Make your own free website on Tripod.com

Namuunga mkono Askofu Shayo, tusiuziwe gunia la chumvi kwa kutoa la almasi

"Haiwezekani kwa sababu mimi ni mwekezaji, nikahalalisha kuishi kwa dola 150 kwa siku, lakini Mwafrika anayeishi mazingira hayo hayo, mwenye mahitaji hayo hayo, akahalalishwa kuishi kwa senti 80 kwa siku. Kama huu si utumwa mambo leo, tuuite nini?"

Maneno hayo yenye kila chembe ya mguso wa nafsi na ukweli ndani yake, yaliyosemwa na Askofu Augustine Shayo wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar wakati wa maadhimisho ya Krismasi ya Mwisho ya Karne ya 20 nani asemaye hayahitaji pongezi?

Tangu Tanzania ilipopata uhuru,hususan baada ya Azimio la Arusha (1967) njia zote kuu za uchumi zilimilikiwa na Umma.

Hii iliweza kupunguza kasi ya kupanuka kwa matabaka ya walio nacho na wasio nacho. Na kwa namna moja ama nyingine mfumo huu ulisaidia zaidi kwanikwa kiasi kikubwa matunda ya jasho la Watanzania yalibaki Tanzania.

Hivi labda suala la kujiuliza ni kuwa ubinafsishaji na uwekezaji unaongeza ajira kwa Watanzania au la? Unaboresha huduma za kijamii kwa gharama ambazo mwananchi wa chini anaweza kumudu?

Kama alivyosema Askofu Shayo siku hiyo, haiwezekani tukawa na furaha anayodai Emmanuel Yaani Mungu Pamoja Nasi, kama masuala nyeti yanayohusu haki na amani hayatiliimkazo

Kwa mtazamo wangu sina shaka kuwa hayupo wa kupinga kuwa uvunjaji wa haki ndicho chanzo cha vita katika jamii, umaskini wa kupindukia kwa wachache na utajiri wa kupita kiasi kwa wachache. Hilo pia ndilo chanzo cha ujinga unaozuia maisha ya furaha ya watu wanyonge, magonjwa, udikteta, maafa yatokanayo na siasa na dini na kupitishwa kwa malengo yasiyokidhi mahitaji ya kweli ya jamii , na hata uchu wa madaraka usiokubali mabadiliko.

Namuunga mkono Askofu Shayo kwa alichosema kuwa wapo wengi miongoni mwetu waliopo jela, wengine wananyimwa haki zao huku wengi wakitumika kama vitega uchumi na zana za kuzalisha mali za wenye uchu wa mali;wasiotaka kugawana kidogo kilichopo pamoja na nguvu kazi zao.

Maneno ya Askofu Shayo kama,

"Haitoshi kukaa mchana kutwa; usiku kucha huku tukiimba nyimbo zote na kuvaa mavazi yote yanayoashiria furaha, amani na haki ya Mkombozi, kama hatujui suala la moyo unaotafuta amani ya kweli. Ni dhahiri kuwa kwa mtindo huo haiwezekani kufukia utumwa na ukoloni mamboleo..

Watanzania tunapenda maendeleo yatakayotuingiza kiurahisi katika milenia ya Sayansi na Teknolojia lakini pia tusingependa kudanganyika kwamba tunapopewa "gunia la Chumvi nasi tukatoa almasi na dhahabu" kwa wawekezaji ndivyo tunavyoiingia millenia hii namna tunavyokusudia. Lazima uwiano mkamilifu wa haki uwepo baina ya Serikali, wawekezaji na wafanyakazi. Lugha tamu na mbinu tamu za wawekezaji na wafanyakazi zisiwanufaishe wenyewe kuliko wazawa.

Si vema kudanganyana kuwa ajira ya watu wetu na wawekezaji ni yenye kuleta tumaini iwapo mshahara wao haufui dafu hata kwa siku mbili Je. ni kweli kwa utaalam na sheria za uchumi,anayezalisha asipate sehemu halisi ya kazi yake ili kesho apate moyo na nguvu zaidi za kuzalisha kwa ufanisi kwa manufaa ya umma?

Wawekezaji na waajiri wote kwa ujumla hawana budi kujua kuwa kama biashara kazi yoyote inahitaji kuwekeza (investment).

Ni kweli kwamba wageni wanapofika nchini, wanalalamika kuwa kodi, hoteli na hata gharama za huduma kadhaa wapatazo zikiwemo za chakula ni ghali mno. Hivi sasa anayefaidika hapo ni nani? Serikali, wageni au waajiriwa? Lakini kama ni Serikali ni ipi hiyo, hali huduma za watu wake zinapoteza tumaini?

