Tunaugua ugonjwa wa maamuzi ya zimamoto

Na Peter Dominic

.

Ni kweli kwamba viongozi wa kisiasa nchini wana kazi kubwa ya kutuongoza na kutuelekeza mahali pazuri kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu,lakini ni wazi kabisa pia kuwabaadhi ya viongozi wamekuwawakitoa maamuzi ambayo hayazingatii uhalisi wa mambo .

Mara nyingi jamii hushangilia na kupiga vigelegele pindi serikali inapotoa tamko linaloonyesha kuwa na manufaa ya umma, lakini kwetu sisi Watanzania imekuwa ni kawaida furaha hizo kuzimika kama kibatari kwenye upepo, kwa vile jambo lililokusudiwa halikufikia malengo yake.

Ni vigumu kugusa kila mahali penye kasoro za namna hii lakini huu umekuwa kana kwamba ndio utamaduni wetu. Mfano mzuri ni ule wa operesheni ambazo zimekuwa zikiendeshwa na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Luteni Yusuf Makamba. Hivi tunapoelezwa kuwa serikali itawakamata Machangudoa kwa lengo la kuwarudisha makwao ili kuleta heshima katika jiji la Dar-Es-Salaam,tafsiri yake ni nini?

Kauli hii imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Dar-Es-Salaam katika mlolongo wa operesheni zake alizozianza kwa kwa kuwakamata wapiga debe na ombaomba huku akiahidi kuwa machangudoa wakae chonjo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuweka jiji katika hali ya usafi na kupambana na Ukimwi.

Nia ya Makamba ni njema lakini haikuzingatia mambo kadhaa ya msingi.

Ni juzi tu Mheshimiwa huyo huyo kwa kutumia kofia aliyonayo kabla ya kuwakamata ombaomba aliutangazia umma kuwa ataondoa tatizo sugu la wapiga debe ili kuwaondolea wananchi kero na adha wanayoipata wanapofika katika vituo vya mabasi. Tujiulize ,

baada ya zoezi hilo ni kweli hakuna wapiga debe tena; wale wasio na sare wanaoendelea kuwabughudhi abiria vituoni kana kwamba hawajui waendako wala watokako?

Tutasadiki vipi basi tunapoelezwa kuwa sasa serikali ina mpango wa kuwaondoa Machangudoa tukiachilia mbali hawa ombaomba ambao tayari wameanza kurejea jijini kama walivyoahidi kuwa wanaenda likizo watarudi?.

Kutokana na udhaifu unaoneshwa na viongozi wa kutoa maamuzi bila kuweka mipango thabiti ya udhibiti wa baadaye kuhusu tukio husika ,ndio maana hata ombaomba walisema wanakwenda likizo kisha watarudi.Walisema hivyo, wakijua hizi ni nguvu za soda utafikia wakati itasahaulika na wataendelea na kazi yao kama ilivyo kwa wapiga debe.

Tuchukue nafasi hivyo tujiulize kama ombaomba wanarejea achilia mbali hawa wapiga debe ambao wanaendelea na kazi yao bila matatizo, itakuwaje kwa machangudoa?

Suala hili ndilo hasa kwa mtazamo wangu nasema kama hatua hii itafikiwa itakuwa ni sawa na kubadilishana makahaba au ombaomba kutoka mkoa huu kwenda mwingine,nahiyo ikiwa kichocheo cha kuishamirisha biashara hii haramu.

Ki-msingi jiji la Dar-Es-Salaam lina idadi kubwa ya watu na mkusanyiko wa makabila mbalimbali wenye kazi tofauti wakiwemo makahaba na wanaume wakware. Labda serikali iweke bayana suala hili kwamba imelenga kuisaidia jamii ipi? Maana kahaba wa Dar-Es-salaam anapopelekwa mkoa mwingine sio kigezo kuwa ataacha biashara hiyo.

Mawazo yangu yananipa nguvu ya kusema kuwa shughuli ya kuwakamata machangudoa haitatofautiana na ile ya wapiga debe na ombaomba.

Ni wazi kila kahaba atarudishwa mkoa alikotoka, wilaya hadi kijijini kwake, lakini tujiulize hivi anaporejeshwa huko amepewa miiko gani ya kuacha kazi hiyo au ndio tunaondoa aibu hii mijini ili kuiotesha mizizi ya ukahaba vijijini?

