Kanisa latapeliwa pesa za sadaka

Na Leocardia Moswery

KANISA la Kianglikana la Watakatifu Wote Dinari ya Temeke, limetapeliwa pesa za sadaka na kupewa noti za bandia

Padre Nathaniel J. Kipalamoto wa kanisa hilo, ameliambia Kiongozi ofisini kwake katika Wilaya ya Temeke, mwishoni mwa juma kuwa, kuwa baada ya ibada ya Jumapili moja ya hivi karibuni, kuna watu waliofika kanisani na kuomba chenji ambapo walikuwa na noti tatu za shilingi elfu moja moja.

"Waliwaomba wakusanya sadaka wawape chenji ya shilingi elfu moja moja. Walikuwa na noti tatu na wao walisema shida yao ilikuwa ni sarafu pekee. Kumbe wao zile noti tatu za shilingi elfu moja moja, zilikuwa bandia na wao wakachukua sarafu zote tena wamefungiwa kabisa kwenye mfuko," alisema Padre Kipalamoto.

Alisema baadaye ndipo kanisa lilizitilia mashaka noti hizo za bandia na hata walipokwenda kuulizia benki, waliambiwa kuwa zilikuwa ni pesa za bandia.

Akitoa tangazo la tukio hilo kanisani, Padre Kipalamoto aliwatahadharisha waamini kujihadhari na watu wenye mitindo hiyo ya kutapeli makanisani wakiwa na imani kuwa makanisani kuna pesa nyingi ambazo zinaweza kuchukuliwa ovyo ovyo kwa njia zozote zikiwemo za utapeli wa namna hiyo.

Aliwasisitiza wahudumu wa kanisa kuwa makini kwa mtu yeyote wanapokusanya sadaka na kuepuka utoaji wa chenji ambayo ni njia pia inayotumika kutapeli sadaka za kanisa.

Alisema anayetaka chenji, aende akatafute huko benki ili kuepuka hila za wenye nia mbaya na mali za kanisa.

Aliwakemea na kuwataka wanajamii wenye tabia hiyo kuachana nayo mara moja kwa kuwa kuiba mahali patakatifu ni kujilaani mwenyewe.

"Hivi kweli unaweza kuleta noti bandia kanisani, ukijidai unatafuta chenji; hata humwogopi Mungu?" alihoji.

Aliwataka wenye noti hizo kufikishwa katika vituo vya usalama ili waonye kwa taratibu za nchi na kanisa.

Wanahabari watakiwa kukemea zaidi mauaji

Na Joseph Nyamhanga, Musoma.

Waandishi wa habari wametakiwa kutumia nguvu zaidi kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya wazee kwa kisingizio cha uchawi na tohara hasa wanawake.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na waumini wa Parokia ya Kiagata katika Jimbo Katoliki la Musoma, kwa Mkuu wa Udekano wa Bunda - Serengeti, Padre Wojciech Koscielniak, Jimboni humo katika homilia ya Misa ya Jubilei ya Waandishi wa Habari, iliyofanyika kijimbo katika parokia ya Kiagata,

Mbele ya Padre Wojciech, ambaye alimwakilisha Askofu Justin Samba, waamini hao walilamikia tamaduni zilizojengeka katika ulimwengu wa vyombo vya habari ambavyo mara nyingi hutenda kinyume cha matarajio ya Yesu au kinyume cha wosia wake kwa kuandika na kutangaza habari zisizo kuwa na msisitizo wa mafundisho ya kiroho bali zenye kwenda na mambo ya kidunia tu.

Walisema mauaji kwa vikongwe kutokana na tuhuma za uchawi yamekuwa yakiongezeka siku hata siku na kwamba hayo, hayana budi kuemeawa na kila mwanadamu mpenda haki na mwenye kuishi kwa kuzingatia mapenzi ya Mungu.

Aidha, walilaani pia tabia ya baadhi ya makabila kuwafanyia tohara watoto wa kike kwa kuwa kitendo hicho ni cha unyanyasaji, chenye kushusha utu wa mtu na kuhatarisha afya na maisha ya waathirika.

