Makanisani Wiki hii

Msijiite Wakristo bila viwango, Ukristo una viwango - Mhubiri

Na Mwandishi Wetu

"Ingawa vipo vidini vingi vingi, siyo vyote wala waamini wote wenye viwango vya kutosha kujiita Wakristo. Lazima Wakristo wote wawe na viwango vya Ukristo maana Ukristo una viwango kamili. Hata kazini watu wanaajiriwa kwa viwango vya kazi na elimu."

Ushauri huo ulitolewa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Keko, katika dayosisi ya Mashariki na Pwani, na Bw. Samwel Lwiza, wa NewLife Crusade usharika wa Yombo alipokuwa akihubiri kanisani hapo hivi karibuni.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakiupaka matope Ukristo kwa kujiita Wakristo wakati matendo yao hayalingani na kiwango halisi cha Ukristo kama alivyokuwa Kristo mwenyewe. "Huwezi kuwambia watu wewe ni Mkristo au Mlokole wakati unashindia kwenye madanguro, bangi, msengenyo na wizi; hivyo sio viwango vya Ukristo."

Alisema Mlokole au Mkristo yeyote ambaye anajihusisha na vitendo vya wizi, uchoyo, majungu, masengenyo, uvutaji bangi, uzinzi au uasherati, mwenye chuki, majivuno na asiyependa kuwasaidia wenye shida bila kutafuta sifa machoni pa watu, bado hajastahili kujiita Mkristo na kwa kufanya hivyo hana budi kujua kuwa anakufuru hadi pale anapokuwa anatumia juhudi zake zote kufanya matendo yenye kumpendeza Mungu.

Bw. Lwiza aliwataka Waamini wote wa dini ya Kikristo kila mtu kwa nafasi na nafsi yake, kujiuliza wana viwango gani katika Ukristo wao.

"Lazima ujiulize wewe mzee wa kanisa, kijana au mama, una kiwango gani cha Ukristo maana hata kazini wanaajiri watu kulingana na viwango vya kazi na elimu; kama ni diploma, digrii au chochote. Ndivyo ilivyo hata kwa Ukristo, una viwango, siyo kujita tu Wakristo ovyo ovyo bila kuwa na viwango vya Ukristo" alisema.

Akifafanua mahubiri yake, Bw. Lwiza alisema, Kiwango muhimu cha Ukristo ni Kubatizwa, kuamini na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu.

Naye Getruda Madembwe: anaripoti kuwa wajane wa kike ulimwenguni kote wametakiwa kutojutia hali ya kufiwa waume zao na badala yake wafanye kazi kwa bidii wakimtegemea Yesu Kristo kama mume wa kudumu.

Hayo yalisemwa na Bi. Anna Semu mjumbe wa New Life Crusade ambaye ni mjane katika ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Kawe, dayosisi ya Pwani na Mashariki, jijini Dar es Salaam.

Alisema wanawake wengi huanza kujuta pindi wanapofiwa na waume zao kwani hufikiri maisha yao hayana thamani tena na kusema haipaswi kuwa hivyo na badala yake wampokee Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wao na mume wa kudumu..

"Tena nataka niwaambie wanawake wenzangu waliofiwa na waume zao wasijute wala kufikiria wataishi vipi kwa kuwa eti hawana waume zao na tena wasibabaike bali wampokee Bwana Yesu kwani ndiye mme bora zaidi wa kuwa naye maana anadumu daima." Alisema

Bi. Semu ambaye ni mwalimu mkuu wa shule moja ya awali inayomilikiwa na kanisa la KKKT la Msasani, alisema wanawake hao hawana budi kudumu katika imani kwa kuwa Yesu anadumu katika ulimwengu wa mwili na ule wa kiroho.

Fichueni maovu ya viongozi, msiogope kufukuzwa

lAsema Mbeya machangudoa huitwa maiti

MWINJILISTI Wilnevly Lyimo wa Kanisa la Kiinjili la Kiltheri Tanzania (KKKT), usharika wa Tandika jijini Dar Es Salaam, ameitaka jamii ya Watanzania kujenga utamaduni wa kuwafichua viongozi waovu, wawe wa dini na serikali bila kuogopa fitina, chuki wala kufukuzwa kazi.

