Makanisani Wiki hii

Mchungaji awataka maharusi kukatiana ugali badala ya keki

Na Elizabeth Steven

Mchungaji Heri Mwakabonga wa K.K.K.T, Usharika wa Tabata, jijini amewataka waamini wake ambao hawajafunga ndoa kuachana na dhana kuwa kufunga ndoa ni lazima iwe shughuli kubwa ya kifahari na yenye kugharimu kiasi kikubwa cha pesa.

"Wengi wanashindwa kufunga ndoa kwa sababu wanadhani kufunga ndoa ni lazima avae shera au suti suti, ya nini yote hayo?

"Njoo na huyo mnayetaka kufunga naye ndoa na mashahidi wenu, mtafunga ndoa na kupewa vyeti vyenu kama kawaida na kisha tunakunywa soda zetu hapahapa ofisini, basi.

"Sio lazima utumie maelfu ya pesa."

Alisema na kuongeza, " Iwapo unaona lazima mlishane kitu, sio lazima iwe keki ya maelfu na maelfu ya pesa, badala ya kula keki, katianeni ugali kisha mlishane mkiwa mmetulia nyumbani kwenu; hakuna ubaya wowote."

Katika ibada nyingine iliyofanyika katika usharika wa Tabata Siku ya Ijumaa Kuu, Mchungaji Mexon Mng’ong’o wa usharika huo aliwataka vijana kuwa mastari wa mbele kuupiga vita ugonjwa wa ukimwi kwa vitendo kuliko kuwa mstari wa mbele kuhubiri ukimwi kuwa unaua wakati wao wenyewe wanachangia kuuneza ikiwa ni pamoja na kushiriki uasherati na kuutolea tafsiri potofu.

"Vijana wengi wanahubiriwa na wengine kuhubiri juu ya AIDS lakini, ndio hao hao tena baadaye utasikia wanaseam eti sio haramu nzi kufia kwenye kidonda na kuna wakati hata wanapotosha kirefu cha AIDS wanasema eti Acha Iniue dogodogo Siachi. Hivi jama tunakwenda wapi?" alihoji kwa mshangao.

Kwa pamoja wachungaji Astorn Kibona wa Usharika wa Keko, jijini, Mchungaji Heri Mwakabonga waliwashauri Wakristo kuacha tabia ya kwenda kanisani siku za sikukuu peke na badala yake wadumishe utamaduni wa kusali na kushiriki mambo ya kanisa siku zote.

Wachungaji hao wa usharika wa Tabata na Astorn Kibona wa Usharika wa Keko walitoa ushauri huo kufuatia kufurika kwa watu katika sharika zao siku ya Pasaka hali iliyopelekea waamini kusogelea madhabahu kutokana na msongamano ulioyafanya makanisa yao yaonekane madogo tofauti na ilivyo siku nyingine ambapo idadi ya watu huwa si kubwa kama ilivyokuwa siku hiyo.

"... najua ingawa leo kanisa limejaa mpaka hapa mbele, wengine ni wale waliokuja kwa sababu ya sikukuu maana wanasali mara mbili kwa mwaka. Najua nikimaliza hapa mtakuwa mmeniaga na hatutaonana mpaka mwakani na wengine mpaka siku watakapofunga ndoa," alisema Mchungaji Mwakibonga wa Tabata.

Naye Mchungaji Astorn Kibona wa K.K.K.T usharika wa Keko siku hiyo alisema kanisani kwake kuwa, "Msiwe kama submarine yani zile meli za kivita ambazo hukaa majini kama hakuna vita na ikitokea vita zinaibuka na kupiga mabomu kisha zinazama kusubiri tena.

Sasa na ile tabia ya Wakristo kuibuka na kuonekana makanisani wakati wa Pasaka na Krismasi kama vile wanaibuka toka majini na sikukuu hizo zikiisha wanazama, sio nzuri."

Ombeeni Tanzania idumu katika amani - Paroko

Na Getruder Madembwe

"Amani tuliyonayo kuna watu ambao wanaihangaikia na kuteseka kuitafuta hawaipati hivyo sisi tusibweteke nayo bali tuitunze zaidi ili isije kutuponyoka,"

Maneno hayo yalisemwa na Padre Seventinus Banulirwa wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Gaspari lililopo Tegeta Jijini Dar-Es-Salaam katika ibada ya Ijumaa Kuu ambapo ibada hiyo ilifanyika katika kanisa hapo kitaifa.

