Make your own free website on Tripod.com

Hakuna Mungu anayetafutwa katika mgogoro K.K.K.T Mwanga

Na Herman Mshana

KISHERIA Kanisa ni kikundi cha watu wenye itikadi moja ya kidini waliojikusanya na kujiita hivyo na pengine wakasajiliwa pale ambapo sheria za nchi zinawataka wafanye hivyo.

Kibiblia Kanisa ni mwili wa siri wa Kristo na hauna mipaka ya kimadhehebu.

Lakini lililo kuu zaidi, kanisa ni chombo cha kiroho ambacho ni njia ya kuwafikishia watu ujumbe wa Mungu na pia ni chombo cha malezi kwa watoto wa Mungu.

Ni chombo cha kumtafuta na kumdhihirisha Mungu.

Kama hivyo ndivyo ilivyo, Kanisa lina wajibu mkubwa zaidi katika masuala ya kiroho kuliko lilio nao katika masuala ya kimwili.

Hii haimaanishi kuwa kanisa halina budi kuwajali watu katika shida zao za kawaida za kimwili, bali kukazia tu kwamba wajibu mkuu wa kanisa ni katika masuala ya rohoni.

Hivi karibuni mvutano uliokuwa umefifia kwa miaka kadhaa miongoni mwa Wakristo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Pare; ambako waumini wa wilaya ya Mwanga wanadai wawe na dayosisi yao, umefumuka upya na kwa namna inayotisha.

Matukio kadhaa yakiwemo ya wachungaji kupigwa na waumini, uharibifu wa makusudi wa mali, kutukanana, mifarakano hadi katika ngazi ya familia ni machache kati ya yanayonifanya na kuwafanya wengi kujiuliza, Je, yupo Mungu yeyote anayetafutwa katika mgogoro huo?

WILAYA ya Mwanga iliyo katika mkoa mdogo kuliko yote wa Kilimanjaro lakini wenye wilaya nyingi ina umri wa miaka ipatayo 20.Awali wilaya hiyo ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Pare kabla ya kugawanywa na kupatikana wilaya mbili; hiyo ya Mwanga na ya Same.

Hivi sasa Mwanga ambayo Wakristo wake karibu wote ni Walutheri ni jimbo la Uchaguzi pia kisiasa, lakini katika muundo wa utawala wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Same inakamilika katika wilaya zote mbili, ya Mwanga na ya Same.

Wenyeji wa wilaya hizo (wa dayosisi hiyo) ambao ni Wapare wamegawanyika katika makundi makuu mawili kiutambulisho. Makundi hayo ni ya Wapare wa Kaskazini ambao ni wa wilaya ya Mwanga na baadhi ya maeneo ya bondeni ya wilaya hiyo na Wapare wa Kusini. Kaskazini katika wilaya ya Mwanga(eneo la milimani) nako kuna makundi mawili ya Wasangi na Wagweno; Wasangi wakiongea Kipare na Wagweno wakiongea Kigweno, lugha ambayo haieleweki kabisa kwa Wapare wengine.

Nia ya kutoa kidogo taswira ya Dayosisi ya Pare ni ili msomaji aweze kuelewa yale ambayo kwa mtazamo wangu ndiyo kichocheo cha hicho kinachoitwa mgogoro wa KKKT Mwanga.

Wale wanaodai kwamba Mwanga wawe na dayosisi yao wanadai kuwa kwa kufanya hivyo wataweza kuleta maendeleo zaidi katika eneo la dayosisi yao ambayo kimsingi ni Wilaya ya Mwanga au Jimbo la Uchaguzi la Mwanga. Wanadai kwamba kuwa kwao ndani ya dayosisi moja na Walutheri wa Wilaya ya Same kunakwamisha maendeleo yao, hasa kwa vile kiuchumi Wapare hao wa Kaskazini (Mwanga) wana rasilimali nyingi zaidi kiuchumi ambazo inalazimika zigawanywe kwenda kwa wenzao wa kusini "kusiko na kitu."

