Makanisani Wiki hii

Wanandoa washauriwa kutoandika makosa yao kwenye vitabu vya kumbukumbu

Na Elizabeth Steven

IMEELEZWA kuwa kitendo cha wanandoa kuandika kwenye kitabu cha kumbukumbu makosa mbalimbali wanayokoseana kinaweza kuchangia kiasi kikubwa uvunjaji wa ndoa yao.

Kauli hiyo ilitolewa na Mchungaji Heri Mwakabonga wa KKKT Usharika wa Tabata Daiyosisi ya Mashariki na Pwani wakati akiwahubiria waamini wa Usharika huo katika ibada iliyofanyika Jumapili iliyopita kanisani hapo.

Mchungaji Mwakabonga alisema kuwa njia pekee ya kuweza kudumisha ndoa ni kuombana msamaha ulio wa kweli badala ya kuandika kosa kwenye kitabu cha kumbukumbu

"Wanaofunga ndoa wanapendana lakini wanapofika nyumbani kila mtu na kijitabu chake pindi anapokuwa amefanya makosa mmoja wao anaandika tarehe fulani alichelewa kurudi nyumbani au siku fulani hukuosha vyombo vizuri."alisema Mchungaji Mwakibonga.

Aliongeza"Yesu ameweka sala, unayoomba usamehewe na Mungu nawe uwe tayari kumsamehe mwenzio na pindi tunapoungama tuuungame kwa mawazo maneno pamoja na matendo hivyo muombane msamaha na kuyasahau makosa yenu na kuishi kwa furaha na amani".

Akitoa mfano alisema kuwa iwapo mama na baba wameza watoto watatu halafu baadaye wakatengana zaidi ya miaka 20 ,lakini Baba kuogopa kutengwa na kanisa na kutoshiriki chakula cha roho kwa muda wa miaka yote hiyo akaamua kumfuata mkewe na kumtaka wafunge ndoa na mkewe akakataa hilo siyo jambo analo litaka Mungu.

"Iwapo mwenzio ametaka mrudiane na wewe bado unamuwekea vikwazo ,hapo unaenda kinyume na Mungu,kinachotakiwa ni kumwambia huyo baba kwamba kweli kama anataka kufunga ndoa na wewe ni bora atengane na huyo mke anayeishi naye (kama ana mke mwingine) baada ya hapo funga ndoa yenu na hakika mtaishi raha msatere"alisema Mchungaji Mwakabonga.

Watakiwa kutoa michango kwa ajili ya nyumba za ibada

Na Neema Dawson

MCHUNGAJI wa Kanisa la Kianglikana Dinari ya Kawe jijini, Canon George Killa amewataka wakristo kujitolea kutoa michango yao kwa ajili ya ukarabati wa nyumba za ibada badala ya kutoa mchango wao kwa ajili ya ofisi za vyama.

Mchungaji Killa aliyasema hayo wakati wa ibada iliyofanyika kanisani hapo hivi karibuni ambapo alisisitiza kuwa watu wanajitolea kutoa mchango wa ujenzi wa ofisi lakini siyo makanisa, kitu alichosema kuwa sio kizuri.

"Watu wako tayari kuchangia viroba vya michele, makopo ya rangi kwa gharama zao ili kukarabati ofisi za vyama na si kujitoleea makopo hayo ya rangi kukarabati nyumba za kufanyia ibada na wala hawaguswi kabisa kuona kuwa nyumba hizo zimechakaa na zinahitaji ukarabati ili zipendeze lakini matokeo yake wanapendezesha ofisi za vyama"alisema Mchungaji Killa.

Alisema kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, baadhi ya wakristo wameanza kujisahau kutofika kanisani na kutumia muda wao mwingi, nguvu, pesa zao katika mambo ya siasa na kusahau kuwa Mungu ndiye muumba wa vitu vyote vilivyomo duniani na yeye ndiye mtoaji wa baraka zote ingawa watu wanamuweka nyuma na kutoa sadaka zilizobakia sokoni ambazo ni kama mabaki.

