Gharama za kurejesha amani ni kubwa kuliko za kuitunza

Na Justine Keto

MOJA ya mambo muhimu na ya msingi sana katika taifa lolote linalowajali watu wake, ni suala la kuwepo kwa amani ya kweli katika taifa hilo.

Ingawa kumekuwepo na tafsiri mbalimbali za neno amani, lakini tafsiri hizo zinakubali ukweli kuwa kuwepo kwa amani ni ile hali ya taifa lolote kutogubikwa au kuzingirwa na machafuko au uhasama wa aina yoyote kama vile wa kidini, kikabila au kisiasa.

Aghalabu kuwepo kwa amani katika taifa liwalo lote, kunachochea na kuimarisha sio tu umoja na mshikamano wa taifa hilo, bali pia kunajenga mazuri ya kuinua maendeleo ya wananchi.

Lakini pamoja na kuwepo kwa amani katika mataifa mbalimbali duniani, viongozi wa mataifa mengi wameshindwa kulinganisha au kutathimini mataifa yao au za kutokuwepo kwa amani.

Uduni au upungufu huo wa kufanya tathimini unasababisha viongozi wengi katika mataifa yanayojiita a"Yenye amani" washindwe kuitunza amani hiyo na wakati huo huo kwa wale viongozi walio katika mapambano ya kuitafuta hiyo amani nao washindwe kuirejesha.

Uzoefu unaonyesha kwamba kuna kazi kubwa sana katika kuirejesha amani iliyotoweka ikilinganishwa na kazi inayokuwepo katika kuitunza au kuiimarisha amani ndani ya nchi yoyote.

Kimsingi mlinganyo huo unapimwa katika suala la gharama za kuitunza na zile za kuirejesha pale inapokuwa imesambaratishwa.

Kwa mfano katika nchi yenye machafuko kama vile ya kivita, nchi hiyo itaingia kwenye gharama kubwa katika masuala nyeti yakiwemo ya madawam silaha na chakula kwani yote hayo yanahitaji fedha 'kichele' ukiachilia mbali misaada mingine ya kutolewa.

Nchi yenye vita vya wenyewe kwa wenyewe itagharimika katika suala la muda kutokana na ukweli kwamba mara nyingi uhasama hudumu muda mrefu kama ilivyo katika Mataifa ya Sudan, Somalia, Burundi, Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Angola, Algeria na hata majirani wa karibu zaidi na Tanzania yaani Uganda. Nchi hizo zote zina machafuko yatokanayo na uhasama ama wa kidini au kikabila pamoja na masuala ya kisiasa mbali na suala la kugharimika katika muda , ambapo muda mwingi huelekezwa katika uhasama, machafuko na mashambulizi, gharama nyingine inayokabili nchi iliyoshindwa kutunza amani, ni kupotea kwa roho nyingi za raia wa nchi hiyo ambao kimsingi ndio nguvu kazi ya taifa.

Nchi kama ya Rwanda inayopatikana na Tanzania mnamo mwaka 1994, inaeleza kuwa ilipoteza malaki ya raia wake wengine kwa kufa, wengine kwa kuikimbia nchi na wengine kupotelea kusikojulikana.

Athari nyingine ya kukosekana kwa amani ni kuathirika vibaya kwa uchumi wa taifa linalohusika kuotokana na ukweli kwamba hazina yote ya Serikali huelekezwa kwenye vita.

Kwa kufanya hivyo Serikali iliyomo kwenye wimbi la vita, hujikuta ikigharimika na kuwa na kazi zaidi huku ikilazimika kuzifanya kazi hizo peke yake.

Lakini katika taifa lengya amani , mara nyingi gharama za kuitunza amani haifanywi na Serikali pekee, bali vyama vya hiari, taasisi za dini na hata vyombo vya habari. Wote hao wataisaidia Serikali katika jukumu la kutunza amani zaidi kwa njia ya uhamasishaji, kuelimisha na hata inapobidi kukemea., kadhalika kwa mtu yeyote anayefuatilia masuala ya demokrasia na haki za Binadamu kwa ujumla, atakubaliana nami kwamba wananchi nao kwa upande wao hufanya kazi kubwa ya kuitunza amani hususan pale panapokuwepo kwa kuchangia hoja za kudumisha amani hiyo.

