Ukosefu wa taaluma unavyowaathiri wanawake

Na Josephat Kiboga

UPUNGUZAJI wa wafanyakazi unaofanywa na serikali katika harakati za kusimika mfumo wa uchumi wa soko huria nchini umekuwa kukiwaathiri zaidi wanawake kuliko wanaume.

Katika moja ya taasisi za fedha nchini, barua za kupunguzwa kazi zinatolewa kwa wafanyakazi kwa kile kinachoitwa "kubana matumizi", na kuwapatia maslahi bora zaidi wale wafanyakazi wanaobakia.

Zoezi hili linatekelezwa kutokana na mapendekezo ya taasisi za fedha za kimataifa.

Aidha, lengo lingine la zoezi hilo ni lile linaloelezwa kuwa ni kuboresha shughuli za taasisi hiyo ya Tanzania ili kuiwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi na kwa faida katika hali ya ushindani wa kibiashara.

Zoezi hilo si tu linawachanganya akili wafanyakazi wa taasisi hiyo ambao majina yao yamo katika orodha hiyo ya kupunguzwa kazi (redundancy), bali pia linaweka ‘roho juu’ hata wale ambao majina yao hayamo katika orodha hiyo, kwani kuna fununu kuwa wafanyakazi zaidi watapunguzwa siku za usoni.

"Hakuna anayejua hatma yake, kwani waweza ‘kupona’ awamu hii, lakini ukakumbwa katika awamu nyingine," anabainisha mmoja wa wafanyakazi wa taasisi hiyo, Bi. Asha Abdul.

Vile vile, tangazo la kuwataka wale ‘wanaojisikia’ kustaafu kuomba kufanya hivyo halijawatuliza wafanyakazi hao ambao wengi wao ni wanawake wakiwa ni makarani wa fedha na wahudumu wa ofisi katika taasisi hiyo.

Hali hiyo ipo pia katika mashirika, makampuni na taasisi za serikali ambazo zinauzwa, kubinafsishwa au zinafilisiwa kutokana na kuonekana kuwa zinaendeshwa kwa hasara.

Katika utekelezaji huo wanaoathirika zaidi, pia ni wanawake.

Wakati wa upunguzwaji wa wafanyakazi, makatibu wahtasi, wahudumu wa ofisi, makarani wa malipo na maafisa wengine wa ngazi za kati wengi wao wakiwa wanawake, ni baadhi ya watu ambao wanatupiwa macho na bodi za vyombo hivyo ambazo zinaundwa na wajumbe wengi wanaume kuliko wanawake.

Katika idadi ya wafanyakazi 5,684 waliopunguzwa mwaka jana huko Arusha na Dar es Salaam, idadi ya wanawake ni 3,047 , ambayo ni sawa na asilimia 5.6 ya idadi yote.

Pamoja na idadi ndogo ya wanawake walioajiriwa katika sekta mbalimbali za umma, vile vile kumekuwa na idadi ndogo ya wanawake walio katika nafasi za juu ambazo ndizo zilizo na maamuzi ya mwisho katika masuala mbalimbali likiwemo lile la kuwapunguza wafanyakazi.

Utafiti uliofanywa nchini na Profesa Luhanga wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unabainisha kuwa hadi mwishoni mwa mwaka 1991 kulikuwa na wanawake 5,434,106 ambao ama wamejiajiri wenyewe au wameajiriwa katika sekta mbalimbali.

Kati yao wengine walikuwa wahadhiri katika vyuo mbalimbali, wataalamu, wahudumu katika maduka, wafanya mauzo, makarani, waendesha mashine na vibarua wa mauzo nafasi ambazo haziwapi uwezo wa juu katika maamuzi ya ajira.

Wanawake nchini ambao ni asilimia 60 ya watu wote kwa mujibu wa sensa ya mwaka 1988 wanakabiliwa na tatizo hilo la kuonekana kama watu ambao hawawezi kufanya jambo wenyewe hali ambayo inakwamisha uwezekano wa kuwepo kwa uwiano katika nafasi za ajira na maamuzi mengine kati ya wanaume na wanawake.

