Ndoa na familia katika maadhimisho ya Yubilei ya Bwana

KATIKA maadhimisho ya Yuilei kama familia ya Mungu, Kanisa mwaka huu linaendelea na maadhimisho ya kijubilei. Katika programu za makanisa mahalia juu ya jubilei yako mengi yaliyojitokeza kama matatizo ya kichungaji, mfano uibukaji wa kasi wa familia za mzazi mmoja. Kwa upande mwingine familia nyingi zimepata nafasi ya kutafakari juu ya Sakramenti ya Ndoa, maisha ya ndoa katika familia, wajibu wa wanandoa na jinsi wanandoa wanavyoshiriki utume wa Kanisa kwa kuwa wainjilishaji wa watoto wao na kuchukua jukumu la kujitakatifuza. Kwetu Afrika ndoa na familia huthaminiwa na ndio maana Sinodi ya Afrika 1994 ilichukua familia kama kigezo kikuu cha Kanisa "Kanisa kama familia ya Mungu".

Katika makala hii, Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturujia katika Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania (TEC), Padre Julian Kangalawe anajaribu kuelezea mtazamo wa idara hiyo kitaifa juu ya masuala ya ndoa na familia katika maadhimisho ya Jubilei ya Bwana.

Katika kusheherekea Yubilei, Idara inatuma kitabu cha "Ibada ya Sakramenti ya Ndoa".

Kitabu kitasaidia kikamilifu taratibu za kichungaji hususani maadhimisho ya Sakramenti ya Ndoa.

Ili kutimiza adhma hii, tutafakari kwa pamoja juu ya sakramenti hii na familia kwani ni sura mbili katika shilingi moja zenye kusaidia uchungaji na uimarishaji wa familia.

1. Sakramenti za Kikristo

Ndoa kama sakramenti nyingine, chimbuko lake kuu ni Kristu katika Kanisa.

Maneno na matendo ya Yesu kipindi cha maisha yake yaliyofichika na huduma yake ya hadhara yalikuwa tayari ya wokovu, kwani yalitazamia mbele nguvu ya fumbo lake la Pasaka.

Hayo yalikuwa yanatangaza na kutayarisha kile ambacho angalikitoa kwa Kanisa wakati yote yatakapokuwa yametimia. Mafumbo ya maisha ya Kristo huunda misingi ya kile ambacho sasa Kristo hukigawa katika sakramenti kwa njia ya wahudumu wa Kanisa kwani kile kilichoonekana ndani ya wokovu wetu, kimepitishwa ndani ya mafumbo yake.

Sakramenti ambazo ni "kazi bora ya Mungu" katika Agano Jipya na la milele, uweza utokao katika mwili wa Kristo, Lk.5:17; 6:19:8-46, ulio na unaohuisha daima, ni matendo ya Roho Mtakatifu anayefanya kazi katika mwili wake yaani Kanisa.

Kwa njia ya Roho anayeongoza kwenye kweli yote, Kanisa limetambua kidogo kidogo hazina iliyoipokea toka kwa Kristo na limepanga ugawaji wake kama lilivyofanya kwa kanuni ya Maandiko Matakatifu na mafundisho ya Imani, likiwa wakili mwaminifu wa Mafumbo ya Mungu (Yo. 16:13; Mt.13:52, 1Kor 4:1).

Sakramenti ni za Kanisa kwa namna mbili, kwamba zipo kwa njia yake na kwa ajili yake.

Ni kwa njia ya Kanisa kwa sababu ni sakramenti ya tendo la Kristo anayetenda ndani yake kwa njia ya Utume wa Roho Mtakatifu.

Na pia kwa ajili ya Kanisa kwani ndizo sakramenti zinazolifanya Kanisa, kwani zinadhihirisha na kuwasilisha kwa watu, hasa katika Ekaristi, fumbo la ushirika wa Mungu ambaye ni upendo mmoja katika nafsi tatu.

Ndani ya kila sakramenti, ni Kristo mwenyewe anayetenda kwa ajili ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa. Sakramenti zimewekwa ili kuwatakatifuza wanadamu, kuujenga mwili wa Kristo na mwishowe, kumtolea Mungu ibada.

