Make your own free website on Tripod.com

Makanisani Wiki hii

Kardinali Pengo awatia moyo vijana

Na Getruda Madembwe

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam Mwadhama Kardinali Pengo amewataka vijana waliopata Kipaimara kumpokea Roho Mtakatifu katika hali ya dhiki na shida na kamwe wasikate tamaa.

Mwadhama Pengo aliyasema hayo Jumapili iliyopita katika Parokia ya Mtakatifu Kamili iliyopo Yombo Vituka jijini Dar es Salaam.

Alisema wao kama vijana waliompokea Roho Mtakatifu wawe Imara na kuhakikisha kuwa hawakati tamaa na badala yake wakubali kuteseka na hata ikibidi kutundikwa juu ya msalaba kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyotundikwa.

"Ninyi vijana mnaopokea sakramenti ya Kipaimara mjue kuwa mnampokea Roho Mtakatifu hivyo basi mkubali kufanya matendo yaliyomema katika hali ya dhiki na shida na kamwe msikate tamaa na wala msisubiri kupongezwa na ulimwengu huu" alisisitiza Mwadhama Pengo Akaongeza kuwa "Mkubali kuteseka na hata ikibidi kutundikwa juu msalabani kama Bwana wetu Yesu Kristo alitenda mema lakini aliishia juu ya msalaba".

Alisema kama ilivyokuwa kwa Kristo ambapo hakupongezwa sababu aliwaponya wagonjwa na hata wale ambao walikuwa na pepo wachafu aliwatoa kinyume chake aliishia msalabani. Kadhalika na Mtakatifu kamili hakupongezwa kwa nia yake njema na kinyume chake ilimbidi kuanguka daima katika msalaba nasi tuwe hivyo.

Makanisa yatakiwa kushirikiana bila kujali tofauti za kiimani

Na Mwandishi Wetu

ASKOFU wa Kanisa la African Inland Church (AIC) Charles Salala ameyataka makanisa yote nchini kushirikiana na kuondosha tofauti zao za kiimani katika umoja wao.

Askofu Salala, aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 2000 iliyojumuisha wanawake wa madhehebu mbalimbali iliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee jijini.

Alisema makanisa hayana budi kufuta tofauti zao na badala yake waamini wake wakae kwa pamoja na kushirikiana kwani wakifanya hivyo watakuwa wamemtukuza Mungu.

"Kamwe nawaambieni msiweke tofauti zenu katika kuabudu kwani utakuta dhehebu fulani hawataki kushirikiana na wengine kwa sababu eti wao wanatumia Liturujia au wale wanaongoza ibada zao kwa kuongozwa na nguvu za Roho Mtakatofu" alisema Askofu Salala.

Askofu huyo wa Kanisa la AIC aliendelea kusema kuwa makanisa yote ni sawa na ua waridi kwani kuna maua ya namna hiyo ambayo ni mekundu, meupe na rangi zingine na aina zote hizo ziko sehemu moja na kusisitiza makanisa yenye imani tofauti hayanabudi kukaa pamoja kwa kuiga mfano wa ua waridi.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Luteni Yusufu Makamba katika maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake wa Kikristo nchini Bi.Debora Mwenda alisema kuwa wao kama wanawake hawana budi kumtangaza Bwana kuwa ni mwokozi na hivyo watazidi kuomba amani zaidi kuwepo katika nchi.

Luteni Makamba kwa upande wake aliyataka makanisa yote kupiga vita rushwa badala ya jamii kuilaumu serikali juu ya suala hilo huku ikijua fika kwamba ilianza tangu zamani.

"Watu wanailalamikia Serikali ya awamu ya tatu eti imejaa rushwa na wakati rushwa imeanza toka zamani hata katika kaburi la Yesu kulikuwepo na mazingira ya rushwa hivyo basi hatuna budi kuchukia suala hilo" alisema Luteni Makamba.

Wakati huo huo: Askofu Basil Sambano wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam amewataka akina mama kote nchini kukemea vikali vitendo vya utoaji mimba ambavyo hufanywa na mabinti zao na kuwahoji pindi wanapogundua kuwa wametoa mimba.

"Wasichana wamekuwa hawana huruma kabisa kwani hawatupa watoto wao na kutoa mimba nyingi akinamama muwahoji hao mabinti zenu pindi mnapogundua wamefanya hivyo. Kwa mfano mwanao leo ana mimba lakini ikifika kesho asubuhi hana. Umuhoji mimba yake imekwenda wapi na wala sio kukaa kimya" alisitiza Askofu Sambano.

Makanisa yaliyohudhuria katika maadhimisho hayo ni pamoja na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) African Inaland Church (AIC) Anglikana, Baptisti, Jeshi la Wokovu, Roman Catholic, Moravian, Presybiteria, Udugu na shirika la Afrika Evanjilist Enterprises (AEE)

Msihubiri kwa kufumbiana, kemeeni maovu-Askofu aonya

Na Neema Dawson

WAKRISTO duniani wakiwamo wahubiri wametakiwa kukemea madhambi bila unafiki, woga wala kuwaonea aibu watu maarufu na wazee, wanaotumia nafasi zao kufanya mambo yenye kuudhalilisha utu na kukiuka mapenzi ya Mungu.

