Makanisani Wiki hii

Wainjilisti 170 wa Kakobe wakacha mafunzo

Agatha Rupepo na Peter Dominic

KATI ya watumishi wa Mungu 243 wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship linaloongozwa na Zacharia Kakobe, 68 pekee ndio waliohitimu mafunzo ya Uinjilisti na kuwekewa mikono sambamba na kutunukiwa vyeti baada ya wengine kuingia mitini.

Jumapili iliyopita katika Ibada ya Pili, kiongozi mkuu wa kanisa hilo, Zakaria Kakobe, aliwawekea mikono na kuwatunuku vyeti wafuasi 68 kati ya 243 waliohitimu mafunzo ya miezi mitatu ya Uinjilisti yenye lengo la kujenga na kuimarisha Kanisa hilo.

Mafunzo hayo yalifanyika jijini Dar-Es-Salaam na wahitimu walipata daraja la uinjilisti.

Kakobe, alisema katika ibada hiyo kuwa ingawa mafunzo yalihudhuriwa na watu wengi lakini wengi walishindwa kwa kuwa anajua ingawa wengine walitoa udhuru, wengi wao hao walikwepa au kushindwa majukumu ya utumishi bora wa Mungu.

"Bwana anapenda utayari wetu kila wakati katika kumtumikia. Lakini, huwa tunatoa udhuru tunapotakiwa na Bwana. Unapoitwa, itikia NITUME MIMI," alisema Kakobe.

Aliwasifu wahitimu hao kwa kusema kuwa uvumilivu wao ndio umepelekea mafanikio ya kuhitimu kwao mafunzo hayo ya uinjilisti ambayo wameyapata baada ya kuwa wavumilivu kutokana na misukosuko waliyokutana nayo.

"Wamekuwa waaminifu na wavumilivu kufanya kazi ya Bwana bila shaka amependezwa nao.

"WACHUNGAJI wa makanisa mengine wanashangaa kuona kanisa letu linavyojengeka kwa Uimara ni kanisa moja lenye watu wengi lakini hatuna migogoro ili ujenge Kanisa imara unahitaji kuchumbia nguzo Imara"

Kakobe aliwataka wafuasi wake kutoangalia uwezo walionao katika kuifanya kazi ya Mungu, maana Mungu anaweza kuwapa nguvu za uongozi kama alivyomfanyia Petro.

"Nawatuma mkawaombee na kuwahudumia watu kiroho. Msifanye kazi kwa kumwogopa mtu," aliasa.

Aidha, katika hafla hiyo watumishi wengine wa kanisa hilo walitunukiwa vyeti maalumu vya uvumilivu na uaminifu.

"Bila shaka wengi wenu mmeoa na wengine mmeolewa. Nawatuma mkawahamasishe vijana na watu wengine ambao hawajafunga ndoa ili wafunge ndoa kuondoa tatizo la uasherati " alisema.

Ili kuhakikisha wafuasi wahitimu hao hawateteleki katika utendaji wao, tayari kanisa hilo limewapeleka kijiji cha Kimanzichana nje kidogo ya jiji la dar Es salaam kuangalia hali halisi ya kazi hiyo kutokana na Mwinjilisti mwingine wa Kanisa hilo Bi. Rebeka Mwaluvanda kutenda kazi hiyo kwa ugumu.

Waamini watakiwa wasiwe vuguvugu

Na Elizabeth Steven

MWINJILISTI, Kishe Mhando, wa Kanisa La Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.KT), usharika wa Mbezi Beach, jijini, amewaasa waamini wa dini ya Kikristo kutokuwa vuguvugu katika imani zao na badala yake wawe na msingi thabiti wa imani.

Akizungumza wakati wa ibada iliyofanyika katika usharika wake ulipo ndani ya dayosisis ya Pwani na Mashariki ya K.K.K.T hivi karibuni, Mwinjilisti huyo alisema baadhi ya Wakristo wamekuwa na imani vugu vugu na akaonya kuwa tabia ya namna hiyo haistahili mbele za Mwenyezi Mungu na hivyo hawana budi kuachana nayo mara moja ili wadumu katika kuifanya kazi ya Kristo.

Alisema katika maisha, kama yalivyo maua yanayopendeza na kunyauka baadaye, mwanadamu hana budi kukubaliana na mabadiliko yanayojitokeza yawe mazuri au mabaya ili maradi yeye mwenyewe awe amelenga kuyafanya yawe yanayokubaliana na mapenzi ya Mungu.