Kwa kuwa ni ishara zinazowafundisha waamini, kwa upande mmoja zinadai imani na kwa upande mwingine zinalisha imani yenyewe kwa maneno na matendo ya Ibada, tena zinaimarisha na kudhihirisha Imani hiyo.

Sakramenti zikiadhimishwa inavyostahili (kama kijitabu hiki cha Sakramenti ya Ndoa kilivyo), hutoa neema ambazo huziashiria.

KWA UFUPI:

Sakramenti ni Ishara zenye nguvu ya neema zilizowekwa na Kristo na kukabidhiwa kwa Kanisa, ambazo kwazo uzima wa Kimungu unatolewa kwetu. Madhehebu yanayoonekana ambayo kwayo sakramenti uandimishwa, huashiria kuzileta neema za pekee za kila sakramenti.

Kwa mtiririko huo, Sakramenti ya Ndoa kama sakramenti nyingine, ina umuhimu wa pekee katika maisha ya wanakanisa.

Tukiwa tunaendelea na Jubilei, tuendelee kutafakari juu ya ndoa na familia tukizingatia Kanisa kama familia ya Mungu.

2. NDOA KATIKA MPANGO WA MUNGU

Maandiko Matakatifu yanaongelea ndoa na juu ya fumbo lake, kuwekwa kwake, na juu ya maana ambayo Mungu ameipa, juu ya asili na lengo lake, juu ya utekelezaji wake katika mtiririko mzima wa historia ya wokovu. (1Kor.7:39), Efe.5:31-32.

Kwa vyovyote vile, Mungu ndiye mwasisi wa ndoa (GS 48KKK 1602-1605).

Wito wa ndoa umeandikwa katika maumbile yenyewe ya mwanaume na mwanamke kama walivyotoka mkononi mwa muumbaji.

Ndoa si jumuiya ya kibinadamu tu, licha ya mabadiliko mbalimbali iliyopitia katika mwenendo wa karne, katika tofauti za tamaduni, miundo ya kijamii nahali za kiroho.

Tofauti hizi zisifanye hali za jumla na za kudumu zisahaulike. Ingawa hadhi ya jumuiya hii haionekani wazi kila mahali kwa uangalifu ule ule, (G.S 47) hata hivyo tamaduni zote kuna maana fulani ya ukuu na muungano wa ndoa.

Mungu aliyemuumba mtu kwa mapendo na amemwita pia kupenda wito ambao ni wa msingi na wa kuzaliwa wa kila mwanadamu kwani mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwa. 1:27 1Yoh 4:8,16) ambaye yeye mwenyewe ni mapendo.

Mungu akishaumba mwanaume na mwanamke, kupendana kati yao huwa na sura ya mapendo kamili na daima ambamo Mungu ampenda mtu. (1Yoh 1:8-16, Mwa. 1:31).

Ndoa huhusishwa na mpango awali wa uhulushi. Kile kinachoashiria umoja usiovunjika wa maisha ya wawili walioungana kwa mpango wa ndoa, hudhihirisha mpango wa Muumbaji (Mt. 19:4) ulivyokuwa tangu mwanzo.

3. SAKRAMENTI YA NDOA

Agano la Ndoa ambalo kwa njia yake, mwanaume na mwanamke huunda kati yao jumuiya kwa maisha ya wote, kwa tabia yake ya asili, liko kwa ajili ya manufaa yao kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Agano hili kwa wabatizwa limeinuliwa na Kristo kwa hadhi ya sakramenti.

Kwa njia ya Ubatizo ambayo ni Sakramenti ya Imani, mume na mke hupandikizwa mara moja tu, na kwa daima katika Maagano ya Kristo na Kanisa lake.

Kwa hali hiyo, muungano wa kindoa unaingizwa kwenye mtiririko wa upendo wa Kiroho na kutajirishwa kwa nguvu ya sadaka yake.