Lakini ni wananchi hao hao hujikuta wakikaa kimya mithili ya Farasi aliyefungwa lijamu kichwani, na kwa hiyo hushindwa kabisa kufurukuta kwa namna yoyote.

Kubwa wanalowaza wakati huo ni namna ya kuyanusuru maisha yao.

Katika siku za hivi karibuni, Watanzania tumeshuhudia mambo kadhaa ambayo mimi naamini kwamba kama hatua madhubuti na zinazokubalika katika jamii yetu hazitachukuliwa tena kwa haraka basi tunakabiliwa na tishio la kutoweka kwa amani.

Mambo hayo ni pamoja na mwenendo wa kesi mbalimbali za kisiasa na suala la marekebisho ya katiba hususan katika mambo nyeti ya Tume ya Uchaguzi na Muungano.

Sambamba na hayo, Suala la madai ya kunyanyasa wapinzani nayo hayana budi kutazamwa kwa jicho la tai ambaye ni ndege pekee anayeona vizuri zaidi kadri anavyokuwa mbali na kitu.

Kama zama hizi ni za ukweli na uwazi basi ni vema tukaambiana kweli bila kificho kwamba ulevi wa amani utatupeleka pabaya.

Ni vema tujihadhari wakati huu (sasa) kwa katumia Umoja wa Kitaifa katika kuienzi Amani tuliyonayo na wakati huo huo tukiepuka gharama kubwa zinazoweza kutokea wakati ule tunapokuwa tukiitafuta amani kwa ncha ya upanga.

Jinsi ya kumwongoa mtoto mchokozi

Afya ya mtoto hujengwa tangu anapokuwa katika hali ya mimba. Katika mfululizo wa makala kutoka kitabu cha " Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo" cha Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni la Beijing, China baada ya kuwaletea umuhimu wa mtoto kutambaa mapema, leo tunaendelea na kuona jinsi ya kumwoangoa mtoto mchokozi

VITENDO vya uchokozi vinavyofanywavyo na watoto wadogo kama vile kuwapiga au kuwatukana watoto wenzao, kuhodhi vitu bila kuwapa wengine n.k. huwakera wazazi wengi. Kwa kuwa watoto hupenda kujitukuza na kufikiria binafsi ni muhimu kuliko wengine, na kwa kuwa hawana ujuzi wa kimsingi wa kijamii, hivyo njia ya kuwaelezea ubaya wa kutenda hivi au vile tu haiwezi kuwaelimisha vya kutosha, bali inapasa kuwafahamisha pia vitendo vinavyowafaa.

Tunaweza kutoa mashauri yafuatayo kwa wazazi wanaotaka kujaribu kuwaongoa watoto wao wenye tabia ya uchokozi:

1. Jaribu kumuweka mtoto katika mazingira yasiyoweza kusababisha vitendo vya uchokozi. Watoto wadogo huwa rahisi kuathiriwa na mazingira kuliko watu wazima. Majaribio yaliyofanywa yamethibitisha kwamba watoto wengi huacha vitendo vya uchokozi iwapo wataweza kucheza michezo ya aina mbalimbali, kufanya uchaguzi kama wapendavyo, wanaweza kucheza kwa wakati wa kutosha, na wanapata pahala pakubwa pa kutosha kujifurahisha na kujitosheleza.

Aidha, michezo au hekaheka za aina mbalimbali zinazofaa watoto zikifanywa huleta matokeo mazuri. Michezo kama vile michezo ya vikaragosi, michezo ya kuchekesha, n.k. huweza kuwasaidia watoto kutambua kipi ni kibaya na kipi ni kizuri. Hivyo watajaribu kujizuia kutenda kile kisichofaa.

2. Jaribu kuwatolea watoto mifano mizuri katika kushirikiana. Wachagulie vitabu vielezavyo jinsi watu washirikianavyo, wapatie vitu ambavyo huchezewa kwa ushirikiano au washirikishe katika michezo ili watoto wapate fursa kubwa ya kushirikiana na waone matokeo mema ya ushirikiano huo. Pia watoto waambiwe maneno yanayosisitiza umoja na ushirikiano mara kwa mara kama vile ' Napenda mfanye kazi hii kwa pamoja' Au 'Mmefanikiwa kufanya kazi hii kwa bidii nyingi nyote'

3. Msaidie mtoto afahamu hisia yake. Hasira husababisha vitendo vya uchokozi.

Ni bora kumfahamisha ubaya wa hasira na msaidie aikabili hasira yake kwa kitendo kinachofaa.

