Makanisani Wiki hii

Msitoe kadi za harusi kwa ubaguzi-Padre

Na Peter Dominic

IMEELEZWA kuwa kitendo cha kutoa kadi za sherehe za harusi kwa baadhi ya watu na wengine kunyimwa ni cha uchoyo hivyo jamii haina budi kuachana na suala hilo.

Kauli hiyo ilitolewa Jumapili na Katibu wa Jimbo Kuu Katoliki la dar-es-Salaam,Padre Andrew Luanda wakati wa misa takatifu iliyofanyika katika kanisa katoliki la Mtakatifu Maurus lilipo Kursani jimboni humo.

Alisema ni jambo la busara kutoa kadi kwa wote bila kujali kama baadhi ya watu wamechanga ama hapana na kama ni suala la kuhofia chakula ni hekima na busara kumuomba Mwenyezi Mungu kuongeza neema ya chakula ili watu wote waweze kupata.

"Wakati wa harusi watu wasiokuwa na kadi hudhibitiwa milangoni ili wasiweze kuingia kula au kunywa,hiki ni kitendo cha hatari hakiendani kabisa na upendo wa Bwana wetu Yesu Kristo"alisema.

Katibu huyo aliongeza kusema kuwa Yesu Kristo katika mafundisho yake hakufanya hivyo badala yake alipoona watu wana kiu na njaa alivichukua vipande vya mikate vidogo akaomba kwa Mwenyezi Mungu akaviongezea ambapo watu wote walikula na kusaza.

Padre Luanda alisema kuwa chakula hakipo kwa misingi ya kubaguana au kuwagawa wanadamu na kusisitiza kuwa chakula ni kiunganishi kwa wale walionacho na wasiokuwa nacho ambacho huwaunganisha pamoja katika furaha ya Mwenyezi Mungu siyo kutangaza ubaguzi kwa kupeana kadi.

"Mbona kwenye misiba hampeani kadi wala kubaguana kwa chakula" alihoji Padre Luanda

Alisema wakati wa misiba watu huuangaika pamoja ,hushirikiana kwa kila jambo hata wakati wa kulahivyo mfano kama huu si vibaya ukitumia hata wakati wa furaha kama sherehe za harusi bila kuwepo na ubaguzi.

Aidha aliwatahadharisha watu ambao hufunga milango yao wakati wakula huku wakidai chakula ni kidogo, akasema watu wanaosema hivyo huwa hawakiombei chakula kabla ya kula kwa vile wanakiona kidogo.

Padre huyo aliwataka watu wa namna hiyo wajifunze ukarimu majumbani mwao kwa kuwa na desturi ya kumuomba mwenyezi Mungu aliyewapa chakula hicho ili awaongezee na kwamba wasiwe kama Bi. Mkora ambaye alimkumbuka Mungu alipokabwa na mfupa wa samaki lakini wakati hajaanza kula alikuwa akimkejeli Mwenyezi Mungu.

Uongozi wa makanisa siyo njia pekee ya kwenda mbinguni-wito

Na Mwandishi Wetu

WAAMINI wa makanisa mbalimbali nchini wametakiwa kuelewa kuwa kukimbilia kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi wa kanisani huku wakijua fika hawana sifa na uwezo wa kufanya hivyo,siyo njia ya kuwafikisha mbinguni.

Hayo yalisemwa na Mwalimu wa Kwaya ya Vijana wa Usharika wa Kariakoo Dayosisi ya Mashariki na Pwani Jimbo la Ilala Bw.Sunday Kihwehe wakati wa ibada ya hitimisho la tamasha la wiki ya vijana.

Katika ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili ya Kilutheri nchini (KKKT) Kariakoo Bw.Kihwehe alisema kuwa waamini wengi wanakimbilia madaraka na wakishayapata wanajisahau.

"Waamini wengi wanakimbilia madaraka ya kanisa na wanaposhika madaraka hayo wanajisahau wakidhani kuwa wameshampokea Yesu" alisema Bw.Kihwele.

Bw. Kihwele aliendelea kusema kuwa baadhi ya viongozi wa dini wakiwa wa ngazi mbali mbali pamoja na wadhifa walionao, hawatendi matendo ya kumpendeza Mungu kama Biblia inavyotaka .