Hivi kweli kondomu itumike kudhibiti Ukimwi; kweli?(2)

Inatoka toleo lililopita

Na Emil Hagamu wa Pro-Life

Ni kweli kuwa unapoona hali ya Ukimwi kwa macho yako barani Afrika kwa mara ya kwanza unapata mshituko na mshangao. Mkosaji anatafutwa na kwa kawaida ni wale wale wanaoshughulikia janga hilo, ndio wanalaumiwa, wakati wengine wanaridhika tu, kwa kulaumu.

Tunu za familia zinatuhakikishia ushindi wa kweli. Kwa hiyo Kanisa Katoliki, limelaumiwa kwa kushindwa kuona ukweli na kwa kuzembea juu ya janga la Ukimwi barani Afrika kwa sababu ya msimamo wake dhidi ya kondomu kama kinga dhidi ya maambukizo.

Katika mikutano mbalimbali, Halmashauri ya Kipapa ya familia imerudia mara kwa mara mafundisho ya Kanisa kuhusu suala hili gumu. Mafundisho hayo yamesimama katika ukweli wa tunu za familia. Lililo mbele yetu ni mtazamo juu ya mwanamke na mwanaume, hadhi yao maana na umuhimu wa jinsia kama ulivyowekwa bayana na vitini vya halmashauri hii, kuhusu mivutano ya kijinsia ya usafi katika ndoa, basi maana halisi ya zawadi ya kujitoa kila mmoja kwa mwenzake inadhihirika na hii inahusu pia taifa na iwapo misukumo ya umalaya imeepukwa, binadamu atapata ushindi wa kweli hata ushindi dhidi ya janga hili la ukimwi.

Katika kukabaliana na janga la Ukimwi, yatupasa kutofuatisha kati ya njia zinazokinga na zile zinazopunguza. Kwa mfano, Malaria, ugonjwa unaoweza kulinganishwa na ukimwi kutokana na madhara yake kwa watu na idadi kubwa ya vifo inayosababisha, njia za kupunguza zilipatikana tangu muda mrefu.

Lakini kwa vile njia hizo hazikumaliza tatizo, yaani hazikugusa kiini cha ugonjwa, kinadharia zilionekana kufaa lakini, kwa hali halisi, njia hizo hazijafaulu kumaliza kuua mazalio.

Mfano mwingine ni taifodi. Uzuiaji uliwezekana kwa sababu tuliweza kuwashawishi watu kutumia maji safi na salama. Hili lilikuwa suluhisho la kudumu kwa sababu watu waliweza kusahihisha makosa yao.

Kama kweli watu wanataka kuzuia Ukimwi, lazima washawishiwe kubadili tabia kuhusu mivutano ya kijinsia ambayo ndiyo chanzo kikubwa cha uambukizo. Hadi hapo jitihada za kweli zitakapofanyika katika eneo hili, hakuna kinga nyingine yoyote itayaofaulu.Kondomu ni njia mojawapo ya njia zitumikazo kupunguza uambukizo wa virusi vya Ukimwi yaani kupunguza kasi ya kuenea. Na hapa inatupasa kuelewa kuwa kupunguza kasi sio kuzuia.

Tukiweka kando ukweli wa kondomu kupasuka au kuvulika, uzoefu ambao ni wa kawaida wakati wa kujamiiana, unaeleweka kuwa kondomu yaweza tu, kupunguza maambukizo iwapo inatumiwa kwa usahihi na ni katika hali hii tu, ndipo uwezo wake waweza kuonekana.

Maelezo ya kina juu ya kushindwa kwa kondomu kuzuia magonjwa mbalimbali ya zinaa ukiwemo Ukimwi, yameelezwa kwa kirefu mahali na kwa nyakati mbalimbali. Upunguzaji maambukizo umelinganishwa na matumizi sahihi ya kondomu bila kudhihirisha kitakwimu juu ya kiwango cha ufaulu wake.

Uamuzi wa kutumia kondomu kama kizuia mimba unaonesha pia usio wa mafanikio.

Takwimu zinaonesha kiwango cha kushindwa kwa asilimia 15 kwa kila vitendo 100 vya zinaa vyenye kutumia kondomu.

Tunajiuliza, virusi vya Ukimwi ambayo ni vidogo zaidi ya chembechembe za uzazi kwa mara 450, vinaweza kweli kuzuiwa na kondomu wakati tukijua kuwa chembechembe za uzazi zinapita katika kondomu kwa kiwango cha 15 katika kila 100 kwa tendo kamilifu la ngono?

