Makanisani Wiki hii

Mobitel zapigwa marufuku kanisani

lWenye imani duni wanazithamini kuliko Mungu

Na Leocardia Moswery

WAAMINI wa madhehebu mbalimbali wametakiwa kutoingia makanisani huku simu zao za mikononi (mobile phone) zikiwa wazi kwa kuwa zinaingilia na kuvuruga ibada.

Akizungumza katika ibada ya Jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Kurasini, katika dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Masenge katika mahubiri yake alisema waamini wamekuwa na tabia ya kuingia kanisani na simu huku wakiwa wameziacha wazi na inapotokea akapigiwa basi huleta usumbufu kwa waamini ambao huwa makini kusikiliza Neno la Mungu.

"Kwa kweli hii siyo tabia nzuri, kwa Mkristo kuja na mtandao wake huku akiwa ameuacha wazi! Unakuta mtu anapigiwa simu katikati ya ibada anainuka kwenda kuisikiliza, je, nani wa muhimu, Mungu ama huyo anayekupigia?’ alihoji.

Alisema pamoja na kuwapo kwa maendeleo ya Sayansi na teknolojia, lazima maeneo muhimu yakiwamo ya ibada yaheshimike na Wakristo ni watu ambao hawana budi kuwa mstari wa mbele kuzingatia na kuyaheshimu maeneo hayo.

"Wakristo wanapaswa kuiheshimu ibada kwa kufunga simu zao na kama mtu anaona anashindwa kufanya hivyo, mimi naona ni bora asiingie kanisani.

Hivi kama umekwenda kumwona Rais na unasimu yako mkononi ambayo umeiacha wazi kama kawaida yako ili upate mawasiliano, ukapigiwa simu je, utamwambia Mzee, samahani ngoja nisikilize simu?" Alihoji kwa mshangao.

Aliwataka waamini kuelewa kuwa Mungu ni mkubwa kuliko yote na kama wataingia katika nyumba za ibada, basi ni vema waziheshimu kuliko kitu kingine chochote.

Matumizi ya simu za mkononi yamekuwa kama onesho la ufahari kwa watu wengi wanaozitumia bila kujali wala kuheshimu unyeti wa mahali walipo na hali hiyo imekuwa kero kwa wengi kwa kuwa inavuruga utulivu na taratibu mbalimbali muhimu zikiwamo ibada na mikiutano mimgine.

Anayependa anasa, anapenda utumwa- Mchungaji Kiongozi

Na Elizabeth Steven

"MTU mwenye dhambi akirithishwa lulu la hazina, hukimbilia kivuli cha anasa ili aketi hapo na kutumia kwa uhuru bila huruma wala aibu. Wala hathubutu kutafuta kivuli cha uzima wa mbinguni kilichopotea kwake."

Hayo amesema Mchungaji Kiongozi, David Kipingu, wakati wa mahubiri aliyoyatoa Jumapili iliyopita katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), Usharika wa Magomeni jijini Dar-Es-Salaam.

Siku hiyo katika ibada ya kanisa hilo lililo katika dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji huyo Kiongozi aliyeshirikiana na Mchungaji Nathaniel Nduba, wa Ushirika wa Hananasif katika kuwashirikisha waamini katika Meza ya Bwana, alisema inashangaza mno mtu anapopata mali hata kwa njia isiyo halali, badala ya kujutia hali hiyo na kuitumia mali kwa kadri ya mapenzi ya Mungu, hukimbilia katika vitendo na maisha ya anasa ambavyo alisema ni hatari na kikwazo katika kuutafuta ufalme wa mbinguni.

Alisema jamii imekuwa ikimkosea Mungu kwa kufanya vitendo vya uhalifu kama wizi na ubadhilifu wa mali ya umma, dhuluma, na kisha kutumia mali hizo kufanyia vitendo vingine vinavyokwenda kinyume na makusudio na mipango ya Mungu.

Alisema wengi wa watu waovu wa namna hiyo, huwa mstari wa mbele katika kusikiliza na kuimba nyimbo za dini hasa wanapokuwa katika mazingira ya ulevi na anasa nyingine.

