Changamoto ya madhehebu mengi kwa kanisa Katoliki na Imani yetu (5)

msukumo wa kuifahamu vizuri imani yetu kama inavyofundishwa na kanisa na kuiishi kwa bidii zaidi.

Imani ndiyo mzizi wa upendo kwa Mungu wa jirani Msingi na mahali pa kuanzia kujua Wakatoliki wanaamini nini ni KANUNI YA IMANI tunayoisali kila Jumapili (NASADIKI). Yeyote anayejenga maelezo ya imani ya Wakatoliki bila kujua kanuni hiyo na undani wake ni mbabaishaji watapotoa ukweli.

Ubabaikaji wa baadhi ya Wakatoliki wetu unatokana na kutoifahamu vema imani yenu na hivyo hamjiamini mnapokumbana na 'Werevu' wa maswali ya wapotoaji. Ubabaikaji pia unatokana na kutoisoma na kuizoea Biblia Takatifu. Haya mawili yanawafanya mshindwe kujieleza kwa ufasaha na hivyo kuaminishwa kwa urahisi kuwa mmedanganywa. na pale mnapoanguka kwa sababu ya uelevu mdogo na aibu huwa vigumu kurudi kama Mtume Paulo asemavyo: "kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru na kukionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo wakaanguka baada ya hayo haiwezekani kuwafanya upya tena wakatubu; kwa kuwa dhahiri" (Ebr 6:4-6).

Kwa sababu hiyo nawasihi waamini wakristu kujitahidi daima kuisoma Biblia na kujiongezea ufahamu mkiongozwa na tafsiri yake inayotolewa na MAMLAKAFUNZI ya kanisa. ni muhimu kwa wachungaji kutoa kipaumbele katika swala la elimu ya Biblia kwa wakristo wetu, maana upungufu wa elimu hiyo hawakusema watafute kusikiliza sauti nyingine zinazopotosha juu ya imani yao. Lazima wafundishwe Biblia na Katekisimu ya Kanisa na kuhimiza maisha mazuri ya Kikristo.

VII Kuepuka 'mitego mingine inayoiba kondoo'

24: Pamoja na kuwaonya wakristo msipeperushwe huko na huko mkichukuliwa na kila aina ya mafundisho (Ebr 13:9), yafaa tuwakumbushe pia kuepo mambo mengine yanayowaiba kondoo. Licha ya kuitwaa ngao ya imani sahihi ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu' (mwizi wa kondoo) kama ahimizavyo mtume Paulo (Ef 6:10-20). lazima kusali daima ili Mungu awaepushe na maisha yanayoshindana na Roho (Gal 5:22-25).

Maisha hayo ya mwili yanaonyeshwa na mitego hii kwanza ni Uvivu ambao huleta. kishawishi cha 'kuharakisha' kila mara juhudi ya kuyarekebisha ama kujishughulisha na mahusiano yetu na Mungu. Kuahirisha huku kuyafanya mahusiano hayo yaote miiba na kuta na misingi yake kubomoka (Mith 24:30-34). Pili ni ulevi uletwao na ukosefu wa kiasi. Ulevi hukaribisha kila aina ya dhambi, maradhi, ama udhaifu wa kimwili na kiroho (Mith 23:29-35). Tatu ni tamaa ya utajiri ambayo humfanya mtu kutumia hata njia haramu kuipata njia zinazokwenda kinyume na upendo kwa Mungu na jirani (Mith 1:19). Mtume Paulo anafundisha kuwa mwenye tamaa ni mwabudu sanamu (Efe 5:5).

Kwa tajiri ni vigumu kuurithi ufalme wa mbinguni (Mk 10:24-27) kwa maana huelekea kuitegemea mali kuliko Mungu! Nne lazima kuwepo Sherehe zinazoleta kifo cha maisha yetu kiroho. Ndiyo maana mhubiri anasema ' Heri kuiendea nyumba ya matanga kuliko kuiendea nyumba ya karamu. kwa maana huo ndio mwisho wa wanadamu wote naye aliye hai atautia moyoni mwake' (Mhu 7:2). Mara nyingi starehe zisizo na kiasi huwameza wengi wakaacha mahusiano na Mungu na kanisa. Tano kwetu sisi waafrika mtego miwili inayotukabili ni Ushirikina na mitala.

