Machache ya kukumbukwa mwaka 1999

Na Dalphina Rubyema

JANUARI 4: Polisi jijini waliwajeruhi watu nne kwa risasi katika matukio mawili tofauti kukabiliana na matukio ya uharifu.

JANUARI 5: Bomu la mkono lililipuka pembeni ya jengo la CCM,kata ya Bilele,wilayani Muleba na kuharibu sehemu za jengo hilo.

JANUARI 19: Msikiti wa Tandamti jijini ulianguka ukuta wake na kuua mtu mmoja na kujereuhi wengine sita wakati wa sala ya Idd-El-Ftri.Aliyekufa ni Bi.Fatma Bakari(12).

JANUARI 28: Hofu ya mabomu ilitanda katika jengo la PPF jijini baada ya lile lililolipua Ubalozi wa Marekani hapo Agost mwaka 1998.

MACHI 8: Walemavu walilala barabarani ,Buguruni jijini kupinga kuvunjwa vibanda vyao.

MACHI 11-12: Ajali ya basi iliuua watu saba na wengine 20 kujeruhiwa katika eneo la Chalinze baada ya basi aina ya ISUZU TZM 536 kugongana na lori lililokuwa limeegeshwa pembeni ya barabara lenye namba za usajili TZC 4355 aina ya Scania .Ajali hiyo ilitokea eneo la Pera,Chalinze mkoani Pwani.

MAHI 27: Watu 14 walikufa na wengine 65 kulazwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro baada ya mabasi mawili kugongana uso kwa uso katika eneo la Kingolwira.Magari hayo ni Sadidline lenye namba za usajili TZL 2626 lililokuwa likitoka Dr-Es-Salaam kwenda Morogoro na gari lingine ni Scandnavia lililokuwa likitoka Mbeya kwenda Dar-Es-Salaam.

APRILI MOSI: Benki ya Tanzania (BOT) ilitangaza rasmi kusimamisha shughuli za Benki ya Greenland nchini yenye makao yake makuu nchini Uganda.

APRILI 11: Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilimuhukumu adhabu ya kifo mshtakiwa Rukasi Manyirizu (50)ambaye alikuwa mchngaji wa kanisa la Emanuel Church of God baada ya kupatikana na hatia kumuua Joseph Rehemeja kwa kukusudia.

APRILI 13: Rais Benjamin Mkapa ,alizindua rasmi nyumba ya Rais wa Awamu ya kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,iliyojengwa Mwitongo ,katika kijiji cha Butiama mkoani Mara iliyojengwa kwa ushirikiano wa serikali na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

APRILI 17: Bw.Augustine Mrema alijiuzulu uwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi.

APRILI 25: Bw.Agustine Mrema alijivua uanachama ndani ya chama cha NCCR-Mageuzi na kujiunga na chama cha Tanzania Labour Party (TLP).

MEI 7: Bw.Agustine Mrema alipokelewa rasmi kuwa kaimu mwenyekiti wa TLP.

MEI 14: Mahakama ilimsimamisha uenyekiti wa TLP Bw.Agustine Mrema.

MEI 14: Ajali iliuwa watu 17 mjini Arusha na wengine 9 kujeruhiwa.

Ajali hiyo ya gari ilitokea katika kijiji cha Kolila wilayani Arumeru mkoani Arusha ambapo gari dogo la abiria aina ya ISUZu lenye namba TZL 8722 liligongana na lori tani 12 lililokuwa limeegeshwa pembeni kando ya barabara.

MEI 23: Watu wawili walikufa kwa ajali ya gari na wengine wanne kujeruhiwa katika eneo la Mawanga,mkoani Songea baada ya basi la Hood lenye namba TZG 3763 kugongana na basi la Tawaqal.

MEI 28: Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)lilitangaza rasmi kutengwa kwa Padre Felician Nkwera na wafuasi wake.

JUNI MOSI: Watu wanne walikufa na wengine 37 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Mwanza kwenda Sirari kup[asuka gurudumu la mbele.Gari hilo lenye namba TZN 757 mali ya Tanganyika Bus Service lilipata ajali katika eneo la Nyamukoma ,Musoma Vijijini.

JUNI 3: Watu wanne walikufa na wengine 22 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria lenye namba za usajili TZH 2540 kupinduka katika kijiji cha Mkonga wilayani Handeni mkoani Tanga.

