Majaji wa jazba vichochoroni wamepitwa na wakati

Na Josephs Sabinus

KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 13, ibara ndogo ya 6 sehemu (b) inasema, "Kwa madhumuni ya taratibu zinazofaa au zinazozingatia kwamba kosa la jinai hutendwa na mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo".

Hata hivyo, dhana hii ya makusudi ya kisheria inayomtaka mtu achukuliwe na kuhesabiwa kuwa hana hatia mpaka sheria itakapothibitisha vinginevyo bado haitiliwi maanani hata kidogo.

Nasema hivyo kwani kwa kawaida mtu anapokamatwa na kuwekwa mikononi mwa watu, polisi au utawala wowote kwa tuhuma fulani, haimaanishi kuwa ana hatia, bali anatuhumiwa tu.

Siku hizi imezuka tabia ndani ya jamii yetu ambapo jamii hujichukulia sheria mkononi na kutoa adhabu za papo hapo kwa watuhumiwa hata kabla ya kuhakikisha mtuhumiwa ana hatia katika tuhuma zinazomkabili.

Labda kwa kujisahau na pengine kila mtu kujidhania ni jaji wa maisha ya mwenzie hata huko vichochoroni imekuwa kawaida kabisa kusikia kuwa fulani eti kauawa na wananchi wanaojiita wenye hasira kali, akituhumiwa kuwa kaiba ni jambazi au hata kwamba amebaka.

Mauaji hayo hutokea muda mfupi tu, kelele za "mwizi mwizi" au "ananibaka ananibaka" zinaposikika na kuwavuta hata watoka mbali na eneo hilo kufika na jazba zao na kile kinachoitwa kwa kimombo, "mob psychology",wanaofika na kuanza mashambulizi dhidi ya mtuhumiwa bila kujali kuwepo kwa ukweli wa mtuhumiwa kuhusika na tuhuma hiyo, wala chimbuko halisi za kelele hizo.

Ni dhahiri kuwa kelele hizo zinaposikika na kuikusanya kadamnasi ya watu, mtuhumiwa hudhulumiwa haki ya kujitetea kwa kuwa mashambulizi mbalimbali huelekezwa kwake, vikiwemo vipigo vya fimbo, mawe, na hata kuvalishwa mataili na kumwagiwa mafuta ya taa na hatimaye kuuawa kwa kuunguzwa moto.

Hata kwa akili ya kawaida haiingii akilini kusema kuwa kwa mtindo huo,hakuna watu wasio na hatia wanao ambulia mauti yasiyotokana na mapenzi ya Mungu au basi tusema yatokanayo na kosa walilodaiwa kulifanya.

Upo uwezekano mkubwa wa mtu, kwa sababu au chuki binafsi, akamzulia mwenzie kelele za namna hiyo akiwa na lengo la kumkomoa, kulipiza kisasi au hata kujikosha ili kujiondolea aibu ambayo ingemsonga kufuatia kosa alilolifanya.

Wapo wanawake wengine wanao oona mazingira yanakuwa magumu kufuatia madhambi yao, wanaoamua aidha kusema wanabakwa, aukutoa kelele za "mwizi, mwizi" ili kujiondolea aibu. Hii pia haina budi kuwa akilini mwa watu.

Kwa mpango wa makusudi, familia nyingine zimekuwa zikisingizia kuwa wanawake au watoto wa familia zao wamebakwa na hali hakuna ukweli wowote.

Licha ya kukomoa au kulipiza kisasi mara nyingine nia ya maamuzi haya huwa ni kumharibia mtuhumiwa jina lake na pengine kutaka kujipatia kipato toka kwake kwa njia hiyo haramu.Mara nyingi visasi hivi huwa kati ya mwanaume na mwanamke au familia na familia.

