Maisha na Mikasa

Mume anyimwa mimba baada ya kuitunza miezi tisa

lKatika jitihada za kuidai, Mama mkwe amwambia; "Mtu mzima hovyo"

lWameishi naye miaka minane na kuzaa watoto kadhaa

Ebu wazia kwamba wewe ni mwanaume na mmeoana na yule uliyempenda na kumuona wa pekee sana katika dunia hii yenye utitiri wa wanawake. Wazia kwamba mmeishi vizuri na Mola amewajalia watoto kadhaa katika kipindi cha miaka minane mliyoishi wote. Kisha fikiria hali utakayokuwa nayo baada ya muda wote huo wa kuaminiana, mkeo anapokuambia kwamba mimba ambayo inasubiri siku chache tu iitwe mtoto, kwa vile inamalizia siku za mwisho katika mwezi wake wa tisa si yako! Ebu sasa fikiria zaidi kwamba unapohamaki na kujaribu kudhani mkeo anakutania, yeye anafanya kweli na kukupa talaka! Kitendawili hiki si cha kubuni, ni tukio la kweli lililompata Bw. Nassoro Tito Kashinje (46) wa eneo la Sabasaba, Temeke, katika Jiji la vituko la Dar es Salaam. Akimhaditihia Mwandishi Wetu PETER DOMINIC, katika mahojiano maalum, Bw. Kashinje anasimulia kwa kinywa chake kisa hicho cha kusikitisha...

"KAMA ningekuwa na uwezo nikaanzisha shule ya kuwafundisha wanawake na wasichana, na nikafanya mchujo baada ya mafunzo, bila shaka ningewapata wale ambao hawastahili kuolewa maana yaliyonikuta nisingependa yamkute mwingine."

"Silali usingizi, naamka usiku wa manane nikimuwaza mke wangu ninayempenda lakini amenigeuka. ingawa niko naye muda mrefu. Ameniambia mimba aliyonayo ya miezi tisa siyo yangu. Sasa amenipa talaka ya kimila lakini chanzo cha yote ni mama mkwe."

Juu ya mahusiano yake na mkewe Juliet James, Bw. Nasoro, ambaye hivi sasa ameachwa na mtoto wake wa kwanza Meshaki Tito anasema:

"Ndoa yetu ilikuwa ya kuelewana, hatujaibariki kanisani wala msikitini, lakini tuna baraka za wazee maana hata nyumbani wanamtambua, ingawa sijalipa mahari. Sikumbuki nilioa lini ,lakini ilikuwa msimu wa pamba (Desemba) na nilimuoa kijijini kwetu Mahaha, Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza.

Nimeishi naye sasa ni miaka minane. Tulipata mtoto wa kwanza tarehe 28 Oktoba 1989 na kumwita Meshaki, mtoto wa pili aitwaye Enock, mwaka 1994 ambaye kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu ni marehemu. Enock aliugua, akafariki dunia akiwa na miezi mitatu.

Mtoto wa tatu ni Baraka ambaye naye aliugua Kansa ya tumboni tukahangaika sana mahospitalini hadi Muhimbili, akafanyiwa upasuaji na kulazwa mwezi mmoja lakini naye Mungu akamchukua.

"Namshukuru sana Dk. Sai, maana alijitahidi kuyaokoa maisha ya mwanangu Baraka lakini haikuwa riziki. Alimfanyia mwanangu upasuaji akatoa figo moja, kisha tukaanza upya matibabu pale Taasisi ya Kansa-Ocean Road, lakini mwaka 98 mwezi wa 10, saa 6, usiku aliaga dunia." (anapangusa machozi na kuwasha sigara baada ya kusimulia sehemu ya kwanza ya mkasa wa misiba.)

Hata hivyo Bw. Nassoro, anasema baada ya hapo alimruhusu mkewe apeleke msiba huo nyumbani kwao usukumani. Aliporejea Dar (mkewe) alikuja na wazo jipya kwamba ikitokea akapata mimba, basi itambidi akajifungulie nyumbani kwao kama alivyoagizwa na mama yake mzazi.

Oktoba, mwaka jana akamweleza mumewe kuwa sasa anayo mimba . "Nilifurahi nikatafuta pesa aende nyumbani kama alivyosema hapo awali. Sikutegemea angenigeuzia kibao eti nafanya njama za kumwacha. Akagoma kwenda huko akinishauri nimwachie ili kwanza mtoto wetu Meshaki apate komunio, nikakubaliana naye. Komunio hiyo ndiyo ikawa chanzo cha matatizo. Nilikusanya kiasi fulani cha pesa ambacho hata hivyo hakingetosha kwa sherehe kama tulivyoikadiria. Lakini mke wangu akaniambia nisihangaike kwani amepata michango mingi kwa ajili ya sherehe hiyo. Nilishangaa kidogo, kwa vile sikujua pesa hizo zimechangwa na nani na kwa nini sikushirikishwa katika mpango huo.Sikusema kitu, nilikaa kimya.

