Makanisani Wiki hii

...Kuweni mkono wa Mungu - Wito

Na Agnes Bisake

WAKATI wa mahubiri yake Jumapili iliyopita katika parokia ya Makuburi iliyopo katika Jimbo Kuu katoliki la Dar-Es-Salaam ilipofikiwa na wageni ambao walikuwa maaskofu wakuu wanne kutoka Brazil, paroko wa Parokia hiyo, Padre Gerardo Derksen, alianza kusimulia hadithi.

Hadithi yenyewe ilikuwa ya kijiji kimoja huko Korea, nayo ilikuwa hivi "wanakijiji hao walijenga Kanisa zuri sana na kuweka sanamu ya Yesu Kristo. Wakati wa vita, sanamu hiyo ilivunjwa vunjwa na kubaki vipande vipande." Paroko alitulia kidogo huku waamini wakiwa na shauku ya kusikiliza zaidi uhondo wa hadithi hiyo.

Kisha akaendelea, "Waamini walipofika pale Kanisani na kukuta vipande vya sanamu hiyo, walisikitika sana na kuanza kuvikusanya ili wavirudishie vyote."

"Walifanikiwa kuviunganisha na kutengeneza sanamu tena lakini, mikono tu, ndiyo iliyopotea kabisa. Akajitokeza fundi mmoja akataka kutengeneza sanamu nyingine lakini, paroko wao akakataa na kusema kuwa Mungu hakutaka mikono ipatikane" alisema na kuongeza kuwa waamini hao wa Korea walibaki wanashangaa kuwa ni kwanini Mungu hakupenda mikono hiyoipatikane.

Ndipo paroko yule akawaambia kuwa lengo la Mungu kutaka sanamu ile ibaki bila mikono, ni kutaka kuwafanya waamini wao ndio wawe mikono yake badala ya ile iliyokosekana.

Kwa hiyo, kila muamini alipokuwa akifika Kanisani, akiona sanamu bila mkono, anajua kuwa yeye kama Mkristo, ana wajibu wa kutumika na kufanya kazi kama mkono wa Yesu.

Alisema wakatoliki wa Makuburi na kote duniani hawana budi kujitambua kuwa wao nao wana wajibu mkubwa wa kutumika kama mikono ya Mungu ilivyo muhimu.

Aliendelea kuwashukuru waamini hao kwa kuwa mkono wa Mungu kwa kujenga makanisa ya Makuburi na Kibangu ambapo Kibangu inatarajiwa kuwa parokia hivi karibuni.

Vilevile, walijenga shule ambayo iko tayari pale parokiani Makuburi na wanatarajia kujenga Makanisa mengine katika vigango vya Makoka, Nzasa na Kilungule, na ikiwezekana watajenga shule nyingine huko Makoka.

Aliendelea kusema kuwa Mungu hapendi tu watu kuwa na makanisa ya matofali, bali Kanisa la watu wa Mungu.

"Tujenge Makanisa katika familia zetu, katika jumuiya ndogo ndogo, tujijenge kiroho na kwa njia hiyo tutakuwa mkono wa Mungu. Lakini, wazazi, mtakuwaje mkono wa Mungu wakati watoto wenu hawajui kusali hata Ishara ya Msalaba na hawajasikia Neno la Mungu?" alihoji

Mungu anasema nendeni mkahubiri na tulichaguliwa Siku ya Ubatizo na tumeimarishwa na Roho Mtakatifu Siku ya Kipaimara. Lazima tuoneshe huruma na furaha ya Bwana wetu Yesu Kristo. Wajibu wetu ni kuwa mikono ya Yesu.

KKKT waambiwa wasiwe na huruma ya mamba

Peter Dominic

JAMII imetakiwa kuondokana na huruma ya mamba ambaye licha ya kutoa machozi ya huruma anapotaka kumkamata na kumuua mwanadamu, bado humkamata, kumuua, kumzamisha majini na hatimaye kumla.

"Kama unataka kujihesabia haki na huruma, lazima uwe na Yesu ndani yako yani uwe umekubali kabisa toka moyoni ili awe Mwokozi wako".

Mchungaji Noah Kipingu wa Kanisa la KKKT Usharika wa Temeke aliyasema haya wiki iliyopita katika ibada ya pili iliyofanyika kanisani hapo wakati akiwafafanulia waamini wa usharika huo juu ya haki na huruma namna yanavyoweza kumpeleka mtu pabaya endapo atayatumia vibaya.