Hao hupenda kuona waliosingiziwa wamefikishwa na kupewa adhabu kali katika mahakama zozote hususan zile za "vichochoroni" zisizojali sheria ukweli wala haki za binadamu, ambazo ndizo hasa ninazozisema zimepitwa na wakati kwa jamii ya Watanzania wa sasa.

Ni mahakama hizo zisizotoa nafasi kwa mtuhumiwa kujitetea wala hazihitaji uchunguzi wala uthibitisho kupata ukweli wa jambo kumtia mtu hatiani.hao hufurahia kuona mtuhumiwa wao hata kama amesingiziwa, anahukumiwa vikali na pengine kuuawa kabisa.

Kumekuwa na dhana kuwa vitendo hivyo hutokea kwa kuwa watuhumiwa wanapokamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola, huachiwa muda mfupi. Lakini, hiyo tu haitoshi kwani jamii haina budi kujua ni lini na ni mambo gani yanayo mtia mtu hatiani na yanayoweza kuwatia hatiani wao wenyewe kwa kuwa wamevunja taratibu za nchi kwa kujichukulia sheria mkononi.

Kinachosikitisha zaidi kwa mtazamo wangu binafsi, ni ukweli kwamba hata wapo hata baadhi ya askari polisi wasiojua kutofautisha kati ya mhalifu na mtuhumiwa.Ndio hao utawasikia wakati wanachi wamemfikisha mtuhumiwa wa wizi kituoni bila kumdhulu, wanaanza kufoka, "Sasa mnatuletea majizi, sisi tulifanyeje hili?Hawa si ni wezi: hamjui dawa ya mwizi?"

Ieleweke kuwa si lazima kuwa kwa vile mtu ametenda kinachodhamiriwa kuwa ni kosa la jinai, basi mtu huyo ana hatia. Sheria haimweki mtu hatiani mpaka inapothibitika kuwa alipotenda kitendo hicho kinachokatazwa kisheria, alidhamiria.

Ijulikane kuwa mahakama ndicho chombo pekee cha kuamua kama mtuhumiwa ana hatia na anastahili adhabu gani kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mara nyingi tumesikia na kuwaona polisi ambao ndio walinzi wa amani ya raia na mali zao, wakijinyakulia madaraka ya mahakama wanapowanyanyasa, kuwatesa na hata kuwajeruhi watuhumiwa kabla hata hawajafikishwa mahakamani.

Kumpiga mtuhumiwa kabla ya kuthibitika kisheria kuwa kweli ameiba, amebaka au amefanya kosa lolote, kazi ambayo ni ya mahakama kuthibitisha tuhuma zake, ni ukiukaji wa hakai zabinadamu na hasa inapozingatiwa kuwa mtuhumiwa anakuwa hajakaidi amri ya kwenda alipoamriwa ili kuthibitisha tuhuma dhidi yake.

Katika hali kama hiyo ya kumtesa au kumwadhibu mtuhumiwa kabla ya kumfikisha mahakamani, ni kukiuka Kanuni za Haki ya Asili (Principles of Natural Justice), ambazo pamoja na mambo mengine zinataka mtuhumiwa asikilizwe kwanza.

Watuhumiwa wengine wamefanyiwa hivyo kwa madai kwamba ni tabia yao na mara nyingi wamefanya hivyo. Je, hiyo tu, inatosha kuonesha kuwa mtu huyo anahatia kwa kosa la sasa?Hivi kama alifanya, akajuta, akatubu na sasa ameacha kabisa uhalifu huo, bado ahesabiwe kama mkosefu? Si Yesu alikuja duniani kwa ajili ya wenye dhambi ili wapate kutubu na kuziacha?

Katika sheria ya Ushahidi ya Tanzania, (Tanzania Evidence Act) 1967, kifungu cha 56, imetamkwa wazi kuwa suala la mtu kutuhumiwa kwa kosa alilowahi kulifanya, haliwezi kutumiwa kama ushahidi kumtia mtu hatiani.