Mwinjilisti Lyimo alitoa wito huo alipokuwa akizungumza katika ibada ya Jumapili iliyopita katika kanisa la K.K.K.T, usharika wa Tabata katika dayosisi ya Pwani na Mashariki, jijini Dar Es Salaam.

Alisema hakuna haja ya kuogopa kumuonya au kumfichua kiongozi yeyote; wa dini au serikali nayekwenda kinyume na maadili ya jamii.

"Watu eti wanaogopa kuwaonya viongozi wao wakihofia eti atakuwa amewashitaki mkubwa wake nae anahofueti asije atafukuzwa kazi. Ni kweli, ndiyo maana siku hizi hata Kanisa limekosa nguvu ya kuonya. Kiongozi yeyote anayekwenda kinyume na maadili ya jamii, anayepotosha; ni lazima aonywe. Hakuna haja ya kuogopa; awe kiongozi wa dini, siasa au nini; wote lazima waonywe ili wafuate maadili."" alisema.

Alisema kuna baadhi ya nchi hapa duniani ambazo hazina makanisa kabisa na nyingine zinayo lakini hayana watu kwa kuwa wamekimbilia mafichoni na ndivyo ilivyo katika familia nyingi hata nchini utakuta baadhi ya familia zina kila kitu isipokuwa vitabu vya dini kutokana na jamii kupoteza imani kutoka kwa viongozi wa dini au hata serikali.

Wakati huo huo: mwinjilisti huyo amewataka wazazi kushirikiana ili kulinda maadili katika familia zao kwa kuwa mzazi ambaye hataonesha mwenendo mwema, ni lazima tabia hiyo mbaya ataiambukiza na kuipotosha jamii nyingine kwa jumla.

"Somo kubwa la watoto wetu ni uwezo wetu wa kuwafunza tabia nzuri. Hata sku moja mlezi usitarajie kuwa kama wewe una tabia mbovu, eti mwanao atakuwa na tabia nzuri, haiwezekani, ataiga hiyo yako chafu na wala usitegemee huyo mtoto awe mcha Mungu huku wewe uko hivyo," alisema

Alionya dhidi ya watu wanaodanganyika na vishawishi vikiwemo vidogovidogo kama chips vinavyowafanya waendekeze maisha ya anasa.

Akitoa mfano wa watu wa namna hiyo huko mkoani Mbeya, Mwinjilisti Lyimo alisema, "Wanawake kule Mbeya wasiojiheshimu; hawa changudoa, kule wanaitwa maiti na wakina baba sasa badala ya kuitwa haya majina ya huku kama eti, buzi, kule wanaitwa mtaji. Ni heri uende kanisani ukaitwe mtaji wa mahubiri kuliko kuitwa mtaji kwa kuhonga."

Mwinjilisti Lyimo aliwatahadharisha wanafamilia kuwa makini na kuepuka migogoro mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile itokanayo na watu wanaofuatilia na kubomoa maisha katika familia za wengine kwa kuwagombanisha kutokana na uchonganishi wao.

"Nyumba nyingine kila siku lazima baba na mam wpeane makonde na hii inatokana na kwamba hawajui ni nani anyesababisha makonde hayo yatokee, baba mjnja ni yule atakaye amua kufuatilia na kugundua ni nani anaysababisha na mara nyingi unawez kusikia kuwa ni wifi." alisema.

Msije kanisani ili kuonekana kwa watu

Na Mwandishi Wetu

Kanisa la Kiangalikana Dayosisi ya Dar es Salaam Usharika wa Tabata limewataka waamini wake kuwa na imani na dini badala ya kuhudhuria kanisani ili kuoneakana kwa watu.

Hayo yalisemwa na Emanueli Mwezimpya ambaye ni muamini wa kanisa hilo alipokuwa akizungumza katika ibada iliyofanyika kanisani hapo hivi karibuni.

"wengi wenu wanakuja kanisani ili mradi wameonekana kuwa nao wanakuja kanisani. Tunakuja kufuata Neno la Kristo siku ya Pasaka kanisa lilijaa kiasi ambacho lilionekana dogo lakini leo hakuna na hao ni wale ukiangalia kwenye kitabu cha mahudhurio utakuta majina yao yaliandikwa mwaka jana kwenye Krismasi na mwaka huu kwenye Pasaka"

Mwezimpya alisema kuwa mambo sana yanatokea katika jamii zetu ndani ya nyumba zetu hiyo yote ni kwa sababu ya kutokuwa na imani.

