Hakuna demokrasia ya kutosha katika kumtangaza mshindi wa kiti cha Rais

Na Arnold Victor

Madai kwamba Tume ya Uchaguzi tuliyo nayo inapaswa iwe na wawakilishi kutoka katika vyama vya siasa, taasisi za kijamii na za dini nayo si mageni hapa nchini, lakini mara zote yalipojitokeza yamekuwa yakipuuzwa, ingawa hakuna hoja ya kueleweka inayotolewa na watawala.

KWA mujibu wa Sheria za Uchaguzi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Tume ya Uchaguzi ikishamtangaza mshindi katika kiti cha Urais, hakuna mtu au chombo chochote kiwe Bunge au Mahakama kinachoweza kuhoji endapo tangazo hilo la Tume lina kasoro. Wakati mwananchi hapewi nafasi ya kuhoji matokeo ya kiti cha Urais, Tume yenyewe ya Uchaguzi huundwa na Rais ambaye anaweza kuwa mmoja wa wagombea au chama chake kinaweza kuwa kinagombea.

Mara zote ninapotafakari mazingira kama haya, nakutana na maswali yasiyojibika. Hivi ni kwa njia gani tume niliyoiteua mwenyewe na ambayo hata ikishanitangaza kuwa Rais haihojiwi inaweza kumtangaza mpinzani wangu kuwa ameshinda? Tume hiyo itakuwa ina wasiwasi gani wakati mtu yeyote itakayeleta kelele baada ya kunitangaza hata kama nimeshindwa ataitwa mhaini na nguvu za dola zitatumika kumdhibiti?

Mimi si wa kwanza kuhoji Sheria hii, watu wengi tu wakiwemo wataalamu wa ndani na wa nje wamekuwa wakihoji na wanaotetea kuendelea kwa Sheria hiyo wanasema ni nzuri kwa vile inaondoa uwezekano wa kurudia Uchaguzi wa Rais ambao ni gharama kubwa mno kuuendesha. Wanaosema hivi bila shaka wanasema kwamba ni heri kuwa na Rais aliyeshinda kwa mizengwe kuliko Rais halali aliyepatikana kwa gharama kubwa.

Lakini kwa mtazamo wangu, ni gharama zaidi kutoa mwanya kwa kiongozi, hasa nyeti kama Rais kuingia madarakani kinyume cha matakwa ya wananchi kuliko kutumia kile kidogo tulicho nacho kuijenga nchi juu ya misingi ya haki ambayo daima ni mzazi wa amani.

Wanaotetea Sheria hiyo pia wanadai kuwa zipo nchi nyingi duniani ambazo matokeo ya Urais hayahojiwi, lakini wanakwepa kusema ukweli kwamba mifumo na miundo ya Tume zao za Uchaguzi na utaratibu wa kutangaza matokeo ni tofauti na huu wa kwetu. Vile vile wanakwepa kueleza ukweli kwamba nchi nyingi zinaruhusu wananchi kwenda mahakamani endapo hawakuridhishwa na matokeo ya Uchaguzi wa Rais na miongoni mwa nchi hizo (kuwataja wachache tena hapa hapa karibu) ni majirani zetu wa Kenya, Uganda na kadhalika.

Katika nchi kadhaa duniani ambapo matokeo ya kiti cha Urais hayahojiwi, Tume ya Uchaguzi huwa ya mseto na huru na matokeo yenyewe hutangazwa na Mahakama Kuu baada ya uchambuzi wa kina. Madai kwamba Tume ya Uchaguzi tuliyo nayo inapaswa iwe na wawakilishi kutoka katika vyama vya siasa, taasisi za kijamii na za dini nayo si mageni hapa nchini, lakini mara zote yalipojitokeza yamekuwa yakipuuzwa, ingawa hakuna hoja ya kueleweka inayotolewa na watawala. Lakini bado ukweli unabaki pale pale kwamba katika mashindano yoyote suala la washindani kuridhika kwanza na sheria na utaratibu wa mchezo kabla ya kuingia kwenye mchezo wenyewe ndio msingi mkuu wa kukubali matokeo pale mmoja anaposhindwa.

