Wajane watakiwa kujiheshimu

Na Benjamini Mwakabinga

WAJANE wametakiwa kuishi maisha ya kujiheshimu kwa muda wote hadi watakapojaliwa kuolewa kuliko kuishi maisha yaliyotawaliwa na tamaa za kimwili.

Hayo yalisemwa na Mwangalizi wa Makanisa ya Tanzania Assembeles of God (T.A.G), sehemu ya Kinondoni, Mchungaji Nathaniel Sasali, alipokuwa akihubiri katika semina maalum ya wajane iliyofanyika katika Kanisa la TAG Ubungo jijini Jumamosi illiyopita.

"Ni mjane mwenye heri yule atakayeamua kuolewa kuliko kuishi maisha ya kuweka tamaa ndani ya ujane", alisema Mchungaji Sasali kwa kunukuu Kitabu cha 1Timotheo 5:9.

Alisisitiza kuwa ni vyema kwa mjane kuwa na maombi kwani maombi ya mjane hayana vipingamizi mbele za Mungu.

Aliwataka kuishi maisha ya kumtumikia Mungu pasipo kuangalia hali zao za maisha ya ujane na kwamba wasiyawazie maisha ya awali ya ndoa zao.

Mchungaji Sasali, alitoa mfano wa mjane wa Sarepta ambapo alisema kuwa mama huyo alimhudumia Nabii Eliya na alifanya hivyo pasipo kuangalia udogo wa mali zake ndipo Mungu akamfungulia milango ya baraka.

Alizitaja baadhi ya sifa za mjane kuwa ni kusaidia wenye shida katika jamii awe amekuwa mke wa mume mmoja na pia mjane ni lazima ashuhudiwe kuwa na matendo mema.

Wajane waliohudhuria semina hiyo walikabidhiwa mavazi na vitu mbalimbali kutoka kwa Umoja wa Wanawake Wa Kanisa hilo (W.W.K), walioandaa semina hiyo kwa lengo la kuwafariji na kuwatia moyo wafiwa hao.

Mchungaji Sasali, aliushukuru uongozi na wanachama wa (W.W.K) kwa kuandaa semina hiyo na kuwataka waendelee kufanya huduma kama hiyo mara nyingine.

Wiki chache zilizopita wamama hao walifanya huduma ya kuwatembelea wagonjwa katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar-Es-Salaam, pia walitembelea makazi ya watoto yatima na kukabidhi vitu mbalimbali kwa wahusika.

Msiogope matatizo, Padre awaambia waamini

Na. Elizabeth Steven

KANISA Katoliki parokia ya Makuburi jijini Dar-Es-Salaam, limewataka waamini kuwa jasiri wasioogopa wala kukata tamaa wapatapo matatizo badala yake, wawe wavumilivu, wenye upendo na utii, na wadumu katika maombi.

Padre Erevias Mwakulila, wa kanisa hilo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, alitoa ushauri huo wakati akizungumza katika ibada ya Jumapili iliyopita kanisani hapo.

Alisema Mungu anawata wanadamu wasikate tamaa wanapopatwa na matatizo, bali wawe wavumilivu, wenye upendo pamoja na utii.

Alisema mtu yeyote anaye kata tamaa, huwa hana mwisho mwema na badala yake huishia katika kufanya mambo ya ajabu ajabu tu kwa kuwa sasa anakuwa naona hakuna nachofanikiwa na wala haoni atafanikiwa wapi. Na hiyo si tu kwamba ni machukizo kwa jamii ya watu anaoishi nao, bali pia machukizo kwa Mwenyezi Mungu.

"Utakuta aliyekata tamaa sasa anajaribu kufanya mambo ambayo unaona labda yatamfaa au kunafanya aonekane kwa watu kwamba nae yumo, kumbe anachofanya ni vurugu tupu. Ukishajua upendo wa Mungu, basi zishike Amri za Mungu, ufuate yale ambayo Mungu anakuamuru".

Aidha amewataka Wakristo wote kuepukana na dhana potofu miongoni mwa jamii aliyoisema kuwa sio makusudio ya dini yoyote, bali ni vurugu tupu miongoni mwa jamii kwamba mtu anapoiba, akatwe mikono vidoleniau achomwe moto na kuuawa.