JUNI 25: Spika wa kwanza wa Bunge la Tanganyika baadaye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Chifu Adam Sapi Mkwawa alifariki dunia na kuzikwa kijijini kwake Kalenga mkoani Iringa hapo Juni 30 1999.

JUNI 28: Padre Nicholaus Msemwa,Padre Lazaro Kilawa ,Padre Mathias Kayombo na Sista Gema Killa OSB, walifariki dunia baada ya boti walilokuwa wakisafiria kuzama katika ziwa Nyasa wakati walipokuwa wakivuka kwenda parokia ya Lumbila jimbo la Njombe.

JULAI 28: Watu 9 walikufa na wengine saba kujereuhiwa baada ya lor i aina ya Fiat lenye namba za usaji TZJ 27498 mali ya kampuni ya Mawe ya Kiwira kugongana na gari ndogo aina ya Pick Up TZ 8048.Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Rubanda wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

AGOSTI 23: Gari aina ya Toyota Pick Up TZG 7697 lilipasuka tairi na kuua watu 11 na kujereuhi wengine 15.Ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Lemanyata Ngaramtoni wilayani Arumeru mkoani Arusha.

AGOSTI 28: Ajali mbaya ya gari ilitokea eneo la Mlandizi mkoani Pwani ambapo watu 29 walikufa na wengine 20 kujeruhiwa.Magari yaliyosababisha ajali hiyo ni DCM TZK 1916 mali ya Anold Temba kugongana uso kwa uso na Canter TAV 665.

AGOSTI 31: Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliondoka nchini kwenda London Uingereza kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

SEPTEMBA 17: Watu 6 walikufa na wengine 14 kujeruhiwa baada ya gari TZM 4191 lenye tera TZ 9959 lilokuwa likisafiri toka Makanya kwenda Dar-Es-Salaam lililpogonga magari kadhaa yaliyokuwa yameegeshwa njiani kisha kupinduka lenye.Lori hilo lililokuwa limebeba shehena ya mawe lilipata ajali hiyo katika eneo la Kimangwe Mbwewe Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

SEPTEMBA 26: Rais Mkpa alitangaza kuwa hali ya Baba wa Taifa si nzuri na kuwataka Watazania wamuombee.

OKTOBA 14: saa 4.30 asubuhi:Baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere alifariki dunia akiwa katika hospitali ya Mtakatifu Thomas Mjini London Uingereza alipokuwa ameleza kufuatia kusumbuliwa na kansa ya damu.

OKTOBA 18 ; Mwili wa Baba wa taifa uliwasili nchini.

OKTOBA 23: Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizikwa nyumbani kwake Mwitongo kijijini Butiama mkoani Mara.

NOVEMBA 7: Watu watano walikufa na wengine 45 kujeruhiwa katika eneo la Hamera Karatu mkoani Arusha baada ya gari TZF 5095 aina ya Layland kukataa kushika breki na kupinduka.

NOVEMBA12:Taifa lilihitimisha maombelezo ya kifo cha Baba wa Taifa ambapo wanafunzi wa Shule ya Sekondari Pugu waliandamana kwa miguu kutoka Pugu hadi kwenye viwanja vya Karimjee jijini.

NOVEMBA 15: Mchungaji Christopher Mtikila walifikishwa katika Mahakama ya Kisutu kujibu shtuma za kuuita Mzoga mwili wa Mwalimu Nyerere.

NOVEMBA30: Rais Benjamin wa Tanzania Benjamin Mkapa,Rais wa Kenya Daniel Arap Moi na Rais wa Uganda Yoweli Mseven walitia saini mkataba wa uwanzishwaji wa ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

DESEMBA 15: Watu 10 walikufa maji kwenye ziwa Victoria baada ya Boti waliyokuwa wakisafiri toka Ikizu Muleba mkoani Kagera kwenda Bandari ya Kasende kuzama.

DESEMBA 20: Watanzania 15 walifariki dunia katika eneo la Nakuru nchini Kenya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Dar-Es-Salaam kwenda Bukoba kupinduka.Gali hilo ni Tawfiq.

DESEMBA 24: kwenye mkesha wa Krismas Kanisa katoliki kote dunia liliadhimisha misa ya ufunguzi rasmi wa Jubilei Kuu.