Hoja nyingine ya muda mrefu ilikuwa kwamba Askofu na viongozi wengine wa Dayosisi ya Pare ni wafujaji na kwamba wamekuwa wakielekeza nguvu nyingi katika kuwaendeleza Wapare wa kusini na kuwatelekeza wa Kaskazini. Viongozi wa Dayosisi ya Pare wanaokataa kuundwa kwa dayosisi hiyo wanasema ni mapema mno kuigawa dayosisi hiyo na kwamba njia zinazotumika kuidai ni haramu kwa vile hazifuati utaratibu wala katiba.

Lakini kwa mtazamo wangu wanaodai Dayosisi wanaongozwa na roho ya uchoyo na ubaguzi wa kimaeneo ambao ni wa hatari si tu kwa Kanisa la K.K.K.T, bali kwa Wakristo wote nchini na taifa. Hivi tukianza kusema kwamba kwa sababu Mwanza kuna utajiri wa madini, basi ijitenge ili ifaidi peke yake matunda ya rasilimali zake, na mikoa mingineyenye rasilimali ifanye hivyo hivyo tutafika wapi? Na je, ikiwa mkuu fulani wa mkoa na watendaji wake watafuja mali za umma, baadhi ya wilaya zidai kuwa mkoa? Je, Ulimwengu utajifunza nini kwa Kanisa ambalo linapaswa kuwa kioo cha jamii na mfano wa kuigwa ikiwa haya ndiyo tunayoyafanya?

Kwa muda mrefu kumekuwa na ubaguzi miongoni mwa Wapare. Kwa mfano vijana wa kaskazini wakioa mpare wa kusini hudharauliwa. Vile vile Wasangi na Wagweno licha ya kupakana na wote kuishi wilaya moja eneo la milimani hudharauliana kiasi cha Wasangi kudai kuwa mwanamke mmoja taahira wa Usangi ni sawa na wanaume 40 wa Ugweno wenye akili timamu!

Mgogoro wa sasa ambao umefikia mahali ambapo ndugu wa familia moja hawatembeleani umekuza zaidi dharau na tofauti hizi, kiasi ambacho kimezaa Babeli (machafuko) ambayo Mungu kamwe hawezi kupatikana ndani yake. Kama Wakristo hili si jambo la kujivunia hata kidogo.

Bila shaka ipo haja ya Wakristo hawa wanaodai maslahi binafsi ya kimwili kupitia visingizio vya kutaka dayosisi kujitosa moja kwa moja katika siasa kwani huko ndiko mahali muafaka wanakoweza kuyadai hayo bila kujipalilia laana kama wanavyofanya sasa.

Au ikiwa ni lazima sana wawe na uongozi wao wenyewe wa kiroho kwanini wasijiorodheshe na kusajili Kanisa lao kama ambavyo tumeona wengi wengine wakifanya?

Kumbukeni Bwana wetu Yesu Kristo alisema: Msijiwekee hazina duniani,nondo na kutu viharibupo,na wevi huvunja na kuiba. Bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi. Kwa kuwa hazina yako ilipo ndipo utakapokuwapo na moyo wako." (Math 6:19-21). Je, utaiweka hazina yako kwenye dayosisi au mbinguni?

 

Uchoraji huwanufaisha watoto (2)

Afya ya mtoto hujengwa tangu anapokuwa katika hali ya mimba. Katika mfululizo wa makala kutoka kitabu cha " Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo" cha Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni la Beijing, China baada ya kuwaletea umuhimu wa mtoto kutambaa mapema, leo tunaendelea na kuona jinsi ya kumwoangoa mtoto mchokozi na uchoraji unavyowanufaisha Watoto

"Je unaweza kubainisha tofauti ya manyoya ya tembo mkubwa na mdogo?" Mwana A alishindwa kujibu, Mwana B akamuuliza tena "Je unaweza kutambua yupi ni twiga dume na yupi ni jike?" mwana A hakuweza kujibu pia, basi mwana B akamweleza huku mwana A akiwa msikilizaji tu na hivyo akawa "Mkia wa Mwana B".

Je nini basi sababu ya mabadiliko hayo? Ziko sababu nyingi , lakini wazazi wao waliona kwamba sababu muhimu ni kuwa mwana B alikwenda kusomea uchoraji mnamo mwaka uliopita.

Mwana huyo si kama alipata maendeleo mema katika uchoraji tu, bali pia katika tabia pia: Akawa mtoto mwenye bidii, utulivu, makini na uangalifu, na ameanza kujua jinsi ya kutumia akili yake na kuweza kujieleza vizuri.