25: Maisha yetu yanatawaliwa na mashaka makubwa iwapo kweli Mungu wa Yesu Kristo ana nguvu na uwezo kuliko chochote kile au zipo nguvu nyingine zinazolingana na za Mungu au zinazochenga uwezo wake. Hali hiyo hutubakiza katika imani isiyo kamili na kutufanya tumwabudu Mungu wa Kristo kwa midomo tu huku mioyo ikiwa kwingine (Mt.15:8-9). Tunajaribu kuvaa ngozi ya wenye dini sana, lakini Yesu hajiaminishi kwetu kwa sababu anajua yaliyomo ndani mwetu (Yn 2:23-25). Tusijaribu kumdanganya Yesu kumwonyesha tunamwamini kumbe ni pale tu tunapoona katenda ishara au muujiza unaoonyesha nguvu zake, na pale tusipoona hilo tunakimbilia kwingineko gizani.

26: Ni pia alama ya utovu au upungufu mkubwa wa imani pale mkristo asipokubali mpango wa Mungu kuhusu ndoa. Mkristo anapopendelea zaidi kujificha katika picha za ndoa za Agano la Kale zinazoonyesha Wayahudi kuwa na wake wengi, inadhihirisha kuwa hakubali ufunuo mpya ulioletwa na Kristo katika Agano jipya (Mt. 19:4-6;Mk10:6-9;1kor7:10-11). Ndoa za mitaala kimsingi huwa alama ya nje ya kutawaliwa na tamaa ya mwili na pia ya kuupinga mpango wa Mungu,. Wengi katika ndoa hizi hujihujumu na kujitenga na Mwili wa fumbo la Kristo, kuyaacha maisha ya uhusiano wa karibu na Mungu na Kanisa. Nawahimiza wale walio katika miungano ya aina hii kutokata tamaa, bali waendelee kumwomba Mungu awape neema ya kuushinda mtengo na kunyoosha maisha yao ya Kikristo (Lk14:26), na siyo kukimbia kujificha. Natambua ulivyo uamuzi mgumu kubanduka na hali hiyo, lakini kwa Mungu kila kitu kinawezekana.

VIII Mwisho

27: Karne tuliyoimalizia ilishuhudia mwanzo mpya wa juhudi za kiekumene ili kuboresha mahusiano baina ya Kanisa Katoliki na ndugu zetu wa makanisa na jumuiya nyingine za kikristo. Lengo ni kutafuta kuponya utengano wetu na kurudisha umoja wa Mwili wa fumbo la Kristo, ili tuwe kundi moja lenye mchungaji mmoja (Yn 10:16). Lakini wakati huo huo pia kumezuka vikundi vingi pia vinavyojivika makoti na majina ya makanisa, lakini yanayozidisha utengano huo kwa sera na mahubiri ya chuki kwa Kanisa Katoliki na kupotoa waamini wake. Sisi tunaamini 'asiye kinyume chetu tu upande wetu' hatuwezi kukusanya pamoja kwa sera za chuki.

28: Baada ya kuwapa onyo hili la kichungaji tulilolitoa mara ya kwanza huko Nyakijoga, Mugana Bukoba, wakati wa mkesha wa hija ya kijimbo tarehe 4 machi, ni furaha yetu pia kuwapa matumanini wale wote waliokumbwa na upotovu wa 'waalimu wa uongo', wanaopenda kurudi. Kama Mungu alivyomtuma nabii Yeremia kuwatangazia Israeli, nami nawaiteni kwa maneno yake nabii wa Kristu waliokwenda bila kujua:"Rudi ee Israeli mwenye kuasi, asema Bwana sitakutazama kwa hasira, maana mimi ni mwenye rehema asema Bwana, sitashika hasira hata milele. Ungama uovu wako tu ya kwamba umemwasi Bwana, Mungu wako na njia zako zimekuwa nyingi kuwaendea wageni chini ya kila mti wenye majani mabichi wala hamkuitii sauti yangu, asema Bwana Rudini enyi watoto wenye kuasi asema Bwana" (Yer 3:12-14). Mtu asiogope wala kuona aibu kuomba kurudi katika ushirika kamili wa kanisa Katoliki. Kanisa ni mfano wa mama ampendaye mwana wake hata muasi anayefurahi kumwona mwana akijirudi na kuacha njia mbaya.