Utafiti uliofanywa na Profesa Fredrick Kaijage, umebainisha kuwa asilimia 1.5 ya wanaume walikuwa wameajiriwa katika taaluma za juu mwaka jana, wakati wanawake ni asilimia 0.2 tu, walioajiriwa katika kiwango hicho cha juu.

Katika nafasi za ukarani na ulipaji malipo, wanawake walioajiriwa ni asilimia 19.0, wakati wanaume ni asilimia 15.3 tu.

Utafiti huo vilevile umeonesha ni jinsi gani wanawake wengi wameajiriwa katika nafasi za chini ambazo haziwapi uwakilishi katika bodi na vikao vingine vikubwa vyenye kutoa maamuzi mbalimbali.

"Wengi ni wauuguzi wa kawaida, walimu, makarani, makatibu wahtasi na wale wanaoshikilia kazi nyingine za aina hizo," imeeleza sehemu ya ripoti ya utafiti huo na kuongeza kuwa ni vigumu kwa wanawake walio katika nafasi hizi kuweza kujitetea dhidi ya maamuzi ambayo yataonekana kuwa si ya haki kwao.

Hali hiyo siyo tu imewaathiri wanawake peke yao, bali pia na familia zao, kwani wanawake wamekuwa wakitumia asilimia 84 ya kipato chao kwa matumizi ya nyumbani hususani kwa ajili ya chakula japokuwa asilimia 90 ya wafanyakazi wote ni wanaume.

Hayo yote ni kwa mujibu wa "utafiti juu ya kujitosheleza kwa chakula kwa familia zinazoongozwa na wanawake" uliofanywa na wahadhiri waandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kapunda na Evelne Maje.

Hali hiyo ya kutegemewa zaidi na familia zao ni kati ya mambo ambayo, kwa kiasi kikubwa yamepelekea kuporomoka kwa maadili katika jamii ambapo mara nyingi hutokana na kushindwa kujikimu kwa familia.

Imeelezwa kuwa sababu kubwa ya ajira duni, kipato kisicho kidhi mahitaji, na kazi zisizo za kitaaluma kwa wanawake katika sekta zote za umma na za binafsi zinatokana na ukosefu wa elimu ya kutosha ya ufundi na mafunzo ya upande wao.

Athari hizo na nyinginezo zinazotokana na ukosefu wa ajira ambao kwa kiasi fulani unatokana na mabadiliko ya kiuchumi.

Kwa hiyo, serikali na taasisi nyingine za masuala ya kijamii, hazina budi kuikabili hali hiyo kwa kuwasaidia wanawake.

Muundo huo wa sera na upangaji wa mipango ya maendeleo ulengwe katika kuwaongezea nguvu za kiuchumi wanawake na kuwafundisha mbinu mpya za kujiongezea kipato.

Hii ni pamoja na kuwarahisishia upatikanaji wa mikopo ya biashara.

Vyama vya mikopo ni vyombo ambayo ni lazima vitangazwe na kuelewesha vyema kwa wanawake ili waweze kuvitumia kwa ajili ya kukopa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo kwa lengo la kipato maridhawa.

Jitihada madhubuti za kuweka usawa wa kijinsia zinapaswa zifanyike kihalisi na wala si kimila ili mabadiliko hayo yaende sambamba na uboreshaji wa hali ya wanawake waliostaafishwa na kupunguzwa kazi kwa sababu mbalimbali.

Serikali inapaswa kulinda ajira za wanawake kuwashirikisha katika maamuzi yanayowahusu wao pamoja na kuweka mazingira mazuri ya elimu ambayo yataondoa hali ya wanawake wengi kufanya kazi ambazo si za kitaaluma.

Wagombea waeleze watafanya nini, kwa njia gani

KAMPENI za Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini 29 Oktoba, 2000 kwa mara ya pili chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa zinaendelea huku zikiwa zimebaki siku chache tu, ufanyike.

Hotuba nyingi zinazoambatana na kampeni hizo zinatoa ahadi za kuvutia kiasi cha kuwafanya wananchi kuamini kuwa baada ya uchaguzi, jamii ya Watanzania itakuwa peponi. Mwandishi wetu ROBERT MFUGALE anafafanua zaidi katika makala hii.

