Imani za wengine

Unywaji pombe na Imani za dini

Na Mwandishi Wetu

UWEPO wa kinywaji pombe ni moja ya kweli zilizo katika maisha ya mwanadamu hapa duniani. Binadamu wa karne zote na wa kabila mbalimbali amekuwa akiitengeneza na kuitumia pombe katika mazingira yake kadhaa.

Matumizi ya pombe ni kitu kinachohitaji mwongozo na maelekezo ya kimaadili kama zilivyo kweli nyingine za maisha ya binadamu.

Leo hii, tunashuhudia imani za kidini na vikundi vinavyokataa matumizi ya aina yoyote ya pombe.

Baadhi ya vikundi vinajaribu kutumia kila njia mojawapo ikiwa ni pamoja na Biblia, kuonesha kuwa pombe ni kitu kibaya na imekatazwa na Mungu.

Baadhi ya wafuasi wa vikundi au madhehebu hayo, husema kuwa pombe ni shetani na yeyote anayeionja ni mfuasi wa shetani.

Wengine wamefikia hatua ya kudai kuwa chochote kile kinachohusika na utengenezaji wa Pombe, mfano, Ndizi au ulezi ni shetani na havifai kutumiwa na binadamu.

Katika kijarida cha Jimbo Katoliki la Moshi (News Bulletin of the Diocese of Moshi-Kilimanjaro) toleo la Mei,2000. Padre Gregory Olomi, alijadili kwa kina suala hili kama linavyozungumzwa katika toleo hili.Jambo lililo wazi ni kwamba, pamoja na kampeni za watu hao, hawajafanikiwa kuiondoa pombe katika maisha ya watu.

Upo umuhimu wa kuwafundisha watu ukweli kuhusu kinywaji hiki kuliko kushikilia tu kwamba ni kitu kibaya.

Mada hii inalenga kwenye kujaribu kudhihirisha machache kati ya mengi yanayofundishwa na Biblia kuhusu pombe.

Maana ya neno hilo POMBE.

Pombe ni kinywaji chenye asili ya kilevi (KWA Kingereza alcohol). Kutokana na kilevi hicho, pombe huitwa pia kileo. Pombe hutambuliwa kuwa ni kali au isiyo kali, kutokana na kiwango cha kilevi kilicho ndani yake.

Kiwango cha kilevi kinachopatikana katika aina fulani ya pombe, kinategemea namna ilivyotengenezwa pombe yenyewe.

Kutokana na kilevi hicho, mtu anapokunywa pombe kupita kiasi, mishipa yake ya fahamu hulegea, mwenyewe hujisikia kuchoka, hushindwa kifikiri na kufanya kazi zake za kawaida na kwa wakati wake, hukosa mpangilio sahihi katika kufikiri na katika utendaji wake.

mara nyingine, hupoteza kabisa fahamu.

Historia inaonesha kuwa makabila na mataifa mbalimbali yamekuwa yakitengeneza na kutumia aina mbalimbali za pombe.

Mfano, Wachaga hutengeneza na kutumia "mbege", Wazaramo - "tembo", na Wahaya - "rubisi".

Pombe za mataifa ya kigeni ni pamoja na divai au mvinyo, bia, Whisky, na hata Brandy.

Kutokana na ukuaji wa teknolojia na mawasiliano rahisi, viwanda na utengenezaji, pia matumizi ya pombe hizo za kigeni, vimeenea kote katika nchi nyingi duniani.

Baadhi ya mafundisho ya Biblia kuhusu kinywaji Pombe:

Mwa.14:18-19 Melkizedeki kuhani anambariki Abraham kwa divai, anasema, "Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa Kuhani wa Mungu aliye juu sana.

Akambariki, akasema, Abrahamu na abarikiwe na Mungu aliye juu sana, Muumba Mbingiu na nchi"

Hes. 15:5 Mvinyo unaotolewa sadaka kwa Mungu. "Na divai kwa sadaka ya kinywaji, robo ya hini, utaiandaa sadaka ya kuteketezwa, au kwa dhabihu ya kuchinjwa kwa ajili ya kila Mwana Kondoo."

Hes. 28:7. Kinywaji kikali kinatolewa kama sadaka mahali patakatifu. " Na sadaka yake ya kinywaji itakuwa robo ya hini kwa mwanakondoo mmoja; hiyo sadaka ya kinywaji, ya kileo, utammiminia Bwana katika mahali hapo patakatifu.