"Hata mali ya umma, ya urithi na dhuluma katika jamii, wanaichuma na kuitafunia katika kivuli cha anasa. Tena ili waburudike vizuri ndani ya anasa zao, huweza na hata wenyewe kuimba muziki wa dini". alisema na kuongeza kuwa hao hupendelea hasa kuimba kuwa, "Kila mtu atauchukua mzigo wake"

alisema lengo la kuupendelea wimbo huo ni ili mtu mwenye nia nzuri ya kuwashauri, asijisumbue kumuelekeza wala kumkosoa hali aliyosema inakwenda kinyume na makusudio ya Mungu ndani ya jamii na kwamba haina budi kukemewa na kila mwenye mapenzi mema asiye na tamaa wala moyo na mawazo ya anasa.

Mchungaji Kipingu ambaye alikuwa anahubiri juu ya mwana mpotevu alizidi kusema, "Mtu anapopata mali na kutoroka na mali; anaacha familia inakufa, watoto na wazazi wake hawana cha kula, wala kuvaa; lakini anaporudi nyumbani ndiye mwenye kusikika akiimba, MUNGU NI MKUBWA ANAPENDA WATU WAKE WOTE, "Sasa mbona unafanya kinyume na yeye?" alihoji.

Alisema dhambi ni matokeo ya kulewa uhuru na kwamba inapoheshimika kama utumwa, huondoa utu wa mtu, "Huondoa utu wa mtu na kumfanya kuwa mtumwa au mnyama; hupenda kula hata wanyama wengine".

Wakatoliki wa Mtakatifu Yosefu wapongezwa kwa kuchangia gari

Na Elizabeth Steven

Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yosefu lililopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, limewapongeza waamini wake kwa moyo wao ulioiwezesha kuchangia shilingi milioni 17 kwa ajili ya kununulia gari la kuwahudumia watoto wa shule ya awali iliyopo Keko jijini.

Akitoa matangazo katika kanisa la parokiani hapo Jumapili iliyopita, Mwenyekiti wa parokia hiyo, Bi. Olive Luena, alisema ingawa awali gari hilo aina ya Toyota Hilux Double Cabin lilikisiwa kugharimu shilingi milioni 15, hali halisi imeonesha kuwa kiasi kinachohitajika ni shilingi milioni 18.5/=.

Alisema kiasi hicho kinachohitajika kitahitajika ikiwa ni baada ya msamaha wa kodi na gharama nyingine za usajili. Kwa kawaida gharama za gari hilo bila msamaha sambamba na gharama za usajili ni shilingi milioni 25.

Bi. Luena aliwapongeza Wakatoliki hao kwa kuwa tangu kuanza kwa mchango huo hivi karibuni, tayari wamekwisha changisha jumla ya shilingi milioni 17 na kwamba sasa wanahitajika kukamilisha kiasi kilichobaki cha shilingi milioni 1.5

Amewataka waamini hao kujitahidi zaidi ili wakamilishe mchango huo ambapo uzinduzi wa gari hilo, unatarajiwa kuwa Agosti 15 ambayo itakuwa siku ya kupalizwa Bikira Maria.

Juhudi na moyo wa Wakatoliki wa parokia hiyo, hazina budi kuigwa na Wakristo wengine ili kujenga moyo wa kujitolea kuzisaidia Kanisa katika kufanikisha kazi ya kueneza Injili na hivyo, kutimiza wajibu wa utekelezaji wa mapenzi ya Mungu.

Hivi sasa Wakristo na Watanzania kwa ujumla, hawana budi kuona kuwa wanatumia michango yao ya hali na mali ili kuona kuwa wanajiletea maendeleo bila kutegemea misaada ya wafadhili kwa kuwa wakati wa kutegemea kusaidiwa kila kitu, umepita.

Wakati huo huo:Paroko Msaidizi wa Parokia Katoliki ya Makuburi jimboni Dar-Es-Salaam, Padre Erneus Mbahulila, amewashauri Wakristo kuacha utamaduni wa kuvaa na kutumia hirizi kama njia ya kukabiliana na matatizo.

Alitoa ushauri huo wakati akizungumza katika ibada ya Jumapili iliyopita parokiani hapo.

"Mtu anazaliwa, anapata Ubatizo, Komunio, Kipaimara; lakini cha kushangaza na kusikitisha, Padre anapopita kwenye jumuiya yake (Muamini), anakuta watoto wamevikwa hirizi mikononi na hata viuno vimejaa hirizi, huo ni utamaduni gani ?"

kwa kuwa unaua mwelekeo na imani ya ki-Mungu, na unarudisha nyuma maendeleo.

Amewataka vijana kukubali ushauri wanaopewa na walezi wao pasipo kupuuza kwani itawawasaidia kupambana na matatizo yanayowapata katika maisha yao.

