Makanisani Wiki hii

Angalieni msitekwe na mihadhara- Tahadhari

Na Elizabeth Steven

KANISA la Pentekoste Tanzania (KLPT), limewatahadharisha Wakristo kuwa makini dhidi yawanaoendesha mihadhara kwa kukashifu dini nyingine kwa dharau huku wakilenga kuwarubuni wahamie katika madhehebu yao na badala yake wawe na msimamo thabiti katika imani zao.

Wito huo uliotolewa hivi karibuni na Mchungaji Moses Mjema wa KLPT, Tabata-Kimanga jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza katika ibada iliyofanyika Jumapili kanisani hapo.

Alisema, "watu wengi wanapata vishawishi kutoka kwa viongozi mbalimbali wa dini na hao viongozi ndio wanaofanyakazi za kukashifu dini nyingine wakiwa na lengo la kuwateka watu na wengine bila kujua, wanajikuta wamehama katika madhehebu yao"

Alisema Wakristo wanapaswa kulifahamu Neno na kulielewa vizuri na kuwataka wasiwe kama maimuna ambao hukubali kila wanaloambiwa hata liwe baya kwao.

Amesema watu hao ni sawa na shetani ambaye anatoa neno upande mmoja na upande mwingine hufunika.

"Hawa watu wanaotoa neno upande mmoja na kulipeleka upande mwingine kufunika; ni sawa na shetani, akitaka kukupa, anakupa neno ambalo anaona kuwa litamfaa katika ubaya wake na lazima utakubaliana naye."

Mchungaji Mjema amewataka viongozi wa vikundi vyote vya dini wenye tabia hiyo waiache kwa kuwa hiyo si njia ya kulitangaza Neno la Mungu bali ni kuchochea vurugu zinazoweza kuhataraisha amani ya nchi.

Waandishi wa habari waambiwa, salini kama mnakufa leo

Na Christopher Kidanka, Morogoro

WAANDISHI wa habari wa vyombo mbalimbali mjini hapa wameshauriwa kusali kwa imani mithili ya watu wanaotarajia kufa leo ili wapate rehema zaidi ya kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa RADIO UKWELI FM Stereo ya Jimbo Katoliki la Morogoro, Sista Gaspara Shirima, wakati wa hija na maadhimisho ya Jubilei kwa wanahabari iliyofanyika jimboni Morogoro.

Alisema kwa kutumia karama na kalamu zao, wandishi wa habari wanaweza kujipatia rehema zaidi mbele za Mungu endapo watafanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya kazi na mapenzi ya Mungu.

"Ndugu waandishi wenzangu, tusali kama tunakufa leo na tusipange mipango kana kwamba tutaishi milele.. ndiyo tunavyopaswa kuishi" alisema.Sr. Shirima

Katika ibada ya kuadhimisha Jubilei hiyo kwa wanahabari iliyofanyika katika Kanisa Kuu Katoliki la mtakatifi Patris, mjini hapa, Padre Alfred Sowa, aliwataka wandishi kuandika habari zenye kujenga maadili mema badala ya kupotosha na kuangamiza jamii.

Alisema siku hizi vyombo vingi vya habari vinajali zaidi maslahi ya kibiashara kuliko maadili na hivyo kuifanya jamii kupotoshwa zaidi na habari zinazoandikwa au kutangazwa na vyombo hivyo.

"Leo mtu akitaka kuanzisha gazeti, anaangalia jamii inataka kusoma habari za namna gani na sio habari gani zinajenga. Mitaani sasa yamejaa magazeti ya ngono ambayo huwezi kusoma nyumbani na kumpa baba yako... na magazeti haya yanasomwa na watu wa rika zote tu,"

Alisema na kuongeza kuwa, ongezeko la idadi ya magazeti yanayoandika zaidi habari za ngono linadhalilisha fani ya uandishi wa habari na kuporomosha maadili ya jamii.

Padre Sowa, alisema kuwa fani ya uandishi wa habari ni wito wa pekee kwa kuwa mwandishi anaweza kuchochea mabaya au kufundisha mema iwapo atakuwa mwaminifu na mkweli na mwadilifu.