Pia utamaduni wa kuwaruhusu wananchi kuwa na mahali pa kukataa rufaa wanapohisi kwamba hawakutendewa haki ni wa muhimu mno kwani kumwacha mtu na hali ya kuhisi amedhulumiwa huku akiwa hana njia yoyote ya kumpata mtu mwingine asiyefungamana na upande wowote kuhukumu, mara nyingi huzaa matumizi ya nguvu kudai kile anachodhani ni haki yake au kuchochea uhalifu wa aina nyingine kama njia ya kupumulia hasira na uchungu wake.

Ninachoamini ni kwamba huenda hata ghasia zilizozuka mjini Zanzibar juma lililopita wakati wa kusikilizwa kwa mara ya kwanza baada ya watuhumiwa wa uhaini kukaa kizuizini kwa zaidi ya miaka miwili ni matunda yatokanayo na watawala kutumia madaraka yao kupuuza sheria. Ni lazima tujiulize kwanini wananchi hawakufanya ghasia wakati wana-CUF hao walipokamatwa miaka miwili iliyopita? Je, tunawezaje kukwepa hisia kwamba baada ya Serikali ya Zanzibar kuwanyima haki ya kujitetea mahakamani Wana-CUF hao kwa miaka miwili, wananchi wameanza kupungukiwa na imani kwamba serikali yao inaheshimu sheria?

Hivi nchi hii itamlaumu nani siku itakapoingia katika ghasia zisizowezekana kudhibiti kwa sababu tulizozijenga wenyewe kwa kuondoa haki ya wananchi kuchagua utaratibu wa wazi zaidi na unaowapa uhuru wa kuamua jinsi ya kuendesha nchi yao? Nasikitika kwamba tunapoelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, katika miswada inayopelekwa Bungeni hivi karibuni hakuna wenye lengo la kuirekebisha Tume ya Uchaguzi iwe ya Wananchi zaidi (ya mseto) kuliko ilivyo sasa na au kuwekwa utaratibu wa wananchi kulalamikia matokeo ya Urais pale ambapo hawakuridhika, kwa nia ya kujihakikishia usalama na amani ya nchi sasa na siku zijazo. Namalizia kwa kusema nina mashaka kama Uchaguzi wa Rais unaweza kuitwa wa Kidemkrasia bila kasoro za Tume na Sheria ya Uchaguzi kuondolewa.

Uhusiano baina ya kicheko cha mtoto na ukuaji wa akili

Afya ya mtoto hujengwa tangu anapokuwa katika hali ya mimba. Katika mfululizo wa makala kutoka kitabu cha " Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo" cha Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni la Beijing, China baada ya kuwaletea umuhimu wa mtoto kutambaa mapema, leo tunaendelea na kuona uhusiano baina ya kicheko cha mtoto mchanga na ukuaji wa akili.

KWA mujibu wa uchunguzi wa kisaikolojia imegunduliwa kwamba kutokana na kicheko cha mtoto mchanga tunaweza kujua kiwango cha uwezo wa akili yake pamoja na matendo mbalimbali ya kisaikolojia yasiyoweza kuonyeshwa kwa lugha. Kwa kawaida akili ya mtoto anayependa kucheka ni nyingi kuliko ya mtoto asiyependa kucheka.

Mtoto anajua kucheka kwa sababu amefahamu kiini cha jambo la kuchekesha kinyume na mtoto asiyecheka ambaye huwa na moyo mzito na majonzi na hivyo kumfanya asiweze kupata ukuaji mzuri wa akili.

Majaribio yanaonyesha kwamba mtoto baada ya kuzaliwa kwa saa 12 anaweza kutabasamu iwapo akipata kunusa harufu ya ndizi na chakula kitamu, hii ni tabia ya ung'amuzi ya silika na inaonyesha kwamba mfumo wa neva wa mtoto huyo unaanza kufanya kazi.

Lakini kicheko chenye maana ni jambo gumu kwani kitatokea baada ya miezi kadhaa iwapo mtoto huyo atasikia sauti tamu basi atatabasamu.

Tabasamu na kicheko cha sauti kubwa hutokea kwa kuonyesha hisia fulani. Katika kipindi hichi mchezo wa "Kujificha" unaweza kuonyesha kiwango cha uwezo wa akili cha mtoto mchanga.