 

 

Mbwa wajiua nchini Argentina kwa kukorofishwa na wamiliki wao

lWatafiti wafanyia uchunguzi vifo hivyo

Mpaka sasa idadi ya waliojiua imefikia 50

Na mwandishi Wetu

DESTURI ya kiumbe kujiua anapoudhiwa inajulikana kuwa ipo kwa binadamu pekee yake. Hii ni kwa sababu viumbe wengine kama wanyama na wadudu hawana ujuzi wa kuchambua mema na mabaya kiasi cha kuweza kuamua ni hatua ipi wachukue wanapoudhiwa.

Mara kadhaa wanyama kama Tembo, Simba, Nyoka na baadhi ya ndege wakubwa wamekuwa wakionesha ghadhabu zao kwa kumshambulia anayewachokoza hasa wanaponyang'anywa au kuuliwa watoto wao. Lakini kamwe haijapata kuwa jambo la kuzoeleka kwa wanyama kujiua wenyewe kwa kuchukizwa.

Nchini Argentina huko Amerika Kusini katika mji wa Rosario uchunguzi, mkali wa watafiti unaendelea katika bwawa mashuhuri katika bustani ya kupumzikia jijini hapo kutaka kujua ni nini chanzo cha mbwa wa wakazi wa jiji hili kwenda kujitosa katika bwawa hilo na kujiua pindi wanapoudhiwa na wamiliki wao.

Kwa mujibu wa taarifa za kiuchunguzi zilizochapishwa na jarida la Straight Times la Singapore, mwanzoni wakazi wa mji wa Rosario walipuuzia hatua iliyochukuliwa na mbwa hao kwa kuiona kuwa ni ya kawaida lakini sasa baada ya mbwa wanaojiua katika bwawa hilo idadi yake kuongezeka kila kukicha imeamuliwa uchunguzi mkali ufanyike kujua chanzo cha mkasa huo wa kuingilia karne mpya.

Ikiwa ni moja ya Bustani kubwa kabisa za kupumzikia nchini Argentina bustani ya "Parque de Espana" imepitiwa kandoni mwake na mto mkubwa wa Parana.

Mto huu wa Parma umetumiwa kujenga bwawa kubwa busatani ambako raia wengi wa Argentina hupenda kwenda kuendesha mashua zao ndani yake na kutoa samaki kwa kutumia ndoano wakati wa likizo.

Lakini katika siku za hivi karibuni mto Parana umekuwa siyo sehemu ya likizo tena bali sehemu ya huzuni. Huzuni hii imekuja kwa wakazi wa mji wa Rosario kuwapoteza mbwa wao wapatao 50 ambao wote hao uchunguzi umebainisha kuwa wamechukua hatua ya kujiua kwa kujitosa kwenye mto Parama baada ya kukorofishana na wamiliki wao.

Mahojiano yaliyofanywa na Chama cha Kutetea Haki za Wanyama cha Argentina na wamiliki wa mbwa wote wapatao 50 ambao walijiua kwa kujitosa kwenye bwawa la Mto Parana kwa nyakati tofauti, yamebainisha kuwa kila mbwa alichukua hatua hiyo dakika chache baada ya kukorofishana na mmiliki wake.

Pamoja na kuwa baadhi ya wataalam wa Wanyama nchini Argetina wamedai kuwa vifo vya mbwa hao kwenye bustani hiyo vinaweza kuchangiwa na kuvutiwa na sauti za ndege na mlio wa maji, waganga wa Kienyeji wa Argetina wao wamekataa kuwa mizimu ya parama ambayo imedumu kuishi katika mto huo miaka nenda rudi ndio chanzo cha vifo hivyo.

Tukio la wanyama kujiua wenyewe liliripotiwa hivi karibuni pia katika eneo la Mbuga moja ya wanyama katika jimbo la Quebec nchini Canada, ambako wanyama wakubwa aina ya Walrus waliripotiwa na jarida moja la Canada kuwa walipanda kwenye majabali yaliyoko kwenye ufukwe wa ziwa katika mbuga hiyo kisha wakajiua kawa kujirusha kwa nguvu wenyewe juu ya miamba.

 

 

Je, unajua tumbaku ilipotoka?

lNani alikuwa wa kwanza kuvuta Sigara Ulaya?