Alisema ni wajibu wa mwalimu, kumfundisha mwanafunzi wake hadi aelewe vema yampasayo kufanya na vivyo hiyo, ni wajibu kwa baba na mama kulinda familia kuanzia jumuiya ndogo ndogo hadi ngazi ya parokia na kanisa lote kwa jumla.

Alisema kinyume na wajibu huo kwa viongozi hao wa kiroho na kifamilia, jamii itaishia katika vurugu zitakazovuruga shughuli za kumtumikia Mungu.

"Matendo tunayoyafanya katika familia ni yale yanayotuletea umoja, amani na upendo, tuwe pamoja naye, tufanye yale aliyoyataka maana hayuko mbali nasi, bali yu pamoja nasi."

Ondoeni tofauti za kidini msiwe waroho wa madaraka

Na Mwandishi Wetu

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limetoa wito kwa Wakristo na jamii nzima kuishi kwa amani, upendo na umoja bila kujali tofauti za kidini, kisiasa na kijinsia wala kuwa waroho wa madaraka katika makanisa yao.

MCHUNGAJI Heri Mwakabonga wa KKKT usharika wa Tabata, uliopo jijini Dar es Salaam alitoa wito huo katika ibada iliyofanyika kanisani hapo na kuwataka Wakristo kutokuwa waroho wa madaraka katika makanisa yao kwani uongozi, dini au dhehebu, hazimfikishi mtu mbinguni bali matendo yake mema.

"Sisi kama Wakristo, tunapaswa kuwa na amani, upendo na umoja kati yetu. Wengi wetu tumemuacha Yesu benchi na sasa makanisani kuna vyeo na ulaji. Hizo tofauti zetu tuziweke kando na tuungane pamoja.

Kuna akina Mwakabonge wengi kuna waislamu, Waanglikana walutheri, lakini tunayemwomba ni Mungu mmoja na mwakabonge jina lake linabaki lilelile waamini hatuna shida, shida ipo kwenye vyeo nani awe askofu na sasa Uaskofu upo kama uyoga.

Mchungaji Mwakabonga amevilaumu vyobo vya habari hasa Televisheni kwa kishindwa kuvipa kipaumbele vipindi vya dini na matokeo yake asilimia kubwa utakuta mambo yasiyo na maana ndiyo yanayopewa nafasi kubwa ambapo dini ni roho nzima ya vipindi vyote.

"Sasa hivi televisheni tunazo wengi hata kama huna basi mtoto ataenda kwa jirani akaone mambo ya kisasa Televisheni nzuri lakini mambo yaliyomo yanatia aibu mambo ya dini yanapewa robo nzima ya nafasi katika televisheni zote hasa hapa Dar-Es-Salaam, zinaonesha nini?" alihoji.

Mchungaji alisema kuwa kila mtu anapaswa kuelewa kuwa binadamu ni watu wa Mungu na hapendi kuwagawa anayegawa maana anayewagawa wanadamu, ni Shetani pekee.

Ndoa 60 zabarikiwa Mwanza

Na Steve Mchonzi, Mwanza

ZAIDI ya wanandoa 60 wamebarikiwa upya katika kanisa Katoliki la Moyo Mtakatifu wa Yesu Ilemela Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.

Wanandoa hao walibarikiwa katika ibada iliyofanyika hivi karibuni katika Jumapili ya Pentekoste ikiwa ni maadhimisho ya miaka 2000 tangu kuanzishwa kwa Kanisa duniani.

Katika ibada hiyo iliyoendeshwa na Padre Richard Makungu, wanandoa hao walivishana upya pete zao za ndoa na kutoa kiapo cha uaminifu mbele ya waamini waliofurika kanisani hapo.

Wakitoa kiapo cha pamoja wanandoa hao waliahidi kuendelea kuzilinda, kuziheshimu ndoa zao kuwa na upendo baina yao, familia na kwa jamii yote.

Awali kabla ya kuanza kwa ibada, wanandoa waliingia kanisani kwa maandamano wakiimba huku wakiwa wameshikana mikono mume na mke na kisha kwenda kukaa katika viti maalum vilivyoandaliwa ndani ya kanisa.

Baada ya wanandoa hao kubarikiwa, kuliendeshwa ibada nyingine maalum ya kuwabariki na kuwaidhinisha, mtawa mmoja na walei wawili kutoa Sakramenti ya Ekaristi kwa waamini.