Takwimu za kutegemewa juu ya uhakika wa kondomu katika kuzuia Ukimwi ni zile za "Groupe &Etudes European".

Hata hivyo, uchunguzi huu ulihusu jozi ambazo mmoja hakuwa na virusi na hapakuwa na magonjwa ya zinaa katika mazingira ya Ulaya ambapo uambukizaji wa virusi vya Ukimwi, umedhibitiwa.

Zaidi ya hayo, takwimu zinazopaswa kutafsiriwa daima zinaonesha kiwango cha kushindwa cha asilimia 10 (kwa kila kondomu 100 zilizotumika).

Janga la Ukimwi haliwezi kudhibitika na kondomu.

Kwa hiyo hakuna tumaini la kusimamisha maambukizo ya Ukimwi kwa njia ya kondomu, kama vile ambavyo hatuwezi kuzuia mafuriko ya mto kwa kutumia magunia ya mchanga wakati nguzo zake zimebomoka. Kwa vyovyote vile, msimamo wa Kanisa katika kuzuia Ukimwi, hauko katika ngazi ya kiafya tu.

Kanisa linachunguza kiini cha tatizo katika mwenendo na tabia za kibinadamu yaani, heshima iliyopo kwa jinsia. Thamani zinazowezesha makuzi ya binadamu katika jamii ya kibinadamu.

Kama uambukizo wa Ukimwi umefikia viwango hivyo katika nchi za Afrika ni kwa sababu umepata mazingira kubalifu ya kuenea kwake. Ukosefu wa ajira, umaskini, mazingira ya wakimbizi, vita vya wenyewe kwa wenyewe, ukosefu wa serikali imara, ukosefu wa huduma bora za afya, uhalifu, ongezeko la watu maskini mijini, na ongezeko la ukahaba.

Zaidi ya hayo, hali ya wanawake walioko kwa ajili ya kuridhia matakwa ya wanaume zao, inaeleza kwa kiwango kikubwa, kwa nini wanaoathirika zaidi na janga hili ni wanawake? (wanawake 12-13 kwa kila wanaume 10).Uwepo wa magonjwa ya zinaa katika viungo vya uzazi vya wanawake unarahisha kuambukizwa virusi vya Ukimwi.

Udhibiti wa Ukimwi unapaswa kugusa eneo hili la kijamii. Kinga ya kweli dhidi ya Ukimwi ambayo ni ya uhakika na ambayo hakuna mtu awezaye kuikana, ni kuacha tendo la kukutana kimwili miongoni mwa vijana kabla ya ndoa na uaminifu katika ndoa. Haya ndiyo mafundisho ya Kanisa. Kuwataka vijana watumie kondomu katika kujamiana kuna maana ya kuendeleza mzunguko wa ngono ambayo ni kiini cha kuenea kwa Ukimwi, ni kujidanganya sambamba na kuoanisha uhakika wa kinga dhidi ya Ukimwi na kiasi cha kondomu zilizosambaza katika eneo moja. Ukweli unaonesha bayana kuwa, kwa kadiri kondomu zinavyosambazwa kwa wingi, ndivyo hivyo kiwango cha maambukizo kinavyokuwa kikubwa.

Leo hii tunapatiwa mifano ya nchi za Uganda na Thailand ambako kampeni za kimataifa na kitaifa za matumizi ya kondomu zinasemekana kuwa zimeleta mafanikio katika kudhibiti maambukizo ya virusi vya Ukimwi. Nchini Thailand jitihada za watu wa afya zililenga kwa wanawake malaya na wateja wao. Matumizi ya kondomu yalisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizo ya magojwa ya zinaa.

Hata hivyo, hatuna hakika kama usambazaji wa kondomu nchini humo ulipunguza kasi ya ongezeko la ukimwi. Matumizi ya kondomu katika mazingira haya, yalionekana kama ovu dogo lakini haliwezi kupendekezwa kuwa kipimo cha ubinadamu na maendeleo.