Na Mwandishi Wetu

MWEZI Agosti mwaka 1492 Christopher Columbus akiwa pamoja na watu wapatao mia moja na ishirini, aling'oa nanga kwenye bandari ya "Port of Palos" safari nchini Uhispania ikiwa ni safari ndefu ya kusafiri kufanya uvumbuzi wa nchi mpya ambazo hazikujulikana.

Waliondoka nchini Uhispania wakiwa na meli tatu ambazo zilikuwa ni Santa Maria, Pinta na Nina huo ndio uliyokuwa ni mwanzo wa safari ambayo baadaye ilipelekea kuvumbuliwa kwa bara la Amerika.

Safari ya Columbus ya uvumbuzi inahusiana sana na zao linaloshamiri leo la tumbaku kwani kama siyo juhudi za mvumbuzi huyu mzaliwa wa Italia, tumbaku leo isingesambaa duniani kote kwa kiwango hicho ilichosambaa sasa.

Colombus baada ya kufika bara la Amerika yeye pamoja na wagunduzi wenzake waliwakuta wakazi wa asili wa eneo hili ambao ni wahindi wekundu wakisokota majani ya tumbaku kwenye vifaa maalum walivyojitengenezea na kisha kuivuta.

Mwanzoni lilikuwa jambo la kushangaza kwao hata iliwabidi kufuatilia nyendo za wahindi hao kwa makini ili kupata kujua majani yale waliyasokota na kupuliza moshi wake hewani waliyatoa wapi.

Colombus alishangazwa kuona kuwa majani hayo yalitokana na mmea uliokuwa ukimea wenyewe porini.

Hatua iliyofuata ilikuwa ni kuchukua mbegu za mmea huo na kurejea nazo Ulaya.

Kwa vile safari ya Columbus ya kufanya uvumbuzi ilifadhiliwa na malkia Isabella wa Uhispania, Mvumbuzi huyu aliporejea alifanikisha usambazaji wa mbegu za tumbaku nchini Uhispania.

tumbaku ikaanza kusambaa kwa kasi barani Ulaya Wareno wakiwa wa kwanza kuichukua toka kwa majirani zao Wahispania.

Wafanyabiashara wa Kiingereza waliosafiri kwenda Ureno na Uhispania nao pia walibeba tumbaku na kuifikisha nchini Uingereza.

Mtu wa kwanza kuvuta tumbaku nchini Uingereza alikuwa ni Sir, Walter Raleigh Huyu Sir, Raleigh alikuwa ni ofisa mkubwa wa kuheshimika sana kwenye baraza la Malkia Victoria aliyeitawala Uingereza karne ya 17.

Siku aliyosokota tumbaku kwa mara ya kwanza na kuivuta mfanyakazi wake wa nyumbani ambaye maisha yake yote alikuwa hajapata kuona sigara alifikiri Sir, Raleigh alikuwa akiungua.

Kwa hivyo mfanyakazi huyo alichota maji ya baridi kwenye ndoo na akaja kumwagia Sir Raleigh kwa kuonyesha kushangazwa na hatua ya mfanyakazi wake kwa kumwagia maji. Sir Raleigh alikuja juu kuhoji kulikoni kwa nini amwagiwe maji wakati akifurahia sigara yake. lakini yule kijakazi alimuomba msamaha na kumwamba alifikiri Sir, Raleigh alikuwa anaungua.

Toka hapo Sigara zilisambaa pande zote za Uingereza, Wareno walipopita Afrika Mashariki wakiwa na nia ya kufika India wakiongozwa na mvumbuzi Vasco Da gama walileta tumbaku na kuiacha Afrika Mashariki Huo ukawa mwanzo wa Tumbaku kufika Tanzania.

 

 

Utamaduni katika maadili ya Kanisa leo

Na Christopher Udoba

HIVI karibuni kumefanyika sikukuu ya Utoto wa Yesu Mtakatifu kwenye ukumbi wa Kituo cha Msimbazi jijini Dar es Salaam .

Katika sikukuu hiyo kuliwakutanisha watoto toka parokia mbalimbali za makanisa ya Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, miungoni mwa parokia zilizoshiriki zilikuwa ni Mbagala, Upanga, Kawe, Chuo Kikuu,Tabata, Mburahati na Manzese. nyingine zilikuwa ni Yombo, Ubungo,Chang'ombe, Mwanyamala, Segerea, Kigamboni, Osterbay, Mtoni, Magomeni, Mkulanga na Kibaha kwa mujibu wa mwandishi wa makala haya aliyeshuhudia.

