Wazazi wanavyochangia uwongo wa Watoto

WAZAZI wanaposoma jina la makala haya watashangaa sana na kusema: Tunawezaje kufundisha watoto wetu uwongo? Kusema kweli, kama utachukua njia mbaya katika kuwafundisha tabia watoto, italeta matokeo mabaya na tabia mbaya. Hebu tuangalie mifano ifuatayo:

A. Kusema Ukweli kunaleta Adhabu.

Alikuweko msichana mmoja mwenye umri wa miaka 5. Safari moja kwa bahati mbaya alimvunja farasi mmoja wa sanaa nyumbani kwao. Baada ya mama kurudi nyumbani,msichana huyo alimwambia jambo hii bila kuficha lakini hakutarajia kwamba mama yake angempiga makofi na kumkaripia. Baada ya kuadhibiwa alijua kwamba kusema ukweli kumbe kunaleta adhabu. safari nyingine alivunja bakuli moja hivyo ikambidi amwambie mama yake kuwa ni paka ndiye aliyeangusha bakuli hilo kutoka mezani.

Mama yake hakumkaripia wala kumpiga makofi. Safari nyingine aliharibu kipuzi wakati alipocheza. Alimwambia mama yake mwenzake ndiye aliyeharibu. Mama yake hakumpiga ila kumlaumu tu. Hivyo ndivyo msichana hiyo alivyojua kusema uwongo mfano huo unatuambia kwamba mtoto anapokosea kufanya jambo fulani huwa pengine hafanyi kwa makusudi. Kama watoto wanawaambia wawe waangalifu safari ijayo.

B. Kama hawezi kupata Haki kihalali basi atatumia njia potofu.

Alikuweko mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 8. Tangu alipoanza shule, masomo yake ni mazuri. alipenda kucheza na wenzake baada ya kumaliza masomo . Wazazi wake hawakufikiri kwamba hiyo ni silika ya watoto na tena mchezo unanufaisha afya ya watoto. Waliohofia kuwa mchezo unaweza kumfanya akawie masomoni na pengine mtoto atapata tabia mbaya. Kwa hivyo waliomwambia mtoto wao akae nyumbani tu baada ya kutoka shuleni. Mtoto alikuwa hana la kufanya ila kuchukua njia ya kusema uwongo.

Kwa kawaida alasiri ya Jumamosi hakuna masomo shuleni lakini mtoto huyo alimwambia wazazi wake kwamba mwalimu atamsaidia kusoma huko shuleni kumbe alitumia wakati huo kucheza na wenzake. Baada ya kuonja utamu kutokana na 'mafanikio' ya kusema uwongo baadaye kila alipotaka kutoka nje kucheza alisema uwongo mfano huo unawaambia wazazi kuwa kwa mujibu wa silika ya watoto, hawawezi kukaa nyumbani tu kusoma baada ya kutoka shuleni ingefaa wapangiwe wakati wa kuchezea. Wanaweza kuwaambia watoto wacheze baada ya kumaliza masomo ya nyumbani au kuendelea na masomo yao baada ya kucheza kidogo. Kama haki haipatikani kwa kupitia njia ya halali, basi watatafuta njia potofu.

C. Baadhi ya Wazazi wana wafundisha watoto waseme uwongo.

Siku moja nilipokuwa ndani ya basi nilisikia mwanamke mmoja akimwambia mtoto wake mwenye umri wa miaka 5 hivi, ' kama leo mwalimu wako anakuuliza kwa nini siku hizi hauji shuleni, mwambie kwamba unaumwa na homa, Usimwambie tulikwenda kumzuru bibi yako' Wakati ule nilitaka kumzuia mwanamke hiyo asimfundishe mtoto wake kusema uongo. lakini ni nilihofia atatahayari baada ya kushuka kutoka kwenye kituo cha basi nilisikitika kwa kuwa kitendo cha yule mwanamke kitamletea yule mtoto athari mbaya.

Wako wazazi wengi ambao husema uongo mbele ya watoto wao. Kwa mfano mke anamwambia mumewe ' Leo iko kazi nyingi sana nyumbani, nenda ukapige simu ofisini kwako na kusema unaumwa kiuno' wazazi hawa hawakujua vitendo vyao vitaleta taathira kubwa sana kwa mtoto wao kama wazazi hawaangalii tabia yao au hawachukui hatua yoyote kwa watoto ambao wanasema uwongo basi ni rahisi kwa watoto kuzoea kusema uwongo.