Baada ya mzazi kujificha kwa muda anapotokea mbele ya mtoto mchanga, mtoto huyo atacheka kwa furaha.

Kicheko hiki kinaonyesha utabiri wa mtoto kwa maendeleo ya mambo.

Mtoto mwenye umri wa miaka 2 hivi akiona jambo la ajabu atacheka.

Kwa mfano soksi ikivaliwa katika miguu haoni kichekesho, lakini kama soksi inaanguka katika sikio ataangua kicheko kikubwa, kwa kuwa anaona kitendo hicho ni cha ajabu.

Pengine kicheko cha mtoto mchanga kinaonyesha usalama wake.

Kwa mfano wazazi wanamshika mtoto mchanga na kumwinua juu, mtoto mchanga atacheka, ingawa kitendo hichi ni cha hatari, lakini anacheka tu kwa kuwa anaona usalama upo chini ya ulinzi wa wazazi wake. kama mgeni fulani anamwinua juu ataona hofu sana na hata kuweza kulia kwa makelele, kwa kuwa hana uhakika na usalama wake.

Wazazi si kama wanaangalia watoto katika chakula na mavazi, bali pia inawabidi kuangalia maendeleo ya akili.

Toleo lijalo tutangalia jinsi ya kumwongoa mtoto mchokozi.

 

Wafahamu mahali ilipotoka mimea ya magugu maji?

lYanahatarisha usalama wa viumbe ziwa Viktoria

Na Mwandishi Wetu

MAGUGU maji mmea mashuhuri kwa lugha kimombo kama Water Hycinth hivi sasa yamesambaa na kuwa tishio kwa usalama wa viumbe na shughuli za kiuchumi kama uvuvi na usafirishaji katika ziwa Victoria. Je nini asili ya mmea huu wa ajabu? ulifikaje hapa Tanzania na ulitokea wapi?

Magugu Maji kwa mara ya kwanza nchini Tanzania yalionekana katika mto Pangani huko Tanga, katika mwaka 1955. kwa wakati huo yalikuwa ni machache na hakuna aliyetarajia kuwa yangeliweza kusambaa na kuwa yangeleweza kusambaa na kufikia hatua yaliyofikia sasa hivi ambavyo sasa ni madhara makubwa.

Asili ya magugu maji hasa ni nchi za America ya Kusini ambako ndiko mmea huu wenye maua ya kuvutia humea kwa wingi. Huko kuonekana mmea huu sio jambo la ajabu tena.

Kunako mwaka 1993 Magugu Maji yalionekana katika Mto Kagera na kipindi kifupi toka yalipoonekana katika mto huo, yakaanza kusamba kwa kasi kwenye ziwa Victoria.

Mpaka sasa wataalamu wanajihoji maswali, magugu maji asili yake ni Amerika ya Kusini yalifikaje Afrika Kusini yakafika hapa Afrika Mashariki na kusambaa kwa kasi yaliyonayo sasa hivi?

Baadhi ya wataalamu wa historia wanasema kuwa mimea hii ya magugu maji kwa vile inavutia macho hasa kwa maua yake mazuri inawezekana yaliletwa na wageni waliofika nchini kwetu toka mataifa ya wazungu lakini wao waliyaleta kama maua na mapambo, siyo kwa lengo la kuyasambaza kiasi cha kuleta hasara kama ilivyo sasa.

Tetesi hii inaweza kuwa na ukweli ndani yake kwa sababu katika mwaka 1889, Wajerumani waliweza kuleta zao la mimea aina ya Derema huko Tanga.

Ambapo walianzisha kituo cha utafiti ambacho pamoja na kutafiti ukuzaji wa mimea ya aina mbalimbali pia ilikazia zaidi ustawishaji wa mmea wa Derema .

Mmea huo hatimaye baada ya Wakoloni wa Kijerumani kuondoka uliweza kusambaa sehemu mbalimbali nchini.

Hapa nchini Magugu maji mbali ya kuonekana ziwa Victoria pia yameanza kusambaa kwenye mabwawa na mito mbalimbali, Magugu haya huathiri sehemu za kuzalia samaki, fukwe zinazotumiwa na wavuvi , huua samaki na kukwamisha usafiri.

