Make your own free website on Tripod.com

Makala

Kwa nini mpango wa Uzazi?

Vitumike vidonge, vitanzi, sindano au...?

Mara nyingi watu wamekuwa wakitumia dawa za kuzuia uzazi bila kujua maana na hathari zake. Katika Makala haya, Mwandishi Maalum anaeleza maana na athari za matumizi ya madawa hayo kama Shirika la Kutetea Uhai la Pro-Life Tanzania, linavyoyatazama.

Maana:

kupanga uzazi kwa njia za kisasa ni kuamua juu ya mpishano wa watoto kati ya mtoto mmoja na mwingine na kuamua juu ya idadi ya watoto wa kuzaa katika ndoa.

Uzazi wa mpango kwa njia za kisasa hutumia madawa zikiwamo kemikali zilizomo katika vidonge vya majira, vitanzi sindano ya depo provera, vipandikizi, lunelle emergency contraceptive na quinacrine

Pia njia nyingine zitumikazo kupanga uzazi ni kwa kutumia kondomu na kutoa mimba.

AFYA YA UZAZI humaanisha kuwafanya wanawake wenye ndoa na wasio na ndoa, hasa wanafunzi mashuleni, kufurahia ngono bila kuwa na wasiwasi wa kupata mimba na magonjwa ya zinaa ikiwemo UKIMWI.

Hii, hutokana na kujiamini kwa kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango zikiwamo kondomu na kutoa mimba.

Dawa ya uzazi wa mpango hufanya mayai ya mwanamke yasikomae; hupunguza uwezo wa kusafirisha mimba katika mirija ya uzazi; huharibu ngozi nyororo ya tumbo la uzazi kwa namna kwamba mimba iliyotungwa hushindwa kujipandikiza; hutoa mimba kwa mimba hiyo kushindwa kukaa na kukua katika tumbo la uzazi.

Ni hatari na dhambi kupanga uzazi kwa kutumia njia za kisasa

Kwa miaka yote, Kanisa Katoliki limefundisha kuwa ni dhambi kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango. Si vidonge wala sindano vilivyo muafaka kwa shughuli hii ya kupanga uzazi bali tu, njia za asili zinazofuatazo maumbile.

Kanisa limefundisha hivyo kutokana na kweli za kiimani zilizomo katika Biblia Takatifu ambazo zinafafanuliwa katika hati mbalimbali za kichungaji kama vile "Uhai wa Binadamu (Human Vitae)" na "Injili ya Uhai(Evengelium Vitae)".

Kweli hizi za kiimani zinatufundisha kuwa binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwa. 1:26).

Uwepo wa binadamu mpya hutegemea kuwepo kwa muunganiko halisi na bayana wa mbegu ya baba, yai la mama na pumzi hai ya Mungu. Baada ya muungano huo, uhai unakuwa ni kitu kitakatifu.

Ndiyo maana tunaamriwa na Mungu tusiue (Kuto. 20:13). Amri hii haihusu tu uhai wa watu waliokwisha zaliwa, bali inahusu pia, tena zaidi watoto wasiozaliwa bado kwani hawawezi kujitetea.

Mungu anamuumba binadamu kila mmoja kwa ajili maalum. Tangu tukingali katika matumbo ya mama zetu, Mungu anatupangia jinsi tutakavyokuwa(Isaya 49:1-3,5; Jer.1:5).

Baadhi yetu tulipangiwa kuwa madaktari ili kutibu magonjwa ya binadamu, wengine mapadre, wachungaji, maimamu; wengine wamepangiwa kuwa wakulima. Kila binadamu hata kama bado yumo tumboni ni binadamu hai anayedumu.

Tofauti kati yetu na huyo aliyemo tumboni ni kuwa, tumboni hatumwoni kwa macho lakini anajimudu kama kiumbe hai (Lk.1:41).

Tunapotafakari umuhimu na utakatifu wa uhai wa bindamu, hatuwezi kufumbia macho vitu vinavyoharibu au kuua uhai huo.

