Make your own free website on Tripod.com

Wasifu wa Askofu Msaidizi Mteule

Dk. Method Mutegeki Nkyabonaki Kilaini

Na Dalphina Rubyema

MIONGONI mwa Mapadre waliopata daraja la upadre wakiwa na umri mdogo ni Askofu Msaidizi Mteule wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam,Method Kilaini ambaye alipata daraja hilo akiwa na umri wa miaka 24. Aliteuliwa na Papa Yohane Paulo ll, Januari 8, mwaka huu kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu katoliki la Dar es Salaam, na anatarajiwa kupata rasmi daraja la Uaskofu Machi 18, mwaka huu.

Askofu Mteule Kilaini ambaye ni mtoto wa Mzee Paulo Mutegeki na Bibi Asteria Kokutona Balilonda, wa Katoma Kyamtwara, Jimboni Bukoba, pamoja na kupata daraja hilo akiwa na umri kama huo lakini alikuwa "moto wa kuotea mbali" kitaaluma kwani kabla hajawa padre tayari alikwishajipatia shahada ya kwanza (B.A) na ya pili (STL) katika somo la Theolojia kutoka Chuo Kikuu cha Urbaniana -Roma.

Askofu Mteule Kilaini ambaye ana Shahada ya juu ya Udaktari (PhD) katika Historia ya Kanisa aliyoipata katika Chuo Kikuu maarufu cha Wajesuiti cha Gregoriana kilichopo Roma, pia amaetunukiwa tunu ya utunzi wa vitabu ambapo moja ya vitabu alivyoandika ni kitabu kinachoelezea Historia ya Kanisa Kagera (Bukoba na Rulenge).

Askofu Mteuele Kilaini ambaye ni mfupi kwa umbo la nje, anaoneka kuwa mtu wa kawaida huku hekima na busara zake zikiwa zimejificha ndani ya kichwa chake kidogo na tabia yake ya kutojikweza.

Pamoja na kuwa na utaalamu wa kutumia Kompyuta na mpenzi wa chombo hicho, lakini vile vile ni mtundu katika upigaji wa picha za video hali ambayo ilimfanya mwaka 1990 akiwa Roma aitwe haraka na Maaskofu kurejea nchini kusaidia kupiga picha za video katika ujio wa BabaMtakatifu.

Ni vigumu kutoamini kwamba Maaskofu nchini waliona wakichelewa kutumia tunu ya kipaji ya Askofu Mteule Kilaini watapoteza mengi, ndio maana waliamua kumpa nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Baraza la Maaskotu Katoliki Tanzania (TEC) ambayo ameishika kwa muda wa miaka tisa kwa awamu tatu tofauti.

Bila shaka utendaji wake mzuri wa kazi ndio uliomfanya hata Baba Mtakatifu amteue kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam kabla hata hajamaliza kipindi chake cha uongozi na sababu kama hizo ndizo zilizomfanya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, akubali kufanya kazi na Askofu huyo.

Historia ya Askofu Mteule Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam

Askofu Mteule Method Kilain alizaliwa mnamo Machi 30 mwaka 1948 katika Kliniki ya Kalema-Kashozi Jimboni Bukoba.Baba yake ni Mzee Paulo Mutegeki mtoto wa Nkyabonaki Kilaini wa ukoo wa Abaiyuzi na Mama yake ni Bibi Asteria Kokutona binti Balilonda wa ukoo wa Abagiri ambapo wazazi wote ni wazaliwa wa Kyamtwara,Bukoba.

Akiwa na umri wa miaka sita,Askofu Mteule Kilaini alianza shule ya awali (chekechea) ya Bushaza -Katoma ambako licha ya kujifunza kusoma na kuandika vilevile alijifunza katekisimu na baadaye kupata komunio ya kwanza.

Baada ya kupata komuni ya kwanza,Askofu Mteule alianza darasa la kwanza katika shule ya Msingi Bushaza ambapo alisoma shuleni hapo hadi darasa la nne na hapo ilikuwa ni 1955-1958.

Mwaka mmoja baada ya kumaliza darasa la nne,alishinda mtihani na kuchaguliwa kujiunga na shule ya Modal Middle School ya Rugongo iliyopo Katoma.

Juhudi katika masomo yake zilimfanya Askofu Mteule Kilaini achaguliwe kuingia darasa la sita katika Seminari ya Bunena kabla hajaingia darasa la saba Seminarini Rutabo Kamachumu.

Mwaka 1962-1966 Askofu Mteule Kilaini alijiunga na Seminari ya Rubya ambako alisoma darasa la nane hadi la 12 ambapo alifanya mtihani wa Cambridge na kujinyakulia daraja la kwanza.