Pengine serikali ya Thailand ingehoji sababu ya kukua kwa biashara ya umalaya nchini mwao.

Mfano wa Uganda ni mzuri kwani jitihada zimefanyika pande zote na hatimaye kufikia kiini cha janga lenyewe. Katika utafiti uliowasilishwa na UNAIDS maswali yaliulizwa kuhusu sababu za kupungua kwa janga hili nchini Uganda.

Maambikizo ya virusi vya Ukimwi yalipungua kutoka asilimia 45 hadi asilimia 35 kwa wanaume waliopimwa magonjwa ya zinaa katika kliniki mjini Kampala na kutoka asilimia 21 hadi asilimia 5 kwa wanawake wajawazito waliochunguzwa mjini Jinja kati ya mwaka 1990 na 1996.

Hoja tunayoitilia maanani ni mabadiliko ya tabia katika suala la mahusiano ya kimapenzi miongoni mwa vijana ambao kwa makusudi wanachelewesha tendo la kujamiana

(Asilimia 56 ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 19 walisema mwaka 1995 kuwa hawakuwahi kuwa na mahusiano ya ngono, ikilinganishwa na asilimia 31 mwaka 1989 na asilimia 46 ya wasichana walisema hivyo hivyo mwaka 1995 ikilinganishwa na asilimia 26 mwaka 1989) wanaoa na wanaolewa katika umri mkubwa. Hoja nyingie ni kuua uzinifu (kujamiana nje ya ndoa) ulipungua kutoka asilimia 22.6 mwaka 1989, hadi asilimia 18.1 mwaka 1995 kwa upande wa wanaume).

Katika kuhitimisha uchaguzi huo wa udhibiti wa janga la UKIMWI, katika nchi za Afrika Kusini mwa Sahara na mchango wa Kanisa Katoliki katika hali hiyo tutaje mifano kadhaa iliyoanzishwa na vijana na ambayo inapaswa kuigwa.

Katika nchi za Uganda, Tanzania na Nigeria, vipo vikundi vya vijana vinavyoratibiwa na mashirika ya kitawa, mapadre na walei ambao wamejitoa kwa dhati kuwasaidia ili vikundi hivi vimejizatiti katika kupambana na janga hili la ukimwi na vinajulikana kama.’Vijana Hai’ (Youth Alive), Youth for live’)

Vikundi hivi ambavyo vinajitegemea kiuendeshaji na ambavyo sio vya kiserikali au nchi vijana wake wa kiume na wa kike wenye umri kati ya 16 na 18, wanajishughulisha na mapambano dhidi ya Ukimwi.

Miongoni mwao, wakiwa wamejitoa katika maisha ya usafi wa moyo (kuacha ngono) hadi wakati wa ndoa na uaminifu baada ya kuoa/kuolewa.

vikundi hivi sio vya kinadharia. Vipo kweli na vimekuwepo tangu miaka mingi ya nyuma vikiwa hai. Ukipata nafasi ya kuongea na vijana hao utagundua kuwa wako safi na ni wa kawaida wenye furaha wanapenda muziki na michezo, wanapenda uhai si kondomu . vikundi hivi haviombi fedha vinaomba upendo, subira, muda kujitoa na imani sahihi inayowaongoza.

Bila kupinda ukweli vikundi hivi ni mifano ya kuigwa, pengine sio rahisi sana kufaulu, lakini vipo katika maisha ya kawaida ya binadamu vilivyojikuta katika imani na matumaini na sio katika kondomu. Mamilioni ya dola yanayotumika katika kutengeneza kondomu yangeweza kutumika katika kuwapa vijana elimu bora na kuunga mkono juhudi wazifanyazo katika kudhibiti Ukimwi. Kanisa Katoliki linaamini katika tunu ya ubinadamu na mali alizonazo. Linaamini kwa mfano wa Mungu.

"Mungu aliumba mtu (mume na mke) kwa mfano wake" (Mwa. 1:27). Katika matatizo haya ya Ukimwi, tumemtendea binadamu kama vile angekuwa mnyama anayeshughulikiwa na bwana mifugo, tukasahau uwezo wote aliokuwa nao ambao tukiutumia vizuri, binadamu huyu anaweza kubadilika na kutenda ipasavyo.