Law. 23:13. Sadaka ya kinywaji cha divai inatolewa kwa Mungu. "na sadaka yake ya unga itakuwa za kumi mbili za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, ni sadaka yake ya kinywaji itakuwa ni divai, robo ya hini.

Kumb. 14:25-26. Maneno yaliyo katika kifungu hiki yanaonesha ridhaa ya Mwenyezi Mungu kuwa wanaweza kutumia vinyaji vikali kwa lengo la burudani."...na zile fedha zitumie kwa chochote itakachotamani roho yako, ng’ombe,, au kondoo, au divai, au kileo, au roho yako itakacho kwako chochote; nawe utakula huko mbele za Bwana, Mungu wako; tena furahi wewe na nyumba yako." (26)

Zab. 104: 15. Divai imeumbwa imfurahishe mwanadamu.

"Na divai imfurahishe mtu moyo wake, aung’aze uso wake kwa mafuta, na mkate umburudishe mtu moyo wake."

Yoh. 2:1-11 Katika arusi ya Kana pombe ilikuwa kinywaji muhimu katika kufanikisha sherehe ya arusi.

Mt. 11:18-19 Katika maisha ya duniani Yesu Kristo alitumia divai pia. "Maana Yohana alikuja hali wala hanywi, wakasema yuna na pepo. Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, wakasema, mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake.

Mt. 26:26-29 Kwa desturi ile ile ya Wayahudi kumtolea Mungu sadaka ya mvinyo, yesu anatumia kinywaji hicho kufanyiza Ekaristi ambayo ni sadaka ya mwili na damu yake aliyoitoa msalabani.

1Tim. 5:23 Kifungu hiki kinaonesha pombe ikitumiwa kama dawa. "Tokea sasa, usinywe maji tulakini tumia mvinyo kidogo kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara.

Lk.10:34 Divai inatumika kutibu majeraha. "Akakaribia, akamfunga jeraha zake, akazitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza."

Meth. 20:1 Tahadhari inatolewa, kwani kileo kinaweza kumwongoza mtumiaji katika maovu. "Mvinyo hudhihaki, kileo huleta ugomvi; na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima."

Law. 10:8-9 Mungu anaelekeza wakati usiofaa kunywa kileo yaani wakati wa kusali hekaluni. "Kisha Bwana akanena na Haruni, akamwambia usinywe divai wala kileo chochote , wewe, wala wanao pamoja nawe, hapo mwingiapo ndani ya hema ya kukutania, ili kwamba msife, Amri hii itakuwa ni Amri ya milele katika vizazi vyenu."

Isa 5:11 Ole wao wanaoamka na pombe asubuhi na kuendelea kunywa bila kiasi.

Isa. 5:22 Usijitafutie ubingwa au umaarufu katika kileo.

1Pt.4:3 Ulevi au kunywa kupita kiasi ni moja ya mambo wanayoyafanya watu wasiomjua Mungu.Tit. 1:7 Kiongozi wa Kanisa asiwe mlevi.

Waam. 13:4 Hana anakatazwa kunywa pombe kama alama ya shukrani kwa fadhili aliyopewa na Mungu (Pia 1 Sam. 1:14-15).

Lk. 1:15Yohane Mbatizaji hakunywa divai wala kileo, kama nadhiri yake kwa Mungu.

YBS. 31:25-31 Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inazungumzia kwa ufasaha sana maadili ya pombe.

Matumizi ya kileo hayajitokezi katika Maandiko Matakatifu peke yake, bali yako katika maisha ya kila siku ya mwanadamu.

Hapa kwetu Afrika pombe imekuwa ikitumika kukidhi mahitaji mbalimbali ya watu kama kuweka na kuwaunganisha watu pamoja, burudani kama harusi, mapumziko na starehe.

Nyingine ni kufanya kazi za kijamii kama kilimo na ujenzi, kupatanisha, kuposa na kufariji katika msiba.Pamoja na hayo matumizi mazuri ya pombe, daima kumekuwa na watu wanaoitumia pombe vibaya. Wanakosa kushika kiasi katika unywaji.