Baada ya sherehe nilimkumbusha kwamba aende nyumbani akarudia tena kauli yake eti nina mpango wa kumtelekeza. Akanijibu:

" Mwenye mimba ni mimi, popote nitajifungua." Nikamwacha.

Mei, 25, mwaka huu, ni siku ambayo sitoisahau. Nilirudi kibaruani mchana, akanipokea mwanangu Meshaki, akaniambia mama yupo kwa bibi yake. Kwa vile kulikuwa na mgonjwa nilienda kumwona na baada ya kumjulia hali mgonjwa, nilimuulizia mke wangu, nikaambiwa yupo. Nikaingia ndani nikamkuta mama mkwe (Mama Nghwan) ameketi barazani. Nilimtaka hali, kisha nikaomba kumwona mke wangu, akanijibu kuwa yupo ndani anaongea na mfanyakazi, lakini alisonyesha wasiwasi. Nikaingia chumbani.

Nilimkuta mke wangu akiwa na mwanaume ambaye simfahamu, tena wamekaa naye kiti kimoja. (Baba Meshaka anapiga funda la sigara kisha anaendelea kusimulia.)

Nilishangaa kidogo maana walikaa karibu mno kwa kuwekeana mikono kama mtu na mumewe. Mezani ilikuwapo chupa ya bia na glasi iliyojaa bia, nilivuta kiti na kuketi pembezoni mwa mlango. Nikajikaza kiume nikawasalimu wote, wakaniitikia.

Ingawa nilikuwa na hasira lakini sikutaka kumdhuru mke wangu, ilichukua muda wa dakika tatu hivi kukiwa kimya, mama Meshaki, akatoka nje. Nilimfuata nikamkuta ameketi na mama yake, nikauliza nifahamishwe aliyekuwa naye ndani ni nani, mama mkwe akadakia:

"Unafikiri ni hawara yake... mtu mzima ovyo!" Sikuonyesha hasira, nikamwomba mke wangu tuondoke, akakubali lakini yeye akatangulia huku tukimwacha yule mwanaume ndani na mimi nikifuatana na mjomba wake ili tukayasuluhishe kimya kimya pale kwangu.

Tulipofika kumbe tukamkuta tayari yeye amekwishachukua kikapu na sanduku, kwa nia ya kuondoka. Sikuwa na jinsi, nikaenda kumwita mjumbe. Mjumbe alipokuja wapangaji wenzangu wakamweleza kuwa alipochukua mizigo aliaga kuwa amekwenda kwa mama yake.

Bw. Nassoro, anasema ingawa Mjumbe alimuita mara nyingine ili wayamalize haikuwezekana maana alirudi na kuchukua vyombo vya ndani vyote bila kuacha kitu "Nilimwomba aniachie angalau bakuli mbili na sufuria kwa ajili ya mtoto akakubali akaniachia baadhi ya sahani na shuka mbili, akaondoka na saba.

Kesi yetu ilifika Serikali za Mitaa kwa usuluhishi. Huko alijitetea kuwa yule njemba (mwanaume) alikuwa ni hawara wa mama yake, yaani mama mkwe wangu Mama Nghwan. Lakini alikuja na talaka ili anipe mimi, kitu ambacho sikutegemea. Nilimwita tena, tuyamalize akakataa. Wengine walinishauri nikatafute haki yangu mahakamani, hata hivyo baada kuhangaika huku na huku mama wakwe zangu yaani Bibi Nghwan na dada yake, Mama Mwinyi, waliniomba nipokee talaka ya kimila na nilikubali tu ili nitue huo mzigo.".

Wakaitwa ndugu Mei, 31, mwaka huu, tukaandikiana talaka ambapo Mama Meshaki alidai mimba aliyo nayo siyo ya kwangu ni ya mwanamume mwingine. Nilikubali talaka hiyo maana mke wangu keshanikataa na huko aliko akipata matatizo nitaulizwa mimi. Nimemsamehe kila kitu lakini lazima aliyempa mimba hiyo anilipe fidia, nimeilea miezi 9 sasa na anakaribia kujifungua mwezi huu wa 6.