Hivi kama wanaozalisha au kufanya yote hayo kwa watalii ni vijana wetu na kinacholipwa ni mathalani dola 150 kwa kitanda, haingewezekana anayefanya matayarisho hayo akapata mshahara wa kukidhi mahitaji yake kama haki ingeheshimiwa?

Kwa mtazamo wangu ili tuweze kuishi kwa amani na furaha katika milenia hii ya tatu ningeomba wale wote waliokabidhiwa dhamana wayaangalie masuala haya kwa kina na wigo mpana. Wawe na sauti thabiti ya kukemea unyanyasaji wa waajiriwa au uovu wowote unaoweza kufanyika kutokana na dhamira mbaya zinazoweza kuwapo miongoni mwa waajiri wa kigeni na hata wa hapa hapa nchini.

Ninasema hivyo nikiamini kuwa kumjua Mungu maana yake ni kulinda haki za wanyonge kama tunavyosoma kuwa "Baba yako alikula na kunywa, akatenda mambo ya haki na mema, ndipo mambo yakamwendea vema. Hii ndiyo maana ya kunijua mimi Mwenyezi Mungu" (Jer-22:15-17) .

Taifa au jamii yoyote haifai kuomba kusamehewa madeni endapo haiko tayari kuwatendea haki wanyonge. Hivi kweli ni haki jamii husika ikaomba kusamehewa mikopo na hali haina malengo yaliyo bayana ya kukidhi mahitaji ya wengi?

Mimi naamini kuwa moja ya mambo muhimu katika kusamehewa mikopo ni kuheshimu na kulinda haki katika nyanja zote zihusuzo maendeleo ya jamii, Je tumekwishafika hapo?

Kama hospitali zetu hazina madawa, elimu bado inashuka kiasi cha kutisha licha ya utitiri wa shule zikiwemo za binafsi zisizoweza kujiendesha badala yake zimekuwa ni biashara tu na bado udhaifu wa watendaji kadhaa unawapa mwanya wachache kuwa matajiri kupindukia na wengine kugeuka watumwa, nchi inastahili kuimba wimbo na amani na upendo? Je itajikomboa kiuchumi?

"Uniondolee uongo na udanganyifu, usinipe umaskini wala utajiri unipatie chakula nichohitaji nisije kushiba nikakukana, nikisema Mwenyezi Mungu ni nani? au nisije nikawa masikini nikaiba na kulikufuru jina lako ee Mungu wangu, Ulimwengu una nafasi ya kila mtu na una chakula cha kila Mtu, kama kweli wote tungekuwa wapenda haki na wapenda amani," kinasema kitabu cha Methali.

Mawazo ya kufananisha vitu ya watoto wadogo

"Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo" cha Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni la Beijing, China baada ya kuwaletea makala juu ya "Uchoraji unavyowanufaisha watoto," leo tunaendelea na mada juu ya "Mawazo ya kufananisha vitu ya watoto wadogo"

Watoto wadogo wana mawazo mengi ya kufananisha.

Mawazo yao huwa hayazuiliwi na kanuni au maadili yoyote kama yalivyo mawazo ya watu wazima.

Tunaweza kuona watoto wengine wanachukua tawi la mti wakilipanda kama kwamba wanapanda farasi huku wakirukaruka kama farasi wakiavyo kwa kufanya hivyo wanafananisha tawi kama hili na fimbo ya uchawi iwezayo kutumiwa kama bunduki, mkuki, ndege au meli.

Wanaweza kulifananisha na kitu chochote wapendacho. Lakini kadiri umri wao unavyozidi kuwa mkubwa ndivyo mawazo yao kama hayo yanavyokuwa na mipaka.

Mfano ufuatao unaweza kudhirisha maneno hayo: Mwalimu wa shule moja kati ya daraja la juu alifanya alama kama tone la mvua kwa chaki kwenye ubao akawauliza wanafunzi "Je nani anaweza kuniambia kili nilichokichora ubaoni?" dakika mbili zilipita kimya bila kupata jibu lolote.

Baadaye mwanafunzi mmoja tu alijubu "ni alama ya Chaki" Mwalimu aliwauliza tena Je alama hii inafafana na nini? mara hii hakuna aliyeweza kutoa jibu lolote ijapokuwa wanafunzi wote walitafakari kwa makini sana.

Swali hilo lilipoulizwa katika shule ya watoto wadogo majibu yake yalikuwa mengi hata yalifikia zaidi ya aina 20.

Watoto waliifananisha alama hiyo ya chaki na Kiluiluwi,nyuki, nyota, wadudu.