Kwa kawaida nchi moja lugha moja jamii huwa na tabia zinazolandana hususani wale wanaoishi sehemu za mijini japo mikoa tofauti. Hivyo itafsirike kuwa yaliyomo kwenye kundi la mbuzi ndiyo utakayokuta kwenye kundi la kondoo.

Ikimbukwe kuwa serikali itakapoanza kutimiza azma yake ya kuwatimua makahaba kama ilivyofanya kwa ombaomba,adha hizohizo ilizozikwepa ndizo zitakuwa zinawapelekea wananchi wa mikoa mingine ambayo nayo haitazivumilia kuwatimua wa mikoa mingine na mwisho wake kwa vile ukahaba hauna mkoa tutakuwa tu tumezuia kahaba kufanya ukahaba nje ya mkoa wake, lakini ukahaba wa uwenyeji utaendelea.

Kutoa maamuzi bila kufanya uchunguzi wa kisayansi na wa kina ambao ni utamaduni uliojengeka miongoni mwa viongozi wengi, unaweza kuiathiri sana jamii kwani ni mfumo ambao si tu kwamba unaleta chuki katika jamii, bali pia unalifedheahesha taifa na jamii nzima kwa ujumla.

Yafaa basi daima kutanguliza mikakati thabiti yenye utafiti wa kina badala ya kukurupuka na kutenda.

Kwa mtazamo wangu, ninaona operesheni kama hizo zikizingatia haki hazitaisha kamwe na zitaletwa mvurugano mkubwa miongoni mwa jamii yetu.

Leo tunawarudisha makwao ombaomba na makahaba, kesho itakuwa zamu ya wezi na majambazi. Hao nao tutawakamata kutoka Dar es Salaam na kuwarudisha makwao wakafanyie huko vitendo vyoa vya uhalifu. Kisha Arusha nao watawatimua wale wa Dar es Salaam warejee na ujambazi wao jijini. Arusha nao watapokea wa kwao kutoka Singida na mzunguko utaendelea hivyo; je, si tutakuwa tunacheza mchezo wa kitoto wa makida makida?

Siungi mkono kauli za baadhi ya machangudoa ambao wamekuwa wakiapa kutokuachana na biashara hiyo kwa kuwa hawana njia nyingine ya kuwawezesha kuishi, tofauti na hiyo inayodhalilisha utu wa mwanadamu.

Ikumbukwe kuwa hata kama tutafanikwa kuwaondoa machangudoa na ombaomba na kuwatelekeza vijijini halitakuwa jibu sahihi,maana kizazi cha namna hii hakitakoma, suala moja la msingi ni serikali kufikiria upya na kuweka misingi imara ya kuisaidia jamii hiyo na pale wanapovunja sheria, sheria ikachukua mkondo wake. Lakini kubwa zaidi tujitibu ugonjwa wa kufanya maamuzi ya zimamoto.

 

Athari za kucheka kwa mtoto wakati wa kula

WAZAZI wengi hupata taabu sana katika kuwalisha watoto wa umri kama wa miaka miwili.

Kwa kuwa watoto hawawezi kula chakula vizuri wao wenyewe, wazazi huona kwamba hawana budi kuwachekesha watoto wakati wa kula.

Mtoto anapocheka mara mzazi hupata fursa ya kumlisha mtoto chakula. Hii ni tabia mbaya sana. Alipata kutokea mtoto mmoja aliyewahi kupewa huduma ya kwanza katika hospitali kutokana na mazazi wake kumtia karanga kinywani mara alipocheka.

kwa bahati mbaya karanga hiyo ilikosea na kuingia katika umio wa pumzi, karanga ilitolewa.

Kwa nini ni hatari kumchekesha mtoto anayekula? sababu ni kuwa ktika sehemu ya koo, umio wa chakula na umio wa pumzi una njia ya pamoja yenye mfupa laini yaani kakakaa laini la kimio.

Katika hali ya kawaida wakati wa kumeza chakula kaakaa laini la kimio linaweza kufunga mara moja umio wa pumzi kutokana na silika ya neva, kwa hivyo chakula hakiwezi kuingia katika umio wa pumzi . kwa kawaida mtoto anapokula chakula huku kucheka na kucheza, wakati mwingine mtoto anapolia kwa kukaripiwa na mzazi na kulazimishwa kula, kaakaa laini la kimio haliwezi kufanya kazi kama kawaida na kufunga umio wa pumzi; zaidi ya hayo chakula kinapofika katika umio wa pumzi na umio wa chakula, huleta hali ya kupaliwa na kukohoa. Wakati huo silika ya neva ya watoto haiwezi kuondosha kitu kwa kujikohoza kama watu wazima wanavyofanya na hivyo kusababisha chakula kuingia katika umio wa pumzi.