D. Kusema uongo hupata sifa au Faida.

Baadhi ya watoto huweza kupata sifa na faida kwa njia ya kusema uwongo. kwa mfano baadhi ya wazazi wanatoa ahadi kama majina ya watoto wao yanatangulia darasani kwa mujibu wa mafanikio ya masomo yao, watawanunulia vipuzi au chakula, kwa ajili ya kupata faida watoto wanasema uwongo kuwadanganya wazazi kwamba wamefaulu mtihani na kusifiwa na mwalimu wao wazazi ambo hawajui ukweli wa mambo wanawatunukia hivyo huwashawishi watoto kusema uwongo.

Kwa mfano mwingine baadhi ya watoto wadogo huwa hawapendi kwenda katika shule ya watoto na wengine huwa hawapendi kwenda shuleni kusoma. Kwa ajili ya kutimiza makusudi yao huwa wanasingiziaa ugonjwa, kama vile wanaumwa na kichwa au tumbo.

Magonjwa hayo hayaonekani kwa urahisi kwa hivyo wazazi wanawaruhusu kubaki nyumbani na kuwatunza vizuri. Hivyo kama watoto hawapendi kwenda shuleni wataendelea kujisingizia ungonjwa. kwa jambo hilo inawabidi wazazi wachunguze kama watoto wamepata ugonjwa kweli, zaidi ya hayo wazazi wanaweza kuchukua hatua zilizofaa kwa mujibu wa hali ilivyo.

Jambo jingine la kuangalia ni kwamba wazazi wasiwashughulikie sana watoto ambao wamepata ugonjwa mdogo.

Hali iliyoelezwa hapo juu inayonyesha kwamba mafundisho mabaya yanasababisha watoto kusema uwongo. Watoto wenyewe wana tabia maalum ya kisaikolojia, ambayo inasababisha waseme uwongo, kama vile wanapenda kujigamba mbele ya watu na hawawezi kutofautisha baina ya ruya na mambo hasa. Wazazi wanatakiwa kugundua mara moja tabia ya kusema uwongo kwa watoto wao na kutafuta sababu ili kuwafundisha vizuri.

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

Uislamu ulivyopenya nchini China (3)

Wakati huo hariri vyombo vya kaure, majani ya chai kutoka China pia vilijaa masokoni huko Baghdad.

Katika sehemu za pwani za kusini mashariki ya China biashara ya kimataifa ilifana sana Wafanyabiashara ambao wengi wao walitoka nchi za Kiarabu na Uajemi walifululiza kuja China kwenye miji mingi ya bandari kufanya biashara. Mji wa Guangzho palikuwa pahala pa kukusanya na kugawanya bidhaa za Kiarabu na za China na pia palikuwa ni bandari kubwa kabisa ya biashara ya China. Merikebu nyingi za Waislamu zilizotoka ghuba ya Uajemi zilitia nanga katika mto wa Zhujiang.

Juu ya msingi huo wa biashara, Tazi na Enzi ya Tang zilijenga uhusiano mzuri wa kibalozi. Mnamo tarehe 25 Agosti mwaka wa pili wa Yonghui Othman wa Tatu (Mwaka 644-656) alileta mjumbe wake hadi mji wa Changan kuonana na Li Zhi mfalme wa Enzi ya Tang (aliyesika madaraka ya ufalme mwaka 650- 683) ambaye wakati huo amekuwa madarakani kwa mwaka mmoja tangu atawazwe kumweleza hali ilivyo nchiini Tazi na nadharia ya kimsingi na Kiislamu Toka hapo maingiliano ya kirafiki kati ya China naTazi yakazidi kukua. Kutokana na takwimu za muda wa miaka 147 toka mwaka wa pili wa Yonghui hadi mwaka wa kumi na nne wa Zhenyuan (651 - 798), nchi ya Tazi ilileta wajumbe wake nchini China mara 36 na katika muda wa mwaka 713 -741 waliteuliwa mara 10. Mnamo mwaka 757 kwa kufuata mwaliko, Tazi ilileta jeshi kuisaidia enzi ya Tang kunyamazisha fujo la An Lushan na lilifanya kazi kubwa katika kurejesha miji ya Dongjing na Xijing mkononi mwa utawala wa enzi ya Tang.

Maingiliano ya uchumi na biashara na mahusiano ya amani na kirafiki yaliwafanya Waislamu wengi zaidi kuhamia China na kuusukuma mbele uhusiano wa kirafiki kati ya China na Uarabuni kufikia katika kipindi kipya.