Ni vema kuzingatia taratibu na sheria . Mtuhumiwa yeyote afikishwe katika vyombo vya sheria na kupewa nafasi ya kujitetea ili ukweli wa kumtia hatiani utafutwe. Hii itasaidia kuepuka mateso na mauaji yanayofanywa na majaji wa vichochoroni; tena waliopitwa na wakati hata kwa viumbe wasio na hatia.

Njia ya kumrudi mtoto mdogo

KWA kawaida binadamu yeyote hupenda kutiwa moyo na hujisikia vibaya anaposhutumiwa, japo anaweza kukosolewa kistaarabu asijisikie vibaya. Kwa watoto wadogo umakini zaidi unahitajika kuliko ilivyo kwa watu wazima kwa vile wanahitaji kutiwa moyo kwa kila wanalojifunza ili wajenge tabia ya kujiamini. Kuwashutumu kila mara kuna madhara makubwa kuliko faida. Endelea na Mfululizo wa makala zetu kutoka kitabu cha Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni la Beijing, China juu ya Afya.

Wazazi wengine hujaribu kumwongoa mtoto mdogo aliyefanya makosa kwa kumrudi au kumpa adhabu. Iwapo wakitumiwa njia inayofaa katika kumrudi mtoto mdogo, huletea matokeo mazuri na mtoto huongoka. Lakini wakitoa adhabu ovyo bila kujali mazingira yenyewe, matokeo yake huenda kinyume na matakwa. Ili kupata matokeo mema katika kumrudi mtoto mdogo inapasa kwanza kuzingatia mawazo yao hasa kwa vile huwa hawawezi kukumbuka vizuri mambo waliyotenda zamani hivyo ni bora kumrudi mapema mara afanyapo makosa. Kwa mfano mtoto, mtoto fulani amechukua kitu cha kuchezea kutoka shule ya watoto wadogo na kukileta nyumbani, hapo wazazi inawabidi wasichelewe kumuuliza na kumfahamisha kosa lake na kisha mmoja wao afuatane naye kwenda kukirudisha kitu hicho shuleni. Katika kufanya hivyo mtoto hupata kuelewa kwamba ni kosa kukichukua kitu kisichokuwa chake bila idhini.

Ikiwa wazazi wamechelewa kuuliza jambo hilo, wakalipuuzia mpaka baada ya siku kadhaa kupita, basi mtoto huwa ameshasahau jambo lenyewe, hata akiulizwa na kupewa marudi mema huwa hawezi kupata fundisho yoyote yenye maana.

Hivyo kushika wakati biashara na kuchukua njia nzuri katika kumfundisha mtoto ni mambo mawili muhimu. Lakini si rahisi kwa wazazi kuweza kushika mambo hayo kwa sababu wengi wao huwarudi watoto wao. Wakati mwingine, wazazi wakia katika moyo wa furaha, huyaachilia mbali makosa yote ya watoto wao, hata wakijaribu kuuliza huwa wanaacha mambo yapite tu bila hata kudokeza makosa ya watoto wala kuyasahihisha. Lakini wakati mwingine wazazi huwa na moyo mzito, wakawa wepesi wa kukasirika hata mtoto akitenda jambo dogo kinyume cha matakwa yao huwakemea, hunguruma na watoto hutishika kutokana na ghadhabu ya ghafla ya wazazi wao na kuwafanya wahangaike na wasijue la kufanya.

Wako wazazi wengine ambao hujaribu kukumbuka makosa ya watoto wao ili kumkosoa mtoto baada ya kujumlisha makosa yote. Kwa kuwa tumewahi kueleza kwamba watoto wadogo hawawezi kukumbuka vizuri mambo yaliyopita, hivyo ni wazi kwamba kumrudi mtoto baada ya kujumlisha makosa yake yote si njia nzuri. Katika hali hiyo watoto huwa hawafahamu sababu hasa ya kupewa adhabu, na kufikiri kwamba wazazi wao wanajaribu kuwataabisha bure wa mambo yaliyopita, hivyo kuweza hata kuwa na moyo na kuyapuuza mafunzo ya wazazi wao.