SI jambo jipya! Watanzania tunayo matatizo mengi katika nyanja za uchumi na huduma za jamii kama vile elimu, afya na maji.

Baadhi ya matatizo hayo ni sugu kiasi kwamba wananchi wengi wanayachukulia kama ni jambo la kawaida; donda ndugu lisilotibika.

Lakini inaelekea matatizo hayo na mengine mengi yatatokomea ifikapo Novemba 2000, baada ya Uchaguzi Mkuu ujao kulingana na hotuba na ahadi zinazotolewa na wagombea mbalimbali katika mikutano ya kampeni!.

Wagombea wa nafasi ya Urais, Ubunge, na udiwani wamekuwa wakitoa ahadi ambazo kama zikitimizwa, Tanzania itakuwa sawa na Pepo.

Ni dhahiri kuwa hotuba za kampeni zina lengo la kuwashawishi na kuwavutia wapiga kura; basi walao zishabihiane na hali halisi .

Lakini, ni dhahiri pia kuwa wagombea wengi hawana habari na kero halisi za wananchi, kiasi cha kuwachukulia wananchi hao kuwa kama watoto wadogo au wapumbavu.

Kwa mfano, mgombea fulani wa kiti cha urais aliripotiwa na vyombo vya Habari akisema kuwa akichaguliwa kuwa rais, atahalalisha umalaya na uzururaji!

Katika mkutano huo wa kampeni, vijana waliohudhuria walimshangilia sana mheshimiwa huyo kwa kauli hiyo, kuonesha kufurahishwa kwao. Watu wazima walibaki wakitazamana kwa mshangao.

Mgombea mwingine wa urais amesema akichaguliwa tu, atawalipa posho kwa miezi mitatu wananchi wote wasiokuwa na ajira! Mtu yeyote mwenye busara atakuwa na wasiwasi kama mgombea huyo anaelewa vyema uzito wa suala zima la ajira na limeathiri kiasi gani cha wananchi mijini na vijijini.

Mbaya zaidi, mgombea huyo hata hakueleza fedha hizo atazipata wapi na atazigawaje nchi nzima.

Mwingine amesema akichukua madaraka atafukuza askari wote wa usalama wa wananchi! Hakueleza akiwaondoa polisi, usalama wa wananchi utalindwaje wala hakuona umuhimu wa kuwaambia waliohudhuria na wananchi kwa ujumla polisi hao akishawafukuza atawapeleka wapi, wakafanye nini!

Wengine wengi huzungumzia kufuta kodi wakichukua madaraka. Ahadi hii na zingine zilizo elezwa hapo awali ni za kuwafurahisha wasikilizaji na kuwafanya kana kwamba wao ni mabwege.

Ni nchi gani ulimwenguni imeendelea bila kukusanya kodi? Ni kweli inasemekana kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi zenye kodi nyingi na kubwa, lakini tatizo la kodi haliwezi kuondolewa kwa kuzifuta tu, kodi hizo.

Je, zikishafutwa mapato ya serikali yatapatikanaje? Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema katika moja ya hotuba zake, "Serikali ‘corrupt’ haikusanyi kodi."

Kwa mtazamo wa harakaharaka, mheshimiwa anayeahidi kufuta kodi anatarajia kutuletea serikali ya wala rushwa? Anataka wananchi wamwelewe vipi?

Si vibaya kwa mgombea kutoa ahadi katika mikutano yake ya kampeni.

Lakini, walao kwa heshima ya wale wanaomsikiliza ambao anatarajia watampa kura, ahadi hizo hazina budi kupatiwa maelezo yakinifu, na ziwe zinaweza kutekelezeka na kutimizika.

Juma Salum Lilingani, mgombea wa udiwani kwa tiketi ya Chama cha NCCR - Mageuzi katika kata ya Mbagala jimbo la Kigamboni jijini Dar-Es-Salaam, anahoji ahadi za kuwafurahisha wananchi zinatolewa na baadhi ya wagombea.

