Makala

Ujue ugonjwa wa ukoma

Huu ni ugonjwa wa kuselelea unaoanza pole pole tena kwa muda wa miaka mingi.

Ugonjwa wa ukoma hauambukizi kwa urahisi isipokuwa, kama mtu ataambatana na mtu mwenye ukoma kwa muda mrefu sana, huyo, inawezekana naye akaupata.

Dalili:

Dalili za ugonjwa huu zinatofautiana sana kutegemeana na kinga ya kibinafsi ya mtu dhidi ya ugonjwa huu.

Kwa kawaida, dalili kuu huwa ni zile za kupoteza hisi. Mara nyingi ugonjwa wa ukoma huanzia mashambulizi yake katika mikononi na miguuni. Mara kwa mara wagonjwa wa ukoma huugua bila kufahamu.

Dalili nyingine muhimu ya ugonjwa huu ni kufa ganzi(vidonda na makovu).

Dalili katika ngozi zinatofautiana, nazo ni madoa meupe yenye ganzi katikati, kuvimba kwa mishipa ya fahamu(nerve) ngozi, na madonda makubwa ambayo hayaumi wala kuwasha.

Katika kila aina moja ya ukoma, ngozi ya uso huwa na yenye vinundu vinundu vingi au masikio manene mafupi na nene na yenye umbo la mraba na hata nyusi za uso, hudondoka kabisa.

Inaelezwa kuwa ukianza kukumbwa na ugonjwa huu, nyusi zinapotea, sikio nene la mraba, mishipa ya neva huwa minene na utapatwa na madoa yenye ganzi.

Ugonjwa huu unapopevuka, mikono na mguu huwauwa imepooza kiasi na kuwa kama makucha.

Vidole vya miguu na mikono au miguu na mikono yote, inaweza kufupika taratibu na kuwa vigutu.

Tiba ya Ukoma:

Kumbuka kuwa, ingawa ugonjwa wa ukoma unaponyeka, unahitaji dawa zitumike kwa miaka mingi na dawa iliyo nzuri kwa matibabu ya ugonjwa huu, ni "Sulphones".

Hakikisha kuwa kipimo kinachoagizwa ni kidogo sana na kinaongezwa taratibu mpaka kipimo kamili kinafikiwa baada ya miezi mingi. Kumbuka kuwa, mgonjwa natakiwa

kufuata maagizo ya wataalamu barabara.

Kukinga mikono na miguu kutokana na madhara.

Majeraha makubwa na vilema vya mikono na miguu ambavyo mara kwa mara vinaonekana kwa watu wenye ukoma, havisababishwi na huo ugonjwa wenyewe na vinaweza kukingwa.

Mara nyingi majeraha hayo yanatokana na sehemu iliyokufa ganzi iwapo mgonjwa mwenyewe hajikingi na vitu vyenye kumdhuru.

Kwa mfano, mtu mwenye afya nzuri akitembea kwa muda mrefu na akianza kupata malengelenge miguuni, atasikia maumivu na hata atasimama kujiangalia na kujiweka katika hali ya usaidizi au basi atachechemea hadi afike alipokusudia.

Tofauti kwa mtu mwenye ukoma ni kwamba, yeye hata akipata majeraha kama hayo, hatasikia maumivu. Ataendelea kutembea na lengelenge hilo na hatimaye litakuwa donda.

Donda hili litaambukizwa na litakuwa haliumi. Hatakuwa na muda wa kuliangalia wala kuliachia lipone.

Kwa njia hiyo, vijidudu vitapenya taratibu mpaka kwenye mifupa na kuiharibu na kusababisha vilema maalum kutokeza.

Kwa uangalifu mzuri vilema hivi vinaweza kuepukwa.

Ili kuepuka matatizo kama hayo, hifadhi mikono na miguu kutokana na vitu vyenye kuweza kukata, kutoa malengelenge au kuchoma na wala usitembee miguu wazi hasa mahali ambako kuna mawe au miiba.