Alisema katika kuondoa vitendo vya namna hii vikundi mbalimbali vya vijana havina budi kuvikemea kwa kutunga na kuimba nyimbo zenye ujumbe wa kulaani kabisa njia hizi potofu.

Alisema pamoja na kwamba vikundi vya kwaya, ngonjera na maagizo nia na madhumuni ni kuwavuta vijana walioko mitaani ili uweze kuwa karibu na Mungu lakini vile vile ni kuandaa watu waweze kuuona ufalme wa Mungu.

Wakati huo huo: Igizo la ‘Usiwe na Imani nyingine’ la vijana wa Kariakoo lilitoa burudani ya aina yake pale lilipo igiza familia iliyokuwa imekosa imani na kuingiiwa na imani potovu za kuanza kushiriki imani za kiganga.

Hata hivyo mchungaji huyo alisema kuwa dawa na kinga ya mganga ni Biblia tu na kusali kwa imani bila kujenga fikra ndani ya mawazo yako.

Wapentekoste kuanzisha chuo

Na Mwandishi Wetu

KANISA la Pentekoste Kurasini lililopo Jijini Dar-Es-Salaam linatarajia kujenga chuo cha Mafunzo ya Uinjilisti Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili mwanzoni mwa wiki ,Mchungaji wa Kanisa hilo Daniel Mshanyi alisema kuwa ujenzi huo utafanyaika katika eneo la Mtoni Manispaa ya Temeke mkoani humo.

Alisema kanisa lake ambalo linashirikiana kwa karibu na Umoja wa Makanisa ya Pentekoste Tanzania (UMPT) limefikia uamzi huo kwa kutambua kwamba jamii inahitaji kufundishwa kikamilifu na watu waliopevuka katika mafunzo ya kiroho na wenye wito wa kujitolea kwa kazi hiyo.

Alisema wainjilisti hao watakaojitolea kwa kazi hiyo watatakiwa kujifunza kwa kipindi cha mwaka mmoja ili wajue kupambanua mambo matakatifu na mambo ya siku zote, pia wajue yote yaliyosafi na machafu na kuongeza kuwa kwa kuyajua mambo haya watakuwa na uwezo wa kuhubiri vema neno la Mungu.

Alisema sababu nyingine ya kujenga chuo hicho ni kutimiliza maneno matakatifu yaliyoandikwa katika Biblia.

"Biblia inasema shamba la Bwana ni kubwa lina mavuno mengi lakini watenda kazi ni wachache hivyo zinahitajika nguvu za hali na mali kuhakikisha watu wanafundishwa mambo ya Mungu na kuyafanyia kazi kama alivyoangiza Yesu Kristo"alisema.

Mchungaji Daniel aliendelea kusema kuwa pamoja na kujenga chuo hicho mahali hapo kuna mipango mingine ya kuwepo kwa shule ya chekechea ingawa alisema mipango hiyo kwa pamoja haijulikani itagharimu kiasi gani .

Alisema kwa hivi sasa linajengwa kanisa kubwa ambalo alisema litakuwa na uwezo wa kuchukua idadi kubwa ya waumini tofauti na kanisa wanalolitumia kwa sasa japokuwa hakuzitaja gharama za ujenzi zilizotumika wala zinazohitajika kwa vile alihofia kutoa takwimu zisizostahili baada ya kudai kuwa wanaohusika na kamati ya ujenzi hawakuwepo.

Mtumikieni Mungu siyo kufikiria kujenga "mahekalu"-Wito

Na Jenifer Aloyce, DSJ

WAAMINI wa madhehebu mbalimbali ya kidini nchini wametakiwa kumtumikia ipasavyo Mwenyezi Mungu badala ya kukaa na kufikiria jinsi ya kutafuta pesa na kujenga nyumba ya mamilioni yenye thamani za hali ya juu ndani yake.

Kauli hiyo ilitolewa Jumapili iliyopita na mchungaji Swai kutoka Nyakato Mwanza alipokuwa akitoa mahubiri katika Kanisa la T.A.G Mbagala Kizuiani.

