Uamuzi wa Serikali kuzitoza kodi taasisi za dini ni wa hamaki

Na Arnold Victor Msuya

HIVI karibuni Waziri wa Fedha, Bw. Daniel Yona, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzitoza kodi taasisi zote za dini na mashirika ya hiyari (Charitable organisations) zinapoaingiza nchini mali yoyote isipokuwa zile tu zinazohusiana na uendeshaji wa ibada, shule na hospitali.

Uamuzi au hatua hiyo ya Waziri wa Fedha vimekuja miezi mitatu tu baada ya Rais Benjamin Mkapa kutamka kuwa Serikali yake itaendelea kutoa msamaha wa kodi kwa taasisi za dini licha ya kuwepo watu wasiopenda hatua hiyo.

Rais ambaye alikuwa akiongea katika Mkutano Mkuu wa BAKWATA mjini Dodoma Agosti, mwaka jana, akasisitiza kwamba pamoja na kwamba Serikali imekuwa ikikosa kiasi kikubwa cha mapato ya kodi kutokana na misamaha hiyo, atahakikisha inaendelea kutolewa kwani mchango wa taasisi za dini katika maendeleo ya jamii ni mkubwa.

Taarifa ambazo naweza kuziita sababu zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato hadi sasa ni kwamba kumekuwa na matapeli ambao wamekuwa wakitumia mwanya wa misamaha hiyo kujinufaisha kibinafsi.

Hilo bila shaka halina ubishi.

Lakini naamini Serikali ilichopaswa kufanya si kufutilia mbali misamaha kwa kila taasisi ya dini na hiyari kama ilivyofanya. Badala yake kwa kuwa serikali inavyo vyombo vyake (machinery) vya kupatia taarifa za uhalifu na kuudhibiti, haikuwa vema kuvinyima kazi vyombo hivyo kwa kupitisha adhabu ya kijumla jumla inayowakumbwa wakosaji na wema.

Je, Serikali imeona ugumu gani kuwatafuta na hata kuwafungulia mashitaka matapeli hao wanaoharibu nia yake njema ya awali juu ya msamaha wa kodi? Naamini kuwa taasisi na vyama vya hiyari vilivyo viadilifu vingekuwa tayari hata kuisaidia Serikali kuwafichua matapeli hao.

Pamoja na hayo, maswali yafuatayo yanatakiwa kujibiwa: Kwanza, yatolewe maelezo ya kisayansi juu ya manufaa ambayo taifa litayapata kwa kuzitoza taasisi hizi kodi, na manufaa hayo yazidi yale yaliyokuwa yakipatikana katika kipindi chote cha misamaha.

Pili: Ielezwe wazi kwa nini hatua hiyo imekuja huku kukiwa na kauli za kupingana kati ya Waziri wa Fedha na Rais, kuna kukomoana?

Tatu: Kwa kuzingatia unyeti na mchango wa taasisi za dini katika maendeleo ya jamii nchini; Je, haikuwa vema hata kutoa taarifa ya muda (notice) fulani ili kuepusha usumbufu au hasara ambayo taasisi hizi zinapata hivi sasa.

Na Nne: Kwa nini hatua yenyewe imechukuliwa kimya kimya bila tangazo la wazi kwa umma wa Watanzania ambao ndio unaoathirika?

Tano: Ielezwe ni bidhaa gani ambazo Serikali inaona kwa mfano Kanisa likiletewa msaada au kuagiza nje ni anasa na hazina manufaa kwa jamii.

Pamoja na kwamba taarifa za TRA zinasema vifaa vitakavyoingizwa nchini na taasisi hizo kwa ajili ya elimu na huduma za afya havitatozwa kodi (ingawa tayari kuna malalamiko kuwa utekelezaji wake umekuwa kinyume), bado haitoshi kwa vile vipo vifaa vingi vinavyotumwa kwa taasisi hizo kama misaada kwa taasisi zenyewe ambavyo taasisi hizo hazina uwezo wa kuzilipia ushuru.

Kwa mfano magari, kompyuta, vifaa kwa ajili ya redio na vya njia nyingine za mawasiliano, baiskeli za msaada kwa walemavu, nguo, vyakula na kadhalika ambavyo taasisi hizo huvitoa bure kwa wasiojiweza au kuongeza uwezo wa kuihudumia jamii. Inafahamika wazi kwamba wajibu wa Serikali ni kuwahudumia raia wake, hivyo pale ambapo Kanisa, Misikiti au wananchi wenyewe kupitia vyama vyao vya hiyari wanapojitoa mhanga kutoa huduma hizo kwa namna fulani wanaijenga na kuipunguzia mzigo Serikali.