Tayari kimeanzishwa kituo cha kupambana na magugu haya huko Mwanza.

Kituo hiki kinatumia wadudu waliotolewa Afrika Magharibi ambao hawatumii chakula cha nyingine isipokuwa magugu maji tu.

Magugu maji pia yanafaida kwani kuweza kutumika kama chakula cha mifugo, chanzo cha gesi na malighafi ya kutengeneza karatasi hata hivyo faida ya mmea huu ni ndogo ikilinganishwa na hasara yake.

Mtakatifu Mose wa Ethiophia

lAlikamatwa na kuuzwa utumwani Misri

KAMWE Mose hakuisahau ile amri ya Mungu isemayo, "Msihukumu ili nanyi msije kuhukumiwa" akaongeza, " Nimekuja na dhambi zangu zinanitoka nanyi mnaniambia nimhukumu mwenzangu?!" aliuliza kwa mshangao.

Mose alizaliwa nchini Ethiophia katika karne ya nne.

Wakati wa Utoto wake alikumbwa na balaa la kukamatwa; akauzwa kama mtumwa nchini Misri.

Huko utumwani Mose alipewa cheo na kuwa mtu mkubwa na mwenye nguvu nyingi.

Baada ya kutawaliwa na tamaa ya wizi na hatimaye kugundulika, bwana wake alimfukuza , sasa Mose akawa kiongozi wa makundi ya watu wabaya wakiwemo vibaka na wezi waliotishia usalama wa maisha ya watu vijijini.

Kimsingi, haijaeleweka ni jinsi gani ilitokea hata Mose nae akaongoka japo tunaelezwa tu , kwamba alikwenda kukaa katika Monasteri ya Petro katika jangwa la Skete nchini Misri.

ilitokea siku moja Mose akashambuliwa na wezi wanne. kwa mujibu wa maelezo yanayopatikana ,Mose alifaulu kuwashinda wote.

Akawakamata na kuwafunga kwa kamba na kisha akawapelekea Kanisani akisema, "sina ruhusa; basi nitafanyaje na wajinga hawa?!"

Hakuwa anajua aamue kuwafanya nini wadhalimu hao waliotaka kumdhulumu uhai na mali zake.

lakini je, angefanya nini hali sheria haimruhusu? Basi akaamua kuwaachilia huru majambazi wale ambao inasaidikiwa kuwa baadaye nao waliongoka na kuwa Wamonaki.

Mose ambaye hukumbukwa kila Oktoba 22 ya mwaka pamoja na Mwenyeheri Yosefina Lemu aliyezaliwa huko Kambre Ufaransa mwaka 1747 na kuweka nadhiri za utawa katika shirika la Masista Fukara la Mtakatifu Klara mwaka 1770, hakugeuka ghafla kuwa mtakatifu.

Kuna kipindi kilifika, Mose akakata tamaa kabisa alipojiona kuwa hawezi kamwe kuishinda hasira yake iliyokuwa kali kiasi cha kutisha namna ile.

Akamuendea Mtakatifu Isdori, aliyekuwa abate wa Monasteri ya Pelusio ya huko Misri ambaye tangu ujana wake alikuwa Mmonaki.

Siku hiyo abate alimtangulia Mose; akamchukua hadi juu ya monasteri. Huo ulikuwa wakati ule wa machweo ya jua.

Abate Isdori akaangalia Mashariki; akasema ' Tazama polepole tu, giza linaufanyia mwanga nafasi, Basi na ndivyo ilivyo pia rohoni mwetu'

Maneno hayo ya abate yaliyomaanisha kuwa Mose asikate tamaa maana giza la dhambi lililotanda moyoni mwake litaondoka lenyewe taratibu na kuipisha neema ya Mungu,

yakaeleweka sawia na kumuingia vyema. Akairudia tena kazi yake nzito ya huduma na sala hali Mungu akimrekebisha sana na hata Askofu wa Aleksandria aliposikia habari za utakatifu wake, akaamua kumpadirisha.

Mose akajulikana mahali pengi kutokana na wema wake.

Siku moja wakati wa Kwaresma, Mose aliyeuawa na majambazi wa Kiarabu katika mwaka 405 akiwa mzee, aliwakaribisha wageni waliokuwa wakiona njaa kwelikweli ingawa wakati ule hasa katika Monasteri amri ya kufunga Chakula ilikuwa kali kwelikweli, lakini Mose alianza kuwapikia wageni wake.