Alisema, watu wengi licha ya kujidai wanampenda na kuomuonea huruma mtu kutokana na hali fulani anayokuwanayo katika mateso, bado hao hao wengine huwa na nia mbaya dhidi yake ingawa huwa hawataki wajulikane dhamira zao mbaya kama alivyo mamba.

hujihesabia haki kimakosa wakati mwingine hulitumia Jina Takatifu la Mungu wakilamba kidole na kupitisha katika mchanga, kisha kupitisha shingoni wakiapa na kusema "Haki ya Mungu" hali aliyoiita ni hatari kwani wanajiingiza katika mtego wa dhambi.

Mchungaji Kipingu alivikemea pia vitendo na vigezo vinavyotumia na wanasiasa kuwashawishi watu kuwapigia kura wakati wa uchaguzi kuwa wakati mwingine humsababishia mtu kuikosa haki yake kwa kurubuniwa na kuiuza kinyume na msimamo wake safi wa Ki- Mungu.

"Wanawarubuni wapiga kura na wakati huo wao wanajihesabia haki na mpiga kura anajihesabia haki. Wengine wanaapa tena wanasema kabisa Haki ya Mungu; wanafanya hivyo kuhalalisha uongo wao," alisema na kuongeza kuwa Mungu ni wa haki na siyo wa kuapia jina lake na kulichezea.

Alionya na kuongeza kuwa jamii haina budi kutoshawishika kuuza haki kwa kushawishiwa vibaya na wanasiasa hao ili kuipoteza haki kwa kuwachagua ingawa wengine hawafai kabisa.

Pamoja na mambo mengine Mchungaji Kipingu alikemea pia vitendo viovu vya kupokea na kutoa na kupokea rushwa ambavyo alisema vinapofusha macho na kutoa mwanya wa kumkosesha mtu haki yake.

Akifafanua juu ya jamii kujihesabia haki, alisema ni sawa na Maandiko ya Biblia ambapo kundi la watu lilimkuta mwanamke kahaba kila mtu akamtuhumu kwa vitendo vyake vya uzinzi lakini walipomfikisha kwa Yesu aliwaambia kuwa yule asiye na dhambi kati yao, awe wa kwanza kumpiga mawe lakini, wote walikimbia kwa vile tayari pamoja na kujiona hawana dhambi, dhamira za mioyo yao iliwashitaki wakaondoka hata bila ya kuaga.

Alitaka jamii ijitambue na kujiona kuwa ni wenye dhambi na hivyo hakuna anayepaswa kujiona asiye na dhambi akijihesabia haki bali, wamuombe Mungu awasamehe dhambi zao na kwamba wasimchukie mtu yeyote akiwamo anayezikana dhambi zake na kutubu.

KKKT Dar wafanya mashindano ya kwaya

Jenifer Aloyce Na Joyce Charles (DSJ)

VIJANA wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), Jumapili iliyopita katika kanisa la usharika wa Kariakoo, Dayosisi mashindano kabambe ya nyimbo na kwaya ya Tabata ikaongoza.

Mashindano hayo yanayoendelea Jumapili hii katika kanisa la usharika wa Ubungo jijini Dar-Es-Salaam, yalizihusisha kwaya tano za kutoka sehemu mbalimbali za jiji.

Lengo Kuu la mashindano haya, lilikuwa kumwinua na kumtukuza Bwana Yesu kwa njia ya nyimbo. Haya yalikuwa ni mashindano ya kijimbo ambapo washindi watatu waliopatikana, watashindana na washindi wengine watatu kutoka kila jimbo.

Katika mashindano hayo, kwaya hiyo ya Tabata iliongoza kwa kupata alama 260 kati ya 300 zilizokuwa zikipiganiwa na kila kwaya ikifuatiwa na Kipawa iliyozoa alama 256.7 kati ya 300.

Kwaya ya Buguruni ilipata alama 240.7, matumbi, alama 236.7, wakati hii ya Segerea ilipata alama 227.7

Mwalimu wa kikundi cha kwaya cha Tabata ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema mara baada ya matokeo hayo kuwa anafurahia ushindi huo kwa kuwa umetokana na msaada wa Mungu."Si mimi niliyesababisha kwaya yetu ishinde, bali ni Mungu mwenyewe kwa sababu hata ukifanya mazoezi namna gani, ni Mungu pekee ndiye anaeamua kwa kuwa ndiye anayeongoza na kuwezesha ushindi. Maksi 260 siyo mchezo; lakini kwa nguvu za Mungu zimepatikana," alisema.