Alisema amani waliyonayo Watanzania, wapo watu ambao wanaililia hivyo basi lakini kulingana na mazingira na hali waliyo nayo, hwaipati kwa kuwa ni zawadi ambayo Tanzania imejaliwa na Mungu hivyo kila mwananchi hana budi kutobweteka nayo bali kuilinda na kuiongeza zaidi.

Aidha alisema wakati Tanzania inaelekea Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge, na Rais Oktoba 29 mwaka huu ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, Watanzania hawana budi kumuinulia Yesu macho ili kumuomba awasaidie nchi idumu katika amani, upendo, utulivu na hakina kuepukana na hali zote zinazoweza kuvuruga amani ya nchi na kuzua michafuko ambayo hakuna mwenye haja nayo.

"Tunapojiandaa katika Uchaguzi Mkuu ujao kuwachagua viongozi, tusiharibu haki yetu ya uzaliwa wa kwanza na wala tusihadaike na vitu vya siku moja tu na wala tusikate tamaa na kuuza haki zetu," alisisitiza Padre Banulirwa.

Padre Banulirwa ambaye ni Paroko wa Parokia hiyo aliwaasa Watanzania kuilinda nchi hii na kusema kuwa hilo ni jukumu la Watanzania wote na wala si kazi ya mtu mmoja

Aliwataka wakristo kote nchini kutomwekea Mungu masharti kwa kusema kuwa mapenzi yetu yatimizwe, "Hata Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa pale msalabani alisema Baba mapenzi yako yatimizwe na wala si kama nitakavyo mimi. Iweje sisi tutake kumwekea Mungu masharti?" alihoji Padre Banulirwa.

KKKT wakana kikundi cha Kwaya kutengwa

Na Agatha Rupepo, DSJ

MCHUNGAJI Lewis Hiza wa (KKKT) Usharika wa Kijitonyama amekanusha habari zilizoenea kuhusu kikundi cha Upendo kuwa kimepigwa marufuku kuendelea na shughuli za uimbaji katika Kanisa hilo.

Mchungaji huyo alisema hivi karibuni ofisini kwake kuwa Upendo ni Kikundi kinachoundwa na baadhi ya waliokuwa waimbaji wa Kwaya ya Uinjilisti ya Usharika wa Kijitonyama na wengine wa nje ya usharika huo, hivyo hakiko chini ya usharika kikamilifu.

Aliongeza kusema kuwa kikundi hicho kinajitegemea katika shughuli zake nyingi ikiwemo kurekodi nyimbo na kuzisambaza au kuziuza.

"Baadhi ya washarika wanaounda kikundi cha Upendo wanatoka katika Usharika wa Kinondoni, Kariakoo na Mabibo, ndio maana nasema hakiko chini ya Usharika," alisema.

Mchungaji Hoza alisema Wakristo wote walio ndani ya kikundi cha Upendo wanapata huduma zote za Kiroho kutoka katika Usharika huo.

Akasema kujitenga kwa vijana hao kutoka katika Kwaya ya Uinjilisti haikusababishwa na Sh 500,000 walizokuwa wameomba kutoka Kanisani kwa ajili ya kwenda kurekodi Mkoani Arusha.

Akifafanua amesema Kanisa liliwaambia wanakwaya hao watafute mtu ambaye anaweza kuwapa hizo pesa na Kanisa litamrudishia mtu huyo pesa zake, kwa sababu kipindi ambacho wanakwaya walihitaji pesa hizo Kanisa lilikuwa halina pesa na mpaka sasa mtu huyo ameisharudishiwa pesa zake.

Naye Bwana Albert Mafuenga ambaye ni mmoja wa kikundi cha Upendo amesema, Usharika huo hautambui kuwa kuna washirika wanaojiiita Upendo.

Amesema huduma zote za kiroho wanazipata kama washirika wengine.

Kanisa la AIC lataka tofauti za kimadhehebu zisikwamishe Injili

Na Getruder Madembwe

KANISA la African Inland Church (AIC), limesema Umoja wa Makanisa ya Kikristo hautakuwa na maana endapo wanachama wake hawataondoa tofauti za kimadhehebu kisha wakaimarisha mahusiano baina yao kwani tayari walishaunganishwa kwa kifo cha Yesu msalabani.