Hivyo inadhihirisha kwamba mawazo ya watoto wadogo ya kufananisha hayana mpaka wala upeo. Wakifahamu mambo mengi zaidi Einstein mwanasayansi maarufu naye aliwahi kusema: "Mawazo ya kufananishaa ni muhimu zaidi kuliko ujuzi. Kwa sababu ujuzi una kikomo, lakini mawazo ya kufananisha yamejumlisha mambo yote ya humu duniani yakasukuma mbele maendeleo na ni chemichemi ya kuendeleza ujuzi." Hivyo tunaweza kusema kwamba mawazo ya kufananisha ni msingi wa uvumbuzi. Hakuna uvumbuzi wowote wa kisayansi ambao haukuanzia na mawazo ya kufananisha au mawazo ya mazingaombwe.

Basi kukuza mawazo ya kufananisha ya watoto ndiko kukuza uwezo wao wa kufanya uvumbuzi hapo baadaye.

Mawazo ya kufananisha yanaweza kukuzwa kwa kupitia mazoezi fulani fulani. Mimi nimewahi kujaribu kwa njia mbili:

Ya kwanza ni kuyaongoza mawazo ya watoto kwa kuwasimulia mashairi, hadithi au kuwaelezea maana ya michoro au nyimbo, jambo ambalo huyafanya mawazo ya watoto kuota mabawa yakaruka mbali yakifuatana na maelezo ya kuvutia.

Njia ya pili ni kuwaambia watoto waangalie mbingu ya kibluu, halafu waambie wafumbe macho na wafikirie mandhari waliyoona.

Baada ya mazoezi ya mara kadha watoto wanaweza kupata picha ya mbingu ya kibluu wakati wowote ubongoni mwao.

Hali kadhalika wanaweza kupata picha ya mbuga isiyo na kikomo, farasi anayekwenda shoti au kundi kubwa la kondoo na mbuzi.

Vivyo hivyo kuanzia mambo madogo mpaka mambo makubwa. mazoezi kama hayo hata yanaweza kuwafanya watoto kukumbuka masomo ya darasani na kufanya hesabu kwa moyo.

Uwezo kama huo huongeza ari za watoto katika kujifunza na kuchunguza mambo.

Ukristo nchini Tanzania ulianzaje?

lUkristo uliingia Msumbiji kabla ya Tanzania

WAJERUMANI wamechangia sana Ukristo kuingia Tanzania. Kabla hata Daktari David Livingstone hajaingia Zanzibar na kusafiri ndani ya Tanganyika kuelekea Ujiji tayari Wajerumani walishaleta Ukristo pande za Kusini mwa Tanzania.

Ni wajerumani hao hao ndio wamekuwa watu wa kwanza kufikisha Ukristo katika mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania ya Kilimanjaro na Arusha.

Wamisionari wa Kijerumani ndio waliofungua misheni ya kwanza ya kanisa la SDA katika eneo la Giti Miamba huko upare, Kilimanjaro katika mwaka 1888.

Eneo la Kusini mwa Tanzania ambalo lilikuwa la kwanza kupokea Ukristo kabla ya maeneo mengine ya Tanzania, liliupokea kutoka Msumbiji kwani kabla maeneo hayo yalikuwa chini ya himaya ya Wareno hususan kwa masuala kidini.

Wamisionari kwa White fathers pia ndio waliofika Kilema Moshi mwaka 1889 huku baadhi yao wakiwa wameingia Tanzania kutoka Kenya na mbegu za Kahawa, walizozisambaza Kilimanjaro yote kiasi cha kupelekea ukanda huo kutegemea zao hilo kwa masuala ya kujinufaisha kiuchumi.

Tangu mwaka 1612 sehemu ya Kusini Magharibi ya Tanzania ambayo leo inafanya majimbo ya Songea, Mbinga na Njombe ilikuwa ni sehemu ya eneo la Kanisa la Msumbiji. Eneo hilo wakati huo liliitwa Prelature Nullius of Mozambique.

Ukristo ulishaingia huko Msumbiji zamani sana kabla ya hapa Tanzania .

Vasco Dagama alikwenda Msumbiji mwaka 1498, na mra kazi ya uenezaji wa Ukristo ilianza huko.

Hivyo Vasco Dagama alichangia kwa kiasi kikubwa ukristo kupenya kuingia Tanzania.

Mjesuiti Goncalo da Silveira alianza kazi ya Umisionari na akauawa kama shahidi mwaka 1561, baada ya kuwabatiza viongozi na watu 500. waliokuwa wakifanya kazi katika jumba la mfalme mara baada ya kuhubiriwa Injili.