Sumu zote zinazotumika katika kile kiitwacho "kupanga uzazi kwa njia za kisasa" huondoa uhai na huharibu afya. Sumu hizi zinaingizwa hapa nchini Tanzania na kutekelezwa chini ya mwamvuli wa "afya ya uzazi(reproductive health) na haki ya kujamiiana (sexual rights).

Zipo sababu nyingine zinazolifanya Kanisa Katoliki kupinga njia za kisasa za kupanga uzazi. Hii ni kwa kuwa Mosi, njia hizo huua.

Njia za kisasa za uzazi wa mpango hutumia sumu zilizomo kwenye vidonge vya majira, vipandikizi, vitanzi, sindano ya depoprovera, emergency contraceptive, 1uinacrine RU 486 na nyinginezo, zina kemikali zinazoua uhai mpya kabla ya mwanamke hajajua kama ana mimba.

Kwa kadiri ya Dk. Bogomiro Kuhar, vita dhidi ya uhai wa watoto kupitia njia za kisasa za kupanga uzazi husababisha vifo vya watoto kati ya milioni 8.1 na 12.75 kila mwaka katika mataifa ya Ulaya na Marekani.

Kwa hiyo njia hizo huwa ni chanzo kikubwa cha utoaji mimba na ikitokea kuwa mwanamke anayetumia njia hizo amepata ujauzito licha ya matumizi yake, ataita mimba (mtoto) hiyo isiyotakikana (unwanted) na kitu kisichotakikana hakitakiwi kwa hiyo huuawa.

Kwa hiyo, mwanamke Mkatoliki anayetumia njia hizo huwa anaua hata kama ni kwa kutojua.

Na kosa la kuua kwa kadri ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki, ni kutengwa na Kanisa moja kwa moja (Iba. 2272). Utoaji mimba na uuaji wa mtoto ni maovu ya kuchukiza mno (GS 51 aya 3 na Katekisimu Iba.2271).

Pili, Sumu hizo za kuharibu uhai huwafanya watumiaji washindwe kuwa waaminifu katika maisha yao.

Hali hii inahusu wanawake walioolewa na wale ambao bado hawajaolewa. Mwanamke akijua kuwa anaweza kufanya zinaa bila kuwa na hofu ya kupata ujauzito anaanza kujiona huru na kuvunja heshima iliyomlinda utakatifu wa tendo la ndoa kwa miaka mingi.

Vijana wa kike na wa kiume wanahimizwa kutumia sumu hizi kwa lengo la kukwepa mimba ambazo zingekatisha masomo yao, au zingeleta aibu kwa familia. Tumepata kushuhudia katika mazingira yasiyokuwa ya kawaida, wanawake ambao waume zao wameondoka kwa muda mrefu, kimasomo au kikazi wametumia sana sumu hizi.

Baadhi wamepata mafarakano katika familia. Aidha, vijana wanapojiingiza katika matumizi ya sumu hizi hukosa adabu na heshima kwa jamii.

Matokeo ya kushindwa kujiheshimu ni kuongezeka kwa magonjwa ya zinaa ambayo ni pamoja na ukimwi. Ndiyo maana vifo vitokanavyo na ukimwi vitaongezeka hadi pale jamii itakapobadilisha tabia na mienendo yao.

Waasisi na watetezi wa uzazi wa mpango kwa njia za kisasa, Marie Stopes a Margaret Sangu walisema, lengo la njia hizo ni kuwaweka wanawake katika vifungo vya ndoa na hivyo hufurahia bila mipaka.

Pia Sumu za ‘kupanga uzazi’ kwa kiasi kikubwa husababisha kuvunjika au kuvurugika kwa ndoa.

Utafiti unaonyesha kuwa asilimia 50 ya ndoa zinazotumia sumu za ‘kupanga uzazi’ huvunjika miaka michache kwani huharibu uzazi ambao unaonekana kama ugonjwa(ndiyo maana zinaitwa dawa ya kupanga uzazi).

Watu hawa hawawezi kujitoa kila mmoja kwa mwenzake katika tendo la ndoa. Pazia linawekwa kati yao.

Wao wenyewe wanatengana nafsi zao na wanajitenga pia na Mungu.