29: Tunao wajibu kama wafuasi wa Kristo kuighairi tabia ya kushindana na kupakana matope kwa lugha mbaya. Mashindano hayo hayamfanyi yeyote kuaminika zaidi bali kuwafanya watu kuwa na mashaka na ujumbe tunaoutangaza. Tuepuke kuifanya njia ya kweli ya Kristo kudharauliwa na kupuuzwa na kuonekana isiyo njia ya kweli ya Wokovu. Kwa hakika Kristo ndiye anayeongoza kuelekea uzima wa milele.

30 Tumwombe Mama Bikira Maria ambaye sote kwa njia ya mtume Yohana Kristo ametupa kama mama yetu, atusaidie kutuombea ili wafuasi wa mwanawe tusifanye kazi ya kutawanya kundi . Badala yake sote tuzidishe nguvu za kukusanya kondoo wake pamoja,ili Kristo alilishe kundi lake likiwa moja na kuliongoza hadi alifikishe kwa Baba; na maneno yake yatimie ' nilipokuwapo pamoja nao mimi nliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza wala hapana mmojawapo wao aliyepotea ila yule mwana wa upotevu ili andiko litimie" (Yn 17:12)

Mungu awabariki.

Yasiyo ya Kawaida

Nchi yenye barabara moja tu

lInaongoza kwa ajali za barabarani, na ina urefu wa Km.19

lHapo awali pia ilikuwa na ndege moja tu

Na Masha Otieno Nguru JR

KWA waliobahatika kuona picha za mwanasayansi bingwa wa Marekani Neil Armstrong alipotua mwezini na chombo cha ‘Apollo’ mwaka 1969 ndivyo mazingira ya picha halisi ya kisiwa cha Nauru yanavyoonekana.

Ukifika Nauru sehemu kubwa ya ardhi yake imechimbuliwa mpaka ardhi iliyo juu ya uso wake ikabadilika mithili ya iliyoko mwezini. Hii ni kwa habari za kutafiti Peter Richardson wa Marekani aliyekitembelea kisiwa hiki.

Kisa na mkasa cha ardhi ya Nauru kuchimbuliwa hivyo ni harakati za makampuni makubwa ya Australia kutfuta ‘guano’ mbolea ya phosphate ambayo yaaminika kutolewa na ndege wa porini.

Hali hii ilipelekea mwaka 1989 eneo la kilomita za mraba zipatazo 21, kuifikisha Nauru mbele ya mahakama ya kimataifa ikidai Australia ilipe fidia kuwa kuharibu mazingira kwenye kisiwa hicho kwa takribani miaka 50 ikichimba phosphate.

Kinachoshangaza ulimwengu ni kuwa pamoja na kuwa na utajiri wa madini na Samaki, Nauru mpaka tumeingia karne mpya sayansi na teknolojia bado ina barabara moja tu, ndege mbili, huku ikiwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa ajali za barabarani.

Sababu nyingine ambayo yaelezwa kuwa inachangia ajali kutokea kwa wingi huko Nauru ni pamoja na Ulevi wa kupindukia unaochangiwa na ukosefu wa ajira na kazi na madini yamepelekea hata watu waliovurugikiwa na akili kununua magari.

Hali hii imepelekea barabara moja tu iliyoko katika kisiwa cha Nauru iwe kama ni balaa kwake badala ya baraka.

Tatizo lingine ni kuwa Nauru inayo idadi kubwa ya magari mengine yakiwa malori makubwa yenye nguvu kupita barabara moja iliyo nayo hali inayochangia pia nchi hii kuzidi kuwa na ajali nyingi za barabarani.

Kutoka mwaka 1919 mpaka 1968 Nauru iliyojipatia uhuru wake, Kampuni ya kuchimba phosphate ya Australia iliyoko chini ya Uingereza ilichimba kiasi cha tani millioni 34 za Phosphate kutoka Nauru na zikauzwa kwa bei rahisi tu huko Australia na New Zealanda.

Bila ya Phosphate kutoka Nauru uzalishaji wa ngano katika ardhi ya magharibi mwa Australia yenye upungufu mkubwa wa madini ya phosphous isingeliwezekana na uchumi wa maeneo kadhaa ya Australia pia ungeliporomoka.