Njia ya kumwadhibu mtoto pia inapasa kuzingatiwa, Baadhi ya wazazi wanafikiri kuwa wanaweza kupata matokeo mema kwa kumchapa vikali zaidi mtoto aliyekosa. Lakini kwa kweli wazo kama hilo linakwenda kinyume cha ukweli wa mambo. Kumchapa mtoto si njia iwezayo kumwongoa isipokuwa maelezo ya upole na yenye hoja huweza kuleta matokeo mazuri.

Baadhi ya wazazi kufikiri kuwa watoto wao ni kama mali yao binafsi, na kwamba wana mamlaka kamili juu yao, hivyo si vya haki hata kidogo. Ijapokuwa watoto ni wadogo kwa umri, lakini wao ni binadamu, nao wana hisia zao na heshima ya utu wao. Kumchapa mtoto ni kuvunja heshima ya utu wake na kumfanya ajidunishe na kujifikiria kuwa si chochote si lolote. Kumwadhibu mtoto mara kwa mara humfanya awe na moyo wa ukaidi kiasi cha kurudia makosa yake kwa makusudi. Vitendo kama hivyo huzidi kuwakasirisha wazazi nao huwapa adhabu kali zaidi. vivyo hivyo mambo yakiendelea husababisha matokeo mabaya yakiendelea husababisha matokeo mabaya sana, Hivyo si njia nzuri kumtia adabu mtoto aliyetenda makosa.

Basi tuchukue njia gani katika kumwelimisha mtoto aliyetenda makosa?

Kwanza wazazi waelewe kwamba madhumuni yao ya kumrudi mtoto ni kutaka afahamu kosa alilolitenda ili asilirudie tena. Hivyo kumkosoa mtoto au kumwadhibu ni njia tu ya kumfunza mtoto na wala si lengo. Hivyo ni njia nzuri kumwelimisha mtoto kwa upole na utulivu na kuzungumza naye kirafiki ili mtoto afahamu kosa alilotenda na awe na imani ya kurekebisha makosa yake.

Pili, wazazi wazingatie mbinu ya kumwelimisha mtoto. Wasimkaripie tu bali wakati wa kumfahamisha mtoto kosa lake wakati huo huo wayapongeze mambo yale mazuri aliyoyafanya ili asivunjike moyo kutokana na makosa yake bali ajue kuwa kumbe anaweza kufanya mambo kwa usahihi badala ya makosa.Mbini nyingine ni kwamba wazazi wasimkosoe mtoto mbele ya watu, hususan mbele ya watoto wenzake, ama sivyo mtoto ataona wazazi wamemvunjia heshima mbele ya watu na baadaye atakataa kwenda kucheza na wenzake akihofia kuchekwa nao.

Tatu, kumfundisha mtoto njia ya kutenda jambo, mwonyeshe mtoto nini wanalostahili kufanya, yaani wazazi si kama tu wanapasa kumfahamisha nini halifai bali wamwambie nini linalofaa kutendewa na wamfundishe njia ya kulitenda barabara.

Jambo la mwisho, Wazazi wanatakiwa kujikamilisha vizuri kwa mawazo na vitendo . watoto hujifunza mazoea mengi kutoka wa wazazi wao,hivyo wazazi wakitaka watoto wawe na mazoea mazuri nao hawana budi kuwa na mazoea hayo kwanza ili wawaonyeshe watoto nao mfano bora.

Watakatifu wafiadini 22: namna kila mmoja alivyouawa kinyama

"Watakuja watu weupe; na hao wataleta dini mpya, utakapowaona, wapokee vizuri na hata uwasadiki" Ndivyo Matiasi Mulumba, alivyoambiwa na baba yake aliyekuwa mzee sana.