Anasema "Mtu utaahidi vipi barabara ya lami wakati hata huwafikirii wananchi watajikinga vipi na magonjwa yanayozuilika. ona jinsi watu wanavyokula ovyo vitumbua na maandazi yaliyoko kando kando ya barabara.

Hakuna anayesemea hayo. Kipindupindu Dar-Es-Salaam hakiishi lakini, hakuna anayeahidi namna ya kutokomeza janga hilo."

Lilingani anaamini kuwa kwanza mgombea yeyote asiahidi kitu, kwa sababu hawezi kuwa na uwezo wa kuleta chochote bila ushirikiano na ari ya wakazi wenyewe kutaka kuleta maendeleo wenyewe. Pili,

"... anzia na kero za mahali pale ulipo, badala ya kuahidi maajabu yasiyotekelezeka," anasema Lilingani.

Kwa kutumia mantiki hiyo, mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Rais Benjamin Mkapa, wakati wote anaponadi sera za chama chake na kuomba apewe nafasi nyingine kuiongoza Tanzania, huzungumzia ‘...ushirikiano na nguvu za wananchi... kama ni nyenzo muhimu iliyoleta maendeleo yaliyopo na yatakayokuja.

Tatizo moja kubwa kuhusu ahadi na mikutano ya kampeni ni kwamba, wengi wanaohudhuria huelekea kufurahia kudanganywa; ni wachache tu wanaoweza kupambanua kati ya masuala na makandokando.

Wengine hufurahishwa tu na msamiati, au kauli anazotoa mgombea na kudhani huyo ndiye anayefaa au chama hiki ndicho kinachofaa. Kuna wanangangari chama dume, wafurukutwa, wakereketwa, n.k wengine hufurahishwa tu na vikundi vya ngoma na kushabikia vyama husika huku wakiahidi kuwapigia kura wagombea wake.

Joe Kadhi, mhadhiri wa siku nyingi katika uandishi wa habari chuo kikuu cha Nairobi nchini Kenya, aliwahi kuwaasa wahariri kuchambua vema habari za uchaguzi zinazotolewa na maripota wao.

Aliwataka wao wenyewe na maripota kutofundisha kati ya masuala (issues) na makandokando au mapambo (appearance and hoopla) pale wanapohudhuria mikutano ya kampeni au mikutano mingine ya kisiasa ambapo watu hunadi sera za vyama vyao.

Na hilo ni jambo muhimu kwa wananchi kulielewa. Nyimbo za kuvutia kauli za majigambo, kauli za kubeza wagombea wa vyama vingine, na ahadi za ahera ni ‘appearance and hoopla’, siyo masuala.

Masuala ni mtafuta kura anaelewa kero na matatizo halisi ya wananchi katika ngazi anayogombea?

Je, anaeleza katika mikutano yake atayatatuaje? Haitoshi kwa mgombea kusema atahakikisha chuo kikuu kinajengwa Sumbawanga, bali ni muhimu kueleza pamoja na mambo mengine fedha za kujengea atazipataje kwa nini chuo kikuu ni kipaumbele kwa Sumbawanga wakati huo.

Kama haelezi hayo basi ni wajibu kwa wanaomsikiliza kumtaka afafanue.

Haitoshi kwa mgombea kuahidi atatokomeza rushwa akipata madaraka bila kufafanua atatekelezaje azma hiyo. Kama hafanyi hivyo ni wajibu wa wanaomsikiliza kumwuliza.

Pamoja na kuwataka wagombea kufafanua ahadi zao, ni muhimu waulizwe maswali yanayohusu masuala. Wananchi wasiridhike tu na kumsikiliza mgombea na kurudi makwao.

Jinsi mtafuta kura atakavyojibu maswali ndivyo atakavyoonesha upeo wake wa kuelewa mambo, uelewa wake wa sera za chama chake na uwezo wake wa kuongoza katika ngazi aliyoomba.

Kwa jinsi hiyo, mwananchi atakuwa amepata nafasi nzuri ya kumpima na kutekeleza uamuzi wake na haki yake siku ya kupiga kura.