Hadi Serikali itakaposahihisha makosa hayo iliyofanya, hakuna sababu ya kutoamini kuwa uamuzi wa Serikali juu ya suala hilo, haukuwa wa kisayansi, bali hamaki.

Kutambaa mapema huleta faida

Afya ya mtoto hujengwa tangu anapokuwa katika hali ya mimba. Katika mfululizo wa makala kutoka kitabu cha " Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo" cha Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni la Beijing, China baada ya kuwaletea miiko 15, wanayopaswa kuwa nayo akina mama wajawazito, leo tunaangalia kutambaa mapema kwa mtoto kunavyoleta faida.

WATOTO wachanga wanapojaribu kutambaa mapema huanza kwa kufanya vitendo vya mfululizo kama vile kupinda mgongo, kulala kifudifudi, kuinua kichwa, kukita mikono chini ili kuwa mhimili wa kuinulia sehemu ya juu ya mwili wake,kukunja miguu na kujisogeza mbele kwa magoti.

Vitendo kama hivyo humwongezea mtoto nguvu ya mapafu, shingo,kiuno, miguu, magoti, mifupa na musuli na pia huleta faida kwa viungo vingine vya mwili. Kabla mtoto hajaanza kutembea, huanza na kutambaa ambako kumpatia fursa kubwa zaidi ya kujongea na huongeza hekaheka zake katika kuhisi mambo, kuonyesha imani na kutafuta shabaha.

Tunaweza kumfundisha mtoto mchanga jinsi ya kutambaa mapema iwezekanavyo.

Kwanza inapasa kujaribu kumshawishi mtoto mchanga awe na shauku ya kutambaa, hapo mtoto hujiwa na nguvu ghafla ya silika kama wale watoto wanavyojitolea kujiunga na michezo ya wenzao, ambao hujitupa ndani bila kulazimishwa, si vizuri kwa wazazi kumlazimisha mtoto mchanga kutambaa.

Ikiwa mtoto wako anaonekana kuwa na shauku ya kutambaa, hapo unaweza kumasidia kujizoeza kwa kitendo hicho: Mlaze mtoto wako kifudifudi, halafu kinga nyayo zake kwa mikono miwili ili mtoto akunje magoti kwa kutumia nguvu zake mwenyewe.

Wakati huo mtoto hujaribu kunyosha miguu, na hapo kinga nyao zake kwa nguvu kidogo, kama mtoto anaonekana kuwa na nguvu ya kujisogeza mbele wakati huo anaweza kujizoeza jinsi ya kutambaa.

Mtoto huonyesha maumbile ya kujifunza kitendo kipya katika hali ya furaha, na hamu ya kitendo kipya katika hali ya furaha, na hamu ya kitendo kipya,ambapo huonekana kuwa na shauku kubwa na hupenda kurudiarudia kitendo kilekile bila kuacha.

Hatua ya pili ni kujaribu kumfundisha mtoto jinsi ya kuinua kichwa, jinsi mikonp na miguu inavyopokezana katika kujisogeza mbele, na jinsi ya kuwianisha vitendo vya sehemu hizo.

Mtoto huweza kujifunza vitendo hivyo katika kujizoesha jinsi ya kutambaa, hatimaye mtoto hudhibiti vitendo hivyo mwenyewe hatua kwa hatua, wakazi wasiwe na papara hata wakataka mtoto wao mazoezi ya kuinua na kugeuza kichwa, kuangalia pembeni, kujisogeza, kujilaza kichalichali, jinsi ya kugeuza shingo n.k.

Mtoto ataongeza mwendo wa kutambaa mwenyewe wakati unapowadia.

Maana ya Umri wa mwaka mmoja kwa mtoto mchanga

Mtoto mchanga akifika umri wa mwaka mmoja ataanza kuingia katika hatua ya kwanza ya kujitegemea.

Hii ni kwa sababu ya kwamba kutoka wakati huo chakula chake kimepata mabadiliko makubwa.

Kwa msingi amepunguza kunyonya maziwa na kutegemea chakula cha kawaida.

