Makanisani Wiki hii

'Viongozi Watanzania wasife kwa Ukimwi kama Wamalawi'

Na Neema Dawson

MCHUNGAJI mmoja wa Kianglikana amewahimiza viongozi wa dini waamini wao kimwili na kiroho ili kulinusuru taifa la Tanzania lisiwe kama nchi ya Malawi ambako viongozi wengi wa serikali wakiwamo wabunge wamekufa kwa ukimwi.

Mchungaji huyo Canon Mtokambali alisema hayo wakati akizungumza katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Nicholaus na Mashahidi wa Afrika lililopo jijini Dar-Es-salaam hivi karibuni.

Alisema kwa kuwa kazi ya Kanisa na viongozi wake ni kumtunza mwanadamu kimwili na kiroho, ni jukumu lao kukemea na kuonya ili kuokoa ambapo binadamu amepata matatizo bila kujali kuwa ni kiongozi wa serikali na kwamba ana cheo gani.

"Sisi tusiposema na kukemea uovu tunaweza kujikuta tukiwa kama nchi ya Malawi ambapo viongozi wake wengi wa serikali wakiwamo wabunge, wamekufa kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Hivyo, viongozi wa dini, ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda vizuri na endapo tutalifumbia macho tatizo hilo, tutakwisha ulimwengu mzima,"Alisema.

Akitolea mfano katika ulimwengu tunamoishi, Mtokambali alisema kuwa wabunge, mawaziri na viongozi wengine wa juu wa serikali, baadhi yao wamekuwa na tabia mbaya wanapokwenda bungeni na hata katika vikao mbalimbali nje na maeneo ya familia zao ambapo huko hujihusisha na vitendo viovu.

"Wengine wakifika huko, wanayakabidhi maisha yao kwa mambo ya kidunia. Mungu wanamuweka pembeni. Matokeo yake, wanaporudi nyumbani, ndipo wanamkumbuka Mungu na wakati huo tayari wanakuwa wamemalizika kiafya na maradhi ya ukimwi," alisema.

Alisema wenyewe hujiona kuwa wamefanikiwa kuzificha familia zao juu ya ukweli wa tabia zao mbaya lakini, husahau kuwa kwa Mungu hakuna kinachofichika.

Alisisitiza kuwa Wakristo wote wanatakiwa kuishi maisha matakatifu kila wakati na si kuishi kwa kupanga muda fulani uwe wa kuishi kwa kumtegemea Mungu hususani siku za Jumapili wakati nyingine wanaishi maisha ya kuwategemea wanadamu, shetani na mambo ya kidunia.

"Wakristo wengi wamejisahau mno. Wengine hawasomi vitabu vya watakatifu. Badala yake, wanasoma novel na vitabu vya kihunihuni. Inafaa Wakristo wasome vitabu vya Watakatifu ili kufahamu waliupataje utakatifu huo na pia, vitawasaidia kuishi maisha yaliyo matakatifu na kujengeka kiroho" alisema.

Watakiwa wasiwe Wakristo wa kuhubiri, kuimba pekee

Na Christopher Gamaina, Tarime

WAKRISTO nchini wametakiwa kuachana na tabia ya kuwa Wakristo wa kuimba na kuhubiri huku matendo yao ni kinyume kabisa na mapenzi ya Mungu.

Ushauri huo ulitolewa Jumamosi iliyopita na Mwenyekiti wa Mara Conference Bw. James Machage, alipokuwa akitoa mahubiri kwa washiriki wa ibada iliyoadhimishwa ndani ya kanisa hilo lililopo barabara ya Nyamwaga mjini Tarime.

Alisema ni wajibu wa Wakristo wote kupokea mioyo mipya ya kuishi kwa kadri ya mapenzi ya Mungu ili waweze kukabiliana kikamilifu na vishawishi dhidi ya shetani ambavyo vinaweza kuwazuia kuingia mbinguni.

