Utamaduni wa kurithi mume au mke umepitwa na wakati

Na Fr. Baptiste Mapunda

WAKATI tunaingia katika karne ya sayansi na teknolojia, bado kuna baadhi ya watu wanaong’ang’ania utamaduni ambao husababisha madhara kwa jamii na hatimaye kifo.

Utamaduni mzuri ni ule unaoleta uhai. Mara nyingi tunasikia katika vyombo vya habari kwamba tohara bado inaendelezwa na baadhi ya makabila hapa Tanzania, hata kama athari zake zinafahamika kwa watu hao.

Pamoja na hilo kuna suala zima la "kurithi mume au mke" wa ndugu katika jamii. Hili ama kweli ni suala nyeti, kwani katika Biblia lipo, lakini je, linaenda sambamba na mazingira yetu ya leo?.

Nilipokuwa Zambia Parokiani Ksaba mwaka 1992 nilikuwa napenda sana kufanya semina juu ya kifo na Imani ya Kikristo . kitu kimojawapo tulichokuwa tunajadiliana ni juu ya mateso yanapopatikana na hatimaye kifo, je vinatoka wapi? Lakini hata kurithi mume au mke wa ndugu, hali hii ilijulikana kwa Kibemba kama "Kupyana" maana yake ni kurithi.

Mtu akifiwa kama hawatamrithi basi, ataweza kudhurika kwa maana moja au nyingine. Lakini mara nyingi ilikuwa ni sababu ya ubinafsi tu, labda tunaweza kusema ni tamaa ya mwili tu. kwa kweli Kibiblia ilikuwa na maana ya kuendeleza ukoo au kumtunza mjane na wanawe.

Lakini nilivyoona huko Zambia na hata hapa Tanzania ni zaidi tamaa ya mali ya marehemu.

mara kadhaa tulibaini kuwa Marehemu alikuwa amekufa kwa Ukimwi, laikini hata hivi sasa kurithi wake au waume kuliendelea bila kujali huyu ndugu kafa kwa ugonjwa wa aina gani.

Mara moja ilitokea kwamba kijana alikufa kwa Ukimwi, lakini ndugu yake akarithi tu mke wake bila kujali.

Nilipojaribu kumshauri juu ya suala zima la Ukimwi alisema huu ni utamaduni wetu, siwezi kuuacha kamwe. nilishangaa sana na niliona huruma, nikajiuliza je kuna maana gani kung'ang'ania utamaduni unaoleta maafa? Baada ya mwaka mmoja yule kijana nilimzika mimi mwenyewe.

Watu kama hao wanaoshikilia tu utamaduni ni wengi hapa Tanzania na Duniani kote

Hali ilivyo nchini Tanzania

Ripoti iliyotolewa na Wizara ya Afya Duniani siku ya Ukimwi Duniani mwishoni mwa mwaka 1999 inatisha sana kwetu Watanzania. ripoti inayosema kwamba Tanzania inashika nafasi ya nne. Wanasema kati ya wanaume watano mmoja ni muathiriwa na kati ya wanawake wanne mmoja ni mwathiriwa Je tunakwenda wapi jamani?

Sote tunajua kwamba Ukimwi ni ugonjwa hatari sana ambao huharibu uwezo wa mwili kupambana na magonjwa mengine. Mpaka sasa tiba bado haijagunduliwa.

Hivi kinachotakiwa ni uaminifu na badiliko la tabia, hasa kwetu sisi vijana. Ukimwi tunaambiwa kuwa huenezwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine ya mwili na mtu mwenye Ukimwi yanapoingia katika mkondo wa damu ya mtu mwingine.

Sasa katika kufuata utamaduni wa kurithi mume au mke, tutapona wangapi na janga hilo? kwa Nyakati hizi basi, kilichobaki ni kila mtu kujiamulia mwenyewe, anataka kuishi au kukatisha maisha yake haraka. Ugonjwa huu unatupa changamoto katika maisha yetu, ni wazi ugonjwa huu unamhusu kila mmoja. Tujihadhari na tamaduni potofu, tuzipige vita kabisa, kijana, msichana fahamu kwamba ukimwi mpaka sasa hauna dawa ya chanjo, hivi jilinde na hasa kutokufuata utamaduni unaodhuru maisha ya binadamu. Vijana wenzangu basi tujiulize: Je. katika utamaduni wetu kuna mila potofu ambayo inaweza ikasababisha watu kuugua Ukimwi? Ni muhimu kufanya majadiliano na wenzenu katika vikundi.