"Watu wameyasahau majumba ya Mungu na hawawezi kuyaangalia kuona kama bado yana faa ama hayafai kutumika kwa ibada ,hawaoni kama kuna sababu ya kufanya ukarabati"alisema.

Amesema watu hawanabudi kuzithamini nyumba za ibada kama wanavyo zithamini nyumba zao hivyo kusisitiza kujitolea kuzitengeneza nyumba za kuabudia.

Sambamba na hayo aliwasisitiza wakristo wote kumtegemea kristo na kuwataka wasimfuate mtu yeyote wala miungu ya mataifa ambayo haitawasaidia.

Walio katika ndoa watakiwa kubaki kama walivyo

Na Getrude Madembwe

WATU walio katika maisha ya ndoa wametakiwa kubaki ndani ya ndoa zao badala ya kuwa na wapenzi wengine kwani suala hilo linaweza kusababisha uvunjaji wa ndoa hiyo.

Hayo yalisemwa mwanzoni mwa Juma na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Maria Kawe Padre Yuda Shayo katika misa ya Sakramenti takatifu ya ndoa na ubatizo iliyofanyika katika mtaa wa mtakatifu Paul Mtume uliopo Makongo area D jijini Dar es Salaam.

Alisema watu wa ndoa hawana budi kulinda heshima ya ndoa zao na wakivunja ahadi hiyo wanakuwa wamekwenda kinyume na maadili ya ahadi zao walizoahidi siku ya ndoa kwamba watakuwa wote hadi hapo kifo kitakapowatenganisha.

"Mnatakiwa muwe wakweli kwani mnaahidi kuwa mtakuwa pamoja hadi kifo kiwatenganishe sasa sio vizuri tena ukawa na mpenzi mwingine nje ya ndoa yako utakuwa umemkosea Mungu pamoja na mke au mume wako", alisema Padre Shayo.

Aidha Padre Shayo aliwataka wanandoa hao ambao walikuwa wakibariki ndoa zao kutowekeana kinyong o mioyoni mwao na badala yake wawe na upendo wa kuvumiliana kila jambo liwe ni zuri au baya kwani wakifanya hivyo watakuwa wamedumisha amani katika ndoa yao.

"Mnatakiwa muwe na mioyo ya nyama yaani yenye upendo na wala msiwe na mioyo migumu ya mawe ambayo huwa ni migumu kusamehe au kuvumiliana" alisema Padre Shayo na kuongeza kuwa "upendo ukikosekana ndani ya nyumba ,mmoja wenu ataugua ugonjwa wa vido nda vya tumbo sababu kila wakati huwa mmenuniana".

Pia aliwataka wazazi ambao waliwabatiza watoto wao wawalee katika njia bora za kumpendeza Mungu.

Msifurahie mwenzenu anapotoka kundini-Mchungaji

Na Mwandishi Wetu

WAAMINI wametakiwa kutofurahia pindi muumini mwenzao anapoingia katika njia za kishetani na badala yake wamatekiwa kumuonyesha njia iliyo sahihi muumini huyo.

Kauli hiyo ilitolewa Juamapili iliyopita na Mchungaji Moses Maarifa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli nchini (KKKT) Usharikia wa Kawe Dayosisi ya Mashariki na Pwani,wakati akitoa mahubiri kanisani hapo.

alisema "ndio maana tunaimba kuwa kunafuraha mbinguni iwapo mmoja wetu ametubu hivyo tusifurahie mmoja wetu akipotea, bali tunachotakiwa ni kusahihishana ili wote siku ile tutakapokuwa mbele za Bwana tuwe pamoja" alisema Mchungaji Maarifa.

Mchungaji huyo pia ameitaka jamii ya Kikristo kukaa na kuelewana hasa pale inapoonekana kutofautia.

"Litakuwa ni jambo la aibu iwapo jamii ya Kikristo itatafautiana na kutoelewana na kamwe Mungu hapendelei migongano itokee katika jamii nzima sasa iweje jamii ya Kikristo iwe na migongano?" alihoji Mchungaji Maarifa.

Pia alisisitiza juu ya kusamehana ambapo alitaka kila mmoja kumsamehe mwenzake katika kila jambo ambalo wamekoseana na wala siyo kuwekeana kinyongo.