Nauru iliendelea kulipwa senti chache tu kwa kila tani ya phosphate yake mpaka mwaka 1927 ndipo bei iliongezeka kidogo. Katika miaka ya karibuni Australia na New Zealand zimeendelea kununua Phosphate kutoka Nauru lakini kwa viwango vya bei ya kimataifa.

Nauru ilianza kidogo kufurahia uchumi wake mwaka 1970 bei ya Phosphate ilipopanda na kufikia dola za kimarekani $60 kwa tani moja hii ilikuwa pia baada ya muungano wa nchi zinazozalisha mafuta duniani OPEC kupandisha bei ya mafuta ya petroli ambayo pia hutegemeana sana na phosphate.

Kwa fedha ilizopata imewekeza kuwa kujenga hoteli za kitalii huko Honolulu, Guam na New Zealand. Pia imejenga mradi wa majengo ya ofisi za kukodi huko London, Melbourne na Manila.

Lakini pamoja na yote hayo Nauru bado ni nchi inayofahamika duniani kwa kuwa na barabara moja tu na iliyoshindwa kulinda afya za wakazi wake.

Nauru ni moja ya visiwa kusini mwa Pacific. Imepakana na visiwa vya Fiji, Papua New Guinea, Vanuatu na Solomon Islands.

Uchaguzi wa Kisiasa kwa nini tujali?

Oktoba, mwaka huu kutakuwa na Uchaguzi Mkuu wa pili wa Rais na Wabunge katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini kwa kushirikiana na Chama cha Wanataaluma Wakatoliki wameona wanao wajibu kama vyombo vya kanisa kuwasaidia wananchi wazijue haki zao katika Uchaguzi huo na kutoka kitabu hiki ambacho tumeamua kukichapisha ili kuunga mkono hatua hiyo. Endelea na toleo hili.

Nia sio kila mhamasishaji ashughulikie mada zote kwa kila kundi.

Mhamasishaji atachagua mada muhimu kwa kundi lililo mbele yake, kisha tafakari na majadiliano vitaendelea kwa lengo la kufikia maamuzi ya ufumbuzi na programu ya utekelezaji. Lazima vipindi vya uhamasishaji visiishie katika mazungumzo tu bali vilenge katika utendaji.

Ili kuweza kufikia azma hiyo lazima kwanza watu wahamasike na wajifunze namna ya kuchambua kwa kina mambo yanayowahusu mara nyingi katika mijadala ya Kisiasa ni rahisi watu hata wakiwemo wasomi waliobeba jazba na hamaki, Kwa ujumla Siasa inaweza kuchochea jazba na hisa tele. Na hii siyo mbaya lakini haipaswi kubakia hapo hapo.

Mhamasishaji mzuri anapaswa kujua hilo ili atafute namna ya kuelekeza mhamasishaji anapaswa kufanya kazi hii kwa kushirikiana kikamilifu na wana kikundi kufikia uamuzi wa pamoja;. Huu ndio Uhamasishaji Shirikishi" na ndio lengo kuu la uandaaji wa kijitabu hiki. Mwongozo wa wahamasishaji katika kujenga ushiriki wa watu".

Katika mada zilizochaguliwa zimewasilishwa kwa kuanza na hadithi toka maisha halisi ikifuatiwa na tafakari na uchambuzi kisha kumalizia na aina ya maswali ya kuwauliza wagombea na watendaji wa Siasa au vyama vya Siasa.

Kijitabu hiki ni kwa matumizi ya wahamasishaji ambao ndio watakaoongoza uhamasishaji kwa ngazi ya Parokia au vikundi fulani pamoja na kitabu hiki, Tume ya Haki na Amani itaandaa vipeperushi kadhaa kila mmoja na vinaweza kutumiwa na vikundi kama vilivyo au kufanyiwa uhakiki upya kulingana na hali na mahitaji halisi ya wahusika. Pengine Tume ya Haki na Amani ngazi ya Jimbo inaweza hata kuandaa vipeperushi vyake kwa kuzingatia hali halisi na matakwa ya wananchi wa eneo hilo.

Wakati huo huo tunaandaa kanda za redio na video juu ya mazungumzo mbalimbali ya mada hizo, kazi ambayo itafanywa kwa kushirikiana na Redio Tuamini. Kila Jimbo litatumiwa nakala za kanda hizo.

