Make your own free website on Tripod.com

Maisha na Mikasa

Aliyetelekezwa na Mzaire ajikuta kwenye kambi ya wakoma

Ahofia kudhulumiwa kiwanja na maafisa wa Ardhi

BAADA ya kumaliza elimu ya msingi kwenye shule ya Futo- Kurasini alijiunga na chuo cha Polisi kilichopo mkoani Kilimanjaro mwaka 1970.

Huyo ni Bi. Asia Ally, mwanamke ambaye hivi sasa ni mkoma na ametelekezwa na mumewe. Mwandishi Wetu DALPHINA RUBYEMA anaandika masimulizi ya mkasa wa Bi. Asia.

Asia ambaye hivi sasa anaishi katika kambi ya walemavu ya Nunge, eneo la Kigamboni jijini, anasema alifanikiwa kuajiriwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay ambapo alikaa kwa miaka miwili.

Mwaka 1976 alihamishiwa kituo cha Urafiki ambapo baada ya muda, yeye na wenzake kadhaa, walipewa tena mafunzo na yeye kwa kuonesha juhudi, alipata nafasi ya kwenda kufungua kituo cha usalama barabarani kilicho jijini.

Anasema kabla hajaamua kuacha kazi hiyo ya uaskari aliyoifanya kwa muda wa miaka 14 tu, alihamishiwa kwenye kituo cha Polisi, Magomeni. Huo ulikuwa mwaka 1983.

Anasema kipindi hicho alikuwa amezaa watoto wake watatu na Mwanamuziki wa Bendi ya Makwizi, Mulamba Kazadi, na kutokana na kuona matatizo kadhaa yanamwandama kazini, ilibidi aombe kustaafu kazi na kupewa haki yake. Hivyo, aliacha kazi mwaka 1984.

Bibi Asia, ambaye ana akili timamu na nguvu za kutosha ingawa anaonekana kudhoofika kutokana na lishe duni anayoipata anasema,

"Niliona bora niache kazi maana watu walianza kuniandama kunipa rushwa, nami niliona hawa wanataka mimi nikamatwe na rushwa kusudi nisipate kiinua mgongo changu, hivyo niliona bora niwawahi, nikaamu kuacha kazi."Ndiyo hayo maelezo yake yeye mwenyewe.

Anasema kwa vile alikuwa amekwishazaa tayari na mwanamuziki huyo ambaye ni mjomba wa Dk. Remmy Ongala, aliona bora akae naye moja kwa moja kama mke na mumewe huko Kasai, Zaire ambapo aliongozana na mumewe na watoto wao.

Bi. Asia ama maarufu kwa jina la Mama Kazadi, anasema baada ya kufika huko Zaire, maisha yalikuwa mazuri sana kwani waliweza kuishi na mumewe raha mustarehe kwa kuwa huyo Mulamba aliweza kufanya safari zake za kuja nchini Tanzania na kuendeleza fani yake huku mara kwa mara, akirejea nyumbani kwake nchini Zaire kuangalia familia yake.

Anasema katika kipindi hicho, walifanikiwa kupata watoto wengine watano hivyo kufanya jumla ya watoto wote kuwa wanane wakiwemo wa kiume wanne na waliobaki ni wasichana.

Anasema baada ya nchi ya Zaire kuanza kuwa na hali ya machafuko, mumewe alimtaka mama huyo atangulie na watoto kurudi nchini Tanzania kwa ahadi kuwa na yeye atafuata nyuma muda si mrefu.

Asia anasema kwa vile hakuwa na mashaka yoyote aliamua kurudi nchini na huo ulikuwa ni mwaka 1990.

Anasema baada ya kufika nchini ambako alifikia katika jiji la Dar-Es-Salaam, alianza kukaa kwa ndugu na jamaa ambao hata hivyo hakupenda majina yao yatajwe.

Mwaka mmoja ulipita bila kumuona wala kupata taarifa za mume wake hali hiyo, ilimpa sana wasi wasi.

Mwaka huo wa 1991 Desemba, alifika ndugu yake mmoja akitokea Zaire na kumwambia kuwa amemwona mumewe na amemtuma amletee taarifa kuwa yeye atafika nchini Tanzania muda si mrefu.

"Mwanangu (Mwandishi),siku hiyo nilifurahi sana maana nilijua kuwa mume wangu baba Kazidi, bado yungali hai.

Nilikuwa tayari nimeshamuwazia vibaya kwa kudhania pengine amekufa," anasema.

Anaongeza kwa kusema kuwa, mwaka ulikatika bila kumwona hadi hivi leo.

"Sasa ni kwa sababu nilikuwa sijui kama yungali hai ama haya machafuko hayo ya Wazaire yamemchukua. Nakumbuka sana Mulamba, nakumbuka hata alivyotamba kwenye bendi mbalimbali ikiwemo Super Matimila, Makwizi na nyingine nyingi," anasema.

Anasema kutokana na utitiri wa watoto aliokuwa nao aliona ni kero kwa ndugu hivyo, aliona njia rahisi ni kwenda ofisi ya Waziri Mkuu enzi hizo alikuwa Samweli Malecela, na bahati nzuri Waziri alimwelewa vizuri.