Mtoto si kama anasumbuliwa na maumivu tu, bali pia anaweza kufa ikiwa atakawia kufikishwa hospitali.

Watoto wenye afya njema wapo katika kipindi cha kukua, hushikwa na hamu kubwa ya kula chakula. Kama watoto wanalishwa kwa busara, hawezi kamwe kukataa kula, sababu ya kutopenda kula kwa mtoto ni kwamba mzazi wanatabia ya kuwapa watoto wao vitu vya udohoudoho kabla ya kula chakula kama vile chokleti, peremende, hivyo shauku ya kula kuhuka. Saa mbili kabla ya kula chakula tusiwape watoto chakula ili kuwafanya watoto wapate shauku ya kula na kuepuka hatari ya kuwalisha vibaya.

Pius wa kumi: Mtakatifu aliyelia machozi akikataa upapa

KANISA linapotualika kuwaheshimu watakatifu, halifanyi hivyo ili tu, tushangilie mambo makuu aliyoyafanya Mungu kutokana na neema zake. Bali pia linafanya hivyo kutushauri ili tuwaangalie kama mifano bora ya kutufaa katika harakati za kuelekea utakatifu kwani ndio wenye kutuonesha sura halisi ya Bwana Yesu Kristo.

Hii inatokana na ukweli kuwa maisha yao na jinsi walivyoishi, ni kielelezo kamili cha hali ya utakatifu wa Kikristo.

Ni dhahiri kuwa kuishi kikristo kunahusisha kila tukio katika maisha ya kila siku kwa sababu mawazo, maneno na matendo yote ya Kikristo, hayana budi kupatana kabisa na Injili ya Bwana.

Mtindo huo wa kuishi hauelekei kuwa rahisi walau kidogo na hii inadhihirisha ukweli kuwa kila Mtakatifu ni shujaa aliye shupavu. Pia ni wazi kuwa huo ushindi wake ni ushindi wa neema ya Mungu dhidi ya ukosefu na udhaifu wa kibinadamu.

Orodha yote ya watakatifu inadhihirisha kuwa Roho wa Yesu Kristo anazo nguvu ndani ya maisha ya binadamu ambaye huwaimarisha wale wote wenye kujitahidi kwa dhati kumtumikia Mungu.

Hata hivyo tofauti iliyopo katika njia walizoishi watakatifu mbalimbali ni kubwa mno. Utakatifu hufikiwa tu, kwa njia ya kumtafuta Kristo na kuiga namna yake ya kuishi kwa imani itokayo moyoni na sio kwa kufanya tu, ili uonekane machoni pa watu.

Kila mbatizwa anapaswa kujizoeza kuyaweka maisha yake yote mikononi mwa Mungu. Afanye hivyo hali akijitahidi kuyatekeleza mapenzi ya Mungu kwa namna yake binafsi kwani ni dhahiri kuwa mtu mmoja anaweza kutilia mkazo namna moja ya maisha ya kikristo na mwingine akakazia aina nyingine.

Kila mtu hana budi kuitambua njia yake mwenyewe kutokana na vipaji alivyojaliwa.

Leo katika safu yetu ya watakatifu, tunaye Mtakatifu Pius wa Kumi ambaye awali aliitwa, Yosefu Sarto.

Inaelezwa kuwa, alipochaguliwa kushika nafasi ya uongozi kama Papa, alikataa kata kata kwa kulia machozi. Hata hivyo, kulia kwake kulikuwa mithili ya maji ya moto yasiyounguza nyumba. Katu hakukusaidia lolote; kulikuwa ni kazi bure tu.

Hata hivyo alipoonywa, aliupokea mzigo huo mzito wa majukumu ya kiroho. Akasema, "Naupokea kama msalaba," na kweli, ndivyo ilivyokuwa. Aliupokea utawala huu kama msalaba alioupata toka mikononi mwa Mungu.

Wazazi wa Mtakatifu Pius wa Kumi waliokuwa wakiishi Riese katika mkoa wa Venis huko Italia, alikozaliwa Pius mwaka 1835, hawakuwa maarufu wala matajiri ingawa walikuwa watu wenye mwenendo mwema katika uchaji wa Mungu.

Mtakatifu Pius alifanya kazi vizuri kama padre msaidizi na baadaye akawa paroko. Kisha alikuwa kiongozi wa mambo ya kiroho wa seminari ya jimbo lake.