Kwa hiyo yanakuja maswali mawili. La kwanza ni iwapo wazazi wataweza kuchanganya chakula chenye siha ama sivyo.

Pili ni iwapo mtoto huyo mchanga ataweza kupokea na kula chakula hicho ama sivyo, na kujenga msingi mzuri katika upande wa chakula na maji kwa ajili ya afya yake mwenyewe.

Swali la kwanza linawataka wazazi kufahamu maarifa ya kawaida kuhusu siha ya mtoto mchanga anayenyonya.

Sasa kuna vyakula vingi sana vyenye siha hata wazazi hawajui wachague chakula cha aina gani.

Kusema kweli, kama tunapanga vizuri vyakula vya nyama, mayai, mboga na nafaka, tunaweza kuwatolea watoto chakula cha aina nyingi chenye siha.

Mende waajiriwa kuwa walinzi

lNi mende aina ya Magnablader

Na Ignatio Obuombe

MENDE kwa kawaida ni wadudu wanaojulikana kuwa ni waharibifu, na huchukiwa na wengi. Hali hii imepelekea mara tu viumbe hawa wanapoonekana majumbani kuuawa mara moja, ama kwa kupuliziwa dawa na wakati mwingine kwa kubamizwa.

Ni wadudu waliotapakaa karibia sehemu zote duniani ingawa wadudu hawa wanapendelea zaidi sehemu zenye joto.

Kulingana na kitabu cha "World Book of Insects" kilichochapishwa nchini Uingereza, zipo zaidi aina 350 za mende kote duniani na kati ya hao wengi wanapatikana Afrika na Ulaya.

Mende wanaopatikana sehemu moja ya dunia wanatofautiana sana na wanaopatikana sehemu nyingine ya dunia.

Hali hii imepelekea katika sehemu zilizo nyingi za dunia ambako mende wanapatikana, kuonekana kuwa hawana faida, isipokuwa hasara tu.

Lakini hivyo sivyo ilivyo kwa mende wanaopatikana katika kisiwa cha Madagascar. Kikiwa kwenye Bahari ya Hindi, Madagascar ambayo ni Koloni la zamani la Wafaransa mji wake Mkuu ni Antananarivo.

Mende wenye faida wanaopatikana Kisiwani Madagascar wameweza kuleta faida kwa kutumiwa kama walinzi.

Labda utashangaa mende mdudu mdogo tu atakuwa mlinzi kwa vipi?

Mende hawa ambao watu wa Madagascar huwaita "Magnablader" ni aina ya mende wakubwa wanaokaribia ukubwa wa panya wadogo.

Mende wa aina hii hawapatikani sehemu nyingine yoyote ya dunia isipokuwa kisiwa hiki cha Madagascar.

Wakazi wa kisiwa hiki huwafuga kwa kuwaweka ndani ya kiota kilichosukwa kwa ukili ambacho huning'ing'zwa mlangoni .

Ndani ya kiota ujira wa Magnablader kwa kazi yake ya kulinda nyumba ni kupewa chakula wakipendacho sana.

Mende hawa wakubwa wanajua wajibu wao na anapoingia mtu yeyote mgeni ndani ya nyumba wanapiga kelele.

Ukelele unaotolewa na mende aina ya Magnablader mara tu anapoona wageni ni kelele zinazoweza kumuamsha hata aliyelala fofofo.

Pengine wangekuwepo hapa nchini Tanzania wangepunguza umuhimu wa makampuni ya ulinzi kama vile Ultimate Security na wengine ambao hutegesha ving'ora katika nyumba za wateja ili mwizi akijaribu kuiba vipige kelele.

Kufuatia mende hawa kuwa walinzi wazuri, watu wengine nchini Madagascar wamekuwa na tabia ya kuwafuga majumbani mwao ili wawasaidie kulinda wezi.

Mende hawa huuzwa kwa bei ghali jijini Antananarivo.

Kwa kawaida mende hawa wenye mazoea ya kuishi na kuzaliana porini, hutegwa na kisha kusafirisha mpaka mjini ambako wanauzwa.

Mtakatifu Basili Mkuu: Kalamu tatu za kusaini afukuzwe, zilivunjika ghafla

Mungu aliwazuia maadui zake wasimuue

Na Joseph Sabinus

"Je U masikini? Sawa lakini wapo masikini kukupita wewe. Vile vichache ulivyonavyo wewe, vinakutosha kwa siku kumi. Lakini alichonacho maskini huyu kinamtosha kwa siku moja tu, ya leo.