Wanashindwa kujiongoza wanapokuwa wamekunywa pombe. Wengine wanakunywa pombe haramu chang’aa (gongo) ambayo ni hatari wa afya zao na jamii kwa ujumla.

Tena kuna wale ambao wakishaonja pombe japo kidogo tu, wanashindwa kujitawala na kutenda mambo kama wendawazimu.

Bila shaka, ni kwa sababu ya matumizi hayo mabaya ya pombe, madhehebu ya dini na vikundi mbalimbali vimejitokeza kulaani matumizi kama hayo.

Lakini, ikumbukwe kuwa ni wajibu wa kila raia mwema kukemea maovu ukiwemo ulevi uliokithiri.

Katika kufanya hivyo tahadhari lazima ichukuliwe; maana kuna tofauti kati ya kunywa pombe na kulewa pombe.

Wale wanaokunywa pombe kwa kiasi na kwa kujali wakati, wasiingizwe kwenye kundi la kukemewa YBS31:28.

Hivi kweli kondomu itumike kudhibiti Ukimwi; kweli?

Na Emil Hagamu wa Pro-Life

KILA mwaka kuelekea mwishoni mwa Desemba dunia inatambua upya ukweli wa janga la UKIMWI

Ripoti ya mwaka 1999 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS), ilitoa takwimu za kutisha kuliko miaka iliyotangulia hasa kuhusu makisio ya balaa hilo katika nchi za Afrika.

Mwishoni mwa Karne ya 20 kulingana na takwimu hizo, watu milioni 26 walikuwa wamekufa kwa UKIMWI. Hiki ni kiwango cha juu mno cha balaa hili kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma, licha ya juhudi nyingi za kupunguza kuenea kwake katika nchi mbalimbali.

Wagonjwa wapya milioni 5.6 wameripotiwa duniani kote mwaka huu. Leo hii duniani watu wazima milioni 32.4 na watoto milioni 1.2 wameambukizwa virusi vya UKIMWI; asilimia 95 ya hao, wanaishi katika nchi maskini.

Takwimu hizi zinashitua hasa tunapoelewa leo hii kuwa UKIMWI unaathiri sana nchi za Afrika kuliko nyingine duniani.

Mkutano wa Lusaka uliofanyika tarehe 12-16 Septemba, 1999, ulitahadharisha juu ya hali mbaya ilivyo.

Kwa kweli asilimia 70 ya watu wenye uambukizo, watu wapatao milioni 23.3 huishi Afrika Kusini mwa Sahara, ingawaje idadi ya watu wake ni asilimia 10 tu, ya watu wote duniani. Wengi wao watakufa katika miaka 10 ijayo.

Asilimia 8 ya watu wazima wanauambukizo (asilimia 0.25 Ulaya ya Magharibi, asilimia 0.13 Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati). Tangu mwanzo wa balaa hili, watu milioni 34, Kusini mwa Sahara wameambukizwa virusi.

Kati yao, milioni 15 wamekwisha kufa(asilimia 83 ya watu waliokufa duniani tangu kuanza kwa balaa hili.)

Mwaka 1998, watu milioni 2.2 walikufa kwa Ukimwi, katika Afrika, Kusini mwa Sahara ukilinganisha na watu 200,000 waliokufa kwa vita. Wastani wa maisha ambao uliongezeka kutoka miaka 44, katika miaka ya 1950 hadi miaka 59 katika miaka ya 1990 utapungua na kuwa miaka 45 ifikapo 2005 na 2010.

Vifo hivi vitawahusu vijana wenye elimu na ujuzi wa taaluma mbalimbali.

Hawa ndio waliokuwa tegemeo. Wengi wao walikuwa wazazi wenye watoto wadogo. Leo hii, wao wamekuwa chanzo cha matatizo, chanzo cha yatima watokanao na UKIMWI. Asilimia 95 ya yatima milioni 11.2 ni Waafrika.Tangu mwanzo, Kanisa limehudumia wagonjwa wa Ukimwi.

Iwapo watu 7 katika kila 10 wanaambukizwa virusi vya Ukimwi, wanaishi Afrika Kusini mwa Sahara, uwiano wa watoto huongezeka kwa 9 katika kila 10. Watoto 570,000 chini ya umri wa miaka 14 wameambukizwa mwaka huu na asilimia 90 walizaliwa na wanamama wenye virusi vya Ukimwi.

