno kutokana na mazingira yaliyotawaliwa na wenzetu wa imani tofauti, na hata wakati mwingine wanatutupia mawe tukiwa tunasali."

Mchungaji Zeno, alisema pamoja na yote hayo, hivi sasa wamefyatua matofali zaidi ya 3000 kwa ajili ya kujenga kanisa imara ambalo litaweza kudumu kwa muda mrefu na akaongeza kuwa linatarajiwa kugharimu Shilingi milioni 2.5 ambapo alidai kuwa hawana akiba yoyote bali wanajenga kwa kutumia nguvu zao wakisaidiwa na kanisa mama la Temeke linaloongozwa na Mchungaji Denis Masalu.

Awali Kanisa hilo lilikuwa likijengwa kwa miti na kuezekwa kwa makuti na hivi sasa wanatumia turubai.

Alisema pamoja na kutopata msaada sehemu nyingine wanatazamia kuanza msingi mwezi ujao kwa kushirikiana na waumini ili kuondokana na giza linalowatawala kila mara.

Hata hiyo Mchungaji Zeno aliwaomba wahisani wa ndani na nje kusaidia kanisa hilo ambalo alisema limekuwa likikubwa na majaribu makubwa.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia vijana kadhaa wa eneo hilo wakiwadhihaki waumini hao wakati wa ibada yao ya Jumapili iliyopita kwa kutumia maneno "Niambpviiie! Niambpviiie Yesu!"

Mapema wakati wa Pasaka, mwaka huu Kanisa moja Katoliki lilichomwa moto huko Tanzania visiwani na jingine la Kipentekoste kuchomwa moto katika maeneo ya Mbagala jijini, hali ambayo ilileta hofu kwamba sasa uhuru wa kuabudu unaohimizwa na wapenda amani na Serikali umeanza kuwa na dosari.

Waumini wa Kanisa la Sayuni wameiomba Serikali kuingilia kati kuwahakikishia usalama wao kwani wana haki ya kuabudu katika eneo lolote halali, ili mradi hawavunji sheria.

Tumieni muda wenu kuzungumza na Mungu - Wito

Na Getruda Madembwe

WITO umetolewa kwa Wakrist kote ulimwenguni kutumia muda wao kuzungumza na Mungu ili kupata wasaa wa kumuelezea shida zao na kujifunza na hatimaye kulitumia vizuri Neno lake katika maisha. Pia, kulitumia vema kuwafundisha wengine bila kupotosha maana.

Wito huo ulitolewa na Bw. Samsoni Luhigo,wakati akizungumza katika ibada iliyofanyika katika kanisa la African Inland Church (AIC), usharika wa Magomeni Jumapili iliyopita.

Bw. Luhigo ni msharika wa kanisa hilo lililopo Jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa ili kuishi katika maisha ya Kikristo ni lazima uwe na muda wa kuongea na Mungu na hapo utakuwa salama katika kila jambo utakalolifanya kwa sababu utakuwa upo karibu na Mungu.

Aidha Bw. Luhigo aliwataka waamini hao kumtegemea Mungu na kumpelekea shida zao zote kwani yeye anatosha katika kila kitu; iwe katika mahitaji ya kimwili au ya kiroho kwa kuwa Mungu ndiye muweza wa yote.

"Wakristo wezangu, tunatakiwa tuwe na muda wa kuzungumza na Mungu kwani kwake tutapata maarifa pamoja na rehema zake kwani ni za milele na uaminifu wake ni vizazi hata vizazi"

Alisema na kuongeza, "Na kama tukiwa karibu na Mungu tutapata mahitaji yetu yawe ya kimwili au ya kiroho hivyo, nawashauri Wakristo wenzangu; nasisitiza zaidi; tuwe karibu na Mungu na kamwe tusiwe mbali naye"

Akiendesha ibada ya Usharika Mtakatifu Askofu wa AIC, Charles Salala, alisema kuwa sasa kila mtu ana haki ya kuisogelea meza ya Bwana na wala si kwa kuwakilishwa na mtu mwingine sababu siku ya Ijumaa Kuu, Yesu Kristo wakati wa mateso yake lilipasuka pazia la hekalu na kuwafanya watu wengine waingie mahali pale patakatifu.

"Sasa hatuna hofu tena ya kuisogelea meza ya Bwana kwa kuwa Yesu Kristo siku ya mateso yake Ijumaa Kuu pazia la hekalu lilipasuka na hivyo kufanya watu wote waingie mahala pale patakatifu na wala si kwa kuwakilishwa na mtu mwingine kama ilivyokuwa katika Agano la Kale" alisema Askofu Salala.

Ugonjwa wa uchoyo unasambaa- Padre

Na Josephs Sabinus

JAMII imetahadharishwa kutotawaliwa na tabia ya uchoyo inayozidi kushamiri na badala yake, kila mmoja awe mkarimu anayejitoa mwenyewe kwa manufaa ya wengine ili kusaidiana katika mazingira mbalimbali inapobidi ikiwa ni moja na kutimiza mapenzi ya Mungu badala ya kung’ng’ania ubinafsi.

Onyo hilo lilitolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Utume wa Walei ya Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania (TEC), Padre Nicholous Segeja alipokuwa akihubiri katika ibada ya Ijumaa ya Kwanza ya mwezi Aprili katika Kanisa la TEC, Kurasini Dar-Es- Salaam.

Alisema hivi sasa sehemu kubwa ya jamii ya watu imetawaliwa na uchoyo wa ukarimu dhidi ya wengine hata pale inapoonekana dhahiri kuwa ukarimu huo unahitajika kwa kiasi kikubwa na akasema hali hii ni hatari mno hasa kwa watu wanaomjua na kumtegemea Mungu katika maisha yao.