Safari ya kuja na kurudi kutoka Uarabuni hadi China kwa wafanyabishara wa nchi ya Tazi ilichukua muda wa miaka miwili ingawa wengi kati yao walirudi makwao katika majira ya baridi, lakini waliobaki pia walikuwa si haba zaidi ya hayo maaskari wa nchi ya Tazi waliokuja kusaidia kunyamazisha fujo pia walibaki huko Changan Inasemekana kwamba ili kuridhisha mahitaji ya maisha yao ya kidini mfalme wa ezi ya Tang Waislamu waliokaa katika miji ya Changan, Guangzhou, Yangzhou kisiwa cha Hainan walifika maelfu. Kutokana na kushughulikiwa na kushajiishwa kwa juhudi na wafalme wa China, wafanyabiashara wa Uarabuni na Uajemi waliokuja kwa ajili ya biashara na kukaa waliongezeka mwaka hadi mwaka. Baadhi yao walileta wake zao na watoto wao na wengine waliowaona wasiachana wa kabila la Han. Mpaka mwaka 1114 Waislamu wa nchi za nje walioishi nchini China zaidi ya vizazi vitano walikuwa wengi. Enzi ya Song ilitoa Sheria ya urithi wa mali zilizoachwa na wafanyabiashara wa vizazi vitano, ili kutatua suala la mgawanyo wa urithi wa mali zilizoachwa nao katika China. Watu wengi kati yao hawakurudi kabisa makwao. 'makaburi ya wageni' yaliyoko mjini Quanzhou yalikuwa mava ya watu hao.

Wafanyabiasha wa Kiislamu waliokuja China kuselelea baadhi yao hawakujali sheria ya kuwakataza wageni kukaa pamoja na watu wa kabala la Han. Hata hivyo wengi wao walikaa pamoja na Wahan katika sehemu kando ya barabara nje ya miji kwa mujibu wa kibali cha kichinichini cha maafisa. Katika sehemu hizo viongozi wao walikuwa ni Waislamu wazee wenye heshima nyingi nao walichaguliwa miongoni mwa wafanyabishara Waislamu na kuidhinishwa na mfalme wa China.

Katika Enzi ya Tang na ya Song, Uislamu ulipoanza kuingia nchini China ulikuwa umeungana na siasa, uchumi, utamaduni na desturi za maisha ya watu wa China katika sehemu zao hali hii ya kuungana na siasa na dini ilikuwa sawasawa na mfumo wa vyombo vya madaraka ya Uislamu katika sehemu ya Uarabuni zama za katikati (500-1500 B.K) Lakini wakuu hao wa Kiislamu walitakiwa kuidhinishwa na kupewa madaraka na watawala wa China na kubeba jukumu la kuvuta na kuingiza wafanyabiashara wa nchi za nje kwa ajili ya ufalme wa China kwa kiwango fulani walipokea usimamizi na uongozi wa ufalme wa China na kuutumikaia utawala wa China. Hii inaonyeshesha kuwa Uislamu ulioko katika sehemu hizo ingawa ulikuwa dini ya makabila ya nchi za nje au ya wageni walioishi nchini China, lakini umefungua ukurasa wa kwanza wa Uislamu nchini China.

B. Uenezaji wa Uislamu katika Enzi ya Yuan

Katika miaka ya katikati ya karne ya kumi na tatu kadiri vikosi vya kijeshi vya mabwanyenye wa Mongalia vilivyokuja na kurudi ndivyo mawasiliano ya nchi kavi kati ya China na sehemu za mgharibi yaliyokuwa makubwa, Waslamu wa makabila mbalimbali ya Kiarabu, Uajemi na sehemu za Asia ya Kati waliingia kwa wingi ndani ya China wakifuata njia hiyo ya mawasiliano kwa kuandamana na jeshi la Mongolia.

Yasiyo ya Kawaida

 

Njiwa waliokataa kuhama katikati ya jiji la London

lSerikali imewanyanyulia mikono sasa inawalisha

lHawaogopi watu na huwakalia vichwani na miguuni

Na Masha Otieno Nguru JR

WANYAMA walio wengi,ndege na hata wadudu hupendelea kuishi porini na mafichoni.

sio jambo la kawaida kwao kuwa na kiburi kiasi cha kukatalia sehemu za wazi hususani kati ya miji mikubwa.

Lakini hivyo sivyo hali ilivyo kwa njiwa fulani wajanja walioamua kuishi kwa makusudi kabisa katikati ya jiji la London kwa miaka mamia sasa.

Njiwa hao waliohamia hapo yapata karne mbili zilizopita wamegoma kuhama kutoka hapo mpaka leo.

Mnara wa 'Trafalgar Square' ni mashuhuri sana katikati ya jiji la London.

Ama kwa hakika ni katika mnara huo mashuhuri uliodumu kwa miaka mingi ndiko njiwa hao wengi wameweka makazi yao ya kudumu kiasi cha kupelekea wapewe jina la 'Pigeons of Trafalgar Square'.