"Inashagaza sana kuona baadhi ya watu mara baada ya kubatizwa, huacha baadhi ya tabia mbaya na kuhamia kwenye tabia nyingine mbaya, mfano mtu anaacha kuacha tabia yake ya kumpiga piga hovyo mke wake na sasa anabadilika na kuanza kumpiga mtoto akidhani kuwa labda uovu wake ulikuwa ni wa kumpiga mwanamke tu.

Wao wanaona kuwa kumpiga mtoto ni jambo zuri tu. Huu si Ukristo timilifu," alisema.

Bw. Machage aliongeza kuwa watu wote hawana budi kuachana na tabia ya kuonesha tabasamu mbele ya wenzao hali ndani ya mioyo yao wamejawa na chuki, uchoyo na fitina vitu ambavyo ni dhahili kuwa vinazorotesha juhudi za kuwafikisha katika mapenzi ya Mungu.

Alisema kutokana na ukweli kwamba mioyo ya watu ni michafu, inapasa kutambua wazi kuwa hakuna daktari au ufumbuzi unaoweza kuleta tiba ya mtu aliyetenda dhambi isipokuwa ni Yesu Kristo Mkombozi.

Alidai inawabidi watu kuwa chonjo kwakuwa wakati huu kwa kuwa ugumu na maghangaiko kwa watu yanayozidi kuongezeka katika jamii ni matokeo ya juhudi za ibilisi kupewa nafasi ya bure katika mioyo ya baadhi ya watu.

Aliwataka wazee wa Kanisa wawe jasiri wa kugusa dhambi za watu ili wafungue mioyo yao iliyoziba na kuipokea mipya ambayo ni Roho Mtakatifu.

"Mtu aliyepokea Roho Mtakatifu daima hujaa upendo, unyenyekevu, furaha na amani na mtu mwenye hasira, chuki, wivu na usengenyaji ni wazi kuwa Roho Mtakatifu hayuko ndani yake" aliongeza.

Sambano awataka watoto kuwatii wazazi, viongozi wa dini

Na Leocardia Moswery

Askofu wa Kanisa la Kianglikana la Watakatifu Wote lililopo Temeke katika dayosisi ya Dar-Es-Salaam na Pwani, Basil Sambano, amewataka vijana na watoto kuwaheshimu wazazi na viongozi wa dini kwa kushika mafundisho yao siku zote.

Alitoa ushauri huo wakati akiongoza ibada aliyotoa Kipaimara katika kanisa hilo Jumapili iliyopita.

"Leo tunatoa Kipaimara kwa ajili ya watoto wetu waliozaliwa upya na tunaimani kuwa kuzaliwa kwao kutawaonesha mwanga zaidi wa kutambua kuwa Yesu Kristo ndiye Mwokozi wa ulimwengu," alisema.

Aliongeza, "Watoto wawaheshimu wazazi, wakuu wa dini na kushika mafundisho siku zote za maisha yao," alisema Sambano.

Ibada hiyo iliyohudhuriwa na waamini mbalimbali wakiwemo wazazi wa watoto hao, mapadre pamoja na kwaya zote tano za Uinjilisti zilizokuwa zikitumbuiza katika sherehe hizo.

Wakati anawapaka mafuta matakatifu watoto 40, ghafla umeme ulikatika kitendo ambacho kilivuruga ibada na waamini kushindwa kusikiliza mahubiri yaliyokuwa yanatolewa.

Baadhi ya wazazi waliokaa nje huku wakiitazama picha ya video kwa ajili ya wingi wa watu walionekana kulalamika na kudai kuwa ni bora kanisa likawa na jenereta kuliko kutegemea umeme wa TANESCO hasa kwa siku zenye tukio muhimu.

"Tumeshindwa kuwaona watoto wetu na kuwashangilia kwani hatuelewi sasa hivi kinachoendelea ," alisema mmoja wa wazazi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

KKKT wasema kwenda mbinguni sio lelemama

Na Getrude Madembwe

MCHUNGAJI Moses Maarifa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Kawe, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, amesema kwenda mbinguni si kazi ndogo inayohitaji lelemama bali inahitaji juhudi katika imani na matendo bora.