Hasira ni hisia isiyoepukika kwa kila mtu. lakini si busara kufanya uchokozi wakati mtu ashikwapo na hasira, kwa sababu vitendo vya uchokozi huleta matokeo mabaya zaidi na pengine husababisha ugomvi mkubwa. Hivyo wakati unapomwelimisha mtoto aliyefanya uchokozi kwa sababu ya hasira unaweza kumwambia hivi:'Naelewa kiini cha hasira yako juu ya mwenzako ni kukataa kwake kucheza pamoja nawe hata hivyo ulikosa kumfinya, ungefaa kumwambia una hamu kucheza pamoja nawe.' Maneno kama hayo yamekubaliana na sababu ya hasira yake, na yamekubaliana na sababu ya hasira yake, na yamemfahamisha jinsi ya kuikabili hasira yake kwa njia inayofaa wala si kwa kufanya uchokozi.

4. Vitendo vya uchokozi havifai kupuuzwa. Kitendo fulani cha uchokozi kinachotokea kwa bahati mbaya kinaweza kupuuzwa, na si lazima kisababishe ugomvi. kwa mfano, Mtoto A amemsukuma mtoto B, lakini B hakutia maanani kikumbo hicho akaondoka bila kufanya kitu.

Hata hivyo si vizuri kupuuza kitendo cha namna hiyo japo hakikuleta ugomvi wowote, kwani yule mtoto aliyefanya uchokozi hufikiri kwamba kitendo chake kimekubaliwa na hukirudia baadaye.

Kwa hivyo wazazi wanatakiwa kuingilia kati na kumwambia mtoto B: 'Nenda ukamweleze A asikusukume tena safari ijao' kwa njia hii itakuwa umemrudi mtoto A aliyefanya uchokozi na pia umemfundisha mtoto B njia ya kujiamini pengine hata kwa watoto waliokuwa wakiangalia pembeni watakuwa wamenufaika sana.

5. Jaribu kumfundisha mtoto jinsi ya kutumia lugha safi. Mtoto akijua jinsi ya kutumia lugha ataweza kujieleza na kutoa mawazo yake vizuri badala ya kujieleza kwa vitendo.

Hivyo maarifa ya kutumia lugha huweza kumwepusha na vitendo vya uchokozi. Watoto wengi huwa hawajui jinsi ya kujieleza vizuri kwa lugha, hivyo kwa kujifunza jinsi ya kutumia lugha hupata manufaa makubwa kwa mfano tunaweza kumwambia mtoto '

Ni kweli binadamu ametokana na nyani?

Na Ignatio Obuombe

MNAMO karne iliyopita Charles Darwin Muingereza aliyesifika kwa Werevu wake wa kuchambua elimu ya asili na mabadiliko ya viumbe aliingia ndani ya meli kubwa na kuzunguka karibia kila kona ya dunia.

Lengo la Daruwin la kufanya hivyo lilikuwa ni moja tu kuchunguza viumbe mbali mbali kila pembe ya dunia ili aweze kuvielezea vilianzaje. Safari yake ilimchukua mpaka Asia, Afrika, Australia na hata Amerika. Ndani ya meli alikuwa na wasaidizi wake.

Hapo ndipo Darwin alipoibuka na taarifa kuwa kila kiumbe tunachokiona duniani kiliznza katika hali ya chembechembe ndogo sana, huku kikikua na kubadilika siku moja baada ya nyingine.

Elimu hii ya Darwin ambayo leo, wataalamu wameipa jila la "Evolution" ina maana ya mabadiliko ya kitu au kiumbe kutoka hatua moja kwenda nyingine ambapo hatua mpya inakuwa ni bora kuliko iliyopita.

Ni Darwin huyu huyu ndiye aliyeibua hoja kuwa binadamu alianza kama nyani (primates) baadaye akawa akibadilika kulingana na wakati na mazingira mpaka alipofikia hatua ya kuwa alivyo sasa (Homosaphiens).