Msumbiji ikawa chini ya jimbo la Goa huko India ambalo nalo pia lilikuwa likishikiliwa na Wareno

Mwaka 1612 Msumbiji ikatengwa na Goa na ikafanywa jimbo linalojitegemea na sehemu zetu za majimbo ya Songea, Mbinga na Njombe zikawekwa chini ya jimbo hilo la Msumbiji.

Lakini shida ya usafiri ilikwamisha sana shughuli za Ukristo kupenya kuingia Tanzania.

Upande wa Kusini mto, Ruvuma ulikuwa ni kikwazo kikubwa kuvuka.

Wamisionari waliofanya kazi huko Msumbiji hawakufika Songea kuwashughilikia watu waliokuwa chini ya jimbo lao.

Huko Kusini mwa Tanzania japo sehemu hiyo ilijulikana kuwa ni ya Kikanisa dini ya Kikristo haikihibiriwa kwa miaka yote hii tangu 1612 hadi mwaka 1898 walipofika wamisionari Wabenediktini wa Mtakatifu Ottilia.

Wamisionari hao Wabenediktini wa Mtakatifu Ottilia kutoka Ujerumani walifika Tanganyika kwa mwaliko wa Wakoloni wa Kijerumani ambao walikwishafika Tanganyika mwaka 1884.

Hapo mambo makubwa mawili yaliingia na wakoloni wa Kijerumani wanafika Tanganyika na miaka hiyo hiyo shirika la Wabenediktini wa Mtakatifu Ottilia lilianzishwa Ujerumani kwa ajili ya kueneza dini Afrika.

Wakoloni wa Kijerumani hawakutaka wazungu toka mataifa mengine waingie Tanganyika kueneza Ukristo. Hivyo ili kuhakikisha wanafanikisha azma yao hiyo waliwaalika wamisionari wa Mtakatifu Ottilia lilianzishwa Ujerumani kwa ajili ya kueneza dini Afrika.

Wakoloni wa Kijerumani hawakutaka wazungu toka mataifa mengine waingie Tanganyika kueneza Ukristo.

Hivyo ilikihakisha wanafanikisha azma yao hiyo waliiwaalika Wamisionari wa Mtakatifu Ottilia, Wajerumani wenzao kuja kueneza dini nchini Tanganyika ili wasije Wamisionari wa Mataifa mengine hasa Wabelgiji na Wafaransa wakafika kueneza dini sehemu zote zilizokaliwa na Wakoloni wa Kijerumani.

Hivyo tofauti za Kisiasa zilizopelekea, Wajerumani peke yao kuwa Wamisionari pekee waliofanikiwa kupenyeza Ukristo na kupenyeza Ukristo na kuuingiza nchini Tanzania kwa mara ya kwanza.

Wakati wa utawala wa Waingereza nchini Tanganyika Wamisionari toka Mataifa mengine waliozuiliwa kuhubiri wakati wa Wajerumani nao pia waliingia nchini.

Kutana na wapiga picha waliokubali kuumwa na nyoka pia wanyama wakali ili kufanikisha kazi yao

lNdio wapiga picha bora wa filamu za wanyama

KWELI kupenda ni wazimu, mtu akipenda kitu anaweza kufanya vituko vinavyoweza kupelekea awaache watu hoi bin taabani bin Mahututi kwa nini nasema hivyo?

Kwa takribani miaka 35 sasa Allan Root na mkewe Joan Root wameonyesha maajabu katika fani ya upigaji picha za wanyama.

Ni wao ndio wapigaji picha sinema za wanyama waliofanikiwa kupiga matendo ya wanyama ambayo ni nadra kunaswa na picha.

Wamepiga picha

za ndege wakiangua mayai na kulisha watoto wao, wanyama wakizaa, nyoka akitema mate ya sumu na wanyama wanaoishi chini ya maji wakijitafutia mawindo yao.

Joan amenusurika kufa baada ya kukwanguliwa na mnyama aina ya kiboko usoni wakati wakiwa katika harakati za kumpiga picha chini ya maji.

siku hiyo hiyo Allan mumewe Joan aling'atwa na Kiboko Mguuni kiasi cha kuumia vibaya na kulazwa hospitalini miezi miwili.

Matukio yote hayo yakawapata wakiwa wanapiga picha za wanyama chini ya maji ya kisima cha Nzimba, kisima cha asili chenye wanyama wa kila aina ndani yake kikiwa ndani ya mbuga za wanyama yya Tsavo.

Allan pia tayari amepoteza kidole kimoja baada ya kung'atwa na nyoka kiasi cha sumu yake kupelekea kidole chake kikatwe katika jaribio la kumpiga picha nyoka aina ya Swilla akitema mate ya sumu Joan alivaa miwani kisha akamchokoza nyoka na kukubali amtemee mate ya sumu kusudi mumuwe Allan apate kupiga picha kitendo hicho.