Naye Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Mhashamu Telesphor Mkude akiongea na waandishi wa habari Wakatokiki katika tafrija aliyowaandalia nyumbani kwake Kilakala mjini hapa, aliwapongeza kwa kuwa bega kwa bega katika uinjilishaji kwa kutumia vyombo vya habari.

Aidha, Askofu Mkude, alikisifu kituo cha Televisheni cha mjini hapa cha ATV kwa kurusha vipindi vya dini zote bila ubaguzi. "Wakati wa Kwaresma tumepata vipindi vya Kwaresma na Waislamu wakati wa Ramadhani," alisema na kuongeza kuwa Kanisa lake litafanya bidii kuwafikishia watu wa vijijini habari hasa kwa kutumia RADIO UKWELI.

Siku moja kabla, waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali, waliungana na Wakristu wengine duniani kuadhimisha Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristu kwa kufanya hija.

Katika hija hiyo, waandishi wa habari walitembelea mwendo wa kilomita nne hadi kwenye Kanisa la Parokia ya Mgolole ambapo walipokewa na Padre Bathlomew Mtemi kabla ya kufanya mafungo na ibada.

Akitoa mafundisho katika mafungo hayo. Sr. Maria Magdalena Bulati, wa Shirika la Moyo Safi wa Bikira Maria, alisema kuwa waandishi wa habari ni maketekista namba moja kwa kuwa wana nafasi kubwa ya kumtangaza Kristu katika kazi zao.

Jumla ya Waandishi 26 wanaofanyia kazi mjini hapa walifanya hija kuadhimisha Jubilei kwa Waandishi wa Habari duniani.

‘Eleweni vema Biblia kuwakwepa manabii wa uongo’

Na. Getruder Madembwe.

Wakristo kote nchini wametakiwa kujenga mazoea ya kuyachambua vema Maandiko Matakatifu ili kuepuka kudanganywa na kuyumbishwa kiimani na manabii wa uongo.

Ushauri huo ulitolewa na Mwalimu Doto Magesa, wa Kanisa la Waadventist kundi la Lugalo jijini Dar Es Salaam, wakati wa ibada iliyofanyika mwanzoni mwa juma lililopita.

Mwalimu Magesa, alisema kuwa ni vizuri kuwa na utaratibu huo wa kusoma na kushirikishana katika kuichambua na kuielewa ili hata pindi atokeapo mtu mwingine mwenye lengo la kupotosha, afahamike kiurahisi kuwa ni muongo.

"Ni vizuri tukawa na mazoea ya kuyachambua Maandiko na siyo kuyasoma na kuyaacha hivyo hivyo kwani watatokea manabii wa uongo watakao taka kuwadanganya na kwa kuwa watu hatuyajui vema Maandiko, utajikuta utakubaliana nao. Ni vizuri kujenga utamaduni wa kuyasoma Maandiko kila wakati na kuyaelewa vizuri ili tusije tukadanganywa" alisisitiza Mwalimu Magesa.

Akihubiri katika ibada hiyo, Bw.Abel Kiyangi ambaye ni msharika wa kanisa la Kimara jijini Dar es Salaam, aliwataka waamini hao kuwa na matunda ya mienendo na imani sahihi ya kumpendeza Mungu na wala sio kuwa kama majani tu ya mmea.

Alisema kila muamini wa dhehebu hana budi kujiuliza katika nafsi yake kuwa ana matunda ya aina gani ili Yesu atakapo kuja amkukute akiwa tayari badala ya kuanza kuhangaika hangaika wakati huo.

Aliyataja matunda hayo kuwa ni pamoja na upole kiasi, upendo ,utu wema, fadhila na mengine mengi yanayotimiza mapenzi ya Mungu.

Aliongeza kuwa Yesu hawaangalii kwa kusema wala kujali idadi, familia au kundi bali humtazama mtu mmoja mmoja kwa kadri ya imani na matendo yake.