Sare za rangi nyeupe na manjano ndizo zilionekana kuvaliwa na watoto wengi katika tamasha hilo na sare hiyo ilikuwa ikiashiria bendera ya Kanisa Katoliki duniani lenye makao makuu Vatikani, huku wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali walionekana kuimba na kucheza kwa furaha kabla ya burudani kuanza rasmi mchana .

Watoto hao walionyesha ngoma, mashairi, michezo ya maigizo hata sarakasi mbele ya Mwadhama Polycarp Pengo " kucheza na kuimba ngoma ni sehemu ya kujengana katika Kanisa" mama mmoja amedai alipohojiwa juu ya mwenendo wa kutumia ngoma za asili katika makanisa ya Kikatoliki ikiwa kutaathiri kiroho watoto.

Mama huyo aliyehojiwa na mwandishi wa makala haya katika sikukuu ya kijimbo siku hiyo ameongeza kuwa ngoma asilia na muziki wa dansi unafaa pia kwa jamii katika sherehe za kikristu siku hizi.Aidha ngoma amedai kuwa zimeruhusiwa na kanisa Katoliki duniani katika mtaguso wa pili huko Vatican.

Baraza linalishughulikia Utamaduni (Pontifical Council on Culture) pia lilianzishwa na Papa Yohane Paulo wa II kwa mujibu wa kitabu kinachoitwa (Papa anayevutia).

Katika kitabu hicho kinachothibitisha kuwa masuala ya utamaduni yatapewa kipaumbele katika makanisa ya Katoliki duniani. Isitoshe maana ya utamaduni si ngoma tu, bali ni pamoja na shughuli nyingine zinazotayarishwa kwa ajili ya kuonyeshwa hadharani, kwa mfano hadithi simulizi, ngojera, michezo ya kuigiza na sarakasi.

Kwa upande wa ngoma, shirika la Utoto Mtakatifu wa Yesu lililopo parokia ya Msimbazi limeweza kuitumia katika kuwasilisha ujumbe wa Injili mbele ya watu.

Wachezaji wa Shirika hilo lililoandaliwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Pengo hapo Desemba 18 mwaka huu walicheza kwa ustadi mkubwa.Pia wavulana chini ya umri wa miaka 14 walionyesha ushujaa kwa kubeba ngao na mkuki.

Kwa kutumia ngao hiyo, wachezaji hao walitoa ujumbe juu ya Neno la Mungu yaani ngao ilikuwa ikimaanisha hasa ulinzi dhidi mafundisho potofu kwao, kuhusu mkuki ulimaanisha kuwa jamii lazima ilelewe kulingana na Biblia,kujiepusha na maovu.Mbali na wasanii wa Shirika la Utoto wa Yesu Mtakatifu pia watoto wa Parokia ya Osterbay walionyesha mchezo wa igizo juu ya mitume.

Katika igizo hilo ulisikika ujumbe ukiagiza kuwa wakristo waende kutangaza injili duniani pote na hapo wengine walionekana wakielekea huko na huku wakiwa ni kulitii agizo hilo.

Ipo haja kwa vikundi vinavyojihusisha na utamaduni kujaribu kutumia maneno yanayotokana na Biblia kwa njia hiyo watu watapata fundisho, muumini wa Parokia ya Kawe Isdory Mtunda ameeleza maoni yake na kusihi upigaji wa ngoma umheshimu Mungu zaidi.

 

 

Kulia na kucheka kwa mtoto mdogo

Afya ya mtoto hujengwa tangu anapokuwa katika hali ya mimba. Katika mfululizo wa makala kutoka kitabu cha " Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo" cha Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni la Beijing, China baada ya kuwaletea miiko 15, wanayopaswa kuwa nayo akina mama wajawazito, leo tunaangalia maana ya mtoto mdogo kulia na kucheka kama kama njia yake ya mawasiliano.

Watoto baada ya kuzaliwa, wana mbinu mbili tu: moja ni ya kulia na nyingine ni ya kucheka. Watoto wanapolia huwa na sababu nyingi.

Wako wanaolia kwa sababu ya njaa, wengine kwa sababu ya kutoona raha baadhi kwa sababu ya hofu,wengine wanalia kutokana na upweke.