Tunategemea pia kuandaa Bango kuelezea shughuli za uhamasishaji. Vitu vyote hivi vitasambazwa kupitia Kamati/Tume za Haki na Amani, Halmashauri Walei na CPT ngazi ya Jimbo.

Wahusika hawa wanaombwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kazi hii ya uhamasishaji.

SEHEMU YA II - MADA

1 Utamaduni wa Kidemokrasia

Ndugu Kazimoto alipanda basi kituoni Mbuyuni akiwa anaelekea kijijini kwake Songambele. Alishangaaa kumwona Ndugu Bahati ambaye anatokea Twendesote kuelekea Mjini Mtakatifu. Baada ya Salamu ya kawaida na kukumbushana kufahamiana kwao kwa zamani walianza kuzungumzia kuhusu hali ya Twendesote.' Nasikia karibu mtapata huduma ya maji katika vijiji kadhaa vya Twendesote". Ndugu Bahati akajibu ni kweli kwa sababu Mbunge wetu alipata fedha toka kwa wafadhili fulani miaka 3 iliyopita lakini Serikali ilikataa kuruhusu eti kwa sababu Mbunge wetu anatoka Chama cha upinzani. Fikiria kama vile maji yatatumiwa na watu wote! kinachoonekana ni kwamba, Serikali ilitaka kutuadhibu kwa sababu wengi miongoni mwetu walimpigia kura mgombea wa Chama cha Upinzani. Hawakutaka kuheshimu maoni ya wapiga kura na hivyo wakatumia uwezo wao wa madaraka kuzuia msaada wa Kijiji chetu" Ndugu Kazimoto akajibu 'ndiyo, hata kwetu tumeshuhudia jambo la aina hiyo.'

Hii ni hadithi ya Michezo ya Kisiasa inayoambatana na kukomoana kulipiziana kisasi. Ni jambo la hulka ya kibinadamu lakini siyo jambo la haki kabisa. Kwa muda mrefu tulikuwa katika utawala wa kikoloni ambao tuliukataa kwa kuwa haukuwa Utawala wa Kidemokrasia. Kisha ukaja Uhuru- wanachi wakataka kujenga Taifa moja la watu wamoja. Wakakubaliana kuwa mfumo wa Chama kimoja ndiyo ungefaa kulinda Umoja na Amani na hivyo kujenga umoja na mshikamano wa watu wa makabila mengi. Kwa miaka yote hiyo tumejifunza kwamba kuweka makabila mengi. kwa miaka yote hiyo tumejifunza kwamba kuweka madaraka yote mikononi mwa Chama kimoja si vizuri kwa vile huchochea matumizi mabaya ya madaraka na kuzuia kuchomoza kwa mawazo mapya na mbinu za utekelezaji. Pamoja na sababu nyingine watu walichoka utawala wa chama kimoja na wakadai njia mpya ya utawala.

Hapo ndipo mfumo wa vyama vingi ukakubaliwa na kuanza kutumika kama njia mpya ya utendaji kisiasa. Tukawa na vyama vingi vilivyoshiriki uchaguzi wa 1995. Baadhi y a watu walipigia kura vyama vipya, lakini wengi wakakipa kura Chama kikongwe na kukiwezesha kupata sehemu kubwa ya viti Bungeni.

Swali linakuja, Je, mfumo huu mpya umesaidia kubadili tabia na mwenendo wa utawala? Je, hatuwezi kuona wazi kuwa hata vyama vya upinzani vimefuata mkondo huo wa kutaka kupewa madaraka kwa faida zao binafsi?

Ili kuwa na Demokrasia ya kweli ya utawala sharti ujali na kutafuta mahitaji ya wote. Kutafuta manufaa kwa wote na kwa kila kimoja ndio lengo kuu la shughuli za Kisiasa. Kwa mwanasiasa kutaka madaraka na mahali pa kutawala ni jambo la kawaida. Lakini siyo iwe kutafuta madaraka kwa manufaa ya binafsi na kwa lengo la kujitajirisha, Mfumo wa Kidemokrasia unapaswa kujenga mazingira ambamo umma unakuwa na madaraka juu yake wale wanaodhaniwa wataweza kutekeleza matakwe ya wananchi.