Takwimu hizi zinaeleza hali halisi ya janga: UKIMWI ni janga linalomaliza Afrika na kuharibu maendeleo ya baadaye.

Januari 10 mwaka huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kujadili kwa kina tatizo hili na kutamka kuwa "Ukimwi ni janga kubwa linaloathiri uchumi na hali ya siasa barani Afrika, "mgogoro wa kiusalama", kwa maneno ya Makamu wa Rais wa Marekani, A. Gore.

Naye Dk. Peter Piot, Mkurugenzi wa UNAIDS, alisema, "Janga hili limeleta maafa makubwa zaidi kuliko vita".

Kanisa Katoliki halijajitenga na hali hii. Tangu janga hili kuanza, Kanisa Katoliki limetoa huduma na misaada mbalimbali kupitia hospitali zake na vituo vya matibabu na maparokiani kwa huduma zitolewazo na watawa wa kiume na wa kike, mashirika ya misaada kwa wagonjwa na huduma mbalimbali kwa matatizo hayo.

Barani Afrika, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kupigana na Ukimwi. Kwa sababu hiyo, Halmashauri ya Familia ya Kipapa, ilishirikiana na mabaraza ya Maaskofu, imekuwa ikishughulikia mafunzo ya familia na maadili, ikifanya mikutano na madaktari na wauguzi wanaoshughulika na vita dhidi ya Ukimwi. Mikutano mingi ilifanyika barani Afrika, hasa katika nchi zile zilizoathirika zaidi.

Lazima tukumbuke kuwa, ushiriki wa Kanisa Katoliki umekuwa wa wazi na imara. Tutambue mifano mizuri ya kujitoa na ukarimu wa watu wengi tuliowaona huko Uganda, Kenya, Tanzania, Ghana, Cote d Avoire, Benin, Jamuhuri ya Afrika ya Kati na Bukina Faso kwa kuwatembelea wagonjwa majumbani mwao kuwapelekea madawa, chakula na vinjwaji.

Ili kuelewa hali halisi ya UKIMWI katika nchi hizi, tunatakiwa kuwafuatilia wafanyakazi wa kujitolea katika mizunguko yao tukiwaangalia wakiingia katika vijijumba vyenye giza wakiinama kwa huruma kutoa huduma kwa mwanamke anayekaribia kifo akiwa amezungukwa na watoto watatu au wanne ambao kesho yake, hawana chakula chochote.

Yatupasa kuwaheshimu wale watawa wa kike ambao wamejitolea kuwahudumia watoto yatima wakiwapa makazi, chakula, elimu na mafunzo. Wengi wa watawa hawa, wanapata misaada kwa njia ya kuomba wakitegemea misaada kidogo kutoka mashirika, wafadhili na jumuiya inayowazunguka.

Tuwaheshimu pia akina baba na akina mama, wakati mwingine kutoka mabara mengine walioleta matumaini, heshima ya uhai na chakula kwa watu walioathirika na UKIMWI na kukataliwa na kila mmoja kama uchafu.

Hapa, tumemwona Kristo Mteseka, Kristo Mdharauliwa, Mnyanyaswa na Mkataliwa, Kristo Mgonjwa na asiyetembelewa na yeyote, Kristo, afaye kwa njaa na kiu.

Tulitambua lindi la upweke wao na hali ya kukata tamaa, lakini, tulimwona pia Kristo akitembelea wagonjwa akiwafariji wateseka, akiwakumbatia wagonjwa wa Ukimwi na kuwahudumia watoto ambao sasa, wameachwa yatima.

Tukikumbuka nyuso za tabasamu za Waafrika wengi wake na waume waliojitoa kwa dhati katika mapambano dhidi ya janga hili la Ukimwi, tulisikitishwa kusikia matamshi ya watu mbalimbali katika vyombo vya habari yalivyoamsha kilio.

Katika matamshi haya, Kanisa Katoliki lililaumiwa kwa kutojihusisha na janga la Ukimwi barani Afrika.