"Kamwe Yesu hawatizami kwa kusema kuwa hawa watu ni wa kundi moja au familia moja, hiyo si kweli. Yeye humuangalia kila mtu kwa nafsi yake mwenyewe,"

Alisema Bw. Kiyangi na kutoa mfano kuwa Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa akienda Betania aliuona mti akidhani kuwa una matunda lakini alipoona hauna aliulaani na kuuambia usizae kamwe na pale kulikuwa na miti mingine lakini hakuitazama miti hiyo mingine bali yeye aliuangalia mti huo huo mmoja"

Wanawake mnasababisha kupinduliwa na 'House girl'

Na Josephs Sabinus, Bagamoyo

MWINJILISTI mwanamke 'amewapiga madongo' wanawake wanowakosesha waume heshima na upendo hivyo kusababisha ndoa zao kupinduliwa na wasichana wao wa kazi.

Mwinjilisti Frida Mangala wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Bagamoyo, alitoa shutuma hizo mwishoni mwa juma alipozungumza na KIONGOZI kanisani kwake mjini hapa.

Alisema ingawa kimsingi haungi mkono waajiri wa kiume kotoroka ndoa zao halali na kufanya mapenzi na 'housegirl' wao, ni dhahiri baadhi ya wanawake wanastahili kulaumiwa kwa kuwa kichocheo cha tabia hiyo chafu.

"Wanawake wenye mahousegirl ndio wanaosababisha; wanashidwa kujua ni kazi ipi amfanyie mmewe na ipi afanye huyo msichana wa kazi" alisema na kuongeza.

"Eti wanataka hata chakula ampangie, maji ya kuoga hata nguo ipi avae wakati mke wake yupo amekalia video? ni hatari sana katika ndoa, lazima 'housegirl' umpe kazi kwa mipaka na kiasi".

Alisema wanawake wengine hubweteka na hali yao ya kuwa waajiri hali inayowapelekea kujisahau kwa starehe na kuwadharau waume zao bila kuzingatia kuwa mume ni kichwa cha familia.

"Hata wanaume nao waache tamaa, mtu anamuacha mke halali eti anamfuata 'housegirl' na matokeo yake anamfukuza mkewe, si vizuri wanamkosea hata Mungu maana wale ni sawa na watoto wao wa kuzaa" alisema.

Mwinjilisti Frida,aliliambia KIONGOZI kuwa alipokuwa akihubiri katika ibada ya Jumapili iliyopita katika Kanisa la Mtaa wa Kigongoni eneo la Gerezani, aliwataka wakristo kujenga utamaduni thabiti wa kuthamini, kujivunia na kutetea imani yao ya kristo bila aibu, uoga wala unafiki ili kuepuka hatari ya kughiribiwa na kutekwa na imani nyingine.

"Mwingine utamwona si popo, si ndege kumbe ana lengo binafsi. kama ni mchumba, omba Mungu, mke au mume mwema kutoka kwa Mungu na siyo kuvamia baadaye unashindwa hata kushuhudia imani yako" alisema

'Msiwe karibu na Yesu, kuweni ndani yake'

Na Leocardia Monswery

MCHUNGAJI Amani Kayuni wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Mbagala, dayosisi ya Mashariki na Pwani , amewataka Wakristo kuacha dhana ya kuwa karibu na Yesu badala yake, wawe ndani yake ili wapate kuuona Ufalme wa mbinguni.

Akihubiri kanisani kwake katika ibada ya Jumapili iliyopita, eneo la Mbagala Zakhiem, Mchungaji Kayuni alisema, inashangaza kuona watu wangi wanaishi katika maisha yanaoyoonekana kuwa karibu na Yesu badala ya Wakristo hao kuwa na uhakika wa mawazo, maneno, matendo na imani yao kuwa ndani ya Yesu.

"Watu wengi wapo karibu na njia lakini, hawapo njiani," alisema na kuongeza kuwa hali hiyo ya kuwa karibu bila kuwa ndani ya yesu, ni mafirifiri akimaanisha madudu fulani yanayoingia katika mishipa ya damu.