Mtawa aliyesimikwa ni Sista Rosemary Milazzo, wa shirika la Maryknoll mwenye asili ya Kitaliani na walei ni makatekista Emanuel Dona na Boneventura Msuka, wote wa parokia ya Ilemela.

Waanglikana Temeke kutupa ndoana kwa vijana mitaani

Na Leocardia Moswery,

UMOJA wa Vijana Wakristo wa Kanisa la Kianglikana, Dinari ya Temeke, wanatarajia kufanya tamasha la kanda litakalofanyika Julai, mwaka huu katika Kanisa la Mtakatifu Albano, Upanga, jijini.

Akizungumza na KIONGOZI, wiki hii, kiongozi mmoja wa TAYO, Bw. John Milinga, alisema madhumuni ya tamasha hilo, ni kuwavuta vijana wengi walioko mitaani kwa makusudi ya kukuza vipaji vyao na kuvitumia kumtangaza Kristo, aliye Mkombozi wa wote.

Bw. Milinga, alisema tamasha hilo pia litawashirikisha vijana kutoka mikoa ya jirani na Dar es Salaam, yaani Pwani, Zanzibar, Morogoro na Arusha.

Alisema pamoja na zoezi la kuwatia moyo na kuwasaidia vijana wenye vipaji vya uimbaji, kutakuwa na semina ya malezi ya vijana na hatari ya ugonjwa wa Ukimwi kwao, hasa kwa kuzingatia kuwa watu wanaoathirika zaidi na ugonjwa huo nchini ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 45.

Milinga, aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi kwa vile ni bora kujiweka karibu na kanisa badala ya kujitumbukiza kwenye hatari za ulimwengu huu muovu.

KKKT wasema ubatizo wa maji mengi si hoja

Kubatizwa kwa maji mengi au hata mwili mzima ni kazi bure na hauna maana kama hakuna mabadiliko ya kiroho katika maisha yake. Amesema Mchungaji Moses Maarifa, kama anavyoripoti Getrude Madembwe.

Mchungaji Maarifa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Dayosisi ya Pwani na Mashariki, usharika wa Kawe aliyasema hayo katika ibada ya Jumapili iliyopita, iliyofanyika usharikani hapo jijini Dar-Es-Salaam.

Alisema mtu anapobatizwa hana budi kubadilika kabisa kiroho na namna yake ya kuishi kwa kuwa kubatizwa ni kuzaliwa upya badala ya kung’ang’ania tu, kusema anataka kubatizwa kwa maji mengi wakati hata yenyewe hayabadilishi maisha yake na kuwa yenye kumpendeza Mungu.

"Pindi unapobatizwa unatakiwa uwe na mabadiliko katika maisha yako na hata watu wengine wakikuona waseme kuwa pale kuna mabadiliko, siyo kung’ng’ania tu majimengi Kinachotakiwa ni mabadiliko ya kiroho sio wingi wa maji. " alisema.

Mchungaji Maarifa alisema anashangazwa na kusikitishwa na baadhi ya watu wenye nyadhifa katika maeneo yao ya kazi lakini, eti ndio huonekana kuona aibu kumrudia Mungu wakidhani na kuhofia kuchekwa na watu walio chini yao ambao wengi wao ni waliokata tamaa na hawana mpango wa kuishi maisha ya kumtukuza Mungu.

Alisema kuwa, hata Nicodemu, mtu mkubwa ambaye alikuwa kiongozi wa Mafarisayo, alikwenda kwa Yesu na akamuuliza kuwa "Rabi nifanye nini ili niweze kuurithi uzima wa milele? Ndipo Yesu akamwambia kuwa ni lazima azaliwe mara ya pili yaani, abatizwe.

"Nicodemu alikubali kubatizwa na akawa amebadilika. Sasa kwa nini wewe usije ukazaliwa mara ya pili sababu eti wewe ni mtu mkubwa? Hata Nicodemu alikuwa Kiongozi mkubwa lakini, alikwenda kwa Yesu na akabadilika" alisisitiza Mchungaji Maarifa.

Alisema kuwa kipimo cha Mungu hakiwezi kufafanishwa na vipimo vya kibinadamu (darubini) ambavyo huweza kujua kuwa mtu huyu ni mgonjwa wa Ukimwi au la, bali yeye (Mungu) hupima kwa kutumia maarifa yake ambayo kamwe binadamu hawezi kufahamu.