"Vijana siku hizi hawakubali ushauri wa wazazi wao. watoto wamebadilika wamekuwa na viburi, wanadharau; hamna budi kuitoa miiba hiyo iliyojipandikiza mioyoni mwenu" alisema.

Padre awataka waamini wakubali kukosolewa

Na Peter Dominic

"JINA la Mungu ni kubwa linastahili kila aina ya heshima, tunaliheshimu, tunapotaka kuabudu tunalifukuzia ubani lakini tunashindwa kulitafakari Neno lake na hapo ndipo tunaisaliti Katiba yetu".

Hayo yalisemwa na padre wa parokia ya Mtoni katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Padre John Waidrop wakati akiwahubiria waumini wa kanisa hilo katika ibada ya pili iliyofanyika Kanisani hapo juma liliyopita.

Alisema watu wamekuwa wakaidi kwa kutotaka kukosolewa wanapofanya maovu na pia hawataki kulipokea Neno la Mungu kwa kulitafakari badala yake huwageuzia watumishi wa Mungu kwa kuwashambulia eti wanachanganya dini na siasa.

Padre huyo alisema, jamii inafurahi pale mtumishi wa Mungu anapotoa huduma za uponyaji na nyinginezo nzuri lakini, anapokemea matendo maovu ya utoaji na upokeaji rushwa na wizi huja juu kwa madai kuwa amesahau wajibu wake na kwamba hivyo, anachanganya dini na siasa.

"Hapa tunaisaliti katiba yetu wenyewe," alisema.

Alisema jamii nyingi haitaki kuelezwa ukweli wala kukosolewa na badala yake, humkaripia na kumpaka matope yule anayehubiri au kusema waziwazi juu ya jambo linalokwenda kinyume au kukiuka maadili na majukumu kwa kuwa huwagusa na huwahukumu.

"Sitaacha kuwagusa watu wanaokwenda kinyume na maagizo ya Mungu, kwa kuwa hii ni kazi yangu ya unabii niliyotumwa kuifanya," alisema.

Padre John alisema Neno la Mungu halijali kabila au rangi ya mtu maana mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu kwa Neno lake na akatufanya taifa moja, akasema hali hiyo ndiyo inayomfanya binadamu asiishi kwa mkate pekee.

Hata hivyo alifafanua kuwa kila Mkristo yeyote aliyeamini na kubatizwa amepewa unabii hivyo inampasa kuwajibika kutenda kazi ya Mungu.

Rais wa Kilutheri afananisha makanisa yasiyofaa na vyama vyenye uchu wa ruzuku

Na Getrude Madembwe

RAIS wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, nchini Cameroon, Joseph Busheke, amesema Kanisa lisilowaita waamini kubadili maisha yasiyofaa na kumrudia Mungu ni sawa na chama cha siasa kinachohitaji watu wajiunge nacho ingawa hakipo tayari kuwasaidia hadi kitakapopata ruzuku, badala yake, kinawakimbia.

Alisema hayo wakati akifunga mkutano wa EUM uliofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Kawe.

Alisema kila kanisa lina wajibu wa kuwapeleka watu kwa Mungu ili wapate kuingia ufalme wa mbinguni na wala sio kuwaangamiza.

"makanisa yote ulimwenguni, hayana budi kuwapeleka watu kwa Mungu na wala sio kuwaacha na kuwafanya kuwa chanzo cha matatizo. Iwapo kutakuwa na kanisa lolote lenye lengo la kuwaangamiza wanadamu au kuwa mradi kwa ajili ya watu wachache hilo litakuwa siyo kanisa badala yake, kitakuwa ni kama chama cha siasa chenye malengo ya kujinufaisha chenyewe bila kujali watu wengine waliomo katika chama hicho," alisema.

Aliwataka Wakristo, wapewe mafundisho ya mara kwa mara kwa kuwa Ubatizo pekee hautoshi. Mafunzo hayo hayana budi kuwafanya wawe manabii kwa watu kwani hata Yesu mwenyewe aliagiza watu wafanywe kuwa wanafunzi wake; wakibatizwa kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, tena wakifundishwa aliyoagiza.

Rais huyo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini Cameroon, alisema kazi ya kuhubiri Injili ni ya watu wote na haistahili kuwaachia wachungaji, wainjilisti na maaskofu pekee.

Naye Bw. Busheke ambaye alikuwa ni miongoni mwa wajumbe kutoka katika nchi wanachama wa EUM, aliwahimiza viongozi wa dini zote kuhubiri Injili bila woga.