"Wengine wanaishi maisha ya vuguvugu, mara wa moto; wakati mwingine baridi mara vuguvugu . hayo si maisha mema ya Kikristo. Lazima uwe na imani kamili kwa Bwana Yesu. . Haya, kadhalika, utamuona hata msichana akimuona kijana amependeza, anadhani hawezi kubalika, anamkimbilia; ukubali usikubali tabia hiyo ya kubadilika badilika, ipo. Mabadiliko yapo na hayo yote yanapita.

Sasa wewe unapoishi maisha ya uvuguvugu, siyo vema lazima ukubali kufanya mabadiliko na kumrudia Mungu ndiyo maana unaona hata ua huchanua na baadaye kunyauka na ndivyo yalivyo hata maisha ya mwanadamu." alisema.

Mwinjilisti huyo alionya dhidi ya tabia ya watu wanaojiona kama watu wanaoishi katika Ukristo bora kumbe ndani yoa wamejaa uozo na dhamira mbaya dhidi ya dini zao na akasema watu wa namna hiyo hawana budi kuachana na kasumba hiyo ya maisha kwani ni hatari kimwili na hasa kiroho.

"Najua kuna watu wengine wanajiona kuwa wanaishi vema katika Kristo, kumbe mioyoni ndani, wana yao tofauti kabisa na Kanisa. Sidhani kama hata humu kanisani wapo watu wa namna hiyo na kama yupo, mwenye nia mbaya au tofauti na mapenzi ya Mungu, nampa pole".alisema.

Aidha, Mwinjilisti huyo aliwataka waamini wenye nia njema na makanisa yao, kushirikiana bega kwa bega na viongozi wao ili kukabiliana sawia na mabadiliko yoyote yanayojitokeza katika mazingira ya nayoweza kuathiri kazi za Kanisa.

"Si kazi ya mchungaji peke yake kufanya mazuri katika kanisa; anatakiwa asaidiwe maana ana kazi kubwa ya kuwakusanya, kuwaongoza na kuwaweka katika kundi moja maana wajibu mkubwa wa mchungaji ni kuhubiri bila uoga." Alisema

Msichanganye mila na Ukristo kutatua matatizo-AEE

Na Josephs Sabinus

SHIRIKA la African Evangelistic Enterprises (AEE), limewaonya Wakristo dhidi ya tabia ya baadhi yao, kuchanganya mila za makabila na Ukristo katika kutatua matatizo ya jamii.

Akizungumza katika ibada ya Jumapili iliyopita ya Kanisa la Moravian Tanzania, Usharika wa Keko Jimbo la Kusini wilaya ya Mashariki, ndani ya Kanisa la Pentekoste Tanzania, Parishi ya KekoMachungwa jijini, Mwinjilisti Nyambilila A. Lwaga, alisema katika mahubiri yake kuwa hivi sasa mambo mengi hayaendi vizuri katika jamii kwa kuwa baadhi ya waamini wenye imani duni wanachanganya imani zao na mila za kiasili hali ambayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

Alisema ni ajabu na inasikitisha kuwa watu wengi wanaokwenda kwa waganga wa kienyeji ni washirika na wale wanaojiita wanaokoka na kwamba ndiyo maana makanisa mengi yamejaa ugomvi, masengenyo, matusi, wizi, na mambo ya ajabu ikiwa ni pamoja na kuchunguzana mavazi mambo aliyoyasema yako kinyume na Ukristo.

"Unajiita Mkristo, umeokoka, unapoamua kwenda kwa mganga wa kienyeji kupiga ramli, hujui kuwa imani ya namna hiyo ni hasara na hatar;i kwa sababu mganga atakufanyia mambo ya ajabu na ya kijinga kwa kuwa anajua una shida na utakubaliana naye."

"Hivi lakini, kwanini uchanganye Ukristo na mila za kikabila? Kama ni Unyakyusa, chagua Unyakyusa na kama unachagua imani ya Biblia, chagua hiyo. Msiingize mila ndani ya Ukristo na wala msichanganye mila na Ukristo kutatua matatizo. Hivi Mkristo kabisa ni vipi useme oo! Mambo hayaendi vizuri; watoto wanauguaugua, nimezaa bubu; eti kwa kuwa sikuchinja ng’ombe kwenye kaburi la babu na wala sijapika pombe. Hivi kweli Mkristo unasema hivyo? Unatoa wapi mawazo hayo potofu?"alihoji.

Aliyahimiza makanisa yote kutoa msukumo bora wa ufundishaji wa "Sunday School" kwa kuwapa walimu wanaofundisha vitendea kazi muafaka.

