Makanisani Wiki hii

Msiwe jeshi la kukatana mapanga shambani, Vilabuni - Kardinali

lMakanisa mawili yawekwa wakfu

Dalphina Rubyema, Kigoma na Mathias Marwa, Musoma

"Jeshi lenu liwe ni la kumtangaza Kristo mahali popote bila kutukana ama kukashifu dini za wengine, msiwe na jeshi la kukatana mapanga, mwabudu Mungu mahali popote hata shambani, vilabuni mkiongozwa na Roho Mtakatifu.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliyasema hayo Jumapili iliyopita wakati wa ibada ya kutabaruku Kanisa Katoliki la Mtakatifu Visenti wa Paulo, lililopo Parokia ya Katubuka katika Jimbo Katoliki la Kigoma.

Katika ibada hiyo takataifu iliyohudhuriwa na maelfu ya waamini, Kardinali Pengo alisema kuwa, waamini wa kanisa hawana budi kuwa mfano bora wa kuigwa kwa kuepuka mifarakano, ugomvi na mengine yoyote ambayo ni machukizo kwa Mungu iwe sehemu ya uzalishaji,katika starehe au shida.

Katika ibada ya siku hiyo ambayo vijana wapatao 70 walipata Sakramenti ya Kipaimara, aliwataka waamini Wakatoliki kuwa mstari wa mbele kuonesha mfano bora wa kutumia nyumba za ibada kwa kutimiza mapenzi ya Mungu badala ya kuhangaikia kutumia majengo makubwa ya makanisa kama kigezi cha kumtukuza Mungu.

Alisema mbele za Mungu kinachotakiwa ni matendo mema na si ufahari wa majengo kutumika kama kigezo.

"Hatujengi majengo makubwa ya ajabu ili kutishia ulimwengu, kunaweza kukawa na kanisa dogo tu la kifukara lakini, matendo ya wanaolitumia, yakawa ni ya kumpendeza Mungu," alisema.

Aliongeza kuwa, "Kanisa hili ambalo nimelizindua leo ni la thamani kubwa. Ombi na dua yangu ni kwamba utukufu wa kanisa hili kwa nje uwe ni utukufu wa waamini wote wanaolitumia."

"Wale wenye uvivu wa kusali, tunapoinua macho na kuliona kanisa kama hili nanaimani tutaona aibu na itabidi twende kusali kila siku hususani siku za Jumapili," alisema.

Katika ibada hiyo takatifu Mwadhama pia alitoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana zaidi ya sabini ambapo aliwataka wanakipaimara hao kumwabudu Mungu mahali popote wakiongozwa na roho Mtakatifu.

Ibada hiyo ya kutabaruku kanisa hili lililopo zaidi ya kilomita tano kutoka Kanisa Kuu la jimbo hilo, ilianza kwa maandamano yaliyoanzia Kanisa Kuu na kuzunguka eneo la Kigoma Mjini hadi lilipojengwa kanisa hilo.

Kutoka Musoma , inaelezwa kuwa; Kanisa la Kikatoliki la Mtakatifu Stanislao lililopo Nyamuswa katika wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara Septemba 7, mwaka huu, linatarajiwa kuwekwa wakfu kutabaruku na mmoja wa maaskofu wa Vatican Septemba 7 mwaka huu, imefahamika.

Kanisa hilo lililopo ndani ya Jimbo Katoliki la Musoma, lenye uwezo wa kuchukua waamini zaidi ya 500 limejengwa kwa ufadhili wa Kanisa hilo nchini Poland kwa lengo la kueneza Injili, upendo na amani.

Akihojiwa na Kiongozi mjini Musoma mwishoni mwa juma lililopita, Mwenyekiti wa Kamati ya Upashanaji Habari na Uhamasishaji ambaye pia ni mlezi wa Kanisa hilo Bw. Charles Komanya, alisema kuwa kanisa hilo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 100.