Vaa viatu au kanda mbili. Hakikisha unaweka ndani ya kiatu kitu laini cha kuzuia mikwaruzo.

Unapotumia mikono yako au unapopika chakula, vaa mifuko ya mikono(gloves). Usinyanyue sufuria au chochote kilicho na joto bila kwanza kuhifadhi mkono wako kwa mfuko mnene au kitambaa kilichokunjwa.

Hii ni kuepuka uwezekano wa wewe kuungua bila khisi kuwa umeungua.

Ikiwezekana, epuka kazi zinazohitaji kushika vitu vikali au vyenye joto mfano, unashauriwa sana usivute sigara.

Kila siku baada ya kazi au kutembea, tazama mikono na miguu yako kwa uangalifu au ikiwezekana mwambie mtu mwingine akusaidie kutazama. Hakikisha unatazama hasa kuona kama kuna majeraha, malengelenge au miiba.

Pia, tazama kama kuna alama katika mikono na miguu ambayo ni nyekundu, zimevimba au kutoa malengelenge. Unapoona chochote, pumzisha sehemu hiyo ya mwili mpaka ngozi ipone kabisa.

Kwa njia hii ngozi itakuwa na kovu zuri na lenye nguvu kuliko kuwa na lengelenge na ubichi. Kwa hiyo majeraha yanaweza kukingwa.

Pia, kama una jeraha au linaanza kutokeza, hakikisha sehemu hiyo inawekwa katika hali ya usafi na kupumzishwa mpaka pamepona kabisa. Kisha hakikisha kuwa hapapati jeraha tena.

Kama ukifuata masharti haya na kutibu mapema, vilema vingi vya ukoma vitaweza kuepukwa. Hivyo ni vema kila mwana jamii awe makini.

MIGOGORO NA VITA INAYOTOKEA AFRIKA

Yadaiwa kuwa ya kipindi cha mpito(3)

Inatoka toleo lililopita

Ni vingumu kuona watu wakipigana kwa sababu ya hali za kisiasa.

Ofisi ya Amani na Udhibiti wa Silaha itafanyaje ili kuzuia na kukomesha vita hivyo barani Afrika?

Fung anongeza kusema katika maelezo yake kuwa " Ofisi yangu haishiriki katika utoaji maamuzi ya usuluhishi wa migogoro kwa kadiri ya mtazamo wa kisiasa, ofisi iliundwa ili kutoa misaada kwa serikali za kiafrika katika juhudi zao mintarafu udhibiti wa silaha ,ujenzi wa moyo wa kuaminiana na wa misingi ya amani kamwe ofisi yangu haihusiki na utengenezaji wa sera za kuwabomoa wanachama wa mataifa hayo".

Anaongeza "shabaha yetu ni kutoa misaada ya utekelezaji wa maamuzi na makubaliano ya amani na Udhibiti wa silaha miongoni mwa mataifa yanayohusika na migogoro/vita hivyo.

Wauonaje Mustakabali wa Afrika?

Mkurugenzi huyo anasema "Mimi mwenyewe ni Mwafrika na nahusika na uzawa wa Waafrika wanaoamini kwamba mustakabali wa bara hili ni wa kuleta matumaini kile ambacho Afrika linakerwa nacho ni cha kipindi cha mpito, kwani mnamo karne ya kumi na nane Ulaya ilishuhudia migogoro na vita ambavyo havihitilafiani na haya yanayoikumba Afrika leo. Amerika ya Kusini na Asia nazo pia zimepata kukumbwa na migogoro na ufukara ambavyo ni madonda ya Afrika".

Tanbahi:

Ni lazima Bara la Afrika kufuata nyayo za maendeleo ya nchi za Ulaya?

Mwalimu Julius Nyerere alitoa dira na falsafa tofauti; ‘lazima tukimbie wakati mataifa ya Ulaya yanaelekea mwezini, hatuna budi sisi waafrika kukimbia kuongea kwa kasi katika kuleta maendeleo yetu, vinginevyo kamwe hatutaendelea’.)

