Makanisani Wiki hii

Wanawake walaumiwa kwa kuthamini kanga kuliko Mungu

Na Mwandishi Wetu

"WAKINAMAMA wengine mmemuweka Mungu kando, mnapenda na kuthamini mno kanga kuliko hata Mungu. Inafikia hatua mama amefua kanga na kuzianika; mwingine amaamua kukaa amezitumbulia macho hata anataka mara kwa mara akaigeuze.

Lakini ukiangalia uzito anaomtolea Mungu, huwezi kuamini."

Amesema Mchungaji Philipo Baji wakati akizungumza katika ibada ya Jumapili iliyopita katika kanisa la Anglikana Dayosisi ya dar-Es-Salaam, katika usharika wa Tabata.

Alisema wanawake hawana budi kuachana na kasumba mbaya iliyojitokeza na kushamiri miongoni mwao ya kuthamini mavazi hususani kanga kuliko Mungu ambaye sasa huamua kumuweka kando hali ambayo ni hatari kwa kuwa inawakosesha nafasi ya kuonesha upendo wao kwa Mungu .

Alisema hiyo ni hatari zaidi hasa kwa kuwa kinyume na ukweli wa hali halisi, wanashindwa kujua kuwa hali hiyo ni kikwazo kwao kufikia mafanikio mengi kadri wanavyokusudia.

"Mtu anaithamini kanga kiasi kwamba hata kama bado mbichi, anaamua kuinyoosha na kuiweka sandukuni; tena chini kabisa. Kwanini usimtangulize Mungu na kumpa walau heshima ya namna hiyo kuliko kumuweka kando na kuanza kutumikia kanga?" alihoji.

WAKATI HUO HUO: Mchungaji Baji, ameilaani vikali tabia ya baadhi ya akina baba kuona aibu kubeba Vitabu Vitakatifu ikiwamo Biblia wakati wa kwenda au kutoka katika maeneo ya ibada na badala yake, wanaamua kuwabebesha watoto wadogo ambao hata hawajui umuhimu wa kuvitunza na kuvibeba kwa uangalifu.

Alisema tabia hiyo ni ya unafiki na kamwe haimpendezi Mungu wala wacha mungu wengine.

"Akinababa mnaogopa kubeba Biblia na hata wengine akibeba kidogo, eti inafikia mahala anaona aibu na kumtwisha mtoto eti kwa kuwa wewe baba unaona aibu.

Kwanini lakini? Usidharau Ukristo wako; tabia hiyo haimpendezi Mungu. Tunapokwenda katika safari zetu, tujihoji kama tayari tumekwisha kuwa wateule wake," alisisistiza. Pia amewataka vijana kujitokeza kwa wingi na bila aibu katika kufanya na kumtumikia Mungu na mambo anayotaka ikiwa ni pamoja na kusali, kumuimbia.

Aliwataka vijana watue mizigo yao inayowalemea ambayo ni dhambi ikiwa ni pamoja na uvivu na aibu katika kumtumikia Mungu.

50 wakimbia kanisa kukwepa mchango

Na Mwandishi Wetu

ZAIDI ya waamini 50 wa Kanisa la Moravian Tanzania Ushirika wa Keko, Jimbo la Kusini katika wilaya ya Mashariki, wameishangaza jamii baada ya kukimbia kanisa lao na kuhamia mengine ya jirani kwa kukwepa jukumu linalowakabili la kukamilisha ujenzi wa kanisa lao.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa pamoja kanisa kwao jijini, Mchungaji wa ushirika huo wa Keko, Salatieli Mwakamyanda na Kiongozi wa Uwakili wa kanisa hilo, Bw. Obedi Kamendu, walisema kwa pamoja katikati ya juma kuwa wanashangazwa na imani duni ya waamini kukwepa jukumu lao la ujenzi wa kanisa lao na badala yake kuwa wakimbizi katika makanisa mengine.

Walisema kwa Mkristo mwenye imani sahihi, ni aibu kuwa mkimbizi kwa kuogopa majukumu ndani ya kanisa lako.

Viongozi hao wa kanisa hilo walisema awali takwimu zilionesha kuwa mahudhurio ya watu wakubwa wenye uwezo wa kuchangia, zilionesha walikuwa 120 na sasa wamebaki wasiozidi 70 ambapo wengine sasa wamelazimika kuhamia madhehebu mengine na sio kwa imani ya mafundisho, bali kwa kukwepa majukumu.