Kama ambavyo Malthus alikosea kwa kutofikiri kuwa binadamu angeweza kutumia vipaji vyake katika kuzalisha mali zaidi ambayo ni muhimu kwa maisha yake, kosa limetendeka kwa kuweka nguvu zetu zote katika kupunguza kasi ya maambukizo ya Ukimwi kwa kutumia kondomu ambayo ni dharau kwa utu na heshima ya binadamu na bado ni hatari mno.

Tunaweza kuelewa malengo ya maofisa wa afya kugawa kondomu kwa wanawake malaya na wateja wao lakini, udhibiti wa Ukimwi lazima uwe zaidi ya hapo, lazima uende ngazi ya juu zaidi na kushambulia kiini chake.

Jambo hili sio kwamba haliwezekani, tunatakiwa kupanua uelewa wetu na kukubali kubadilika kwa kuweka uzito katika heshima na hadhi ya binadamu.

Vikundi vya vijana Youth Alive au Youth for Life, wameamua, ni uchaguzi wa manufaa kwa Bara la Afrika.

Maisha na Mikasa

MSICHANA MLEMAVU ASEMA:

Ingawa naandikia miguu, lazima niwe Mbunge

lNi msichana pekee, kitinda mimba wa familia

lMikono yake yote haina kazi

Peter Dominic na Elizabeth Steven

INGAWA miguu ndiyo mikono yake kwa kuwa kazi anazopaswa kufanya kwa kutumia mikono, yeye anatumia miguu ikiwa ni pamoja na kuchora na kuandika, msichana huyu ambaye ni tishio darasani kwake na hata katika mtihani uliopita alipata alama 70 katika somo la Uraia, anatamani sana; na anasema lazima awe mbunge.

Ingawa si rahisi kuamini, sawa kwa kuwa huo ni uhuru wa msomaji kuamini ama kutoamini hadi atakapoona mwenyewe. Lakini, kinachoelezwa hapa si tungo wala simulizi, ni ukweli mtupu ingawa unaonekana kama muujiza wa Kimungu mbele ya uso wa dunia.

Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu nchini, Bw. Hosea Kalumuna, aliwahi kusema kuwa kama bado wapo wazazi wanaowaficha watoto wao ndani kwa sababu ya ulemavu walionao kwa kisingizio eti hawajiwezi na wataharibu pesa zao, na wengine hata bila haya wanadiriki kusema kuwa watoto wanaozaliwa na ulemavu, wanaaibisha familia.

Basi, kalumuna aliitaka jamii kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa kuwa hao wanawanyanyasa, kuwanyima huduma na haki za msingi za kibinadamu na kulinyima taifa watu muhimu wenye vipaji vinavyoweza kutumika kwa manufaa ya taifa kwa siku za usoni.

Miongoni mwa watoto ambao ni walemavu lakini, bahati nzuri wazazi wake wakabahatika kujua umuhimu wake katika jamii na kuamua kumsomesha kwa kadri ya uwezo wao, ni msichana Patricia Edward.

Patricia ni msichana mwenye umri wa miaka 14. Anasoma katika shule ya msingi ya Jeshi la Wokovu (Matumaini), iliyopo katika manisapa ya Temeke jijini Dar-Es-Salaam.

Msichana huyu kitinda mimba na msichana pekee katika familia yao ya watoto wanne, huongea kwa taabu huku mikono yake yote isiyo na nguvu kabisa ikiyumba na kueleaelea hewani sambamba na kichwa kisichotulia kwa kuinama.

Mtoto huyu kitindamimba kati ya wakubwa zake, Livingstone, Paschal na Aristariko, hawezi kushika kitu chochote kwa mikono .

Anasema wakubwa zake hao pamoja na wazazi wake wote ni wazima wasio na ulemavu wowote na tayari mkubwa wake mmoja amemaliza masomo ya sekondari na wengine bado wanasoma sekondari.

Msichana huyu huishi shuleni kwake wakati wazazi wake, Bw. Edward na Bi. Rosada Tesha, wote kwa mujubu wake, wanaishi Dodoma ambapo wanafanya kazi katika Jeshi la Magereza.