Wamonaki wenzake walipogundua alichokuwa anakifanya Mose wakamkasirikia na kumjia juu wakisema 'Mose anavunja Sheria; itabidi baadaye tumkaripie sana kwa kosa hili'

Lakini kwa nguvu za Baba wa Mbinguni wao wenyewe walikuja badili nia yao wakikiri na kukubali ukweli kuwa ingawa Mose alikuwa anavunja sheria ya wanadamu lakini pia alikuwa anatimiza mapenzi ya Mungu.

Siku nyingine Mose aliyeacha nyumba yao ikiwa na wafuasi Sabini waliodumu katika sala na utakatifu wa maisha, aliitwa katika mkutano wa Wamonaki ili wamhukumu mmoja wao aliyekuwa ametenda dhambi kubwa.

Mose alikwenda Shingo upande akiwa amebeba pakacha lililojaa mchanga uliokuwa ukivuja taratibu; ndipo aliposema 'Nimekuja na dhambi zangu zinanitoka, nanyi mnaniambia nimhukumu mwenzangu' akasena na kuongeza 'Msihukumu ili nanyi msije kuhukumiwa'

Nchi iliyopata kuwa na mgodi wa nyama

lWatu walichimba usiku kucha

lNi kwa kuzidi kete Serikali

KAMA inavyojulikana na ilivyozoeleka, mgodi huwa ni sehemu ambako madini ya aina fulani yapo na huchimbwa .

Madini hayo hutofautiana kwa ubora, bei yake matumizi na hata mwonekano wake.

Ni jambo la kushangaza kusikia nyama inaweza kuchimbwa Ardhini kiasi cha kufikia hatua ya kufunguliwa migodi rasmi. Hii ni kwa sababu hata kibaiolojia nyama ipo kwa viumbe hai vinavyotembea tu. Udongo na miamba na hata elimu ya Geology inayohusiana na miamba na madini haiusiani kabisa na nyama.

Sasa basi kama ni hivyo je machimbo ya nyama yalikuwepo hapa duniani? Mwaka 1988, Zambia katika mkoa wake wa Copper belt ilikabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.

Ukame ulitokea na mahindi hayakutoa mavuno mazuri.

Kulingana na hali ya chakula jimboni humo ilivyokuwa mbaya, Serikali ya nchi hiyo chini ya aliyekuwa rais wa wakati huo Mzee Kenneth Kaunda iliomba msaada wa chakula kutoka kwa nchi wahisani na Marafiki.

Nchi ya Australia ilijitolea kuipatia Zambia msaada wa nyama za kusindikwa kwenye makopo kufuatia kilio hicho cha Zambia.

Hapo ndipo jambo lilipozua jambo nyama zile zilisafirishwa vizuri mpaka bandari ya Dar es Salaam ambako sasa zilichukuliwa na Malori makubwa kupelekwa nchini Zambia.

Lakini zilipofikishwa Lusaka, Mkemia Mkuu wa Serikali ya nchi hiyo alizipima na kugundua kuwa zilikuwa na walakini. Muda wa nyama hizo kutumika kama chakula ulikuwa umeishapita.

Sasa Serikali ya Zambia ingefanya nini? izirejeshe Australia? chakula cha msaada? wahisani wasingekaa wawaelewe asilani.

Kilichofanyika, iliundwa tume ya dharura ya kushughulikia operesheni ya kuhakikisha zile nyama zinazoharibiwa ama kutupwa pahala ambako hazitapatikana kwa urahisi tena.

Hivyo maafikiano yalifikiwa kuwa mashimo makubwa yachimbwe na matingatinga jimboni Copper Belt na nyama hiyo ifukiwe humo.

Sehemu zilizokwishafikia nyama zilikandikwa kwa kokoto na saruji. Lakini hiyo haikuvunja azma ya wakazi wa jimbo hilo wenye njaa kufungua mgodi wa nyama.

Ghafla watu kutoka vijiji vya mbali walihamia kijiji ambacho nyama hizo zilifukiwa na kuanza kuchimba kwa juhudi na maarifa. mkebe mmoja wa nyama, hapo mgodini uliuzwa Kwacha 300.