Lakini njiwa hawa wana vituko vya kushangaza moja ya vituko vyao ni kuwa wakimuona yeyote ameutembelea mnara huo na kuketi karibi nao wao huja mara moja na kumrukia na kutua kila sehemu ya mwili wake kama ana bahati nao.

Nyakati zingine Nijiwa mmoja ndiye huja kutua kwenye kiganja cha mkono wa mtu aliyeketi karibu na mnara huo. na mara nyingine njiwa hao hutua kichwani kwa mtu pasipo kumuogopa hata kidogo.

Pembeni mwa mnara wa 'Trafalgar Square wapo wachuuzi wadogowadogo wanaouza chakula cha njiwa kwa watalii wanaotembelea mnara huo karibia kila siku iwapo wangelipendelea kuwalisha njiwa hao werevu.

Njiwa hao walianza kuishi kwenye mnara huo toka ulipojengwa mwaka 1895 kama ishara ya kumbukumbu ya Lord Nelson aliyeliletea jeshi la majini la Uingereza ushindi mkubwa katika vita mwaka 1805.

Mnara huo ulio na urefu wa futi 185 (56.3 m) kwa pembeni umezungukwa na sanamu za Simba 4 ambao walibuniwa na kutengenezwa na msanii mashuhuri wa zamani nchini Uingereza Victorian Landseer.

Juu kabisa kwenye kilele cha mnara huu wenye njwa kuna sanamu ya Lord Nelson mwenyewe akiwa amevalia mavazi yake rasmi ya kivita huku akitazama upande unaotazamwa na mmojawapo wa Simba waliopo kwenye mnara huo.

Na ukisimama kwenye mnara huu pia unaweza kuuona ukumbi mashuhuri wa 'White Hall' ambao unakuongoza kuelekea eneo mashuhuri la Westminster Abbey majengo ya Bunge na mto mashuhuri wa Thames.

Pia tao la Admiralty linaloongoza kuelekea kasri ya 'Buckinghama Palace' ipo jirani kabisa na mnara huu.

pasipo kusahau chemichemi inayorusha maji masafi juu juu kwenye mnara huu wa 'Trifalgar Square'.

Bw. John Lewedson mwandishi wa kitabi mashuhuri kuhusu madhhari na historia ya jiji la London. 'The Ladybird Book of London' anayo haya ya kusema kuhusu njiwa wenye vituko wa Trafalgar Square.

'They seem to consider themselves to be one of the sights of London'

'Inaonyesha wanajichukulia kama wao pia ni sehemu ya jiji la London'.

Padri Geofrey Riddle ni mzaliwa wa jiji la London na ameishi Tanzania kwa muda mrefu sasa kwa sasa yeye anahukusika na fungamano la kuweka mahusiano mazuri katika ya makanisa nchini Tanzania, nilipomtembelea kwenye makazi yake jengo la Hataman House jijini Dar es Salaam alikuwa na yafuatayo ya kusema kuhusu njiwa hawa.

"Nimezaliwa London, nimeanza kuwaona hapo toka nikiwa mdogo, wanapendeza na kuvutia macho wakiondoka mnara huo hupungukiwa na vivutio vyake, na nina uhakika hawawezi kuhama"

Lakini wakati njiwa wa Trafalgar Square wakiwa wapole na wakarimu kwa wageni wanaotembelea London Kunguru katika sehemu ya utalii katika pwani ya Maputo wao wameonyesha kwenda kinyume.

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa kukitegemea Cypriam Mchenyela anayeishi Maputo, Msumbiji Kunguru hao wakorofi wamegoma kuhama kwenye mahoteli na migawahawa iliyo ufukweni mwa bahari ya Hindi ambapo wamekuwa wakiwanyanganya watalii chakula mezani, kuwashambulia na hata wamefikia hatua ya kwendaa jikoni na kufunua sufuria yenye chakula kinachochemka jikoni kisha wakadokoa nyama na kuondoka nayo hata ikiwa ni ya moto.

 

Si Vema kuwazuia watumishi wa Mungu kukosoa upotovu wa Kisiasa

Na Justine Kivugo

KATIKA miaka ya hivi karibuni, viongozi wa nchi hii wa kanda mbalimbali wamekuwa wakionya au kukemea kile wanachodai kuwa ni viongozi wa dini kujihushisha na masuala ya Siasa.

Katika madai yao hayo, wamekuwa wakisema kwamba ni kosa kwa viongozi wa dini kuzungumzia siasa na kwamba viongozi wa dini hawategemewi kuchanganya dini na siasa.