Maisha na Mikasa

ASIYE NA VIGANJA VYA MIKONO ALIA AKISEMA

Kifafa kimeniletea 'ukoma' wa mikono yote nitaishije

lAlisema aliungua majirani wakasikia harufu ya nyama, kumbe ni yeye

lAlitekelezwa akadandia treni kuja Dar

lMarehemu Wazazi wangu, niiteni mnichukue

Na Dalphina Rubyema

MWANADAMU unaweza kuzaliwa na viungo vyako kamili lakini, ukweli kwamba kabla hujafa haujaumbika, ukajidhihirisha wenyewe baadaye.

Ukweli wa usemi huu tunaushuhudia katika matukio mbalimbali yanayotokea na kuwasibu watu kadhaa, ndani na nje ya nchi.

Wengi wamepoteza ama kiungo kimoja, ama idadi tofauti ya viungo vya mwili wake katika mikasa, matukio na hata pengine ajali au ugonjwa.

Bi. Yunis Mika, ni mwenye umri wa miaka 34. Yeye amezaliwa kama walivyo binadamu wengine akiwa na viungo vyake vyote na wala pasi na ulemavu wa aina yoyote.

Kwa kuwa kuishi kwingi ni kuona mengi, mama huyu katika kuishi kwake duniani, amejikuta akipoteza vidole vyake vya mikono yote miwili. Si kwamba alipigwa au kujeruhiwa aidha katika ajali au lolote la hasha.

Mwenyewe anasimulia yaliyomkumba hata sasa amegeuka kuwa ombaomba katika mitaa na barabara za jiji la Dar-Es-Salaam.

Anasema kuwa hali hiyo inayomsibu ya ulemavu wa mikono yote ambao hakuzaliwa nao, imetokana na ajali ya moto baada ya kuungua kutokana na matatizo ya afya.

Wengi inawawia vigumu kuamini kuwa je, ni kweli mtu unaweza kupoteza vidole vyote vya mikono, tena yote miwili kwa sababu ya moto?

Ni dhahiri kila mtu atajiuliza ni kwa vipi na ilitokeaje.

Au alikuwa anachezea moto? Lakini, sio mtoto mdogo kiasi cha kufikia hatua hiyo.

Yeye mwenye we amedokeza katika mazungumzo yake na gazeti hili jijini Dar-Es-Salaam, hivi karibuni kuwa, ulemavu wake aiupata baada ya kuungua kwa moto kutokana na ugonjwa wa kifafa.

Anatia huruma sana anaposema ingawa alikuwa na kifafa, masumbuko yake , yalitosha sasa itakuwaje na ulemavu wa mikono yote?

Bi. Yunis mwenyewe anasema ugonjwa huo wa kifafa ulianza kumsumbua tangu mwaka 1993.

Anasema tukio hili lililomsababishia kilema cha maisha, lilimtokea Aprili 3, mwaka huu katika eneo la kituo kikuu cha magari(mabasi) Mwanza ambapo alianguka chini na kupoteza fahamu.

Kutokana na kutokuwepo na mtu wa kumsaidia, alijialagaza huko na huko na katika hali hiyo, mikono yake iliingia kwenye moto uliokuwa karibu yake katika eneo hilo.

"Mimi zamani nilikuwa mzima kama wewe dada, nipe angalau shilingi 100 nikanunue dawa," alidai dada huyo na baada ya dada huyo(mwandishi wetu) kumpaalichokuwa nacho, Bi.Yunis aliendelea,

"Hali hii unayoiona imesababishwa na kuanguka kifafa. Niliungua moto, mimi ni mgonjwa, naanguka kifafa," alisema mama huyo wakati akihojiana na mwandishi wetu.

Kuonesha ni jinsi gani ombaomba wote wanavyomuogopa Mkuu wa Mkoa wa dar-Es-Salaam, Luten Yusuf Makamba, Bi. Yunis hakuamini sawasawa kuwa anaozungumza na mwandishi wa habari.

