Make your own free website on Tripod.com

Maisha na Mikasa

MZEE WA FAMILIA ALILIA ULEMAVU AKISEMA:

Nimekatwa miguu yangu yote kuokoa maisha yangu

"NILIKUWA mkakamavu mwenye nguvu kama ulivyo wewe. Toka niko mdogo nimesoma, nimefanya kazi hadi nimestaafu sikuwa na kasoro wala tatizo lolote katika mwili wangu".

"Sikujua kama ingetokea siku moja nijikute niko hivi nilichoshindwa kukifanya wakati ule sitegemei kukiweza tena. Miguu yangu yote imefyekwa kama miti, si hata wewe unaniona.

Sasa nimebakia kiwete, kila kitu ni kuomba msaada, tumaini langu pekee ni Mwenyezi Mungu na wanadamu wenzangu kunisaidia. Wakati ninakatwa nilijua hata huyu mke wangu niliyekuwa ninamtegemea kuwa ndiye angekuwa.

Wa kwanza kunikimbia lakini, mke wangu sitamsahau, aliyonihakikishia wakati wa ndoa yetu ni kweli; amevumilia yote mpaka sasa hivi unaona anavyo nihangaikia.

Naomba hata kama sitakuwapo duniani, Mungu amsaidie katika maisha yake.".

Baada ya kuugua ugonjwa mbaya wa kisukari na hatimaye kansa nayo kumshambulia na kumfanya mguu uoze na hata kukatwa mara kadhaa kidogokidogo hadi kwenye magoti, Mzee Peter Emmanuel Isaka (60), Mkazi wa Buguruni Dar-Es-Salaam,

amesema alipoelezea masaibu yake kwa mwandishi wetu nyumbani kwake hivi karibuni.

"Sikutegemea kuwa mimi mwalimu ambaye pia nilifika chuo kikuu, katika ujana wangu sikutegemea kuwa ipo siku nitapata matatizo kama haya yanifanye sasa nifanyiwe kila kitu kama mtoto mdogo anayenyonya.

Ninasema hivi kwa kuwa hadi ninastaafu kazi, nilipokuwa mkaguzi wa Elimu ya Watu Wazima katika Kanda ya Kaskazini, sikuwa na tatizo lolote.

Sasa, ni mwaka mmoja tu, ulipita baada ya kustaafu ndipo nilihisi kukohoa kohoa. Nikawa nasumbuliwa kidogo na kifua hadi nilipokwenda kupimwa nikaambiwa eti nina kifua kikuu.

Hata hivyo ingawa nilikuwa ninatibiwa vizuri, lakini bado hali yangu ilikuwa inazidi kuwa mbaya. Kifua kilizidi kunisumbua.

Nikashauriwa na rafiki yangu mmoja yeye ni Daktari, kwamba bora niende Hospitali ya Amana Buguruni wanipige X-ray.

Sasa baada ya X-ray, nikaelezwa kwamba pafu langu moja la kushoto lina kitu kama mawingu wingu hivi, nikaanza matibabu palepale kwenye Hospitali ya Amana ambapo nilikazana na matibabu hadi nikapona."

Alipoulizwa kama kabla ya kustaafu kwake alikuwa katika ndoa, alisema, "Ndio nilikuwa na mke lakini huyo tukatofautiana nikaamua kukaa hivyo hivyo ingawa tulikwisha zaa naye watoto watatu."

Akasema na kuwataja watoto hao kuwa ni Rozi (32), Ester (30) na Mary (27)ambao kwa sasa hawapo wametawanyika, "Wamekwisha olewa wametawanyika na siwezi kuwalaumu kwa kuwa nao najua hawana uwezo wowote," akatulia kidogo.

Niliendelea na shughuli zangu kama kawaida huku nikiwa mzima wa afya lakini, baadaye, katika shavu langu la kulia kukatokea vipele vidogo vidogo kama chunusi hivi.