Hata hivyo, alipokuwa Papa hakuacha maisha yake ya zamani.

Aliendelea na unyoofu wake na hata alipokaribia mwisho wa maisha yake aliweza kuandika bila uongo; akasema "nilizaliwa maskini, nikaishi maskini, napenda kufa maskini".

Akisha kuwa Papa, Yosefu Sarto (Pius wa Kumi) aliliongoza Kanisa kwa uthabiti usiomithilika maana alikumbana na misukosuko mingi mwanzoni mwa karne ya 20. Mlengo na msimamo wake ulikuwa kuviweka vitu vyote chini ya usimamizi wa Kristo.

Papa Pius alianzisha vyama mbalimbali vilivyovutia baadhi ya vyama hivyo vilivyokuwa vya muziki wa kanisa uliorudishwa baadae katika hali nzuri na utukufu wake kama ilivyokuwa zamani.

Huko Roma alianzisha mafunzo ya Biblia na kulitengeneza kwa ustadi mkubwa Baraza Kuu la Kanisa la Roma. Haukusahau mpango wake thabiti juu ya kuanzisha mafunzo ya katekisimu na hata akamudu kuingiza desturi ya kupokea komunyo mara nyingi na hata kila siku. Pia alikubali watoto wadogo wanapopata akili wapokee komunyo.

Kwa juhudi zake kubwa, Mtakatifu Pius wa Kumi anayekumbwa kila ifikapo tarehe 21 mwezi Agosti, aliweka msingi wa Utume wa Walei Wakatoliki kulingana na mpango rasmi. Utume huo uliitwa "Aksyo Katoliki" yaani Utendaji wa Kikatoliki.

Juhudi zake na usafi wa kiroho,vilizaa matunda mengi mazuri ikiwa ni pamoja na kuimarisha zaidi maisha ya Kitawa na kuongeza seminari katika nchi kadhaa.

Mtakatifu Pius wa Kumi, aliyefariki Agosti 20, mwaka 1914 kutokana na kulemewa na kazi nyingi na ngumu, sambamba na vita vilivyoanza Ulaya siku zile, alizilaumu na kuzionesha waziwazi hila, njia na mila potofu na hatari katika kueleza Biblia na mambo makuu ya Kikatoliki zilizoitwa "Mordenism" yaani "Mambo leo"

Alikataa na kutupilia mbali ile haki ya Serikali kuwa na usemi katika Uchaguzi wa Papa.

Kwa shangwe kubwa, hoi hoi, nderemo na vifijo vingi, Pius wa kumi alitajwa kuwa mtakatifu mwaka 1954, baada ya kudhibitika kuwa alifanyika miujiza mingi iliyotokana na maombezi yake yaliyojaa imani ya kiroho.

Hukumbukwa kwa pamoja na watakatifu Sevus, Pritus, Zotikus, Moiseus, Astriusius ,Diomedes, Kwadratus na Zatamgelus.

Kwa nini kama taifa tunahitaji msingi wa maadili (3)

v Wazazi

Muundo wa maisha ya familia ndio mtima wa jamii. Hapo uhai huzaliwa na mioyo na akili za watoto kulelewa. Mitazamo, tabia, utathimini wa mambo hukuzwa hapa. Kusimama au kuanguka baadaye maishani huandaliwa hapa.

Familia inaonekanaje katika Tanzania leo hii? maisha ya familia leo yanapitia matatizo mengi na wazazi wengi hawajui watakavyoyakabili katika miaka ya usoni. Mashaka na wasiwasi huvunja nguvu na kuvuruga uwezekano wa watoto kulelewa katika mazingira yakuzayo vipaji na utundu. Matatizo kiuchumi ndio yanayoarifu siasa kama suala la kuchangia gharama katika afya na elimu litekelezwe. Uwezo tofauti wa sekta mbalimbali za watu kulipia gharama litekelezwe. Uwezo tofauti wa sekta mbalimbali za watu kulipia gharama hizo hauchunguzwi yakizuka matatizo kama Ukimwi na ongezeko la idadi ya watu njia za utatuzi hubuniwa bila kujali kwamba zinaharibu misingi ya kimaadili. Fedha nyingi hutumika pamoja na miswada toka nje lakini masuala ya kimaadili katika jamii hayaangaliwi.