Kwa hiyo usiogope kuvitoa hivyo vichache ulivyonavyo Usiangalie faida yako mwenyewe kuliko mahitaji ya wengine. Umpe mwombaji aliyemama mlangoni pako chakula chako cha mwisho na baada ya hayo, utegemee wema wake Mungu".

Ni maneno ambayo mara nyingi Mtakatifu Basili Mkuu alipenda kuyatoa katika mahubiri yake. aliona kuwa wajibu wa kutoa msaada hakukuwa tu wa watu. Matajiri na wenye vyeo, bali pia hata maskini nao walipaswa kuwasaidia maskini wenye uwezo wa chini yao.

Mtakatifu Basili aliyekuwa mtoto wa Mtakatifu Basil Mzee na Mtakatifu Emilia, alistahili kuitwa Mkuu wa sababu ya akili na utakatifu wake.

Yeye na ndugu zake watakatifu Makrina aliyekuwa dada yake, Gregori wa Nisa na Petro wa Sabaste walipendana sana.

Akiwa masomoni Konstantinopoli huko huko Uturuki na katika Atene nchini Ugiriki, alimpata rafiki mmoja;ndiye Mtakatifu Gregori wa Nazianza huko Atene wakapendana sana huku wakijibidisha kuendeleza katika utakatifu na hata maarifa yote.

Basili alikuwa fundi wa kutumia lugha kiufasaha na laiti angekuwa mpenda makuu, hakuna ambalo lingempita maana angeweza kuyapata yote aliyoyataka toka kwa watu. Lakini Mtakatifu huyu anayekumbukwa kila mwaka ifikapo Januari 2 ya mwaka pamoja na Watakatifu wengine akina Gregori wa Nazianze aliyekuwa Askofu na Mwalimu wa Kanisa, Mtakatifu Gaspari De Bufalo; padre na mwanzilishi wa Shirika na Watakatifu wa Afrika kama askofu Isidori na Makarius Mzee;Mtawa wa Misri, aliyapuuza hayo,alichotaka ni ujiko na sifa toka kwa Mungu.

Huko Asia Ndogo-Uturuki wafuasi walipokusanyika na kumzunguka, aliamua kuanzisha nyumba ya kitawa.

akatunga sheria zilizoendelea kutumika na kuwaunganisha watawa kwa karne nyingi na hadi leo zinatumika na watawa wafuatao madhehebu ya Mashariki.

Ingawa aliishi maisha kamili ya kitawa, kwa miaka mitano tu,maongozi yake na ya Mtakatifu Benedikto yalikuwa ya msingi wa kitawa katika karne ya sita.

Mtakatifu huyu aliyetunga vitabu vingi vya mafundisho ya kidini alipata Upadrisho mwaka 363 na kuwa Askofu wa Kaisarea mwaka 370; akipinga vikali wazushi wafuasi wa Arios.

Kitendo cha ujasiri na kutokuwa mwoga katika kutetea haki za Kanisa,kiliwafanya makaisari kumwogopa sana Mtakatifu huyu. Mungu mwenyewe aliwazuia maadui zake wasimuue.

Kaisari Valentine alipotaka kumfukuza Basili wakati wa kutia saini, ghafla kalamu yake ilivunjika. Ikaletwa kalamu nyingine ya pili;nayo ikavunjika ghafla, ikaletwa kalamu ya tatu, nayo vilevile ikavunjika ghafla.

Kaisari yule akajawa na hofu na wala hakuthubutu tena kumfukuza Basili katika miliki yake.

Mtakatifu Askofu Basili alijitahidi kuhakikisha kuwa mapadre wa jimbo lake wanautekeleza vema wajibu wao na tena bila wasiwasi,Askofu Basili katika kipindi chake alikataa kata kata kumpadrisha yeyote ambaye kwa mujibu wake hajafaa kuwa padre. hali ya jimbo lake ikawa ni mfano bora kwa majimbo mengine.

Askofu huyu aliyekuwa Mwalimu wa Kanisa na kwa ajili ya kazi nyingi nzito, ugonjwa na kujinyima kwake vilimdhoofisha upesi hata akafariki akiwa na miaka 49 hapo Januari 1 mwaka 379.