Kulia ni njia muhimu kwa watoto kuwasiliana na watu wazima na mzingara , huwa ni njia ambayo inaweza kuwafanya watoto wajirekebishe na mazingira na kuwashughulisha watu wazima.

Watoto wanapolia si kama wana hali mbaya bali ni dalili njema. Kwa hiyo wanapolia, wazazi wasiwe na wasiwasi au kuwanyamazisha kwa ziwa. Kufanya hivyoo badala ya kuwatunza huwadhoofisha au hata kuwanyima uwezo wao wa kujirekebisha na mazingira ya kimaumbile, na hivyo huwafanya wawe wanyonge wasiomudu kupambana na mazingira. Kutokana na sababu hiyo, ndipo inapowapasa wazazi kuchunguza ili wafahamu chanzo cha kilio, na wachukue hatua zinazofaa kukidhi mahitaji yao. Si njia nzuri kuwazuia watoto tu wasilie bila ya kujua sababu, kwani pengine yatatokea mambo mabaya ambayo watakuwa wazito kuyashughulikia baadaye.

Kama kilio cha watoto kinavyoweza kumaanisha mengi, hali kadhalika na kicheko pia kina maana nyingi. Kwa kawaida wazazi waanachukia watoto kulia na wanafurahia tu wanapocheka, hivyo wanatumia kila njia kuwachekeshachekesha. Kwa kweli wazo hilo kwa kiasi fulani lina madhara yake. Kwa sababu kicheko cha watoto ni tofauti na kicheko cha watu wazima. Kwanza watoto hucheka na watu waliowazoea kama vile mama, baba na watu wengine ambao mara kwa mara wanawatunza au kuwaona. Kicheko chao kinaonyesha hisia zao za kuridhika ambazo zinaweza kupatikana wakati wanapopapaswa au wanapojiegemesha kifuani kwa watu. Majaribio ya kisaikolojia yameadhihirisha kwamba baada ya mtoto kuzaliwa tu na kuchukuliwa kulelewa na mwingine, baada ya muda mtoto huyo akimwomna mama yake atamkwepakwepa ingawa mama atajitahidi kumkumbatia, kumpapasapapasa kwa upole. Kukwepa kwa mtoto ni umbile lake la kujilinda. Mtoto huyo baada ya kukua ataendelea kuwa na pengo la mama yake mzazi, siku zote ataona ugeni mbele ya mama yake mzazi.

Kwa hiyo mtoto hacheki mbele ya mtu yeyote bali huwa na uchaguzi wake, na uchaguzi huo utamletea athari kubwa katika tabia yake ya mawasiliano na wengine.

Kutokana na sababu hii ndipo huwa ni busarakwa mama kumapatia mtoto wake nafasi za kuwasiliana na watu wengi ili aweze kuzoena na wengine. Uhusiano huo unaweza kumpatia mtoto maendeleo ya kifikra na kitabia.

Lakini kinamama wengi wanachelea kwamba watoto wao wageshitushwa na wageni, hiki ni kitendo cha kinyume na ukuaji wa watoto katika saikolojia, na hakina budi kusahihishwa.

Pili, kucheka kwa watoto kunaonyesha kwamba mtoto ameridhika kifiziolojia, kwa mfano, mama anapomnyonyesha, mtoto akiwa ananyonya huku akipapasa matiti, kwa mama mwenye maarifa anafahamu mara moja kwamba mtoto wake bado hajashiba.

Lakini wakati mtoto ananyonya huku akiinua kichwa mara kwa mara akimwangalia mama yake , hii ni ishara kwamba mtoto ameshiba na mama akitabasamu naye mtoto pia atatabasamu ili kuonyesha ridhaa yake.

Mfano mwingine ni kwamba mtoto anapolala ndani ya kitanda cha kubembea akiwa anachombezwa na mama yake mpole kwa wimbo, mtoto hutabasamu.

Kwa hiyo, mzazi hodari anapomchombeza mtoto hulingalinisha mapigo yake na mwendo wa wimbo, ili iwe rahisi kumwingiza usingizini.