"Wazazi wanahitaji wasaidiwe kuelewa wajibu wao kama walezi ili wawalee watoto wao, hivi kwamba thamani ya utu wao inatambulika." Wazazi wapewe fursa ya kutoa maoni yao waziwazi mathalani mintarafu utata unaowakabili nchini leo hii. wasachwe wakae kimya sababu hawajui watoeje maoni yao. Maamuzi ya mipango ya jamii lazima yawahusishe wazazi ndipo wategemewe kuchangia yatakiwayo kwa utatuzi wa masuala. Leo tunahitaji vyama vya wazazi.

Serikali kazi yake ni kukuza ushirikikishaji wa aina hii badala ya kuwaamrisha wazazi.

v Waalimu

Kazi ya walimu yahusiana na ile ya wazazi katika jamii licha ya kuelimisha ndio wanaoliunda taifa. Umuhimu wao katika taifa unajulikana wazi.

Lakini katika hali halisi sasa hivi, kazi ya ualimu imedhalilishwa sana. Mfano ni mgomo wa walimu hivi majuzi. mishahara finyu wapatayo inawaletea shida nyingi na kuwafanya watafute shughuli nyingine ili kuhakikisha huduma kwa familia zao. mfumo mzima wa elimu unabomoka na wanaoathirika ni walimu, wanafunzi, wazazi na taifa lote. hali hii imetuletea utata. Taifa linaelekea kushindwa kuendesha vema mipango ya elimu kwa watoto Serikali inapoanza kuwalaumu walimu na wanafunzi au watu kuilaumu Serikali ni kuyafumbia macho matatizo halisi. lazima walimu warejeshwe mara heshima wanayostahili. Tutegemee utendaji kazi bora kwao na tuwasaidie kwa kazi na juhudi yao.kuyaacha mambo yalivyo sasa hivi ni kufanya mchezo na hasara kubwa itatokea. Ni mtazamo wa kijinga kuyaacha maamuzi ya kiuchumi kutawala mipango ya elimu. kudidimiza viwango vya elimu ni kubomoa misingi ya jamii nzima haiwezekani upungufu wa fedha uwafanye watu waachie majukumu yao ya kuelimisha yawezekana kushindwa kuendeleza aina fulani za elimu ya kishule lakini jukumu la kuelimisha labakia palepale. Haiwezekani kabisa watu wazima kukwepa jukumu la kuelimisha watoto.

Hapa kufikiri na kutafakari kwingi kunatakiwa kuanzisha shule, mathalani kama huwezi kuiendesha ni tendo la udanganyifu.

Mfumo wa elimu sharti uone na ushirikishaji wa watu zaidi kuliko kuiachia Serikali kuu kuongoza kila kitu. Serikali za mitaa zipewe madaraka nazo ziwashirikishe wananchi. Hii haina maana kudai tu kuwe kuchangia gharama .

Lazima wanataaluma watoe maoni yao na usaidizi uwepo kwa ajili ya wale wasiojiweza kifedha.

Yakiachiwa mambo yaendelee kwa mwelekeo wa sasa hivi basi wenye mabavu na wajanja wachache watafaidi wakati walio wengi watavunjika moyo. Hii ni suala la jamii nzima na sio wakuu fulani wa Serikali.

Suala la walimu lina umuhimu mkubwa sana. mambo yalivyo sasa hayawasaidii walimu kutimiza wajibu wao wa kuridhisha mitazamo bora na thamani ya mambo pamoja na kuelimisha.

vViongozi

Maisha ya jamii yataka kiongozi katika nyanja zake mbalimbali kama siasa, taaluma, uchumi, dini na kadhalika.

Hivi uongozi wa kisiasa ni aina moja tu ya kuongoza lazima nafasi za aina hizo nyingine za uongozi zitambuliwe. uroho wa madaraka huhatarisha jamii. Wakishirikiana, viongozi wa nyanja hizo mbalimbali watajenga jamii. Wakigongana wataibomoa na kuharibu umoja.

Wakati uongozi bora uhudumia jamii uongozi mbovu hufakarisha jamii kwa kuwafanya watumwa, Aina zote za uongozi zilizotajwa zahusika hapa.

Haifai kuweka mamlaka makubwa mikononi mwa watu wachache, wengi hutumia vibaya mamlaka hayo. Mgawanyiko kati ya Serikali, Bunge na Mahakama inakusudiwa kuthibiti mgawanyo wa mamlaka unaodaiwa mgawanyo katika mfumo wa demokrasia.

Ndio maana demokrasia yadai kutenganisha Serikali na dini Tanzania hujisema kuwa Serikali yake haina dini ndio kudai kwamba hakuna kuingilia kati dini na siasa. Hili ni rahisi kutamka, gumu kulitekeleza kama tutakavyoona zaidi katika ibara ya 3.