Je vijana huko mliko mnaliongelea suala la Ukimwi bila kuficha au bila woga? Je mna kikundi chochote cha kuongelea maswala haya?

Sisi hapa Nyakato tumeunda kikundi kinachoitwa 'Youth Alive Club' maana yake Vijana Hai. Kikundi hiki kinasaidia sana kuelimisha vijana hata jamii nzima juu ya suala la Ukimwi na mila potofu.

Neno kubwa katika Youtha Alive Club ni Behaviour Change 'kubadili Tabia' Na waasa vijana wote kuunda kikundi kama hiki ambacho ni chombo cha kupambana na kuthibiti Ukimwi kwa pamoja na kwa umoja. "Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu"

Wana Youth Alive wanafanya mambo mengi kadiri ya mazingira yao.

Pia ni lazima wawe mifano mizuri na halisi ya tabia njema kwa jamii. wanasaidiana kwa njia ya mijadala na mikutano, wanajihusisha na kutoa Elimu ya Ukimwi na mabadiliko ya Tabia. Wanakuza vipaji vyao kwa michezo, nyimbo, maigizo na uchoraji, kwa kifupi wanajiwekea malengo ya misha yao ya baadaye.

tukumbuke kwamba 'Utamaduni wa kurithi mume au mke umepitwa na wakati' na hasa katika Mwaka huu wa JUBILEI KUU YA UKOMBOZI WETU.

Acha mtoto ashiriki katika kusimulia hadithi

UMRI wa utotoni ni umri uliojaa udadisi mwingi. Ni wakati ambapo ubongo wa mwanadamu una njaa kuliko wakati mwingine wowote kwa vile unakuwa haujahifadhi kumbukumbu nyingi. Ni wakati muhimu pia wa kumjenga mtoto katika misingi ya kimaadili ambayo itamsaidia baadaye. Kusimulia hadithi ni moja ya njia ambazo ni rahisi kutumika kumuelimisha mtoto. Endelea na Mfululizo wa makala zetu kutoka

kitabu cha Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni la Beijing, China juu ya Afya.

INGAWA kuwasimulia watoto hadithi kunaleta manufaa makubwa lakini hakutoshi.

kwa mujibu wa uchunguzi wataalamu wanaona kwamba kuna haja kubwa kuwahimiza watoto wajaribu kusimulia hadithi ili kukuza uwezo wao wa lugha.

Wataalamu walichagua watoto thelathini wenye umri wa miezi 28 kufanya uchunguzi. Waliwagawanya watoto hao kuwa vikundi viwili:Watoto wa kikundi cha kwanza walifundishwa nyumbani kwa njia ya kawaida, yaani mama zao waliwasimulia hadhithi kwa sauti kubwa. Watoto wa kikundi cha pili walipokea mafundisho maalum yaani wazazi wao waliwaacha watoto wao kushirikiana nao kusimulia hadithi. Kwa mujibu wa mpango uliowekwa, wazazi wa vikundi hivyo viwili walisimulia hadithi mara nane kwa wiki na waliendelea kwa miezi minane.

Kwenye semina ya kikundi cha pili wazazi waliposimulia hadithi, wataalamu waliwataka wazazi wao kwanza waeleze muhusika mkubwa wa hadithi ni nani, kisha walitoa maswali ,ambayo yaliweza kuwafanya watoto watambue kitu au mtu kama vile hii ni rangi gani? anafanya nini? Wazazi wanatakiwa kuwasifu watoto wao mara kwa mara ili kuchochea hamu yao ya kutaka ujuzi na wajitahidi kuwatajirisha misamiati ya kueleza mambo.

Kwa mfano baada ya mtoto kujibu swali moja si kama wazazi wanahakikisha majubu tu, bali pia wanaweza kuongeza kidogo juu ya jibu la mtoto kwa mfano mtoto anapojubu swali la Mbwa kafanya nini kwa kusema mbwa anakaa ingawa jibu la mtoto ni sawa lakini kama wazazi wanajibu ndio mbwa anakaa chini ya meza jibu kama hilo litakuwa zuri zaidi.