Yeye hakuwa akikaa kimya kila alipotambua kuwa wenye vyeo na matajiri walikuwa wakitenda kinyume cha wajibu wao wa kikristo na hata siku moja alipopata nafasi ya kuwahubiria alisema hvi;

"Wakataa kutoa fedha eti kwa sababu fedha zako hazitoshi kwa mahitaji yako mwenyewe; lakini huku ulimi wako ukiomba radhi, mkono wako unakuhukumu kwa maana ile pete ya kidoleni mwako yadhihirisha uongo wako. Nguo zako za ziada zingewatosha maskini wangapi? Nawe unathubutu kumwondoa mtu maskini mlangoni pako bila kumpa kitu chochote?"

Mtakatifu huyu ni mfano bora wa kuigwa na viongozi wa dini , au wa serikali na jamii yote wanaosahau wajibu, majukumu,na hivyo kujisahau na kuanza kujineemesha wenyewe kila mtu kwa nafasi yake;tena kama watumishi wa Mungu wanakuwa hawana haya mbele ya Mungu.

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

ASHOKADOHODA: Mti unaoabudiwa na Wahindu

lHuufanya ishara ya upendo na kuuabudu kwa heshima ya miungu yao iitwayo Kamadeva

Na Ignatio Obuombe JR.

NI aina ya mti unaomea, kustawi, na kupatikana karibu katika majimbo yote ya India. Ni mti wa Ishara ya Upendo na huabudiwa kwa heshima ya KAMADEVA, miungu ya Wahindu ya upendo.

Ukisafiri India yote kwenye majimbo ya Ladakh, Punjab,Haryana, Uttar Pradesh, Rajasthan, Himachal Pradesh na Andhra Pradesh, mti wa Ashokadohada ama kwa kifupi Ashoka unaheshimiwa na kila Mhindu.

Tofauti na miti mingine ambayo huwa inaenziwa ili kuhifadhi mazingira, hali ni tofauti kwa mti huu wa Ashoka ambao hupewa tu heshima kwa sababu wanaamini ni mti wa miungu ya upendo.

Je, ni kwa njia gani Wahindu huabudu mti wa Ashoka?

Maua ya mti huu huchumwa, kisha maua hayo husokotwa na kuwekwa kwenye vifaa vya ibada ambavyo hutumiwa na makuhani wa Kihindu wakati Wahindu wakiabudu miungu yao ya upendo au Kamadeva kama inavyojulikana.

Ashoka, mti ambao pia huhusianishwa sana na wasichana na wanawake warembo, unaaminiwa na Wahindu kuwa unaweza kutoa maua pale tu ngoma za matambiko ya miungu ya Kihindu inapochezwa chini yake kisha mguu wa kushoto wa msichana anayecheza ngoma hizo kugusana na mizizi yake; wanaamini hapo ndipo mti huu unapoweza kutoa maua.

Dansi hilo ambalo huandaliwa rasmi kwa ajili ya kufanya mti wa Ashoka utoe maua linaloitwa kwa lugha ya Kihindi " Malavikagnimitra".

Desturi ya ngoma za Kihindu huchezwa kando ya mti wa Ashoka ili kuupelekea uchipue maua hazijaanza leo, desturi hii ilianza mwaka 1800,wakati msichana mrembo wa Kihindu aitwaye "Malavika" alipokuwa amependana sana na Mfalme Agnimitra.na ndipo walipoandaa dansi wote wawili na kucheza kando ya mti wa Ashoka.

Inaelezwa katika simulizi za Kihindu kuwa Malavika mwenyewe aliyekuwa muumini wa dini ya Kihindu alicheza na kuchukua mguu wake wa kushoto na kukanyaga juu ya mizizi ya Ashoka na kusema "Mti huu wa Ashoka utakuwa wa miujiza kama usipotoa maua sasa hivi", na toka hapo mti huo ulichipua maua mazuri sana ya kuvutia. Simulizi zinasema toka hapo Wahindu wamekuwa wakitumia mti huo kuabudu miungu ya upendo hata leo.

Kwa vile Ashoka hufanikishwa na msichana mrembo, sanamu za wasichana zilizochongwa na mti wa Ashoka hata leo pamoja na mashairi ya kusifia mti huo zimehifadhiwa katika majumba ya makumbusho katika miji ya New Delhi, kwa mujibu wa jarida moja la India, Perspectives la Oktoba 1999.

Mti huu kwa Wahindu unadumu kuwa dalili ya furaha, upendo, amani na heshima kwa miungu yao.