Jambo la ajabu ni kuwa wanasiasa hao wameshindwa kabisa kutetea kauli zao hizo kwa hoja za kueleweka zinazoweza kupenya katika akili sio tu za watumishi wa Mungu (viongozi wa dini),bali na kwa Watanzania wote kwa ujumla.

Mathalan,, inapotokea kwamba kiongozi wa dini anaonya au kushauri kuhusu mwenendo mbaya wa kisiasa au kiongozi wa nchi kwa lengo la kuitazamisha jamii hatari inayoweza kutokea huyo anaitwa 'mchanganya siasa na dini'. Au inapotokea kwamba Kiongozi wa dini anakemea maovu kama utapeli, wizi, uhuni, ufuska, rushwa au ukandamizaji unaofanywa na viongozi wa nchi huyo naye atapewa jina lile lile la 'Mchanganya siasa na dini'.

Hivi kwa ubaya gani kwa mfano Askofu anapoamua kuwatahadharisha viongozi wa nchi kuwa macho na wachokozi wa kisiasa au watu wanaotaka kuvuruga amani nchini?.

Ipo mifano lukuki inayoonyesha kwamba Viongozi kadhaa wa dini walifanikiwa kwa kiasi kikubwa walipokuwa wakikemea kuonya au kushauri juu ya mambo yaliyokuwa yakiashiria kutoweka kwa amani na mshikamano.

Mwanzoni mwa miaka ya tisini wakati mihadhara ya kashfa dhidi ya dini moja au zaidi iliposhamiri, Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliwakemea waendesha mihadhara hiyo ambapo aliitaka serikali kuwa macho na watu wa aina hiyo ambao aliwaita 'Wendawazimu'

Kardinali alisema watu wanaendesha mihadhara hao hutumia dini na hasa mihadhara ya kashfa kama kichaka cha kuficha madhambi yao huku wakiwa na nia ya kuchuana kisiasa.

Ingawa mwaka 1997 vuguvugu la mihadhara hiyo lilipungua sana, Kardinali Pengo hakuacha kuendelea kutahadharisha juu ya athari za mihadhara hiyo kauli aliyoitoa mara tu alipoteuliwa kuwa Kardinali alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu jijini.

Ama kwa hakika hakuna atakayebisha kwamba jitihada hizo za Kardinali Pengo zimezaa matunda 'ya kutosha' ambapo zile pilika pilika za mihadhara iliyoitetemesha sana Serikali katika muongo uliopita sasa zimefifia kabisa, huku wananchi wakiendelea kushika 'elimu nasaha' ya kuipuuza mihadhara hiyo.

Ni Kardinali huyo huyo ambaye hivi majuzi tu alitoa ushauri kwa Serikali ya Mapinduzi (SMZ) juu ya azma ya kutaka ' kupindua; Katiba ya nchi eti kwa manufaa ya mtu mmoja aliyejiita 'Komandoo'

Akasema kwamba ni lazima Serikali ya Muungano iwe makini na masuala yanayoweza kuivuruga jamii ya Watanzania, kauli ambayo pia iliungwa mkono na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) katika waraka wake lililoutoa kwa vyombo vya habari hivi karibuni.

Mara kadhaa tumesikia pia viongozi mbalimbali wa dini wakiwashauri watanzania kuchagua viongozi waadilifu na wacha Mungu, wito uliokuwa ukitolewa katika chaguzi mbalimbali zilizopita. Je wito wa aina hiyo ni mbaya? Je huko ni kuchanganya siasa na dini?. Je Viongozi wa dini kujali demokrasia na maslahi ya wananchi wa taifa lao na kuhimiza kumcha Mungu ni Kosa?.

Ni kweli kwamba kuna viongozi wanaoweza kuwa na azma ya kificho yaani kama vile kutaka kupewa ngome ya siasa kwa mlango wa dini hawa mara nyingi huwa na ubinafsi na sio kwa maslahi ya umma na kwa hakika hawa hutawaliwa na tama ya umaarufu.

Hawa ndio ambao kwa makusudi kabisa humdhalilisha Mungu kwa kutokuwa waaminifu katika utumishi wao na wakati mwingine watu wa aina hiyo huwa rahisi sana kutumiwa na wasioitakia mema nchi hii yaani maadui wa nchi yetu.

Ni lazima tukubali kwamba maoni ya watumishi wa Mungu yanayoitakia mema nchi hii au changamoto zinazolenga kukosoa utendaji mbovu ni muhimu kwa jamii yetu.