Alisema kuwa kila mtu awe Muislamu au Mkristo ni vizuri akawa na imani matumaini na aamini kuwa Yesu amefufuka na asiyeamini basi amrudie tena kwani kila mtu atabeba mzigo wake.

Kuna wengi waliobahatika kuwa wazuri wa sura maumbo rangi na hata tabia zao kuwa nzuri lakini kwa kuwa hawamwamini Yesu mfufuka, hawana imani na dini zao hawajaolewa na wala kupata mchumba.

"Kuna nchi ambazo hawajui kanisa kwa sababu ya kutoamini nenda Uganda mauaji yanatokea ya kusikitisha maiti zinafukuliwa ovyo, yote hayo ni sababu ya kutokuwa na imani. Imani ndiyo itakupeleka katika nyumba yake Bwana"

Aidha aliongeza kusema kuna watu waliobahatika kuwa viongozi katika ngazi mbalimbali Serikalini na hata kanisani lakini bado wanadhani na kuamini eti vyeo hivyo wanavipata kwa juhudi za waganga wa kienyeji.

"Wengine wanaenda kwa waganga kutafuta wachumba kutafuta vyeo kutafuta watoto kwa nini usimuamini Yesu? Omba Yesu akusaidie; Hivi kwa nini ulikubali Yesu afe na kufufuka wakati humuamini?" alioji kwa mshangao

Waanglikana wawafadhili maalbino

Na Agatha Rupepo

KANISA la Anglikana Ukonga limetoa jumla ya shilingi 50,000 kama msaada wa miamvuli kwa maalibino wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Akitoa msaada huo kwa niaba ya waamini wa kanisa hilo hivi karibuni Mchungaji Mathayo Machoya amesema ni wajibu kwa Taifa kuwasaidia walemavu hao kwa sababu wao hawakupenda kuzaliwa na ulemavu huo.

"Inashangaza sana kuona baadhi ya wanajamii wanawatenga maalbino , hebu fikiria ungekuwa ni wewe ungejisikiaje? Jamani tuwapende wenzetu kwani wao hawakupenda kuwa hivyo".

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Ustawi wa Jamii na Uchumi Tanzania (CHAUJUTA) Bw. Nicolas Lameck amesema lengo kubwa la CHAUJUTA ni kuzunguka katika makanisa mbalimbali kuomba misaada ya mwamvuli kwa ajili ya maalbino.

Kwa mujibu wa Bw. Lameck mpaka sasa wameishazunguka katika makanisa saba ambapo Kanisa Katoliki Ukonga limetoa jumla ya miamvuli 160.

Amesema CHAUJUTA inampango wa kuwasaidia walemavu wa shule ya Jangwani vifaa vya kujimudu kuwawezesha kutembea. Ikiwa ni pamoja na kutoa vitabu kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba wa shule ya jeshi la wokovu, ubalozi wa Uingereza umeahidi kuwasaidia katika zoezi hilo .

Mpaka sasa tayari maalbino wanane wameshapelekwa katika shule ya jeshi la wokovu "Tumeamua kuwakusanya pamoja ili misaada itakapotokea iwe rahisi kuwasaidia watoto hao".

Kwa kuanza CHAUJUTA inawasaidia maalbino wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na hapo baadaye itakuwa ni kwa nchi nzima.

Bw. Lameck amesema tatizo kubwa kwa sasa chama hakina mfadhili wa kudumu kitu ambacho hakina kinasababisha wanachama watafute misaada kutoka makanisani

Wanawake nchini wadaiwa kuchangia kubomoa maadili

Na Mwandishi Wetu

Wanawake nchini kote wameleumiwa na kuelezewa kama watu ambao baadhi yao huchangia kwa kiasi kikubwa, mmomonyoka wa maadili katika jamiii kutokana na mitindo ya maisha wanayoishi na kuwalelea watoto wao.

Lawama hizo zilitolewa hivi karibuni na Paroko wa Parokia Katoliki ya Magomeni katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es alaam, Padre Merikiyoni Butambi alipokuwa akiendesha ibada kanisani hapo siku ya kusherehekea Jubilei ya Akina Mama iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Magomeni jijini Dar Es Salaam .