Ni jukumu la wanasiasa na vyama vya kisiasa kushawishi watu juu ya uzuri wa programu zao na ubora wa wagombea wao. Ni hapo tu ndipo tunaweza kuwa na Demokrasia ya kweli. Aidha dalili za kuwa na mfumo wa kweli wa Kidemokrasia ni kuwa na wanasiasa na vyama;

- Vinavyoendesha shughuli zao kwa uhalali na ukweli

- Vinavyoheshimiana vyenyewe na pia kuheshimu maoni ya watu.

- Vinavyovumilia ile hali tofauti katika kuona mambo

VIDEO: Namna inavyoweza kutumika vema kama yenzo ya uelimishaji

Kwa kuwa kama iliyoelezwa katika chapisho la kitabu cha UCHAGUZI WA KISIASA KWANINI TUJALI, video itakuwa miongoni mwa nyenzo bora zitakazotumika kwa kuelimisha jamii kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa uchaguzi. Ili kutumia nafasi hiyo kwa ukamilifu na ufanisi zaidi katika kufanikisha az ma ya Tume ya Haki na Amani, Dk. A. Hokororo wa Idara ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), anajaribu kuelezea namna nzuri ya kutumia video katika ufundishaji.

MWANZO

Ni Muhimu kufafanua kwa nini kikundi kinatazama kanda hiyo maalum ya video. Huenda ikawa kinatazama kanda hiyo kwa shughuli za burudani au elimu. Iwapo kinatazama kanda ya video ili kujielimisha,anayeongoza maonyesho (Mwalimu au Mchokozi) afanye matayarisho yafuatayo:

-1.KUDADISI KANDA:

Mchokozi au Mwalimu aitazame kanda kabla kikundi

hakijatazama kanda hiyo ili ajue yote yanayoelezwa na kuonyeshwa katika kanda. Inafaa pia kuweka kumbukumbu ya sehemu muhimu ili ziweze kuonyeshwa na urahisi na mara moja kama ikibidi (Memory Counter Index)

Television iwe katika sehemu ambapo kikundi kitaona na kusikia vizuri; na hakikisha kanda itakayotazamwa inaanza mwanzoni.

Ukubwa wa kikundi ulingane na ukubwa wa Televisheni. Mfano televisheni ya ukubwa wa inchi 19 21 inatosha kwa watu 30.

2. KUKITAYARISHA KIKUNDI

a) Mwalimu/ Mchokozi akisaidie kikundi kujikumbusha yale wanayofaamu kuhusu somo ili isaidie kuelewa mambo mapya. marudio hayo yanaweza kufanywa kwa kujibu maswali ya 'ndiyo' au ' hapana'. Kikundi kinaweza pia kuuliza maswali ambayo wangelipenda wajibiwe kuhusu somo.

b) Mwalimu/Mchokozi atoe maelezo mafupi kuhusu kanda ambayo kikundi itatazama.

c) Mwalimu/Mchokozi aeleze kikundi sehemu muhimu ambazo watapaswa kusikiliza kwa makini, Itasaidia pia kama wanakikundi watakuwa na kalamu na karatasi za kuandika habari ambazo wataona ni muhimu.

3. KUONYESHA KANDA

Wakati wa kutazama kanda ya Video,Mwalimu/ Mchokozi akae kwenye sehemu ambapo ataona kikundi kinafuataje maelezo ya Kanda kama: kusisimka, kuchoshwa n.k.

4. BAADA YA KUTAZAMA KANDA

Baada ya kumaliza kutazama kanda, Mwalimu /Mchokozi aulize kikundi maswali yanayohusiana na kanda kwa mfano:-

a) Je Kanda ilikuwa na ukweli?

b) Ilielemea upande mmoja?

c) Waigizaji katika kanda waliaminika?

d) Kanda ilisisimua n.k

Mchokozi awaulize wanakikundi iwapo walihisi kama kanda ilikuwa na ujumbe wowote kwao binafsi.

Inasaidia pia kuwagawa wanakikundi vikundi vidogo vikiwa na viongozi ili wafaye majadiliano katika vikundi hivyo vidogo. Majadiliano hayo yahusu.

a) Mambo ambayo Mwalimu/Mchokozi aliyaeleza kabla ya kutazama kanda.

b) Waeleweshane juu ya mambo magumu au yenye utatanishi waliyoyaona kwenye kanda.

c) Wanaweza pia kujadili mambo maalum ambayo Mwalimu/ Mchokozi ameyatayarisha kabla ya kipindi.