Nimeshangazwa na alivyogeuka mke wangu wakati alikuwa muumini Mkristo mzuri. Nikiwa Muislamu, alinishauri hapo awali nikasoma mafundisho ya kiroho ya Kikatoliki ili baadae tufunge ndoa, lakini alinigeuka tena eti hawezi kufunga ndoa na mimi kwa vile sijalipa mahari kwao.

"Ingawa nilikuwa nahudhuria ibada kanisani lakini sijawahi kubatizwa. Mke wangu amenikatili, sijui la kufanya."

Pamoja na kusimulia kubadilika kwa mkewe, Bw. Nassoro, anasema mbaya wake ni aliyejifanya mkwe wake (Mama Ng'hwan) ambaye alikuja kuomba hifadhi kwangu kwa vile ni kabila langu. Nikakaa naye baada ya kuambiwa na mke wangu kuwa ni mama yake mdogo. Nilimsaidia kumbe nasaidia adui mkubwa. Sitegemei kuwa na mahusiano naye... sitegemei kuwa na mahusiano naye, amemdanganya mke wangu... anampeleka kwa mahawara" alisema kwa uchungu. Mbaya zaidi nimekuja kugundua kuwa kumbe Mama Ng'hwan, hata hakuwa mama yake mdogo ila rafiki yake tu- yaani mkwe wangu bandia.

Gazeti lilipofuatilia ukweli wa tuhuma hizo kwa upande wa pili, mambo yalikuwa hivi:

Katika hali iliyodhihirisha kuhusishwa na uvurugaji wa ndoa hiyo,Gazeti lilipogonga hodi kwa "mama mkwe" anayemuhifadhi Mama Meshaki, ili kupata ukweli, Mwandishi alikaribishwa na Mama Nghwan, mama mkwe bandia wa Nassoro.

Ingawa makaribisho yalikuwa mzuri lakini uungwana huo haukudumu, kwani Mama Nghwan, alibadilika ghafla baada ya mwandishi kujitambulisha na kuomba kuonana na mama Meshaki.

"Hatutaki mambo ya magazeti kama umemfuata Mama Meshaki, hapa hayupo, kwanza simjui...ukitaka nenda polisi wakupe barua. Sisi si wasemaji wake. Kwanza yeye kaondoka, yuko Mbagala kwa ndugu zake. Kwanza najua umetumwa na Baba Meshaki, amezidi kunionea, nitamfuata huko huko kwake. Mwishowe atanitumia watu wa kuniua," alifululiza maneno kama chereheni mama mkwe huyo huku akimwamuru mwandishi wa habari hizi atoke nje, vinginevyo angeweza kupigiwa kelele za mwizi ili apate kibano.

Licha ya mwandishi kujitahidi kumbembeleza apunguze jazba, ili kuwepo na uhakika wa kumpata Mama Meshaki au Bi Juliet ambaye ndiye muhusika wa suala hilo haikuwa rahisi, kwani mama wakwe hao ambao tayari walikwishajikusanya wawili nje ya chumba chao walikuja juu kama mto wa kifuu na kurusha maneno makali kana kwamba mwandishi ndiye Baba Meshaki, "Tunakutuma nenda kamwambie asitufuatefuate tumemchoka na mambo yake ya kujinga. Hapa mkewe hayupo na sisi hatumjui," alisema mmoja wao.

Kazi haikuwa rahisi kwa mwandishi maana alianza kuulizwa maswali yaliyopambwa kwa matusi na kejeli ndani yake "Hivi wewe ni mwandishi gani hadi unafuata watu hadi majumbani mwao?! Usione hivi, mimi nafanya kazi katika gazeti, sheria nazijua usitubabaishe!" alisema mama mwingine ambaye ilielezwa kuwa ni ndugu wa Mama Nghwan.

Ingawa msimamo wa Mwandishi kumpata mama Meshaki ulikuwa pale pale haikuwa rahisi kumpata maana mama Mwinyi alikuja juu kuliko hapo awali, " Hivi wewe uliona wapi mwandishi anatafuta habari kwenye nyumba za watu, kwanza tupe kitambulisho chako. Wewe na aliyekutuma mna matatizo maana huyo Baba Meshaki namzidi elimu mara tano, yeye ni darasa la pili, ni mjinga, mimi ni mfanyakazi wa magazeti; hapa hupati kitu," alitamba mama huyo bila kufafanua anafanya kazi gazeti gani, ingawa hali halisi ilionyesha ni vitisho vyake tu.

Katibu wa Serikali ya Mtaa wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake litajwe alithibitisha kuwepo kwa kesi ya wanandoa hao ambayo ilifikishwa ofisini hapo na kuamuliwa na Baraza la Usuluhishi, bila mafanikio.