Bw. Komanya amesema kanisa hilo litakuwa la kwanza kuweka wakfu katika karne hii katika Jimbo hilo la Musoma na pia la tatu kuwekwa wakfu mkoani Mara.

Ameyataja mengine yaliyowahi kuwekwa wakfu kuwa ni Kanisa Kuu la mjini hapa na Kanisa la Huruma la Mungu lililopo Kiabakari Musoma vijijini.

Viongozi mbalimbali wa Serikali vyama vya siasa madhehebu ya dini na waandishi wa habari watahudhuria sherehe hiyo.

Linusuruni taifa kwa mafunzo mema ya watoto- Wito

Na Getrude Madembwe

WAZAZI kote nchini wametakiwa kutoa malezi yenye misingi bora kwa watoto ili kulinusuru taifa lisiangamie kimaadili na kuliwezesha kuwapata viongozi safi wa wa siku za usoni.

Wito huo ulitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Askofu Method Kilaini katika ibada aliyotoa sakramenti ya Kipaimara kwa watoto 214 iliyofanyika katika Kanisa la Kikatoliki Mtakatifi Petro (St. Peter’s)clililopo Osterbay Dar-Es-Salaam Jumapili iliyopita.

Askofu Kilaini alisema kuwa jamiii kama wazazi na walimu kwa vijana, haina budi kutoa malezi bora yenye mfano bora wa kuigwa na kila mwenye mapenzi mema.

Alisema kamwe jamii hiyo ambayo ni kioo kwa watoto na vijana kujifunza, haina budi yenyewe kuepukana na kutenda mauovu kwa kuwa endapo watafanya hivyo, watoto wao wataiga mfano wao na hivyo kuwa hasara na machukizo kwa taifa zima na hata Mungu.

"Nyinyi kama wazazi mnatakiwa muwalee watoto wenu vizuri. Kila mmoja aseme nataka mwanangu alelewe kwa mfano wangu; mfano bora hivyo basi nanyi muwe na matendo yaliyo bora," alisisitiza Askofu Kilaini.

Alitaka kuimarishwa kwa jumuiya zote ndogo ndogo ili ziwe zenye mapenzi ya Bwana kwani endapo hazitakuwa na matendo yanayompendeza Bwana, mtoto au kijana anaweza ataiga mfano na kuharibikiwa na pengine akawa na matendo mabaya hata kupita hayo ya wazazi wake.

"Tunatakiwa kuziimarisha jumuiya zetu ndogondogo kwani mtoto au kijana anaweza akapata malezi bora (yenye maadili) lakini jumuiya iliyomzunguka hufanya matendo yasiyompeza Bwana na hivyo huwa rahisi kwa mtoto huyo kupokea mafundisho mabaya kuliko mazuri.

Hivyo nawaombeni mziimarishe jumuiya zenu ndogo ndogo," alisema Askofu Kilaini. Askofu aliwataka vijana hao waliopokea Sakramenti ya Kipaimara kuwa wanasali kila wakati na hata kuwafundisha watu wengine na mna ya kuishi kwa kadri ya mapenzi ya Mungu na Kanisa lake.

Aliwahimiza pia kufundishana na kuonyana wao wenyewe pindi wanapoona mwenzao anapotea katika mafundisho ya Kristo, na kwamba kamwe wasikubali kudanganywa na mtu yeyote yule kwani wao sasa ni watu wazima ambao wanajua lipi zuri nalipi baya.

Mzee wa TAG ataja kanuni nne za kushirikiana na Mungu

Na Jenifer Aloyce, DSJ

"KILA jambo duniani lina kanuni zake, kadhalika maisha ya kiroho yana kanuni zake za namna ya kushirikiana na Mungu, kanuni hizo za kiroho zipo nne."

Hayo yalisemwa katika kati ya juma na Romano Daudi ambaye ni Mzee wa Kanisa la TAG la Mbagala Kizuiani jijini Dar-Es-Salaam, wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake.