Uchunguzi wa mwezi wa kwanza ulipokaribia kumalizika wataalamu walifanya mtihanid juu ya uwezo wa akili. Baada ya mieze tisa wataalamu walifanya mtihani ule ule kwa watoto hao. Matokeo ni kwamba hakukuwa na tofauti yo yote kwa upande wa uwezo wa kufahamu lugha, lakini katika upande wa uwezo wa kujieleza watoto wa kikundi cha pili walijua misamiati mingi zaidi kuliko watoto wa kikundi cha kwanza ni sawa na kuwatangulia kwa kiasi cha miezi sita katika kujua misamiati hiyo.

Kwa watoto wenye umri wa miaka 2-3 hvi wataalamu wanatoa shauri la kwamba wazazi wanapaswa wasaidie watoto kusimulia hadithi kwa kutumia picha.

Zaidi ya hayo jambo muhimu ni kudumisha hamu ya kusimulia hadithi njia nzuri ni kusimualia hadithi kwa zamu kati ya wazazi na watoto.

Haiwezekani kwa watoto wachanga kusimulia hadithi bila kutazama picha kwa vile hawajui kuchagua mambo muhimu kutoka kitabuni.

Mtakatifu Elisabeti Ann Seton: Alisuswa na ndugu kwa kuingia Ukatoliki toka Uanglikana

Na Josephs Sabinus

"Lengo la kwanza la kazi yetu ya kila siki ninaloliweka mikononi na mbele yenu, ni kutimiza mapenzi ya Mungu. La pili ni kufanya kazi hii kwa mapenzi yake Mungu"

Ndivyo Mama Elisabeti alivyowahimiza mara kwa mara masista wenzake wakati ule umeanzisha shirika lile la kwanza la masista Wamerikani ili waifanye kazi ya Mungu.

Yeye, alizaliwa mjini New York huko Marekani mnamo mwaka 1774, katika Ukoo wao uliokuwa bora na tajiri mno.

Ingawa baba yake Elisabeti Ann Seton hakuwa na kawaida ya kusali, Mama yake Elisabeti Ann Seton hakuwa na kawaida ya kusali, Mama yake Elisabeti (mzazi) na hata baadaye yuke mama yake wa kambo wote wawili walikuwa wafuasi wa dhehebu la Kianglikana. Wakati huo hata Elisabeti mwenyewe ndivyo alivyokuwa Mwanglikana.

Mtakatifu huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka arobaini na sita tu alipatwa na mkosi wa kufiwa na mama yake mzazi akiwa mtoto mdogo sana mwenye umri wa miaka mitatu tu. Muda mfupi baada ya kifo hicho baba yake alioa mwanamke mwingine (mama wa kambo wa Elisabeti)

Hata hivyo akiwa na umri wa miaka kumi na tisa, Elisabeti mfanyabiashara mmoja maarufu aliyekuwa na mali nyingi. Akafanikiwa kuwazaa watoto watano katika ndoa yake na mfanyabiashara huyo aliyeitwa William Seton.

Ulifika wakati familia hii inasumbuliwa na matatizo mengi - mengi yakiweko magonjwa yaliyoisonga. Matatizo mengi yakiwemo magonjwa yaliyoisonga. Matatizo mengi makubwa yalianza mara tu ili biashara ya mmewe Elisabeti yaani bwana William Seton ilipoanza kuugua kifua Kikuu (T.B).

Katika juhudi za kutafuta palipo na matibabu bora ambayo yangeweza kuyanusuru maisha yake ambazo hazikuzaa matunda bora, Bi Seton (Elisabeti) alijikuta anaitwa mjane akiwa na umri wa miaka 30 Bw. Seton alipofariki akiwa huko Italia.

Kinachosikitsha zaidi ni wmba dbaada ya kifo cha William Seton, Elisabeti ahakuwa na pesa yoyote kwa ajili ya kuwasaidia watoto wake wote watano waliomtegemea. Akapata kipindi kigumu mno kuwalea.