"Kuna Wakristo ambao wameacha kuja kusali na wengine wamediriki kuhamia hata makanisa mengine eti kwa kuwa kila siku mchungaji anasisitiza ujenzi wa kanisa.Watu kama hao wanalichezea tu, jina la Mungu na hawana mapenzi ya kweli kwake maana wanapenda penye miteremko tu

Mimi kwa kuwa ninafanya kwa ajili ya nyumba ya Mungu ili Wakristo wapate mahali pa kuchapia Injili, sitaacha kusema mpaka tumalize kazi hiyo kwa kuwa ni yetu wenyewe." alisema Mchungaji Mwakamyanda.

Naye Bw. Kamendu alisema, "Ujenzi wa kanisa letu ni vita tumeamua kupigana, hakuna haja ya kukimbia. Hivi huo ni ushujaa kweli katika kazi ya Mungu? Je, huko nako wakianzisha ujenzi hawa watafanyaje, au watahamia tena katika makanisa mengine!" alisema kwa mshangao.

Aliwataka wanajamii wenye mapenzi mema na wafadhili wa ndani na nje ya kanisa, kujitolea ili kusaidia ujenzi huo ambao umebakia sehemu kidogo ili kukamilika.

Viongozi hao wa kanisa hilo la Moravian Keko, walisema wanatarajia kuanza kutumia jengo la kanisa lao mwezi Septemba mwaka huu na kwamba kiasi cha shilingi milioni saba kinahitajika haraka ili uwepo uwezekano wa kusali kanisani hapo wakati juhudi za kukamilisha ujenzi zikiendelea.

Hivi sasa Wamoravian hao wanatumia jengo la kanisa jirani la Wapentekoste wa Parishi ya Keko Machungwa na huanza ibada zao kila siku saa 12:00 hadi saa 3:30 asubuhi ambapo huwapisha wenyeji wao.

Ujenzi wa kanisa la Moravian tangu awali, ulihitaji kiasi cha jumla ya shilingi milioni 100/= ambazo zilitakiwa kutoka kwa waamini wenyewe kwa michango yao ya hali na mali.

Wanawashukuru Wapentekoste kwa kuwahifadhi kwa upendo na uvumilivu na kusema kuwa makanisa yote hayana budi kujenga ushirikiano na uhusianao mzuri kama huo kwa kuwa wote ni ndugu katika Kristo.

Msikatae wito - K.K.K.T

Na Mwandishi Wetu

WAKRISTO kote nchini wametakiwa kutokataa kupokea wito pindi wanapoitwa na Bwana Yesu Kristo ili wamtumikie bila kutoa visingizio.

Ushauri huo ulitolewa na Kanali E.S Mvuoni kwenye mahubiri yake aliyoyatoa katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Kawe Jumapili iliyopita.

Alisema Bwana Yesu Kristo anawaita watu kwa maneno mepesi na yenye kueleweka hivyo jamii haina budi kumgeukia ingawa sasa hali ni kinyume na matarajio yake kwakuwa haiitikii na badala yake, watu wengi wanatoa visingizio.

"Tumekuwa ni watu wa kutoa visingizio pindi tunapoitwa na Yesu kwani yeye hutuita kwa maneno mepesi na yenye kueleweka lakini kinyume chake tumekuwa hatuitikii wito huo na tunaweka visingizio, "alisema na kuongeza,

"Tunapoitwa na Yesu ili tuyaache yaliyo mabaya au kumtumikia yeye huwa tunasema kuwa tuna kazi nyingi au tunauguliwa hivyo basi tunajikosesha nafasi ya kumtumikia."Aliwashauri waamini hao kuachana na tabia hiyo ya kutoa visingizio,

Alitoa mfano wa Yesu Kristo ambaye aliwaasa wafuasi wake waliokuwa wanataka kumtumikia Mungu lakini walikuwa na visingizio vingi (Luka. 9:62), unasema kuwa Yesu akamwambia, mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma hafai kwa ufalme wa Mungu Alisema kuwa kuacha au kutekeleza nusunusu mambo ambayo yanampendeza Mungu ni dhambi zitakazowafanya waishie motoni.

WAKATI HUO HUO: Kanali huyo amewashauri wanandoa kuwa imara katika ndoa zao ili waepukane na kuwa na mwanamke au mwanaume mwingine nje ya ndoa yao kwa kuwa kufanya hivyo ni kuenenda kinyume na taratibu za ndoa.

"Mtu ataachana na wazazi wake na ataandamana na mkewe nao watakuwa mwili mmoja sasa kwa nini uwe na mwanamke mwingine au mwanamme mwingine wa pembeni"alihoji Kanali Mvuoni.

Wakatoliki Mbagala wahitaji milioni 6/=

Na Mwandishi Wetu

ZAIDI ya shilingi milioni sita, bado zinahitajika ili kufanikisha ujenzi wa Kituo cha Hija na Kigango cha Kanisa Katoliki eneo la Misheni Msalabani katika Parokia ya Mbagala, Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam.