Alisema kanuni ya kwanza ya kiroho ni Upendo kwa Mwenyezi Mungu kwa kutimiza anavyotaka kwa mipango yake yenye wema na ya ajabu kwa maisha ya mwanadamu kwa kuwa Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa pekee ili kila amwaminiye yeye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Alisema kanuni nyingine muhimu, ni mwanadamu kukataa kuziruhusu dhambi kumtenga na Mungu kwa kuwa hajui upendo wala mpango wa Mungu katika maisha yake.

"Mungu alimuumba mwanadamu kwa makusudi ili ashirikiane naye lakini, inashangaza mwanadamu anapokwenda kinyume cha mpango wake. Yaani eti utafikiri Mungu alichagua amuasi kuliko kumtii," alisema.

Alisema kila mwanadamu hana budi kujua na kukiri kuwa Mungu ni Mtakatifu na wala hana na hataki dhambi wala ushirika wowote wa dhambi yoyote baina yake na mwanadamu.

Aliwataka Wakristo kudumu katika juhudi za kumtafuta ili kumfikia Mungu kwa njia nyingi kwa matendo mema, sala za kuomba msamaha na baraka na sadaka.Aliitaja kanuni nyingine kuwa ni kuondoa dhambi ambayo ni kikwazo cha mahusiano mema na Yesu Kristu kwa kuwa alikufa kwa ajili ya wanadamu ili wajue upendo wa Mungu na mpango wa Mungu kwa maisha yetu kwa maana Kristu aliteswa kwa ajili ya dhambi.

"Mwanadamu peke yake hawezi kushirikiana na Mungu bila kuwa pamoja naye kwa kuwa Yesu alikufa msalabani ili awe daraja kati watu na Mungu," alisema.Alisema kanuni nyingine bora kujenga urafiki imara na Mungu, ni mwanadamu kumpokea Yesu ili awe mwokozi na mtawala katika maisha yote.

Kwa maana mmeokolewa kwa njia ya imani ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu ni kipawa cha Mungu wala si kwa matendo. Mtu yeyote awaye, asije akajisifu," alisema akinukuu kitabu Cha Waefeso 2:8-9

Mzee huyo wa Kanisa Bw. Romano Daudi, alifafanua kuwa, mwanadamu hatakiwi kutegemea mawazo ya moyo wake bali aongozwe na mapenzi ya Mungu.

"Unaweza kujisikia leo una furaha lakini, kesho ukawa na huzuni kwa vyovyote utakavyojisikia" alisema na kuongeza kuwa Yesu Kristo habadiliki.

Katibu wa Askofu ahimiza jamii kusameheana

Na Waandishi Wetu

KATIBU mpya wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Padre Andrew Luanda, ameitaka jamii kujijengea utamaduni bora wa kuombana msamaha na kusameheana unapotokea kutokuelewa ili kudumisha amani, umoja na upendo.

Padre Luanda aliyasema hayo mwanzoni mwa juma alipokuwa akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu jijini Dar-Es-Salaam.

Akinukuu Maandiko Matakatifu ya Biblia (Mat.18:15-17), alisema kuwa iwapo ndugu amekosea, mkosewa hana budi kwenda kumuonya nduguye kwa upendo na kwa lengo la kusameheana. Tena wakiwa peke yao.

Padre Luanda alisema watu wenye busara, hekima na upendo wa ki- Mungu, ni muhimu sana kuombana radhi na kuwa tayari kusameheana kama alivyofundisha Bwana Yesu Kristo na akasisitiza kuwa endapo ndugu huyo hatataka kusikia, mkosewa hana budi kumchukua ndugu mwingine mmoja au wawili ili wakatafute mapatano baina yao. "Akikusikia, utakuwa umempata ndugu yako," alisema na kuongeza, "Kama hatakusikia, mchukue ndugu yako mwingine au hata wawili ili kwa vinywa vya mashahidi hao wawili, kila neno lithibitike na asipowasikiliza hao kaliambie Kanisa."Aliendelea kusema kuwa endapo nduguyo mkosefu ataendelea kutokulisikiliza hata Kanisa, basi mchukulie kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru."