Watoto wanapojifunza uchoaraji hujiokoa katika mawazo mazito, hivyo hupata uwiano mzuri kisaikolojia.

Data zilizopatikana kutokana na uchaguzi uliofanywa katika shule ya watoto wadogo na shule ya msingi zinathibitisha kwamba asilimia 25-30 ya watoto hao wana upungufu wa kisaikolojia. Watoto kama hao wana upungufu wa kisaikolojia. Watoto kama hao wana shida katika kuelewa mambo barabara, nao huwa wakaidi, kiburi, wachokozi bila ya sababu, na hawawezi kujitegemea.

Hali hiyo ya watoto kuwa na upungufu wa kisaikolojia imetokana na malezi mabaya ya muda mrefu. Malezi mabaya husababisha hali ya kutokuwa na uwiano wa kisaikolpjia kwa watoto. hali hiyo inaporudia rudia mara kwa mara, huweza kujenga tabia ya watoto.

Ili kuwatia watoto hali njema ya kisaikolijia inawapasa wazazi wawe na ujuzi kuhusu malezi bora. Kwa upande mwingine, kuwaachia watoto wachore kama wapendavyo ni njia nyingine ya kuwajengea watoto hali nzuri na uwiano wa kisaikolojia.

Hitilafu katika saikolojia au kuwa na kinyongo moyoni kwa watoto huwa tabu kutenzuliwa au kuondolewa kwa haraka kama watu wazima wafanyavyo.

Watu wazima huweza kuondoa kinyongo chao kwa njia ya kuzungumza na marafiki. Lakini watoto huwa hawajui kufanya hivyo ili kwa kuchora kama wapendavyo, ili kueleza mambo yaliyo moyoni mwao. Watoto wanaweza kuonyesha hitilafu yao ya mawazo na uzito wa nyoyoni kwa kuchorachora na hivyo kuwaletea uwiano wa mawazo na moyo.

Mtoto mmoja alipata kuchora duara moja, na alipoulizwa nini maana hasa ya duara lake alijubu huku akiwa nusura alie "duara hili ni pete ya dhahabu na almasi" Baada ya kusema hayo alilia. Kisa chenyewe ni kwamba mtoto huyo aliyepewa pete bandia na shangazi yake, na akaipenda sana.

Usiku alipofanya mazoezi ya hesabu kwa kufuata amri ya mama yake, alikuwa hawezi kutuliza mawazo yake juu ya hesabu kwa kuingalia pete yake huku akifanya hesabu. Mama yake hakupenda mtoto wake kufikiria kitu kingine wakati akijifunza akamnyang'anya pete ile na kuitupa kwenye pipa la takataka. Mtoto huyo hakufurahishwa na jambo hilo lakini hakuwa na la kufanya kwa sababu mama yake alimlazimisha alale baada ya kumaliza hesabu.

Siku ya pili asubuhi alipoamka tu alimlilia mama yake ili arudishe pete yake, mama mtu akamwambia aende mwenyewe kuiokota kwenye pia la taka, lakini takataka zenyewe zimeshatupiliwa mbali na baba yake . Mtoto alilia na kufanya ghasia, lakini mwishowe wazazi wake walimtuliza kwa njia ya kumbembeleza na kumtishatisha.

Jambo hilo lilitia kinyongo katika moyo wa mtoto huyo na hivyo kuchora pete aliyokuwa akiiependa na kukieleza kitu kilichomkera moyoni kwa njia ya michoro yake, na kupungukiwa na uzito uliomlemea moyoni mwake. Moyo wake ukapoa akaweza kutuliza mawazo yake kwenye masomo mapya.

Watoto wanapochora huwa ndio fursa yao ya kujieleza. Wakiwa na uchungu moyoni huwa hawana lugha ya kujieleza, lakini wanaweza kuueleza kwa michoro yao.

Hivyo uchoraji huwasaidia watoto kuwa na moyo wa furaha.

Kutokana na tulivyoeleza hapo juu tunaweza kusema kwamba watoto wanaweza kuongezekewa na akili na kuwa na afya njema ya kisaikolojia kwa kupitia kuchora.