Wachimba nyama walifanya kazi nzito ya kupasua tabaka la saruji na kokoto usiku kucha ili kuweza kuifikia nyama iliyokuwa chini. Matokeo yake wanavijiji toka eneo linalozunguka mgodi wa nyama walipata ahueni. Baadhi yao walinunua pikipiki,magari,na hata kufungua duka na kujenga nyumba kwa fedha toka mgodi wa nyama.

Lakini habari ilipoifikia serikali, dola iliamua kutuma wanajeshi wenye silaha kwenda kulinda mgodi wa nyama usichimbwe na walafi mpaka hapo nyama zitakapooza kabisa.

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

AUM SHRIMKYO: Dhehebu linalofanya ugaidi

VIONGOZI wa dini mara nyingi wanatarajiwa kuwa taa, dira na mfano kwa waumini wao wanaowaongoza.

Na viongozi hao wa dini wanapotokea kuwa vinara wa matendo ya uhalifu hupelekea jamii kuishindwa kuwaelewa.

Moja ya madhehebu duniani yaliyojitokeza waziwazi kujishughulisha na ugaidi na uhalifu ni madhehebu ya kishetani ya " Aum Shrinkyo" yenye asili ya Japan.

Madhehebu hayo ambayo yameibuka huko Japan mwanzoni mwa miaka ya 1980 yanaongozwa na Mjapani anayejulikana kwa jina la Shoko Asahara ambaye mpaka sasa anatuhumiwa kuhusika na hujuma mbalimbali nchini Japan hususan katika jiji laTokyo.

Alama za ibada zinazotumiwa na madhehebu ya Aum Shrikyo ni pamoja na jua, jambia, mwezi, nyoka na mnyama aina ya Dragon.

Utafiti uliofanyika huko Japan umegundua kuwa alama hizo pia hutumiwa na waabudu shetani walio wengi nchini humo.

Mwaka 1995 Shoko Asahara alikamatwa wakati wafuasi wake walipofyetua hewa yenye sumu ndani ya njia za treni inayosafiri chini ya ardhi katika jiji la Tokyo.

Katika tukio hilo watu wanane walikufa papo hapo baada ya kuvuta hewa hiyo na mamia wengi walioathirika walilazwa hospitalini.

Sheria za madhehebu ya Aum Shrinkyo inasema kuwa muumini ni lazima atoe sehemu ya fedha zake na mali zake kama sadaka na kafara kwa Shoko Asahara kiongozi mkuu wa dhehebu hilo.

Sadaka hiyo anayopewa Shoko Asahara imepelekea kuwa mmojawapo kati ya watu matajiri sana nchini Japan, huku akimiliki pia viwanda.

Aum Shrinkyo pia wana kikosi chao maalum cha jeshi ambacho kimejifunza matumizi ya silaha za aina zote ya mbinu za kujihami kwa mapambano ya mkono katika Judo, Karate,Taekwondo na Kungfu.

Askari wa dhehebu la Aum Shrinkyo ambao wengi wao ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 15- 30 wanatumiwa na kiongozi wa dhehebu hilo Shoko, katika kutekeleza hujuma zake sehemu mbalimbali nchini Japan.

Asahara pia anatuhumiwa kuwa na mahusiano ya karibu na genge la majambazi waliopata kuitikisa Japan kwa uhalifu 'Yakuza Gang'. kufuatia hali hiyo Serikali ya Japan sasa imeelekeza jicho lake sana kwa kiongozi huyo wa dini yenye kila dalili za Ugaidi.

Aum Shrinkyo pia huabudu kwa kutoa kafara ikibidi hata ya kuua. wakiwa na imani kuwa shetani anapokunywa damu waliyoitoa sala zao zinakuwa zimesikika.

Kwa mujibu wa magazeti ya Straighr Times ya Singapore na Asahi Shimbun ya Japan wapo zaidi ya waumini millioni 1 wa dhehebu hilo katika visiwa vyote vya Japan Honshu, Kyushu na Hokkaido.

Aum Shrinkyo pia imeanza kujipenyeza miongoni mwa Wajapani waishio Marekani.