5 TATHIMINI

Baada ya mazungumzo katika vikundi vidogo ni vyema Mwalimu/ Mchokozi atakakikutanisha kikundi chote kwa pamoja na kujadili maswali yafuatayo, Maswali yanaweza kujibiwakwa maandishi iwapo hali inaruhusu.

a) Kwa kifupi kila mwanakikundi aleze ujumbe alioupata kutokana na kanda aliyoitazama na majadiliano katika vikundi.

b) Aeleze mambo mapya ambayo amejifunza

c) Aeleze ni mchezaji gani kwenye kanda aliyemfundisha mambo mengi, na kwa nini

d) Aeleze atatumiaje mambo mapya aliyojifunza:

- katika maisha yake binafsi?

- Katika maisha ya wengine?

Tunaamini kuwa kwa kufuata baadhi ya maoni hayo tutaweza kutumia video kwa ukamilifu zaidi hasa kuongeza elimu yetu badala ya kutazama picha kama burudani pekee.

Maisha na Mikasa

Mama mzazi anapochukua nafasi ya 'Girl Friend' !!

 

lSiwezi kusema chakula kilikuwa kibaya lakini sikujua nilikuwa ninakula nini

lNimefika miji ambayo sasa nilijiona niko katika dunia tofauti na ile ninayoifahamu

MTU yeyote akiulizwa leo,"Je rafiki yako ni nani" Ni vigumu kuwazia kwamba mmoja angemtaja mama yake mzazi. Kwa wengi Mama ni mama na rafiki ni mtu mwingine. Lakini mtazamo huo hauna thamani kwa Michael Simbeye(17) aliyerejea hivi karibuni kutoka mjini Paris, Ufaransa. Kisa kifuatacho pamoja na mambo mengine kinaelezea jinsi Simbeye alivyompa mama yake mzazi hadhi ya kuwa rafiki yake mkuu. Endelea...

Hivi karibuni, Watanzania 12 walirejea nchini kutoka Paris, Ufaransa, ambako walikaa kwa muda wa wiki moja na kurudi na kumbukumbu za kila aina kuhusu jiji maarufu la Paris.

Kundi hili lilikuwa ni la washindi wa shindano la "Furahia Fanta" lililoandaliwa na watengenezaji wa kinywaji maarufu cha Fanta mwaka jana, na washindi wa bahati nasibu wakajulikana mwezi Desemba mwaka huo huo wa 1999.

Mchezo ulichezwa katika vituo mbali mbali nchini Tanzania vikiwemo kituo cha Dar- es-Salaam kilichohusisha mkoa wa Dar es Sala am na Visiwa vya Zanzibar na Pemba, pamoja na vituo vya kanda vya Mbeya, Moshi, na Mwanza.

Kila kituo kilipaswa kutoa mshindi mmoja kutokana na mchezo wa bahati nasibu ya shindano la Fanta, na kila mshindi alipewa fursa ya kuchagua marafiki wawili wa kufurahia nao maisha jijini Paris ambao nao walichukuliwa kama washindi.

Ni utaratibu huu ambao uliwezesha kupatikana washindi 12 kutoka sehemu mbali mbali nchini, ambao ziara yao ya kwenda Paris, Ufaransa, ilidhaminiwa kikamilifu na watengenezaji wa Fanta.

Wakati ushindi wa moja kwa moja wa mchezo wa bahati nasibu ulitegemea bahati tu, ule uliotokana na kila mshindi kuchagua marafiki wa kumsindikiza ulitegemea mahusiano maalum kati ya mshindi na rafiki zake.

Inaelekea washindi wa bahati nasibu walitumia vigezo mbalimbali katika kuchagua marafiki wa kwenda nao ili kufurahia Fanta jijini Paris.

Michael Simbeye, kijana wa umri wa miaka 17 ambaye alishinda katika kituo cha Mbeya, alimchagua mama yake Merina Mwembe, mwenye umri wa miaka 58 ambaye ni mkulima, na kaka yake John Simon Simbeye ambaye ni mfanyabiashara, ili waende naye Paris kama marafiki zake.

"Sikuwa na tatizo kubwa kuchagua watu wawili wa kwenda nao maana baada ya kushinda shindano la Fanta na kupata fursa hii, tulikaa kama familia na kuamua jinsi ya kuitumia.