Ndipo ghafla akashituka,

"Dada! Mbona unaandika ninayozungumza! Wewe ni askari nini, niache niende hata msaada usinipe, nyie askari ni watu wabaya. Tunazungumza vizuri kumbe unataka unipeleke kwa Makamba," akalalama.

Juhudi za Mwandishi Wetu kumsihi Bi. Yunis aendelee kumsimulia mkasa huu kwa urefu, zilifanikiwa baada ya kumbembeleza kwa takribani dakika 20 hivi na hatimaye, akaendelea kusimulia historia yake.

"Sikiliza dada. Mimi nilizaliwa Mwanza, ni msukuma na nilizaliwa mwaka 1966 huko huko Mwanza mjini njia ya kuelekea Butimba.

Wakati wa usichana wangu, nilifanikiwa kuolewa na Baba mmoja lakini hatukuzaa mtoto na huyo baba tukaachana naye(anakataa kumtaja jina).

Wakati huo, nilikuwa na nguvu zangu zote kwa kuwa nilikuwa sisumbuliwi na ugonjwa wowote. Nikarudi kwetu kwa kuwa huyo mimi na huyo mzee aliyekuwa amenioa, tulikuwa hatuishi mbali sana na kwetu."

"Nilikaa naye kwa muda wa miaka sita. Tangu mwaka 1998 hadi 1987. Kwa vile katika muda huo hatukupata mtoto, basi nikaona bora tutengane. Isitoshe hata yeye alikataa kutoa ng’ombe kwa baba. Na hiyo nayo ikachangia sana.

Sasa nikaendelea kukaa nyumbani kwetu weee lakini, baada ya miezi sita, nikaanza kuugua ugua. Nikaanza kusikia watu wanasema eti kuanguka kifafa! Hata hivyo, nilivyokuwa ninaanguka na kuugua, ndivyo watu wenye kifafa wanavyofanya.

Sikuwa na la kufanya ndugu yangu. Sasa nifanye nini Mungu mwenyewe amependa hivyo.

Mwanzoni nilikuwa ninaugua kwa faraja na matumani ya kupona na kuishi vema na jamaa zangu kwa kuwa ndugu wengi walinisaidia mno kunitunza.

Cha ajabu na kinachoniliza mpaka leo hii ninaombaomba hivi, baada ya ndugu zangu kuona kuwa siponi, kadri siku zilivyoendelea, ndivyo mmoja mmoja kati ya hao ndugu zangu, alivyozidi kuniacha wala kunijali; kila mtu akawa hana taimu na mimi. Mpaka sasa dada.

Nilipoona hali inazidi kuwa mbaya, niliona bora niende mjini Mwanza kuomba msaada kwa wasamaria. Sasa ningefanyaje, nifie ndani kama mnyama huku nina watu lakini hawanijali?

Ni kweli dada nilikuwa ninateseka kweli hata chakula licha ya kuwa mgonjwa nilikuwa ninakibahatisha. Sasa ukawa ugonjwa na njaa.

Basi, kulala kwangu kukawa ni Stendi ya Mwanza huku nikiwa naombaomba na usiku ukifika, nawasha moto ili nipate joto."

Bi Yunis anazidi kudokeza kuwa, katika maisha hayo ya uhamishoni katika stendi ya Mwanza, hakuwa peke yake , bali alikuwa na ombaomba wenzake wengi tu wa kutoka maeneo mbalimbali na wenye matatizo yao tofauti.

Anaendelea kusimulia. "Siku hiyo ya tarehe 3 mwezi wa 4 mwaka huu nilienda kufanya shughuli zangu za kuomba. Ilipofika saa 11 jioni hali yangu ilianza kubadilika.

Nilijua kabisa kwamba huo utakuwa ni ugonjwa wangu wa kifafa. Hivyo, sikutaka kuendelea na kazi. nikaamua kurudi Stand na ilipofika saa 1 kama na nusu hivi jioni, nikawasha moto. kumbe siku hiyo nikaanguka kifafa.