Darwin pia akaelezea kuwa ili binadamu atoke kwenye hatua ya nyani ilimbidi apitie hatua ya "Homo Eractus" au "Uprifht Man" Hii ikiwa ni hatua ya kusimama wima badala ya kujikunja kama walivyo manyani.

Mwingereza huyu akafundisha juu ya wanyama wakubwa kama "Dinosaur" ndio mababu za wanyama wote na ndio waliokuwa wakubwa kupita wanyama wowote wale waliopata kuishi.

Tukisoma kitabu kitakatifu cha Biblia kwenye mwanzo tunaelezwa kuwa ni Mungu ndiye aliyemuumba mtu kwa mfano wake. Kisha Mungu huyo akaumba dunia, bahari, mimea, milima na chemchemi za maji.

Darwin anapinga kuwa asili ya vitu havikuanza kwa kuumbwa bali kwa kubadilika badilika. Ubishi wa Darwin leo baada ya kifo chake umepelekea kuibuka kundi la watu wanaoamini sera zake zinazoitwa "Darwinism". Watu wa aina hiyo baadhi yao wakiwa ni Wasomi waliobobea wamepata kutamka kuwa "hakuna Mungu".

Biblia yasema gharika ya wakati wa Nuhu iliharibu sura ya dunia. Darwin naye bila kujijua kwenye maandishi yake aliyoandika wakati wa uhai wake ameelezea kuwa Dunia ilipata kukumbwa na aina fulani ya gharika ambayo ndiyo iliangamiza wanyama wakubwa kama Dinosaur. Basi ikiwa Darwin anakiri kuwa gharika ilipata kuwepo ukweli kuwa chanzo cha binadamu ni kuumbwa na Mungu ni bayana.

Biashara ya viungo vya binadamu yashamiri Afrika Kusini

lRaia watembea kwa hofu

Na Ignatio Obuombe

WINGU la wasiwasi limetanda nchini Afrika Kusini baada ya kuibuka biashara haramu ya aina yake ya kuuza viungo vya binadamu.

Kwa mujibu wa gazeti la "Rand Daily Mail" la Afrika Kusini linaloandika habari za kiuchunguzi, matukio ya watu kutoweka na kupotea katika mazingira ya kutatanisha sasa yameongezeka nchini humo.

Gazeti hilo limeelezea kuwa pamoja na kuwa miji mikubwa kama Johanesburg, Cape Town, Durban na Pretoria jimbo la Gauteng ndilo uchunguzi umebainisha kuwa linaongoza kwa biashara ya viungo vya binadamu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Makao Makuu ya Polisi jimboni Gauteng kati ya watoto 1-5 hupotea kwa wiki jimbo humo na na baadaye miili yao huokotwa huku viungo vyao vikiwa vimeondolea kwenda kuuzwa.

Soko la viungo vya binadamu vinavyotolewa Afrika Kusini limegundulika kuwa liko Marekani, India, Uingereza na Ujerumani.

Kufuatia hali ya maisha kuwa ngumu, baadhi ya vijana wa Afrika Kusini sasa wamegeuka majambazi "Tptsi" kazi yao kubwa ikiwa ni kuteka watu kuwaua kisha kuwanyofoa viungo vyao.

Wakazi wa miji mikubwa ya Afrika Kusini sasa wanaogopa kupanda magari ya watu wasiowafahamu sawasawa.

Katika tukio moja lililotokea jijini Durban hivi majuzi mtoto mmoja mvulana aitwaye "Magulane" aliponea chupuchupu kukatwa viungo vyake na Majambazi wa "Totsi"

Magulane 10, ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Amanzimtoti jijini Durban alikuwa akitembea toka kwa rafiki yake majira ya jioni wakati alipoitwa na watu ambao hakuwafahamu.

Watu hao ambao wote walikuwa wanaume walimwambia Magulane kuwa wancho kikundi cha Sarakasi na wanatafuta vijana wadogo kama yeye wakashiriki.

Lakini baada ya kufika kwenye jengo walimomwelezea kuwa ndiko usajili unafanyika mambo yalibadilika baada ya aliyonekana kuwa Mkuu wa watu hao kuamuru kwa ghadhabu, "Take him to a slaughter house" "Mpelekeni Machinjioni".