Haukupita muda mrefu, Waarabu wakafika Uganda. Mulumba akawafauata. Baada ya miaka michache, wamisionari, Waprotestanti nao wakatua huko Uganda. Mulumba akawafuata, akasikiliza mafundisho yao na kuyasadiki.

Alipokuwa karibu kubatizwa wakaingia Wamisionari wa Kikatoliki. Matiasi Mulumba aliyekuwa mjumbe na kiongozi wa wazee washauri akayasikia vema zaidi mafundisho yao. Roho ikamlipuka na kupata nuru kali. Akajisikia furaha ambayo katu hakupata kuisikia katika dini nyingine.

Mei 28, 1882, akabatizwa pamoja na mkewe na hii ni tangu siku ile alipoanza kufuata mafundisho ya mapadre.

Mulumba alipendwa na watu wengi hasa alipoanza kuwafundisha watoto wake ili wawe Wakristo. alijenga nyumba ili kuwasaidia watoka mbali waliokuja kwenye mafundisho huku akiwapa chakula.

Alipokamatwa na wauaji ili wamshurutishe aikane dini yake, aliwashangaza aliposimama mbele yao na badala ya kuikana kama walivyotegemea afanye, akaungama dini yake kwa uhodari bila kuogopa mauti.

Wauaji wale wakachukizwa na kughadhabika sana. Wakaanza kumtesa Wakamkamata mikono na miguu kisha wakaanza kumkata nyama ya mgongoni na kufuatia ya kifuani. Ajabu ni kwamba licha ya mateso yote hayo Matias Mulumba hakulia hata kidogo.

Aliomba Mungu akisema "Eee Mungu wangu Mungu wangu" Shahidi hiyo akafa Mei 28, 1886, Mwili wake ukakaa porini kwa siku kadhaa bila kuliwa na ndege, wanyama wala wadudu hadi mapadre walipouchukua kuuzika.

Tunaambiwa kuwa wafiadini hawa 22 waafrika walipata mbingu wakati wa dhuluma ya Mwanga aliyekuwa mfalme huko Uganda. Ilikuwa ni kati ya miaka ya 1885 - 1887.

Inaelezwa kuwa katika vijana wake, mwanga alipendelea kusikiliza mafundisho ya mapadre na kwa taratibu akaanza kuyaacha mambo yote ya kipagani huku akiwashauri watu kufuata mafundisho ya dini ya Yesu Kristo.

Wajumbe na wapagani walipoona mfalme wao anayakataa mambo yao ya kipagani, wakaunda njama wamuue. Siri hiyo ikafichuka kwa Wakristo watatu waliokuwa watumishi wake.

Akamkuta Katikiro (Waziri Mkuu) na wote waliopanga shauri la kumuua. wakatubu nae akawasamehe Tangu siku hiyo Katikiro wazee na wafumu wakala njama ya kuwaua na kuwaangamiza Wakristo. Kila siku walikwenda kwa mfalme Mwanga kuwashitaki Wakristo huku akadanganyika kirahisi kwa mali na furaha za dunia. Akawalazimisha wakristo watende mambo mabaya. walipokataa kushiriki matendo maovu akawakasirikia na kutaka wauawe.Miongoni mwa wafiadini hao 22 alikuwa kijana hodari wa miaka 20. Huyo alikuwa Karoli Lwanga, aliyependwa na mfalme kwa kuwa alimuona mzuri, hodari na mwenye tabia njema. akimfanya msimamizi wa vijana 300, aliowatangulia kusikiliza mafundisho ya mapadre.

Mwanga aliposhikwa na tamaa mbaya za kimwili, akawashawishi vijana wale kuridhia tamaa zake chafu. Karoli akawatorosha na kuwaficha ili wapate kukaa kwa moyo safi. Hata walipokamatwa aliwashuhudia na hata kuwabatiza wanne waliokuwa wakatekumeni.