Hutumia mguu wa kushoto kushikia kalamu ambayo huichomeka katikati ya kidole gumba na kinachofuatia, wakati ule wa kulia mara nyingi huutumia kushikia rula.

Katika kutafuta kifaa chochote cha darasani kama kalamu, karatasi au daftrai kutoka katika mfuko wake, hutumia miguu yote na hutumia visigino vya miguu yake kushikia karatasi au daftari linapokuwa katika kimeza chake maalumu au chini ya sakafu.

Miguu huwa kamwe haipati ushirikiano wowote wa mikono kwa kuwa mikono haiwezi kabisa chochote.

Waandishi wa gazeti hili waliomtembelea shuleni kwake walimshuhudia akiendelea na masomo yake kama kawaida kwa kutumia miguu ambayo licha ya kuitumia kuandika, huitumia kwa kutembea na kucheza mpirakama kawaida na anasema 'napenda sana michezo ili kujiweka fiti'.

Akielezea namna alivyofanikiwa kuwashawishi wazazi wake kumpeleka shule, Patricia anasema, "Nilikuwa nikiwatamani akina Livi (anamaanisha wale wakubwa zake) na marafiki zangu (watoto wa jirani), wanapokwenda shule, mimi ninabaki peke yangu nyumbani halafu wanaporudi, eti tunacheza pamoja halafu wenyewe wanaimba nyimbo za shule ambazo mimi sizijui," anasema kwa maringo na aibu aibu.

Anaendelea kusema, "Nikawalilia (Wazazi) mpaka wakanionea huruma."

Anasema wazazi wake walipomkubalia kumpeleka shule alifurahi na kujiona kuwa anathaminika ndani ya jamii kama ndugu zake ambao sio walemavu.

"Baba waliposema eti watanileta shuleni nilifurahi sana maana nilijua mimi sitasoma shule kama kaka zangu. Nikaona eti kumbe na mimi wananipenda kama akina Livi," alisema Patricia, kwa taabu.

Gazeti lilipotaka kujua namna anavyopata huduma nyingine kama kula na kuoga, patricia alisema, "wananilisha na kuniogesha." Alipoulizwa ni akinanani, alijibu, " Akina dada." Alikuwa akimaanisha watumishi wa kike wa shule hiyo ya walemavu.

Mtoto huyo aliyesema anatamani sana asome hadi awe mbunge katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema anapenda sana somo la Uraia, likifuatiwa na Kiswahili ambalo katika muhula uliopita, alipata alama 70, Kiingereza na Sayansi na pia, anasema lazima asome hadi Chuo Kikuu.

Hata hivyo msichana huyu ambaye katika mtihani uliopita alikuwa wa 7 kati ya wanafunzi 18 wa darasa lake, alishindwa kuelezea kuwa ni kwanini aliwaambia waandishi wa gazeti hili kuwa anaupenda uongozi wa Waziri Mkuu, Bw. Fredrick Sumaye.

KIONGOZI lilipotaka kujua asili ya mtoto huyo kuanza kuandika kwa kutumia miguu, Mwalimu Rehema Ibrahimu aliyekuwa naye tangu Darasa la Kwanza, alisema kuwa walimpokea na akaanza kufundisha kuitumia chaki na kibao kwa kuwa ilishindikana kabisa kutumia mikono kwa kuwa haina kazi na kwamba wakati huo kazi ilikuwa ngumu zaidi tofauti na sasa.

"Alipomudu kutumia chaki na kibao ndipo tukaanza kumpa penseli na karatasi," alisema na kuongeza, "Uzuri wake ni kwamba ni brihgt mno, ukimfundisha anaelewa haraka ila, tatizo lake ni kwamba anaandika taratibu mno kwa ajili ya miguu."

Hata hivyo Mwalimu Ibrahimu alisema kadri siku zinavyokwenda, ndivyo spidi ya Patricia inavyoongezeka kwa kuwa hata masomo nayo yanaongezeka.

"Ni Mtu wa kwenda naye taratibu akifanya kazi nyingi anachoka kwa kuwa sehemu kubwa ya viungo vyake, vimelemaa" alisema.