Alisema kuwa watu wengi hawajijui kuwa wanayo mishipa miwili ambayo ndiyo mikuu inayoweza kuishi ndani ya binadamu ukiwa kama Mkristo.Mchungaji huyo wa KKKT, alizidi kufafanua juu ya mishipa hiyo na kusema kuwa mishipa hiyo miwili ni ile ya neema ambao Mkristo aliyenao ataweza kuingia mbinguni pasipo shida, na mshipa mwingine ni ule wa majuto ambao ukiwa nao, moja kwa moja una uhakika wa kwenda kwenye ziwa la moto.

Hata hivyo mchungaji huyo aliwataka waamini hao kuacha tabia ya kuwaona wachungaji na wahubiri kama picha za video ambazo ukishatazama, basi huambulia upuuzi uliooneshwa na kuondoka huku umesahau kila kitu.Aliwataka wajenge utamaduni wa kuwaheshimu kuwasikiliza na kuuamini kisha kufanyia kazi mafundisho wanyokuwa wamewapa.

"Hivi wewe hujisikii kuingia ufalme wa Mungu, na kwanini uwe na gia moja badala ya tatu".

Hata hivyo, alibainisha kuwa katika ibada nyingi makanisani, wapo watu wengi wanaokwenda kwa nia na malengo tofauti na yale yanayolenga mapenzi ya Mungu.

Msiende kanisani kufuata wachungaji

Na Dalphina Rubyema

WAUMINI wa madhehebu mbalimbali wametakiwa kuachana na tabia ya kwenda makanisani kutegemea uwepo wa mchungaji na badala yake, wajenge msingi na imani kuwa wanakwenda katika nyumba ya Mungu.

Hayo yalisemwa katika ibada ya Jumapili iliyopita na Mchungaji Laurence Kametta, wa Kanisa la Tanzania Asemblies of God(TAG), Usharika wa Tabata-Liwiti jijini Dar-Es-Salaam, wakati akizungumza kanisani hapo.

Alisema wapo baadhi ya waamini wenye tabia ya kutokwenda kanisani kwa kuwa wamesikia mchungaji hayupo na akaonya dhidi ya tabia hiyo kwani ingawa mchungaji anaweza kuwa hayupo, lakini bado Kanisa na uongozi wake mwingine wanakuwapo kushirikiana nao katika kumuomba Mungu.

"Tusiwe wafuasi wa mchungaji bali tuwe wafuasi wa Yesu Kristo. Siyo mimi sipo halafu na nyie jioni mshindwe kufika. Wapo wazee wa kanisa; wapo watatoa Neno badala yangu," alisema.

Aliwahimiza waamini wake kurudi kanisani kwa maombi ya jioni na kuachana na visingizio visivyokuwa na maana kiimani.

Akihubiri katika ibada hiyo, mwana ushirika Bw. Kiliani Haule, aliwaambia waamini wa kanisa hilo kuwa wasiugeuze Ukristo kuwa wa kusali kwa kupitia kwenye mahubiri yanayooneshwa na vituo vya television, bali ni muhimu kwao kufika kanisani na kujumuika na wenzao.

"Unakaa nyumbani kwako na kuwasha TV unaona mahubiri ya Kenya, Tanzania nzima, Rwanda na hata Ulaya, wewe sasa unajiona umeokoka na hakuna mlokole mwingine kuliko wewe, Ukristo ama ulokole siyo huo; njooni kanisani ujumuike na wenzako na kupata utakaso" alisema Bw. Haule.

Aliwataka watu waliookoka kusimama Imara kuyashinda majaribu kwa kutumaini kuwa baada ya kifo watauona na kuhufurahia Ufalme wa Mungu.

"Ulokole siyo ulokole kamili mpaka upitie vikwazo vingi jitahidini kuvishinda hali mradi unajua kila uliofanyika haliendi kinyume na matakwa ya Mungu na hapo ndipo utakapo urithi uzima wa milele" alisema.