Mwaka uliofuata baada ya kumaliza darasa la 12,alijiunga na Seminari Kuu ya Ntungamo iliyopo Jimboni Bukoba na kujifunza Falsafa ambapo alichukuwa masomo hayo kwa muda wa mwaka mmoja.

Baada ya kumaliza masomo ya Falsafa,mwaka 1968-1972Askofu Mteule Kilaini alijiunga katika Chuo Kikuu cha Urbaniana lichopo Roma ambapo alijipatia Shahada ya kwanza (B.A) na ya pili (STL) katika somo la Teolojia pamoja na kujinyakulia cheti cha lugha ya Kiitaliani kutoka katika chuo kikuu cha Perugia na cheti cha lugha ya Kifaransa katika Chuo Kukuu cha Paris na katika chuo cha Goethe kilichopo Roma alijipatia cheti cha lugha ya Kijerumani.Wakati huo pia alijipatia stashahada ya elimu katika Afrika kutoka Chuo Kikuu cha Urbaniana.

Baada ya kumaliza masomo yake,akiwa bado Roma Machi 18 mwaka 1972 Askofu Mteule Kilaini alipata upadrisho na Kardinali Rosi ,Mkuu wa Idara ya Uinjilishaji.Katika ibada hiyo ya upadrisho pia alihuzulia na Kardinali Gantin Mkuu wa sasa wa Idara ya Maaskofu.

Kabla ya kusoma misa ya kwanza katika nyumba ya makao makuu ya Wamisionari wa Afrika (White Fathers) ambao ndio waliombatiza na kumpa kipaimara,Askofu Mteule Kilaini alipokelewa na kupewa mkono na Baba Mtakatifu Paulo wa VI.

Agosti 1972 baada ya kupata upadrisho,Askofu Mteule Kilaini alirudi nchini na kuanza kazi yake ya kichungaji katika Parokia ya Mwemage Jimboni Bukoba ambapo kama Msaidizi wa parokia hiyo alishughulikia vigango vya Rutete na Nyakigando kabla ajahamia katika Seminari ndogo ya Rubya ambapo alikaa hapo kwa muhula mmoja tangu Julai 1973- Desemba 1973 akiwa anafundisha masomo ya hesabu, historia na dini.

Baada ya kutoka katika seminaro ndogo ya Rubya,Kilaini alifanya kazi katika parokia ya Rutabo kwa kipindi cha mwaka mmoja (Desemba 1973-Septemba 1974) ambapo alishughulikia masuala ya vijana hasa wale wa Mtakatifu Kizito.

Septemba 1978-Januari 1981 Askofu Mteule Kilaini alihamishiwa Jimboni ambapo alikuwa mweka hazina Msaidizi wa Jimbo la Bukoba na wakati huo ilibidi awajibike katika kutafuta vitu muhimu kwa ajili ya parokia,hospitali na shule za jimbo hilo.

Wakati huo akiwa Mweka hazina msaidizi,Akofu mteule pia alifundisha somo la Historia ya kanisa katika seminari Kuu ya Ntungamo na kwakuwa ilidhihilika kuwa hawezi kufanya kazi mbili kwa wakati mmoja basi ilibidi apewe kazi ya kufundisha tu katika seminari hiyo na kuacha nafasi ya uhasibu ambapo alikaa Seminarini hapo tangu Januari 1981-1985.

Juni 1985-Juni 1990 Padre Method alitumwa tena kwenda Roma kujifunzia shahada ya juu ya Kanisa katika Chuo Kikuu maarufu cha wajesuiti cha Gregoriana ambapo baada ya kupata shahada ya M.A (Licence) ya somo hilo aliendelea na kupata shahada ja juu ya udaktari (PhD) katika somo hilo,ilikupata shahada hiyo aliandika kitabu juu ya historia ya kanisa katika Kagera (Bukoba na Rulenge).

Katika miaka hiyo pia alijifunza namna mbalimbali za kichungaji katika maparokia mbalimbali Italia na Ujerumani pamoja na kujifunza elimu ya kompyuta ambayo wakati huo kilikuwa kitu kigeni sana.

Januari 1991,Askofu Msaaidi Mteule aliteuliwa kama kama Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na kamati tendaji ya Baraza hilo ambapo Julai mwaka huo huo alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa baraza hilo kuwa katibu Mkuu kwa miaka mitatu lakini bidii yake zilifanya ashike wadhifa huo kwa kipindi cha miaka tisa mufululizo na kabla hajamaliza kipindi chake cha uongozi,Januari 8 mwaka huu Ilitangazwa kuwa Baba Mtakatifu amemteua kuwa Askofu Mkuu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam.