Katibu huyo mpya ambaye amaeteuliwa kushika nafasi hiyo hivi karibuni baada ya kupata Daraja ya Upadrisho aliwataka mapadre , watawa na watumishi wote wa Mungu wenye mapenzi mema, kuombeana na kutakiana heri katika maisha ili waifanye vyema kazi ya kuwachunga "kondoo" wa Mungu.

Padre Andrew Luanda na Padre Charles Raymond, ni "matunda" ya kwanza kuchumwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini ambaye aliwapa Upadrisho Julai 14, mwaka huu katika kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu la jijini, baada ya Askofu Kilaini kupewa Uaskofu katika viwanja vya kanisa Katoliki la Msimbazi jimboni humo Machi 18, mwaka huu

Mabadiliko ya uongozi na nyadhifa katika Kanisa, ni ya kawaida ili kujenga na kupanua wigo wa watumishi wa Mungu kufahamiana zaidi toka kitengo au sehemu moja hadi nyingine.

‘Life Ministry’ wataka jamii isiwe na maisha vuguvugu

SHIRIKA la Kuhubiri Injili kwa Kushirikiana na Makanisa (Life Ministry Tanzania), limesema Wakristo hawana budi kuyakana maisha ya kuwa vugu vugu baina ya mambo ya dunia na mapenzi ya Mungu; anaripoti Elizabeth Steven.

Mwinjilisti Yohane Japhet Hassan, wa Shirika hilo lililopo jijini Dar-Es-Salaam, alitoa wito huo wakati akihubiri katika ibada ya kanisa la Moravian Tanzania Ushirika wa Keko Wilaya ya Mashariki , Jimbo la Kusini iliyofanyika katika Kanisa la Pentekoste Tanzania (KLPT) parishi ya Keko Machungwa, Jumapili iliyopita.

Makanisa hayo hutumia kanisa moja la KLPT kwa kuwa ujenzi wa kanisa la Wamoravian haujakamilika na uko mbio kumalizika.

Alisema inashangaza kuona kuwa watu wengi wanaojiita Wakristo, hawaishi maisha ya Kikristo kweli yakiwemo yale yanayohimizi maombi na sala na badala yake, wanakuwa mstari wa mbele kuenenda kinyume kwa kusingizia matatizo mbalimbali wanayokumbana nayo yakiwamo ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

"Lazima Wakristo waishi kwa kumpenda na kumtegemea Mungu kama alivyoishi Kristo, yeye hakuwa vuguvugu, aliishi kwa kumtegemea Mungu kikamilifu kwa maombi na sala zenye imani," alisema na kuongeza, "Ingawa ni dhahiri utapata vikwazo vya kukutenganisha na Kristo, ni lazima umtumainie ili upate kuvishinda na kuzidi kuishi katika imani."Alisema kufuatia ugumu wa maisha na hali ya uchumi, baadhi ya waamini wamejenga kasumba mbaya ya kuishi mguuu mmoja kwa Mungu, na mwingine duniani na akaongeza kuwa ugumu huo kisiwe kisingizio cha mwanadamu kukubali kutenganishwa na Mungu.

"Imefikia hatua hata watu wengine wanatumia nguvu za giza kama uchawi kutatulia matatizo yao badala ya kuyakabidhi kwa Yesu.

Alipoulizwa na gazeti hili endapo anadhani hata mambo ya mila na desturi ikiwamo ngoma na michezo mbali mbali vinachangia jamii kuishi maisha hayo ya vuguvugu, Mwinjilisti Yohane alisema, "Mila nyingine ni nzuri na nyingine huleta machafuko katika jamii, hizo lazima Wakristo tuziepuke. Michezo kama michezo ndani ya mila nzuri husaidia kuimarisha urafiki na kujenga mwili."

Katika ibada ya siku hiyo, Wakristo wa kanisa la Moravian walichanga jumla ya shilingi 40, 460/= kwa ajili ya ujenzi wa kanisa lao.