Mtakatifu Antoni wa Misri: Alishambuliwa na mashetani yaliyovaa sura za wanyama

Na Josephs Sabinus

"MSISHANGAE eti kwa kuwa mfalme ametuandikia barua, Hata hivyo, Shangaeni kwa kuwa Mungu sasa ametuandikia na kwamba ameongea nasi kwa njia ya mwanae"

Mtakatifu Antoni anayejulikana kama mwanzilishi wa maisha ya kitawa, ndivyo alivyosema wakati mfalme Konstantino Mkuu alipomuandikia barua kuomba sala zake na hali hiyo kuwashangaza watawa wengi.

Inaelezwa kuwa Antoni aliyezaliwa mwaka 251, nchini Misri, kuwa ndiye aliyevikusanya vikundi kadhaa vya Waeremita (wakaa pweke) vilivyokuwa vimetawanyika tawanyika. Akaviweka pamoja karibu karibu na kuviongoza ingawa ni dhahiri kuwa yeye mwenyewe maisha yake yalikuwa ya upweke.

Alipokuwa na umri wa miaka 9 Mtakatifu huyo Antoni, aliyekufa mwaka 356 akiwa na miaka 105, alikwenda uwandani kumtazama mweremia aliyekuwa mzee.

Ingawa tangu mwaka 272, alijitenga na watu akaishi maisha yake ya upweke, hakuridhishwa na maisha ya uwandani. Akaamua kwenda kukaa pangoni. Akiwa huko, mawazo yake yote aliyaweka kwa Mungu huku akisali sana kwa imani na matumaini.

Tunaelezwa kuwa toka ujana wake Mtakatifu Antoni alikaa daima katika hali ya kutokuwa na kitu chochote kiletacho raha wala anasa yoyote.

Kwa kipindi cha uwepo wake pangoni, mashetani yalimwonea wivu, yakamstaajabia na hata kuchukizwa naye. Yakakaa chini kwenye himaya yao; yakapanga mipango kamambe ya namna ya kumkomoa. Yakataka yamtikise kiimani na kumtesa ipasavyo; mradi tu Antoni akome kwenda kufunga na kusali peke yake pangoni.

Mashetani hayo yakavaa sura za wanyama mbalimbali wakali na tena waliotisha na kuogopwa na kila mtu. Yakalizunguka na kulivamia pango huku yakifanya makelele mengi na vitisho vya ajabu ajabu na hata yakamudu kubomoa pango lake.

Laiti kama Antoni asingelikuwa na ujasiri na imani ya kutosha; inayomtegemea Mungu maisha yake yote, angelizimia. Hata hivyo, inaelezwa kuwa kufuatia mashambulizi nusura azimie.

Kilichomuokoa Antoni ni silaha imara ya Imani kwani alizoea mara kwa mara kusema ukweli kuwa, "mashetani huogopa kufunga, sala, uvumilivu na kazi njema inayompendeza Mungu" Imani hiyo ikamponya na akaendelea katika maisha ya mtindo huo hadi mwaka 285.

Akiwa na umri wa miaka 35, Mtakatifu huyu anayekumbukwa na watakatifu wengine wa Afrika kila Januari 17, ya mwaka kama Mtakatifuu Teusa, Veneria, Miselianus, Musius, Fortunatus, Hortisianus, Viktorika, Mistrianus, Viktori, Alba, Leusius, Ingenula,Viktoria, Vinsentia na Timoteusi, walikuwa wafia dini wa Afrika Kaskazini, alienda kushindia kwenye mahame katika milima akiishi kipweke.

Aliweza kukaa kwa takribani miaka 20 bila kuonana na mtu mwingine yeyote tofauti na aliyempelekea chakula kila baada ya miezi 6. Hii ni kwa kuwa alisumbuliwa na watu wengine waliotaka kufuata mfano wake na alitoka huko mlimani akiwa na miaka 54 hivi. Akaanzisha monasteri yake ya kwanza.

Licha ya kufa akiwa na umri mkubwa namna hiyo kama tulivyoona awali, tunaambiwa kuwa mtakatifu huyu hakupata kuugua na hadi kifo chake, hakuwa ameng'oka jino hata moja na wala halikuwepo lililolegea.