Katika ujumbe wake katika Jubilei hiyo ,Padre Wojciech alisema, habari ya maana ambayo waandishi wa habari wanapaswa kuwashirikisha watu ni habari za Mungu zinazowapa watu uzima amani, faraja, nguvu, tumaini, utakatifu na kuwasaidia a zenye kuwafikisha katika uzima wa Kimungu.

Mkuu huyo wa Udekano wa Bunda-Serengeti alisema hati tatu muhimu na mafundisho ya Mama Kanisa ambazo ni Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Barua ya Kitume ya Baba Mtakatifu Yohane Paul wa Pili ya mwaka 1988 na Barua ya Kitume ya mwaka 1995 juu ya Kanisa barani Afrika zinaeleza vema mafundisho ya Kanisa namna waandishi wa habari wanavyoweza kutekeleza vema wito wao kwa kadri ya mpango wa Mungu.

Katika sherehe hizo zilizofanyika Juni 4, mwaka huu, wandishi walitakiwa kusaidia kuwapa watu ukweli wa uzima kama utume na fahari ya kazi yao.

Walokole wakanywa kuwadharau wasiookoka

Na Josephs Sabinus

MCHUNGAJI Nathanael Mitachi, wa INTERNATIONAL EVANGELISM CHURCH, usharika wa Mivinjeni, mkoa wa Dar-Es-Salaam, amewaonya baadhi ya wanaookoka kuacha kuwadharau ambao hawajaokoka na kuwaona shetani badala yake, wawaone kama ndugu na kuwasaidia ili nao wajue kuutafuta Ufalme wa Mbinguni.

Mchungaji Nathanael, aliyasema hayo wakati akizungumza katika ibada ya Jumapili, iliyofanyika katika kanisa la Mivinjeni katika wilaya ya Temeke jijini.

Alisema, tabia ya baadhi ya wanaookoka kujiona wa maan na kuwadharau watu ambao alisema hawajamtolea Mungu maisha yao, imekuwa kikwazo kwa watu wengi wasio okoka kukata tamaa na kuogopa kujihusisha katika shughuli za kumtolea Mungu maisha.

"Msiwadharau wasiookoka bali muwaombee ili nao wazijue Habari Njema za Wokovu kwa kuwa Siku ya Mwisho, wa kwanza atakuwa wa mwisho, na wa mwisho atakuwa wa kwanza," alisema na kusisitiza,

"Watu wa Mungu wengi, eneo hilo la kuwa kikwazo na kuwadharau wengine, ni sugu na linakomaa. Msijenge ubinafsi baina yenu na kujiona mnafaa zaidi kwa Mungu kuliko wengine. Kwa Mungu watu wote ni sawa na yeye pekee ndiye anayejua nani, anastahili nini."Aliwahimiza wana jamii wote kuwa wepesi wa kukiri makosa yao na kukusudia kuyaacha kabisa ili wazidi kuyafanya yenye kumpendeza Mungu na akaulaani uovu unaotendeka ndani ya jamii ikiwa ni pamoja na kwa baadhi ya watumishi wa Mungu kujihusisha na vitendo vya usengenyaji, wizi, ubadhilifu, majivuno, tamaa, uchawi, ubakaji na matumizi ya madawa ya kulevya.

"Kubalini makosa yenu kwa kuwa anayekiri na kuungama, atafanikiwa lakini, anayeogopa kuungama na badala yake kubaki ameng’ang’ania,...Kwa sababu, hata ukitaka kuwa kiongozi bora katika nchi au familia, ishi katika Biblia kwa kuwa mambo yote uvumilivu, upendo , uaminifu na mambo yote mazuri, hupatikana ndani ya Biblia."Alisema wanadamu hawana budi kuishi maisha mema ili tu, si kwamba wakifa waliliwe na watu wengi, bali pia wapate thawabu mbele za Mungu."Sio unaishi maisha mabaya na watu hata inafikia ukifa, watu wanaamua kusherekea kufa kwako, au wanashangilia eti umehama eneo lile. Lazima uwe mwenye kuishi kwa kadri ya mapenzi ya Mungu.

Mchungaji huyo wa IEC, amewataka Wakristo kuwa imara katika imani zao na kuepuka vishawishi vinavyoleta kulegalega kiimani.

"Sio ulale njaa, utoke nje ya ndoa yako, au ukaibe mahindi kwenye shamba la jirani yako,"alitahadharisha.

