Make your own free website on Tripod.com

MAKALA MAALUM

Siku ya msamaria mwema 3, Septemba 2000

+ Askofu Agapit Ndorobo Mwenyekiti: Caritas Tanzania.

Wapendwa Wakristu na watu wote wenye mapenzi mema,

MWAKA 2000 ni Mwaka Mtakatifu, mwaka wa ukombozi uliotuingiza katika karne ya Ishirini na moja, Milenia ya Tatu.

Katika mwaka huu mtakatifu, Mama Kanisa anamwalika kila mmoja wetu kupokea neema za pekee kutoka kwa Mungu Baba ili ziweze kutusaidia katika safari yetu ya maisha hapa duniani katika kumwelekea Baba wa mbinguni.

Kama ilivyo kawaida ya kila mwaka inapofika mwezi Septemba, Jumapili ya Kwanza, tunaadhimisha Siku ya Msamaria Mwema.

Siku ya Msamaria Mwema inamkumbusha kila mmoja wetu juu ya upendo kwa jirani. Ni nafasi ya pekee kwetu kujichunguza katika kipindi cha mwaka mzima uliopita tumeonesha upendo gani kwa jirani zetu.

Katika Injili ya Mtakatifu Mathayo, husisitizwa juu ya upendo kwa jirani na kusema, "Mpende jirani yako kama nafsi yako." (Mathayo 19:19). Upendo kwa jirani siyo jambo la hiari ni Amri inayotutaka tutekeleze ili kuingia Ufalme wa Mungu.

Yesu mwenyewe alimwambia waziwazi mmojawpo wa waandishi aliyekuja kumuuliza ipi ni Amri ya Kwanza. Akimweleza, alisema, "Sikia, Ee Israel, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja, nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote na kwa nguvu zako zote."

Na ya pili ndiyo hii, "Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna Amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi." (Marko 12:29-31).

Isitoshe upendo kwa jirani ni kanuni bora ya maisha kama Injili ya Mathayo inavyotueleza. "Basi yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo maana hiyo ndiyo torati na manabii (Mathayo:7:12). Kumbe basi upendo kwa jirani ni Amri aliyoagiza Yesu mwenyewe; ni sheria ya Musa na mafundisho ya manabii yaliyoelekezwa kwa watu wote ili wayafuate.

Tunapoadhimisha Siku ya Msamaria Mwema, tunakumbuka jinsi Msamaria Mwema alivyomsaidia msafiri aliyefikwa na majanga ya kupigwa na kunyang’anywa mali yake yote na kuachwa mahututi.

Fundisho hilo amelitumia Bwana Yesu kwa kumuelimisha mwanasheria aliyetaka kujua jirani yake ni nani. Yesu alimpa mfano huu: "Mtu mmoja alishuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, akanguka kati ya wanyang’anyi, wakamvua nguo, wakampa jeraha, wakaenda zao wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu, kuhani mmoja alishuka kwa njia ile na alipomwona alipitia kando.

Na Mlawi vivyo hivyo alipofika pale akamwona akapita kando. Lakini Msamaria mmoja katika kusafiri kwake, alifika hapo alipo na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akamtia mafuta na divai akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza.

Hata siku ya pili akatoa dinari mbili akampa mwenye nyumba ya wageni akisema, "Mtunze huyu, na chochote utakachogharimia zaidi mimi nitakaporudi nitalipa’. Luka 10:30 -36.

Kwa kupitia shirika la LILIAN la Uholanzi, Caritas Tanzania imepokea shilingi 32,670,311.95 kusaidia watoto 167 wa kuanzia umri wa mwezi mmoja hadi miaka 25 tu, wenye ulemavu mbalimbali.

Katika kipindi hiki cha 1998-1999 Caritas imepokea shilingi 367,074,042 kutoka kwa wahisani mbalimbali kununulia chakula cha njaa. Tani 1,330 za chakula zilinunuliwa na kugawiwa watu zaidi ya 216,602 katika majimbo 22. Na katika kipindi cha 1999-2000 Machi, zoezi hili liliendelea baada ya kupata msaada wa shilingi 102,649,864 na kununua chakula katika majimbo 10.

Aidha, Caritas imepokea Shs 359,610.04 za kusaidia wakimbizi katika Jimbo la Kigoma. Wakimbizi 341 walihudumiwa katika ofisi ya Taifa kwa ufadhili uliotoka shirika la Secour Catholic lililotoa shs.10,837,195.

Yesu akazidi kumwuliza, "Waonaje wewe katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake, yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi?’ Naye Mwanasheria alijibu akasema, "Ni huyo aliyemwonea huruma." (Luka 10:36-37).

Na kwetu sisi mfano huo wa Msamaria Mwema unatuonesha jinsi tunavyopaswa kufanya. Yaani, kuwahurumia wenye shida, kutoa huduma kwa kuwatunza na kutoa chochote kwa ukarimu.

Katika Waraka wake wa Kwanza kwa Timotheo 6:17-19 Mtume Paulo aliagiza yafuatayo; "Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune wala wasiutumainie utajiri usio yakini bali wamtumainiye Mungu, atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha.

Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo; huku wakijiwekea akiba, iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli."