Sasa, nilipotaka kuvitoa, vikaanza kutoa majimaji na kuvimba. Nikaona hili ni tatizo maana kadri siku zilivyozidi kwenda, ndivyo hivyo vipele navyo viliendelea kukua na kuleta uzito mkubwa katika shavu langu la kulia huku pakitoka majimaji meupe kama usaha mpaka nilipokwenda hospitali nikafanyiwa operesheni.

Hospitali wakaniondoa hilo pande la nyama ambalo lilikuwa linazidi kukua. Hapo sasa nikaona ninaanza kuwa katika hali ya kawaida".

"Ugonjwa huo ulinipata mwezi wa Pili hadi mwezi wa 6 mwaka 98," anazidi kusimulia Bw. Peter.

Anasema mwezi wa 8 mwaka huo huo, akapata tena kijeraha kidogo katika kidole gumba cha mguu wa kushoto. Jeraha hilo lilianza kama lenge lenge.

Hata hivyo anasema alielezwa kuwa alikuwa na ugonjwa wa kisukari. Akazuiliwa asiwe anakunywa pombe wala chai yenye sukari jambo analosema alilizingatia ingawa lilikuwa gumu kwake.

Hata hivyo Bw. Peter anasema alishauriwa kufika hospitali mara kwa mara ili kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

"Nilijitahidi kufanya hivyo lakini nilikuwa na majukumu mengi maana sikuwa na kazi tena nilikuwa nikizunguka huku na huko kwa ajili ya maisha ya baadaye.

Anasema baada ya kuona kidole kikizidi kuvimba na kutoa maji maji, alienda kufunga bandeji pale pale katika hospitali ya Amana.

"Kilichonishitua na kuniogopesha, ni siku moja ambayo Daktari huyo huyo aliyekuwa rafiki yangu, aliponiuliza eti ninafikiri kidonda changu kitapona." "Mimi nikamwambia ninatumaini lolote litakalo tokea, ni mapenzi ya mungu. Lakini, nilijua nitapona tu.

Basi, ndipo akasema, nenda katika chumba cha matibabu ya kisukari nilipopimwa nikaambwa tayari sukari ilikuwa imeongezeka eti toka kiwango cha 26 hadi 29.

Halafu, akaniambia eti hiki kidonda, hakitaweza kupona, nikatakiwa nilazwe.

Mguu ulianza kuvimba zaidi na sasa kwa mara ya kwanza, ikabidi waanze kunikata kidole lakini, bado hali ikazidi kuwa mbaya. ikabidi mguu ukatwe katikati ya kisigino. Wakati huo hali niliyokuwa nayo, usiseme. Nilikuwa ninashuhudia kabisa mauti yanavyoninyemelea.

Bw. Peter anasema wakati wanamkata mguu, tayari kisukari kilikwisha mzidi pale walipolenga,

"Nilishuhudia mara nyingine mguu wangu ukipunguzwa kama mti juu ya goti nikakaa hospitali kwa wiki mbili zaidi halafu nikaruhusiwa kurudi nyumbani".

Kwa kweli hapa kweli mwanangu (mwandishi) ndipo nilipoanza kuona maisha mapya yenye uchungu maana sikuzoea hali ya kutembea na mguu mmoja.

Nikaanza kuhangaika huku na huko ili walau nipate mguu bandia maana kutuimia mguu mmoja, nilikuwa naumia kweli kwa kuwa sikuzoea hivyo.

Nikaenda hadi Muhimbili. Huko nikaambiwa mguu wangu wa bandia, ni shilingi laki tatu na ishirini.

Sikuwa na uwezo wowote wa kununua huo mguu nikarudi zangu nyumbani. Sasa nifanye nini pesa sina, nao wanataka hela.

Sasa siku nyingine wakati nasikiliza redio, nikasikia tangazo kuwa hawa "Rottery Club" wanatoa huduma ya viungo bandia kama mikono na hii miguu."