"Inabidi watu tuchoteane ukarimu hata kama ni kwa kitu kidogo. Hapo ndipo Mungu anaweza kutubariki zaidi. Hivi sasa tumekuwa na ugonjwa wa uchoyo. Tunakuwa wachoyo wachoyo hata katika familia zetu. Tunakuwa wachoyo wa vitu, hata tunakuwa wachoyo wa kumtolea Mungu sadaka."

"Inakuwa ni vigumu hata kuonja matunda mema ya ufufuko wa Yesu kwa sababu ya ugonjwa huu wa uchoyo. Tunapaswa kuwa na moyo wa ukarimu ili mwenyezi Mungu atuongezee zaidi."alisema Padre Segeja na kusisitiza kuwa tabia hiyo aliyoiita ugonjwa, haina budi kutokomezwa kabisa ili isizidi kusambaa.

WAKATI HUOHUO: Akitoa maombi maalumu kanisani hapo, Padre Segeja aliiombea Tanzania kufikia mfumo bora wa uchumi na soko huria utakaowawezesha wananchi wote kunufaika na matunda yake na hivyo kuboresha hali zao za maisha.

Kila Ijumaa ya Kwanza ya mwezi, wafanyakazi wote wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), huendesha ibada ya pamoja ili kumshukuru Mungu kwa mapaji yote aliyowajalia na kutoa maombi yao kwa Mungu, juu ya neema katika mwezi mpya.

ASKOFU MWALUNYUNGU AWAAMBIA WANAWAKE:

Mwigeni Bikira Maria, msizuzuke na suruali mpya

Na Peter Makanile, Masasi

ASKOFU Magnus Mwalunyungu wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi, amewataka wanawake kuiga na kufuata msimamo wa Bikira Maria na badala ya kurubuniwa na wanaume na kubadili misimamo ya kimaisha.

Akiongea katika misa ya kuhitimisha Jubilei ya WAWATA, adhimisho lililofanyika kijimbo katika Parokia ya Mangaka hivi karibuni, Mhashamu Mwalunyungu alisema, "Mama Bikira Maria alikuwa na msimamo thabiti alipotokewa na Malaika Gabrieli na kuelezwa kwamba atamzaa mtoto mwanaume, naye atamwita Emanuel. Akamuuliza Malaika, litawezekanaje hilo?

Aliuliza swali hili kwa sababu alikuwa na msimamo na alijua kuwa yeye bado bikira. Malaika Gabrieli Maria kuwa litawezekana kwa uwezo na nguvu ya Roho Mtakatifu, na ndipo Mama Maria alipokubali na kutamka kuwa yeye ni mjakazi wa Mungu na ifanyike hivyo."alisema na kuongeza,

"Msikubali kwa urahisi eti kwa sababu mwanaume amekuja na mavazi au sura nzuri; waulizeni litawezekanaje jambo hilo"? alisema

Aliwataka akinamama kuwa wavumilivu katika magumu mfano wa Mama Maria ambaye alivumilia alipomfuata mwanae Yesu Kristu aliposulubiwa mpaka kufa.

Katika hotuba hiyo, Askofu aliwasisitiza waumini wasiweke kiraka kipya katika vazi kuukuu.

Alisema kiraka ni Ukristu wetu na vazi kuukuu ni mambo ya kipagani. Akitoa mifano katika usemi huu alisema, Mkristu kuwa na wake wengi au mke kuwa na wanaume zaidi ya yule mmoja wa ndoa, na kuangaliwa kwa ramli au kupigiwa bao ni kuweka kiraka kipya katika vazi kuukuu.

Aliongeza kuwa kwa watumishi wa Mungu kama mapadre na watawa kujihusisha na matendo ya ndoa ni kuweka kiraka kipya katika vazi kuukuu.

Kadhalika Mwenyekiti wa Parokia ya Mangaka aliusifu mshikamano uliooneshwa na wanawake wa Jimbo hilo katika kufanikisha adhimisho hilo. Alivitaka vyama vingine vya kitume kuiga mshikamano huo.

Adhimisho hilo lilifanyika kuanzia Machi 23 hadi 25, mwaka huu, kwa mafungo, mafundisho, ibada za Rozari, Moyo Mtakatifu wa Yesu, Njia ya Msalaba na misa.

Adhimisho hilo lilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Utume wa Walei Jimboni hapa Padre Jakobo Mchopa na Paroko wa Parokia ya Mangaka Padre Fransis S.D.S

Wakristo wahimizwa kuwa na imani ya matendo

Na Elizabeth Steven,

WAKRISTO kote nchini wametakiwa kuonesha imani ya kiroho kwa vitendo, kwani imani haiwezi kuonekana kwa macho ila kupitia matendo ya mtu.

Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Kenan Kilo, ambaye ni Padre wa Kanisa la Kianglikana Parishi ya Mwenge, jijini.

Akihubiri katika ibada ya kawaida Jumapili iliyopita Kenon Kilo, alisema ni kwa njia ya kuuchunguza mwenendo wa kila siku wa mtu pekee ndipo unapoweza kumtambua Mkristo mwenye imani na asiye nayo.

Alisema baadhi ya Wakristo huonesha wazi kuwa hawana imani kwa tabia zao za kupuuzia kuhudhuria ibada kanisani.

Kenan Kilo, alionya kwamba Wakristo wa namna hiyo hutaka kumwona Mungu kwa macho kama alivyokuwa Tomaso, lakini akaonya kuwa heri wale wanaoamini bila kuona.

Juu ya wale wanaowategemea wanadamu Kenan Kilo, alisema hawawezi kamwe kumwamini Mungu kwani wataziona Habari za Mungu kama karaha kwao.