Mwenyekiti wa Parokia hiyo Bw. Emil Hagamu, ameliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa shilingi 780,000/= kati ya milioni 7 zinazohitajika, tayari zimekwisha patikana kutokana na michango toka kwa waamini na wahisani mbalimbali ikiwemo mitaa mbalimbali ya kanisa parokiani hapo.

Ingawa aliwasifu wachangiaji kwa juhudi na moyo wao wa kujitolea kufanikisha shughuli hiyo kwa ajili ya kazi ya Mungu, alisema bado wanayo kazi kubwa na muhimu ya kukamilisha mahitaji yanayopungua ili kufikia lengo lao.

Katika sherehe za Jubilei Kuu ya Mwaka 2000, zilizofanyika parokiani hapo hivi karibuni, zaidi ya shilingi laki 4, zilichangwa kupitia mitaa mbalimbali ya Kanisa sambamba na matoleo mbalimbali ya waamini ambayo yalikusudiwa kuuzwa kwa njia ya mnada.

Kwa njia hiyo ya uchangiaji, kila mtaa ulikusudiwa kuchanga kiasi kisichopungua shilingi 20,000/=.hata hivyo, katika zoezi hilo, muitikio ulikuwa wa kufurahisha zaidi.

Hagamu amewataka waamini wa parokia hiyo kuendeleza moyo wao wa kujitolea kwa juhudi, uaminifu na upendo katika kuifanya kazi ya Bwana.

Hata hivyo katika ibada ya Jumapili iliyopita, Hagamu aliwasisitiza wahisani, wachangishaji na waamini wa mitaa ambayo haijakamilisha uchangiaji, kuiga mfano wa wengine waliokamilisha mapema ili kufanikisha shughuli hiyo kwa wakati uliokusudiwa.

Mbali na michango kupitia kwa wahisani na mitaa ya Kanisa, parokia ya Mbagala imeandaa na kugawa fomu 50, zenye majina 60 kila moja ili wahisani wachangie walau kila jina kwa shilingi 1000/=.

Amewaomba Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kujitolea kusaidia kuchangia ujenzi huo kwa njia hiyo ya fomu au moja kwa moja parokiani.

Hagamu amewasisitiza wanajamii kuwa kutoa ni moyo na kuwa katika kazi ya Mungu, hakuna sababu ya kuwa na tofauti zozote kwa kuwa Mungu ni mmoja.

Wanaume walaumiwa kwa kutowapenda watoto

Na Mwandishi Wetu

MLEZI wa nyumba ya Watawa wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Padre Castary Msemwa, amewashutumu wanaume wengi wa Kiafrika kwa kuwa hawaoneshi mapendo sahihi kwa watoto wao na badala yake, wanawapa mapendo nusunusu.

Akiongoza ibada katika sherehe za maadhimisho ya Moyo Mtakatifu wa Yesu zilizofanyika mwishoni mwa juma lililopita, katika kanisa la Baraza la Maskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Msemwa alisema, wanaume wengi wa Kiafrika wamekuwa dhaifu katika kuonesha upendo kwa watoto wao tofauti na ilivyo kwa wanawake ambao humfurahia mtoto hata tangia hatua zake za awali za kuanza kujifunza kutembea.

"Sisi wanaume hatuoneshi upendo kwa watoto wetu, tunachokifanya ni kuitikia tu, hii ni tofauti na wanawake; wao wanawafuatilia watoto wao kwa karibu nao na kuwaonesha upendo wao kwa waziwazi tangu mtoto anapoanza kunyanyua miguu na kadri anavyozidi kukua na mapenzi yananaongezeka.

Alisema katika maisha ya kawaida ya wanadamu, hakuna mwenye haki ya kuambiwa au kuoneshwa kuwa anachukiwa na kinyume chake, kila mmoja anayo haki ya kupendwa.

Aliwataka wanaume kutokuwa wachoyo wa kuonesha upendo katika familia zao.

"Mke wako ameugua lazima umpe huduma, sio lazima kila kitu utumie watoto kumhudumia; mbona nyie akina baba mkiwa mnaumwa huwa hampendi kuhudumiwa na watoto na badala yake mnajisikia vizuri mkihudumiwa na wake zenu? Na wenyewe wanataka hivyo." Alisema.

WAKATI HUO HUO: Sista Regina wa Shirika la Dada Wadogo Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, amewataka Wakristo kutozidharau jumuiya ndogondogo za kanisa kwa kuwa zina mchango mkubwa katika kuimarisha amani, upendo na uelewano katika familia.aliyasema hayo wakati akizungumza katika ibadailiyofanyika nyumbani kwa muamini mmoja wa maeneo ya Mbagala, Mama Magdalena, mwishoni mwa wiki.