Wamemudu pia kunasa picha za Malkia wa mchwa akiwa ndani ya kichuguu chini picha ilivyowapa taabu kupiga kuliko picha iliyowapa taabu kupiga kuliko picha zote walizopata kutengeneza za wanyama na wadudu.

Miongoni mwa mbuga za wanyama ambako Allan na mkewe Joan wamepiga picha zao katika mazingira ya hatari ni pamoja na Tsavo na masai mara nchini Kenya, na Ngorongoro na Serengeti nchini Tanzania.

Kwenye mbuga ya wanyama wa Serengeti wamepiga picha za wanyama kwa kutumia ndege yao ndogo iitwayo Oscar Charlie pia nyakati zingine wametumia mwamvuli uwakao (Ballons).

Kwenye nyumba yao wanayoishi karibu na ziwa Naivasha huko Kenya wamefuga wanyama wa kila namna wakiwemo fisi, Mbweha,Sokwe, na Ndege wa aina mbalimbali. Wanyama wa porini huketi nao mezani wanapokula chakula.

Nyumba yao ni kama mbuga ya wanyama pia wanafuga kiboko ambaye Allan hufanya naye mazoezi ya kuogelea ndani ya ziwa Naivasha.

Allan na Mkewe Joan walizaliwa Kenya walikutana mara ya kwanza wakiwa vijana wadogo na wakagundua kuwa wote walipenda sana wanyama, upendo wao ulianzia hapo na wakaishia kuoana.

Joan alizaliwa kwenye familia ya wakulima wazungu wenye uraia wa Kenya.

Wazazi wake pia walikuwa wazungu wa kwanza kuanzisha kampuni ya upigaji picha za filamu nchini Kenya.

Allan kwa upande wake aliacha shule akiwa na umri wa miaka 15 tu. Baada ya kuacha shule aliamua kufanya kazi moja tu kupiga picha za wanyama.

Akiwa na umri wa 18 aliazima kamera na kupiga picha kadhaa za wanyama porini ambapo aliziuza kwa watengeneza filamu za wanyama.

Mwaka 1964 yapata miaka 2 tu toka waoane wote wawili walichukuliwa na kampuni ya SURVIVAL ili wakapige picha za filamu ya wanyama katika visiwa vya Gallapagos

Vipo vitu kadhaa vilivyochangia Allan na Joan kufanikiwa kufanya kazi katika mazingira hatari kwanza wanasubira ni wavumilivu ni wajasiri wanao upendo kwa wanyama na kwa bara la Afrika wanakoishi, wamegundua mambo ya ajabu katika maisha ya wanyama ambayo pengine yasingelijulikana kama siyo juhudi zao.

Watoto Watakatifu: Waliuawa kwa amri ya Herode

"HUENDA ipo siku mtoto huyu ataninyang'anya ufalme wangu hapa Yudea" mara kwa mara mfalme Herodi aliwaza na kuwazua juu ya jambo hilo. Wazo hili likamfanya atoe amri inayoashiria dhahiri kuwa wapo binadamu wenye unyama zaidi ya unyama ule wa wanyama wa mwituni.

Maskini kwa uchu wa madaraka ya dunia, akatoa amri hiyo ya mauti kwa viumbe wadogo namna hii, tena wasio na hatia. Pasi kujua kusudi la kuzaliwa kwa Yesu kama alivyoelezea mwenyewe alipo karibia kufa kuwa hakuwa na haja ya mamlaka ya duniani, bali alitaka kuitawala mioyo ya watu, akaamuru watoto wote wa kiume wenye miaka miwili na chini yake wauawe.

Ndugu yangu msomaji unajua mambo yalikuwaje hadi siku ya Desemba 28, ikawa maalum kwa ajili ya kuwakumbuka watoto watakatifu wafiadini sambamba na watakatifu kadhaa wa Afrika kama Mtakatifu, Teodori aliyekuwa mtawa nchini Misri na wengine akina Kastor na Rogasian waliokuwa wafiadini wa Afrika Kaskazini.

Ulikuwa ni mtego wa panya uliokusudia kuwanasa waliokuwamo na wasiokuwamo. Lakini, "Kamba zile za karatasi" zilizotumika kwa kudhaniwa kuwa ni chuma zingeweza kuvuta kichwa cha treni? au kamba za msusa ni vipi zingemfunga na hata kumzuia baunsa asiondoke?

Unajua mambo yalikuwa hivi:- Mamajusi wale wataalamu wa nyota walikuja Yelusaremu toka nchi ya Mashariki ili wapate kumwabudu Bwana Yesu Kristo na ndio walioileta habari ya kuzaliwa kwake Yesu.