Aliyasema hayo katika mahubiri yake aliyoyatoa Kanisani hapo Jumapili iliyopita.

Alisema upo uwezekano mkubwa wa mtu kujiona na kudhani kuwa ni mtenda mema kumbe, sivyo na kwamba hali hiyo ni hatari kiroho kwa kuwa ikifika siku ya mwisho, upo uwezekano mkubwa kwa mtu kukataliwa kuingia mbinguni.

"Jamani tufundishane na kuelimishana juu ya Ufalme wa Mbingu kwa kuwa kuingia huko sio lelemama," alisema na kuongeza, "Utakuta siku ya mwisho mtu wa namna hiyo usishangae kuona unaambiwa hakuna kuingia na ingawa utajitetea, Ooh! Bwana mimi nimetoa pepo kwa jina lako, Oooh! Mimi nilikuwa mwimbaji lakini utaambiwa, ondoka mimi sikujui na hapo kutakuwa kilio na kusaga meno".Aliwataka waamini wa dhehebu hilo kutoshiriki mambo ya kidunia bali wajitayarishe na kuanza upya kuishi maisha ya kiroho kwa kuwa kwa kufanya hivyo, wataishi milele.

Alisema watu wengi wanaogopa kufa lakini kufa ni lazima na akasema kuwa wasiwe waoga katika jambo hilo kwani kinachotakiwa ni kuishi katika maisha ya ya kujiweka tayari kutimiza na kupokea mapenzi ya Mungu.Alihimiza kuwa ni lazima mwanadamu yeyote mwenye makusudio meama na Mungu, awe tayari kuvumilia mateso yanayoweza kumkuta katika maisha yake ya kumpendeza Mungu na kuwa jasiri kwa kuwa Yesu Kristo ni kimbilio la watu wote.

"Ukitenda mambo ambayo yanampendeza Mungu kupata mateso ni lazima tuwe wajasiri kwani Yesu Kristo ndiye kimbilio letu," alisema.

Paroko ahimiza kuruhusu mapenzi ya Mungu yatendeke

Na Christopher Gamaina, Tarime

Wakristo wameshauriwa kuyakubali na kuyaruhusu mapenzi ya Mungu yatendeke ndani yao kama alivyofanya Bikira Maria.

Kauli hiyo ilitolewa na paroko wa Parokia ya Tarime Mjini, Padre Mathew Burra, Jumapili iliyopita iliyokuwa ya Kupalizwa Bikira Maria Mbinguni, alipokuwa akiendesha ibada iliyofanyika katika Kanisa hilo mjini hapa.

Aliwataka watu wote kufahamu kuwa Bikira Maria aliwatoa kwenye utupu ili kuwa na kitu kwa jinsi alivyoshiriki kikamilifu katika kumleta Mkombozi Yesu Kristo kwa kuwa alikingiwa dhambi ya asili.

Alieleza kuwa maisha ya Maria yalikuwa ya kujitolea ndio maana alikuwa tayari kuyaruhusu mapenzi ya Mungu yatimizwe ndani yake ambapo matokeo yake, aliuzalia ulimwengu mkombozi ambaye ni Yesu Kristo ili dhambi za wanadamu zisamehewe.

Paroko huyo alisema kuwa ni vema watu watambue kuwa Wakatoliki hawamwabudu Bikira Maria bali wanamuheshimu na kwamba wanaodhani na kudai hivyo, wanase,ma wasichokijua na ni vema watafute mbinu za kuelimishwa.

"...mfano, mtu hawezi kuongelea mtoto wa familia fulani bila kugusia baba na mama wa mtoto huyo. Hivyo tunapoongelea juu ya Yesu ni lazima tugusie Maria kwa heshima yake kutuzalia mkombozi," alisema Padre Burra.