Tunachotaka ni kwamba kauli au maoni hayo yatolewe kwa uwazi na kwa wakati na pia yawe na mtazamo wa kuinufaisha jamii nzima na wala si mtu au kikundi cha watu.

Jambo la ajabu nala kuchekesha ni kwamba viongozi hao nao wa nchi wanaodai kwamba kuna uchanganyaji wa siasa na dini ndio ambao ' huwaangukia' watumishi wa Mungu pale yanapotokea matatizo magumu ya nchi.

Wakati wa El-Nino mwaka 1997/1998 tulishuhudia kuhaha kwa viongozi wa nchi wakiwasaka na hatimaye kuwaomba viongozi wa dini kuiombea nchi. Ni watumishi hao hao wa Mungu walioombwa kutoa matamko mbalimbali na kisha kuiombea nchi wakati wa msiba mkubwa wa kitaifa wa aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,aliyefariki dunia Oktoba 14 mwaka jana (1999) na hasa baada ya kutokea matishio mbalimbali ikiwa ni pamoja na uvumi wa kuyumba kwa muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar kufuatia kifo hicho cha mwasisi wa Muungano.

Tunapohitimisha makala hii si vema kuwasahau watu kama Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini na Askofu Abel Muzolewa wa Zimbambwe, ambao walijitoa Mhanga kutetea bara la Afrika mbali na nchi zao, dhidi ya ubaguzi wa rangi.

kadhalika nani asiyejua kwamba mmoja wa watu maarufu duniani Papa Yohane Paulo ambaye ni Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani amekuwa kwa miaka mingi sasa akitetea haki na amani duniani kwa kuwakemaea viongozi wa nchi mbalimbali wanaokiuka misingi ya haki za binadamu na suala zima la demokrasia!?.

Kiongozi huyo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuzipatanisha baadhi ya nchi zilizokuwa na mgogoro ya wenyewe kwa wenyewe au hata na ile inayohusisha zaidi ya taifa moja. tena ikumbukwe kuwa Wabunge wa nchi mbalimbali yana wabunge ambao ni viongozi wa dini na ambao pia wamekuwa wakitoa michango yao madhubuti katika kuendeleza jamii za nchi zao.

Kitu cha muhimu kwa viongozi wa nchi si kulalama tu kwamba watumishi wa Mungu wanawaingilia au wanaingilia siasa bali kufanya upembuzi wa kusifu katika yale yanayosemwa na hao watumishi na kisha kufanyia kazi kwa faida yao na taifa kwa ujumla.

 

 Maisha na Mikasa

Mtoto agongwa na treni na kupasuka kifua , lakini akaendelea kuishi

lAlikuwa anavuka reli kufuata maji, ni wa miaka miwili

l'Niliokota vidole kumpelekea Muhimbili nikidhani atapona lakini..'

Getruda Madembwe na Joseph Sabinus

"NILIPOFIKA nyumbani na kuona watu wamejaa, nikashangaa kuna nini tena; maana mbona wananiangalia hivyo sasa nikasema kuna nini. Wengine wakaniambia ukweli. Nikaenda alipogongewa mwanangu.

Tukakusanya vidole vya marehemu wangu, tukavifunga vizuri kwenye karatasi, vidole vitatu vya mkono. tukamkimbizia huko Muhimbili na majirani wengine maana tayari tulishaambiwa kwamba Temeke (hospitali) imeshindikana.

Nikavibeba kumpelekea mwanangu Ismail maana niliamini kuwa kwa kuwa amefika hospitali, atapona tu, vidole kukatika siyo hoja, cha maana ni uzima. Lakini, maskini tulipofika hospitali tukaambiwa kuwa kumbe treni ilipomgonga na kumrusha mbele kabla ya kumkanyaga mikono, kifua kilipasuka na damu ilikuwa inamwagikia tumboni.

Wakasema marehemu mwanangu Ismail; amekwenda, amekufa. tayari Mungu amekwishamchukua".

Anaelezea kwa huzuni Bw. Abdala Ismail Linda, mkazi wa Mtoni Sabasaba jijini Dar es Salaam, Mkewe Bi. Lucia Abdalah Athuman pamoja na shemeji wa Bw. Abdala, Bi. Sophia Abdala ambao mtoto wao Isamil Abdala (2), alifikwa na mauti katika wodi ya Kibasila katika hospitali ya Muhimbili baada ya kupata ajali ya kugongwa na kisha kukanyagwa na treni ya TAZARA, mnamo Aprili 6, mwaka huu siku ya Alhamisi.