"Ilikuwa tarehe 29 mwezi wa 3 mwaka wa jana.

Nikasema Mmh! Ngoja na mimi niende kujiandikisha."

Mzee Peter ambaye alikuwa anazungumza pamoja na mkewe Bi. Emma (34)kwa kuwa Peter mwenyewe baadhi ya mambo amekuwa na kawaida ya kuyasahau, akasema aliambiwa angojee maana miguu ilikuwa ikitengenezwa huko Nairobi Kenya na ile iliyokuwapo awali iligawanywa kwa wengine ikaisha."

Bi. Emma ambaye ndiye mke wake wa ndoa na tegemeo pekee la Mzee Peter, katika maisha yake aliolewa na mzee huyo miaka 9 iliyopita na wamefanikiwa kuwapata watoto wawili Emmanuel(8) na Paul (6).

Mama huyo anasema alifuatilia hadi mwezi Septemba na Novemba mpaka alipoelezwa kuwa hakukuwa na uwezekano wa kuipata hadi awasiliane na wakubwa wa kitengo hicho ambao walikuwa Nairobi.

Nilijitahidi kufuatilia hadi Januari mwaka 2000 nikaambiwa mguu wetu ulikuwa tayari umetengenezwa lakini ilikuwa si rahisi kuupata kwa vile walikuwa katika mapumziko ya sikukuu.

"Ilikuwa mwezi wa 3 ndipo tukapata mguu huo wa bandia; nilifurahi nikawa ninafanya mazoezi lakini furaha yangu haikudumu", anasema Mzee Peter.

Ilionekana mguu huo bandia ulikuwa mzito mno maana nilianza tena kuvimba mguu wangu pekee uliobaki nikaamua kutoutumia huo mguu wa bandia. Uvimbe uliongezeka hadi nilipofika hospitali ya Muhimbili mnamo tarehe 19mwezi wa 5, nikalazwa kipindi cha wiki moja nao pia wakaukata.

Hakukuwa na jinsi maana walipopima kisukari ilikuwa imepanda kupita kiasi. Sina kumbukumbu vizuri lakini ilikuwa jumamosi ya tarehe 27/5 ndipo mguu wangu wa pili ulikatwa.

Roho iliniuma zaidi maana swala la kutembea au kusimama halikuwepo tena, nilikuwa na kawaida ya kukata tamaa baada ya kuona hali imeniwia hivi

Bahati nzuri, padre mmoja wa Muhimbili alikuja akanipa ushauri mzuri nikaona hakuna haja ya kukata tamaa nikavumilia yote.

Mguu wangu wa pili ulikatiwa chini ya goti nikawa na imani kwamba labda nitautumia mambo bado yalikuwa magumu kwa kuwa sasa hakukuwa na unafuu, shida ni shida tu maana nilikuwa nategemea faraja za Mwenyezi Mungu na wala sielewi kama watanikata tena ama vipi.

Mama huyo ambaye kwa sasa ndiye tegemeo pekee la familia hiyo, akasema mzigo mkubwa unamwelemea maana hakuna msaada wowote anaoupata kutoka nje ya familia hiyo anayoishikilia.

"mwanangu nina shida kweli maana hivi unavyoniona, ninategemea kuuza maandazi ili kupata cha kuhemea kwa siku.

Bibi huyo anasema hali hiyo tayari imemfanya mtoto wake wa mwisho, Paul aache masomo kwa ajili ya familia kushindwa kumudu gharama.

"Mwanangu Paul, alikuwa anasoma vidudu sasa ameacha hatuna hela ya kumsomesha sasa ni kaka yake, Emmanuel, mwenyewe ndiye anasoma darasa la pili huko Arusha baada ya kuchukuliwa na ndugu".

Mama huyo anasema pamoja na mme wake kukumbwa na matatizo hayo ya kukatwa miguu, bado anampenda na ataendelea kumhudumia kila atakapohitaji msaada wake mpaka kifo kitakapowatenganisha.