Tunasoma pia katika Mithali 14:21 mstari wa pili: "Bali amhurumiaye maskini ana heri, na katika Mithali 31:9 mstari wa pili, tunakumbushwa tuwapatie maskini na wahitaji haki yao.

Baada ya kusikia hayo yote, je tutaiadhimishaje Siku ya Msamaria Mwema ya Mwaka 2000.

Kama dhamira ya Siku ya Msamaria Mwema inavyotuambia waziwazi; "Tuipokee neema ya Mungu na tutende mema daima." Kutenda mema ni wajibu wa kila mmoja wetu, ndiyo maana ya ujirani mwema, ni kusaidiana katika shida hata kushirikiana katika furaha.

Wakati wa maisha yake Yesu hapa duniani, alituonesha mfano wa mambo mengi ya kuigwa. Alihubiri na kutenda matendo mema, alikuwa ndiye Msamaria wa kwanza kwa kuwatibu wagonjwa na kuwapa chakula wenye njaa.

Tunaona hata leo, wafuasi bado wanafuata mfano wake wa kuhubiri Habari Njema na kutoa huduma.

Wanajenga makanisa mahali pa kuhubiri Habari Njema. Wanajenga hospitali mahali pa kutoa huduma za afya na malazi kwa wasiojiweza yaani maskini, yatima, na wazee.

Wanajenga shule ili kutoa elimu na kuleta maendeleo kwa watu na wanatoa vyombo mbalimbali kufuatilia utekelezaji wa kila huduma.

CARITAS Tanzania ni chombo cha Maaskofu Katoliki Tanzania ambacho hushughulikia maendeleo ya jamii.

Muundo wa chombo hiki ni kuanzia kwenye jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, parokia, jimbo na mwisho ndiyo kitaifa yaani CARITAS Tanzania.

Kama CARITAS inavyojieleza yenyewe "KILA BINADAMU NI NDUGU" , hivyo chombo hiki hutoa huduma yake bila ubaguzi wa rangi au dini. Katika kipindi cha mwaka 1999 CARITAS imetoa msaada wa Shs.4,016,819/= kwa watu wenye shida 115 Wakati mapato yalikuwa ni shilingi 1,688,386/= tu.

CARITAS Tanzania mwaka 2000, inataka kuimarisha huduma yake huko majimboni, ambako ndiko kwenye chimbuko la walengwa na wenye kutoa misaada. Kwa kuzingatia kuimarisha huduma za maendeleo kwa jamii yote katika nyanja zote ili kuondokana na matatizo mbalimbali yanayoisonga jamii wakiwemo watoto, vijana, wanawake na wazee. k.m, njaa, magonjwa, umaskini na hivyo kuinua hali zao za maisha ili yawe bora zaidi.

Hivyo lengo la CARITAS Tanzania ni kuhamasisha Wakristo na wote wenye mapenzi mema hasa kwenye jumuiya ndogo ndogo ambako ndiko kwenye familia, ili kwamba kila mmoja aguswe na neno hilo.

Kwa hiyo tuipokee neema ya Mungu na tutende mema daima.

Ujumbe wa Kwaresma wa 1996 unakumbusha kuwa "Wajibu wetu wa kuishi matendo mema na uadilifi unatokana na ukweli kwamba imani peke yake bila matendo imekufa. (Yak. 2:17), na tunda bora la Imani, ni upendo ambao ndio kifungo cha ukamilifu.

Sisi tukisukumwa na Imani thabiti, lazima tujinyime hata kile kidogo tulichonacho na tuwajali wale wenye shida zaidi.

Kama tunavyoona hali mbaya ya hewa imeathiri kilimo na njaa, bado inaendelea, pamoja na kwamba hali ya uchumi inakuwa nzuri kidogo, lakini ni wachache tu wanaofaidika, wengine wote tuko bado maskini, tunashindwa hata kujihudumia kwa matibabu.

Vita katika nchi jirani, hakuna amani, hivyo wakimbizi wanazidi kuingia hapa nchini. Na janga la Ukimwi linaloacha watoto wengi yatima na familia nyingi kuwa maskini kutokana na gharama kubwa wanazotumia kwa matibabu.

Kwa hiyo, tunawahimiza watu binafsi, familia, Jumuiya ndogoNdogo za Kikristo, Vikundi mbalimbali na Vyama vya kitume, wote waendelee kukuza na kudumisha moyo wa ukarimu kwa wahitaji wote.

Tunapofanya hayo si kwamba tu, mnadhihirisha ukomavu wa Ukristo wenu, na maisha yenu bali mnavuta huruma ya Mungu iwajie nyinyi wenyewe.

(Rejea Ujumbe wa Kwaresima 1996 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania). Kufanya yote upya katika Kristo. Uk. 8.Kif.8.

Kama tunavyoalikwa na Mwenyezi Mungu, "TAZAMA NIMEKUCHORA KATIKA VITANGA VYA MIKONO YANGU", (Isaya 49:16). Mwenyezi Mungu anatuona, anatujua, anatupenda, basi nasi hatuna budi kuoneana huruma.

Tuipokee neema ya Mungu Daima na tutende mema daima.