Kwa amri ya Mfalme Mwanga siku moja Karoli aliwakusanya vijana wote. Mwanga, akawaambia "kati yenu wale wote ambao hawataki kusali wala kufuata dini ya Kikristo wakae hapa karibu na mimi. Na wale wote wanaotaka kusali na kuifuata dini ya Kristo waende pale ukutani.

Karoli Lwanga na vijana wenzake akiwa kati yao 14 wakaenda kukaa ukutani. wakaungama wazi kwa kauli moja kwa wao ni Wakristo na hawataki kuikana dini yao.

Wengine walikuwa akina, Kizito, Ambrosi Kibuka, Yakobo, Mbaga Tuzinde, , Mugaga, Aldofo Ludigo, Mukasa, Achile Kiwanuka, Gyavira, Anatoli Kiligwayo, Atanas Bazekuketa na Gonzaga Gonza.

Walifungwa pamoja wakapelekwa kilimani. Namugongo ili wachomwe moto na ndipo juni 3, 1886 wakateketezwa kwenye tanuru la moto. wakafa wafiadini na hii ndiyo siku ya kuwakumbuka yaani kila juni 3.Luka Banabakintu naye aliuawa nao siku hiyo hiyo kwa kuchomwa moto huko kilimani. Noe Mawagali aliyekuwa mfinyanzi aliuawa kwa kupigwa mkuki siku ya mauti ya Matias Mulumba.

"Wewe U Mkristo?" Ponsiano aliyekuwa mtumishi wa Mwanga akamjibu muuaji, "Ndiyo ni kweli. mimi ni Mkristo kabisa" Aliposikia jibu hilo, muuaji huyo akamuua kwa kumchoma mkuki.

Yohana Maria Muzeyi ambaye siku moja kabla ya kifo chake cha kutupwa ziwani, alikwenda kupokea Sakramenti ya Ekaristi ili apate neema ya ushindani maana alisikia kuwa atauawa, ndiye aliyekuwa wa mwisho kuuawa kati ya wafiadini hao.

Mwingine aliyeuawa katika dhuluma hiyo ni Yosefu Mukasa (26) aliyekuwa msimamizi wa nyumba za mfalme zilizokuwa na vijana 500. Ndiye aliyewatangulia wote kwa kukatwa kichwa na kuchomwa moto.

Gonzaga Gonza kati ya wale wafiadini 14 walioungama dini yao mbele ya Mwanga alipigwa mkuki mbele ya wenzake Katekisimu huku akiwa na miaka 16, Mwanga alimpiga mkuki Dionis Sebugwao na kumuua.

Mwingine ni Adrea Kagwa (30) aliyeonewa kijicho na Katikiro kwa sababu ya kuwafundisha wenzake ili wabatizwe na hasa baada ya kusikika kuwa mfalme alitaka kumfanya Adrea Kagwa kuwa jemedari wake. Andrea naye akakatwa kichwa.

Mungu alichukizwa na mauji hayo, akawaadhibu kwani Mwanga alipokuwa anaenda vitani alikamatwa mikononi mwa Waingereza, akafukuzwa katika nchi yake na kufa kwa hasira na uchungu katika kisiwa cha Seychelles.

Adhabu ya Kitikiro ilikuwa mbele ya mfalme Mwanga kwani katika vita alipigwa risasi nyumbani kwake Maiti yake ikaliwa na mbwa.

Senkole, aliyemuua Karoli Lwanga, alikamatwa na kuliwa na mamba katika ziwa Victoria wakati hali Makujanga aliyekuwa Mkuu wa wauaji, alikufa vibaya kwa vidonda na ugonjwa wa tumbo

Mashahidi hao 22 Waafrika walitangazwa wenye heri Juni 6,1920 na Oktoba 18,1964, Papa Paulo wa VI aliwatangaza kuwa watakatifu.

1969, Papa huyo alifika Uganda mahali walipofia. Akasali pamoja na maelfu ya watu toka nchi mbalimbali za Afrika.