Jambo la muhimu kukumbuka hapa ni kwamba kwa manufaa ya jamii yetu aina hizo mbalimbali uongozi zinatakiwa kutenda kazi kwa ajili ya wote, huku migongano kati yao ikiepukwa.

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

Yesu bandia azaa na wake wa wafuasi wake

MATAPELI wengi wamepata kuibuka wakijiita wao ni Yesu kiasi cha kupelekea watu wajenge imani kwao na hata kutoa mali zao zote kuwapa lakini aliyevunja rekodi kwa kwa utapeli wa kujuta Yesu ni Emmanuel Odumosu raia wa Nigeria.

Akawa ni msomi aliyefika chuo Kikuu Odumosu aliibuka na harakati zake mwanzoni mwa miaka ya 1980 ambapo alidai Mungu amemshukia na kumuonyesha kuwa yeye ndiye Yesu atakayeokoa ulimwenguni kwa mujibu wa jarida Africa Now.

Toka wakati huo mpaka sasa Odumosu ambaye ni mmoja wa matajiri wakubwa wa Nigeria ameishadanganya watu wengi sana wengi wanatokea kumuamini hasa kwa vishawishi vyake na jinsi alivyotapeli aliyebobea.

Jijini Lagos Bw. Odumosu amejenga mji wake mkubwa anaouita Yerusalem ndani yake kumejengwa nyumba za kifahari huku magari ghali yakiwa yameegeshwa ndani ya mji huo unaoitwa Jerusalem ulio kimbilio la ombaomba ndani ya Lagos cha kushangaza ni tabia aliyo nayo Yesu Odumosu ya kuwapora wafuasi wake wake zao mara tu wanapojiunga naye na kuhamia ndani ya Yerusalem.

Odumosu amewapiga marufuju wafuasi wake kushirikiana na wake zao kwa madai kuwa wakifanya hivyo watazaa kizazi chenye dhambi. Badala yake amewaagiza kuwa ni yeye pekee ndiye mwenye haki ya kuwa na uhusiano nao kwa sababu akifanya hivyo atawapelekea kuzaa kizazi kisicho na dhambi wala mawaa.

Masharti ya kujiunga na imani ya Odumosu ni kwanza kamkabidhi mkeo na mama yako na hata dada zako wote wawe wake zake halali wa ndoa.

Kufuatia mtindo wake huo wa kuwapora watu wanaohamia Yerusalemu wake zao sasa hivi mji huo umezaa watoto na vijana wa rika mbalimbali wanaofanana sura zao mithili ya Wachina.

Wote hao wanafanya kazi kwenye miradi mbalimbali inayoendeshwa na Emmanule Odumosu jijini Lagos.

Miradi hiyo ni pamoja na kiwanda cha kuoka mikate, kiwanda cha mfuta ya kupikia chakula, maduka ya jumla, Mahoteli magaru ya usafiri.

Mradi wa upasuaji mbao na utengenezaji fenicha (samani) na kampuni kubwa ya kuagiza na kusafirisha bidhaa mbalimbali kwenda ndani na nje ya nchi.

Pamoja na kuwa baadhi ya wanaume waliomshitukia Odumosu wameamua kuchukua wake zao na kutoroka toka "Yerusalemu" hiyo iliyoko eneo la Ikeja jijini Lagos. Wanaume walio wengi wenye ukata wao wamekubali kuwatoa wake zao dhabihu halali kwa Odumosu ili mradi wapate kula yao na nyumba nzuri za kuishi bure ndani ya 'Yerusalemu'.

Emmanuel Odumosu alizaliwa mnamo mwaka 1948 huko Abeokuta Nigeria. alisemea kwenye chuo Kikuu cha Iloron State Univerisity kilichoko Nigeria na kisha akaajiriwa Serikali kama mwalimu kwenye vyuo vya ufundi.

Baada ya kufanya kazi ya ualimu wa miaka 8 , Odumosu alijiuzulu kazi na kufungua mradi wa upasuaji mbao na utengenezaji fenicha mradi anaomudua kuuendesha hata leo baada ya kujegeuza Yesu bandia. Ndoto za kujigeuza Yesu aliibuka nazo baada ya kuacha kazi ya ualimu.

Odumosu ni Yesu wa aina yake yeye ni Yesu mfanya biashara kutenda dhambi zote za dunia hii.