Hali hii pia ilichochewa na wazazi wake Elisabeti ambao hawakuridhika na maamuzi yake ya kubadili dini hasa baasa ya kugusana na dini Katoliki tangu alipokuwa akimuuguza mmewe huko Italia.

Inaelezwa kuwa alianza kidogo kidogo lakini kadiri siku zilivyoongezeka ndivyo Elisabeti alivyozidi kupendezwa na kuifahamu vema Imani thabiti na ya kweli ya Ukatoliki. Akazidi kufungamana nayo zaidi.

Yakiwa ni matokeo ya kukiri imani hiyo Katoliki, mwezi Machi mwaka 1805, Elisabeti aliungana rasmi ndani ya Ukatoliki na habari hiyo iliwafikia wazazi wake, hawakufurahishwa nayo kabisa , walichukia na hata kujenga chuki dhidi yake labda hawakujua kuwa masuala ya kiroho hayahitaji kulazimishana.

Elisabeti aliporudi nyumbani kwao Marekani ndugu zake hao walimkasirikia mno. Wakaonesha waziwazi namna walivyochukizwa na uamuzi wake wa kubadili dini toka Uanglikana kwenda Ukatoliki.

Hata marafiki zake wengi walimsusa na kumtenga. Hawakutaka kushirikiana naye tena kwa lolote. Wakamwacha kabisa mwenyewe akihangaika na maisha. Hata alipowaomba pesa na misaada mingine kwa ajili ya wale watoto wake walikataa kata kata kumsaidia. wakazidi kumsemea na kumbeza tu bila usaidizi wowote.

Kama Elisabeti angekuwa dhaifu kiimani angelazimika kugeuka na kula matapishi yake, lakini kwake haikuwa hivyo.

Aliushikilia msimamo wake kiimani kama nafsi yake ilivyoongozwa na Mungu, ilivyomtuma.

Hata hivyo katika juhudi zake za kuwalea wanae na hata kuifanya kazi ya Mungu Elisabeti ambaye hukumbukwa Januari 4 ya kila mwaka, Pamoja na watakatifu wengine wa bara la Afrika akina Mavilus, aliyekuwa mfia dini wa Tunisia na Watakatifu Akwilinius, Geminus, Trifon, Augenius, Marsiamus, Kwinktus na Teodotus, wpte wakiwa wafia dini wa Moroko, alifanya kitu kimoja chemaa.

Huko mjini Boston Marekani alianzisha shule na huu ulikuwa mwaka 808. Akawavuta akina mama wengi na kuungana nao wakawa walimu walioshirikiana veima baada ya muda nao wakaishi kana kwamba ni watawa.

Hiyo ndiyo ilikuwa hatua ya kwanza ya kuanzishwa kwa shirika la kwanza la masista Wamarekani waliojiita 'Masista wa Upendo'.

Akafungua shule nyingi za msingi na pia akajenga shule nyingi za msingi na nyumba za kuwatunzia mayatima na huku akiendelea kuwatunza wale watoto wake watano.

Elisabeti Ann Seton aliyefariki dunia Januari 4 katika mwaka 1821, ni kioo cha mfano mzuri wa mtu aliyetambua imani sahihi ya kikatoliki.

Alikuwa imara kuitetea na kuilinda pasi kujali shida za dunia hii.Alijua si busara kufanya jambo ili kuwafurahisha wanadamu wa dunia hii wasioridhika kamwe bali kila jambo kufanyika kwa mapenzi ya Mungu. Alijua kila jambo hupangwa na kutoka kwa mwenyezi.

Ndiyo maana baadaye aliwaita pamoja masista wenzake akawambia hivi "lengo la kwanza la kazi yetu ya kila siku ninaloliweka mbele yenu ni kutimiza mapenzi ya Mungu, la pili ni kufanya kazi kwa jinsi anavyopenda yeye, na la tatu ni kuifanya kwa sababu tu ni mapenzi yake"

Mwaka 1975 Baba Mtakatifu alimtaja Elisabeti kuwa katika orodha ile ambayo ni tamanio la kila mtu mwenye mapenzi mema; orodha ya Watakatifu. Akaitwa Mtakatofu mwaka 1975