Katika uwepo wake juu ya uso wa dunia, Mtakatifu Antoni aliwafundisha watawa wake kutafakari kila asubuhi kuwa pengine wasingeweza kuishi mpaka usiku. Na kila jioni aliwahimiza kutafakari kuwa pengine isingeliwezekana waione asubuhi tena. Tena Antoni aliwahimiza kufanya kila tendo kana kwamba ndilo tendo la mwisho katika maisha yao.

Kwa mujibu wa masimulizi ya namna Watakatifu walivyoishi, mwaka 315 kulipotokea dhuluma na uonevu dhidi ya Wakristo, Antoni alienda Alexandria huko huko Misri kuwatia moyo waliotesekea dini yao.

Akavaa nguo yake nyeupe na ngozi ya kondoo ili aonekane kama mtawala. Hata hivyo alifanya hivyo kwa uangalifu mkubwa ili asiwakasirishe waamuzi kama wengine walivyofanya bila umakini.

Mwaka 355, Maaskofu walimuomba arudi tena Alexandria kuwapinga wafitini wa Arios, akihubiri kuwa Mungu Mwana sio Mtu bali ni Baba.

Lakini alipoombwa na mtawala kukaa zaidi, Antoni alijibu akisema "kama Samaki aliyekufa akitolewa majini ndivyo mtawa anavyofifia akiacha maisha ya upweke"

Kwa nini kama taifa tunahitaji msingi wa maadili

WATU hukasirika wanapowaona wenzao wanafanya mambo kinyume na tabia zinazokubalika katika jamii mfano mtu anapotumia cheo chake kujinufaisha binafsi kwa kujipatia utajiri mkubwa kujijengea majumba ya fahari kununua pajero, kufanya harusi za anasa na fahari kubwa. Hukasirika pia kuwaona watu wanatumia hovyo mali ya jamii, wanapopata mishahara mikubwa kuliko stahili yao. Huudhika pia wasipolipwa haki yao au malipo ya jasho lao yanapocheleweshwa.

Kwa nini watu hudhika hapo? Sababu huyahesabu matendo hayo kuwa mabaya.

Lakini pengine watu hufanya mambo ambayo si sawa lakini bila kuyaona kuwa ni mabaya. Mathalani Tanzania imelimbikiza madeni mengi bila kuongeza tija na pengine fedha kuingia katika mifuko ya watu binafsi. Huku ni kukosa uwajibikaji kwa watu wazima wanaobebesha watoto wao nataifa lao mizigo kwa maisha ya baadaye. Wangapi wanakihesbabu kitendo hiki kuwa ukiukaji wa kanuni za maadili?

Twahitaji kuwa na kanuni za kutuwezesha kupima tabia za watu kuwa nzuri au mbaya. Kanuni hizo hutoa mwongozo kwa jamii nzima na watu binafsi.

Hapo tunaweza kusema, mathalani, namna hii ya kutenda mambo au siasa hii inafuata kanuni zetu au la. Hutusaidia kujibu maswali yafuatayo:

wKwanini watu wavumiliane?

wkwa nini kuwaheshimu watu ambao ni tofauti nawe?

wkwa nini watu wa rangi moja wawajali wale wa rangi nyingine?

wkwanini watu wa dini moja wawavumilie wale wa dini tofauti?

wkwa nini sharti serikali zitumie uwezo wao kujenga amani na kuepuka vita?

wkwa nini kikundi chenye uwezo mkubwa kiuchumi hakina haki kufyonza uchumi wa nchi kwa manufaa yao?

wkwa nini ni lazima tutende mema tuache maovu?

Sio lazima tuende mbali kuona wapo watu wenye tabia za ubaguzi, choyo, aibu na bila subira. Mifano imejitokeza Afrika Kusini, Burundi, Rwanda, Somalia, Sudan na kadhalika. Angalia mkaa wa maadui wa taifa, ubadhirifu na kukwepa kodi.

Hapo ni mifano ya watu ambao wanafikiri matendo yao hayapashwi kufuata kanuni maalum zinazokubalika, wanafuata yalle yanayokidhi haja zao tu.

Watanzania wengine wanafikiri mtu asipogundulika sio vibaya kudanganya. Hivyo kwao tendo lenyewe la kudanganya sio baya ila ukibainika. Kanuni huwa ya nje tu hapa. Ikiwa tutaruhusu tofauti hivi katika mitazamo tutawezaje basi kushirikiana?