Alisema hali ya mtu kutokubali kumsamehe mwenzake ni sumu kwani inaweza ikafikia hatua ya mtu anaamua kujiua sababu ya kuwa na kinyongo na mtu mwingine.

"Ukiona umekosekana na mwenzako ni heri ufanye naye mazungumzo ili kuondoa hasiria" alisema Mchungaji Maarifa.

Wakati huo huo: Kumetokea uhamisho wa wafanyakazi katika Usharika huo ambapo Bi. Bi.Anna Mbaga ambaye alikuwa akifanya kazi usharikani hapo (Parish Worker) amehamishiwa Usharika wa Msasani na Mama Sanga amehamishiwa Usharika wa Kawe akitokea Usharika wa Kijitonyama.

Njia pekee ya kumuona Mungu ni kulisikiliza, kulisoma,kulitafakari neno lake-Mchungaji

NaJenifer Aloyce, DSJ

"NJIA pekee ya kuweza kumwona Mungu ni kusikiliza neno la lake na kuwa na tumaini nalo pamoja na kuyaweka moyoni maneno uliyosoma,bila kuyasahau na kutafakari neno lake kwa kusoma biblia takatifu".

Kauli hiyo ilitolewa jumapili iliyopita na Mchungaji Kadago kutoka Iringa alipokuwa akitoa mahubiri ya kuwaaga Waamini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Mbagala Kizuiani.

Mchungaji Kadago ambaye alikuwa ametembelea kanisa hilo kwa muda,alisema watu wa Mungu hawana budi kuwa wavumilivu, watakatifu pia kutiana moyo pale wanapoona wenzao wanaelemewa.

"Mtu anayemtegemea Mungu ni lazima awe mvumilivu kwani Mungu aliyasema maneno haya akijua vikwazo utakavyokutana navyo ni vingi na hakuna msaada wowote ila ni kutoka kwa yeye peke yake"alisema Mchungaji Kadago.

Aliongeza kusema kuwa kuna watu wanaosema Yesu aje katika mioyo yao, lakini akafafanua kuwa Yesu hawezi kusikiliza ombi hilo kama anaona hakuna chochote kilichofanyika ambacho kinaweza kumfanya afanye masikani yake pindi atakapokuja kwako.

"Yule anayesema Yesu aje haraka mtu huyu ni sawa na mtu aliyevaa miwani ya mbao kwani hatakuwa haoni mbele,kinachotakiwa kwanza isafishe nafsi yako na hapo Yesu atakuwa tayari kuja kwako bila kuchelewa"alisema.

Aliendelea kwa kutoa mfano wa mtu akipanda mti kama hautahudumiwa ni lazima udhoofike lakini kama utahudumia kwa samadi na maji ni lazima ustawi vizuri na kuzaa matunda mazuri.

"Mungu ameweka ahadi za kweli kama tukitafakari na kuangilia maneno yake hatakosa kuwa naye, inatakiwa kumtumainia Mungu kwa hali zote shida na raha yeye awe ndio kiongozi na mtawala wako pekee"alisema.

Mchungaji huyo aliendelea kusema kuwa kila mtu ni lazima kuwa tayari na parapanda itakapolia ni kuondoka tu haijalishi kuwa siku hiyo utaota mbawa au utaondoka vipi hamna haja ya kuogopa wala kuhofu kwani Mungu ndio kimbilio lako.

"Inatakiwa ufahamu kuwa silaha zote nikuwa na moyo wa ushujaa ,uhodari na uvumilivu kama Yesu pale Msalabani alikuwa hodari hakukata tamaa, alivumilia mateso na mwisho alisema Baba mikononi mwako naiweka roho yangu akakata roho;

hivyo kwa kuwa alimtumainia Mungu mpaka dakika za mwisho na sisi hatuna budi kuwa wavumilivu mpaka mwisho" alisema.