Maisha na Mikasa

Familia ya Albino yashambuliwa na Kansa

lAsema imemtesa na mkewe kwa miaka sita

lAhofia kula chakula kitokee kwenye kidonda

Na Dalphina Rubyema

"Hapa unapopaona, pataendelea kuchimba mpaka ndani. Patakula koromeo lote. Ninajua itafikia mahali, nitakuwa nikinywa maji au nikila kitu, kitakuwa kinatoka nje kupitia kwenye hili tundu. Ni shimo kubwa usilione hapo,"

Anasema huku akionesha kidonda chake kilichokuwa kimefunikwa kwa plasta.

Kisha anaendelea, "Jua ndilo linatuumiza, si unaona hata hii kansa inavyoniua. Usinione hivi kansa ya ngozi inatutesa sana mimi na mke wangu; tunakufa. Tena huu ni mwaka wa sita."

Jua ndilo linatuumiza, si unaona hata hii kansa inavyoniua. Usinione hivi kansa ya ngozi inatutesa sana mimi na mke wangu; tunakufa. Na huu ni mwaka wa sita ikitutesa namna hii na sasa ninazidi kuchimbika shingo."

Hadi sasa tumeshindwa tufanye nini kwa kuwa hali ndio hiyo, kila siku tunaomba tusaidiwe walau miavuli, lakini ndio hivyo; tunashindwa hata ni lini na tutapata wapi msaada ili tutibiwe hata kwa kuwekewa barafu. Nasikia barafu inaua wadudu wote wa kansa."

Naomba ndugu zangu mtusaidie walau twende kwenye matibabu. Usinione hivi ndugu yangu, ninateseka kweli. Walau niende KCMC kuwekewa barafu, nasikia barafu inaua wadudu wote."

Maneno hayo ya kusikitisha yanatoka kinywani mwa Bw. Nicholaus Lameck (53), mkazi wa Mtoni-Kijichi wilayani Temeke katika mkoa wa Dar-Es-Salaam.

Bw.Lameck ambaye ni albino anasisitiza kuwa, "Niamini ninachokuambia. Ni kweli nimedumu na ugonjwa huu kwa miaka sita sasa." Kisha anaongeza, "Hata mke wangu (Anamtaja kwa jina la Mwanaisha Athumani mwenye umri wa miaka 30). Sasa sijui watoto itakuwaje."

Akielezea hali hiyo kwa undani asili ya kansa hiyo ya ngozi inayo muathiri shingoni na, albino huyo anasema,

"Ilikuwa ni mwaka 1994 nilipotokewa na kiupele kama chunusi hivi. Kilijitokeza katika shingo upande wa kushoto. Kwa kuwa niliwa sifahamu matatizo ambayo nitayapata hapo baadaye, nikaitumbua sijui ni chunusi, sijui ni upele.

Lahaulah Kumbe Mungu wangu hapo nilikuwa nimeharibu; nimetibua kila kitu kwa sababu sasa kile kialama kidogo hakikutaka kufutika wala kufutika tena, badala yake, kalianza kutoa majimaji.

Nilikaa hivyo hivyo kwa karibu wiki moja hivi kidonda na huku hicho sasa kinaanza kuwa kidonda kikubwa ambacho kinasambaa na kufikia ukubwa wa shilingi hivi.

Nikawa nimegundua kwamba sasa huu si upele ila ni ugonjwa. Nikaona nisizidi kuchelewachelewa kupata matibabu. Nilichofanya ni kuwahi sasa hospitali kwa kuwa hata mimi sasa nilianza kuwa na mashaka.

Nikaenda kwenye hii hospitali ya Ocean Road (ipo jijini Dar-Es-Salaam), na huko, wakaanza kunipa dawa ya kukaushia vidonda, wanaiita "yuso". Hatimaye, wakanipa ngozi, pamba na plasta kwa ajili ya kukifunika kidonda changu.

Maana kilikuwa kinatisha na hata huwezi kukiona mara mbili maana kilikuwa kinazidi kuharibika kila kukicha."

Bw. Lameck ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Ustawi wa jamii na Uchumi Tanzania,

hivi karibuni alivililia vyama vya siasa na vikundi vya dini viyanusuru maisha ya albino wa mikoa ya Dar-Es-Salaam na Pwani wapatao 1800 akiwamo yeye mkewe, na watoto dhidi ya ugonjwa wa kansa ya ngozi kwa kuwasaidia miavuli ili kuwakinga na jua.