Binadamu huzaliwa katika jamii na pamoja wanatakiwa kujenga jamii lakini hili halitokei tu holelaholea . Lazima kila mmoja awe na nafasi yake ya kuchangia maendeleo, kutenda madaraka,kutimiza wajibu na kufaidi matunda ya haya yote. Kulazimishana na kutumia nguvu hakufai lolote hapa Watu lazima wachague kwa hiari yao kuishi pamoja kama wanadamu.

Ni lazima kuwepo kukubalika katika maoni. Kukubalika huko kunamaanisha kuwa tunavihesabu vitu fulani fulani kuwa ni vya muhimu, vya kuvitunza sana na kutowaruhusu watu kuviharibu kadhalika vitu fulani fulani vya hesabika kuwa havifai na tunawazuia watu kuvitenda.

Ndio kusema kama jamii lazima tukubaliane juu ya mitazamo na thamani ya mambo muhimu kijamii.

Jinsi maisha yanavyobadiliaka pamoja na makandokando yake ndiyo tunavyotakiwa kuafikiana.

mila na desturi zetu ni za thamani kubwa lakini, ili zihifadhi umuhimu wao ni lazima nazo zibadilike kuenda na wakati.

Muafaka unaozungumziwa hapa wahitaji watu wote wajitoe kushughulikia kwa manufaa ya wote. Huo ni wajibu wa watu wetu vinginevyo jamii haijengeki.

Umoja na amani hutoweka ikiwa watu wataweka mbele tofauti zao za kikabila, kidini au kilugha.

Hivi lazima mtu ampime matokeo ya matunda yake na akishayatenda akubali kuwajibika kwa matokeo yake.

Maamuzi mengi hufanyika bila fikra katika mwelekeo huoo na hivyo kuidhuru jamii na kubomoa uelewano na mshikamano. Ni vibaya zaidi ikiwa hata hivyo watu hatukubaliana kuwajibika. Hapo kuaminika kunapotea na maelewano kuvunjika..

Ili kuwepo maelewano na uwajibikaji katika jamii lazima watu wakiri kwamba thamani ya binadamu kama binadamu ndiyo kigezo cha kuamua lipi ni jema na lipi ni baya kwa jamii. Sababu ya kuishi pamoja ni kuboresha maisha ya binadamu.

Kuamini msingi huu na kudhamiria kuutendea kazi ndio muhimili wa jamii yetu. Hivi twaamini kuwa lile lijengalo maisha ya binadamu ni bora na lile liyabomoalo ni baya.

Huu ndio msingi wetu wa maadili. ndio kipimo chetu cha tabia katika jamii.

Kwa maoni yetu basi, Kiongozi asiyeshika kanuni atakuwa mroho wa madaraka bila kujali watu wengine huzaa ubinafsi , wizi na ujambazi.

Ni uzingatiaji wa dhati wa thamani ya maisha ya binadamu ndio utakaohakikisha kwamba tabia za watu na maamuzi ya kisiasa hufuata misingi tunayoizungumzia hapa.

Ndipo tutakapoweza kuchunguza tofauti zilizo kati yetu na kuona jinsi ya kushirikiana na hivyo kujenga umoja na mshikamano.

Tofauti zipo Tanzania mathalani kati ya makabila na dini kati ya watu wa mijini na wale wa mashambani kati ya matajiri na mafukara; kati ya wenye kisomo na wasio na kisomo. Hizi ni tofauti zinazoweza kukifanya kikundi kimoja kukifanya kingine watumwa wake. au yawezekana kukiangalia zaidi kikundi kimoja kuliko kingine tena kwa makusudi na kwa purukushani!

Hivi ni muhimu kuafikiana jinsi ya kukabiliana na tofauti hizo katika jamii yetu. Lakini kwa nini tuthamini maisha ya binadamu na jamii yake? Je, hii ni kwa ajili ya kujihami tu au kuna msukumo mwingine unalolifanya hilo la umuhimu kimaadili daima na popote?.

Wapo watu wanaosadiki kuwa hilo ni neno la kibinadamu tu. Mfano ni yule mwizi asemaye kuwa wizi ni mbaya ikiwa ukithibitishwa kuvunja sheria.