Mipango ya Mungu si ya mwanadamu

Askofu Mteule Kilaini aliazimia kuwa Juni, mwaka huu baada ya kumaliza kipindi chake cha tatu cha Ukatibu Mkuu wa TEC, angekwenda kufanya utafiti na kufundisha somo la Historia ya kanisa kwenye Chuo Kikuu cha Dayton kilichopo nchini Marekani, mpango ambao ulishafanikiwa.

"Nilikuwa napanga yangu wakati Mungu naye anapanga yake,"

Sifa za Pekee

Askofu Mteule Kilaini ameweza kukutana na kupeana mkono na kupata baraka za Baba Mtakatifu Yohana Paulo wa II zaidi ya mara saba.

Ameyatembelea karibu majimbo yote ya Tanzania na katika nchi za nje ametembelea nchini KenyA,Malawi, Uganda, ZImbabwe,Italia,Belgium, Ujerumani, Marekani, Uswizi,

Austria,Uholanzi na kupata nafasi ya kuongoza hija huko nchi Takatifu.Kilaini Ana uwezo wa kuongea lugha ya Kihaya, Kiswahili, Kingereza, Kiitaliano,Kifaransa na Kijerumani.

Misukosuko

Askofu Mteule Kilaiini anakumbuka ajali mbaya ya gari aliyoipata huko Pasiansi, mkoani Mwanza ambapo aliumia vibaya na kupoteza fahamu kwa muda wa wiki moja. Ilipochunguzwa na Daktari Bingwa ilibainika kuwa fuvu la kichwa chake lilikuwa kimepasuka na kugawanyika likishikiliwa na ngozi tu.

Akielezea mkasa huo mzito,Askofu Mteule anasema kuwa ilikuwa Novemba 15 mwaka 1981 akiwa na viongozi wengine wa kiroho walipopata ajali mbaya ya gari katika eneo hilo la Pasiansi, Mwanza wakati wakielekea uwanja wa ndege kupanda ndege kuelekea Dar-Es-Salaam kwenye mkutano.

Alisema katika ajali hiyo ambayo yeye binafsi alikuwa anakuja kwenye mkutano huo akiwa kama Mwalimu wa Seminari Kuu ya Ntungamo na Mtunza fedha wa seminari hiyo iliyopo Jimboni Bukoba,pia alikuwemo Askofu Castol Sekwa ambaye alivunjika mguu,Gombera wa Seminari ya Rubya Padre Simon Rutatekululwa,Padre Peter kutoka Rulenge na Padre Deogratias Rweyemamu ambaye naye aliumia vibaya.

Alisema baada ya ajali hiyo majeruhi wote walipelekwa katika hospitali ya Bugando ambapo Daktari mmoja wa hospitali hiyo aliyemtaja kwa jina la Dk.Makwani, alimchunguza afya yake na kukuta kichwa kimepasuka.

Alisema alikaa hospitalini hapo kwa muda wa mwezi mmoja kabla ya kwenda kwenye hospitali ya KCMC kwa matibabu zaidi.

Mwaka mmoja baada ya ajali hiyo mbaya, Askofu Mteule Kilaini alitakiwa kwenda Roma kuchunguzwa zaidi lakini akiwa katika safari ya kwenda huko alikumbwa na mkasa mwingine wa kutisha; ndege aliyopanda ilitekwa na maharamia.

Akielezea mkasa huo uliotokea Februari 27, 1982 Askofu Mteule alisema kuwa akiwa amepanda ndege ya ATC kutoka Mwanza kwenda Dar-Es-Saalam ambapo alitarajia kupanda ndege nyingine kwenda Roma ,ndege hiyo haikuweza kufika Dar-Es-Saalam na badala yake ilitekwa ikiwa njiani na kupelekwa Nairobi, Kenya, ikaelekea Jeddah, kisha Athens, Ugiriki. Huku ikitua tu na kuweka mafuta katika maeneo hayo na sehemu nyingine ikinyimwa, ilikwenda moja kwa moja London, Uingereza. Ndege hiyo ilitekwa na wahaini watano, wawili kutoka Zanzibar na wengine Tanzania Bara.

Akieleza zaidi juu ya mkasa huo mzito katika maisha yake,Askofu huyo Mteule alisema kuwa maharamia hao ambao walidai wanataka kuikomboa Tanzania walimpiga risasi mmoja wao katika tako, hali iliyosababisha hofu kuu ndani ya ndege.