Walikuwa ni wageni katika nchi hiyo na hivyo hawakuwa wakiijua njia ya kwenda Bethlehemu wakamuendea mfalme Herodi ili apate kuwaelekeza na pengine hata awape msaada wowote unaoweza kuwa.

Masikini!! Hawakuwa wakijua kuwa kwa kufanya hivyo, walikuwa "wanamuunguzia picha" maana Herodi hakuwa na habari yoyote hata kidogo juu ya kuzaliwa kwa Yesu.

Hata wale walimu wa Sheria walizidi kumwambia Herodi kijiji husika alipozaliwa Mfalme wa Ulimwengu ni Bethlehemu Herodi akawaruhusu Mamajusi wale waende kumwabudu mtoto yule kisha warudi kumhabarisha mahali rasmi alipo Yesu ili naye aende kumtukuza. "Nendeni mkamwabudu mtoto na baadaye mnipe habari za mahali alipo ili nami nikamtukuze".

Lakini watu hao wa Mungu wakaonywa katika ndoto ili wasifanye kosa kurudi kwa Herodi maana lolote baya lingeliwatokea.

Ndoto hiyo kweli ikawa imewaongoza na kuwalinda mamajusi wale.

Mfalme Herodi akasubiri na kusubiri; kwa uchu usiomithilika, maana yeye alijua kuwa mfalme aliyezaliwa ni hatari mno kwa utawala wake na huenda ingekuja siku akaweza kumnyang'anya ufalme wa Yudea. kwa hiyo kwa kuhofia kupoteza madaraka yake, akawahi kutoa amri ile mbaya na ya kinyama.Akaamuru eti watoto wa kiume wote mjini Bethlehemu wenye umri wa miaka miwili wakamatwe na kuuawa mara moja.

Hata hivyo Mwinjili Mathayo katika Injili yake ameonesha dhahiri kwamba Herodi hakufahamu kwamba dhumuni la Yesu Kristo kuzaliwa halikuwa ufalme wa dunia hii, bali tu, kuotawala mioyo ya watu na hata kuwakomboa.

Hivi kweli "kamba hiyo ya msusa" ni vipi ingemudu nguvu na uzito wa baunsa? Hivi yeye (Herodi), alisadiki kabisa kuwa huu ndio ulikuwa mpango madhubuti wa kumuua Yesu wakati huo?!

Siku ya kuwaheshimu watoto Watakatifu hao kama wafiadini waliouliwa kwa ajili ya Bwana Yesu bila kumshudia kwa maneno yao bali tu, kwa mateso na vifo vyao, inatufikirisha kuwa hakubaki mwanadamu yeyote awezaye kuuthibitisha mpango wa Mungu na kuugeuza atakavyo yeye.

Mfano mzuri ni zamani zile za kale wakati Farao wa Misri alipojaribu kuutangua mpango wa Mungu kwa kuamuru watoto wote wa kiume wauliwe.

lakini hata hivyo, Musa aliokolewa; akawa mwokozi wa Wayahudi na tena Kiongozi wao.

Ni ukweli usiofichika kuwa Yesu ni Mkuu kuliko Musa , na ni mwokozi wa watu wote watakao kumfuata.

Kama vile Farao, Mfalme Herodi naye alijaribu kumuondoa yule aliyemuona atakuwa hatari kwake pasi na kujua kuwa aliandaliwa kwa makusudi mazima na Mungu mwenyewe.

Lakini kama vile Musa wa zamani Yesu naye aliokolewa kwa nguvu ya Mungu akawa Mwokozi

 

Kwa nini kama taifa tunahitaji msingi wa maadili (2)

Mungu anatutaka kwa pamoja tujenge jumuia kadiri ya mipango yake. Je imani yetu katika Mungu inatusaidia kukubali ukweli huo?.

Lazima tuhoji hilo kati yetu. Katika mambo kama ndoa, elimu ya maadili Shuleni, kazi ya dini katika siasa tunaweza kutofautiana mintarafu jinsi ya kuyaratibu ingawa tunakubaliana kwamba Mungu ni muumba wa yote. katika maisha ya jamii hapa kunaweza kuzaliwa utata, wengine wanataka kutojishughulisha na suala hilo na kutaka kuishi kwa amani kwa kutenganisha dini na siasa. Neno hili tutaligusia tena ekatika sehemu za 2 na 3.

Inafaa tuone ni wapi tunapoungana katika imani yetu katika Mungu muumba kabla ya kuangalia tofauti zetu.

- Kusadiki kuwa Mungu ndiye muumba wa wote ni kushika pia na binadamu na viumbe vyote.