Aliendelea kusema, "Kama hiyo haitoshi, kidonda kikazidi kupanuka na sasa kikawa kinachimba kuingia ndani. Kule Ocean Road (Hospitali), walipoona hivyo, wakaamua kunitibu kwa kutumia mashine maalum ya kutibu kansa ya ngozi. Mashine hiyo inaitwa "radiesheni thielapizi"

Bw. Lameck anaishi na familia yake yenye mke na watoto wanane. Wanne, ni watoto wake wa kuzaa, na wengine waliobaki, anaishi nao kutokana na wazazi wao kushindwa kuwatunza(wote ni maalbino).

Anasema kuwa, kuna kipindi ugonjwa huo unaoishambulia familia yake, ulitoweka kabisa lakini cha kusikitisha, baada ya miaka miwili, hali ilibadilika tena.

"Baada tu ya miaka miwili yaani mwaka 1996, ugonjwa wangu uliibuka upya tena kwa kasi ya ajabu kwani sasa haukusambaa kama mwanzo ila, ulianza kwa kuchimba kuingia ndani ya shingo," alisema.

Kisha akaongeza, "Hii ilikuwa ni hatari sana hivyo kama kawaida, nikakimbilia tena Ocean Road kuchoma tena hiyo radiesheni. Nikachoma lakini, imeshindika kupona."

"Hadi hivi sasa nimeisha maliza milioni 15, na ukishafikia kiwango hicho hauruhusiwi kuchomwa tena na kifaa hicho kwa kuwa sasa unaweza kupata madhara makubwa mwilini mwako."

Anasema tangu mwaka huo wa 1996, anaendelea kuuguza kidonda chake ambacho alisema kinamnyima raha kutokana na maumivu makali anayoyasikia.

Kibaya zaidi, Bw. Lameck anasema kuwa kidonda hicho kinaendelea kuchimba kwa undani zaidi kwenye koromeo hali ambayo anasema anaona inahatarisha uhai wake.

"Hapa unapopaona, pataendelea kuchimba mpaka ndani. Patakula koromeo lote. Ninajua itafikia mahali, nitakuwa nikinywa maji au nikila kitu, kitakuwa kinatoka nje kupitia kwenye hili tundu. Ni shimo kubwa usilione hapo,"

Anasema huku akionesha kidonda chake kilichokuwa kimefunikwa kwa plasta.

Niliona nisichelewechelewe sana kupata matibabu hivyo nilichofanya ni kwenda hospitali Kama haitoshi Bw. Lameck alifunua kidonda chake ambacho kwa hakika hakitamaniki kurudia kutazama mara mbili.

Kwa mujibu wa mwandishi wetu ambaye alikishudia, kweli endapo ufumbuzi wa haraka hautapatikana juu ya tatizo hilo, maisha yake yako katika hatari na mateso makubwa.

"Unaona hapa jamani kama siyo msaada wa watu nini, nisaidieni jamani ndugu zangu hivi sasa roho yangu imebaki mikononi mwenu," anasema.

Anaongeza, "Nasikia KCMC kuna matibabu tofauti na yale ya Ocean Road, eti badala ya kutumia radiesheni, wanatumia barafu na hapo wadudu wote wanakufa. Sasa mimi huko siwezi kwenda sina uwezo wa kifedha, ndugu zangu Watanzania na watu wengine wote tusaidieni; tunaumia sana na mke wangu," anasema huku akifunika uso kwa viganja vya mikono yake.

Kisha anasimulia hali ilivyo kwa mkewe Bi. Mwanaisha Athumani ambaye pia ni albino.

Anasema, mkewe huyo yeye kansa yake imemshika sehemu ya kwapa na mkono wa kushoto na sasa inachimba kuelekea kuukata mkono huo.

Anasema kuwa naye kaisha chomwa hiyo rediesheni thielapi lakini, pia imeshindikana kupona na kwamba naye anahitaji msaada kama huo anaouomba wa kwenda kutafuta matibabu huko KCMC Moshi.

"Yaani ni hatari sana mimi kansa itanikata shingo ina maana nitakufa, mke wangu itamkata mkono, atapata ulemavu mara mbili. Swali linakuja, akibaki yeye na ulemavu wake wa mkono, yeye na watoto watatunzwa na nani, si watakufa kabla ya siku zao?" alihoji na kuongeza, "Tena wote ni maalbino na jamii inavyo wachukulia maalbino, sijui kama watapata msaada kutoka mahali popote, bora mimi ninapokuwepo naweza kuzunguka huko na huko na kufanikiwa kurudi jioni na kitu kidogo."