Mungu amewachagua wafiadini hao ili watufundishe kuwa anataka tumjue tumpende na tumtumikie. Wakubwa kwa wadogo wakati wote tuwe tayari kumfia na yeye atatufanyia chema na kutulipia mbali mabaya tunayofanya kwa ajili yake.

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

Mfalme aliyeaminiwa kuwa kiumbe kisichokula chakula

Na Masha Otieno JR.

MOJAWAPO ya eneo la Afrika ambalo kwa miaka mingi limesifika kwa kutoa wafalme waliokuwa hodari waliovuma na walioonyesha misimamo ni eneo la Afrika Magharibi.

Ukanda huu ulitoa wafalme waliosifika sana kama Jaja wa Opobo, Nana, Asantehene na mfalme wa kike wa Taghaza ambaye wafuasi wake waliamini kuwa yeye ni karibia sawa na Mungu.

Mfalme Fante Waa wa Taghaza katika karne ya 17 aliweza kuweka rekodi akiwa katika kasri yake iliyokuwepo katika mji wa Taghaza, uliosifika Afrika Magharibi kwa kuwa kituo kikubwa cha machimbo ya chumvi.

Mfalme Fante, alijifanya kuwa yeye ana nguvu za kutenda miujiza, hasikii njaa, haoni kiu, hasikii uchungu, hafi wala haugui.

Siku zote akiwa ameketi ndani ya kasri lake la heshima alionekana kumeremeta huku afya yake ikionyesha kuwa na uchangamfu wa kutosha, hali iliyowapelekea watu kuamini uvumi ulioenea kuwa yeye alikuwa na nguvu zinazokaribia kuwa sawa na za Mungu.

Mfalme Fante alidai kuwa hukumu alizotoa kwa mdomo tu zilikuwa na uwezo wa kumuathiri mtu aliyekuwa chini ya utawala wake kiasi cha kumpelekea asiweze kuwa na mafanikio wala mwelekeo.

Pia ilidaiwa kuwa bararaka alizotoa zingeweza kumbariki mtu kiasi cha kumpelekea kuwa na mibaraka tele na maisha mazuri iwapo angelienenda kulingana na matakwa yake.

Mfalme huyu aliweza kutabiri mvua, njaa na hata ukame. Pia aliweza kutabiri msimu wa mavuno mengi na baraka na mafanikio ambayo yangelikuja kuipata nchi.

Siku zote katika utawala wake aliendesha mambo kwa mfumo wa kidini.

Dhehebu la Ufalme wa Taghaza liliamini juu ya miungu ya miamba ambao waliamini kuwa ni chanzo cha kuwepo chumvi kwa wingi katika Taghaza.

Chumvi kutoka Taghaza iliweza kunufaisha serikali zote za Afrika Magharibi nyakati hizo na kuvuka jangwa la Sahara na kupelekwa Arabuni, Misri na Libya.

Siku zote Mfalme Fante, aliwasisitizia raia zake kuwa endapo wangeacha kuzienzi nguvu za miungu wa miamba ya Taghaza, basi na chumvi ya Taghaza ingekoma kupatikana.

Karibu watu wote waliokuwepo katika dola hii walitoa kodi ya malimbuko yao ya kwa mfalme Fante, wakiamini alikuwa ni mmoja wa miungu.

Pamoja na ujanja wote ulionusuru na kumwezesha kujisetiri kwa kipindi chote cha utawala wake, siri iliyofichika kwa muda mrefu kuhusu undani wa Mfalme Fante ilifichuka siku alipokufa.

Watu wa Taghaza walishangaa kuona amefariki hali ilijulikana hafi. Pia baada ya kifo chake, mtumishi wake wa muda mrefu alitoa taarifa kuwa mfalme huyo alikuwa akila kwa siri mafichoni usiku wakati watu wamelala, ili kulinda dhana kuwa yeye hali chakula.