Nasikia mikono yangu yote Mungu wangu; nikaiweka kwenye moto. Watu waliokuwa ng’ambo ya pili ndio waliokuja kuniokoa.

Nasikia eti walisikia harufu ya nyama ya kuchoma ndipo wakataka kujua nini kinaunguzwa. kumbe naona hiyo ilikuwa mikono yangu motoni baada ya kutapatapa bila kupata msaada.

"Mama, mama, Baaba, jamani wazazi wangu nyie marehemu niiteni mnichukuwe," anapaza sauti mama huyo.

Mwandishi anambembeleza atulie na kuendelea na simulizi zake ambazo hakika ni za kusikitisha.

Nilivyopata fahamu na kusimuliwa yaliyotokea, kwa kweli nilisikitika sana. kilichonisikitisha zaidi ni vidole na mikono yangu," akaviangalia kisha akasema, "Sikutegemea kuwa nitakuwa hivi".

Alisema kuwa aliendelea na kazi ya kuvilea vidonda vyake bila msaada na alipoona haponi, akaamua kuja Dar-Es-Salaam kutafuta riziki kwa kuwaomba wasamaria wa wamsaidie kuitibu mikono yake.

Anasema bila kujali ambayo yangemkuta njiani, aliamua kudandia treni itokayo Mwanza kuja Dar-Es-Salaam. Njiani(Tabora), ilikuwa hali manusura kuteremshwa na wafanyakazi wa treni kwa kuwa hakuwa amelipia chochote lakini, alipoonesha mikono yake, kila mtu aliyemuona, alimuonea huruma.

Anasema hali hiyo ikawa imempa nafasi ya kufika Dar-Es-Salaam bila kulipa nauli.

"Wasafiri wenzangu walinisaidia kuninunulia hata chakula" anasema.

Anasema baada ya kufika jijini Dar-Es-Salaam bila kutarajia, alijitokeza mama mmoja aliyemtaja kwa jina la Mama-P. Huyo alimuonea huruma, akaamua kuondoka naye kwenda kuishi naye nyumbani kwake na hadi hivi sasa anaishi naye huko Yombo Madafu jijini hapa.

Anasema mama huyo ambaye amemtaja kuwa anafanya kazi katika Hospitali ya Huruma, alimtibia na gharama zote za hospitali alizipata yeye (Mama-P).

Hata hivyo, Bi. Yunis anasema kuwa bado vidonda vyake vinamsumbua kidogo. Hivyo, anaomba msaada toka kwa Watanzania na watu wote wenye mapenzi mema ili afanyiwe uchunguzi na matibabu zaidi.

"Naomba mnisaidie. Mama-P kanihudumia sana naye ni mtu wa familia, naomba hela nikafanye uchunguzi zaidi," anasema.

Anawaomba hata ndugu zake wamuonee huruma na wakubali kumpokea na kumtunza kwani yeye siyo mapenzi yake na hakujifanya, wala hapendi aanguke kifafa na kuishi maisha ya kuombaomba.

"Ni Mungu siyo mimi. Hata wao wanaweza wakapata maradhi kama haya yangu. Au watoto wao, tena bora mimi Kifafa wao wakipata... (kabla hajatamka ni ugonjwa gani, anabadilisha mawazo).

Ghafla Bi. Yunis anabadili mawazo na mtazamo wake na mwandishi wa mkasa huu, anasema, "Nipe hayo makaratasi unayoandika. Nimekumbuka wewe unatoka kwa Makamba. Sitaki. Nipe kabisa makaratasi yangu. Hata hiyo hela yako siitaki na wala usinipe tena," anasema Bi. Yunis na kabla ya kujibiwa anaondoka na kutokomea kwenye msongamano wa watu waliokuwa wakisubiri magari katika kituo cha Shule ya Uhuru jijini Dar es Salaam ambapo mahojiano hayo yalifanyika.