GRC lawataka wanajamii kuwa watii

Na Mwandishi Wetu

KANISA la The Gospel Revival Centre (GRC), limewataka Watanzania kujenga na kuimarisha utamaduni sahihi wa utii kwa viongozi wote ikiwa ni njia mojawap ya njia za kuepuka machafuko yasiyo ya lazima.

Mwenyekiti wa GRC ngazi ya kitaifa, Mchungaji George Kilango, aliliambia KIONGOZI mara baada ya ibada ya Jumapili iliyofanyika katika kanisa la Kurasini jijini Dar- Es- Salaam, kuwa waamini hawana budi kuwa na utii kwa viongozi wao wote; wa dini na wale wa serikali kwa kuwa viongozi hao wamewekwa na Mungu.

"Washirika wa dini zote lazima wajenge utamaduni wa kumpendeza Mungu kwa kuwa watiifu, wanyenyekevu na wenye mapendo kwa viongozi wao. Wawe na mapenzi na utii kwa Mungu na viongozi wao kwa kuwa unapomtii kiongozi, umemtii na Kristo kwa kuwa ndiye aliyemuweka." Alisema Mchungaji Kilango na kuongeza,

"Mshirika awe msikilizaji na mtendaji wa mafundisho au maagizo anayoyopata toka kwa kiongozi wake."

Alisema ingawa katika makanisa yote wapo baadhi ya waamini waadilifu, ipo haja kwao kulisaidia kanisa katika kuwabadili wenye mienendo mibaya ili nao wapate kumtumikia Mungu kwa usahihi

"kama ilivyo katika mashamba ya ngano, lazima makanisani nako kuna magugu; hakuwezi kukosekana magugu ambayo yana lengo kuvuruga kazi za Mungu. " alisema

Alisema inashangaza kuona miongoni mwa wana jamii, wapo watu ambao pindi wanapokosea, badala ya kuomba radhi na kutubu ili wapate utakaso, huwa msitari wa mbele, kulaumu kwa madai kuwa wao ndio wanaonewa na kuanza kueneza shutuma dhidi ya viongozi wao wasio na kosa.

"Mungu anasema heshimu na kuwatii viongozi wao; ukosefu wa utii kwa viongozi ndicho chanzo cha machafuko katika nchi zote duniani." Badala ya kukalia kulalamika na kuzua uvumi dhidi ya viongozi wao, waamini wa madhehebu yote kidini, kuwaombea viongozi wao ili wawe na hekima ya ki-Mungu ili kuongoza jamii kwa amani.

Waombeni radhi mliowakosea - Ushauri

Na Mwandishi Wetu

WAKRISTO wametakiwa kujijengea utamaduni wa kukubali na kuomba radhi kwa wanaowakosea ili kurudisha mahusiano mema baina yao badala ya kuishia kuungama tu kwa Mungu.

Ushauri huo umetolewa na Padre Yuda wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Kawe alipokuwa akizungumza katika ibada iliyofanyika kanisani hapo hivi karinbuni ambapo alisema kuungama pekee mbele za Mungu endapo hauna mahusiano mazuri na binadamu wenzako unaoishi, ni kazi bure kwa kuwa Mungu hapendezwi na hali hiyo.

"Kuna Wakristo hawataki kuomba radhi wanapokosea kwa mtu. Wengine wanajirundikia mizigo ya dhambi kwa kuishi bila kuungana ili waweze kupunguziwa mizigo mingi waliyo nayo".

"Ungameni mara kwa mara ili mioyo yenu iweze kufanana na Moyo Mtakatifu wa Yesu na si kuungama mara moja kwa mwaka," alisema Padre Yuda.

Padre alisema kuwa kurudisha Upendo wa Yesu ni kutenda yote yaliyo mema mbele ya Mungu na wanadamu kwani Upendo hauwezi kurudishwa kwa Mungu bila ya kupendana sisi kwa sisi na bila ya kupenda wale walio katika hali ya juu kimaisha na wenye uwezo na kuwachukia wale wenye hali duni.

"Mtu anaomba msamaha kwa yule aliyemkosea kwa kumuangalia hali yake ya kimaisha na kuona kuwa nisipo muomba msamaha na hivi ninaelewana naye siku nyingine ataacha kunisaidia na kunidharau aliye na hali ya chini kimaisha"

Aliwasisitiza Wakristo wote kuvumilia mabaya ili kukabili hali ya kuteseka na kuumia kwa ajili ya watu walio na shida mbalimbali ili waweze kupata thawabu mbele za Mungu.