Alisema pia kuwa ni muhimu kanisa yakawapa kazi ya kuwafundisha watoto wa Sunday Schools ambao wanamafundisho ya kutosha ya elimu ya dini na wana ujuzi na mbinu za ufundishaji.

"Lazima wanao wafundisha watoto wa Sunday School wawe na walau ka ujuzi kidogo sio tu, leo huyu, kesho huyu. Mwingine hajui hata mbinu moja ya kumfundisha mtoto na pengine hata kipaimara hajapata. Sasa mtu kama huyo atamfundishaje mtoto. Tazama hata wenzetu hawa "Watoto wa mama mdogo" hata wazee walioiva mafundisho wanashiriki kuwafundisha watoto. Wanajua umuhimu wao kwa siku zijazo," alisema.

...Wamoravian walazimika Kusali makanisa mawili kwa ibada moja

Na Mwandishi Wetu,

WAUMINI wa Kanisa la Moravian Tanzania, ushirika wa Keko, Jimbo la Kusini,Wilaya ya Mashariki, wamelazimika kutumia makanisa ya madhehebu mawili tofauti kwa ibada moja kufuatia tatizo la ukosefu wa kanisa lao.

Tukio hilo lililoshuhudiwa na mwandishi wa habari hizi, lilitokea Jumapili iliyopita wakati Wamoravian walipokuwa wakisali ndani ya jengo la Kanisa la Pentekoste la Parishi ya Keko na kulazimika kuhama na kwenda kumalizia ibada nje ya jengo lao la Kanisa la Moravian lililopo kando ya barabara eneo la Keko Machungwa jijini kwa kuwa muda wao wa kutumia kanisa la Pentekoste ulikwisha na kulazimika kuwapisha wenyeji wao.

"Nitakuwa ninapiga kelele mpaka wasiopenda maendeleo wanichukie mpaka tutakapoondoa hali hii," alisema Mchungaji Salatieli Mwakamyanda, wa Kanisa la Moravian, akiwahimiza waamini kuongeza juhudi za kuchangia kukamilika kwa ujenzi huo huku akiwataka wajionee hali halisi ya ujenzi ambao sasa umefikia hatua ya kuandaa sakafu ya ghorofa ya kwanza.

Tangu Aprili 30, mwaka huu Wapentekoste wa Parishi ya Kekomachungwa, wamekuwa wakiwahifadhi waamini wa Kanisa la Moravian Tanzania Usharika wa Keko kufuatia ujenzi unaooendelea kanisani kwao.

Kwa mujibu wa makubaliano yao, Wamoravian wameruhusiwa kulitumia kanisa hilo siku za Jumapili kwa ibada za Jumapili kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:30 asubuhi ambapo Wapentekoste wanaanza.

Akisisitiza umuhimu wa Wakristo hao wa Kanisa la Moravian Usharika wa Keko kutumia nguvu zao kukamilisha ujenzi wa kanisa, Mwinjilisti Lwaga alisema," Lazima Wamoravian wa Keko muone uchungu wa kuwa mnasali kwa kukimbia kimbia ili kuwapisha wenye kanisa hili watumie. Tunajua suala la ujenzi au pesa huwa ni gumu kidogo kwa kuwa unapozungumzia pesa nyuso za ukali huanza kuonekana.

Katika kuhimiza kujinyima na kuwa mfano bora wa kuigwa na waamini hao, Mwinjilisti Lwaga anayejishughulisha zaidi katika kitengo cha mafunzo kwa akinamama cha AEE, Katika kuhamasisha ujenzi wa Kanisa hilo, Mwinjilisti Nyambilila wa AEE, ameahidi kufunga mwezi mzima bila kula chips ili kuchangia ujenzi wa kanisa.

Alisema mbele ya umati kanisani hapo kuwa, kwa kipindi cha mwezi mzima ujao badala ya kutumia zaidi ya shilingi 700/= ambazo amekuwa mara nyingi akitumia kwa chakula cha mchana awapo kazini, sasa atatumia shilingi 200/= kununulia maziwa kwa ajili ya mlo huo.

Alisema kiasi kinachosalia atakuwa akikitunza kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa kanisa la Moravian la Keko na akawataka waige mfano huo ili kukamilisha ujenzi wa kanisa lao bila kutegemea misaada ya wafadhili

Ujenzi wa jengo la kanisa la Moravian, usharika wa Keko lenye ghorofa mbili linalotarajiwa pia kuwa na shule ya chekechea, hospitali na ofisi ya mchungaji, ulianza mwaka 1996 na umekwisha gharimu zaidi ya milioni 25 kati ya 100 zinazohitajika.