Wito huo ulitolewa na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar-Es-Salaam, Basil Sambano, katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Kristo Mfalme, Dinari ya Kinondoni hivi karibuni.

Alisema kila Mkristo na hata jamii nzima, haina budi kuwa jasiri na yenye mshikamano katika kukemea maovu yanayotendwa na baadhi ya watu maarufu na wenye nafasi muhimu wakiwamo wazee bila kuwaonea aibu, kuwa na unafiki wala kwaogopa wahusika.

"Ni ajabu na inasikitisha kuona hata Wakristo wengi siku hizi wanaoneana aibu kusemeana maovu yao na inafikia hatua hata wahubiri nao, wanahubiri kwa kufumbianafumbiana bila kufahamu kuwa ni wajibu wao kukemea maovu yote kwa kuwa Roho Mtakatifu yupo juu yao na hata ulimwengu unalitegemea Kanisa katika kusaidia na kuwaokoa watu wanapokwama kimaisha na kiroho.

"Mimi niko tayari kufa kwa ajili ya kukemea dhambi kwani wapo wazee wanaotawala vyema nchi na pia, wapo wazee wasiojiheshimu na wanautumia uzee wao kujipatia umaarufu kwa kutenda mambo ya ajabu ajabu. Lazima jamii iwakemee hao, wafike mahala watambue thamani kubwa ya wao wenyewe kujiheshimu."

Aliwashauri viongozi wenzake wa dini kukaza uzi katika kulinusuru taifa kutoka maangamizo ya kimwili na kiroho kwa kuonesha upendo kwa kuwa ulimwengu wa sasa ni mgumu kuliko wa siku za nyuma.

Alisema ulimwengu huu wa sasa ni wa mashakamashaka hali inayopelekea watu kupenda kuthamini fedha kuliko utu wa mtu na akahimiza kuwa viongozi wa dini wanaweza kuliokoa Taifa kwa njia ya kuonesha upendo pekee kwani ulimwengu huu tunamoishi ni mgumu kuliko wakati uliopita ambapo upendo wa watu wengi ni wa mashaka mashaka kwani imefikia hatua watu wanapeda fedha kwa kuuza utu wa mtu na kwamba hali hii, inasababisha unafiki katika kukemea maovu kwa baadhi ya watumishi wa Mungu.

Alisema Wakristo ambao wamekuwa wakijitangaza kuwa wameokoka, kujua kuwa hiyo ni kazi na neema ya Mungu.

Aliwahimiza kujua kuzingatia kuwa huwezi kusema kuwa unampenda Mungu usiyemjua na wakati huo unamchukia binadamu unayemfahamu.

Wakristo watakiwa wasiwe hovyo kwa ushirikina

Na Agatha Rupepo DSJ

"Eti utakuta Mkristo anakwenda kwa Sangoma kutafuta utajiri, hivi yeye Sangoma angekuwa na uwezo wa kukupa wewe utajiri, unafikiri yeye angeendelea kuwa Sangoma? kama huo si udhaifu wa kiimani , ni nini?"

"Hiyo yote ni kazi ya shetani ya kutaka kuwapotosha wanadamu. Lazima kila mtu ujue kuwa, mwili wako ni Hekalu Takatifu na mtu atakayeuharibu mwili wake na Mungu atamharibu".

Maneno hayo yenye onyo kali yalitolewa Jumapili iliyopita na Mchungaji Shadrack Sabaya, wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora, wakati akizungumza katika ibada iliyofanyika katika kanisana la Ukonga, jijini Dar-Es-Salaam.

Alisema hivi sasa, Kanisa la Mungu limechafuka kwa kuwa baadhi ya Wakristo wenye imani haba, wamekuwa wakijishughulisha na matendo mbalimbali ambayo ni machukizo kwa Mungu ikiwa ni pamoja na imani za ushirikina hususani wanapopatwa na matatizo.

Aliwasisitiza kuwa badala ya kuutumia ushirikina kama ufumbuzi wa matatizo yao, hali ambayo huyakaribisha mno, hawana budi kumtegemea Mungu kwa kuwa ndiye pekee anayeweza kuyatatua na hata kuyamaliza kabisa badala ya hao wanadamu ambao wanaweza kuyachochea.

Alisema wanadamu wenye uwezekano mkubwa wa kwenda mbinguni, ni wale wasiojihusisha na vitendo vya ulevi, uzinzi wala ushirikina, na wala sio kwa kuogopa shari na matatizo ya duniani, bali kwa imani na lengo la kutimiza mapenzi ya Mungu.

Mchungaji huyo alionya kuwa hivi sasa Wakristo wengi wameiharibu miili yao kwa ulevi, kuvuta sigara, uzinzi na ufisadi vitu ambavyo havipendezi machoni pa Mungu na kwamba hali hiyo haina budi kuepukwa.

