Hatuombi msamaha kwa kuwa ni machangudoa, majambazi - Paroko

Na Peter Dominic

"Tunasema Eloi Eloi, Lama Sabaktani baada ya nusu saa tunaungana katika dhambi kumsulubisha Yesu Kristo katika dhambi zetu tunapotamka neno hili lenye tafsiri ‘mbona Mungu unaniacha tusilichukulie kama mzaha wala igizo ...

Tunaposema kukosa na kuomba msamaha isichukuliwe kwamba ni machangudoa, wala majambazi na wabakaji, sisi ni wa kawaida ila tunalazimika kuomba msamaha kwa ajili ya wote waliotenda na wanaotenda dhambi".

Hayo yalisemwa na Paroko wa Parokia ya Mtoni katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam, Padre John katika ibada ya Jumapili ya Matawi.

Katika siku hii, Wakristo huikumbuka siku Yesu alipokaribia mji wa Yelusalem karibu na mlima wa Mizeituni ambapo umati uliokuwa ukimfuata ulitandaza nguo na matawi ya miti zikiwa zimebaki siku chache kuisherehekea sikukuu ya Pasaka Mt.21-1,21-8.

Alisema tatizo linalowakabili watu wengi ni kushindwa kukiri makosa kwa moyo wa dhati na kuomba msamaha kwa imani na matendo yao.

Aliyafananisha maneno hayo na hukumu ya Pilato kwa kusema kuwa kama makutano wangesema Yesu asisulubiwe huenda anageachiwa huru, lakini wote walipaza sauti wakisema asulubiwe .

aliongeza kuwa kuitikia kwa umati huo ndiko kulikopelekea dhambi hiyo isambae ulimwengu mzima na ndiyo inayotupelekea kuomba msamaha kabla na baada ya kutenda kosa.

Aliendelea kusema kuwa inapotokea mtu mmoja akatenda dhambi ya kuiba ni sawa na kumwambia Pilato amsulubishe Yesu msalabani na akaonya kuwa kwa Mungu hakuna dhambi ndogo.

"Ili kutambua umuhimu wa kurejea kwa Mungu na kuomba atusamehe, isitafrike kwamba dhambi aliyoitenda fulani si yako bali tuungane pamoja ili tulete ukombozi hapa ulimwenguni".

Msiuonee haya Ukimwi - Kauli

JAMII imetakiwa kuupiga vita ugonjwa wa ukimwi na kuuchukulia kama magonjwa mengine na hivyo kuepukana na tabia ya kuunea haya wala kuuficha.

Akizungumza katika Ibada ya Jumapili ya Sita ya mfungo wa Kwaresma, Paroko wa Kanisa la Angalikana katika parokia ya Mtaa wa Watakatifu Wote, Temeke, Padre Nathaeli J. Kipalamoto, alisema ugonjwa wa ukimwi ni kama malaria ama maradhi ya tumbo na akawataka kuacha tabia ya kuficha ugonjwa huo na kuuonea aibu.

"Wakristu, Wazazi na watu wa madhehebu mengine wanapaswa kuona ugonjwa wa ukimwi kama malaria na kuwaelimisha vijana bila kuwaficha,"alisema Paroko Kipalamoto.

Alisema Wazazi wamekuwa wakiwaficha vijana wao ugonjwa huu wanaouona kama ugonjwa wa aibu wakati huo ni ugonjwa wa kawaida kama magonjwa mengine na unaohitaji tahadhari kubwa na uwazi ili kuepuka maambukizo kwa kuwa hadi sasa hauna kinga wala tiba.

Aliongeza kuwa kitendo cha kuuficha ugonjwa huu hata bali inapoonekana wazi kuwa ndio, kimechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maambukizo.

Baadhi ya wanajamiii wamekuwa wakiwatenga na kuwapa huduma duni wagonjwa wa ukimwi.

Padre Kipalamoto, alisema kuwa Jumapili hii ni Wiki Takatifu ambapo Wakristo kote ulimwenguni wanasherekea Sikukuu ya Pasaka kama ishara kukumbuka mateso, kifo na hatimaye kufufuka kwa Mkombozi Wetu Yesu kristo.

Alisema katika kipindi hiki Wakristo kote duniani hawaa budi kujipima maisha na matendo yao na kutubu na kuacha kabisa matendo maovu.

Wakati huo huo. Umoja wa Wanawake Wakristo {UMAKI} umeanzisha mradi wa kufuga kuku wa nyama na mayai pamoja na kuanzisha bustani ya mboga za majani.

Umoja huo umewaomba wahisani wa ndani na nje ya nchi wenye mapenzi mema kujitokeza kufadhili chama chao ili kikue na kujiimarisha mapema.