HEKA HEKA ZA UCHAGUZI MKUU

Taasisi za kidini zashauriwa kuwaombea wanahabari

Na Leocardia Moswery

ILI kuandika habari zenye ukweli ndani yake katika kipindi hiki cha shamrashamra za uchaguzi mkuu,taasisi mbalimbali za kidini zimeshauri kuwaombea kwa sala Waandishi wa Habari ambao ndiyo kioo cha jamii.

Ushauri huo ulitolewa Jumapili iliyopita na Katibu Mtendaji wa Idara ya Uchungaji katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ,Padre Theobald Kyambo wakati wa Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika kanisa la TEC. Katika ibada hiyo ambayo pia ilikuwa ni Jumapili ya Upashanaji Habari Ulimwenguni na alisema kuwa pamoja na kuombewa lakini vile vile vyombo vya habari havina budi kuzingatia wajibu wake wa kuandika habari za ukweli bila kuwa na upendeleo wa kukuza chama kimoja cha siasa na kuvikandamaiza vyama vingine.

"Tunapoazimisha siku ya Upashanaji Habari ambapo kitaifa inaadhimishwa mkoani Tanga, si vibaya tukawaombea waandishi wa habari ili wakaweze kutoa habari kamili", alisema Padre Kyambo.

Aliongeza "waandishi wa habari pia mnapaswa kutoa habari bila upendeleo wowote kwa kila chama cha siasa bila kujali rangi wala kabila huku wvile vile vile mhamasishe jamii nzima juu ya umuhimu wa kupiga kura".

Padre Kyambo amesisitiza kuwa kuwaombea wanahabari ni sawa na kumtangaza kristo kwa njia ya upashanaji habari.

Mbali na hilo,Padre Kyambo pia amewataka waamini wa madhehebu mbalimbali nchini kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji na upigaji kura katika uchaguzi huo utakaofanyika oktoba mwaka huu.

Alisema kuwa waamini wajitokeze kwa wingi katika upigaji kura ili kuwapata viongozi wanao wapenda.

Alisisitiza kuwa kila mtanzania ana kila sababu ya kupigia kiongozi yoyote kura kwa hiari yake bila kushwishiwa na mtu mwingine.

Aliongeza kuwa kama yupo kiongozi anayetumia rushwa huyo siyo Kiongozi bali ni wale viongozi hata kama wakipata madaraka huyatumia kwa fujo bila kujali ahadi alizotoa wakati akiomba kura.

Siasa isitutenganishe-Mchungaji

Na Christina Mbezi,DSJ

WAAMINI wa madhehebu mbalimbali nchini wametakiwa kutokubali kujenga uhasama miongoni mwao kwa kutumia visingizio vya siasa.

Kauli hiyo ilitolewa Jumapili iliyopita Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Kigogo katika Daiyosisi ya Mashariki na Pwani,Aman Lyimo wakati akitoa mahubiri katika ibada iliyofanyika kanisani hapo.

Mchungaji Lyimo alisema kuwa pamoja na kila muamini kuruhusiwa kujiunga na chama chochote cha siasa anachotaka lakini kuna kila sababu ya kuangalia kwa undani suala hilo kwani linaweza kuleta mgawanyiko ndani ya kanisa.

"Jihadhali sana siasa isitutenganishe maana humo humo ndani ya kanisa yanaweza kujengeka makundi ,kundi hili likawa chama fulani na lingine chama fulani sasa kwa mabishano ya kisiasa mnaweza mkakuta yanaingia hadi kanisani hivyo kuleta utengano. alisema

Mbali na kusisitiza juu ya suala hilo,Mchungaji Lyimo pia amewataka waamini wa Kanisa hilo kuwachagua viongozi wacha Mungu na wale wasiopenda rushwa.Katika mahubiri hayo Mchungaji Lyimo amewataka waamini hao kuepeuka kabisa wale viongozi wanaotoa ahadi za kuwaadaa kwamba watafanya jambo fulani lakini wakisha chaguliwa hawakubali kutekeleza ahadi hizo.

"Mtu mwenye sifa za kiongozi ,anakuwa na hekima na pia kiongozi wa kweli anakuwa na sera za ukweli na mwenye kumcha Mungu"alisema Mchungaji Lyimo.