Mtoto baada ya kushikwa na usingizi mara nyingine anamumunya midomo wakati anapoota. Mwisho ni kwamba wazazi wanapohitaji kumchekesha mtoto humtekenya sehemu yake ya ashiki, kicheko chake huonyesha furaha yake halisi. Lakini mtoto akitekenywa mara nyingi kupita kiasi hisia zake zitapungua, na kiini cha neva yake katachoka. Kama hali hiyo ikiendelea kwa muda mrefu mtoto atakapokua atashindwa kujirakibu hisia kwa mujibu wa mazingira.

 

MARGARETA MARIA ALAKOK: Mtakatifu aliyetokewa na Yesu akaoneshwa vidonda vitano

"Margareta! Ukiniacha mimi na kumtaka mchumba mwingine, mimi nitakuacha kwa siku zote"

Na Mwandishi Wetu

"Ukiniacha mimi na kumtaka mchumba mwingine, mimi nitakuacha kabisa; tena kwa siku zote" Margareta aliyatafakari kwa kina maneno hayo yaliyoelekezwa kwake toka kinywani mwa Yesu alipomtembelea siku moja na kumsemea.

Yeye Margareta alizaliwa mwaka 1647 nchini Ufaransa. Inaelezwa kuwa baada ya kifo cha baba yake, Margareta Maria Alakok aliingia katika shule moja ya shirika la Mtakatifu Klara.

Akiwa na umri wa miaka 11, Mtakatifu Margareta alipatwa na ugonjwa uliomsababisha asieweze kutembea kwa takribani miaka minne mfululizo.

Alipoanza kupona Margaretha Maria Alakok aliamua "kuingia barabarani" akazamia na kuzipendelea mno anasa za dunia huku akivalia kiumaridadi sana. Ndipo Yesu alipomtokea na kumwambia kuwa endapo Margaretha ataacha kuyaishi maisha yenye kumpendeza Mungu, Yesu naye angemwacha Maria kwa maisha yote.

"Margareta! Ukiniacha mimi na kumtaka mchumba mwingine, mimi nitakuacha kwa siku zote"

Inaelezwa kuwa kunako karne ya 17 kule nchini Ufaransa, Upendo kwa Mungu ulikuwa umepooza mno. watu wengine walikubali na kuufuata uzushi wa Jansenio aliyehubiri kwamba Mungu hawapendi watu wote kwa kiwango kilicho sawa. Yeye alisema na kuwaaminisha kuwa Mungu anawapenda baadhi ya watu na wengine anawaacha kabisa hivi hivi tu.

Katika kuwaamshia Wakatoliki ule upendo kwa Mungu katika miaka kati ya 1625 na 1690, walitokea Watakatifu watatu waliotumia juhudi zao kueneza ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Watakatifu hao ni Mtakatifu Yohani aliyezaliwa mwaka 1601 na kufariki mwaka 1680 ambaye hukumbukwa kila Agosti 19 ya mwaka tarehe aliyofariki na alitangazwa kuwa Mtakatifu mwaka 1925.

Ukiachalia mbali Mtakatifu Margaretha Maria Alokok tunayemzungumzia leo katika safu hii Mtakatifu mwingine aliyeshirikiana na watakatifu hao wawili kuona kuwa watu wa Ufaransa wanafikishiwa Injili sahihi ni Klaudio wa Kolombiere. yeye alizaliwa mwaka 1641 na kufariki dunia 1682.

Mtakatifu Margaretha Maria Alakok aliyekuwa mtawa alipokuwa na umri wa miaka 22 aliingia katika shirika la Masista wa Maonano (Vasitation Sisters) huko Poray-Le- Manial huko huko Ufaransa.

Ilitokea tena kuwa mwaka 1673 alipokuwa akisali mbele ya Sakramenti Kuu bwana Yesu alimtokea na kumuonesha moyo wake huku akisema "Tazama moyo wangu unawaka mapendo kwa watu. ningetaka kuwafumbulia watu moyo wangu na kuwagawia neema zote zilizomo"