Tukisema kuwa jambo latakiwa lifanyike hivi au vile ni ikiwa tunakubaliana vile tunakuwa tunasema kwa binadamu ndiye aamuaye yaliyo mema au la kwa maisha ya binadamu, Wale wanaotetea utoaji mimba, mathalani husimamie hapa.

Tunaweza tu kudadisi kwamba tunatakiwa kuheshimu uhai wa binadamu kadiri muumba alivyokusudia ikiwa tunakubali kuwa Mungu ya juu ya yote na ndiye aliyeupa ubinadamu thamani yake.

Hivi sisi tunalazimika kuyajali matakwa ya Muweza.

Hapo tutakuwa na misingi ya maadili ambayo haitegemei maamuzi ya binadamu tu. Mipaka ya uhuru wa watu huwekwa hapa pia.

b) Twahitaji msingi wa maadili katika jamii yetu ya mchanganyiko.

Walio wengi Tanzania humwamini Mungu. Hata hivyo kuna kumkana Mungu pale watu wanapokataa kukiri kuwa Mungu anayo mipango na maisha ya binadamu ambayo sharti kuizingatia. Kuna tofauti za mila na desturi nchini zitokanazo na tofauti za dini.

Wapo watu wasiojua namna ya kuishi maisha mema.

Wapo wale waliopofushwa na uroho wa mali hivyo kwamba wapo tayari hata hudhuru wenzao kwa mwisho huo wa kupata mali.

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

Ijue dini inayofungisha ndoa na picha ya mchumba

MYUNG Sun Moon ni mtu ambaye jina lake linazidi kuvuma kila kukicha kona zote za dunia.

Mtu huyu jina lake siyo geni kwa watu watu wanaofuatilia kwa karibu habari za kuzuka dini mpya kila kukicha.

Moon ambaye ni mzaliwa wa Korea hivi sasa amejiimarisha sana baada ya kujianzishia dini inayoitwa International Federation for world peace (IFWP). Hii ni dini inayoruhusu ndoa za halaiki.

Ndoa hizi zinazofungwa na Myung Sun Moon mwenyewe ni za ajabu kwa sababu wahusika kufungishwa pingu za misha na picha ya mwenzi tu na siyo mtu halisi.

Dini ya Moona ambayo sasa hivi imesambaa katika mataifa mbalimbali ya Kiafrika ikiwemo Tanzania ambako haina nguvu sana hutafutia watu wa chumba kutoka mataifa mbalimbali duniani baada ya hapo muhusika ama mvulana anayetarajia kuoana naye. Ajabu ni kuwa hata siku ya ndoa anaishia kuoa picha tu na siyo mwenzi binadamu.

Kila mtu anayejiunga na dini ya Moon hunyweshwa kinywaji maalum, ambacho kabla ya kujiunga nao ni sharti ukionje kama ishara ya kula kiapo kuwa mtiifu kwa Moon.

Barani Afrika tayari dini hii imeingia Kenya, Tanzania, Uganda, Afrika Kusini, Nigeria, Zimbambwe na Zambia.

Makao makuu ya dini hii yako Seoul Korea lakini Moon pia analo tawi imara sana la dhehebu lake hili huko Tokyo, Japan ambako ndiko wamisionari wake wa Kijapani hutoka kwenda kuhubiri sehemu mbalimbali duniani.

Dini ya Moon inaamini kuwa Mungu alitoa agizo kuwa watu wazaane wajaze nchi hivyo nao pia wanahimiza waumini wao kuoana wao kwa wao na kuzaa, kutekeleza agizo lao.

Hapa Afrika Mashariki ni mji wa Nairobi, Kenya ndio umevunja rekodi kwa kuwa na ndoa nyingi zilizofungwa chini ya dini ya Moon.

Jijini Dar es Salaam ndoa za Halaiki za dini hiyo zimepata kufungwa katika ukumbi wa hoteli ya Star light mwaka 1997 ambapo vijana wengi wa kitanzania waliopapatikia dini hiyo walifunga ndoa na picha.

Jijini Nairobi ndoa hizo za halaiki zilifungwa kwenye uwanja mkubwa wa Moi International Sports Centre Kasarani ambako mamia ya wakenya walioana na picha za wachumba wao mwaka 1988