Dini zote zadi kuwa tuheshimu uhai, tuseme kweli, tujali mali ya wengine tuishi vema kimaadili tuwaheshimu wazazi na wazee na tuwapende watoto. Kanuni za kupanga maisha yetu kiuchumi na kisiasa zajegwa hapa.

Dini zote zakubali kwamba maisha mema ni zaidi ya kushika tu sheria. Utu wema upo ndani ya nafsi ya Mungu. Huu ndio unaotusukuma kuwatendea wengine mema. Mtu mwema huwatendea wengine anavyotaka wengine wamtendee yeye.

Mambo hayo tunayoyathamini pamoja kama mema ndio msingi wa kujenga pamoja licha ya tofauti zilizopo kati yetu. Zinapojitokeza tofauti na mivutano yatubidi kurejea kwa msingi huo.

Tabia ya watu katika jamii yaweza kuhisiwa imejengwa katika msingi imara. Watu wakifanya purukushani hapa madhara yaweza kutokea hata jamii kusambaratika.

Wakristo, Waislamu, washika dini za jadi wote kurejea kwa msingi uleule, ndio kusema sisi sote:

w Tunamthamini kila binadamu na mkuu wa ubinadamu na wa dhamira.

w Tunakubali kuwa kuamua lipi ni jema , lipi baya sio madaraka ya binadamu awe na uwezo wa kijeshi , kisiasa, kiuchumi au kidini.

wTunaamini kuwa upendo, huruma, ukweli, uwazi huendeleza utu wakati chuki, uadui, ubinafsi na mabavu humdidimiza.

Tunajali kwamba fukara na walemavu lazima watunzwe na waonje heshima yao. Vinginevyo watabakia nyuma kama raia hafifu.

Mtazamo wa kiutu sharti uundwe hauji wenyewe. Lazima tujifunze:

w Kuwa watu wa wazi

w kuwa waaminifu

w kuepuka ubinafsi na roho mbaya

w kuamini kuwa wengine ni wema

wKujua ni za wenzetu.

Binadamu wamekuwa wanatafiti wafikie msingi huu wa pamoja wa kuwaongoza wote. Majaribio ya hivi karibuni yameratibishwa katika Tamko la Haki za Binadamu ( 1948) na hapa Afrika kumekuwa na Hati ya Afrika ya Haki za watu (1981) iliyoanza kutumika mnamo 1986.

Ibara nyingine zenye fundisho hilo tumezinukuu katika viambatanisho mwishoni mwa kijitabu hiki.

Wadhamini wa msingi huo

Umuhimu wa msingi tunaozungumzia hapa upo hivyo kwamba lazima uangalifu uwepo ili kuulinda, ili udumu na uwe na uwezo wa kutumika.

Jamii ya watu lazima iwe macho na vikundi maalum vya watu lazima viongozwe kuulinda msingi huu uwe msingi wa maisha ya watu. Historia yaweza kudai marekebisho fulani fulani, lakini kanuni lazima zibakie.

Tumeona katika kijitabu cha kwanza kuwa Tanzania sasa hivi inapitia kipindi cha mageuzi kuendea siasa ya vyama vingi.

Marekebisho yafanyike lakini bila kukiuka misingi yetu ya kimaadili na yenye manufaa kwa wote.

Ni nani anayepanga mwelekeo katika mageuzi ? Tunazingatia kanuni ya heshima usawa na kujali usawa na kujali mapendeleo ya wote? Au, je masuala ya uchumi ndio yanayoathiri maamuzi bila kujali.

Je watu wanatawala hatima za maisha yao? Wana uamuzi katika upangaji siasa au wanalazimika kufuata mambo ambayo hawakuchagua? Je mathalani siasa za sasa hivi mintarafu mishahara afya, elimu zinazingatia hali halisi au zinafuata tu kanuni za uchumi? Nani wadhamini kuona kuwa utanishi kadiri ya kanuni tulizo jiamulia?

Hayo ni maswali ambayo lazima tuendelee kujiuliza sio viongozi wa siasa peke yao ndio watakotuamulia siasa zetu. Wapo wengine wanaozipasisha kanuni za kimaadili na wanaolinda yale tunayoyathamini na tunayotoka yaongeze maisha yetu.

Wadhamini na wenye kulinda msingi wetu wa kimaadili ndio hawa:

w wazazi: warithishao mila za mapokeo na za kisiasa; hao huelekeza mitazamo ya watoto.

w Walimu: walio katika mfumo wa elimu kadhalika wasanii, washairi na waandishi.

w Viongozi wa siasa wa dini na wanataaluma

w Vyama huria, vikundi vya watu wenye mapendeleo sawia n.k.