Mama mzazi na kaka yangu mkubwa ambao wote wamenifanyia mengi maishani, ndio walioteuliwa na mimi niliuafiki na kuufurahia uamuzi huu maana hawa ni jamaa zangu lakini vile vile ni marafiki wa kweli," alisema Michael Simbeye.

Mohamed Hilal mwenye umri wa miaka 25 aliyeshinda katika kituo cha Zanzibar, aliwachagua vijana wenzake wawili ambao anaishi karibu nao na ni marafiki wanaokuwa pamoja wakati mwingi. Mshindi katika kituo cha Mwanza, Musa Mustapha Katambale, ambaye ni mfanyabiashara mdogo, aliwachagua wafanyabiashara wawili ambao humsaidia katika shughuli zake ili aende nao Paris.

Kwa ujumla, Watanzania hao waliokwenda katika ziara hii, kwa nyakati tofauti wanasema maandalizi ya ziara na mapokezi waliyoyapata, yalikuwa mazuri mno kwao. "Tulikuwa na watu wa kutuongoza safarini na tulipofika tulikuta maandalizi ya malazi, chakula na hata ratiba ya matembezi vimekamilika.

Hivyo mambo yalikwenda vizuri" alisema Fateh Dewji, Mfanyabiashara wa Tabora na kuongeza,

"Maendeleo ya watu wa Ufaransa kwa ujumla yaliwavutia pia."

"Nilijiona kama niko katika Dunia tofauti" alisema Bi. Merina Mwembe, mama wa makamu ambaye katika maisha yake hajawahi kutembelea mji wo wote mkubwa.

Wanasema miongoni mwa vitu vilivyowavutia zaidi ni sehemu mbalimbali za mji wa Paris ambazo hutembelewa na watalii wengi kila wakati kama vile Mnara wa Eiffel na sehemu inayoitwa Disneyland.

Kuhusu sehemu hizi mbili maarufu za jijini Ufaransa, Fateh Dewji anasema:

"Katika mnara wa Eiffel kuna teknolojia ya kukupandisha na kukuzungusha katika sehemu mbali mbali huku ukipata fursa ya kuliona vizuri jiji la Paris kutoka juu.

Nayo Disneyland ina mambo mengi ya kale yenye kuelezea historia ya Ufaransa".

Dewji anaendelea kueleza kuwa mahali hapa kuna watu wengi kila wakati, kukiwemo wafanyabiashara wenyeji, lakini wengi wao wanakuwa ni watalii

"Inaelekea Wafaransa wamewekeza sana katika sekta ya utalii," alisema.

Naye Badru Mohamed Haji anaeleza kuwa, "Matembezi ya jioni kwenye mto Seine ambao unapita katika jiji la Paris ulikuwa ni kivutio cha pekee.

Mandhari ya mto, majego, na shughuli za biashara zinazoendelea katika eneo hili ni baadhi ya mambo yanayowavutia watalii katika sehemu hii" alieleza kijana.

Kuhusu chakula walichopewa nchini Ufaransa Watanzania walikuwa na maoni tofauti. Wakati baadhi ya vijana walikisifia, Bi. Merina Mwembe alisema: " Siwezi kusema hakikuwa kizuri lakini kinakuwa ni mchanganyiko wa vitu vingi na hivyo wakati mwingine huwezi kujua unakula nini."

Kwa ujumla Watanzania waliopata bahati ya kwenda Paris wanawashukuru watengenezaji wa Fanta kwa kuandaa shindano hili lililowapatia fursa ya kutembea nje ya nchi.

"Hili lilikuwa ni mojawapo ya matukio makubwa katika maisha yangu.

Nimefaidika sana maana mtu unaposafiri unajifunza mengi,na hivyo nawashukuru watengenezaji wa Fanta kwa kunipa nafasi hii" Alisema Joshua. D. Donald, mshindi kutoka Moshi.

Naye Mohamed Hilal, wa Zanzibar alitoa shukrani zake kwa kusema kuwa, "Fanta wamedhihirisha kwamba mashindano yao sio ya upendeleo na zawadi wanazoahidi wanazitoa.

Mwanzoni nilipoambiwa nitakwenda Paris sikuamini lakini baadaye ndoto yangu ilitokea kuwa kweli. Nawashauri wananchi wasisite kushiriki katika mashindano ya Fanta ya aina hii yanapotokea.