UVIKIKEDA, kufyatua nyimbo Arusha,

lTEC nao kurekodi TVT

UMOJA wa Vijana wa Kikristo wa Keko Dar Es Salaam (UVIKIKEDA), Jumapili hii unatarajia kufanya tamasha la michezo mbalimbali ikiwemo ya kuigiza na kuimba ili kuchangia safari ya kikundi hicho kwenda Arusha kurekodi nyimbo na kufanya shughuli za uinjilishaji ambapo shilingi 500,000/= zinahitajika; anaripoti Josephs Sabinus.

Kwa mujibu wa Katibu wa UVIKIKEDA, Bw. Elineema Massawe, baadhi ya vikundi vitakavyoshiriki tamasha hilo katika michezo mbalimbali ni pamoja na,Vijana KANA cha Tanga, Ifata Choir ya Kariakoo, Vijana, AVC Band ya Ilala na Kikundi maalumu cha kuigiza cha Watoto wa K.K.K.T usharika wa Keko.

Alisema katika safari yao ya vijana 40 kuanzia Mei 5 hadi 8, watarekodi kanda yao ya tatu katika studio za Redio Habari Maalumu ya mjini Arusha na kwamba Kanda hiyo itaitwa Nitayainua Macho Yangu na akadokeza kuwa sababu ya kurekodi katika studio hiyo ya RHM, ni kuwa na mkataba nao juu ya utafutaji wa masoko ya kanda hiyo ndani na nje ya nchi. Albamu zao za awali ni Tanzania na Afrika.

Alizitaja nyimbo zitakazorekediwa katika albamu hiyo kuwa ni pamoja na Mjini Nazareti, Njooni Tumwimbie Bwana, Bwana Ndiwe Mlinzi Wangu, Safari ya Mbinguni, Mle Kaburini na Mumgu Baba Aliupenda Ulimwengu.

Bw. Massawe aliwataja baadhi ya viongozi watakaokuwa katika ziara hiyo sambamba na uinjilisti katika kanisa la K.K.K.T, usharika wa Kimandolo, kuwa ni Mwenyekiti wa Kikundi, Bw. Edwin Kimaro, Makamu wa Mwenyekiti, Godfrey Ezekiel, katibu Msaidizi, Remmy Dizombe, Mtunza Hazina, Bi. Mary Sima, Msaidizi wake, Bi. Neema Masika na Mwalimu wa Uimbaji Bw. Stanley Kilasi.

Wakati huo huo:Kwaya ya Watakatifu Wote ya Kigango cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC) ya Kurasini jijini, inatarajia kurekodi nyimbo zake mpya katika Televisheni ya Taifa (TVT).

Kiongozi wa Kwaya hiyo Bw. Steven Msowoya na Makamu wake Bw. Bernard Peter walisema kwa pamoja kuwa nyimbo watakazo rekodi na baadaye kuuza kanda ni pamoja na ule usemao Mwana wa Mungu.

Hivi karibuni kwaya hiyo ilipata viongozi wapya ambapo Mwenyekiti wake ni Bw. Dismas Sambala, Makamu wake ni Bi. Janeth Dismas na Katibu ni Bro. Msungu wa TEC, wakati msaidizi wake ni Bi. Jane. Mweka hazia wa kikundi hicho ni Bi. Theresia, anaripoti Leocardia Moswery.

‘Ombeni Tanzania isigeuzwe kuwa Burundi, Kongo’

Na Mwandishi Wetu

WAKATI taifa linaelekea Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu, Kanisa la Moravian limewataka Watanzania kuuombea ili uwe wa haki , amani na huru ili kuliwezesha taifa kuwapata viongozi wanaofaa katika kuliletea maendeleo.

Mwenyekiti wa Wilaya ya Mashariki wa Kanisa la Moravian katika Jimbo la Kusini, Mchungaji Eli D. Ambukege, alisema katika Kanisa hilo usharika wa Keko Jumapili iliyopita kuwa ili kuwapata viongozi wanao weza kuifanya nchi yetu isigeuke na kuwa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,

Wananchi wa madhehebu na vikundi vyote vya dini havina budi kuuombea heri uchaguzi huo ufanyike kwa amani na utulivu.

"Ombeeni Uchaguzi ujao ili tupate viongozi wazuri wa kuiendeleza nchi na sio viongozi watakaotuchafulia wala kusababisha nchi yetu igeuke kuwa Burundi na Kongo." Alisema.Alisema kwa muda wa takribani miaka 40 sasa tangu uhuru Tanzania imepewa tunu ya kuwa katika amani hivyo ni jukumu la Watanzania kuona kuwa amani hiyo haipotei kamwe.

WAKATI HUO HUO: Katika ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na katibu wa Uwakili wa Kanisa hilo wilaya ya Mashariki, Yona Sonelo, Mwenyekiti huyo wa wilaya amewataka waamini wa kanisa lake kutotumia vyombo vya habari kama njia ya kutatua migogoro ndani ya makanisa yao bali watumie vyombo na ngazi husika katika makanisa hayo.