Alisema yeye alipata msukosuko zaidi kwani kwa vile alikuwa na tiketi ya daraja la kwanza (first Class) hivyo alidhaniwa kuwa ni mwanasiasa.

Alisema walipofika London, Waziri Mkuu wa Uingereza enzi hizo akiwa Magreth Thatcher alitoa amri kwamba ndege iachiwe iingie lakini kwa vyovyote isiruhusiwe kuondoka. Alisema maongezi ya kina yalifanyika kati ya Serikali ya Uingereza na watekaji hao na hapo ndipo waliporuhusiwa kutelemka kwenye ndege hiyo na kuanza kupata huduma nchini humo, lakini wakiwa wameshateseka kwa njaa vya kutosha.

Baada ya mkasa huo, Askofu mteuele alisema kuwa serikali ya Tanzania ilitaka watu wake kurudi nchini lakini kwa vile yeye alikuwa na vyeti vya daktari,paspoti na vitambulisho vingine vilivyoonyesha alikuwa akienda Roma kwa matibabu, kwake tukio hilo likageuka kuwa lifti, japo yenye "kasheshe" kwani aliruhusiwa kuendelea na safari yake.

Akiwa huko aliweza kufanyiwa uchnguzi wa kichwa chake ana kukutwa hakina matatizo makubwa na kwamba anaweza kuendelea na kazi bila matatizo.

"Sitaweza kuusahahu mkasa huo," hiyo ni sentensi yake ya mwisho baada ya hadithi hiyo ndefu.

Mafanikio kama Katibu Mkuu wa TEC

Tangu achaguliwe kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) mwaka 1991 hadi hivi leo alipoteuliwa nafasi hiyo uaskofu ameweza kufanya mambo mengi. "Usiseme nimeleta maendeleo makubwa, hapana sema Sekretarieti kwa sababu hakuna nililofanya peke yangu; nashirikiana na wenzangu," anasema Kilaini, japo dai hilo haliondoi ukweli kwamba yeye kama kiongozi ana umuhimu wa kipekee kupongezwa katika maendeleo hayo.

Baadhi ya maendeleo hayo katika eneo la Makao makuu ya TEC ni kumalizia ujenzi wa nyumba ya mapadre, ujenzi wa hosteli ya Rugambwa yenye ghorofa nne, ujenzi wa nyumba ya Masista, nyumba ya kulia chakula Mapadre, ghala, pamoja na ununuzi wa kiwanja kilichopo nyuma ya hosteli ya Rugambwa.

Askofu mteule pamoja na kuimarisha idara za utume wa Walei,Uchungaji na Liturjia, Caritas,Uhasibu , Elimu, Afya na Mawasiliano pia ameweza kuunda Idara ya Katetesi ambapo Idara hiyo imefikia hatua ya kutafsiri kitabu cha Katekisimu kwa lugha ya Kiswahili, kazi iliyochukua muda wa miaka miwili.

Mahusiano na dini nyingine

Askofu Mteule Kilaini katika uongozi wake pia ameweza kuimarisha mahusiano na viongozi wa taasisi nyingine za kidini ikiwemo BAKWATA, CCT na kadhalika.

Kwa ushirikiano wa Kanisa Katoliki na Waprotestanti imewezekana kuandika kitabu kinachotumika mashuleni cha elimu ya jamii kwa ajili ya kujenga maadili mema.

Kadhalika kwa ushirikiano huo limeanzishwa shirika la pamoja la huduma za jamii ambalo limekuwa na mafanikio makubwa. Hayo ni machache kati ya mengi.

Salamu na mtazamo wa Rais Mkapa

Askofu Mteule Method Kilaini, amepokea Salamu nyingi za Pongezi kutoka kwa watu mbali mbali wakiwemo Maaskofu karibu wote nchini, marafiki wa nchi za nje, ikiwemo Roma, Ujerumani, Uswisi na kadhalika. Pamoja na hao yumo Rais wa Tanzania, Benjamin william Mkapa.

Katika Salamu zake za pongezi kwa Askofu huyo Mteule, Rais Mkapa amesema yafuatayo:

"Nimearifiwa rasmi na Balozi wa Vatican nchini, Mhashamu Luigi Pezzuto, kuwa Baba Mtakatifu, Yohane Paulo ll, amekuteua uwe Askofu (Auxiliary Bishop) katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Wanaojua uhodari wako na bidii, usomi wako na uelewa wa hali ya juu, umakini wako na nidhamu ya kupigiwa mfano, miongoni mwa sifa zako nyingine, sikushangazwa hata kidogo na uteuzi huo, ambao mimi binafsi umenifurahisha sana."