Katika mazungumzo yao na gazeti hili yaliyofanyika nyumbani kwao, baba wa marehemu Bw. Abdala ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo katika eneo la mitaa ya Agrey na Mkunguni jijini, alisimulia,

"Siku hiyo ya Alhamisi mimi niliondoka kwenda kwenye mihangaiko. Hapa nyumbani, nikawaacha mama yake na hako kadogo kake (anaonesha mtoto mdogo anayenyonya); kenyewe kanaitwa Sharifa ni ka miezi miwili".

Sasa nilipofika, majirani wakanisimulia yaliyotokea hapa nyumbani, unajua marehemu alikuwa amezoea kumfuata mama yake anapokwenda bombani kuchota maji.

Ilifikia hatua hata saa nyingine marehemu akawa anatoroka na kwenda mwenyewe kisha anarudi. Hata hivyo mama yake alikuwa makini kumuangalia asivuke vuke reli hovyo.

Lakini Bwana Mungu mwenyewe akishapanga, amepanga."

Kisha Bw. Abdala ambaye ni Mmakonde kutoka kijijini Liteku huko Tandaimba mkoani Mtwara akaendelea kusimulia kwa huzuni katikati ya jumalililopita, "Sasa siku hiyo mchana mama yake alikuwa anafua, marehemu nae alikuwepo anamsumbua sumbua, sasa mama akaenda huko uani kidogo.

Kaliposhituka kakadhani amekwenda tena bombani kufuata maji mengine ya kufulia.

Ismail(marehemu) akaamua kumfuata kule bombani si alikuwa amezoea njia.

Hata hivyo siyo siku nyingi zimepita, kama mwezi mmoja hivi sasa, marehemu ndio kwanza maskini alinusurika kugongwa na treni hiyo hiyo." Akatulia kidogo. "Kilichomuokoa ni kijana mmoja wa jirani (simjui jina, hata mama wa marehemu hakumfahamu).

Kijana huyo ndiye aliyemvuta kutoka relini treni ikapita maskini kumbe Mungu alishampangia kifo cha treni." akatulia kidogo akimtazama mama wa marehemu aliyeongeza,

"Sasa nilipotoka nikawa simuoni mtoto,mara treni ikapita lakini sikumbuki ilikuwa na mabehewa mangapi maani nilichanganyikiwa kabisa.

Lakini treni ikasimama na haukupita muda watu wakaanza kupita wanakimbia huku wanasema eti kuna mtoto amegongwa na treni, nikajua ni mwanangu Ismail"

Anasema baada ya muda mfupi ndipo alipohakikishiwa kabla hajaenda wala kufika kwenye tukio maana tayari alikwisha haha kumtafuta mwanae. "Wakaniambia eti ni marehemu amegongwa, niliposikia hivyo, nguvu zikaniishia kabisa" akatulia mama huyo wa marehemu Bi. Lucia Abdalah Athumani, wa kabila la Wayao huko Masasi.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba kama ambaye alitokewa ndoto kuwa mwanae wa kwanza atafikwa na mauti kwa ajali ya relini, Bw. Abdala aliwahi kupiga picha ya huzuni na ya kusikitisha akiwa amekaa relini amejishika tama na kujawa na mawazo mengi.

Kisha Bw. Abdalah akaendelea, "Sasa huyu mama yake hakujua kinachofanyika wala kinachoendelea; hakuwa hata na nguvu kabisa.

Kama mama mwenye nyumba wetu na majirani zangu wasingetoa msaada kwa moyo wa upendo, labda marehemu mwanangu Ismaili angeozea relini.

Basi wakamikimbiza hospitali ya Temeke lakini hali ikazidi kuwa mbaya; wakaona ngoja wampeleke Muhimbili".

Bw. Abdala akaendelea kusema kuwa baada ya kumfikisha Muhimbili na kulazwa katika wodi ya Kibasila, alianza kutibiwa mkono ule uliokatika vidole na majereha mengine.

"wakati huo marehemu alikuwa anatia moyo maana kila mtu alijua atapona tu. Muda huo, ukimwambia lala, analala mara anaita, "Babaa! babaa," "mamaa! Mamaa!" "Baai! Baaai!" ni kweli matendo hayo aliyafanya kumbe ndio alikuwa anaaga hivyo."

Awali, jirani mmoja wa Bw. Abdala aliyeshiriki kumpeleka mtoto huyo aliyefikiwa na mauti ya kutisha (hakutaka jina litajwe kwa kuwa si mwana ukoo), aliigiza namna mtoto huyo marehemu alivyokuwa akilia na kucheza huko hospitali, akasema,

"Maskini kakawa kanalia, "babaa, gari ya babaa! Gari ya babaa! Kanatulia kisha kanalia tena; mara kanalala" akasema jirani huyo.