Licha ya kwaya ya Tabata kushinda katika nyimbo, pia ilishinda kwa unadhifu ikifuatiwa na Kipawa, Buguruni, Matumbi na Segerea.Kwaya nyingine kati ya 18 zilizotarajiwa, hazikushiriki mashindano hayo kutokana na ukosefu wa pesa.

Baadhi ya vigezo vilivyotazamwa katika kumtafuta mshindi kwa jumla ya alama 300 ni pamoja na namna ya kuingia jukwaani, wimbo wa siku ambao ulikuwa KAA PAMOJA NASI KWA KUWA KUMEKUCHA, wimbo wa asili na matendo yaliyooneshwa katika wimbo huo.

Mengine ni matamshi ya maneno, ujumbe katika wimbo, namna kiongozi anavyomaliza wimbo, unadhifu na sare, na matumizi ya jukwaa.

Katika tukio jingine, Joyce Charles anaripoti kuwa Kwaya ya Pentekoste Holliness ya Manzese jijini Dar-Es-salaam, maarufu kwa jina la Ukombozi Kwaya,imeanza kuuza toleo lake la pili la kanda ya nyimbo iitwayo Mungu Awashangaza.

Baadhi ya waimbaji wa kwaya hiyo, Bi.Musa na Bi. Clement walisema kwa nyakati tofauti kuwa wanamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kutoa kanda hiyo yenye nyimbo nane.

Kutubu hakuhitaji suti, gauni jipya-Padre

Na Neema Dawson

WAKRISTO wameshauriwa kujiepusha na hali ya kukaa na dhambi kwa kuwa kutubu hakuhitaji kuwa na suti, gauni jipya wala gharama yoyote ya kiuchumi mbali na kujitakasa kiroho.

Padre Peter Shayo ambaye ni Mwalimu katika Semimari Kuu ya Mitume wa Yesu iliyopo Nairobi nchini aliyasema hayo alipokuwa akihubiri katika Kanisa Katoliki la Kawe katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Alisema watu wengi wamekuwa wakiogopa kutubu dhambi zao ili waweze waondolewe dhambi hali inayowafanya wengi kendelea kuishi katika hali ya dhambi hivyo kupata matatizo mbalimbali ya kimaisha.

"Sidhani kama ukitubu dhambi na kusamehe watu waliokukosea tena bila kutumia gharama yoyote ile wewe mwenyewe binafsi unayefanya hivyo hutapata amani na neema katika maisha, lazima sasa utakuwa na amani rohoni mwako" alisema.

Alisema Mungu alimuumba mwanadamu kwa mfano wake na hivyo watu wote bila kujali dini wala dhehebu hawana budi kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na si kuishi maisha ya dhambi.

"Tunao uwezo wa kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na si kuishi maisha ya dhambi kwani Mungu ametuchagua wanadamu wote kuwa watoto wake na tunatakiwa kutubu dhambi tulizonazo kwa kufanya hivyo tutapata mafanikio katika maisha".

Aliwasisitiza Wakristo kuteseka kwa ajili ya mambo yanayowapa mafanikio ya kimwili na kiroho badala ya kusumbukia ya anasa yasiyo na mafanikio yoyote mbali na kuchochea matatizo.

‘Vijana msipoepuka disko, anasa mtakwisha’

Na Leocardia Moswery

Mkurugenzi wa Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki wa Sekondari na Vyuo (TYCS), Taifa, Padre Lucas Mzuwanda, amesema ugonjwa wa ukimwi unazidi kuenea kwa kuwa jamii nyingi hazitaki kuwajibika na badala yake, zinahusudisha ulevi na anasa ukiwamo uchezaji wa disko.

Padre Mzuanda aliyasema hayo, hivi karibuni wakati akizungumza katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Alisema katika kipindi hiki cha Jubilei Kuu ya Mwaka 2000, jamii haina budi kujitambua kuwa ina umuhimu mkubwa katika kupambana na mambo yote yanayo hatarisha usalama wa mwanadamu kimwili na kiroho ukiwamo ugonjwa hatari wa ukimwi.

"Kila mtu hana budi kujiuliza nini alichofanya na amejitakasa vipi?" alisema na kuongeza, "Huu ni Mwaka wa kurudi ndani. Je, Wakristo mmerudi ndani ya Kristo? Hilo naliongea kwa uchungu sana, maana watu tunapenda starehe hatupendi kuwajibika na kila siku tunazika. Ulevi na madisko kwa wengine vimekuwa ndivyo imani, je, watoto wetu atawalea nani endapo tutajiachia namna hiyo?"