Aliwataka watu kutopuuza ukweli kwamba Bikira Maria alikuwa na nafasi yake tangu zamani katika Kanisa lililoko mbinguni (malaika) na kanisa linalosafiri (sisi wanadamu) na kwamba kumkataa Maria ni kumkataa Yesu Kristo.

"Kumheshimu Maria ni kuutukuza upendo alioufanya Mwenyezi Mungu kwetu wanadamu kwa kutuletea mkombozi hapa duniani. Hivyo, hatuna budi kuyakubali mapenzi yake yatendeke katika maisha ya kila siku ili shetani asipate nafasi ya kuipokonya mioyo yetu na kuiangamiza," alisema.

Aliongeza kuwa kwa kupalizwa mbinguni, Bikira Maria ametuonesha kuwa uwezekano wa kwenda mbinguni upo ili mradi tu, wanadamu wawe wenye imani safi, unyenyekevu na matendo bora.

Jiandikisheni, mpige kura- Wito

Na Elizabeth Steven

WAUMINI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzani (KKKT), usharika wa Buguruni dayosisi ya Mashariki na Pwani, wametakiwa kuungana na wananchi wenzao nchini kujiandikisha na hatimaye kushiriki kikamilifu katika zoezi la upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajia kufanyaka Oktoba 29, mwaka huu.

Wito huo umetolewa na Mchungaji Michael Kitale, wa usharika huo alipokuwa akihubiri kanisani hapo Jumapili iliyopita na kuwataka waamini hao kutojitenga na shughuli hiyo muhimu kwa Watanzania wote.

Alisema kutokupiga kura kumchagua kiongozi anayefaa kuliongoza taifa, ni kukwepa majukumu yako katika uwajibikaji muhimu ndani ya taifa na hivyo ni kumkosea Mungu.

"Ndugu zangu washarika, narudia tena; nawaombeni mkajiandikishe katika upigaji kura. Msidhani kuwa ninyi hamhusiki, mnahusika sana. kutokupiga kura ni kosa kubwa sana na utakuwa unamkosea Mungu wako," alisema.

Alisema kuwa kutompigia kura mtu au kutopiga kura ni kosa kubwa ambalo linachangia nchi kupata viongozi wasiojali maslahi ya jamii hali ambayo kwa kiasi kikubwa, huchangia kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Wakati huo huo: Mwinjilisti Lilian Mollel ambaye yupo mazoezini katika usharika huo, amewataka waamini wa Kanisa hilo kutojiona kuwa wakati wote wao ni wazima kumbe ndani ya mioyo yao wamekufa na akasema hawana budi kumtumikia Mungu wao kwa imani na matendo bra ili wapate kuurithi Ufalme wa Mbingu.

"Mara nyingi sisi binadamu tunapotembea, tunajiona tu watu wema mbele za Mungu. Lakini, yatupasa kufahamu kuwa tumekuwa mbele ya Mungu tunatembea huku tukiwa tumekufa. Ili tupate kuurithi Ufalme wa Mungu, basi tuzishinde tamaa za mwili, wizi na mambo yote yanayomchukiza Bwana Mungu Wetu," alisema.

Aliwaasa kuacha Ukristo wa mdomo ambao hauna matendo ambao alisema kuwa yeyote afanyae ama kuwa na Ukristo wa namna hiyo, hatauona Ufalme na urithi wa Mungu. Kadhalika, alisema wanaoishi kwa tamaa za mwili, nao hawatarithi Ufalme wa Mungu.

Alisistiza kuwa njia pekee ya kurithi Ufalme wa Mungu, ni kukubali mateso na shida ambayo mara nyingi watu wengi wameshindwa kuzishinda tamaa hizo na hivyo kujikuta wamenasa katika mitego ya anasa.

"Mkristo ambaye yuko tayari kuishi katika mateso na shida, hakika hataurithi Ufalme wa Mungu Baba. Yule ambaye hatakubali, basi huyo kamwe hatauona," alisema.