"Mimi walau, ninasema kama sitafukuzwa, sioni sababu ya kuhama hapa maana msaada niliopewa ukianzia kwa mama mwenye nyumba (Mama Maimuna) na majirani zangu wote akiwemo Mama Bariki, umenifariji sana, nimejiona naishi na ndugu zangu. Marehemu alifariki Alhamisi hiyo usiku; karibia kabisa saa tano na nusu na mazishi tuliyafanya Jumamosi maana ilibidi watu wa TAZARA waidhinishe na kuruhusu maiti itoke Muhimbili.

Tumezika saa 8 mchana maeneo ya Mtoni-Mbuyuni hata vile vidole vyake. Ndivyo alivyopanga Mungu hakuna ujanja.

Marehemu alikufa hiyo saa tano na X-ray ilionyesha kumbe ile treni ilivyomgonga, kifua kilipasuka na damu ikawa inavujia tumboni ndipo ikamsukuma mbele na kuanguka mikono ikawa hivi (natoa mfano wa namna marehemu alivyoanguka baada ya kugongwa na kuanguka akielekeza mikono relini), ndipo akaweka mikono relini na kukanyagwa.

Basi vikakatika vidole vitatu , ndipo tukavibeba kwenye karatasi kupeleka Muhimbili lakini wapi.

Hata hivyo, baada ya maelezo hayo, mahojiano baina ya wafiwa na gazeti hili la Kiongozi yalikuwa hivi:-

Gazeti: Marehemu alikuwa ni mtoto wa ngapi kwenu?

Mama: Alikuwa wa kwanza; tena alikuwa mvulana na alikuwa na miaka miwili.

Mama mkubwa wa Marehemu: Si hako kadogo kake ndiko kanakomfuatia; alikuwa na miaka 2 tu. (anaonesha kidole kwa mdogo wa marehemu; aitwaye Sharifa, mwenye umri wa miezi miwili aliyekuwa amelala kitandani).

Gazeti: Sasa msiba mlifanyia wapi?

Baba: Hapa hapa nyumbani.

Gazeti: Mwenye nyumba alikubali kuleta msiba na kujaza watu nyumbani hali msiba sio wake?

Baba: Kweli hata watu na mimi mwenyewe tumeshangaa sana kwa wema wa huyu mama. Huyu mama amesaidia hata kumshughulikia marehemu tangu mwanzo; mpaka alipofia Muhimbili. Msiba ulifanyikia hapa hapa na hata hivyo hatukuwa na nguvu ya kufanya msiba usiwe hapa.

Gazeti: Kama mwenye nyumba angekataa msifanyie hapa, mngefanyaje?

Baba: Angekataa tungepeleka kwa ndugu zetu ambao walitaka tupeleke kwao msiba.

Gazeti: Sasa kwa nini hamkutaka kwenda kwa ndugu zenu?

Baba: Kwa kuwa hakutufukuza na marehemu wetu na wala hakuwa na manung’uniko yoyote ya chini chini na kwa kuwa alionesha moyo na msaada mkubwa kwetu toka mwanzo, hadi wakati wa mazishi, kama nilivyosema kuwa hata majirani walitusaidia mno, niliona nikihama hatajisikia vizuri. Na hii kufanyia hapa msiba ni kwa heshima na shukrani kwake.

Gazeti: Si umesema hamkuwa na uwezo wa kufanyia msiba mahali pengine?

Baba: Ninamaanisha kwenda Mtwara; tusingeweza kusafirisha maiti hadi mtwara, lakini kuhamisha msiba ningefanya hivyo kama tuna ubaya nae au ameninyanyasa na msiba wangu.

Gazeti: Hawa watu wa TAZARA wanasemaje?

Baba: Wao waliniita nikatoe imani yangu kwao. Na mimi ukweli ni kwamba sina chuki nao kwamba wameua mwanangu hii ni ajali tu kama ajali nyingine. Na hata hivyo licha ya kuwa nina washukuru kwa kunihudumia mpaka kumtoa kule marehemu, bado pia nanamuombea radhi marehemu kwa hawa watu wa TAZARA kwa usumbufu ambao wameupata ili mwanangu akae kwa amani huko aliko.

Hata hivyo, kwa mkasa huu, gazeti la Kiongozi linawashauri wakazi wengine wa maeneo jirani na reli wawe makini zaidi kuwadhibiti watoto wasivuke reli ovyo kwani ni hatari sana kwa usalama wao

Na Pia gazeti la Kiongozi na wafanyakazi wake wote, linawapa pole ndugu, jamaa na marafiki katika msiba huo . Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema Peponi AMINA.