Padre Mzuanda aliongeza kusema kuwa, Wakristo na jamii nzima kwa kushirikiana na serikali, hawana budi kuupiga vita ugonjwa hatari wa ukimwi ambao huenezwa kwa kiasi kikubwa na vitendo vya zinaa na uasherati ambavyo pia ni kinyume na Amri ya Mungu isemayo USIZINI.

Alisema wazazi kwa kushirikiana na jamii nzima, hawana budi kuwaelimisha kwa uwazi na usahihi vijana juu ya njia za maambukizo, athari na namna ya kuepukana na ugonjwa huu.

Aliwaonya vijana kutokutumia anasa kama njia ya kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira na kazi nyingine kwa kuwa hali hiyo ndiyo inayowazidishia maangamizo na akasema vijana, Wakristo na serikali, hawana budi kushirikiana kuupiga vita ugonjwa huu.

Mhubiri wa KKKT ataka jamii isifanyiane udhalimu, unafiki

Na Getruda Madembwe

"Mungu hapendi uovu wala udhalimu, ndio maana hata Yusufu hakuwatendea uovu ndugu zake walipoenda Misri kutafuta chakula wengine hupenda kuwazia mabaya kwa lakini, hii ni tofauti na Mungu ambaye siku zote huwazia mema hata kama tumemkosea."

Hayo ni baadhi ya maneno yaliyosemwa wakati wa mahubiri ya Bi. Ninaeli Mnuo katika ibada iliyofanyika katika Usharika wa Kawe wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jumapili iliyopita.

Alisema katika maisha ya kila siku, Wakristo hawana budi kutenda haki kwa wanadamu wenzao bila kuwa na upendo wenye upendeleo wala ubaguzi na akaonya dhidi ya upendo wa kinafiki ambao alisema haumfikishi mtu katika meza ya Bwana.

Akitoa mfano wa kauli yake Bi. Mnuo alisema kuwa, "Hata Mungu mwenyewe kama angekuwa anatoa upendeleo kwa watu wachache eti kwa kuwa ndio watendao mema, basi kusingekuwa na mtu hata mmoja wa kwenda mbinguni," alisema.

Aliwataka waamini wa dhehebu hilo kutokuwa wepesi wa kutoa au kutangaza hukumu dhidi ya ndugu, jamaa na marafiki wanaowakosea na badala yake wakae kwa subira na matumaini ya kuombana radhi na kusameheana.

Bi. Mnuo ambaye ni Katibu wa Fellowship wa usharika huo, alimfananisha atendaye haki na huruma sawa na mti uliopo kando ya maji ambao hustawi na kutoa matunda mazuri.Aliwaonya wasiotaka kumtangaza Yesu Kristo na wale wasiotaka Ukristo wao ujulikane na akasema watu hawana budi kuepuka tabia hiyo kwa kuwa haimpendezi Mungu na ni unafiki dhidi ya Ukristo wao.

"Tunatakiwa tumtangaze huyu Yesu kwa watu wote na wala tusione aibu kuusifia Ukristo wetu kwa watu wote kwani tukiukataa Ukristo wetu Mungu hatapendezwa nasi" alisisitiza.

Wakati huo huo: Usharika wa Kawe umepata viongozi wapya wa Fellowship baada ya waliokuwapo kukataliwa kuongoza kutokana na misingi na muongozo wa KKKT.

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika kanisa hilo la Wanafellowship wa usharika huo, Bw. Lunyuliko Nyauringo amechaguliwa kuwa Mwenyekiti akisaidiwa na Bw. Joseph Mkini.

Habari zinasema, Bi. Ninaeli Mnuo alipewa nafasi ya ukatibu na Bi. Kimaro amepewa jukumu la kutunza hazina akisaidiwa na Bw. Ndoo. Bw. Nyauringo alisema kuwa wao kama viongozi wa Fellowship hawana budi kufanya kazi hiyo ya Utume wa Mungu kwa amani na upendo bila ya kuwashutumu au kuwalaumu viongozi waliotangulia.

Hivi karibuni kulikuwa na mgawanyiko wa wanafellowship hao baada ya kugundulika kuwa kazi walizokuwa wanazifanya hazikuwa za KKKT badala yake, zilikuwa chini ya New Life Crusade.