"Nimefunga naye ndoa, tumefanikiwa kupata watoto, maisha ya raha tumepitia huu ni wakati wa shida; siwezi kumwacha mme wangu bado nampenda. hata kama nikisema niondoke unafikiri atakuwa mgeni wa nani, sipo tayari kumsaliti mme wangu" anasema mama Paul (Bi. Emma).

Mzee Peter ambaye ni mzaliwa wa Dodoma wilaya ya Kondoa kijiji cha Haubi Mtoto wa nne katika familia ya mzee Emmanuel Kilnoro, anasema hajasahau mchango mkubwa aliotoa katika taifa hili baada ya kumaliza masomo yake ya ualimu huko Morogoro mwaka 63 na anazitaja baadhi ya sehemu alizopata kulitumikia taifa.

"Nilipangiwa kazi Mtwara miaka miwili ya majaribio nikahamishiwa Kitangali huko Newala. Mwaka 67 nikarudi Dar-Es-Salaam, nikafundisha shule za (TAPA) wakati huo, nilihamishiwa Buguruni mwaka 68 hadi mwaka 70 nikateuliwa kuwa mwalimu Mkuu.

Mwaka 72 nikabadilishwa nikawa Afisa Elimu wa Wilaya ya Mzizima baadaye ilivunjwa zikaundwa wilaya 3 ambazo ni Ilala, Temeke na Kinondoni.

Mwaka 77, nilienda kusoma elimu ya juu hapo Mlimani (Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam).

Mwaka 78, nikapangiwa kazi huko Mafia - Rufiji kwa vile yalifanyika mabadiliko ya wakaguzi nikachukuliwa kusoma kozi ya miezi 3 huko Bagamoyo.

Nilipomaliza, nikapelekwa Kanda ya Kaskazini kama Mkaguzi Mkuu wa Elimu ya Watu Wazima."

Anaendelea kusema kuwa Mwaka 1982, alirudi Kanda ya Mashariki kama Mkaguzi hadi mwaka 1995 alipoamua kustaafu kazi.

Mzee Peter anasema ingawa ameitumikia Serikali kwa muda mrefu hakuna msaada wowote anaoupata zaidi ya malipo ya Pensheni ya uzeeni,

"Ni kiasi kidogo mno hakiwezi kukidhi mahitaji yangu," anasema.

"Nawashukuru sana hawa watu wa shirika la misaada la CARITAS wamenipa msaada mkubwa mimi na mke wangu kwa kuwa hii baiskeli ya kusukuma (wheel chair) waliyonipa, inatusaidia sana na imetupunguzia kazi."

Alisema na kuongeza kuwa toka alipopata matatizo hakuna mtu wala shirika lililompa msaada kama huo zaidi ya (Rottery Club) ambao nao walimsaidia sana kwa kumpa mguu bandia ingawa sasa hautumii kwa kuwa miguu yote sasa imekatwa.

"Ningekuwa na uwezo ningekuwa napitapita maofisini hata huko Serikalini kuomba msaada lakini, siwezi kutembea ni mtu wa kubebwa mgongoni kama mtoto na uwezo wa kukodi gari sina."

Mzee Peter anasema bado hawezi kumsahau padre Benedict wa Parokia Katoliki ya Msimbazi katika Jimbo Kuu katoliki la Dar-Es-Salaam, ambaye amempa msaada mkubwa wa kiroho.

"Padre huyo amenisaidia sana anafika mara kwa mara kututembelea. Kwa kweli amenifariji mno" alisema na kuongeza,

Mzee huyo na familia yake yote kutokana na namna wanavyohangaika, anaomba vikundi vya dini na ndugu wengine wenye mapenzi mema kwa wenzao wenye masumbuko, wawasaidie kwa uwezo wao unavyowaruhusu kwa kuwa kutoa ni moyo na wala siyo utajiri.