Kwa vile mlango ulikuwa wazi Magulane alitimua mbio na baadhi ya vijana wa kundi hili walimfukuza sana lakini walipoona ameingia sehemu yenye watu walimuacha.

Magulane siyo kijana peke yake wa Afrika Kusini aliyeangukia mkononi mwa wafanya biashara ya viungo vya binadamu, wapo vijana wengi waliopoteza maisha na kuchukuliwa viungo vyao. Wapo waliouawa na hawa kuonekana tena.

Zipo baadhi ya hospitali zinazoendeshwa kijambazi nchini Afrika Kusini ambazo pia hujishughulisha na kununua viungo vya binadamu kisha kuvisafirisha nchi za Magharibi kuuzwa.

Uchunguzi wa Polisi nchini humo pia umethibitissha kuwa jamii za "Waasi" wanaoishi nchini Afrika Kusini ndio hujishughulisha na kuuza viungo vya binadamu kupita jamii zingine zote.

Wahindi hao wana soko zuri la viungo vya binadamu katika nchi za Magharibi. Lakini siyo pesa peke yake inayochochea mauaji hayo gazeti la "Rand Daily Mail" inahitimisha kwa kusema kama ilivyo sehemu zingine barani Afrika uchawi na imani za ushirikina nazo ni kigezo kingine kinachochangia.

Selestini wa tano: Mtakatifu aliyejiuzulu Upapa

Aliiacha kazi yake ya Upapa na kurudia Utawa

AKIWA na umri wa miaka 84, alishitushwa na taarifa ya uteuzi ule aliyopewa na ujumbe ule wa Maaskofu wanne na Kardinali mmoja alipokuwa maskani yake.

Mwaka ishirini baada ya kuanzisha Shirika la Walestini lililoenea sehemu kadhaa wa kadhaa katika nchi za Italia, Ubelgiji na Ufaransa chini ya uongozi wake Selestini mwenyewe, shirika hilo jipya la Watawa lilitilia mkazo kanuni ya Mtakatifu Benedikto, lilistawishwa sana baada ya kulifungua kwa kibali cha Papa.

Selestini mwenyewe alizaliwa mwaka 1215, huko Italia akiwa ni mtoto wa kumi na moja kati ya wale kumi na mbili wa familia yao.

Mtakatifu huyu alipotimiza umri wa miaka ishirini hivi, aliingia Umonaki na akaishi pangoni kwa miaka mitatu kisha akasafiri kwenda Roma alikopewa Upadre na kisha kuamua kuishi kwenye milima ya Majella huko Italia.

Tunasimuliwa katika vitabu vya historia za Watakatifu kwa ujumbe ule wa Kardinali na Maaskofu wanne walifikiwa kwa madhumuni ya kumchukua na kumfanya Papa, ulimshitua sana lakini, akauheshimu na kuutii, akachagua jina la SELESTINI WA TANO. Akawekwa wakfu kuwa Askofu wa Roma.

Hata hivyo, licha ya utakatifu wake Selestine hakufaa kuwa Baba Mtakatifu (Papa) na hivyo matokeo yake katika utendaji hayakuwa mazuri.

Hii ni kwa kuwa Selestini hakuwa akizielewa vema sheria za Kanisa, pia Kilatini alichokijua kilikuwa cha 'Kuombea maji ya kunywa' tu.

Hata kazi za ofisini Mtakatifu Selestini hakuzimudu kabisa kiasi cha kwamba mara kwa mara mtawa huyu alikuwa akifanya makosa kadhaa.

Yeye mwenyewe kila mara alishikwa na woga na mashaka alipokabiliana na mazingira yenye utata, magumu na yenye kumfadhaisha.

Akajihisi dhahiri kuwa hakujaliwa uwezo wa kushika madaraka ya Papa. Ndivyo basi wazo la kujiuzulu lilivyojipandikiza na kumea kichwani mwake.

Ni dhahiri kuwa kwa Papa (Baba Mtakatifu) kujiuzulu sio jambo la kawaida na ndiyo maana ilimbidi mtakatifu Selestini aombe ushauri wa Wataalam waliothibitisha kuwa jambo hilo lingewezekana kabisa kwa kuwa lipo katika mazingira ya kipekee.