TAG wala ng’ombe, bado mkia

Na Dalphina Rubyema

HATIMAYE Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Ushirika wa Tabata Liwiti, limepata kiwanja cha kununua kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mbali mbali na upanuzi wa kanisa hilo na sasa imebaki kazi ya kutafuta pesa za kukilipia.

Akitoa matangazo katika ibada iliyofanyika Jumapili iliyopita, Mchungaji wa kanisa hilo Lawrence Kametta, alisema kiwanja hicho ambacho kimetolewa na mmoja wa waamini wa kanisa hilo, kinahitaji kununuliwa kwa Sh. Milioni 3.2 ambapo kila mmoja ameombwa kutoa mchango wake wa hali na mali.

Alisema kwa kuanzia, wazee wa kanisa hilo wameahidi kutoa jumla ya shilingi milioni 1.1 na ng’ombe wa maziwa mwenye thamani ya shilingi 100,000.

Mchungaji Kametta amewataka waamini wa kanisa hilo kuiga mfano wa wazee wao wa kanisa kwa kutoa kile walichonacho kwa moyo wa upendo.

"Jamani Mungu anazidi kutushushia neema na utukufu wake maana sasa tatizo letu sugu la ukosefu wa kiwanja kwa upanuzi wa kanisa letu sasa limepata ufumbuzi maana mwenzetu mmoja, amejitolea kutuuzia kiwanja chake tena kwa bei nafuu, kiwanja chenyewe hakipo mbali ni hicho hapo, "alisema Mchungaji Kammeta huku akielekeza mkono kuonesha waamini wake kilipo kiwanja hicho karibu kabisa na kanisa hilo.

Alisema kuwa kiwanja kikisha kuwa mikononi mwa kanisa, shughuli itakayofuatia ni ujenzi wa ofisi mbalimbali yakiwemo madarasa ya watoto wa chekechea na upanuzi wa kanisa hilo.

Wakati huo huo,Mchungaji Kametta amewataka waamini wa kanisa hilo kuheshimu na kuhudhuria ibada za zoni (vituo) ambapo alisema kuwa kushindwa kufanya hivyo ni sawa na kudharau kanisa zima kwa ujumla.

Alisema kufuatia utaratabu wa sasa, kanisa hilo litakuwa na zoni kumi alizozitaja kuwa ni Kanisani, Bima, Kimanga NHC, Kilimanjaro, Magengeni, Machimbo ,Mazda, Dewji, Sigara na Msimbazi.

Alisema kila zoni itakuwa na wasimamizi wawili ambapo muunganiko wa zoni mbili utakuwa chini ya Mzee wa kanisa mmoja na wahusika wote walitajwa kanisani hapo ambapo watabarikiwa Jumapili hii.

Vijana watakiwa wasivamie ndoa kwa pupa

Na Elizabeth Steven

INGAWA sheria ya kanisa haijasema wazi kipindi kinachofaa cha uchumba ni muda gani, ushauri umetolewa kuwa wachumba watumie muda mrefu ili kuweza kufahamiana vema wao kwa wao na koo zao.

"Ni hatari kijana kuchumbia au kuchumbiwa na mtu ambaye hawafahamiani kwa undani tabia zao, undani wao, ukoo, mila na desturi," alisema Padri Henry Mchamungu, katika Parokia Kristo Mfalme, Tabata, jijini wakati wa semina ya ndoa kwa vijana.

"Zipo familia ambazo ni za majambazi, vichaa na kuna makabila ambayo hayakai pamoja."

Padri Mchamungu, alisema wengi wanadhani uchumba ni kitendo rahisi cha kuvalishana pete ya kufungana (engagement), na baadhi hujaribu hata tendo la ndoa kwa kujifurahisha tu, au eti waone kwamba wanaweza kuzaa au la!

Alisema dhana hiyo ni potofu kwani ndoa haijaribiwi hata siku moja. "Uchumba si ndoa, ni matayarisho ya ndoa ambayo kimsingi yanahitaji muda mrefu," alisema.

Alisema jamii haina budi kuvifahamu vipingamizi vya ndoa ambavyo alivitaja baadhi kuwa ni pamoja na tofauti za kimaumbile, sheria za kanisa, baadhi ya mahusiano ya ukoo na tofauti ya kubwa kubwa ya umri.