Mkristo anayeshiriki ushirikina ni kama ua lisilopata maji-Paroko

Na Leocardia Moswery

PADRE mmoja Mkatoliki, ameifanananisha hali ya baadhi ya Wakristo kushindwa kuupokea mwili wa Bwana Yesu na kushiriki imani za ushirikina kama mwili uliokufa na kusinyaa mithili ya ua lililokosa maji likanyauka.

Padre huyo Andrew Komba ambaye ni paroko katika Kanisa la Mt. Fransisca wa X savery Chang’ombe katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika ibada ya Jumapili iliyopita kanisani kwake.

Aliitaka jamii kuachana na imani za kishirikina kwa kuendekeza masuala ya waganga wa kienyeji ambao huwadanganya kwa kuwapa mizizi ya migomba kwa madai kuwa ni dawa huku wakiwapigia ramli kwani huko ni kuwachanganya na kuwalaghai kwa lengo la kuwaibia mali zao.

Akihimiza umuhimu wa kuachana na dhana hizo potofu na badala yake kuyashirikisha maisha ya wanadamu na Mungu kwa kupokea Ekaristi takatifu, Padre Komba alisema,

"Wewe umeacha kupokea mwili wa Bwana wetu Yesu Kristo unakwenda kwa waganga kutibu magonjwa ambayo hayapo na waganga wenyewe unajua kabisa kuwa wanachotaka ni kufaidi pesa yako unategemea nini, watakutafutia mizizi ya migomba na kukupatia wakikudanganya kuwa ni dawa."

"Achilia mbali kupewa hiyo mizizi ya migomba, kuna watu wengine ambao hudanganywa na waganga hao kuwa walete kuku mweupe atakayeweza kwenda sambamba na matibabu. Huyo kuku akiletwa tayari mganga amekuwa kaisha jipatia kitoweo. Hivi huyo kuku kwanini usimle wewe mwenyewe."

Hata hivyo Padre Komba alisema kuwa wapo waganga wa kweli ambao hutoa dawa za asili ambazo hutibu magonjwa kama ya kichwa, tumbo na mengineyo lakini hawa ukienda kwao wanakupa dawa palepale na wala hawakuambii usubiri kesho au lete kuku mweupe; mganga wa kweli anakupa dawa hapo hapo na huyu anatoa dawa za kawaida kama ya tumbo na kichwa, huyu siyo mganga wa kupotosha" alisema.

Wahimizwa kuanzisha jumuiya ndogondogo

Na Dalphina Rubyema

WAAMINI wa Kanisa Katoliki nchini wametakiwa kutilia maanani uanzishaji wa jumuiya ndogondogo mitaani kwao kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuimarisha na kujenga Kanisa nchini.

Changamoto hiyo ilitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Method Kilaini wakati akitoa Sakramenti ya Kipaimara kwenye Kanisa la Kristu Mfalme Tabata misa iliyofanyika Jumapili iliyopita kanisani hapo.

Mhashamu Kilaini alisema kuwa Wakristu wanapaswa kushikamani mitaani ambako kuna jumuiya kabla ya kujuika sehemu nyingine.

Alisema Kanisani ni sehemu ya maadhimisho ya mshikamano wa mtaani kupitia jumuiya ndogondogo ambapo huko wamechanganyika na madhehebu mengine.

Askofu huyo Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam alisifia jumuiko na mshikamano wa wakristu wa Tabata na maeneo ya jirani kwa kuweka nguvu zao pamoja hadi kuwezesha ujenzi wa kanisa la Parokia hiyo ambalo hivi sasa limefikia hatua za mwisho.

Askofu Kilaini pia alisifia Parokia hiyo kwa kuweza kufanikiwa kujenga shule ya Msingi ambayo inahadhi ya kimataifa inayojulikana kama ‘Christ The King".

Aliwataka vijana hao waliopata Sakramenti ya Kipaimara wawe viongozi wa ibada nyumbani kwao."Nawatuma mkaongoze ibada nyumbani kwenu bila woga wala kuona aibu" alisema.

Aliwaita vijana hao kuwa ni matawi madogo yaliyolishwa vema na yale makubwa ambao ni wazazi wa vinana hao na wametakiwa kuunga mkono jitihada hizo.

Kanisa la Kristu Mfalme Parokia ya Tabata linajengwa kwa nguvu za waamini wa eneo hilo na wahisani mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa misaada ya hali na mali kufanikisha ujenzi huo kufuatia lile la awali kushindwa kutosheleza mahitaji kutokana na ongezeko kubwa la waamini.