Yesu alikuwa na makusudio yake makubwa kwa Mtakatifu huyu maana siku nyingine Mwokozi huyu wa ulimwengu alimtokea na kumuonesha vidonda vitano mwilini kwake huku akisema; "Nimewapenda watu kwa mapendo makubwa;lakini watu hawana shukrani laiti watu wangeyafikia mapendo yangu, ningekuwa tayari kufanya zaidi na kufanya bado zaidi kwa ajili yao. Lakini watu wananionesha ubaridi na ugumu wao. Ewe mwanangu;Unifurahishe kidogo mahali pa wakosefu hao".Hakuishia hapo tu mwezi Juni wa mwaka 1675 Bwana alimuonesha tena moyo wake. Safari hii alikuwa akisema;"Ndiyo moyo huu unawapenda sana watu nao watu hawaupendi lakini bado naona uchungu kuona ubaridi wa watu wale waliojitoa kwangu. Nataka siku ya Ijumaa ya kwanza ifuatayo baada ya siku nane ya sikukuu ya Sakramenti Takarifu iwe ni siku ya kuheshimu moyo wangu"

"Wakristo waipokee Komunyo kwa kunituliza kutokana na matusi niliyotukanwa hapa altareni nitazibariki nyumba zote zile ilimowekwa heshima ya sanamu ya moyo wangu"

Mtakatifu Margaretha pamoja na watakatifu wengine wa Afrika akina Saturninus, Nereus, Senea, Mariniano na Sarurand wote wakiwa wafiadini wa Moroko na ndugu wa tumbo moja hukumbukwa kila ifikapo Oktoba 16, ya mwaka. Alikufa Oktoba 19 mwaka 1690 na kutajwa Mtakatifu mwaka 1920. Alijishungulisha sana na kuieneza popote ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu na sasa imeenea katika nchi zote ulimwenguni.

 

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

PAPUA NEW GUINEA na Ibada ya Milima na Mito

lWangali wamefungwa na imani hiyo tukiingia karne mpya

Na Ignatio Obuombe JR.

UKITEMBELEA kwenye mitaa ya Jiji la Port Moresby, Mji Mkuu wa Papua New Guinea inakuwa vigumu kuamini kama wakazi wa kisiwa hiki wangali wakiabudu milima na mito.

Hii ni kwa sababu jiji la Port Moresby sasa linakuwa kwa kasi na kuingiliwa na utamaduni mgeni,kutembelewa na idadi kubwa ya watalii tofauti na ilivyokuwa miaka 20 iliyopita.

Juhudi za idara ya utalii nchini humo kutangaza kisiwa hiki zimezaa matunda na sasa idadi kubwa ya wageni wanaitembelea Papua New Guinea kila mwaka.

Unaposafiri kwenda sehemu za vijiji vilivyoko katika kisiwa hiki ndipo unapogundua utamaduni Mkongwe uliodumu miaka nenda rudi.

Wakazi wa kisiwa hiki baadhi yao wangali wanatembea bila nguo huku wakijisitiri na kipande kidogo cha ngozi ya mnyama upande wa mbele.

Nyweleni mwao huvaliwa manyoya ya ndege wakubwa wanaopatikana kisiwani huko na karibia katika vijiji vingi vilivyoko porini kuna kuhani wa kuwaongoza wanakijiji katika ibada ya milima na mito.

Makabila ambayo hayajastarabika nchini Papua New Guinea wanaamini kuwa nguvu zenye uweza wa kuneemesha nchi kwa mvua na mazao wanapolima hupatikana kwenyee milima mikubwa na mito.

Wamejenga imani pia kuwa kama wasipofanya hivyo jamii zao zinaweza kuadhibiwa vibaya na miungu hiyo inayodumu kukaa kwenye mito na milima.

Kila mwaka katika vijiji hivyo sherehe za kubadilishana mavuno ya mazao mbalimbali ya mashambani hufanyika.

Sherehe hizo ambazo hushirikisha hata watu wasomi ambao hurudi likizo vijini wakati wa maadhimisho yake zinaaminika kuwa zinapomalizika roho ya miungu hufurahi na kukibariki zaidi kisiwa hicho.

Pamoja na kuwa juhudi zimefanyika za kusambaza elimu katika vijiji mbalimbali vya Papua New Guinea, kuwabandua wakazi wake wa asili kutoka katika imani ambayo wameolewa ndani yake toka zama za mababu imeshindikana.Utafiti uliofanywa na tahasisi ya International Geographic Society ya New York Marekani katika kisiwa hiki mwaka 1995 umebainisha kuwa sehemu kubwa ya makabila yake yangali yakimuamini juu ya ibada ya mito na milima.Utafiti huo pia ulichapishwa kwenye jarida la taasisi hiyo.