Mchungaji Swai alisema kazi ya kuhubiri injili inashindikana kwani watu wamekuwa wakiweka misingi yao hapa dunia niya kuangalia jinsi gani ya kujenga nyumba ya milioni 20 na yenye vitu vingi vya thamani kushindwa kumtumikia Mungu ".

Alisema,mwanadamu anaouwezo wa kufanya mambo makubwa hapa duniani lakini anacho takiwa kufahamu ni kwamba hapa dunia si mahali pake anatakiwa kuwa na makao yake mbinguni.

" Mtu aliye na mitazamo mizuri atafanya jambo jema alilokusudia makusudi mema ndio mapenzi ya Mungu"alisema Mchungaji huyo.

Aliendelea kusema Mungu anajisikia heri na baraka mbele ya Malaika akiitwa na watakatifu wake na anajisikia haya akiitwa Mungu na watu wanaopenda kuitumikia dunia hii.

Mchungaji huyo pia aliwahimiza vijana kuwa wakae ndani ya Yesu Kristu ili wasije kularuliwa na shetani kama mbwa mwitu alaruavyo.

"Mwanadamu akikaa hapa duniani inambidi kukaa mguu mmoja nje na mmoja ndani,

,Wapenzi nawasihi muishi kama wasafiri kwani mnatakiwa kuwa na mwenendo mzuri kati ya mataifa kwani sisi wote ni wapita njia anasa zote za dunia utaziacha"alisema.

Aliongeza kuwa mwanadamu anatakiwa atayarishe makao yake mbinguni sio duniani. "Usifanye kana kwamba Yesu anarudi miaka 200 ijayo bali fanya kama Yesu anarudi leo hii" alisema.

Waombwa kuchangia elimu ya Masista

Josephs Sabinus na Christopher Gamaina, Tarime

WAKATOLIKI wa parokia ya Tarime katika Jimbo Katoliki la Musoma wameombwa kuwachangia masista wa shirika la Moyo Safi wa Maria ili wafanikishe suala la Elimu ili kiwe kichocheo cha utumishi wao bora.

Ombi hilo lilitolewa na padre Godfrey Ocamringa wa parokia ya Komuge Jimboni hapo, wakati wakizungumza katika ibada ya Jumapili iliyopita katika Kanisa la Parokia hiyo mjini Tarime.

Kila jumapili ya mwisho Julai, jimboni Musoma huwa ni kwa ajili ya kuwasaidia masista kujiendeleza kwa namna mbalimbali za utumishi wao. Wazo la mwaka huu ni elimu.

"Ili masista wadumu kufanya vema utumishi wao katika utoaji wa huduma zao mbalimbali zikiwamo ufundishaji, uenezaji injili, utoaji wa huduma za afya na kuwasaidia wenye shida kadhaa, masista wanapaswa kusaidiwa katika kuwapatia elimu ya kutosha.

Wakatoliki wenye mapenzi mema ni jukumu lao kuwasaidia kwa kuwa kazi za masista ni za kujitolea, hawalipwi na sisi tunahitaji huduma zao, sasa watatoaje kama hatuwasaidii?".

Katika jumapili hiyo ambayo masista wa shirika hilo walitawanywa katika parokia zote 30 za jimbo , ili kueleza shida zao, masista kadhaa waliambia Kiongozi kuwa wanaomba jamii iwasaidie na kuachana na dhana potofu kuwa masista wanapata kila kitu.

"Wengine wanadhani masista wana kila kitu eti hawahitaji kusaidiwa... si kweli; tunahitaji kusaidiwa na jamii." Alisema sista Rosemary Nyanzala aliyekuwa parokiani Nyamongo pamoja na sista Suzana Kache, alisema, "Shirika lina masista 34, shuleni na vyuoni; siyo rahisi kuwasomesha wote bila kusaidiwa... wengine wanadhani tunasaidiwa na wafadhili kweli wangejua tunavyoishi kwa shida hata kulazimika kula mlenda..." alisema.

Toeni kwa Mungu mlichonacho -Paroko

Na Elizabeth Steven

WAAMINI wa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine wameambiwa kuwa hawana budi kumtolea Mungu kile walichonacho hata kama ni kidogo.