Alikemea tabia ya kurithi mume au mke na kusema vitendo hivyo, vinakiuka haki za binadamu na kanisa halizitambui ndoa za namna hiyo.

Wakati huo huo; Ameitaka jamii kuepukana na njia zote za kisasa zinazotumika kwa uzazi wa mpango kwa kuwa zinahatarisha afya za watumiaji na badala yake, akashauri kutumia njia za asili.

Makanisa yaonywa juu ya majigambo

Na Getrude Madembwe

MAKANISA yote nchini yametakiwa kutojisifia bali kutoa maongozi mazuri ambayo yanaweza kuwafikisha watu mbinguni.

Wito huo umetolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Ki-Anglikana Dayosisi ya Ruaha, Iringa, Donald Mtetemela, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 2000 ya kuzaliwa Kristo. Maadhimisho hayo yalifanyika katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa juma.

Alisema umefika wakati kwa kanisa kujua kuwa kujisifia hakufai, kwani hata Bwana wetu Yesu Kristo alikuja kwa wote na wala sio kwa ajili ya dhehebu au kanisa fulani.

"Kumezuka tabia ya madhehebu kujisifia eti kuwa wao ndio wanaoweza kukufikisha mbinguni au wao ndio wana Roho Mtakatifu wakati Bwana wetu Yesu Kristo, alifika duniani na kufa kwa ajili ya watu wote, hivyo hakuna maana ya kujisifia," alisisitiza Askofu Mtetemela,na kuongeza kuwa:

" Kwa kawaida kanisa halileti ujumbe kwa kujisifia bali sifa pekee hutoka kwa Mungu Baba aliye mbinguni.

Askofu Mtetemela, alisema kuwa sasa hivi kumekuwa na kutoelewana kwingi kwa sababu kila mtu anataka kuwa Askofu au kiongozi wa kanisa na mengi ya makanisa hayo hayana matumaini na akasema kuwa tumaini ni Yesu tu wala hakuna mwingine kama yeye."Makanisa mengi sasa hivi yana mvurugiko. Alisema hakuna budi kumrudia Yesu, kwani yeye ndiye tumaini letu".

Katika maadhimisho hayo ya Jubilei ambayo yalifanywa na Umoja wa Makanisa yaliyohudhuriwa na Walutheri, Waangalikana, Tanzania Assembeles of God, Udugu Presybetanian na Jeshi la Wokovu.

Ishini utakatifu, msiogope mateso-Wito

Na Benjamin Mwakibinga DSJ

WAKRISTO wametakiwa kuishi maisha ya utakatifu bila uoga wa mateso kwa kuwa hata Yesu Kristo alisema duniani mna dhiki, jipeni moyo maana mimi nimeushinda ulimwengu.

Wito huo ulitolewa na Mchungaji Jima Mpanda, wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), la Tandale jijini katika mahubiri yake ya Jumapili jioni kanisani hapo."Usinung’unike wala kuona haya unapopatwa na mateso kwa ajili ya Bwana Yesu, kwa sababu mateso kwa mtakatizo, ni lazima," alisema.

Mchungaji Mpanda, alisema Wakristo hawana budi kutokuwa kama Petro ambaye baada ya kuona Yesu amekamatwa ili kwenda kuteswa, alimkana akisema kuwa hamjui.

Akinukuu kifungu cha Biblia toka ZABURI 22:24, alisistiza kuwa Mungu hudharau teso la mteswa na kuongeza kuwa hata Rutu na Nuhu, ni baadhi ya watakatifu waliopata mateso kwa kuona maovu katika jamii zao na kuwa hata Ayubu na Mfalme Daudi, waliteseka kwa kutaka kulinda utakatifu wao.

Katika ibada hiyo iliyofurika watu isivyo kawaida kwa ibada za jioni za kanisa hilo, kwa niaba ya wazee wa kanisa, Bw. Emmanuel Sote, waliisifia kwaya ya SHAROME ambayo imekuwa ikitunga nyimbo zenye kusisimua na kuigusa jamii na kwamba huenda taarifa za kuwepo kwake jioni hiyo, pia zilisababisha watu kuongezeka.