Akisha kuwa Papa kwa miezi mitano, Mtakatifu Selestini alitamka rasmi katika mkutano maalumu wa makadinali kuwa angejiuzulu kutokana na umri wake kuwa mkubwa na pia kubwa zaidi, kwa ajili ya yeye mwenyewe kutokuwa na vipaji vya kumuwezesha kumudu kushika wadhifa huo wa Upapa.

Basi akawaomba makadinari waliohudhuria Mkutano huo wamsamehe kwa makosa yake yote aliyotenda.

Akiwasihi wayarekebishe mambo yote yaliyokwenda kombo.

Aliwasihi makadinali hao pia wamchague Baba Mtakatifu mwingine badala yake;tena mwenye sifa na uwezo kiasi cha kushika sawia wadhifa huo.

Akiwa mwenye furaha Selestini aliyefariki dunia mwezi Mei Mwaka 1296 na jina lake kuandikwa katika orodha ya watakatifu mwaka 1313; miaka 17 tu kabla ya kifo chake. aliiacha ile kazi yake ya Upapa; akayavua mavazi yake mazuri na kuanza tena maisha ya kitawa.

Alirudi kwenye nyumba yake ya kitawa baada ya makadinali hao kumkubalia kujiuzulu.

Tunaambiwa kuwa Papa aliyeshika madaraka badala ya Mtakatifu huyu Selestini ambaye hukumbukwa kila ifikapo Mei 19 siku ya kifo chake, aliogopa kuwa huenda yangetokea machafuko kwa ajili ya Mtakatifu Selestini.

Akamtoa porini alikokuwa amejificha na kumfungia katika chumba kidogo mjini Anagni karibu na Roma. Selestini mwenyewe kuona hivi akasema,"Sikutaka kitu chochote duniani isipokuwa kijumba hiki walichonipa. Baada ya miezi kumi iliyojaa shida na mateso, Selestini akafariki dunia Mei 19 mwaka 1296.

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

Wajua kuwa ipo Misikiti miwili tu, mikubwa iliyo tumaini la Waislam

Na Ignatio Obuombe JR.

KILA mwaka Waislamu wanaopenda kuhiji Mecca ziara hiyo haikamiliki na kuhesabika ni takatifu pasipo kuizuru misikiti miwili ya Al-Mukarramah na Al- Madinah Al- Munawarah.

Misikiti hii miwili mikubwa ya kale iliyoko mjini Makkah imekuwa kama ni kitovu cha imani ya dini ya Kiislamu.

Ndani ya msikiti wa Makkah Al- Mukarramah ndipo palipokuwepo na nyumba ya kale ya mtume Mohamed S.A.W na ndani ya msikiti Al- Madinah Al - Munawarah ambao maana yake ni Mji mtakatifu wa Duniani ndimo kuna kaburi la mtume Mohemed S.A.W linaloaminika kuwa lingali chumba mwangaza na nuru kwa waislam kote duniani hata sasa.

Sala zinazofanyika ndani ya misikiti hiyo miwili na zaka zinazotolewa hapo zaaminika ndizo humfikia Allah na kupelekea Waislamu kote Duniani kubarikiwa kulinganga na imani yao.

Mpaka sasa mwangalizi Mkuu wa Misikiti hiyo miwili mikubwa ni Mfalme Fahdd Bin Abdul Aziz. Kufadhiliwa kwa misikiti hiyo na Serikali ya Saudi Arabia kunaonyesha ni kwa kiasi gani Serikali hiyo inathamini maeneo hayo yaliyo muhimu kwa imani ya dini ya Kiislamu.

Waislamu wanaamini kuwa misingi ya mahala misikiti hiyo iliposimama iliwekwa na Abrahamu katika mji ulioitwa Al-Kurah (Makkah ya Leo).

Lakini kasi ya Waislamu kuchukulia maeneo yalipo misikiti hiyo kuwa sehemu yao muhimu sana ya Hija iliongezeka maradufu wakati mtume Mohamed alipoenda kujenga makazi yake hapo. Leo maeneo ya misikiti hiyo yanahesabiwa kuwa ardhi takatifu na mamilioni ya waislamu kote duniani huyazuru kila mwaka