"Jambo dogo la ndani ya kanisa kulikimbiza kwenye magazeti sio ufumbuzi wa matatizo ndani ya kanisa bali hiyo ni njia ya kuchochea na kuongeza migogoro.

Ni vizuri Wakristo tukajenga tabia ya kutatua mambo ya kiimani ndani ya makanisa yetu." Alisema.

Mmenonite awataka Wakristo wasiwe ‘sura mbili’

Na Getruder Madembwe

WAKRISTO kote nchini wameshauriwa kutokuwa na sura mbili kwa kujificha katika dhambi huku wakijua kuwa wametenda madhambi, badala yake, watubu na kuziacha kabisa.

Ushauri huo ulitolewa juma lililopita na Mchungaji Abunieli Mathube wa Kanisa la Mennonite Tanzania, alipokuwa akihubiri katika kanisa hilo lililopo Upanga Jijini Dar-Es-Salaam Dayosisi ya Mashariki.

Alisema Wakristo wengi wamekuwa ni wepesi mno kutenda dhambi lakini hawako radhi kutubu makosa yao na kusema kuwa kamwe Mungu hapendezwi na hali ya kuwa Wakristo wa "sura mbili".

Akifafanua kauli hiyo, Mchungaji alisema kuwa sura ya kwanza ni pale wanapoonekana kuanzia siku za Jumatatu hadi Jumamosi ambapo ni vigumu na hawawezi kutambulika kama ni Wakristo kutokana na matendo yao maovu.

Alisema sura ya pili huonekana kwao katika siku za Jumapili ambapo wanakwenda makanisa huku wakionekana wema kwa masaa machache. Alisema Wakristo wa namna hiyo, wakitoka kanisani huendeleza chuki pamoja na matendo ambayo humchukiza Mungu.

Alipendekeza kuwa iwapo tunaona haya kuungama mbele za watu ni vyema tuungame makosa yetu kwa siri yaani kuwa na muda wa kuijifanyia toba mwenyewe bila ya mtu au watu kujua ila Mungu peke yake tu.

Akinukuu katika Injili ya Mathayo 6:5 isemayo, "Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia ili waonekane na watu. Amini nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao," alisema ni vema Wakristo wakajenga utamaduni wa kuungama mara kwa mara ili kupata upatanisho na Mungu.

Hata hivyo alisema ni vema Wakristo kwenda kwa viongozi wao kuungama ili wapate ushauri zaidi wa kiroho kuliko kukaa na nafsi iliyojaa mzigo wa dhambi kutoka na kuona haya kuungama mbele za watu.

Vile vile Mchungaji Mathube aliwataka Wakristo wote wabadilike hasa katika kipindi hiki tunapokumbuka mateso, kufa na kufufuka kwa Bwana Wetu Yesu Kristo.

Walezi wa Masista wapatiwa kozi

Na Fr. Raphael Kilimanga

WALEZI 34 wa mashirika ya masista Tanzania wapo katika kozi ya malezi ya masista iliyoanza Januari 28 na kuendelea hadi Oktoba 26, 2000 na kufanyika katika Makao ya Mapadre wa Damu Azizi yaliyoko Mlima Kola, mkoani Morogoro.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mama Wakuu wa Tanzania (RWSAT), Sista Fides Mahunja.

amesema mwishioni mwa juma ofisini kwake kuwa kozi hiyo ya mihula miwili tangu Januari 28 hadi Mei 26 na Julai 14 hadi Oktoba 26 inawakutanisha walezi wa mashirika 82 ya Umoja huo na inatoa mada juu ya malezi, maisha ya kitawa, maisha ya kiroho, saikolojia, ushauri na uongozi wa roho.

Mada nyingine ni pamoja na Maandiko Matakatifu, Teolojia, Liturujia na Sakramenti, uongozi na Uchumi.

Juu ya uchumi washiriki watajifunza pamoja na mambo mengine athari zinazoletwa na matatizo ya uchumi kitaifa mintarafu watoto wa mitaani, Ukimwi, uvutaji bangi, madawa ya kulevya, utoaji mimba na utoro mashuleni.

Aidha Katibu huyo amesema pia kuwa washiriki wa kozi hiyo wanatoka katika kanda zote za umoja huo ambazo ni pamoja na ya Ziwa, Kusini, Kati , Magharibi na Kaskazini.

Kozi hiyo inaendeshwa na wakufunzi wakuu Masista Judith Mahembe wa Wateresina Iringa, Martha Ngua wa Bibi Yetu wa Afrika - Sumbawanga na Tinie Holschen wa Msola.

Awali kozi za namna hiyo ziliendeshwa kwa nyakai tofauti kwa vipindi vya miezi mitatu mitatu.