KKKT wakemea maombi kinyume na imani, matendo

Na Mwandishi Wetu

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limewataka Wakristo wenye tabia ya kusisitiza maombi ya mdomoni tu, kuachana nayo na badala yake, maombi yao yaende sambamba na imani na matendo yao bora ili wauone Ufalme wa Mungu.

Akizungumza katika ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Kanisa la KKKT, usharika wa Tabata jijini, Mchungaji Ezekieli Mwakisu wa KKKT, usharika wa Manelomango, "aliwaponda" wanaofanya maombi na kutoa sadaka zao kwa lengo la kujionesha mbele za watu, wakati maombi yao ni ya mdomoni tu, yasiyoendana na imani zao sahihi toka mioyoni na kwamba watu wa namna hiyo, ni wanafiki na wanastahili kujirudi.

"Kuna wengine wanaomba wakidhani kuwa ili kuonesha kuwa yeye ni Mkristo sahihi, lazima aombe na kutoa sadaka hata kama anajua wazi kuwa maombi yake ni ya mdomoni tu wala hayatoki moyoni. Na hata huko moyoni mwake, hayuko kama anavyoonekana wakati huo."

Alisema na kuongeza kuwa umuhimu wa maombi unaanza kuonekana kufuatia nia, imani na matendo sahihi yenye kumpendeza Mungu vinginevyo, maombi yote ni kazi bure na wala hayasaidii kitu.

Alibainisha kuwa ili maombi ya mtu yafanikiwe, mwombaji hana budi kujihakikisha kuwa hana kikwazo cha aina yoyote ya dhambi na akiwa amekusudia kabisa kuiacha huku akiwa amejinyenyekeza kikweli mbele za Mungu.

"Mtu anapopata matatizo anapaswa kuomba ili Mungu amsaidie. Lakini unapofanya maombi huku moyo hautaki, ujue kuna kikwazo moyoni na ili ukishinde, hakikisha unajichunguza nafsi yako na kukiondoa kabisa kile kikwazo utakachokuta. Mwingine anakuwa si kwamba hataki kuomba, bali anatawaliwa na mambo ya kidunia tu." Alisema.

Alitahadharisha dhidi ya maombi yenye kumjaribu Mungu na kusema kamwe hayo hayazai matunda. "Mara nyingi tunakuwa tunaomba tukitaka haraka haraka. Yani tunataka kupata leoleo na hii ndio inasababisha mara nyingi tunaanza kulalamika, Oooo! Mungu hanipendi , hanipendi. Mungu ana wakati wake.

Anaweza kukupa gari, pesa, hata nyumba. Hata hivyo, wengine wanaomba kwa nia mbaya na hao Mungu anajua nia zao na anajua akiwapa, watamsahau na kupotea.

Aliwahimiza Wakristo kutokukata tamaa katika maombi yao na wadumu katika sala zinazoendana na imani na matendo yao sahihi.

Msiwatenge wagonjwa, mkihofu kuambukizwa - Wito

Na Elizabeth Steven

JAMII imetakiwa kuichukia na kuikemea dhana potofu ya kuwatenga wagonjwa kwa kuogopa kuambukizwa maradhi kwa kuwa hata mbele ya Mungu, wagonjwa wanathamani sawa ya kibinadamu.

Wito huo ulitolewa na Padre Gerard Derksen, wa Kanisa Katoliki Parokia ya Makuburi katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, wakati wa ibada ya Siku ya Wagonjwa kanisani hapo.

Alisema kwa watu wa Mungu, si busara kuwatenga wagonjwa kwa kuhofu kuambukizwa kwa kuwa moja ya vipimo vya Mungu katika kuwajua wanaomtumikia vema, ni pamoja na namna mtu anavyowatembelea na kuwahudumia wagonjwa kwa upendo.

"Wagonjwa wana thamani kubwa mbele za Mungu. Hivyo basi, jamii haina budi kuwaonesha moyo wa upendo ikiwa ni pamoja na kuwafariji," alisema.

Hata hivyo, licha ya kuwasisitiza kutowabagua wagonjwa, Padre Derksen, aliihimiza jamii kuwahudumia kwa kuzingatia maagizo na ushauri wa wataalamu, bila kukiuka mapenzi ya Mungu.

Aliwataka viongozi wa jumuiya ndogondogo kuweka katika jumuiya zao, utaratibu wa kuwatembelea wagonjwa katika maeneo yao kwa kuwa wagonjwa wanapotembelewa, hufarijika na kujiona kuwa jamii haijawatenga na iko pamoja nao.

Aidha, amewataka wagonjwa au wauguzi wao, kwa pamoja kuwa na matumaini ya kuuona ufalme wa Mungu kufuatia maombi, imani na matendo yao na hivyo wote kujikabidhi mikononi mwa Mungu.

Jumapili iliyopita, Padre Derksen, alitoa Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa kwa wagonjwa kadhaa , uliofuatiwa na chakula kilichoandaliwa mahususi kwa siku hiyo ya Wagonjwa.