Wakizungumza juu ya msichana huyu, walimu wa shule hiyo, Hamis Fumao, Grace Mabeyo na Nyamisango Mtaki walisema kwa pamoja na mwalimu Ibrahimu kuwa ingawa mwandiko wa Patricia unaridhisha sana na mara nyingi majibu yake ni sahihi ukilinganisha na hali yake ya kuandikia miguu, ipo hatari wakati wa usahihishaji wa mitihani ya kitaifa, wasahishaji wakapuuza karatasi yake na wengine wenye ulemavu ingawa majibu ni sahihi.

Walishauri wakati wa kusahihisha majibu ya watoto wenye ulemavu kama huo, walimu wanaofahamu na wenye uzoefu na miandiko yao wahusishwe ili kuepuka kuwaonea kwa kuwa nyima alama kutokana na ulemavu wao.

"Walimu wanaomfahamu na mwandiko wake wawe karibu kwa sababu vinginevyo walemavu kama hawa watakuwa wanaonewa ingawa majibu yao ni sahihi kuliko wengine pengine wote," alisema mmoja wa walimu hao.

Mwalimu wake wa Jiografia Bw. Fumao alisema, "Tatizo lake ni utendaji. Hawezi kutumia miguu akawa na kasi na usafi kama anayetumia mikono. Ingawa kwake kuelewa ni mwepesi, lakini ni kazi sana kuchora kitu kama ramani. Lakini bado anafanya vizuri na kupata zaidi ya nusu huku maswali mengi anakuwa ameshindwa kuyamaliza." "Inabidi kuwa naye karibu maana yapo mambo mengine yanayomshinda kama kuyatoa madaftari yake katika begi. Hivyo ni vema wakati wa mitihani, awepo mtu maalumu wa kumsaidia huduma anazotaka."

Akizungumzia uwezekano wamsichana huyo kupewa muda wake wa ziada katika mitihani ya taifa, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo Bw. Alexander Robert, alisema hiyo siyo rahisi kwa kuwa wanafunzi wenye ulemavu wanaokuwa katika shule maalumu kma hiyo, hupewa muda wao sawa wenye nyongeza kuliko shule nyingine hivyo hadhani kama ni rahisi kuanza kumtenga mmoja mmoja.

"Serikali inawajali sana hawa watoto inawapa muda wa ziada na mitihani yao husahihishwa tofauti na ya wengine. Hata wewe fikiria kama kila mmoja atapewa muda wake, kwa walemavu mbalimbali kote nchini, itakuwaje," alisema.

Walimu wote walikiri kuwa mtoto huyo anahitaji muda mwingi wa ziada hali ambayo pia ni tatizo kubwa lakini wakasema, wanajitahidi kwa nguvu zao zote kuona kuwa wanamsaidia kwa moyo yeye na wengine wenye matatizo hayo.

Ingawa watoto hao hupewa uangalizi mkubwa wawapo shuleni lakini bado kuna unafuu wa kulipia gharama za masomo na malazi ikizingatiwa kila kitu hupata pale pale shuleni.

Mwalimu huyo Mkuu Msaidi ametoa wito kwa serikali, mashirika na watu binafsi kujitokeza katika kuwasaidia watoto walemavu badala ya kuelekeza juhudi zao katika maashirika na watu wenye uwezo wa kujiendeleza kwa nguvu zao peke yao.

"Ingawa ni hiari yao, lakini wafadhili wengine wanaelekeza misaada sehemu ambazo sio muhimu sana lakini , wanawaacha watoto kama hawa ambao ni tegemeo la kesho kwa taifa, " alisema.

Patricia mwenyewe anaushukuru uongozi wa shule hiyo akiwamo Mwalimu Mkuu Bi. Rozi Sato, na msaidi wake pamoja na walimu wote kwa kusimamia haki zao kupatikana ikiwa ni pamoja na elimu kwa kadri ya mazingira yaliyopo.

Pia anawashukuru hasa mwalimu mkuu kwa kuwa simamia kuona kuwa wanapatiwa huduma na usaidizi unaostahili kama binadamu.