Akielezea maisha yake kwa undani Bw. Lameck anasema katika miaka ya nyuma alishawahi kufanya kazi kwenye Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ambapo alikuwa ni Mratibu wa Kitengo cha Utafiti wa Kansa ya Ngozi (skin Canser Reserch) kazi ambapo aliifanyakazi tangu mwaka 1978- 1985.

Baada ya hapo, anasema alijiunga na Chama cha Ustawi wa Jamii na Uchumi Tanzania ambapo hata hivyo anafanya kazi kwa kujitolea bila kulipwa malipo yoyote.

"Mimi siyo mwajiriwa; hivyo sitegemei mshahara, ninaishi kwa huruma na upendo wa watu wanaojua matatizo ya maalbino’ anasema.

Anawataja na kuwashukuru baadhi ya watu hao wanaompa msaada kwa niaba ya wengine pia kuwa ni, Bi. Grace Mnyani ambaye anafanya kazi Ero-Bank, Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Bi. Thelesia Ngaluli, Bi. Singa (NBC 1997) na Bw. Simon Samo anayeishi kwenye nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), eneo la Kariakoo (Breweries).

"Kwa kweli hawa watu wananisaidia sana ndio wanaotuwezesha mimi na familia yangu kuishi hapa mjini na naomba Mungu awazidishie na kuwapa wengine uwezo wa kupata na kusaidia kama wanavyofanya hawa," anasema.

Anasema mbali na hao, mkewe kwa kushirikiana na watoto nao wanasoma katika shule moja ya Jeshi la Wokovu, wanauza maji.

"Wanakinga maji mengi na kuyahifadhi. Hivyo, watu ambao hawataki kwenda bombani wanafika kwetu na kuuziwa maji kulingana na kiasi wanachokihitaji. Isitoshe, wanafanya shughuli mbalimbali na hivyo pesa kidogo inayopatikana, inatufanya tuishi, hivyo hivyo tu," anasema.

Bw. Lameck anaendelea kusema kuwa katika maisha yake, amewahi kumuoa mwanamke mweusi ambaye aliweza kumzalia mtoto wa kiumue mwenye umri wa miaka 20 sasa.

"Mwanangu huyo wa kwanza naye ni mweusi lakini nilikuja kutengena na mama yake hivyo wanaishi wote huko Tabata,"

Hakutaka kufafanua sababu ya kutengana kwao.

Anaendelea, "Baada ya hapo, sikuoa tena ila niliweza kuzaa tena na albino mwenzangu. Huyu, tulifanikiwa kupata mtoto wa kike ambaye naye ni albino, haikuchukua muda mama yake akafariki. Huyu mwanangu mwenye umri wa miaka (15) sasa, anasoma darasa la sita Jeshi la Wokovu."

Anasema mke wake wa sasa amefanikiwa kuzaa naye watoto wanne ambapo kati yao wawili wamefariki kutona na ugonjwa wa "sikoseli" na waliobaki mmoja ni mvulana anayesoma shule ya awali (wote ni maalbino).

"Familia yangu ni kubwa kidogo; kuna watoto wanne ninaoishinao kwa kuwasaidia. Hawa wazazi wao ni weusi hivyo wameshindwa kuwatunza watoto wao. Mimi kwa vile naelewa vizuri matatizo anayoyapata albino, sikuaona sababu ya kukataa kuwasaidia. Pamoja na kwamba sina uwezo, lakini hicho ninachopata tunatumia wote, ni mapenzi ya Mungu," anasema.

Hata hivyo Bw. Lameck alilalamika kwamba ingawa maalbino wanamahitaji zaidi ya watu wengine na akatoa mfano kuwa wanalazimika kuoga na kujipaka mafuta ya kulainisha ngozi mara nne ya mtu wa kawaida, jamii inawatenga katika kuwasaidia kama walemavu wengine.

Maalbino ni walemavu wa ngozi na macho. Wengi wana maisha magumu kutokana na ukweli kuwa hawakusoma sawasawa kwa kuwa hata wawapo shuleni, kutokana na matatizo ya macho, hawawezi kumudu masomo