Hayo yalisemwa na Paroko Msaidizi wa Kigango cha Maria Consolatha Kigamboni Padri Gianni Treglia wakati wa Misa takatifu iliyofanyika Jumapili iliyopita katika Kigango hicho kilichopo chini ya Kanisa Katoliki.

Padre Treglia aliwaeleza waumini wa Kigango hicho kuwa kama ni watu wenye mapenzi mema na upendo kwa muumba wao hawana budi kutoa chochote hata kama mbele ya macho yao kinaonekana ni kidogo.

"Tusiogope kuchangia kile tulichonacho ingawa machoni petu kinaonekana kidogo , kukiweka mikononi mwa Bwana"alisema.

Alisema kuwa mara nyingi watu wanapotakiwa kuchangia kitu fulani kwa ajili ya kanisa husema hawana kitu na wengine kuona haina maana kuchangia.

" Dhana hizo potofu ni lazima zipigwe vita miongoni mwenu,mara nyingi tunapotakiwa kuchangia kitu fulani kwa ajili ya kanisa tunasema hatuna basi tujue kwamba Yesu katika kutenda kazi yake anahitaji misaada kutoka kwetu."alisema.

Wakati huo huo: Makamu mwenyekiti wa Kigango hicho Joseph Kiluma amewataka waumini wa kigango hicho kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanajiunga katika jumuiya ndogondogo

Akisoma matangazo katika ibada hiyo,Bw.Kiluma alisema"Ni aibu kwa kanisa au kigango kuwa na watu au wakristo ambao hawataki kufuata maadili ya kanisa lao, Padri haruhusiwi kutoa kipaimara, ubatizo bila kupata taarifa kutoka kwa viongozi wa jumuiya ndogo ndogo.

Aliendelea kusema kuwa "kanisa au Kigango halitakuwa tayari kumsaidia muumini pindi anapopatwa na matatizo bila kupata taarifa kutoka kwa viongozi wa jumuiya ndogondogo iwapo Padri atafanya hivyo basi atakuwa amefanya makosa".

Waimbaji wa Dar-Es-Salaam msijione "vinara"-Padre

Na Leocardia Moswery

WAIMBAJI wa madhehebu mbalimbali Jijini Dar-Es-Salaam wametakiwa kuachana na wazo la kujisifu na kujiona kwamba wao ni waimbaji wazuri kuliko wale waimbaji wa vijijini kwani suala hilo halina ukweli ndani yake.

Rai hiyo ilitolewa na Padre Edwin C. Taji kutoka chuo cha Mapadre Buguruni wakati wa ibada iliyofanyika Jumapili iliyopita katika kanisa la Kianglikana la Watakatifu wote Dinari ya Temeke

Alisema"waimbaji walio wengi hapa Jijini wanajiamini sana kupita kiasi wakidhani kuwa uimbaji wao ni zaidi kuliko waimbaji wa vijijini", na kuongeza kuwa waimbaji wa vijijini wanajituma mno kupita kiasi wakijua jukumu kubwa ni kueneza injili kwa njia ya uimbaji".

Padre huyo anayesoma katika chuo hicho cha Mtakatifu Marks kilichopo Buguruni, alisema vijana wa kwaya ya Tunguli kutoka mkoa wa Tanga wilayani Handeni ni vijana wanajituma na kuonyesha moyo na jinsi gani wanavyoweza kumvuta mtu aliyepotea na kuwa karibu na Mungu.

Kwaya hiyo ya Tunguli ni jina lililotokana mganga mmoja ambaye alikuwa anatumia tunguli katika uganga wake na baada ya kuokoka aliwakusanya waganga wote wanaotumia tunguli kuzichoma moto na kufuata maisha ya kuokoka na baada ya wote kuokoka ndipo walipounda kwaya na kuipa jina la "Tunguli".

Kwaya hiyo ya Tunguli yenye wanakwaya 45 iliambatana na padre wao Jonas Maarifa kutoka Dayosisi ya Morogoro anayeshika parishi 14, mitaa 8 ,ndiyo iliyoimba Jumapili hiyo kanisani hapo .