Anasema kutokana na kujieleza na kueleweka vizuri, Waziri aliamuru watendaji wake wampeleke huko Kongowe, mkoani Pwani na kumnunulia kiwanja pamoja na kumjengea nyumba.

"Alimanusura, tuliongozana na bwana mmoja anaitwa Penza, kutoka ofisi ya Waziri Mkuu. Kufika Kongowe, tulienda kwenye ofisi ya CCM katani hapo mwaka 1998"

"Kufika hapo Penza aliwaeleza nia yetu sisi kufika pale. Walituelewa na kutuonesha kiwanja, kisha walitaka tuwape Sh. 300,000/= lakini tuliongea kibiashara na kuafikiana kutoa sh 130,000," anasema.

Anaongeza kuwa, siku hiyo Penza hakuwa na hela hiyo, akarudi kupeleka taarifa ofisi ya Waziri Mkuu ili apewe, tayari kwa kulipia kiwanja hicho na kuanza ujenzi.

Anasema hadi leo hajui kama kiwanja hicho kimelipiwa ama la, kila akienda Wizarani anaambiwa aonane na Penza na akionana na Penza anampiga dana dana ingawa anasema ana tetesi kuwa Penza huenda ameitia mfukoni pesa hiyo.

Mama huyo mwenyeji wa mkoa wa Singida, anasema wakati huo Waziri Mkuu, aliwaagiza watendaji wake wampeleke Nunge apatiwe hifadhi na watoto wake wakati juhudi za kumjengea nyumba huko Kongowe zikiendelea.

Hivyo, mwaka 1994 ndipo alipoletwa Nunge na kupata hifadhi kwa amri ya serikali na hadi hivi sasa anaendelea kuishi hapo.

Mama huyo kwa vile aliona watoto wake ambao walikuwa wadogo enzi anatoka Zaire na sasa kuanza kukua kiumri aliona hawezi kuendelea kuishi nao kwenye nyumba hiyo yenye vyumba viwili tu.

Hivyo, akaona aingie mtaani na kuomba msaada kwa wasamaria wema.

Anasema siku moja katika pitapita zake mitaani, alifanikiwa kuingia kwenye nyumba moja ya mama wa Kizungu ambaye alimueleza matatizo yake na huyo Mzungu alimpatia kiasi cha fedha na katika fedha hiyo ambayo hata hivyo hakumbuki ni kiasi gani kwa vile alikuwa akipewa kwa awamu tofauti, amefanikiwa kununua kiwanja eneo hilo la Nunge na kuanza ujenzi wa nyumba.

Hata hivyo mama Kazadi, anasema kuwa kwa vile Mzungu huyo ambaye alimaliza mkataba wake na kurudi kwao Uholanzi, hakufanikiwa kumaliza ujenzi wa nyumba yake hivyo, hadi leo ipo haijamalizika.

Mama huyo anasema akipata msaada wowote kutoka kwa wafadhili na watu wenye mapenzi mema wa kumalizia ujenzi wa nyumba yake ambayo iko katika hatua za kuwekewa kenchi tayari kwa kuezeka, atafurahi sana kwani huo utakuwa ni msaada mkubwa kwake na watoto wake.

Nyumba hiyo yenye vyumba vitatu na sebule anasema akipata bati 25, milango mitano madirisha na mifuko kumi ya sementi ana uhakika itakamilika ujenzi wake.

Anataja msaada mwingine ambao anahitaji kuwa ni wa elimu kwa watoto wake wanne wanaosoma shule ya msingi Vijibweni ambapo wawili wa kiume wanasoma darasa la sita na wa kike mmoja la tatu na mwingine la kwanza.

Mama Asia, ambaye mtoto wake wa kwanza tayari ameolewa anasema kuwa watoto wake wakubwa wa kiume ambao wanaume kati ya miaka 15-19 wana vipaji vya kuimba kama baba yao hivyo anaomba msaada ili kuendeleza vipaji vyao.

"Tena huyo Kazadi ni mcheza shoo mzuri sana mwanangu anacheza kwenye kumbi mbalimbali na kuniletea pesa ya chakula kwa ajili yangu mimi na wadogo zake huyo tayari ameishamaliza la saba," anasema.

Hata hivyo, mama huyo anasema kuwa siku za nyuma alikuwa anaenda kwa Dk. Remmy na Ubalozi wa Zaire nchini kwenda kupewa matumizi madogo ya watoto wake lakini, Hivi sasa anasema anashindwa kufanya hivyo kwa vile kifedha hayupo vizuri hivyo anakosa hata nauli ya kwenda huko.

"Mimi Asia Ally, sikujua kabisa kama maisha yangu yangeweza kubadilika namna hii, Asia ambaye niliwiki kwenye miaka ya sabini na thamanini, hivi leo naishi hapa Nunge kwenye nyumba za watu wenye ukoma? Ama kweli hujafa hujaumbika," anafunga mahojiano Bi. Asia.