Alisema, "Inasikitisha sana kuona akina mama wanakuwa wa kwanza kupotosha watoto wao, kimaadili , mama anadiliki kutoa maneno machafu na hata kutoa matusi mazito mbele ya watoto wake. Mama anakubali binti yake aishi na bwana bila ndoa , azae watoto kila mtoto na baba yake, kwa nini usimshauri mwanao akafunga ndoa na kuishi maisha ya amani kama wewe unavyoishi na mumeo?"

Alisema Kanisa linamtambua mwanamke kama nguzo thabiti na kioo katika malezi ya familia kwani ndio walimu wakuu na kwamba endapo hawatakuwa makini katika malezi yao,wanaweza kuyumbisha, kuiweka imara , kuibomoa ama kuijenga.

Alisema wanawake licha ya kuwafundisha watoto wao kufanya na kuzungumza mambo mema katika jamii, pia wanalo jukumu la kuwahimiza wakue katika sala.

"Eti mwanamke anajiweka kando akidhani kazi ya kuelimisha watoto, ni kazi ya wanaume; wanafanya makosa kufikiri hivyo. Hii ni kazi ya jamii nzima; si baba wala mama peke yake. Wote wahakikishe watoto nao wanatimiza wajibu wao wa kuwatii wakubwa zao."alisema.

Paroko huyo na Shemasi Revocatus Mgukuyaweni, walisema katika milenia hii mpya, wanawake Wakristo wanapaswa kuona kuwa wanamfungua Kristo katika maisha ya jamii.

Aliongeza kuwa endapo jamii itafanikiwa kuwalea watoto katika maadili muafaka, Kanisa na serikali vitawapata watumishi bora wakiwamo masista, watawa, wabunge na mawaziri.

Imarisheni Jumuiya ndogondogo za Kikristo - Askofu

Na Fr. Raphael Kilumanga

MHASHAMU Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Method Kilaini amewataka wakristo waimarishe jumuiya ndogondogo za Kikristo (JNNK) ili kuimarisha imani yao.

Alitoa wito huo wakati wa halfa ya kumpongeza kuwa askofu iliyofanyika Msimbazi jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita. alisema kuwa JNNK zilikuwa shule za awali na hivyo kuwataka pia watu wajifunze kutoka jumuiya hizo.

Akihubiri wakati wa misa, Mhashamu Kilaini aliwaambia waaminwaliofurika katika Kanisa la Msimbazi kuwa katika JNNK watu wanajifunza namna ya kusali, kutataua matatizo na kujengana na kwa kufanya hivyo wakristo wanaimarika katika imani yao na kujenga familia bora. Aidha Kiongozi huyo wa Kanisa alisema pia kuwa ili kujenga familia bora kulikuwa na umuhimu wa kujenga pia tabia na moyo wa kujitoa kwa wengine kama alivyofanya Kristo mwenyewe ambaye alijitoa ili binadamu awe na uzima wa milele.

"Tunda la ufufuko ni kuishi pamoja mithili ya wakristo wa kwanza"alisema.

Askofu Kilaini na kuongeza kuwa mfano mzuri ni Mt. Fransisko wa Assizi ambaye katika maisha yake alizingatia zaidi moyo wa kujitoa kuliko kupokea tu na kuongeza pia JNNK zilikuwa shule za kujengana na kujitoa moja kwa mwingine.

Mhashamu Kilaini pia aliwataka wakazi wa Dar es Salaam wapafanye mahali hapo pawe pazuri pa kuishi bila kujali sehemu walikotoka na kuishi bila kujali sehemu walikotoka na kuwahimiza wajiunge na JNNK zilizopo.

Sherehe hizo ziliandaliwa na ndugu na marafiki wa Mhashamu Kilaini na kuhudhuriwa pia na Mhashamu Askofu Paul Ruzoka wa Kigoma na Mwenyekiti wa Utume ya Haki na Amani katika baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Wengine waliohudhuria ni wabunge mbalimbali wakiwemo Paul Rupia wa Ukonga na Bw. Sebastian Kinyondo Mbunge aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri Mnamo Machi 18 mwaka huu Method Kilaini aliyekuwa Katibu wa Baraza laMaaskofu alipewa daraja hilo