Changamoto hiyo ilitolewa na Askofu Charles Salalah, wa AIC Dayosisi ya Pwani alipokuwa akihubiri katika ibada maalum ya Umoja wa Makanisa iliyofanyika katika Kanisa la Assemblies of God lililopo Kinondoni jijini Dar Es Salaam, Jumatatu iliyopita.

Alisema Umoja huo hautakuwa na maana iwapo madhehebu mengine hayatakuwa tayari kuungana na kushirikiana kwa pamoja kuwa familia moja katika Kristo bila ubaguzi wa jinsia au dhehebu kwani tayari washapatanishwa na damu ya Yesu ambayo ilimwagika msalabani.

Askofu Salalah alisema jamii ya Kikristo itakuwa inajiingiza yenyewe katika matatizo pindi itakapoanza kujitenga na Kimadhehebu kwa madai na visingizio na kashfa kuwa dhehebu fulani linaabudu kitu fulani au hata wengine kudiriki kusema dhehebu fulani hawana Roho Mtakatifu.

Alisema Mungu huwapa rehema watu wote bila ya upendeleo kwani hata katika Maandiko Matakatifu (Mdo.10:34-35), imesemwa kuwa, "Petro akafumbua kinywa chake akasema, hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye."

Katika ibada hiyo iliongozwa na Padre Samwel Sepeku wa Kanisa la Kiangalikana, maombezi ya kuliombea Taifa walifanywa na Askofu Zakayo Swai, wa Kanisa la Assemblies of God.

Lengo la ibada hiyo ambayo hufanyika kila Jumatatu ya Pasaka ni kuyashirikisha madhehebu yote ya Kikristo na kumshukuru Mungu kwa ajili ya Ufufuko wa Yesu na jumla ya Shilingi 123,085 zilipatikana katika ibada hiyo kwa njia ya sadaka.

Baadhi ya madhehebu yaliyoshiriki ibada hiyo yalikuwa Waanglikana,Walutheri, Wakatoliki, Wapentekoste, African Inland Church, Tanzania Assemblies of God na Wabaptisti.

Makanisa ya Sabato Mkoa wa Dar kuwa na siku moja ya wageni

lMahubiri wao toka Jamaica awasili jijini

Na Masha Otieno Nguru

FUNGAMANO la Kanisa la Wasabato SDA Mkoa wa Dar Es Salaam limeandaa kwa mpigo siku moja ya kukaribisha wageni katika kila Kanisa lao lililoko jijini.

Akiongea na waumini wa Kanisa hilo eneo la Kurasini jijini mmoja wa waandalizi wa programu hiyo Bw. John Marwa amesema mpango huo umewekwa ukiwa ni maandalizi ya awali ya mkutano mkubwa wa Injili wa ‘Explo 2000’ utakaoendeshwa na mhubiri wa Kimataifa wa Kanisa hilo Mwinjilisti Fritz Henry kutoka Kingston Jamaika.

Bw. Marwa amesema kuwa siku hiyo ya kukarimu wageni katika Makanisa yote ya Wasabato jijini Dar es Salaam itafanyika Aprili 29 ambapo mpaka sasa kadi za mialiko tayari zimeisha kusambazwa katika makanisa mbalimbali ya Kisabato jijini.

Parish za Kanisa la Sabato zitakazoshiriki mpango huo zimetajwa kuwa ni pamoja na Ilala, Ukonga, Kurasini, Temeke, Mwenge, Magomeni, Ubungo na Kinondoni.

Wageni mbalimbali watakaohudhuria siku hiyo ya ‘Church Big Day’ wanatarajiwa kupata zawadi mbalimbali ikiwemo chakula cha mchana kitakachotolewa bure kwa kila atakayehudhuria.

Mapema mwezi huu Mwinjilisti Raia wa Jamaica Firtz Henry aliyekuwa akihubiri huko Kumasi Ghana mwaka jana aliwasili jijini Dar es Salaam na kukaa Tanzania kwa siku kadhaa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wake mkubwa wa Explo 2000 utakaofanyika kwenye viwanja vya Jangwani jijini kuanzia mwezi Julai mwaka huu.