Je tunaweza kusema kuwa waweka mielekeo hawa wanapewa umuhimu unaostahili katika jamii yetu? Mathalani je wazazi huulizwa kitu juu ya masuala ya Elimu? Wafanyakazi wanaulizwa maoni yao kabla ya zoezi la upunguzaji wa wafanyakazi ingawa hatupo kijijini lakini bado maamuzi ya kitamaduni y anaarifu tabia zetu pamoja na mambo mengine mengi.

Yafaa tukubali ugumu uliopo na kujali kuhakikisha kuwa kanuni zetu zaendelea kuongoza tabia zetu. Inabidi tuwe wazi juu ya mambo yaliyo mema na yale yaliyo mabaya. Na hapa lazima tushirikiane.

Haiwezekani kuacha mambo mikononi mwa wenye mamlaka yawe ya kisiasa au kiuchumi. Hao waiachiwe kamwe kufanya mambo peke yao, watu wenyewe walio wadhamini wa misingi ya kimaadili ya jamii yetu ndio wapewe fursa kuelezea mambo kwa manufaa ya jamii yetu ndio wapewe fursa kuelezea mambo kwa manufaa ya jamii nzima. Hao wahimizwe kusema wazi na wapewe fursa ya kutimiza wajibu wao. Ndio kusema wazazi, walimu, viongozi wa dini na vyama huria wawe watendaji.

Ili kutekeleza hayo, mengi lazima yatabadilika. hapa Tanzania mtindo mpya wa siasa upendekezwe wakati mitazamo ya watu bado ni ile ya zamani ushirikishwaji hauhimizwi na viongozi sasa hawaelekei kupendelea neno hilo.

Wengi wa wadhamini wa misingi yetu ya maadili hawaelekei kuona njia ya kufanya wajibu wao. Wanasubiri kuambiwa.

Wapo lakini viongozi wengine wa dini wanaofanya wajibu wao. Hawa wameanza kutoa matamshi yao waziwazi hata kama sio kila wakati yanapendeza masikio ya viongozi wa siasa.

Tujaribu hapa kuona makundi hayo yenye mamlaka ya kuona kuwa tunatunza yale

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

Daraja latumiwa kwa ibada za Shetani Afrika Kusini

DARAJA moja refu na kubwa lililoko umbali wa kilometa 10 nje kidogo ya jiji la Port Elizabeth sasa limeingia kwenyee orodha ya sehemu mashuhuri nchini Afrika Kusini.

Daraja hilo halijajipatia umashuuri huo kwa kumudu kuvusha vyema bali kukithiri kwa idadi ya vijana wa kiume na kike wanaolitumia. kijana hulitumia kwa kutoa kafara ya dini ya waabudu shetani inayokua na kushamiri kwa kasi huko Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa gazeti la "Rand Mail" linalochapishwa Johanesburg mpaka sasa idadi ya vijana wapatao 15 wameripotiwa kujiua kwa kujitupa toka juu ya daraja refu kupita yote nchini Afrika Kusini.

Pamoja na vijana kujiua kwa kujitupa toka juu ya daraja hilo, vijana hao pia wamekuwa wakilitumia kwa uhalifu kama uvutaji bangi, kupangia mipango ya uporaji, ubakaji na utekaji nyara magari na watu wanao pita maeneo hayo.

Polisi katika jiji la Port Elizabeth wameanzisha msako mkali unaolenga katika kuwasaka vijana wote ambao ni wafuasi wa mafundisho mageni ya ajabu yanayowapelekea wajutupe kutoka juu ya daraja.

Vijana ambao tayari wamekamatwa katika msako huo wanafikia 100 na watachuguzwa akili zao kisha kuwekwa chini ya uangalizi maalum wa madaktari wa matatizo ya akili.

Wakati polisi wa Afrika Kusini wakitatua tatizo hilo kwa kukamata vijana wanaowashuku kuhusiana na ibada za ajabu katika daraja hilo, Mtaalamu mmoja wa sayansi ya jamii nchini humo Paul Holones ametoa ushauri tatizo hilo lishughulikiwe kiimani zaidi kuliko kutumia nguvu ya dola.

Bw. Holmes ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, ameendelea kufafanua kuwa kwa vile vijana hao wanafanya vituko hivyo kwa kufungamanishwa na imani zaidi kutatua matatizo yao masuala ya kiimani yangepewa kipaumbele.

Katika matukio kadhaa vijana wa kiume wamejiua kwa kujitupa toka juu ya daraja hilo wakiwa na wapenzi wao wa kike. Wengi wa vijana wanao umri kati ya miaka 15 mpaka 28.